Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA SITA

★★★★★★★★★★★★★★


Hee! Mariam alikuwa amefika hapo saa ngapi? Dakika chache za kutoangalia upande huu zilikuwa zimetosha kumweka hapo, na sikuwa na uhakika alikuwa ameona ama kusikia nini. Yaani kujua tu kwamba angeweza kuwa ameona ama kusikia niliyokuwa nimetoka kufanya, kukanipa hisia mbaya moyoni. Na alikuwa akinitazama usoni kwa umakini kiasi.

Lakini nikajitia usabuni na kusema, "Mamu? Mbona umekuja hapa? Vipi?"

Akiwa ananiangalia kwa njia ya kawaida sasa, akasema, "Nilikuja... kukuita, tukale."

"Aaaa... sawa. Umekuja hapa zamani? Mbona hujaniita sasa?" nikajitoa akili kuuliza hivyo.

Akaangalia chini huku akianza kuvifikicha-fikicha vidole vyake, kama vile anaona aibu. Duh!

"Eti? Mbona hujaniita sasa?" nikamuuliza tena.

Akasema, "Niliogopa."

Nikamuuliza, "Unaogopa nini Mamu?"

"Nim... nilikuwa... nasubiri... umalize... kojoa..." akasema hivyo.

Ahueni ikiwa imeingia ndani yangu kiasi, nikamwambia, "Aaa... sawa. Haina shida, usi... usiogope wala."

Akaniangalia usoni kwa macho yenye ugeni fulani hivi.

"Kwa hiyo ulikuwa tu unasubiria nimalize kukojoa ndiyo uniite, eh?" nikamuuliza.

Akatikisa kichwa kukubali.

"Sawa. Nimemaliza. Ila... usimwambie dada na mama mkubwa kama umekuta nakojoa huku, eti? Watanichapa," nikamwambia hivyo kwa ule ushawishi wa kitoto.

Akatikisa kichwa kukubali, nami nikamshika begani na kumwambia tuelekee ndani ili kupata chakula sasa.

Inaonekana nilikuwa nimeponea chupuchupu, ila sikuwa na uhakika sana. Ikiwa Mariam angekuwa amesikia ama kuelewa yaliyofanyika baina yangu na Dina, basi ningekuwa nimeiingizia akili yake jambo fulani ambalo halikutakiwa kabisa kumwingia kwa wakati huu, yaani ingemvuruga. Lakini nilitumaini kuwa haikuwa hivyo, maana binti hakuwa mwongo, kwa hiyo tukaenda ndani kujiunga na wengine kwa ajili ya msosi. Ikawa kama vile hakuna chochote kilichokuwa kimetokea baina yangu na mwanadada Dina.

★★

Kwa hiyo sote kwa pamoja tukapata msosi mtamu kabisa kutoka kwa mpishi maridadi, bibie Miryam, na wageni walifurahia sana na kumsifu Miryam kwa ubunifu wake katika mapishi. Katika mazungumzo, Bi Zawadi akawa ameniambia kuwa kesho angekwenda tena kule Chamgando kuhudhuria ibada kanisani, na kama nilivyokuwa nimemwahidi mama mchungaji, basi na mimi ningepaswa kwenda naye. Na nilikuwa nimesahau, lakini baada ya kukumbushwa hivi, nikamwambia tungekwenda pamoja bila shaka. Ndiyo akawa ameniambia kwamba hata Mariam angekwenda pamoja nasi kesho.

Kulikuwa na kitu kilichoniambia kwamba suala langu na Dina pale nje lilikuwa limechafua hali ya hewa kwa wengine kiasi, maana nilihisi kama vile Mariam alijua, ila ni kama tena hakujua, yaani alikuwa ameanza kunitendea kwa njia fulani ya woga woga hivi; siyo ule woga wa kukuta tu mtu anakojoa nyuma ya nyumba yao. Ikiwa alijua nilichokuwa nimefanya na Dina, basi angeanza kunichukulia kwa mtazamo tofauti kabisa, na sikujua hiyo ingeathiri vipi ufahamu wake kiujumla.

Mpaka tunamaliza kula na kurudi kukaa tena masofani, Doris pamoja na Dina wakaendelea kuwa hapo kumalizia matembezi yao kwa story chache zilizohusiana na kitchen party ya mwanamke huyo, na pia alikuwa ameshaalikwa kuhudhuria birthday party ya Bi Zawadi hapa nyumbani na kukubali kuja pamoja na watu wengine wa familia yake. Niliendelea pia kuwa hapo mpaka mida ya saa tatu na nusu hivi, ndiyo wageni wakaaga hatimaye.

Tukanyanyuka kwa pamoja ili kuwasindikiza kuelekea nje, na inaonekana Shadya angelala hapa leo, kwa hiyo baada ya Doris na Dina kuwaaga wote kwa upendo, Miryam, Tesha na mimi tukawatoa nje na kutembea nao mdogo mdogo kuelekea huko barabarani ili wakapande daladala. 

Tesha alikuwa anajua kuhusu ishu yangu na Dina, maana yeye ndiye aliyekuwa mtengeneza mitambo, lakini ingawa nilitembea kwa ukaribu na wawili hawa sikuonyesha hulka yoyote ile kumwelekea Dina, ambaye naye alitulia kama vile haikuwa yeye aliyekuwa amekunywa glucose zangu. Nilipendezwa zaidi kuwasikiliza Miryam na Doris walipokuwa wakizungumza kirafiki sana. Sanasana Miryam. Yaani alijiachia kiasi, nikaanza kuona utu wake mwingine uliojaa uchangamfu alipotaniana kidogo na mwenzake na jinsi alivyofurahia sana ushirika wake. 

Nilipenda mno yaani kumwona akifurahi, mara kwa mara nikimtazama kwa kuibia ili niendelee kuhisi raha niliyokuwa nahisi kwa kumwangalia tu, na kiukweli mpaka nikajishangaa. Yaani, nilikuwa tu nimeanza kujihisi kuwa mtu mwingine kabisa pindi zote ambazo ningekuwa karibu na mwanamke huyo, na ni kitu nilichokuwa najaribu kupotezea sana lakini, hakikuwa mbali na mimi kabisa; hasa kwa pindi kama hii. 

Tulipowafikisha barabarani na kuwaacha wakivuka kwenda kuchukua usafiri, sisi watatu tukaanza kurudi nyuma. Tukiwa njiani, Tesha akawa akizungumzia hasa kuhusiana na mechi ya kesho.

"Dah, kaka! Nina hamu kubwa kinyama ya kuitazama hiyo mechi pamoja nanyi wote, yaani naona kama kesho haifiki," Tesha akasema hivyo.

"Itafika tu. Me mwenyewe nina hamu kweli," nikamwambia hivyo.

"Tena na hivi Adelina wako anakuja? Bia kama zote tukishashinda. Najua umejiandaa," Tesha akaniambia.

Nikacheka kidogo kwa pumzi na kutikisa kichwa.

"Adelina ndiyo nani?" Miryam akawa ameuliza.

"Ni dada yake na yule Joy," nikamwambia.

"Ahaa... sawa," bibie akasema hivyo.

"Haumjui na yeye?" Tesha akamuuliza.

Miryam akatikisa kichwa kukubali.

"Umeshawahi kumwona," nikamwambia hivyo Miryam.

"Wapi?" akaniuliza.

"Aliwahi kuja kwa Ankia. Siku ile tumeacha funguo na Tesha kwa Ankia, ulipokuja kuzichukua uka..."

"Oooh, sawa. Yule dada mrefu mrefu?" Miryam akaonyesha kukumbuka.

"Yeah," nikamjibu.

"Ndiyo dada yake na Joy kumbe?" akauliza.

"Eeeh, ndiyo dada yake. Kesho anakuja. Anamwelewaga kweli JC, lakini jamaa hamtaki," Tesha akasema hivyo.

Nikamwona Miryam anatabasamu kiasi na kutikisa kichwa chake, nami nikamsukuma Tesha begani kidogo na kumwambia, "Acha mambo yako wewe. Yule dada ni rafiki yangu tu. Me sinaga hizo habari kabisa."

Niliposema hivyo, Miryam akanitazama usoni kwa ile njia ya kuhukumu huku akitabasamu, nasi kwa pamoja tukacheka kidogo.

Tesha akasema, "Ila vibe kama lote akija, na yeye apunguze stress na nini, si unajua? Halafu da' Mimi..."

"Mm..." Miryam akaitika.

"Si na wewe tu uje na sisi kuangalia mechi kesho?" Tesha akasema hivyo.

Nikamwangalia bibie. Hilo lilikuwa wazo zuri!

Miryam akasema, "Sidhani kama nitakuwa na muda..."

"Aaaa, kesho si Jumapili? Tena mechi saa moja jioni... unaenda wapi kwani?" Tesha akasisitiza.

"Siwezi kujua nitakuwa wapi, siwezi kujua. Na... mnaenda kwenye klabu kuangalia mechi, si ndiyo? Me siwezi kwenda huko," Miryam akasema hivyo.

Mimi na Tesha tukacheka kidogo, nami nikamwambia, "Ni Masai tu hapo Miryam. Siyo klabu. Itakuwa fresh ukijiunga nasi, usikilize falsafa za mpira na nini..."

Miryam akanitazama usoni na kutabasamu kiasi. Alikuwa ameelewa upana wa maana ya maneno yangu, nami pia nikatabasamu kidogo.

"Eeh Mimi... uje tu. Na we' dada unahitaji kutuliza stress, eh? Nimemiss sana kipindi kile ulipokuwaga unakuja na sisi Masai kunywa kidogo, unatetemesha macho ya watu, safi," Tesha akasema hivyo.

Miryam akatabasamu zaidi. Nilipenda sana kumwona namna hiyo.

Tesha akasema, "Baada ya huo upuuzi wote wa Joshua, dada unahitaji kutuliza akili na wewe from time to time, au siyo? Kesho ndo' nafasi nzuri sana..."

Nikaona Miryam akiweka uso wa kuishiwa pozi kiasi, na najua hilo lilisababishwa na mdogo wake kumsema Joshua. Nikamfinya Tesha mkononi kwa nguvu, naye akanitazama kimaswali na mimi nikamkunjia sura kama kumwambia ameenda mbali mno. 

"Sawa, nitakuja kesho," Miryam akasema hivyo.

Sote mimi na Tesha tukafurahi sana baada ya kusikia hivyo.

"Ila mie sinywi bia, nakunywa wine. Kwa hiyo mjipange," Miryam akatania.

"Ah, ondoa shaka Mimi. JC yupo... na yupo tayari," Tesha akasema hivyo.

Nikamkata jicho kali kimasihara, naye Miryam akatabasamu kwa hisia. 

Alifanya nihisi furaha sana baada ya yeye kusema angejiunga nasi kesho, na Tesha ndiyo akaanza kuniambia kuwa dada yake ni mpenzi wa Yanga kama Ankia lakini aliachana na ushabiki wa mpira kitambo tu, hivyo tungehitaji kujua kesho angekuwa upande upi. Akasema ingawa hakufatilia mipira sana, bado aliipenda Yanga, kwa hiyo kesho angekuwa mtani na adui yetu sisi wanasimba.

Tukawa tumefikishana makwetu hatimaye, nami nikaagana na wawili hawa na kwenda huko kwa Ankia kupumzika nikiwa nahisi furaha sana moyoni. Furaha ambayo ilikuwa inazidi kukua tu kwa kutambua jambo fulani jipya lililokuwa limetokea ndani yangu mimi mwenyewe, lakini bado uhakika wa ikiwa ningetakiwa kuendelea kuifurahia hiyo furaha ndiyo sikuwa nao. Nikatumia muda mfupi tu kupeana ushirika na Ankia, kisha ndiyo nikaelekea kulala.


★★★


Jumapili ikakucha. Nilijitahidi kuamka mapema hasa kwa kuwa nilijitahidi kulala mapema pia, na baada ya kumaliza usafi wa mwili, nikatia viwalo vya ukweli mwilini, Tshirt jeupe la mikono mirefu na suruali nyeusi ya jeans, saa yangu kali mkononi pamoja na kiatu changu cheupe miguuni, nami nikakaribishwa chai kavu ya mapema na mwenye nyumba wangu ambaye kama kawaida yake alikuwa ameshaamka na kuanza kuandaa mambo. Ilinibidi ninywe kavu tu kwa sababu hakukuwa na kitafunwa, na hata alipotaka kunifatia mkate nikamwambia asiwaze.

Hii ikiwa ni saa mbili na nusu asubuhi, nikachukua simu yangu baada ya kumaliza kupasha tumbo ili niende sasa kuwapitia wakina Bi Zawadi, na sikukuta simu wala jumbe yoyote ile kutoka kwa madam Bertha, ikionekana bado kanuna, hivyo nikamrushia sms fupi ya salamu nikimwambia nimem-miss. 

Waliokuwa wamenitafuta tayari asubuhi hii ilikuwa ni yule Kevin, Dina, Bi Zawadi, pamoja na Soraya, na aisee Soraya nilikuwa nimemtenga sana. Ila hata sasa nikaamua kuachana na hao wengine na kumpigia Bi Zawadi kumwambia ninakuja sasa hivi, kisha ndiyo nikamuaga Ankia na kuondoka hapo. 

Kabla sijalifikia geti, Adelina akawa amenipigia, nami nikatabasamu kiasi na kupokea. Alianza kwa salamu na kusema sasa hivi alikuwa anaenda ibadani, nami nikamwambia vilevile na mimi pia nilikuwa naelekea kwenye ibada. Akagusia kuhusu suala la kuja huku baadaye kwa ajili ya kujiunga nasi, akisema sanasana jioni, nami nikamwambia angetukuta tunamsubiri kwa hamu, kisha tukaagana vizuri kwa utani kidogo.

Nilipofika getini kwa majirani zetu, nikakuta bado kimlango cha geti kikiwa kimefungwa kwa ndani, kwa hiyo nikagonga na kusubiri. Aliyekuja kunifungulia alikuwa Tesha, na mwonekano wake uliniambia kwamba yeye pia alitaka kutoka. Alivaa vizuri yaani, na kiatu mguuni, nami nikauliza ikiwa na yeye angekwenda kanisani ama alikuwa amejiandaa ili aende kwa Happy huko Tandika.

Ndiyo akaniambia kwamba wote tulikuwa tunaenda kanisani leo, ukitoa tu Bi Jamila na Shadya, kuanzia mimi, yeye Tesha, Mariam, Bi Zawadi, pamoja na Miryam, tungekwenda huko kanisani. Lilikuwa jambo zuri sana kuwaza kuwa ningepata nafasi zaidi ya kuwa karibu na Miryam kwa leo, basi tu yaani nilipenda. Nikamwambia jamaa hiyo ilikuwa poa sana, na ilieleweka kwa nini Bi Jamila angebaki, pamoja na Shadya ambaye angemsaidia kwa mambo ya hapa na pale mpaka wakati ambao tungerejea.

Walikuwa wameshakunywa chai tayari, yaani Tesha akaniambia Miryam alikuwa ameshughulika na mambo mengi upesi sana kwa asubuhi hii mpaka wote kukamilisha maandalizi, kwa hiyo nilikuwa nikisubiriwa mimi tu ili twende. Na kweli kabla hata sijaenda ndani, binti Mariam akawa ametoka, akipendeza kwa kuvalia gauni refu jekundu na kilemba kichwani kama mwanamke yaani, nasi tukasalimiana vizuri na yale ya jana kuonekana kuwa yamesahaulika kwake.

Wakafata na wengine pia, Bi Zawadi akipendeza kwa gauni la kitenge lenye rangi mchanganyiko za mimea, na bibie Miryam akiwa amevaa gauni refu la samawati lililokuwa laini na lenye mtindo wa kufunika bega moja, na lingine wazi. Aliziachia nywele zake laini mpaka mgongoni, akiwa amezilainisha zaidi kwa mafuta nafikiri, nami nikajikuta nimebaki kumtazama tu kwa upendezi wa hali ya juu mno. 

Miryam alikuwa mrembo jamani! Halafu wala, yaani ni kama hata alikuwa hana habari na hilo. Kukamata mpaka hisia za mwanaume hatari kama Festo, sidhani ikiwa huyu mwanamke alielewa ama kujali ni namna gani alivyokuwa na mvuto mkubwa sana wa kumfanya amiliki ama kuwa katika sehemu za gharama ya hali ya juu. Yaani, alikuwa wa gharama, lakini alipenda kuwa simple. Familia yake kwanza, na hilo ndiyo lililomwongezea mvuto si kwenye urembo wa sura yake tu, bali na utu wake pia.

Nikasitisha kumwazia sana baada ya Shadya kututaka tupige picha za pamoja kwanza kabla ya kuondoka, na Miryam alikuwa hataki lakini Mariam akamlazimisha. Tukapiga picha kwa pamoja usawa wa gari la bibie, na ndiyo lingetumiwa kutupeleka mpaka Chamgando, hivyo tulipomaliza tukapanda na Miryam akaliondoa hapo. Nikawa nimeketi siti za nyuma pamoja na Tesha na Mariam, tukipiga story na Bi Zawadi aliyekuwa ameketi mbele na bibie Miryam, na safari ya kwenda kanisani ikaendelea. 

Siku ya leo ilionekana kuelekea pazuri mno, nilihisi hivyo. Matarajio mengi niliyokuwa nayo baada ya mikasa yote mibaya ya pembeni kuisha, yalikuwa niwe na pindi zenye kuburudisha na kujenga kama hii tu ya sasa, na kwenda kumwomba Mungu abarikie hilo kwa leo ndiyo ingekuwa jambo kuu.

★★

Basi, tukawa tumefika huko Chamgando kwenye mida ya saa nne, tukiwa tumekawizwa kiasi barabarani kutokana na msongamano wa dakika kadhaa. Tulifika kanisani na kukuta mchungaji akiwa ameshaanza maombi yake, ibada ile ya kutoa hotuba, na yaani ujio wetu hapo ulifanya wadau watutazame mno kutokana na kuonekana kuwa kama familia moja ya wanajamii wa hali ya juu. Watu walikuwa wengi kiasi kwa hii Jumapili tofauti na ile Alhamisi nilipokuja hapa na Bi Zawadi, na mama huyu alikuwa na furaha sana sisi wote kuwa pamoja naye sehemu hiyo. 

Tukaachiwa nafasi za kukaa, mimi nikiwa katikati ya Bi Zawadi na Mariam, kisha Miryam na Tesha pembeni zaidi, naye mchungaji akaona akatishe hotuba yake kwa ufupi ili kutupa nafasi ya kujitambulisha kwa waabudu wengine. Najua wengi walikuwa na hamu ya kutusikia wageni tukijitambulisha, na kwa sababu nilijua Mariam angehisi uzito kiasi wa kutojua ya kusema, nikaona nisimame kwanza huku nikimshika mkono, kwa hiyo na yeye akasimama pamoja nami.

Nikasema jina langu, mahali tunakoishi pamoja na huyu mdogo wangu, na shukrani kwa mchungaji kutukaribisha hapa kwa ajili ya ibada, nao waamini wakanipigia makofi kwa shangwe. Nikamnong'oneza Mariam kuwa aseme jina lake, naye akajitahidi kusema 'ninaitwa Mariam' kwa sauti iliyosikika vyema, na Tesha akaanzisha kupiga makofi yaliyofanya wengine pia wajiunge naye. 

Tukakaa huku nikimwekea Mariam kiganja changu karibu naye kwa chini, naye akaweka chake kwangu huku akitikisa vidole na kunionyesha ishara kwa mdomo wake 'broop,' kitu ambacho kikafanya nitabasamu kwa furaha. Wengine pia wakafata kujitambulisha, nafikiri sauti ya Miryam alipokuwa akiongea ikiwafanya waumini wa hapo wajiulize ikiwa alikuwa anashindia mayai mabichi ya kienyeji kila siku, na baada ya hapo ibada ikaendelea.

Ilikuwa ni kusikiliza hotuba, kutoa sadaka, kufanyiwa maombi ya hapa na pale, na sisi pia tulinyanyuka kwenda kuombewa. Kwa kuwa sakafu lilikuwa la michanga, waliweka mikeka chini kwa wale ambao wangelala kabisa, lakini mimi na Tesha tukakaza, hakuna kwenda chini. Vile ambavyo wachungaji husukuma kichwa taratibu huku wakiombea mtu ilifanya Mariam, Bi Zawadi, na hata Miryam waelekee chini, kwa hiyo mimi na Tesha tukasaidia kuhakikisha hawaanguki ama kuchafua nguo zao. 

Aisee! Kuna wadada wawili baada ya sisi kuwa tumerudi kukaa waliokuwa wamepagawa na mapepo. Walipiga kelele huku wakiwa wamelala chini na kugaagaa mchungaji alipokuwa anashusha zile 'toka katika jina la Yesu!' Mariam mpaka akaogopa na kunishikilia kwa nguvu mkononi, kwa sababu mmoja wao alikuwa akija upande wangu, yaani ni kama vile pepo lilikuwa linataka kumtoka halafu liingie kwangu sijui?!

Basi nikageuka kumwangalia Tesha na kukuta amenikazia macho huku akibana tabasamu, nami nikashindwa kujizuia na kutazama pembeni huku nikijitahidi kubana kicheko kilichokuwa karibu kunipasukia mbele za watu wote. Ingepaswa kuwa pindi yenye kugusa sana, lakini kila mara jicho langu lilipokutana na la Tesha, ilikuwa ngumu ku-focus, ila nikajitahidi kujidhibiti. Akili zetu hizi zilijuana zenyewe tu.

Kwa hiyo ibada ikaendelea mpaka kufikia mida ya saa saba na nusu hivi, ndiyo ikafikia hitimisho. Na tulilazimika kutoa sadaka kwa mara ya pili ili kuchangia maendeleo ya kanisa, kisha ndiyo sote tukatoka hapo ndani na kuelekea nje. Baadhi ya waumini walitusalimu kwa heshima sana, na wengine wakionekana kutuogopa sijui, nasi tukawa tumeletewa viti na kuambiwa tukakae kivulini ili kumsubiri mchungaji na mama mchungaji kwa ajili ya maongezi machache.

Tukaletewa na soda kabisa baada ya kukaa, nasi tukaendelea kusubiri huku tukipiga story pamoja na Bi Zawadi hapo kuhusu jinsi gani tulijisikia baada ya ibada kuisha. Aliyeanza kuja ilikuwa ni mama mchungaji, naye akaketi pamoja nasi baada ya kutusalimia vizuri sana na kuanza kujuana na wengine tuliokuja nao leo mmoja baada ya mwingine. Mchungaji bado alikuwa akihudumia watu fulani kule ndani kwa hiyo naye angekuja baada ya muda mfupi.

Mama mchungaji akaongea na Tesha, akajaribu pia kumsemesha Mariam na kuambiwa kuhusu changamoto zake. Alikuwa amemtia moyo Tesha kwamba angekuja kupata kazi nzuri sana na kuoa mapema mno, ndoa yaani, na alimwambia Mariam kwamba ndani ya kipindi kifupi tu kila jambo baya ambalo limewahi kumpata lingebaki kuwa historia ambayo hakuna mtu angekuja kuikumbukia, kwa sababu na yeye angefika sehemu nzuri sana maishani.

Akaongea na Miryam pia. Kama kawaida ya mwanamke huyu, hakusema mengi sana zaidi tu ya yeye kuwa nani na upendo wake kwa familia yake yote, lakini inaonekana mama mchungaji na maono yake alikuwa ameshaona vitu vingi. Miryam alifanya ionekane kwamba alikuwa poa kabisa, lakini mama mchungaji akasema kitu ambacho kilizunguka mno hata kichwani kwangu. 

Akamwambia, "Una nguvu, na moyo mzuri sana binti yangu. Lakini bado kuna sehemu ndani ya hatma ya maisha yako imefichwa ndani sana ya gamba gumu kama la kobe, na wewe unaogopa kwamba ikitoka nje... utaumia. Kwa Mungu hakuna kuogopa. Na ninaona Mwenyezi Mungu akikuandalia njia itakayokusaidia ili uwe huru zaidi, hatma hiyo isijifiche tena. Wewe uko sawa kabisa Miryam. Hauna tatizo la kimwili au kiroho. Lakini, hakuna mwanadamu aliye kamili kwa kila jambo, ndiyo maana tumeumbwa wawili-wawili ili kuweza kusaidiana, kukamilishiana yale mambo ambayo hatuwezi kukamilisha sisi kama sisi. Mungu amekuandalia njia iliyo kama zawadi ya kukukamilishia, na hatma hiyo kufunguliwa. Amini kwamba utaipata, na maisha yako yatajaa amani na furaha ukishaitambua zawadi hiyo kutoka Kwake."

Baada ya maneno hayo yaliyokuwa yamejaa fumbo fulani, Miryam akasema tu 'amen,' vilevile na Bi Zawadi, halafu mama mchungaji akatabasamu kiasi na kunitazama machoni kwa umakini. Mimi pia nilikuwa namwangalia, na sijui ni kwa nini tu lakini ni kama vile alikuwa akijaribu kuwasilisha kitu fulani kwangu ambacho sikuelewa, nami nikamtazama Miryam kwa utafakari. 

Sijui maneno ya huyo mama yalinihusisha na mimi? Nilijikuta nikitaka kuhusika yaani, maana aliongea kama mganga, au mtabiri fulani hivi au nabii, na kiukweli sikuwaga mtu wa kuamini sana hivi vitu lakini kwa wakati huu, vilinisisimua sana. Mawazo mengi yalikuwa yanapita akilini. Mengi mno. Bila matarajio yoyote kabisa, simu yangu ikaanza kuita, na baada ya kutazama aliyekuwa akipiga, nikakuta ni Festo. 

Ikanibidi ninyanyuke na kwenda pembeni kwanza, kisha nikapokea. Jamaa aliongea kifupi tu, akisema amepata nafasi ya kukutana na mimi, na alitaka niende kule kule kwake walikonipeleka watu wake kipindi kile; ndiyo tungekutana huko. Sikujua ikiwa ningepakumbuka vizuri, lakini nilijua ilikuwa huko Kawe, hivyo nikamwambia 'sawa, ninakuja.' Akasema isipite saa kumi jioni sijafika huko, maana alikuwa na ratiba zingine, kisha ndiyo akakata. Doh! 

Hapa ningehitaji kuwakimbia hawa marafiki zangu maana tayari ilikuwa saa nane, na kutoka huku mpaka huko Kawe ingekuwa ni mwendo mrefu mno. Lakini nikawafata tu wote na kuwaambia kuwa kuna dharula ilikuwa imetokea na nilihitajika mahala fulani mara moja, kwa hiyo ningetangulia kuondoka. Bi Zawadi alionelea ingekuwa vizuri kumsubiria mchungaji kwanza, lakini nilipomwangalia Miryam usoni kwa njia ya kumaanisha jambo fulani, nafikiri akaelewa ni mambo yaliyohusiana na ishu yangu na maaskari.

Kwa hiyo bibie akanisaidia kwa kumwambia tu mama mkubwa wake kwamba inaonekana ni dharula ya wagonjwa na nini, hivyo ningetakiwa kuwahi ili kuokoa uhai. Bi Zawadi aliporidhia, nikawaaga wote vizuri na kuomba samahani kwa mama mchungaji kwa sababu ya kutakiwa kukimbia kwa mara nyingine tena leo, naye akasema haikuwa na shida. Tesha akanikumbusha kutochelewa sana ili jioni wasinikose kwenye kujumuika pamoja, nami nikakubali na kutimka upesi.

★★

Yaani ilikuwa ni kutimka upesi kwelikweli, tena kwenda kwa mtu niliyemwona kuwa adui. Ilinibidi nipande bodaboda kutokea Chamgando mpaka barabara kuu, kisha nikapanda tena bodaboda mpaka Mbagala. Kutokea Mbagala tena, nikapanda bodaboda kwa kumlipa jamaa elfu kumi anikimbize mpaka Kawe, na nikafanikiwa kufika huko ikiwa imeingia saa tisa alasiri.

Nikamwongezea kiasi kingine ili anisogeze maeneo ya ndani zaidi, nikijitahidi kukumbuka njia ya kupita, na hatimaye nikafanikiwa kuiona nyumba ya Festo kwa umbali mfupi shauri ya ukubwa na ughorofa wake. Nikamwambia boda asimame tu, nikashuka, kisha akarudi alikokuwa ametoka. Nilitaka kuhakikisha hakuna ufatiliwaji na yeyote yule mpaka huku, kwa hiyo nikatembea taratibu na kwa uangalifu kuelekea upande wa nyumba hiyo.

Nikawa nimefika nje ya geti hatimaye, na nyumba ilionekana kuwa kubwa na nzuri zaidi ya mara ya kwanza kabisa nilipoletwa hapo. Nikampigia simu Festo kumjulisha kwamba nilikuwa getini, naye akasema sawa na kukata. Mazingira ya eneo hilo yalikuwa na miti na barabara nzuri sana ya lami, kukiwa na majengo mengine mazuri lakini si kwa umaridadi wa hali ya juu kama hili. Na hakukuonekana kuwa na wapita njia wengi, zaidi ni magari tu ndiyo yaliyofanya mizunguko mara moja moja.

Sekunde chache baada ya Festo kukata simu, geti la hapo nje likafunguliwa na yule yule mlinzi wa siku ile, nami nikaingia taratibu huku nikisikia kelele za mibweko ya mbwa kutokea sehemu aliyokuwa amefungiwa, na magari manne ya kifahari yakipumzika maegeshoni. Mlinzi akaniambia niende tu mpaka huko ndani, nami nikatii.

Mdogo mdogo tu, nikiwa nakumbuka vizuri pa kwenda hadi kuifikia sebule ile maridadi ya jamaa, nami nikawa nimeifikia. Halafu milango ya kuingilia hapo ilikuwa inafunguka kama vile milango ya lifti ifanyavyo, na muundo ulikuwa wa aina hiyo hiyo kabisa; chuma. Festo kweli alijua kujilinda, yaani kufika huku ndani ilikuwa ni kama nimetokea eneo tofauti kabisa na hii nyumba hapo hapo nje. Kwa hiyo nikabonyeza kitufe cha kengele na kusubiri, halafu milango hiyo ikafunguka, kisha ndiyo nikapenya ndani.

Mwonekano mzuri wa sebule pana ya hapo bado ulikuwa vile vile kabisa, isipokuwa wakati huu nikakuta kitu kimoja tu ndiyo kimebadilika; yule mpishi aliyekaa sehemu ya jikoni. Nilimkumbuka vizuri mpishi yule niliyemkuta kipindi kile, Shefu Saidi, ambaye hadi tulipeana namba za mawasiliano na kuna nyakati ndani ya huo mwezi mmoja tulikuwa tumewasiliana kupeana salamu na nini, lakini wakati huu haikuwa yeye niliyemkuta hapo.

Wakati huu alikuwepo jamaa mwingine, mweupe, mwenye mwonekano usiotoa ujumbe wowote kwamba alikuwa mpishi wa kawaida tu. Yaani alijazia, jinsi ambavyo aliniangalia ilikuwa kama vile ana njaa ya kutaka kunichinja, na alikuwa ameshikilia visu viwili akivinoa-noa tayari kukata-kata nyama iliyokuwa kwenye ubao mdogo juu ya sinki. Nikashindwa hata kumsalimia na kusimama tu kwa utulivu huku nikimtazama kwa umakini, na yeye akinikazia macho yake kikatili fulani hivi.

"JC..."

Nikageuka baada ya kusikia sauti ya Festo akiniita hivyo na kumwona akiwa anashuka kutoka juu ya ngazi zilizoelekea ghorofani. Mwamba alikuwa amevalia kwa njia iliyoonyesha kuwa alitoka kupiga tizi, labda kwenye gym ndogo hapa hapa kwake iliyokuwa huko juu, kwa sababu alikuwa ametia nguo za mazoezi mwilini zilizolowana kiasi, na zilizokuwa na rangi ya kijivu. Alikuwa pia amevaa glovu mikononi, na alishuka ngazi huku akizivua na kufungua bandeji zilizofungwa viganjani.

"Festus..." nikaita hivyo pia, kama kurudisha ile 'nimekuona.'

"Niite tu Festo. Festus ina-sound kama mtu fulani hivi ambaye simpendi," akasema hivyo kiutani.

Nikatabasamu kiasi na kumwambia, "Basi inawezekana hauko peke yako."

Akatabasamu kiasi pia na kunifikia, naye akanipiga ngumi kidogo begani kwa njia ya kirafiki na kunipita, akielekea kule kwa mpishi. Nikaendelea kumwangalia tu mpaka huyo mpishi alipompatia chupa ndogo ya maji kutoka kwenye friji, naye Festo akaanza kunywa.

Alipotosheka, akaishusha na kusema, "Unajua kukariri maeneo, nilifikiri ungepotea."

"Niko makini na kila kitu kinachonizunguka," nikamwambia hivyo.

Akaniangalia na kusema taratibu, "Is... that... right?"

"Ahah... well, I try," nikamwambia.

"Unajitahidi. Kazi zako zote na Bertha mpaka sasa, very impressive..."

"Asante."

Akaanza kunifata huku akisema, "Na nina-suppose kilichokuleta hapa ni ili uongelee ishu inayom-concern... mwanamke wako?"

"Ni... vitu vingi, ila..."

"Make it quick, friend. Nataka ku-bounce," akanikatisha kwa kusema hivyo.

"Ooh, kuna sehemu unaenda?" nikamuuliza.

"Yeah, so niambie. Unahitaji nini ambacho hungeweza kusema kwenye simu tu mpaka unione?" akauliza huku akianza kunywa maji tena.

Nikamwambia, "Nime... nilifikiria maneno ambayo uliniambia siku ile... na... nataka unisaidie."

"Maneno gani?" akauliza baada ya kumaliza kunywa maji.

"Uliniambia nikiwa kwenye hili game, sipaswi kuwa mtu vulnerable. Natakiwa niwe na means... njia yaani, za kujilinda ili nisiwe mtu rahisi kurukiwa," nikamwambia hivyo.

"Hmm... na hiyo ni baada ya mwezi mzima kupita? Nini kimekupa motisha ya kutaka kuwa na hiyo... means?" akaniuliza.

"Game lenyewe tu, Festo. Huwezi kuwa mwangalifu sikuzote," nikamwambia.

"No, no... nataka uniambie. Niambie ikiwa unahisi kuna mtu, au watu... wanataka kukurukia," akaongea kwa msisitizo.

"Siwezi kusema ni mtu fulani kwa uhakika, ila ndo' point yenyewe. Kutojua tu ni nani anaweza akanirukia ni sababu tosha ya kujua kwamba naweza nikarukiwa na yeyote. That's why nahitaji kujilinda mimi mwenyewe badala ya...."

"Kutegemea Bertha ndo' akulinde?" akanikatisha kwa kuuliza hivyo.

Nikaangalia pembeni.

"Ikiwa unataka hiyo means kutoka kwangu moja kwa moja, inamaanisha Bertha hajui kwamba uko hapa, si ndiyo? Na kwa sababu fulani, hautaki ajue," Festo akasema hivyo.

Nikamtazama tu usoni kwa umakini.

"Napata hisia kwamba kuna kitu unanificha, JC. Na unajua, huwa sipendi... kufichwa vitu, ama vitu kufanywa nyuma ya mgongo wangu na watu ambao ni wangu. So kama kuna chochote unajua napaswa kujua ila unahofia kuniambia, ni bora useme sasa hivi... la sivyo nikijua mimi mwenyewe, haitakuwa nzuri kwako mbeleni," akaniambia hivyo.

Nikatulia kidogo, kisha nikamwambia, "No. Hakuna kitu chochote kikubwa namna hiyo. Nataka tu kujilinda. Mimi kama mimi. Basi."

Akiwa amenikazia macho, akauliza, "Are you sure?"

"I'm sure," nikamwambia kwa uhakika.

Akasema, "Okay. So unataka nikupe piece moja?"

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Utaweza kutumia?" akauliza.

Nikatikisa kichwa tena kukubali.

Akaangalia pembeni kiufupi na kusema, "Xave..."

"Boss..." yule mpishi akaitika.

"Niletee taurus moja. 9mm," Festo akasema hivyo.

Nikamwangalia huyo "mpishi" alipotoka sehemu ya jikoni na kuja upande wetu huku akiniangalia kwa macho makini, naye akatupita na kuelekea upande wa vyumba vingine huko mbele; siyo ghorofani yaani.

"Bado uko Mbagala?" Festo akaniuliza hivyo.

"Ndiyo. Kwani haujui hilo?" nikamuuliza pia.

"Najua."

"Ooh, unamaanisha... pale kwa Miryam na nini?"

"Yeah. Anaendeleaje?" Festo akaniuliza hivyo kwa sauti ya chini.

"Yuko poa. Si bado mnawasiliana?" nikachimba.

Akavuta pumzi na kuangalia pembeni, naye akasema, "Bado, JC. Bado ananigomea, yaani... nafanya mengi, ila anayasukuma mbali, sijui kwa nini tu."

"Labda... unaweza ukakuta ana mtu wake..." nikaona nimchokoze.

"Ungekuwa umeshasikia msiba," akaniambia hivyo kwa hisia kali.

Nikashindwa kujizuia kucheka kidogo kwa pumzi, nami nikajidhibiti zaidi na kusema, "Kwa hiyo una uhakika hana mtu? Basi. Komaa tu."

"Unajua nini...."

Kabla Festo hajamaliza kuongea, mpishi Xave akawa amerejea na kutufikia karibu, naye akampatia Festo bastola yenye mwonekano mpya wa chuma yenye rangi ya shaba kwa juu na nyeusi kwenye kishikio na kisha kuondoka. We! Kitu chenyewe yaani, chuma chuma, kikiwa kifupi kiasi kutoshea vizuri kuficha kiunoni ama mfukoni mwa suruali kabisa, naye Festo akainyanyua hewani akiielekeza juu, huku akinitazama kwa utulivu.

"Subira huwa ni kitu muhimu maishani. Siyo wote wenye vitu kama vyangu wanavipata baada ya kuzaliwa tu, wengine tunahangaika mno mpaka kufika tunapofika... ndoto zetu kutimiza. Iwe unataka kujilinda, au kupata pesa, au kupata gari, au kufika sehemu fulani na kitu chochote unachokipenda, unahitaji subira, na ku-time vizuri mambo yote ili ufanikiwe kutimiza ndoto yako... na isikuponyoke kamwe," akaniambia hivyo.

Nikiwa namtazama kwa umakini, nikamwambia, "Na hiyo inamaanisha kwa mtu nayempenda pia. Bertha, na wewe Miryam vilevile."

"Yeah. Kama ni msemo naopenda zaidi maishani mwangu, ni kwamba maamuzi magumu sikuzote huwa yanatuhitaji tuwe na nia zenye nguvu sana ili kuyachukua, na ukiyafanya ukafanikiwa kupata unachotaka... hautakuwa mtu wa kupoteza lolote. Never," akaniambia hivyo huku akinikabidhi bastola kiganjani.

Nikaipokea bastola hiyo na kuishikilia kwa uangalifu, nikiwa natafakari maneno yake. Kwa njia fulani niliona kwamba alikuwa akizungumzia jambo lingine kabisa, jambo fulani zito, na ilipofika kwenye suala la maamuzi, alikuwa sahihi. Ni kama vile tu ambavyo mimi nilikuwa nimeamua kuchukua uamuzi huu wa kuwa daktari-mtembea-na-bastola kuanzia sasa, kitu ambacho sikuwahi kudhani kabisa kwamba kingekuja kuingia akilini. 

Maisha yangu yalikuwa yananibadilisha kwa kasi sana, ndani ya kipindi kifupi tu yaani nilikuwa nimejikuta ndani ya mambo mengi yenye kutatanisha, lakini haya ndiyo yalikuwa maamuzi magumu kweli yaliyoonyesha nina nia yenye nguvu ya kuyachukua. Kwamba hata kama ingehitajika kuua, basi nilikuwa ndiyo najiandaa kwa ajili ya hilo. Aloo! Siyo mchezo.

Nikiwa nimeishikilia bastola hiyo kwa viganja vyangu, Festo akauliza, "Umeshawahi kutumia hii kitu, JC?"

Najua alikuwa anataka kuhakikisha ikiwa naelewa kile ambacho nilikuwa nimejiingiza kufanya, nami nikamwambia, "Sijawahi kuitumia kuumiza mtu, ila najua kutumia."

"Wewe ni daktari, my boy. Umeundwa kutibu majeraha, siyo kuyasababisha. Ikitokea ukahitaji kuitumia kuumiza mtu... utaweza?" akaniuliza.

Nikamwangalia usoni kwa umakini, nami nikaikoki bastola hiyo kwa makusudi, kisha nikasema, "Asilimia mia."

Akaachia tabasamu la pembeni na kisha kusema, "Uwe care, usije kuitumia kifala kabisa. Chuma zangu zote siyo traceable, kwa hiyo ikitokea ukatia mtu yeyote risasi, la muhimu ni wewe kutogundulika. Ukigundulika hata kwa kutembea nayo tu ndiyo imekula kwako. Do you understand?"

Nikamwangalia usoni kwa umakini kiasi, nami nikamwambia, "Ndiyo naelewa. Asante. Pistol nzuri sana. Una... unanisaidia, yaani... unanipa bure... kama... vile nahisi yaani, kama unataka kuhakikisha niko care sana pia...."

"Don't get it twisted, mimi siyo rafiki yako, nakupa hii kwa sababu umeniomba. Ungemwomba hata Bertha, lakini umeona uje kwangu ili asijue, si ndiyo?" akaniambia hivyo.

Nikaangalia chini na kusema, "Yeah. Sorry. Natumaini tu itabaki kuwa hivyo lakini... Bertha kutojua."

Akasema, "Unajua... group langu lote, nimeligawanyishia himaya zao hapa jijini mpaka mikoani, na Bertha ndiyo mwenye territory kubwa... and thanks to you, ananipa faida kubwa mno kwa sababu umeifanya biashara yake imekua zaidi. So that means... wewe ni muhimu. Hatutataka lolote likuhatarishe, and to be honest... najua kuna watu wanaweza wakataka kukumaliza, ila ndiyo sijui wa kumnyooshea kidole kwa uhakika. Sipendi kusingizia. Ikiwa unahisi kuna shida ndani ya network yangu me mwenyewe, niambie. Singependa uje uchukue maamuzi mabaya kwa mikono yako bila utambuzi wangu, ndiyo maana nakwambia kama kuna shida sehemu, iseme. Ukifikiri utaweza kuhandle kila kitu peke yako kwa sababu una kipisi mkononi... then bado hujaelewa jinsi hili game linavyofanya kazi mdogo wangu. Sikwambii haya kwa sababu nakujali, ila kwa sababu sitaki kazi zangu zichafuke. Nina nguvu yote ya kukusaidia ukitaka, ila usipotaka hilo... halafu mambo yangu yakaharibika, ujue kwamba mimi ndiyo nitakuharibu wewe. Umenipata?"

Alikuwa ameongea kwa ile njia ya kutikisa yaani, nami nikatikisa kichwa kwelikweli kuonyesha uelewa.

"Haya nenda. Ikiwa ni hayo tu..." akaniambia hivyo.

Nikaichomeka bastola mbele ya kiuno changu na kusema, "Sawa. Asante. Sijui sana kuhusu shift za hapa, ila utamfikishia na Saidi salamu zangu..."

"Saidi ndiyo nani?" Festo akaniuliza hivyo.

Nilikuwa nimeshaanza kuondoka, lakini nikasimama kwanza na kusema, "Saidi... yule chef mwingine. Nilikuwa namaanisha, akija kwenye shift yake labda...."

Festo akatabasamu kiasi na kumwangalia yule mpishi wake kule jikoni, ambaye alikuwa anakatakata nyama huku ananitazama kwa umakini.

"Au aliacha kazi?" nikamuuliza hivyo Festo.

Festo akaanza kuelekea kule ngazini huku akisema, "Hakuna mtu anaitwa Saidi amewahi kufika hapa. Utakuwa umekosea..."

Eh! 

Nikabaki nikimtazama jamaa mpaka alipokuwa ameanza kuzipanda ngazi, nami nikamgeukia yule mpishi Xave pale jikoni, ambaye akafanya kuninyooshea kisu kuuelekea mlango; kwamba niondoke. Maneno ya Festo yalikuwa yameiingizia akili yangu taarifa fulani ambayo haikuwa nzuri hata kidogo, na kiukweli nilihitaji kuthibitisha kama nilichofikiria alikimaanisha ndiyo kile alichokuwa amemaanisha.

Nikajaribu kumpigia Shefu Saidi mara tatu, lakini simu yake ikawa haipatikani. Nikaendelea tu kwenda mpaka nje, na wakati nikielekea getini na mlinzi, nikawaza labda nichimbe kitu kutoka kwake. 

Nikajisemesha hivi, "Nyumba nzuri kweli bro. Sisi tunatamani tu hivi vitu, wenzetu ndo' wanavipata."

Mlinzi, akiwa anafungua geti, akasema, "Ndo' maisha. Ila na wewe si ni... mvulana wa boss?"

"Ee, ndo' nimeanza-anza. Mara ya kwanza nililetwa nimefungwa macho kabisa," nikamwambia hivyo.

Akatabasamu kiasi na kusema, "Nakumbuka. Mtu mkubwa ana mambo makubwa, ndiyo hayo sasa. Shukuru tu haukufa."

Nikajichekesha kidogo na kutoka sehemu hiyo ya getini, nami nikamuuliza, "Halafu, unamkumbuka yule mpishi mwingine niliyemkutaga hapa?"

"Nani? Wako wanabadilishana. Au unamwongelea Saidi?" akauliza hivyo.

"Eeh... Saidi, sijamkuta. Ila inaonekana hajakuwepo hapa muda. Aliacha kazi?" nikamuuliza pia.

Akageuka kuangalia upande wa nyumba hiyo, kisha akaniangalia tena na kutoa ishara kwa kiganja chake, akikipitisha mara moja usawa wa shingo yake huku akinitazama kwa umakini.

Nikiwa nimeelewa alichomaanisha, nikaingiwa na hisia mbaya sana, nami nikamuuliza, "Ilikuwaje?"

"Sijui. Inaonekana alim-diss boss... akapotea," akasema hivyo.

Nikaangalia chini kwa huzuni kiasi.

Akaanza kufunga geti huku akiniambia, "Jitahidi usivuke mistari usiyopaswa kuvuka mdogo wangu, kama mimi tu. Itakusaidia usipotee mapema. Sawa?"

Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa, naye ndiyo akamaliza kufunga geti hilo.

Dah! Kwa hiyo kumbe Shefu Saidi alikuwa ameuawa, sijui hata alimfanya nini Festo baba wa watu masikini wakati alikuwa mpole na mwenye heshima sana. Jambo hili likawa limeigeuza siku yangu niliyodhani ingekwenda vizuri kuanza kuonekana kuwa mbaya, kwa sababu ya kuwaza ni namna gani Festo alivyokuwa hatari sana. 

Namaanisha kuna watu hatari sawa, ila hatari nayoongelea ilikuwa ile ambayo angekuwa nayo kwa familia nzima ya Miryam kwa sababu ya yeye kumtaka mwanamke huyo. Festo alionekana kuwa mwanaume mwenye subira sana, lakini ikiwa ungefika wakati ambao subira yake ingechoka, angefanya lolote lile ili kupata alichokitaka, na najua hilo lilikuwa karibu kutokea kwa upande wa Miryam pia. 

Haingefaa hata kidogo, kwa njia yoyote ile, mwanaume huyo awe pamoja na Miryam kimahusiano wakati nilijua alikuwa mtu wa aina gani, na Miryam kumwekea kigingi bado ndiyo jambo ambalo najua mwisho wa siku lingeweza kufanya Festo achukue maamuzi mabaya ili tu apate faida ya kulazimisha mapenzi pamoja naye. Nisingekaa kutazama tu hilo litokee. Hata kama jamaa alikuwa na nguvu nyingi kiasi gani, kwa hali na mali yoyote ile, ningehakikisha namlinda Miryam dhidi yake. 

 


★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next