MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA SABA
★★★★★★★★★★★★★★
Safari ya kurudi Mbagala ikaanza nilipofanikiwa kufika Kawe stendi na kupanda daladala ambayo ingenifikisha huko moja kwa moja. Nilijihisi upya yaani. Kutembea nikiwa nimechomeka bastola kiunoni ilinifanya nijihisi kuwa mtu mwingine kabisa, sawa sikuwa nimeitumia bado, lakini mpaka kufikia hatua hii, ni wazi nilikuwa ndani ya badiliko kubwa kwenye maisha yangu. Na nilikuwa kwenye utayari wote kuishi nalo haijalishi matokeo yangekuwa vipi. Kistelingi yaani, au siyo?
Nikiwa mwendoni mpaka kufika Mbagala, niliona nitumie muda mfupi kumsalimia Soraya. Bwana, mwanamke huyo alikuwa amenikumbuka sana baada ya yale matembezi niliyomtembezea wiki kadhaa nyuma, na alikuwa tayari kukutana na mimi muda wowote ule hata kwa gharama yake mwenyewe. Kiukweli sikuwa nimefikiria tena kuja kutoka na Soraya, yaani kuna kitu tu ndani yangu kilihitaji suala la mimi na mwanamke huyo libaki kuwa historia, na tubaki kuwa na uhusiano kama niliokuwa nao na Ankia kwa sasa.
Lakini Soraya, dah! Alijua kusisitiza mpaka ungejihisi kuwa na hatia yaani. Aliniomba sana, sana, sana, tuje kukutana tena, nami nikamwambia sawa. Ila nikaweka sharti kuwa tutakapokutana tena ndiyo ingepaswa kuwa mara ya mwisho, kwa sababu sikutaka ishu yetu ije kuibua utata mkubwa mno kati yake na mume wake, naye akaonekana kuridhika na hilo.
Nimekuja kufika Mzinga ikiwa imeshaingia saa kumi na mbili jioni, na nilikuwa nahisi njaa. Ankia akawa amenipigia simu wakati nilipokuwa nikielekea kwake kuuliza nilikuwa wapi, maana mechi ilikuwa karibu kuanza, nami nikamwambia ndiyo nakaribia kufika. Nikamuuliza ikiwa tayari Adelina na yeye alikuwa amefika kwake, lakini akasema hapana, tena kwamba mwanamke huyo alimwambia kuwa hangeweza kuja leo shauri ya kubanwa na jambo fulani.
Adelina hakuwa amenitafuta kunijulisha kuhusu hilo, kwa hiyo nikaamua kumuaga Ankia ili nimpige yeye kumuuliza kama kila kitu kilikuwa sawa. Nikampigia mara mbili, lakini hakupokea, kwa hiyo nikamtumia ujumbe nikimpa pole kwa kutingwa na kwamba tungeonana tu wakati mwingine, hivyo amalizane salama na aliyokuwa akifanya.
Nikafika kwa Ankia giza likiwa limeshaanza kuvizia, na huko nilikopita shamra-shamra za mechi zilikuwa zimeshaamka mapema sana. Kilichokuwepo hapa ilikuwa ni mimi kufika hapo kwa Ankia na kuiweka bastola hii kwa kificho huko chumbani, kisha nijimwagie upesi na kuondoka na marafiki zangu hao. Nilikuwa natarajia kwamba bibie Miryam na Tesha wangekuwa tayari pia, kwa hiyo kweli nikajitahidi kuwahi. Angalau huu ungekuwa muda ambao ungenisahaulisha kidogo mambo mengine yenye kukwaza.
Ile nimefika tu ndani kwa Ankia, nikashangaa kidogo baada ya kumkuta mwanamke huyo akiwa sebuleni pamoja na Tesha, mama Chande, na Adelina mwenyewe. Kwa jinsi tu ambavyo niliachia tabasamu hafifu huku nikimwangalia mwanamke huyo ilifanya Ankia na Tesha waanze kucheka kwa furaha, naye Adelina akawa ananiangalia huku akitabasamu. Kumbe walikuwa wananizingua tu.
"Kwa kuniona kolo kiasi hicho, eti?" nikamwambia Ankia hivyo huku nikitabasamu.
Wote kwa pamoja wakacheka kidogo, nami nikatikisa kichwa na kuufunga mlango.
"Basi karoho kalikuwa kamekuuma masikini! Umepiga na simu kabisa mwanaume, usiniambie ulikuwa karibu kulia kisa Adela hajafika..." Ankia akasema hivyo na kucheka.
Nikasema, "Yaani huna idea! Ningeahirisha kabisa kama Adelina hangetokea."
Nikasogea karibu na sehemu ya sofa alilokuwa amekalia Adelina na Ankia, naye Adelina akasimama taratibu na kunifungulia mikono yake ili tukumbatiane. Nikajitahidi kumkumbatia kwa kutoubana mwili wangu kwake kabisa, ili asiweze kuhisi ugumu kiunoni kwangu ambao ungeweza kumfanya atambue nilikuwa nimebeba bastola.
"Adelina, karibu sana," nikamwambia hivyo.
"Asante," akaitikia.
Nikamwachia na kuendelea kumwangalia usoni kwa upendezi.
Alikuwa amevalia jezi nyeupe ya Simba kwa juu, iliyombana vizuri kuonyesha unawiri wake, pamoja na suruali nyeusi iliyombana vizuri sana kuonyesha umbo lake matata kuanzia kiunoni mpaka miguuni. Alisuka mtindo fulani hivi wa nywele nyeusi zilizoviringika-viringika, nyingi zikiwa juu ya kichwa chake mpaka kufikia uso na pembeni akiwa kama amesuka mistari miwili kwa mkono. Alipendeza usoni pia na macho yake ya kungu, na kilichofanya tuache kutazamana ikawa ni mguno wa kejeli alioutoa Tesha.
"Hmmm... basi JC hapo! Wengine hatatuona," Tesha akasema hivyo.
Nikamwangalia usoni kwa kuweka macho kizembe, nami nikamwambia, "Ulikuwepo kumbe?"
Wanawake wakacheka kidogo, naye mama Chande akanisalimu, "Mambo vipi jembe?"
"Fresh, Yanga lady. Naona uko tayari kwa mechi," nikamwambia hivyo.
"Yaani kama vile nimeiandaa mie!" mama Chande akasema hivyo huku akinyanyua tatu hewani.
"Hahaaa... leo lazima watu wachezee kipigoo," Ankia akaunga.
"Kaka... tuondoke, hawa bata leo lazima tuwachinje, wamezidisha mno kelele..." Tesha akasema hivyo huku akisimama.
Mama Chande akaanza kurusha michambo kwa Tesha, Ankia akimuunga mkono pia. Wanawake hawa kwa pamoja walikuwa wamevaa jezi za Yanga juu, Ankia nyeusi, mama Chande njano, huku suruali za skinny nyeusi zikitokelezesha makalio yao vyema, nami nikaona niwaulize swali muhimu zaidi.
"Miryam yuko wapi?"
Tesha akasema, "Yupo ndani huko, amesema tutangulie anakuja. Tutamwekea siti. Twende tuwahi, patajaa."
Nikaangalia saa mkononi na kumwambia, "Bado bado, nusu saa. Ngoja nikapige maji fasta halafu..."
"Aagh, mwana unazingua! Maji ya nini? Mbona unakuwa mrembo hivyo?" Tesha akalalamika.
"We' unafikiri mwenzako mchafu kama wewe? Mwaya JC kaoge... tutakusubiri," mama Chande akaongea hivyo.
"Yaani kanavyo... JC, hakuna kununulia mtu bia hapa..." Tesha akasema hivyo kama vile ananinong'oneza, makusudi yaani.
"Nyoo... kwani me sina hela yangu? Acha dharau we'! Mashabiki wa Simba mkoje?" mama Chande akamsuta.
"Na hapo umemaanisha na JC..." Tesha akasema hivyo.
"Basi jamani, msije kutoana meno wakati mechi yenyewe bado," Adelina akawaambia hivyo.
Sote tukacheka kidogo, kisha nikawaambia, "Sikieni. Tesha yuko sahihi, tangulieni, me nipige maji kwanza halafu nitawakuta. Nafasi zitajaa mkinisubiri, ila sichelewi sana. Tangulieni nakuja, eti?"
Nilikuwa nimemwangalia Adelina niliposema hivyo, naye akatikisa kichwa mara moja huku akinitazama kwa umakini. Basi eti wengine wakaangaliana na kujichekesha kimakusudi tu, nami pamoja na Adelina tukatabasamu pia.
Huyu mwanamke alionekana... tunasema 'kunimaindi,' na mimi nikaamua tu kuachana na hilo wazo upesi kwa sababu sikumchukulia namna hiyo hata kidogo, yaani nilimheshimu kama dada mkubwa fulani hivi. Lakini kwa wengine, sijui kwa nini waliona ulazima wa kusukumia uvutiano baina yangu pamoja naye, labda waliona tunapendezeana, sijui.
Mi' nikaamua tu kuelekea chumbani upesi, nikiwaacha marafiki zangu wakiwa kwenye harakati ya kuondoka, nami nikaichukua bastola niliyokuwa nimekabidhiwa na kuiweka sehemu nzuri iliyojificha. Angalau kwa usiku huu nilijua nisingeihitaji, kwa hiyo kilichofuata ikawa ni kwenda kuoga kwanza, kisha nikarejea na kuvaa vizuri. Masai hiyooo... nikaelekea.
★★
Nimefika Masai mechi ndiyo inataka tu kuanza, nami nikawaona wenzangu wakiwa wamekaa kwenye viti virefu vya plastiki kuzunguka meza ndefu ya mbao, ambayo tayari ilikuwa na vinywaji. Kuongezea kundi hapo alikuwa ni Bobo, ambaye alikaa pembeni kiasi, na baada ya Ankia na mama Chande kuniona eti wakaanza kushangilia kwamba mwamba nimefika. Walikuwa wameacha nafasi kwa viti viwili ambavyo hakuna mtu alipaswa kukalia isipokuwa mimi hapa na bibie Miryam, na bado hakuwa amefika.
Nikasalimiana na Bobo vizuri, kisha nikakaa pembeni yake Adelina. Watu walikuwa wamejaa haswa mpaka nje kabisa, na baada tu ya kuagiza vinywaji vyangu vichache, mechi ndiyo ikawa imeanza. Dakika zikatembea bila Miryam kuwa amefika, mpaka kuna watu wakawa wanataka kukibeba kiti chake shauri ya wateja fulani kukosa viti, naye Bobo akawaambia wachukue tu na kusema pindi ambayo Miryam angefika, basi angepata kiti bila wasiwasi wowote.
Yanga ikatangulia kufunga. Fujo! Kelele na maneno yakaongezeka, nasi wanasimba tukaendelea kuwa wapole. Kidogo Simba wakasawazisha. Wee! Ilikuwa kama vile ndiyo goli la ushindi yaani, fujo zilipita zile za mashabiki wa Yanga. Tukiwa suluhu mpaka mwisho wa kipindi cha kwanza, hali ikatuliapo kiasi huku ahadi za kukatana maneno zikitolewa kuhusu kipindi cha pili ambacho kingeanza muda si mrefu. Tukaendelea kusubiri huku tukinywa bila wasi, story za hapa na pale zikiniteka mimi na Adelina, na ndiyo Miryam akawa amefika.
Yaani ile nilipomwona tu, macho yangu hayakuondoka kwake. Aliingia na kusimama kwanza kututafuta, na baada ya kutuona, akaanza kuja kwetu. Ni hivi, watu, tena hasa wanaume, wote, walimwangalia utadhani ndiyo alikuwa kitu kitamu zaidi kwenye menyu zote ambazo wamewahi kuyaonjesha macho yao. Siyo siri ujio wake hapo ulifanya mioyo mingi iingie matatani. Na alikuwa amevaa kawaida tu, lakini yeye kama yeye hakuonekana kuwa wa kawaida kwa wengine.
Alikuwa amevaa blauzi nyepesi ya mikono mirefu, iliyochorwa mistari myeusi na ya kijivu kwa njia za pembetatu zinazojirudia kuizunguka, pamoja na suruali ya jeans ya blue iliyokoza sana, hips zake zikionekana kushiba kinoma, huku miguuni akivaa ndala zake nzuri za kike. Wakati huu, alikuwa amesuka nywele ndefu za rasta, zenye rangi iliyokaribia kuwa njano yenye weusi, uso wake ukionekana kuwa mweupeeh ndani hapo kuendana na ngozi ya mwili wake mwanga ulipommulika vyema. Alikuwa mzuri huyu dada! Sijui tu hata nisemeje.
Alipofikia meza yetu, Bobo akatoka kwenye kiti chake na kuja kukiweka upande wa pembeni na Adelina, na kuna watu walikuwa wameegamia hapo lakini wakapisha. Mwanamke akakaa. Hakushika kingine mkononi zaidi ya simu, nasi tukaanza kumsalimia vizuri huku Ankia na mama Chande wakimsifu kwa kupendeza sana na msuko wake. Miryam akiwa ni shabiki wa Yanga pia, wawili hao wakaanza kusema yeye ndiyo bahati nzuri iliyokuwa imekuja kuwapa ushindi wa magoli kumi kabisa ndani ya kipindi cha pili, na maneno baina yao na Tesha yakaanza tena Bobo alipofanikiwa kuleta kiti kingine ili akae.
Kwa jinsi tulivyokaa kuizunguka meza, kwenda mkono wa kushoto kwangu alikaa Adelina, kisha Miryam, Tesha, Ankia, mama Chande, Bobo, mpaka mimi tena. Kwa hiyo ni kama tulitazamana na Miryam sawia. Mhudumu akaja karibu yake Miryam, nami nikamponda na kisoda kisha kumwita aje kwangu. Miryam akanipa tabasamu na kutikisa kichwa chake kidogo, nami nikaelewa aliyokuwa akiwaza. Nikiwa nakumbuka vizuri kwamba bibie alipendelea wine tu, nikamwambia mhudumu alete chupa moja kubwa ya Dompo, pamoja na glasi, naye huyo akasepa.
Tesha alikuwa amechangamka sana hasa baada ya kumwona dada yake, akisema leo wangekunywa mpaka kukuche, na hata baada ya Miryam kuwekewa Dompo yake hapo, jamaa akasema yaani tutulie ndani ya dakika kumi tu, meza ingejaa bia kwa idhaa ya dada yake. Hata mimi nilikuwa nahisi uchangamfu kwa kweli, moyoni yaani, kuwa hapa na hawa watu, na pale kipindi cha pili cha mechi kilipoanza, mambo ndiyo yakavurugika. Aah! Yanga?
Wakaipiga Simba mabao manne zaidi na kufanya tupoteze mechi kwa jumla ya magoli matano kwa moja! Mashabiki wa Yanga walifurahia kupita maelezo, na kweli wachezaji wao walijituma mno. Tesha akazimishwa mdomo na Ankia na mama Chande, yaani walifurahia mpaka basi! Mimi, Adelina, na Bobo tukawa wapole tu, tukiwaangalia wenzetu walivyofurahia ushindi wao, na bibie Miryam alikuwa akitabasamu tu kwa utulivu huku akiendelea kunywa taratibu.
Na maneno ya Tesha yakawa kweli. Bia zilikuwa zikiongezeka tu mezani, wahudumu wakisema Miryam ananunuliwa na watu ambao hata hakujali kuwafahamu, kwa hiyo zikawa zinasambazwa tu kwetu ili tuburudike. Yaani maumivu ya Simba na utamu wa bia ukafanya nisahau hata kama nilikuwa na njaa, ila haimaanishi nilikuwa nimechomwa saaana na Simba kufungwa, mm... nilifurahi tu kuona furaha ya wengine, na muziki wa kuwapongeza watani ukapigwa na kuwanyanyua. Walicheza haswa! Pombe ikamwagwa! Viuno na makalio yakatikiswa, yaani eh!
Mama Chande na Ankia walikuwa wanampondea kweli Tesha, wakimwambia aongee sasa, mbona yuko kimya, na Tesha kweli akawa kimya tu huku akinywa bia na kuwaangalia wanawake hao kwa njia iliyoonyesha amekerwa. Mama Chande alikuwa anacheza muziki, kuendana na mashabiki wengi wa Yanga ambao waliserebuka na kupiga mavuvuzela kwa shangwe, naye hata akawa akimchanganyia Miryam pombe yake kwenye wine ya bibie, na wao na Ankia wakijichanganyia wine kwenye bia, yaani raha ya ushindi ikiwa imewateka haswa.
Adelina akawa amenisogelea sikioni kuninong'oneza. Akaniambia kwamba alihitaji kwenda msalani lakini hakupajua, hii ikiwa ndiyo mara ya kwanza amebanwa na mkojo, nami nikamwelekeza upande wa kuelekea. Akanyanyuka na kuondoka, huku nikimfatilia kwa macho kuhakikisha hakuna mtu anamchokoza, na ndiyo alipoishia huko vyooni nikawa nimemtazama Miryam. Mwanamke alikuwa ametulia tu kama vile hayupo ama siyo shabiki wa Yanga na makelele yao, walikuwa wananikera kweli lakini ni yeye tu ndiye ambaye hakukera. Angekunywa wine taratibu na kuendelea kubofya-bofya kioo cha simu yake, nami nikaendelea kunywa pia.
Kidogo tu akafika jamaa mmoja mweusi karibu zaidi na Miryam, akiwa ameshika chupa ya bia mkononi, naye akaanza kumsemesha. Alikuwa mweusi, akivaa kofia kichwani, na mwili wake ulikuwa mnene na mfupi kiasi. Nikamtazama kwa umakini alipokuwa akijaribu kumtongoza-fulani hivi Miryam, na alisema anaweza kumwongezea bibie bia na sisi wote kama Miryam angetaka, lakini Miryam hakumsemesha wala kumtazama. Nikachukua kisoda na kumponda jamaa, na akanitazama.
Nikamtolea ishara kwa kiganja kuwa aondoke huku nikimtazama kwa umakini, naye akaendelea tu kuniangalia. Wengine walikuwa bize na mambo yao isipokuwa Bobo, ambaye naye akamwonyesha huyo pimbi ishara kuwa aondoke. Jamaa akatunyooshea kidole na kukitingisha kidogo, akifikri tunamtania sijui, lakini nikaendelea kumkazia macho mpaka akaona asepe tu. Miryam alionekana kukerwa sana na hilo jambo, lakini akaendelea kutulia tu, na mimi sikujisikia vizuri kumwona akikosa raha. Ndiyo maana kumbe hakupenda sana kuja hizi sehemu.
Tesha akawa amenirushia kisoda ili nimwangalie, na nilipomwangalia akanionyesha ishara kuwa anataka tuondoke. Eti kero ya kipigo ilimzidia. Ah! Nikamwambia atulie tu. Mama Chande na Ankia wakamwongezea kero zaidi kwa kumsema-sema, huku Bobo pembeni yangu akisema kweli leo hao wanawake walikuwa mawinguni mno mpaka wangeenda kulala na chizi yeyote yule wa Yanga ambaye angewazoa. Nikamwambia acha mambo yako bana, hawako namna hiyo, naye akasema labda Ankia siyo mama Chande. Nikataka kumuuliza alikuwaje na uhakika kuhusu hilo, na ndipo nikahisi nashikwa begani kutokea nyuma yangu upande ambao sikuuangalia.
Nikageuka na kumtazama aliyenishika hivyo, maana hakuliachia kabisa bega langu, nami nikaendelea kumtazama kwa umakini kwa sababu nilimfahamu, lakini hatukujuana. Namaanisha sikuwa na ukaribu na huyu mtu, na alikuwa ni mwanamke, mweupe kiasi, mwili mnono, na nilimtambua upesi kuwa mdogo wake na yule Rukia. Yule yule Rukia niliyemrukia pia halafu nikamtosa.
Kunishika kwake huyu mwanamke hakukuishia begani, bali akauweka mkono wake kupita bega na kuishika shingo yangu, huku akinikaribia usoni kama vile anataka kunisemesha na macho yake yaliyowekewa kope ndefu. Ilikuwa njia ya kawaida ya kuvuta umakini wa mtu, lakini kutotarajia ujio wake wa moja kwa moja kwangu na kunishika utafikiri tulijuana sanaaa ndiyo uliofanya nimwangalie kwa macho ya 'we vipi?'
Huku macho yake yakionekana kukolezwa na pombe, akanisemesha namna hii, "Mambo handsome?"
Alikuwa amevaa nguo nyeusi, kama gauni, fupi kuyaacha mapaja yake wazi, na ilionyesha sehemu kubwa ya ndani ya mwili wake kama night dress vile. Yaani sidiria aliyovaa na nguo ya ndani viliweza kuonekana kwa mbali, na wigi lake la nywele ndefu za kizungu lilimkaa vizuri kichwani.
Nikiwa namwangalia kwa umakini, nikamwambia, "Poa, vipi?"
"Safi. Leo umeniweza... nimekufata mwenyewe..." akaongea hivyo.
Alikuwa ameanza kulielekea sikio langu ili aniambie jambo fulani kwa ukaribu zaidi, na nilipoangalia usawa wa sehemu ambayo Miryam alikaa, nikakuta mwanamke huyo ananitazama usoni sawia. Ah, sikupenda hiyo picha mbele yake aisee, na huyu mwanamke nilitakiwa kumtoa hapa upesi sana.
Akiwa amenisogelea sikioni, mwanamke huyo akasema, "Twende ukani(.....) basi!"
"Ih, hapana. Asante. Nenda katafute mtu mwingine," nikamwambia hivyo huku nikijaribu kuutoa mkono wake.
Akalazimisha kuning'ang'ania shingoni na kusema, "Jamani, hata kidogo tu. Wewe mzuri sana, ni(.....) hata kidogo tu... nimekuja na kondo...."
"Wewe, em' niachie..." nikamwambia hivyo kiukali.
Alikuwa amelewa, kwa hiyo nikautoa mkono wake kutoka kwangu kwa nguvu na kutazama pembeni.
Bobo akamwambia, "We' si uende? Jamaa hakutaki."
"E-eeh chonde! Sijakufata wewe," mwanamke huyo akamwambia hivyo Bobo.
Bobo akamnyooshea kiganja na kumwambia, "Aisee, nitakuzibua! Toka hapa!"
Nikakishika kiganja chake na kumtuliza.
"We' Naomi wewe... si una mume wako huko? Umalaya waziwazi, huna hata aibu? Hebu nenda, usilete fujo hapa wakati tuna-enjoy siye..." Mama Chande akamwambia hivyo.
"Ah kwenda huko, huna lolote! Mmekaa hapa na mwanaume mzuri mnajishaua tu, kumbe wote mnamtaka. Mwanamke halisi ni mimi, acheni nimwonyeshe raha astarehe," huyo Naomi akasema hivyo.
Mama Chande akamtukana tusi kubwa na kuanza kusemeshana naye kwa njia ya ugomvi, na huyo Naomi akashika chupa akitishia kuitupa kwa Mama Chande. Nikawahi kuinyakua kutoka mkononi mwake, na kasi ya kuivuta ikafanya ianguke chini na kupasuka. Watu wengi walikuwa wameshaanza kuangalia upande wetu shauri ya mama Chande kupaza makelele ya ugomvi kumwelekea mwanamke huyo huku akitaka kumfata, naye Bobo akamwita mwanamke mwingine ambaye alikuwa ni mhudumu wa hapo ili amwondoe huyo Naomi sehemu hiyo.
Nilijawa na hasira kiasi, maana sijui tu huyo mwanamke aliingiwa na nini kilichomsukuma aje kutuharibia amani hapa, na ndiyo akawa amefanikiwa kuondolewa hapo na kurudi kwa mashoga zake huko. Ikageuka kesi sasa, mama Chande akiwa na pombe kichwani hakuacha kuongea, akimsema huyo Naomi kwa Ankia na Tesha, huku Bobo akiwa ameenda huko ambako Naomi alielekea.
Nikakaa kitini tena nikiwa nahisi kuvurugwa, na macho yangu yalipomwangukia Miryam tena, nikakuta akiwa ananiangalia kwa utulivu tu, kisha akaendelea na mambo yake kwenye simu. Nikajiona kama fala tu yaani, sijui kwa nini ila nikawa nafikiria kama vile bibie alikuwa amenisoma vibaya shauri ya hilo tukio, nami nikajitahidi kutulia huku nikiwasikiliza Tesha na mama Chande wakiwa wanatoa kero zao kuelekea wanawake malaya.
Adelina akawa amerejea na kukuta mhudumu anasafisha vipande vya chupa hapo chini, naye akauliza kulikoni. Ndiyo alipokaa na yeye akaanza kusimuliwa yaliyotokea.
"Yuko wapi huyo mwanamke?" Adelina akawa amemuuliza Ankia.
Mama Chande akanyoosha kidole kuelekea kule ambako Naomi alikuwepo, naye Adelina akawa amemwona.
"Yule pale, malaya tu aliyeshindikana..." mama Chande akasema hivyo.
"Amelewa tu, hata sijui ni nini kingine kimempa kiburi akamfata JC," Ankia akamwambia Adelina.
"Kwani sisi hatujalewa? Mbona akijaga na mume wake huwa analewa na hamfati JC? Ni umalaya tu. Kaona mpenzi wake JC ameenda chooni ndiyo akajua amepata nafasi... hana hata aibu..." mama Chande akaongea hivyo na kusonya.
Aliposema hivyo, nikamtazama usoni kiumakini, naye Tesha akauliza kikejeli, "Mpenzi wake JC tena? Ndiyo yuko wapi?"
Mama Chande akamnyooshea kidole Adelina huku akimwambia Tesha, "Huyu ndiyo mtoto sasa JC ameleta. Huyo mjinga anakuja hapa, eti anatusema wote tunamtaka lakini tunajishaua. Amekuwa Mungu? Eti akafikiri kijana wetu atahangaishwa na hilo limtako lake bayaa lililomshuka kama chupi ya mtoto iliyoning'iniza mavi... toto hilo hapo pembeni yake JC, halina nyash kwani? Tena nyash iliyoenda chuo kikuu, limetuliaaa... zuri, safi... halafu huyo mk(....) analeta bangi zake hapa?"
Aliongea hayo na kusonya kuondoa kero, naye Tesha na Ankia wakacheka sana na kujaribu kumtuliza huku mama Chande akicheza-cheza muziki. Pombe hii!
Nikamwangalia Adelina pembeni yangu, naye akaniangalia usoni pia na kutabasamu kwa njia yenye hisia kiasi, kisha akavuta na kunywa bia yake taratibu. Itikio lake kwa maneno aliyosema mama Chande lilionyesha dhahiri kwamba aliyafurahia kwa kiasi fulani, kwa hiyo ikawa wazi kwamba alikuwa na upendezi wa hali ya juu kunielekea.
Lakini mimi kiukweli niliboeka. Nilikuwa nimeingiwa na hali ya umakini kiasi kwa kutofurahishwa na kile kitendo cha Naomi, na bila kujizuia nikawa nimemwangalia Miryam tena. Niliganda kumtazama tu kwa sekunde chache, yeye akionekana kuwa bize na simu yake, ndiyo alipovuta glasi yenye wine ili anywe akakutanisha macho yake na yangu na kutulia pia. Yaani glasi alikuwa ameshainyanyua, lakini ikaishia njiani kabla ya kuufikia mdomo wake, naye akawa ananiangalia kwa macho yenye utulivu.
Tukaangalianaa... mimi nikihisi kabisa kuwepo na maana kubwa na nzuri mno kwa jinsi tulivyotazamana, naye ndiyo akaacha kunitazama na kuangalia pembeni huku akinywa kileo chake. Nikamwangalia na Ankia pia kukuta amenikazia macho yake kwa umakini, nami nikampa tabasamu hafifu, na yeye akatabasamu pia kwa furaha.
Baada ya dakika chache Bobo akawa amerejea tena, na chupa za bia zilikuwa zinaisha mezani kwetu, hivyo Adelina akafanya wema wa kuongeza zingine ili tuendelee kupoza koo. Inaonekana jamaa tuliyemfukuza alikoma kuongeza zingine, najua ilikuwa ni yeye ndiye aliyetuwekea bia kwa kudhani angejipatia Miryam. Ha! Ikawa imekula kwake.
Pombe ilikuwa inanigonga haswa maana nilikuwa nimepitisha muda sijanywa, kwa hiyo niliendelea tu kukaa kwa utulivu huku nikisindikiza story za akina Tesha, mama Chande, na Bobo, kwa kusema hiki au kile. Na sasa angalau Adelina na Miryam walikuwa wameanza kupatana maana walianzisha mazungumzo baina yao yaliyoonekana kufurahisha. Nilipenda sana kuwaangalia.
Katika kumtazama tena Ankia, nikakuta bado akiwa ananiangaliaaa, yaani kama vile alikuwa ananisoma sijui, mpaka nikamuuliza 'wewe, nini?' lakini akaacha kunitazama na kutabasamu tu huku akitikisa kichwa kuonyesha hakuna kitu. Sijui pombe labda ilikuwa imemkolea sana ama ishu ya mdogo wake Rukia kunifata hapo mpaka kumfukuza ndiyo ilimfanya aniangalie kwa hiyo njia, lakini nikapotezea tu na kuendelea kunywa taratibu.
★★
Tukaendelea kunywa kistaarabu tu, na kufikia sasa wote tuliokuwa tunakunywa kistaarabu zaidi tulikuwa tumeshalegezwa na nguvu ya pombe, yaani hadi Miryam alikuwa akitaniwa na Tesha kwa jinsi macho yake yalivyokuwa yakirembua mno shauri ya kileo chake kumwingia. Lakini baada ya muda mfupi nikawa nimetambua kwamba Miryam hakujisikia vizuri sana, ikionekana kichefuchefu kilikuwa kinampanda ama anaelekea kutapika, hivyo nikamwomba Adelina amuulize ikiwa alihitaji usaidizi.
Adelina mwenyewe alikuwa ameshapaa kwa pombe, lakini ustaarabu wake bado ulikuwepo, hivyo akanong'onezana kidogo na Miryam, kisha akaniambia kwamba Miryam alihisi vibaya mwilini ndiyo, shauri ya kutokunywa sana kwa kipindi kirefu, na hivyo huenda sasa alihitaji tu kurudi nyumbani ili akapumzike. Lakini nikaona hiyo kuwa haifai, najua kilichomkoroga zaidi ilikuwa kuchanganyiwa bia kwenye wine yake, nami nikamuuliza Bobo ikiwa kulikuwa na supu za mbuzi au ng'ombe hapo Masai kwa muda huo, na kwa sababu ya kutokuwa na uhakika sana, akaamua kumwita mhudumu ili amuulizie.
Mhudumu akaleta jibu kwamba supu zilikuwa zimeisha. Baada ya Miryam kutambua kwamba nilikuwa nataka nimtafutie supu, akasema nisijali kwa kuwa kama angetapika basi hali hiyo ingemwisha kufikia asubuhi, lakini mimi nikakataa. Nikamwambia angetakiwa kunywa supu usiku huu huu la sivyo angeumwa vibaya sana kesho, ila yeye bado akasisitiza haikuwa na shida. Hata wengine wakawa wanasema haitawezekana kupata supu mpaka asubuhi, lakini sikutaka hilo.
Nikawaambia tunyanyuke, twende kule Mzinga barabarani kuna sehemu wangekuwa wanatengeneza supu, nami nikatoka kwenye siti yangu na kwenda kumshika Miryam mkono. Alionekana kunishangaa kiasi, mpaka na wengine walinishangaa, ila ni pombe tu ndiyo iliyokuwa inaongoza hisia zangu zinifanye nitende namna hiyo. Nikawaambia wote tuondoke ili tukanywe supu kabla ya kurudi nyumbani, na sauti yangu ilisikika kama amri yaani.
Nikaanza kuungwa mkono na Bobo na Tesha, ambao waliona kwamba kileo cha Miryam kilikuwa kimemkoroga vibaya, hivyo tukaamua kuyaacha mambo yote ya hapo Masai hapo hapo Masai. Nikamwomba Tesha akachukue na maji ya kunywa ya baridi sana pale kaunta ili tuondoke nayo kama tahadhari, naye akatii na kwenda.
Miryam aliposhuka kutoka kitini, alikuwa akitembea kwa kuyumba kiasi, kwa hiyo nikawa nimemshikilia kwa kuuingiza mkono wake ndani ya kiwiko changu, hivyo mwili wake ukawa umeegamia zaidi kwenye wangu akiwa kama hana habari yaani. Tesha akarejea na kujiunga nasi, sisi wote tukiondoka hapo kasoro mama Chande, aliyeamua kubaki na mwanaume fulani wa Yanga aliyejuana naye. Bobo alikuwa sahihi kumbe!
Watu walikuwa wameanza kututazama sana tulipokuwa tunaondoka, lakini tukaendelea kujali yetu. Ilikuwa ni suala la kuchukua boda mpaka huko mbele shauri ya uzito aliokuwa nao Miryam, lakini yeye mwenyewe akasema tutembee tu; uzuri mimi, Tesha, na Bobo tulikuwepo na wanawake, kwa hiyo hakuona haja ya kuchukua bodaboda kwenda eneo la karibu mno.
Basi, tukaendelea kutembea mdogo mdogo. Kiukweli kwa mtu ambaye angetuona jinsi ambavyo nilitembea kwa ukaribu sana na Miryam, angefikiri tuna ule ukaribu wa ndaniii, lakini hata mimi mwenyewe nilielewa kwamba kumshika mwanamke huyu namna nilivyokuwa nimemshika sasa hivi, ilikuwa ngumu sana. Lakini alistareheka, pamoja na kwamba alijisikia vibaya, ila tulipokuwa tunaongea na wengine yeye pia alichangia maongezi na kuonyesha uchangamfu.
Nilifurahia sana mwili wake karibu yangu. Nilijisikia vizuri mno. Si unajua kwenye pindi za namna hii unakuwa unajifanya kama vile hiki ni kitu ambacho haukitilii maanani sana, kumbe moyoni unarukaruka. Nilitamani wakati ambao ungefika nimshike mwanamke huyu namna hiyo na nisimwachie tena. Mguso wake ulinitia uradhi wa hali ya juu sana mpaka... ngoja kwanza, hivi haya mawazo yalikuwa yanatoka wapi? Akili yangu ilikuwa sawa kweli?
Ile tulipokuwa tunaelekea kufikia lami, Miryam akaonekana kuzidiwa zaidi na kuanza kuyumbia upande mmoja, nami nikamwelewa. Ikanibidi nimshike pande za mikono yake na kumsogeza pembeni ya barabara, huku mwili wake ukiwa umeinama, naye akaanza kutapika hapo hapo. Wengine wakawa wamesimama na kutuangalia, Tesha akimtania dada yake kwa kusema huo ndiyo ulevi, na kwa kweli Miryam alikuwa amelewa.
Alipomaliza kumwaga matapishi, Ankia akanipatia chupa ya maji ya baridi ili nimpe Miryam anywe, naye akaanza kunywa taratibu. Nilikuwa namnywesha. Yaani nilimtendea kama yai vile, Tesha akiendelea na masihara yake tu kuhusu dada yake kunywa supu na kurudi kupiga bia tena, na ndiyo hapo jambo jipya likazuka.
Bobo akasema, "Tatizo hilo linakuja."
Nikageukia upande wake na kuona maaskari watatu wa usalama wa mtaa, polisi jamii, wakiwa wanakuja upande wetu kutokea upande mwingine wa barabara, nami nikamshikilia Miryam vizuri alipokuwa ametulia kidogo baada ya kunywa maji ya baridi.
"Wanakuja kutuzingua sasa hivi..." Ankia akasema hivyo kwa sauti ya chini.
"Watuzingue, tumeiba?" nikamuuliza.
"Si tunatembea usiku?" Ankia akasema.
"Agh..." nikafanya hivyo na kutoa kitambaa changu ili nimfute Miryam mdomoni.
Na alikuwa amelegea kweli sasa hivi, sijui kama supu ingenyweka.
Hao polisi viazi wakawa wametufikia, wakibeba na silaha nakwambia, wote wakiwa ni wanaume, na mmoja wao akauliza, "Na nyie? Mnatoka wapi?"
"Tulikuwa Masai hapo... ndiyo tunaenda nyumbani... mwenzetu anaumwa," Bobo akasema ukweli lakini kwa kudanganya.
"Kuumwa, kuumwa na nini? Pombe? Ndiyo imemng'ata?" polisi mwingine akauliza.
"Ndiyo tulikuwa tunarudi nyumbani..." Ankia akamwambia hivyo.
"Ee, wewe! Sikukuuliza wewe, sawa? Naongea na bwana wako. Kaa kimya," polisi namba 1 akamwambia hivyo Ankia.
"Nimepewa mdomo wa kuongea na Muumba. Nitaongea ninapojisikia, nikae kimya kwa nini?" Ankia akamwambia hivyo.
"Una jeuri eeh?" polisi namba 2 akamuuliza hivyo Ankia.
"Sikieni. Hapa hamna shida. Sisi tunaenda tu hapo mbele, tunapita hivi... tunaingia home. Na hata muda haujaenda kihivyo," Tesha akasema hivyo huku macho yake yakiwa yamelegea.
"Muda haujaenda? Ni mchana sasa hivi?" polisi namba 1 akamuuliza Tesha.
"Kwani sa'hivi saa ngapi?" nikamuuliza kistaarabu.
Akaniangalia na kuuliza, "Yaani unaniuliza mimi sasa hivi saa ngapi?"
"Eeh, nimekuuliza wewe, sa'hivi saa ngapi?" nikamsemesha kwa sauti makini.
"JC..." Adelina akaniita hivyo kwa sauti ya chini kama kunizuia.
Polisi namba 1 akanisogelea na kusema, "Wewe nakujua. Ndo' yule jamaa aliyejifanyaga shujaa kipindi kile mpaka wakamfunga yule jamaa, eti?"
Alikuwa kama anawasemesha wenzake, nami nikamuuliza, "Kwa hiyo unasemaje?"
"Usiniongeleshe hivyo, nitakuchafua!" jamaa akaniambia hivyo.
"Kwani tumefanyaje jamani? Si tunarudi nyumbani?" Ankia akawauliza.
"Unaulizia hivyo kama vile hujui sheria za kutembea usiku? Tena mkiwa mmelewa?" polisi namba 3 akauliza pia.
Bado nilikuwa nikitazamana na polisi namba 1 kwa mkazo, nikisubiri akorome tena.
Bobo akasema, "Sisi ni wa hii hii mitaa, tunatambulika kabisa, mjumbe wetu ni Yusufu. Sasa hivi saa tano, tunatoka kunywa kidogo ndiyo tunarudi nyumbani. Sa' shida ni nini?"
"Shida umeisema. Mnatembea usiku sasa hivi, mnatafuta nini?" polisi namba 2 akamuuliza hivyo.
"Kwa hiyo mtaa wooote ni sisi tu ndiyo tunaotembea sasa hivi? Mbona Emirate hamfiki? Wale wavuta bangi wanaokaa pale kila siku mpaka saa nane mbona hamwasogelei kuwaambia wamevunja sheria? Mnachotaka kwetu ni nini eh?" Ankia akasema hayo na pombe yake kichwani.
"Halafu we' ndo' unajifanya una mdomo sana," polisi namba 3 akamwambia Ankia huku akimnyooshea rungu-bunduki.
"A-ah... msamehe tu bro, amechangamka sana..." Tesha akasema hivyo.
"Hapa hatujali mmechangamka wala nini. Twendeni hapo ndani sasa hivi!" polisi namba 1 akasema hivyo.
Eh!
Ankia akaanza kulalamika, twende huko pamoja nao, KWA NINI? Ilionekana kuwa uonevu, Bobo na Tesha wakijaribu kuendelea kutuliza upande wa maaskari hawa, lakini umakini wangu ukavutwa zaidi na Miryam. Ikaonekana anakaribia kutapika tena, naye akainamia pembeni na kuanza kutoa maji mengi mdomoni, kwa kasi. Kichefuchefu kilikuwa kimemkaba haswa, ni lazima alikuwa anajutia.
Nikawa nimesimama karibu yake zaidi, nikisugua mgongo wake kwa kiganja changu, naye akachuchumaa kabisa na kuendelea kuinamisha uso wake. Polisi wale wakaendelea kulazimisha kwamba twende nao, eti tutajibu kila kitu huko huko, na wenye maneno mengi haswa ilikuwa ni Ankia na polisi namba 3, huku Bobo akiwa refa wao kwenye maongezi.
Ikanibidi niwageukie na kusema, "Aisee, tunarudi tu nyumbani, drama za nini? Tunaonekana kama watu wabaya sisi, au basi tu mnatafuta sababu ya kuonea mtu? Angalia tunawaambia kuna mtu hajisikii vizuri hapa, halafu mnataka tumpeleke huko ili...."
"Kaa kimya!" polisi namba 1 akanifokea namna hiyo.
Nikamtazama kwa umakini sana.
"Huko! Nimesema tembeeni! Huko!" akaamrisha hivyo.
Nikamtazama Miryam, ambaye bado alikuwa ameinama hapo pembeni, na ile nimemwangalia tena polisi namba 1, nikakuta ametoa kitu kama waya mweupe, wenye muundo kama jinsi siafu hutengeneza mstari wao, naye akaukunjia kiganjani kwake na kuacha sehemu ndogo inaning'inia. Alikuwa akitaka kutishia kunichapa sijui?
Akasema, "Anzeni kutembea sasa hivi. Wewe! Nyanyuka hapo!"
Alielekeza hayo maneno kwa Miryam, nami sikutarajia hili aisee. Akamsogelea na kutumia hicho kisiafu kumtandika mgongoni! Eh, eh, eh, eh, eh, eh!
Miryam akatoa sauti ya maumivu na kujikunja kiasi mgongoni, naye Ankia akapiga kelele ya kushangaa sana baada ya huyo jamaa kufanya hicho kitendo. Aisee, hapana... huyu angekuwa Joshua wa pili!
Nikang'ata meno kwa nguvu nikihisi hasira kali vibaya mno, nami nikamfata kwa kasi na kumsukuma kwa nguvu mno! Polisi namba 1 akawa ameweweseka vibaya na kuanguka chini kwa kishindo, nami nikamrukia hapo hapo chini wakati akijaribu kusimama na kumtandika ngumi mbili nzito kwenye taya yake, naye akaufunika uso kwa mkono.
Mapolisi wenzake wakaja juu yangu na kuanza kunipiga mgongoni kwa virungu, kisha wakanitoa na kunisukuma. Bobo alikuwa mwenye nguvu sana, naye pamoja na Tesha wakaweka kama ukuta kuendana na sehemu niliyokuwa nimesimama, huku Adelina na Ankia wakiwa wamesaidizana kumwondoa Miryam pale alipokuwa na kusogea mbali kidogo.
Polisi namba 1 akasimama, na yule namba 2 ndiye ambaye alikuwa ameshikilia bunduki kabisa, na sasa akawa ametunyooshea huku kwa pamoja wakituamrisha tupige magoti chini. Nilikuwa nikiwatazama kwa hasira sana, hasa yule ambaye alithubutu kunyanyua mkono wake dhidi ya Miryam, naye Bobo akawa akiwaambia watulize jazba huku akitusihi mimi na Tesha tupige magoti. Yeye na Tesha wakaanza kupiga magoti chini, kisha mimi pia nikafata.
Polisi hao wakatusogelea na kuanza kutusengenya kwa kutupiga-piga vibao, huku wakiwaita na wanawake waje upande wetu, na kwa ujasiri, Miryam akawaacha nyuma Adelina na Ankia na kuanza kuja tulipokuwa, kisha nao wakafuata. Bado alikuwa akiyumba na alionekana kuchoka, lakini akaja kando yetu na kupiga magoti pembeni yangu, nami nikamtazama usoni kwa hisia sana.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments