Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA NANE

★★★★★★★★★★★★★★


Adelina na Ankia wakaja nyuma yetu na kupiga magoti pia, hivyo sote tukawa tumewekwa "chini ya ulinzi." Wakati wa burudani ukawa umeingiwa na jini kisirani. Tukawa tumepigishwa magoti kwa kunyooshewa bunduki kutokana tu na mimi kujaribu kumtetea Miryam, lakini sikupiga magoti kwa sababu ya kuogopa watu hawa, bali tu ilikuwa kuangalia usalama wa wenzangu. 

Mapolisi wenyewe walionekana kuwa wavutaji tu, hawakuwa na ufundi uliofikia nyenzo halisi za kuwa katika nguvu waliyokuwa nayo, ni basi tu kushikishwa mitutu na virungu ndiyo mambo yaliyowajaza viburi kufikiri wanaweza kufanya lolote lile kwa raia. Nilitaka kuhakikisha ninawapa somo leo hii.

Kufikia wakati huu, kuna watu wa ujirani ambao walikuwa wametoka majumbani mwao na kuonekana hapa na kule wakitazama yaliyokuwa yametokea, na ndiyo maaskari uchwara wakawa wametuambia tusimame ili watupeleke kwenye kituo chao eti kutupa adhabu. Mhm... haya. 

Sote tukasimama, huku bado Miryam akiwa hajiwezi vizuri shauri ya hali yake, lakini angalau kutapika vile kulikuwa kumemwondolea uzito mzito mno, sema bado alikuwa mzito kiasi, kwa hiyo alishikamana na Ankia pamoja na Adelina katika utembeaji. Mimi nilihisi maumivu mgongoni kutokana na virungu walivyonitandika hao mbwa, lakini sikuyajali sana. 

Tukaelekea huko walikokuwa wanataka twende, nikiwa bado nina hasira kali mno iliyozidi kupanda tu shauri ya polisi namba 1 kupenda sana kunisukuma-sukuma, na mpaka tunalifikia jengo lile lile lililotumiwa kama ofisi ya mwenyekiti au mtendaji, bado ilikuwa ni saa tano. Wakatupeleka huko ndani ambako kulikuwa na chumba maalumu cha kuwafungia wahalifu, nao wakatuambia tuingie humo; yaani eti tungelala hapo mpaka kesho na hatua zaidi ndiyo ingechukuliwa.

Nikawauliza, "Hivi nyie mna matatizo, eti?"

Polisi namba 1 akasema, "Haki ya Mungu we' mjinga ukisema neno lingine tena nitakufanyi..."

"Nimeshaanza kuongea, na nataka unisikilize kwa umakini," nikamwambia hivyo kwa ujasiri.

Mapolisi wote walikuwa wananiangalia kwa umakini, na hatukuwa tumeingia kwenye hicho chumba, bali Miryam alikuwa amekaa kwenye benchi moja pembezoni mwa ukuta pamoja na Tesha huku Bobo, Adelina, na Ankia wakisimama kando yangu.

"Msije mkafikiri kila mtu huwa ni wa kuonea tu. Sijaja na nyie hapa kwa sababu ninaogopa hilo bunduki lenu, ila nina watu naowapenda, na nyie mkiwaumiza watu naowapenda, ni lazima nitawaumiza nyinyi," nikawaambia hivyo kwa mkazo.

"We' panyammoja unafikiri unaweza kunifanya nini mimi? Unajifanya unajua sana kupigana kisa nimemgusa huyo mwanamke wako?" polisi namba 1 akasema hivyo.

"Umemgusa? Wakati umempiga! Tena umempiga na hicho kiwaya chako wakati tumekwambia anaumwa!" Ankia akaongea kwa hasira.

"Ndiyo nimempiga! Ni haki yake kupigwa!" polisi namba 1 akaongea kwa kiburi.

"Wewe ni fala sana! Mwanaume gani unajitoa akili kupiga mwanamke? Kama unataka kupiga mtu, pigana na sisi hapa... waachie hawa waende nyumbani, tupige sisi hapa sasa!" Tesha akaongea kwa hisia kali pia.

"Kumbe mnataka na nyie eh?" polisi namba 2 akasema hivyo.

"Ingieni huko ndani la sivyo tutawacharaza virungu wote!" polisi namba 3 akapayuka.

"Niambieni ni sheria gani inawaruhusu kupiga raia wakati hajafanya jambo lolote la kuwadhuru nyinyi? Mh? Sheria ipi?" Adelina akasema hivyo kwa hisia kali pia.

"Wameshazoea kuwatisha watu wote, wengine wanawaburuzaga kabisa wakati hata hawajafanya lolote..." Ankia akasema hivyo pia.

"Kwa hiyo hamtaki kuingia huko ndani si ndiyo?" polisi namba 2 akasema hivyo.

"Bobo, mpigie mzee Hamadi. Una namba zake?" nikamuuliza hivyo.

Bobo akasema, "Ninazo," na kutoa simu yake.

"Mmpigie ili iweje? Mnafikiri ndiyo atawatoa hapa? Aisee, nimesema ingieni huko!" polisi namba 2 akasema hivyo na kumshika Adelina kwa kutaka kumsukuma.

Nikautoa mkono wake kwake kwa nguvu na kusimama mbele yake, naye akanipandishia kidevu juu.

"We' ndo' una damu ya moto sana eti?" polisi namba 1 akaniuliza hivyo.

"Jibuni swali lake. Ni sheria gani inawaruhusu kumpiga raia wakati hana kosa? Huyu, au mimi, tumekuwa ng'ombe? Tunawaambia tuko njiani kurudi nyumbani halafu mnampiga mwanamke anayeumwa? Kwa nini?" nikauliza hivyo kwa hasira.

Bobo alikuwa ameshampigia mzee Hamadi na kuanza kuongea naye, na Miryam alikuwa amekaa tu kwenye benchi akionekana kuchoka huku Tesha akimshika kwa ukaribu.

"Na wewe unajua adhabu ya kumpiga askari ngumi? Eh? Umenirukia ukanirushia ngumi, unafikiri tutakuacha tu?" polisi namba 1 akaniuliza hivyo kwa hasira pia.

"A-ah... kwa nini umpige? Kwa nini umpige huyu mwanamke? Jibu swali langu. Unajua ni kosa gani umefanya we' mwanaume? Unajua? Au unafikiri kila mtu atakuwa mwoga wa vitendo vyenu vya kikatili mnavyofanyia raia kwa kujisikia tu? Alikufanya nini huyo dada? Alikufanya nini mpaka unyanyue huo mkono wako kumpiga?" nikaongea kwa hasira ya wazi kabisa.

"Basi, JC... acha tu," Adelina akaniambia hivyo huku akinishika mkono.

Mapolisi wakawa wananiangalia kama vile wananipangia njama mbaya kwa pamoja.

Bobo akasema, "JC, mzee Hamadi amesema yuko hapo karibu... anakuja. Anataka kuongea na sisi wote..."

"Kwa hiyo mnafikiri mmemaliza sasa kwa sababu mnajuana na mwenyekiti?" polisi namba 1 akasema hivyo.

"Hapa hamwondoki, na mpaka mtoe faini!" polisi namba 3 akasema hivyo.

"Unamaanisha rushwa?" Adelina akamuuliza.

"Tena faini ya nini? Tumefanya nini? Hivi nyie mnafikiri... ehee... yaani watu! Wewe utatoa faini ya kumpiga Miryam? Tena na JC mmempiga na mavirungu yenu!" Ankia akafoka.

"Eeeh tena tunawapiga tena! Mtafanya nini?" polisi namba 2 huyo.

"Jaribu! Jaribu!" Ankia akawa anafoka huku Bobo akimshikilia.

"Msijione mnaweza sana kuongea. Hatujali nyie mnatoka wapi. Ingieni huko ndani, la sivyo..." polisi namba 1 akatishia.

"Mtatufanyaje? Mtatufanyaje?" Ankia akaendelea kufoka.

"Ankia, tulia..." Bobo akaendelea kumtuliza.

Ankia, akiwa hadi ameanza kutokwa na machozi, akasema, "Niachie Bobo. Waache na me wanipige, ama waniue. Kwa nini wampige Miryam? Eh? Aliwakosea nini? Eee... baba, njooni mtufanyie sasa. Na huko ndani hatuingii. Fanyeni mnachotaka, si mnajiona mnaweza sana? Fanyeni halafu mwone itakavyokuwa!" 

Hao mapolisi jamii wakacheka na kuendelea kumwangalia Ankia na sisi wote kwa dharau.

Nikamnyooshea mkono Bobo ili amwachie Ankia, naye akatii. Ankia akaja mpaka usawa wangu na kusimama, nami nikawaambia hao viazi, "Huyu hapa mwanamke mwingine mnayeona ana haki ya kupigwa. Pigeni."

Polisi namba 1 akaniambia, "We' jamaa huwa unajisikiaga sanaaa... unafikiri kila kitu unajua yaani... huwaga nakuangalia tu ila, nakupania siku moja tuje tukutane sehemu..."

Nikasogea mbele yake na kusema, "Kwani hii si sehemu? Isingekuwa ya Mir.... isingekuwa ya hawa marafiki zangu leo, ungetumia hata hilo bunduki lako kunifanyia unachotaka, lakini mimi siwezi, kamwe, kuogopa mtu mdogo kama wewe."

"Mdogo eh?" akaniuliza hivyo.

"Tena mwanangu wa kuzaa kabisa!" nikamwambia hivyo.

Akanisogelea usoni na kusema, "Ingia. Wewe na familia yako, sijui wapenzi wako, nimesema ingieni HUKO NDANI!!!"

Nikatulia tu na kuendelea kumwangalia usoni kwa umakini.

"Yaani nyie jamaa nawashangaa sana. Sijui ni chuki binafsi tu?" Tesha akasema hivyo.

"Eti?!" Ankia akadakia.

"Na ni viburi tu, hamna lolote. Tumefanya nini kibaya, na mnataka kuthibitisha nini sasa?" Adelina akaongea hivyo.

"Wanataka hela tu, eti faini! Tumekojoa ukutani kwa mtu? Hatutoi hata senti yaani," Tesha akasema hivyo.

"Halafu we' dogo!" polisi namba 3 akamnyooshea Tesha kirungu.

"Nini? Haki ya Mungu, naweza kucheza sindimba na wewe mpaka asubuhi na ukalala mimi bado nacheza tu, hunitishi kwa lolote! Nilikuwa mpole mwanzoni, halafu mkaona mmpige dada'angu?! Yaani JC... usingekuwa hapa, hakuna cha kumsubiri mzee Hamadi wala nani, tungeuana tu na hawa mafala!" Tesha akasema hivyo kwa hisia kali.

Polisi namba 2 akafanya kutuelekezea bunduki lake na kusema, "Ingieni huko!" 

"Piga! Piga!" Ankia akamwambia hivyo kwa ujasiri.

"Hey, hey nyie! Kulikoni hapa?" 

Mzee Hamadi akawa amefika hatimaye na kuuliza hivyo, na alikuwa amevalia jezi ya Simba kwa juu pamoja na suruali ya kitambaa, huku kichwani asikose kibaghalashee chake.

"Juma, hebu shusha hiyo bunduki," mzee Hamadi akamwambia hivyo polisi namba 2.

Jamaa akaishusha na kusema, "Hawa wajinga wamevunja sheria halafu wakamvamia Mzamiru na kumpiga... huyu hapa mwarabu huyu!"

"Kwenda huko! Unaongea kwa kudeka kama litoto ili iweje? Tulia na sisi tuongee suruali ikushuke, halafu mjinga mwenyewe!" Ankia akamwambia hivyo.

"Umeona walivyo na dharau?" polisi namba 3 akadakia.

Mzee Hamadi akamwambia polisi namba 1, "Bobo amesema nyie ndo' mmewavamia halafu mkampiga mgonjwa wakati wanarudi kwao. Ni kweli Mzami?"

"Siyo mgonjwa, amelewa. Wote hawa wamelewa, husikii wanavyonuka mapombe?" polisi namba 1 akalalamika.

"Ndiyo ikupe ruhusa ya kumchapa huyu dada? Kosa lake ni kunywa? Mbona hukwenda Masai kuwachapa wote waliokuwa wanakunywa?" Bobo akamuuliza hivyo.

"Si ndiyo hapo?" Ankia akaongea pia.

"Kwa hiyo hii shida yote imeanza kwa sababu umempiga Miryam? Miryam mama... Miryam..." mzee Hamadi akajaribu kumwita.

Miryam alikuwa amekaa kimya tu, akiunganisha viganja vyake kwa pamoja na kuinamishia uso wake hapo, nami nikamtazama kwa hisia sana.

"Hajisikii vizuri. Tena alikuwa anatapika, huyo msenge akampiga eti kuonyesha anaweza sana kupiga wanawake!" Tesha akamwambia hivyo mwenyekiti.

"Umeniitaje we' mjinga?" polisi namba 1 akafoka na kutishia kumfata Tesha.

"Kama ulivyosikia, msenge wewe!" Tesha akaongea kwa sauti na kusimama, akija upande wetu kwa hasira pia.

Mzee Hamadi akamwambia polisi namba 1, "Basi! Hebu acheni haya mambo bana!"

Nikamwekea Tesha kiganja kifuani ili atulie pia. Nilikuwa kimya tu kwa sababu ya kumkazia macho huyo Mzamiru. Alikuwa amenichukiza sana. Sana!

Mzee Hamadi akasema, "Hivi nyie kuna amani kweli kabisa kwenye familia yenu? Eh? Kwa nini mizozo kila mara?" 

"Kila mara katika maana gani? Sisi ni watu tuliotulia, lakini wajinga kama hawa ndiyo wanapenda kutuchokoza tu wakifikiri sisi ni wa kuyumbishwa sijui? Hawa kama hawajatumwa na mtu kutufata na kutuzingua leo... basi shida yao ni hela tu. Walikuwa wanataka hongo, eti wanasema 'faini,' faini itoke wapi? Tumekojolea hii ofisi au? Baba... hapa lazima haki ipatikane. Wametuonea sana. Wamempiga Miryam, amewakosea nini? Ah!" Ankia akaongea kwa hisia sana.

Alifanya mpaka hasira yangu ikaniweka kwenye ukaribu wa kutokwa na machozi, maana kitendo alichofanyiwa Miryam kiliendelea kujirudia akilini mwangu kila mara yaani. Nafikiri kulikuwa na watu huko nje ambao walisikia yaliyokuwa yakiendelea hapa, kwa hiyo kuna ambao walisogea karibu zaidi na jengo hilo, na polisi uchwara wengine watano wakawa wameongezeka hapo na kuwafukuza. Kundi lao likaongezeka.

Polisi namba 1 akasema, "Mwenyekiti, hakuna kuwasikiliza hawa! Walale humo mpaka asubuhi! Na lazima walipie kwa kuvunja sheria... wamenirukia wakanipiga mimi askari!" 

"Nyooo... askari gani wewe?" Ankia akasema hivyo.

"Na nani alikudanganyaga kwamba maaskari huwa hawapigwi? Mkivunja sheria, kwa nini tuwaache?" Bobo akamuuliza hivyo.

"Nini kinaendelea?" polisi uchwara mwingine akauliza.

"Hebu tulieni basi!" mzee Hamadi akaongea kwa kukereka.

"Hawa ni wapumbavu! Nimewakuta wanatembea usiku, wamelewa, halafu...." 

"Wewe Mzamiru, nimesema kaa kimya! Mbona huelewi?" mzee Hamadi akamwambia polisi namba 1 hivyo.

"Hawa siyo wa kunyenyekea mwenyekiti! Sisi siyo Joshua aisee! Na hatuogopi hiyo ngozi yenu. Mkizingua, tunawazingua kweli. Na hamuwezi kutufanya lolote!" polisi namba 1 akasema hivyo huku akiniangalia usoni.

"Unajua... huwa sipendi kutumia maneno makali, ila Tesha yuko sahihi. We' ni msenge sana," nikamwambia hivyo polisi namba 1.

"Jayden..." 

Hatimaye Miryam akawa amezungumza kwa mara ya kwanza kabisa toka tumefika hapo, na sauti yake ilikuwa ya chini, akiniita kama vile kuniambia hakufurahishwa na maneno yangu hasa kwa sababu yalitoka kwangu, nami nikageuka na kumwangalia. Wote tulimwangalia.

"Inatosha... please..." akasema tena hivyo bila kuinua uso wake.

Polisi namba 1 akacheka kidogo na kuwaambia wenzake, "Eti wazungu sasa..."

Nikakunja ngumi kwa nguvu, nami nikamgeukia mzee Hamadi, na kwa sauti tulivu nikamwambia, "Mzee... nisikilize. Mimi siyo mjinga. Ninajua sheria vizuri sana, na najua wewe pia unaijua, kwa hiyo unajua kuwa huu upuuzi waliofanya watu wako uko kinyume na sheria. Hawa siyo maaskari, ni walinzi tu. Lakini hata IGP Wambura ashasema, vitendo kama hivi vinavunja code of conduct waliyonayo wanausalama wa taifa wote, na kuna hatua za kinidhamu zinazochukuliwa dhidi yao wakibainika. Mzee Hamadi nimekupigia ili tusifike mbali, lakini kwa huu ujinga unaoendelea tutafika huko, kwa sababu hawa watu hawatutendei sisi tu hivyo... kuna wengi wameshazoea kuwatendea hivyo. Ninakutaka uchukue hatua kuukomesha huu utawala wao wa kipuuzi wanaoufanya badala ya kazi jamii iliyowaweka kufanya, unajua nina tie in kubwa sana na watu kama detective Ramadhan. Nikivuta waya wangu hapa kumpigia akaleta mvua yake ya moto huku... hawa vijana wako watakwisha. Sijui umenipata?"

Niliongea maneno hayo kwa mkazo sana, na wote walikuwa wakiniangalia kwa umakini. 

Mzee Hamadi akasema, "A-ah, JC... mbona unataka kwenda mbali sana?"

"Unamaanisha nini tutakwisha?" polisi jamii mmoja akauliza hivyo.

"We' Karim hayakuhusu. Pita hivi," Bobo akamwambia.

"Hapana Bobo, ni wote! Wote wako hivyo hivyo," Tesha akamwambia hivyo.

Mzee Hamadi akasema, "Kimya, nasema kimya!"

Wote wakatulia.

Mwenyekiti akaniangalia usoni na kusema, "Nimekuelewa JC. Hii haifai najua, ni... imeenda mbali, na haikupaswa kufika mbali. Nawaomba nyie wote mwondoke, nendeni tu nyumbani. Nitaongea na vijana hawa..." 

"Tunajua toka mwanzo tulikuwa na haki ya kutokuwa hapa mpaka wakati huu, kwa sababu tumeonewa. Na zaidi... wamemwonea huyu dada, wamempiga bila sababu..." nikamwambia hivyo mwenyekiti.

"Tena na JC wamempiga na marungu mgongoni! Anajikaza, lakini wamemuumiza," Ankia akasema hivyo.

"Haina shida Ankia, niko sawa," nikamwambia.

"Kwa hiyo unachotaka ni nini?" mzee Hamadi akaniuliza.

Nikamwangalia huyo polisi namba 1 usoni na kusema, "Ninataka huyu... amwombe msamaha Miryam."

"Eeh... amwombe msamaha Miryam kwa alivyompiga!" Tesha akaongea pia.

"Kwa hiyo nikimwomba msamaha ndiyo atasahau kwamba alipigwa?" polisi namba 1 akaniuliza hivyo.

"Nimekurudishia ya kumpiga. Nataka umwombe msamaha... na upige magoti!" nikamwambia hivyo.

"Nini?!" jamaa akashangaa.

"Kama ulivyosikia!" Tesha akamwambia hivyo.

Polisi uchwara wakaanza kuongea kwa ubishi, wakisema huo ni upuuzi usiowezekana hata kidogo.

"Yaani mimi nipige magoti? Wewe ni mwendawazimu eti? Nikipiga magoti, yaani naacha na kazi leo leo hii..." polisi namba 1 akaongea kwa kujitutumua.

"Ni leo hii hii, yaani hata kiswahili kuongea ni matatizo... hayajui," Ankia akasema hivyo, naye Bobo akacheka kidogo.

"Simama hapo hapo mpaka kesho, uone kama nitapiga magoti!" jamaa akaniambia hivyo.

Nikamwangalia mzee Hamadi kwa mkazo, naye akasema, "JC... si mngeenda tu nyumbani? Eh? Miryam amechoka, nyie wote mmechoka, haya yote ya nini? Usiku umeishaingia, em' nendeni..."

"Kweli JC, tuondoke tu. Haina faida yoyote," Adelina akaniambia hivyo.

"Nasema hivi... apige magoti amwombe Miryam msamaha. Mzee Hamadi haunijui vizuri, lakini niamini nikikwambia kwamba tukiondoka hapa huyu mbuzi hajamwomba msamaha Miryam, nitaitia hii ofisi dosari. Sikutanii," nikaongea hivyo bila utani hata kidogo.

"Yaani wewe! Unafikiri unatutisha sisi? Ulete nini labda wewe mbwa tukiogope?" jamaa akaongea kwa dharau.

Mzee Hamadi akamwangalia na kusema, "Mwombe msamaha huyo dada, Mzamiru."

Wote tukamwangalia jamaa.

"Nimwombe... haki ya Mungu! Mzee... huyu mkorogo huyu ndiyo anakutetemesha huyu... akija kukwambia ule mavi utakula kwa hiyo?" 

"Nimesema mwombe huyo dada msamaha. Ulichomfanyia siyo kizuri. Hakuna kosa lolote hawa wamefanya, na usiendekeze jeuri. Mwombe msamaha, yaishe," mzee Hamadi akamwambia hivyo.

Polisi namba 1 akasema, "Wewe siyo boss wetu mwenyekiti kutuamulia..."

"Nani anawalipa pesa mnayotumia kula ili mzurure usiku kulinda mitaa? Hmm?" mzee Hamadi akamkatisha kwa kuuliza hivyo.

"Si ni wajumbe?" polisi namba 2 akajibu hivyo.

Tesha akacheka kidogo kwa pumzi na kusema, "Yaani... bogus!"

Mzee Hamadi akasema, "Hao wajumbe wanazitoa wapi? Kabla hujajibu, nitakwambia. Wanawatoza hawa hawa raia ambao mnawaonea, wanaziwasilisha kwa viongozi wenu, mnapewa share yenu. Lakini hayo yote hayakamiliki nisipohusika, kwa sababu hao hao wajumbe wanategemea nguvu yangu, sijui mnanipata? Kwa hiyo ni mimi ndiye nayewalipa nyie, hao ni wasaidizi wangu tu. Akili zenu inaonekana bado ndogo sana hata hayo hamwelewi!"

"Sana!" Bobo akawaambia hivyo.

"Huyu dada ni moja ya watu wastaarabu sana hapa mtaani, hanaga zogo na mtu. Imekupa raha gani kumpiga hivyo, eh? Umejiona super sasa? Mzamiru, nasema mwombe msamaha. Mwombe msamaha haraka," mzee Hamadi akamwambia hivyo kwa uthabiti.

Huyo Mzamiru, akacheka kidogo kama vile hataki eti, halafu akasema, "Haya, nisamehe... we' dada? Nisamehe kukupiga, sawa eh?"

Alikuwa anajiona ana dharau mno, nami nikasema, "Piga... magoti."

Akaniangalia usoni kwa umakini.

"Kama ulinisikia tu kwa watu kwamba nilimfunga mtu kwa sababu ya upuuzi wake, basi cheza na mimi uje uone mwisho wake, siyo kuusikia tu. Unaongelea kuacha kazi? Nitahakikisha unafutwa na hupati kazi kwingine tena kwa sababu ya huu upumbavu ili uhangaike mpaka familia yako iteseke. Acha kucheza na watu usiojua mwanangu, siyo wote wameumbwa kuonewa, na usichezee kazi yako ukajiona umefika sana na kuitumia kama fimbo kumchapa yeyote unayetaka... wengine siyo wa kuguswa. Piga magoti umwombe huyu dada msamaha, sasa hivi..." nikaongea hayo kwa hisia kali.

Yaani niliongea kwa sauti yenye mamlaka, pakatulia mpaka tuli. Sasa watu wote hapo walikuwa wakitutazama, na sikujua Miryam alikuwa vipi huku nyuma yangu lakini nilitaka kuhakikisha hili jambo linakubali ili iwe somo kwa wote kutokuja kamwe kurudia kitendo kama kile. Haingefanya kazi kwa wote, najua, lakini baada ya hapa ningekuwa nimehakikisha wote wanamwona Miryam kuwa malkia. 

Niliona wazi kwamba jamaa alianza kuogopa, na alikuwa akiona aibu; kiburi chake pia kikimfanya awaangalie wenzake ili kupewa 'support,' lakini wote walibaki kimya zamu hii na kubaki kuangalia angefanya nini. 

Akasema, "Kwa hiyo...."

"Nimesema piga magoti!" nikamkatisha kwa ukali.

We! Mpaka mzee Hamadi akanishangaa. 

"Jayden..." sauti ya Miryam ikasikika akiniita hivyo.

Nikageuka na kumwangalia, na sasa alikuwa amenyanyuka kutoka kitini huku akiniangalia usoni kwa macho makini ingawa yalikuwa mazito, na kwa sauti ya chini nikamwambia, "Hautoki hapa Miryam kabla huyu hajakuomba msamaha."

Akaendelea tu kuniangalia kimkazo kiasi.

Nikamgeukia polisi namba 1 na kusema, "Fanya hivyo."

Mzee Hamadi akashusha pumzi na kusema, "Aisee! Mzamiru harakisha, yote ni makosa yako. Piga magoti."

Heeee!

Ilionekana kuwa kizungumkuti na bonge moja la drama ya kuigiza, lakini mbona jamaa akaenda chini! Alishuka kwa mguu mmoja, kisha wa pili, akapiga magoti huku sote tukimtazama kwa umakini. 

"Nisamehe," akamwambia hivyo Miryam kama hataki.

"Iseme vizuri," nikamwambia hivyo.

"JC..." Adelina akaniita kama kuniambia imetosha.

Nikamgeukia na kusema, "Nini Adelina? Sasa hivi me ndo' naonekana namwonea, au? Hicho kitu hakipo. Hakipo!"

Nilikuwa nimefura!

Nikamwangalia jamaa usoni tena hapo chini, akiwa amepiga magoti kama litoto, nami nikamwambia, "Iseme vizuri."

Akamwangalia Miryam na kusema, "Naomba nisamehe dada. Nisamehe kukupiga."

"Angalau," Tesha akasema hivyo akiwa amekunjia mikono yake kifuani.

Nikamwangalia Miryam usoni, yeye akiwa anamtazama huyo polisi mwenye akili 0 kwa mkazo, kisha akaniangalia machoni pia.

"JC, basi. Miryam mama... nenda nyumbani ukapumzike, sawa? Nendeni tu. Hey nyie wote, nendeni... toka hapo," mzee Hamadi akaongea hivyo na kuwaambia hivyo wengine huko nje.

Miryam akaanza kuja upande wangu taratibu huku akiniangalia usoni kwa sura iliyoonekana kukwazwa sana, naye akanipita tu na kuelekea nje huku Adelina akimfuata. 

Nikafumba macho na kung'ata meno kiasi kutokana na kuhisi kwamba sababu ya yeye kukwazika ilitokana na mimi kulazimisha aombwe msamaha namna hiyo, haijalishi kama kweli huyo polisi alistahili hiyo fedheha. Na aliistahili, nilikuwa natamani hata na yeye atandikwe na hako kamjeledi, basi tu!

Bobo na Tesha wakaniambia tuondoke, huku Ankia akiwa ameshatangulia nje pia, na huyo polisi akawa ameshasimama na kuonekana kuudhika sana kutokana na "kudhalilishwa" mbele ya wenzake. Na wote walinitazama kwa macho makali kweli.

Lakini nikamsogelea huyo jamaa karibu na kumwambia, "Huo ndiyo wendawazimu wangu sasa. Nitafute tu kwenye ile siku uliyoisema, niko tayari kwa ajili yako."

Jamaa akaniangaliaaa, yaani kama vile haelewi kabisa ujasiri niliokuwa nao ulitoka wapi, na mzee Hamadi akasema, "Ah, JC! We' kijana hapana. Hebu nenda kale ugali ulale. A-ah..."

Tukaondoka tu hapo hatimaye pamoja na wenzangu, ikiwa imeingia saa saba usiku sasa, na bado kukiwa na watu kadhaa ambao walitutazama sana tulipokuwa tukitoka kwenye eneo la hiyo ofisi. Miryam, Adelina, na Ankia walikuwa wakitembea taratibu tu mbele yetu, huku nikiona jinsi Ankia alivyowasemesha wenzake kwa manung'uniko, vilevile na Tesha upande wetu aliyekuwa akiongea haswa na Bobo kuhusiana na hiyo ishu. Nilikuwa kimya tu, wenzangu wakiona kwamba bado nina hasira, na ndiyo ikawa imepita bajaji isiyokuwa na wateja kando yetu.

Nikawaza upesi kwamba ingekuwa vizuri wanawake wakipanda kwenda mpaka nyumbani, kwa hiyo nikaisimamisha na kumlipa mwendeshaji na kumwambia akawabebe. Bajaji ilipowafikia, ilionekana wameelewa kuhusu kupanda lakini wakawa wanataka kupanda pamoja nasi, kwa hiyo tulipowafikia karibu tukawaambia watangulie tu; sisi wanaume tungekuja mdogo mdogo. 

Ni Miryam ndiye ambaye akaonekana kutopenda hilo wazo, kwa hiyo akaanza kutembea tena taratibu kuelekea mbele. Tesha akawa anamwita, Ankia vilevile, lakini hakusimama, hivyo mimi nikamfata upesi na kumshika mkono. Akaniangalia usoni kwa njia iliyoonyesha kuchoka sana kihisia, nami nikamsihi kwa upole kuwa aingie kwenye bajaji, sisi tungekuwa sawa na tungefika. Awahi tu kupumzika. 

Ndipo akautoa mkono wangu kwake taratibu na kuacha kunitazama, halafu polepole akarudi kwenye bajaji na kwenda kuingia humo, akiniacha nimesimama tu hapo huku nikimtazama. Adelina na Ankia wakaingia bajajini pia, nayo hiyo ikatuacha wanaume tukitembea mdogo mdogo kuelekea majumbani. Siku hiyo kwa kweli haikuwa imeenda kama nilivyodhani ingekwenda. Tofauti kabisa na nilivyokuwa nimetarajia.

★★

Mimi na Tesha tumekuja kufika makwetu ikiwa inaelekea kuingia saa nane kabisa, maana tulianza kupita Masai kwanza na Bobo, ambako bado kulikuwa na watu, na kwa ushawishi wa hawa wenzangu nikawa nimeshusha bia moja tu ili niende kulala usingizi mzito. Tesha alihakikisha amepiga mbili zaidi ili aongezee kulewa, na ndiyo tukawa tumerudi sasa vichwa vikiwa vimepondeka haswa. Na nilihitaji tu kulala aisee.

Ile nimefika ndani tu, nikamkuta Ankia sebuleni, kwenye sofa, akiwa anaangalia marudio ya tamthilia fulani ya wagiriki kwenye TV. Inaonekana alikuwa ananisubiria tu, kwa hiyo bila hata kumsemesha nikachukua funguo na kwenda kufunga geti, kisha nikarejea hapo sebuleni na kukaa sofani nikihisi kuchoka mwilini.

"Mmepita Masai tena?" Ankia akaniuliza hivyo na macho yake legevu.

Sikumjiibu, bali nikawa nimetazama mbele tu.

"Mhm... ya leo makubwa jamani. Hao wajinga wametuonaje sisi?" akauliza hivyo.

"Adelina?" nikamuuliza hivyo, nikiwa sitaki kuongelea hayo mambo.

"Amelala."

"Na wewe? Si ukalale?"

"Nimelewa lakini sina usingizi."

"Kaulazimishe. Muda umeenda," nikamwambia hivyo.

"Halafu wewe?"

"Naenda kuoga kwanza..."

"Ngoja, hhkh... kun... kuna kitu nataka nikuulize..." akasema hivyo na kunishika begani.

"Utaniuliza kesho Ankia, twende tukalale. Zima TV..."

"A-aah... nisikie kwanza..."

"Sitaki kuongelea hayo mambo sa'hivi, me nataka nikalale... kesho nayo siku," nikamwambia hivyo.

"Tayari hiyo kesho unayoisema ni leo... haijakucha tu bado..."

"Agh..." nikafanya hivyo na kusimama.

Ankia akasimama pia na kuniambia, "Ngoja, nataka nikuulize kitu..."

"Utaniuliza kesho Ankia. Halafu ukiwahi kuamka, na me uniamshe pia, nipige nikigoma, sawa? Ndiyo utaniuliza maswali yote ya dunia. Baadaye..." nikamwambia hivyo na kutaka kumpita.

Akanizibia njia na kusema, "Subiri! Nataka nikuulize kitu kuhusu Miryam."

Nikamwangalia usoni kwa umakini na kumuuliza, "Amefanyaje? Halafu nimesahau, hujaniambia... am-amefika... yuko huko kwao... amefika salama?"

"Enhee... umeona? Hicho hicho..." Ankia akasema hivyo huku akinikazia macho.

Nikaendelea kumwangalia kwa umakini.

"Sisi wote tumekasirika... hao wapumbavu walivyotufanyia... tena hasa walivyomfanyia Miryam. Lakini wewe JC.... maneno yako... jinsi ulivyokuwa unatenda... hapo mwishoni yaani... mpaka nimeshangaa. Kwa nini?" akaongea hivyo.

"Sikuelewi bana..." nikamwambia.

"Nimeanza kukuona toka tupo Masai, nimekuangaliaaa... ulivyokuwa ukimtizama Miryam... tulipokuwa tunatembea, hata alipokuwa anatapika ukamfuta kabisa matapishi, mpaka kuwapigisha magoti watu wababe... ili uwe mbabe... kwa ajili ya Miryam tu... nimeona kuna kitu hakipo sawa kabisaaaa..." akaongea kama vile hana akili.

Nikamnyooshea kidole na kumwambia, "We' umelewa wewe. Zima hiyo TV, ukalale. Me naenda kuoga kwanza..."

"'Hauondoki hapa mpaka akuombe msamaha!'" Ankia akaiga maneno yangu niliyoyasema kumwelekea Miryam muda ule.

Nikabaki nikimtazama kwa umakini.

"'Nitahakikisha hauajiriwi sehemu yoyote...' JC! Leo nimemwona mtu mwingine kabisa... diffarant kabisa na niliyefikiri ni wewe tokea umekuja," Ankia akasema hivyo.

"Sijui unajaribu kuongea nini. Na ni different, siyo diffarant," nikamwambia hivyo.

"Sijalewa kufanya akili yangu ipotee, najua nayomaanisha. JC uliniambia kwamba wewe siyo mtu wa hisia za... mpaka kulazimisha vitu, kwamba haujali sana na nini... lakini today? Hapana. Huyo hakuwa wewe niliyemjua. Kuna kitu kinakusumbua... na nakwambia kwa sababu nimekujua, hao wengine siyo rahisi, me ndiyo nakaa na wewe. Nakujua. JC, umebadilika. Utafanya kitu CHOCHOTE kile kwa ajili ya Miryam. Chochote! Yaani nimeshaona, siyo Bi Zawadi, Tesha, Shadya, Mamu... yaani, nimeshaona. Ni Miryam. Unafanya hhkh... yote, ili kuhakikisha Miryam... haumii," Ankia akaongea hivyo kwa sauti tulivu.

Nikaangalia pembeni kwanza.

"Ahah... si unaona, niko sahihi. Kwa hiyo imeanza lini hii? Nini... ni wapi ambapo alikugusa sana mpaka...."

"Ankia naomba uniache, nenda ukalale!" nikamkatisha na kuanza kuondoka huku nikivua T-shirt..

Akanishika mkono kwa nguvu na kusema, "Hapana JC, nataka uniambie..."

Nikamgeukia na kuuliza, "Nikwambie nini?"

"Unampenda Miryam, JC?" 

"What the.... yaani nikwambie hivyo... nijibu hilo swali ili iweje? Ume...? Hebu niachie!" nikautoa mkono wake kwangu.

"Niambie ukweli tu JC. Nimeshakuona. Niambie. Unampenda huyo dada, si ndiyo?" Ankia akaniuliza hivyo kwa sauti ya chini.

Nikabaki nikimtazama machoni bila kuwa na uhakika wa jibu la kumpa.

"Eti? Tena siyo... siyo ile kwamba tu unamtamani yaani, kama ulivyosemaga na besi lako 'tunaanzaga kutamani kwanza, kupenda baadaye,'  a-ah! Hii hapa ya sasa hivi ni kwamba umeanza kumpenda Miryam kwanza, na baadaye utaendelea kumpenda si ndiyo? Kile kitu ambacho ulikuwa unajaribu kuepuka kwangu eh?" akaniuliza hivyo huku akiniangalia kwa hisia.

Dah! Maneno yake yalinigusa! 

Akanishika shingoni kwa mikono yake yote na kusema, "Niambie JC. Unampenda Miryam?"

Nikashusha macho taratibu na kuangalia chini tu, nikiwa nimekazwa na hisia nzito sana moyoni, nami nikatikisa kichwa na kusema, "Ndiyo Ankia. Nampenda Miryam."

Hatimaye, hatimaye... nikawa nimefunguka!

Ankia akaachia tabasamu hafifu tu, lakini alionekana kuwa amefurahi sana. Sijui hata kwa nini!

Nikamwangalia usoni na kusema, "Ah, aisee! Mpaka nakuwa sijielewi... haikupaswa kuwa hivi Ankia..."

"We' ulitaka iweje?"

"Sikutaka iwe chochote mimi! Haya mambo ya nampenda, nakupenda, Ankia...."

"Wewe ni mwanadamu JC. Hata ukimbie vipi upendo wa kweli lazima utautaka tu. Hauwezi kuwa Playboy maisha yako yote..."

"Mimi siyo Playboy... na hata kama, ningekuwa... Playboy... ningeweza kuwa wa maisha yote..."

"Ahahah... nimeangalia movie ya Tony Stark, na yeye alikuwa kama wewe tu... anafikiri maisha ya mapenzi ni mchezo...."

"Sijawahi kusema nafikiri ni mchezo... acha kuangalia movie za kipuuzi..."

"Lakini umekuwa ukiishi kwa namna hiyo..."

"Ankia... please... basi," nikaona tupumzike kwanza, maana mabishano yasingeisha.

Ankia akarudi nyuma kidogo huku akinitazama na tabasamu lake mwanana, nami nikajishika kiuno na kuinamisha uso huku nikitabasamu pia.

"Aww... JC is in love!" Ankia akasema hivyo.

Nikamnyooshea kidole nikijifanya kuudhika, naye akaziba kicheko chake kwa kiganja.

"So... umepanga kumwambia lini?" akaniuliza hivyo.

"Kumwambia?! Ankia are you serious?" nikamuuliza hivyo kwa sauti ya chini.

"Yes. I mean... siyo pombe tu, yaani I'm deadass serious..."

"Hapana, you're not deadass serious..."

"Unaogopa nini kwani?"

"Siogopi lolote, Ankia. Sitaki tu kujiumiza. Faida itakuwa wapi kwenye hilo?" nikamwambia hivyo.

"Oooh, kwa hiyo unafikiri ukiendelea kukaa kimya ndiyo hautaumia?"

"Unataka nifanye nini? Unamjua vizuri. Hawezi kukubali, Ankia. Yaani... Miryam? Kwa nini ilipaswa kuwa Miryam? Yaani... pisi kibao... and I had to fall in love with Miryam? Ah..." nikaongea hivyo kwa hisia.

"JC, najua mapenzi hayalazimishwi, sawa, hata mimi nilifeli kwako, baada ya muda nikazoea. Lakini sikukaa kimya. Nilikwambia. Usipomwambia Miryam ukweli wakati upendo wako kwake unazidi kukua, JC... utaumia vibaya zaidi... hasa kama muda mrefu utapita. Nina experience, najua. Nimekuangalia, siyo leo tu, toka muda nilikuwa nimeshaona unampenda huyu dada. Tafuta nafasi umwambie, uondoe hicho kilongolongo moyoni maana naona kimeshaanza kukutafuna... usione hata mende anamsogelea yaani uko tayari kumuua kwa panga..."

Nikajikuta nacheka tu mwenyewe utadhani alikuwa anatania.

"I'm serious JC. Mwambie tu. You never know," akasema hivyo.

"Na ukweli ni kwamba I'll never know. Ankia... kilichofanya mpaka nikampenda huyu dada ni kwa sababu yuko tofauti sana, tofauti ambayo mpaka inanifanya nijione kuwa simfai yaani. Nina dhambi nyingi kinoma, achana na umri tu kuwa mdogo, yaani kweli unafikiri Miryam anaweza kuniangalia mimi kwa macho ya mara mbili mbili... hata tu akasema 'ngoja nifikirie upuuzi wako?'"

"Kwa nini unajikatisha tamaa hivyo?" 

"Kwa sababu sitaki kuumia zaidi ya ninavyoumia sasa. Kuumia kwa kutomwambia ni bora kuliko kumwambia halafu anikatae. Sijajua kama nitaweza kubeba hilo Ankia. Miryam... yuko kwenye level nyingine yaani ya kina cha upendo naohisi kumwelekea. Ni bora nizame mwenyewe tu, kuliko yeye ndiyo aje kuwa mtu wa kunizamisha kabisa na kuniacha nijifie humo..." nikamwambia hivyo.

Ankia akawa ananiangalia kwa utulivu tu. 

"A... hhh... yaani... sijui hata... sijui hata naongea nini. Ila Ankia... please... nakuomba usije kumwambia mtu yeyote kuhusu hili," nikamwomba hivyo kwa hisia.

"Unanichukuliaje JC? Nimwambie nani sasa?" akasema hivyo.

"Wewe ukiwa na mama Chande, huwa zinapaa. Kuanzia leo, hakuna kunywa pombe tena! Sitaki ulewe ukaja ukaropoka!" nikamwambia hivyo.

"Ahahahah... we' ni mjinga! Niongezee zingine now uone kama nitamropokea hata Adela. Kichwa changu siyo lege namna hiyo," akasema hivyo.

Nikashusha pumzi tu na kutikisa kichwa, kisha nikasema, "Nilipitiliza sana leo kuwa mkali namna ile."

"Haukufanya lolote baya wala. Mimi tu hapa ndiyo ilinipa picha kamili. Na ni jambo zuri JC," akaniambia hivyo.

Nikamwangalia usoni kwa hisia.

Akanisogelea na kusema, "Usijali. Nimekuelewa. Fanya unayoona ni sawa, ila usisahau na maneno yangu pia. Yanaweza yakajalisha siku moja."

"Ahah... yatajalisha ukija kusikia nimepondwa na chupa ya chai usoni..."

Ankia akacheka kwa furaha sana.

"Na ndo' unachotaka..."

"Mbona umeanza kuwa mwoga? Hauogopi kuwapigisha magoti polisi jamii, ndiyo unamwogopa Miryam hivyo?" akaniuliza.

Nikamkazia macho.

"Okay, sawa naelewa. Nakutania tu. We' nenda kaoge, me pia nakuja kujimwagia. Tutaongea zaidi kesho. Sawa?" akaniambia hivyo.

Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa, naye akatabasamu kiasi na kuanza kuelekea chumbani kwake.

Nikatoka hapo na kuelekea chumbani kwanza, nikiwa natafakari maongezi yangu na Ankia, na mpaka nimeenda kuoga na kurudi chumbani tena, bado nilikuwa nawaza tu. Nilijitahidi kuonyesha kwamba nilikuwa imara sanaaa mbele yake Ankia, lakini ukweli ni kwamba nilikuwa naogopa. Yaani nilikuwa nikiogopa hisia zangu mwenyewe, kwa sababu sikuwa nimetaka zinifikishe huku kote, lakini sasa nikiwa ndiyo nimefika, na sikujua zingenipeleka wapi.

Miryam nilimpenda. Sana. Lakini hata baada ya mimi mwenyewe kuwa nimekiri ukweli huu, bado sikujua ikiwa ungenipa faida kutoka kwa upande wake yeye mwenyewe. Kukaa kimya tu kungeendelea kunitafuna kama Ankia alivyoniambia, na kumwambia Miryam ukweli halafu akatae upendo wangu kwake ndiyo kungenipasua-pasua hata zaidi. Lakini najua bado hisia zangu zingekuwa pale pale tu. Ningefanya nini sasa? 

 

 

★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next