NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TISA
★★★★★★★★★★★★★★
"JC... we' JC... amka..."
Nilikuwa nasikia sauti hiyo ikiniita, lakini sikutaka kuamka kabisa maana nilijihisi uzito wa ajabu. Ndipo nikashtukia nawashwa kofi mkononi lililofanya niumie kiasi, nami nikajitahidi kufumbua macho.
"Amka! Amka... pameshakucha."
Ilikuwa ni Ankia bwana.
Nikaangalia mazingira vizuri; ndiyo, bado nilikuwa kitandani, na kweli palikuwa pamekucha. Nikamuuliza, "Ndiyo nini na wewe kuamshana na makofi?"
"Uliniambia nikuamshe mapema, na nikupige ukizingua. Ahadi ni deni, imetimia," akasema hivyo.
Nilikuwa nahisi kichwa changu ni kizito kweli, nami nikiwa nimelala kwa ubavu, nikaendelea tu kufumba macho na kumwambia, "Umefanya vizuri, ila bado nina usingizi!"
"Kwani unataka kwenda wapi? Huko Sinza kwenu, au?"
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Ndo' unyanyuke sasa. Me nataka nikatafute supu, ukisinzia tena shauri yako..."
"Saa ngapi?"
"Saa mbili," akajibu.
"Niletee basi maji ya baridi darling..." nikamwambia hivyo.
"Umeme umekatika... friji haijawaka."
"Kanunue basi. Unaenda kufata supu yako tu?"
"Eeeh, na Adelina. Ila ye' bado kalala. Unataka na we' nikuletee? Niongezee hela basi.." akasema hivyo.
"Kuna elfu tano hapo... juu ya droo. Kachukue supu ya elfu nne, na... maji ya baridii... ongezea, utaona," nikamsemesha huku bado nikiwa nimejisinzisha.
"Mhm... haya ngoja niwahi basi," akasema hivyo.
"Poa."
Nikahisi alipokuwa amenyanyuka kutoka kitandani na kuondoka, nami nikajivuta hivyo hivyo tu na kukaa. Matukio ya usiku uliotangulia yakajirudia wee akilini mwangu, huku nikihisi maumivu mgongoni kutokana na marungu niliyoshushiwa jana, nami nikaamua kuifata simu kutoka chajini. Ndiyo, niliiweka chaji kabla ya kulala.
Nikajitahidi kupambana na wenge la kichwani, nami nikaona kwamba kuna watu walikuwa wamenipigia, na jumbe chache kuingia. Bertha, Soraya, yule Kevin, namba fulani ngeni, pamoja na Bi Zawadi walikuwa wamenipigia kwa asubuhi hii, huku jumbe zikitumwa na Soraya pamoja na hiyo namba ngeni. Nikaona nianze na Bertha.
Nikampigia, na baada ya kupokea, akauliza nilikuwa wapi. Nikamwambia ndiyo nilikuwa najiandaa kwenda kule supermarket Ubungo, yaani sikuwa nimeondoka bado, naye akasema niende kwake kwanza. Kwa kuwa hii ilikuwa Jumatatu, yeye angefanya kawaida yake ya kwenda pale supermarket na sehemu zingine, na ndiyo ningemwonea huko, ila leo alitaka niende kwake kwanza. Bila kuuliza sababu, nikamwambia nakuja, naye akasema nisichelewe.
Wa pili akawa Soraya. Huyu nikamtumia tu ujumbe kuwa bado nilibanwa na kazi fulani, maana alikuwa anataka nimpe ratiba ya makutano, na aisee! Kutokea hapa sidhani kama ingekuwa rahisi tena kwa kweli. Yaani, nilikuwa nimetoka tu kukiri hata mbele ya Ankia kuwa nilimpenda Miryam, na kukumbuka hilo kila mara kukawa kunanifanya nitake kuwa mtu mpya ingawa bado hata sikuwa nimemfikishia mwanamke huyo hisia zangu, na nilikumbuka vizuri sana kwamba bado upande wa Bertha ungeendelea kunipa changamoto.
Yaani hako katabia ka kutoka na huyu na yule nilitaka na nilipaswa nikakomeshe kutokea hapa, na kwa kujua kwamba bado Bertha angekuwa kikwazo, nikaona nimtafute askari Ramadhan. Nikamtumia sms nikiuliza tu 'imefika wapi?' nikiwa na lengo la kutaka kujua kama siku yetu ya kuyamaliza hayo mambo ya Bertha ilikuwa imekaribia. Sawa alisema wiki na nini, lakini nilitaka tu iwepo njia ya kuharakisha haya yote ili hatimaye niwe na uhuru uliotosha kufanya jambo fulani ambalo moyo wangu ulitamani sana kufanya. Kumsemesha Miryam.
Maneno ya Ankia huo usiku kwa kweli yalikuwa yanazunguka mno kichwani. Kwa kiasi kikubwa nilikuwa nataka sana kujaribu kumfikishia Miryam hisia zangu, sema tu niliona muda kuwa haufai, na yeye vilevile angeweza kuukataa upendo wangu. Kama hilo la pili lingetokea, ningetakiwa kuwa nimeshaona mwelekeo kabla hata ya kujaribu kumwambia nampenda, kwa hiyo nilihitaji kuwa na uhakika KWANZA. Hivyo yaani.
Kwa kuwa Bertha alinitaka niwahi, nikaona nipitie ile namba ngeni upesi kwanza; Bi Zawadi ningemwambia tu niliwahi mahali fulani maana kama siyo kuongea nami kuhusiana na yaliyotokea usiku wa kuamkia sasa, basi huenda ilimhusu tu Mariam. Nilipoangalia ujumbe wa hiyo namba ngeni, nikakunja uso kiumakini kwa sababu haukunipendeza kabisa. Ulisomeka, 'Muda umekwisha JC. Nipe jibu haraka, mengine yafate.'
Moja kwa moja nikawa nimeelewa kwamba ujumbe huo ulitoka kwa Sudi, kama siyo Chalii Gonga. Uharaka wao wa kutaka jibu langu ulionyesha kwamba walipanga kutimiza hila zao kumwelekea Bertha upesi sana, na sijui ni kwa nini tu waliona umuhimu wa kunitaka mimi niwe kama mpiga muhuri wao, ama kuwapa ruhusa. Walikuwa wanajishaua, na inawezekana hata yule jamaa aliyenifatilia kule Kariakoo alikuwa mtu wao, kwa hiyo nikaamua kwamba kutokea hapa mpaka huko nitakapofika, bastola ingekihusu kiuno changu.
Hii ndiyo ingekuwa mara ya pili ambayo ningetembea na hiyo silaha, lakini ndiyo ingekuwa mara ya kwanza ambayo ningehisi uhitaji wa kuitumia. Lolote lile lingeweza kutokea, hasa kwa sababu sikutaka kuwajibu, na sikujibu ujumbe huo alioutuma. Nikaifuta na hiyo namba, kisha nikaanza kufanya maandalizi ya kuondoka huku nikihisi kichwa kimeanza kuachia kabisa shauri ya jambo hilo kunitatiza na kunipa umakini ulionifanya nihisi nguvu mpya.
★★
Kufikia mida ya saa nne nikawa nimeshaondoka hapo kwa Ankia baada ya kuvaa vizuri na kunywa supu na maji ya baridi aliyoleta mwanamke huyo. Niliondoka Adelina akiwa bado amelala, kwa hiyo nilimwambia Ankia ampe salamu yangu na tungewasiliana baadaye. Nikiwa nimeshapanda gari la kuelekea Makumbusho ndiyo nikapata nafasi ya kumpigia Bi Zawadi na kumsalimu.
Sikuwa nimekosea kuwa alitaka kunijulia hali baada ya yaliyotokea jana, nadhani Tesha akiwa amemwambia kwamba nilipigwa na virungu, kwa hiyo nikamtuliza kwa kusema nilikuwa sawa na tungeongea zaidi nikirejea. Alinijali kweli huyo mama. Lakini ningepaswa kufanya jambo fulani kuhusu maumivu ya mgongoni maana nilihisi yakiendelea kuongezeka kwa ndani kila dakika.
Toka nilipokuwa nimepanda daladala ya kuelekea Makumbusho, nilikuwa nimesimama, na watu kadhaa na nini walikuwa wakiniangalia kama nilivyozoea, lakini kulikuwepo na mwanamke mmoja aliyevutia sana kwa sura na mwonekano wake ambaye alisimama karibu nami zaidi kwa muda mrefu. Hata muda mwingine angepisha mtu mwingine akae kwenye nafasi zilizoachwa ili tu aendelee kusimama, nikiona wazi kuwa alipendezwa nami, lakini sikutaka tena majaribu mimi. Moyo wangu ulikuwa kwingine kabisa.
Dakika kadhaa zikakatika mpaka tulipofika maeneo ya Vunja Bei, Mkwajuni hapo, nami nikaanza kushuka. Huyo mwanamke akaanza kutembea pia nyuma yangu, ikionekana alitaka kushukia hapo, na mimi sikujali sana yaani, nilikuwa nimetangulia mbele tu, sema tulitazamwa mno utadhani tulikuwa pamoja. Nikiwa ndiyo nimeshuka tu na kusimama pembeni ya barabara, mwanamke huyo akaja karibu zaidi na nilipokuwa. Kwa kufikiri anataka kupita, nikampisha, lakini akanifata huku akinitazama moja kwa moja. Nikamwangalia pia.
Alikuwa mweupe, mrefu kiasi, akivaa gauni refu lenye kubana mwili wake lililokuwa na rangi ya blue, lililobana umbo lake lenye hips nene na kalio lililotokeza kwelikweli mpaka kulichoreshea gauni lake mistari ya nguo aliyovaa ndani. Alionekana kutovaa sidiria, kwa kuwa matiti yake yasiyo makubwa sana yalichoresha vizuri chukuchuku zake hapo kifuani, na alisuka mtindo wa rasta za kahawia ndefu sana kufikia mpaka kwenye kalio lake. Alikuwa na sura na mdomo mzuri, macho makubwa yaliyorembwa kwa wanja kopeni, na alishika kimkoba kidogo kiganjani mwake.
Mrembo akasema, "Mambo kaka?"
Alikuwa na sauti ya kipole.
Nikamwambia, "Fresh. Niaje?"
"Poa tu. Samahani, nilikuwa naomba kuongea nawe..." akaongea kwa njia ya kawaida.
"Ah, usijali, toa hiyo samahani. Nambie..." nikamwambia hivyo.
"Wewe ni mwenyeji wa haya maeneo?" akaniuliza.
"Hapana. Me ni mgeni huku," nikamdanganya.
"Umekuja kutembea?"
"Yeah, kuna sehemu nimealikwa. Ndiyo nawahi sasa hivi..."
"Ahaa, sawa... basi, kama una haraka naomba tuachiane mawasiliano," akasema hivyo.
"Kwa nini?"
Akabana midomo yake na kuangalia pembeni, akionekana kuwa na wasiwasi sijui, nami nikaelewa kuwa aliniogopa kidogo. Najua alichokuwa anakitaka, ila kujitoa akili ilikuwa lazima. Na bado nilikuwa nawaza kwamba huenda huyu angekuwa ametumwa hata na hao wakina Sudi, kwa hiyo nilihitaji kuwa mwangalifu. Na tulikuwa tunaangaliwa sana na baadhi ya watu eneo hilo.
"Unaitwa nani?" nikamuuliza mrembo.
Akaniangalia na kusema, "Pendo."
"Wewe ni mwenyeji wa huku?"
Akatikisa kichwa kukubali.
"Unasoma?"
"Me nesi," akajibu.
"Wapi?"
"Agha Khan," akajibu.
"Kumbe? Okay. Sa' Pendo, kwa nini unataka kuwasiliana na mimi?"
"Kuna kitu nataka nikwambie..."
"Niambie sasa hivi."
"Ni vitu vingi. Si umesema una haraka?"
"We' sema."
"Eh... aheh... mpaka niseme jamani... we' si ni mtu mzima?"
"Ahah... sawa. Ila hatujuani, unaweza ukawa mke wa mtu," nikamwambia.
"Me sijaolewa mbona," akasema hivyo.
"Kwa hiyo umenielewa eh?"
Akatabasamu kwa haya na kuangalia chini.
Nikasema, "Okay. Nimekuelewa. Ila Pendo, me ni mume wa mtu. Na ninampenda huyo mtu. Sidhani kama nitaweza kukupa unachotaka."
"Kwani ni lazima mke wako ajue?"
"Kumbe na we' wa hivyo? Nilikuona mpole, nikadhani utaelewa," nikamwambia.
"Mhm... haya. Kwa hiyo hujanipenda?" akaniuliza hivyo.
"We' mzuri. Ila me wa mtu. Siwezi kumdanganya mwenzangu, hata wewe itafika mahala tutadanganyana mno nikifanya hilo. Siyo wa hivyo mimi," nikamwambia hivyo.
"Ahaa... basi. Safari njema," kakasema hivyo bila kuniangalia.
"Na we' pia," nikamjibu.
"Poa," akasema hivyo.
Huyoo akaendelea na mwendo kuelekea upande mwingine, nami nikajiondokea hapo kama vile siyo mimi. Yaani huyo angekuwa amenikuta kipindi kile! Ningemwonyesha ushetani wangu maana alikuwa wa moto, siyo mchezo. Ila sasa hivi nilitaka kutulia tu mpaka suala langu kwa Miryam lieleweke kabisa, la Bertha limalizike pia, ndiyo ningejua nisimame wapi baada ya hapo.
Nikiwa naelekea Royal Village sasa, nikampigia simu madam Bertha kumwambia ndiyo nilikuwa nimeingia getini na ningefika huko juu upesi, na alipopokea, kabla hata sijaongea akaniambia nielekee kule nyuma alikopenda kuegeshea gari lake halafu nimsubiri hapo; maana ndiyo alikuwa anashuka. Ilikuwa kama vile anajua nimeshafika yaani, nami nikasema tu sawa, ninaelekea huko, ndiyo nikaanza kuelekea huko kweli.
Nikiwa ndiyo nimefika huko kwenye egesho la magari, nikaona kitu kilichofanya niingiwe na umakini zaidi. Ilikuwa ni Dotto, akiwa amesimama usawa wa magari mawili; moja ikiwa ni lile la madam Bertha la Harrier, na lingine likiwa la aina ya Lexus LX570, kubwa na zuri, likiwa na mwonekano mpya wa rangi ya shaba (silver) iliyoelekea kuwa dhahabu kabisa. Alisimama karibu nalo hilo kama vile lilikuwa lake ama labda yeye ndiye aliyekuwa dereva wake, nami nikamwangalia kwa umakini zaidi.
Alikuwa amevalia T-shirt nyeusi ya mikono mirefu, iliyobana mwili wake vizuri kuonyesha namna misuli yake iliyokuwa imara, pamoja na suruali nyeusi pia na kiatu cheusi. Akawa ametazama upande wangu na kuniona, naye akaacha kuniangalia na kutazama pembeni kama vile hanijali. Kuna kitu tu kikanisukuma nimfate mpaka hapo alipokuwa na kusimama mbele yake, nikiwa nahisi hata uwezekano wa kutoa bastola hapo hapo ungetokea, lakini sikutaka ifike huko. Yeye akanitazama usoni kwa umakini.
"Imekuwa hivi tokea lini?" nikamuuliza hivyo.
Akaniangalia kwa njia ya kuonyesha kwamba hakuelewa nilichomaanisha, lakini najua alinielewa vizuri.
"Oh, hujaelewa? Okay, let me rephrase that. Umeanza kumfanyia usaliti madam tokea lini?" nikamuuliza tena.
"Usaliti? Usaliti gani?" akajitoa akili kabisa na kuniuliza hivyo.
"Naongelea usaliti ambao hadi ukafanya utamke maneno 'tutamuua' with such ease..."
"Ah, ongea kiswahili dogo, wengine hatukwenda shule..."
"Mbona 'game on' uliweza kuisema?" nikamuuliza hivyo kwa kuudhika.
Akacheka kidogo na kuifuta-futa pua yake kwa kidole, halafu akaniambia, "Ukijua nini kimeanza lini, itasaidia nini? We' si uangalie kile ambacho kipo sasa hivi, hayo mengine yatakupa faida gani?"
"Ah, nashangaa tu yaani, ghafla tu... goon namba moja wa madam kamgeuka, akiwa pamoja na mume wake wanapanga kumuua. Sishawishiki kirahisi na bullshit yote eti kisa Chalii ni kaka yako... mbona kipindi hicho chote ulikuwa umetulia tu? Eh? Tena ukifanya bidding zake madam... zote? Nini kime-change ghafla? Sudi amekuahidi mengi mazuri zaidi ya unayopata kutoka kwa madam, au?" nikamuuliza hivyo.
"Hayo hayakuhusu. Jiangalie wewe. Umepewa muda kutoa jibu, utumie vizuri," akaniambia hivyo.
"Sihitaji kujibu chochote. Mngekuwa mmeniambia labda mnataka kumwibia sijui... labda ningekubali. Yote ya kumuua ya nini? Halafu eti mnafikiri nitaogopa kumwambia kwa kusema sijui ataniua kwa sababu anakuamini zaidi wewe..."
"Mbona bado hujamwambia sasa? Mwambie. Si anakuja hapa hata sasa hivi... mwambie tu," Dotto akaongea kwa kutojali.
Nikabaki nikimtazama usoni kwa umakini.
Akanisogelea karibu zaidi na kusema, "Fanya uamuzi dogo. We' si una akili sana? Kila kitu kipo juu yako. Wala usiwaze kuhusu mimi."
Baada ya Dotto kusema maneno hayo, sote tukabaki kutazamana machoni umakini sana, akinionyeshea ubabe wake, na mimi nikimwonyeshea ujasiri wangu. Kutokana na hali kuwa nzito hapo hatukutambua upesi kwamba kuna mtu alikuwa akija upande wetu mpaka sauti yake iliposikika akisema...
"Hey..."
Nikatazama pembeni na kumwona madam Bertha akiwa anakuja upande wetu. Dotto akasogea nyuma kidogo huku naye pia akimwangalia madam, na kama kawaida yake alikuwa amependeza sana.
Alivalia nguo laini sana ya moja kwa moja mpaka miguuni, ikiwa ya suruali, na iliyokuwa na rangi kama ya ngozi ya mtu anayeelekea kuwa mweupe. Kwa kuwa ilimbana, yaani ilionekana kama vile ni ngozi yake kabisa, kwa hiyo kwa kumtazama vibaya ungedhani alikuwa uchi. Mabuti marefu ya kike ya kuchuchumia ya rangi ya maziwa yalimrefusha zaidi, na nywele zake nyekundu za kusuka alikuwa ameziachia kama namna ile ile nilipomwona majuzi. Mikononi aliweka mkoba mweusi pamoja na koti zito la nanyonya lenye rangi ya maziwa, na aliyaficha macho yake kwa miwani nyeusi ya urembo.
Akiwa anatembea kwa mwendo kama wa miss, akatukaribia zaidi na kuuliza, "Kuna nini hapa? Mbona kama mnataka kupigana?"
Nikamtazama Dotto usoni, yeye pia akinitazama kwa utulivu, nami nikamwambia Bertha, "Hamna kitu. Tulikuwa tu tunasalimiana."
Bertha akamwangalia Dotto.
Jamaa akasema, "Umependeza madam..."
"Shut up! Shika... tangulia kwenye gari," Bertha akamwambia hivyo.
Alikuwa akimkabidhi koti na mkoba wake, na jamaa akavipokea na kuniangalia kwa jicho la chini lenye hila. Nikaendelea kumtazama tu mpaka alipoanza kuondoka kwa kudunda na kuviingiza vitu vya Bertha kwenye lile gari la Lexus, ndiyo na yeye akaingia humo. Nikamtazama madam usoni, naye akaitoa miwani yake na kunisogelea zaidi huku akitabasamu kwa njia yenye kuonyesha madaha.
Sikutarajia anipe hilo upesi, kwa hiyo nikiwa makini tu nikamuuliza, "Umenunua gari jipya?"
Akatikisa nyusi kukubali.
"Zuri. Hongera," nikamwambia hivyo.
"Sifa ziende kwako," akasema hivyo huku akinishika mkono.
Nikatulia kidogo nikitafakari kitu, kisha nikamuuliza, "Kila kitu kiko poa madam?"
Akapitisha mikono yake kiunoni kwangu na kuuegemia mwili wangu huku akinitazama kwa hisia, naye akasema, "Kwa nini kila kitu kisiwe poa?"
Nikajitahidi kuupa mwili wangu wepesi ili asinikandamize sana kiunoni na kuihisi bastola, nami nikamshika shingoni na kumwambia, "Mara ya mwisho nimekuja, tuliishia sehemu siyo nzuri sana, nikafikiri labda...."
"Ah, achana na hayo. Nilikuelewa. Na sasa hivi tuta-focus kwenye mimi na wewe tu... mengine pembeni."
Nikakunja uso kimaswali kiasi, kwa sababu sikutarajia angekuwa ameliachilia lile suala kiurahisi namna hiyo, lakini wala hakuonekana kama ameliweka moyoni kabisa. Tena akakishika kidevu changu kwa makucha yake na kujing'ata mdomo wake wa chini huku akiuelekea wa kwangu, halafu akanipiga busu moja laini na kunifuta-futa lipstick iliyobaki kwa kidole chake kimoja.
"Umekunywa pombe asubuhi-asubuhi?" akaniuliza hivyo.
"Jana. Nilikunywa kidogo wakati wa game la Simba," nikamwambia.
"Haikuwa kidogo, bado harufu ipo japo umesugua ulimi. Pole... inaonekana ni machungu ya Simba kubondwa ndo' yalikufanya ukalewa wewe..." akasema hivyo na kucheka kidogo.
Nikatabasamu kwa kutoamini kabisa huu wonyesho wa upendo, au nia nzuri aliyokuwa ameanza kuijenga kwangu, nami nikamuuliza "Mood nzuri namna hii unaitoa wapi wakati nilikuwa nimeku-diss?"
"Lini umeni-diss?"
"Si ile juzi?"
"Well... wewe ndiyo unaifanya day inakuwa nzuri. Ya juzi hata siyakumbuki maana umenifurahisha sana leo," akasema hivyo.
"Kwa kipi?"
"Kumkataa Pendo," akasema hivyo.
Nikamkazia macho kiasi, naye akatikisa nyusi kimchezo, ndiyo nikamuuliza, "Pendo? That was you?"
Akatikisa kichwa kukubali huku akitabasamu kiasi.
"Ahah... kwa hiyo, kumbe ulikuwa umemtuma huyo mwanamke anitongoze, ili..."
"Ili nione kama kichwa chako kiko kwenye game, na moyo wako uko kwangu. Ilikuwa ni test ndogo tu, ila kumkataa Pendo ni ishu kubwa. Huyo mwanamke huwa hakataliwi kirahisi hata na wazee wa upako na maaskofu," akaniambia hivyo.
"Ameanza kunifatilia tokea... tokea Mbagala? Yaani... ulikuwa umeshampanga asimame nami mpaka huku?"
"Me hayo siyajui. Karudisha taarifa kuwa umemkataa, that's what I wanted..."
"Utajuaje hilo kuwa kweli? Je kama nimemkubali na amekudanganya?"
"Nilikuwa nasikia maongezi yenu yote," akaniambia hivyo.
Nikanyanyua kidevu juu kiasi huku nikimwangalia kwa utambuzi, nami nikasema, "Alikuwa anachukua sauti..."
"Mm-hmm. Na kama ingetokea umemkubali, me na we' ndiyo ingekuwa bye bye... na tena una bahati yako. Ipo siku nitakushika kivingine," akajibu hivyo.
Nikatulia kidogo, kisha nikamuuliza, "Kwa nini Bertha? Mpaka ufanye hayo yote... why?"
Akasema, "Kwa sababu nataka uwe wangu peke yangu. Sasa hivi sitajali sijui nini, au nini... JC, nataka uwe WANGU PEKE YANGU. Sahau ishu ya me kutaka mtoto, tutauangalia huo mpango baadaye. Sasa hivi nataka kichwa chako kiwe sehemu moja, na moyo wako hapa tu. La sivyo, mimi na wewe kuachana inamaanisha itakuwa vibaya. Unaelewa jinsi navyokuwa nikipenda kitu sana, si ndiyo?"
Hmm! Hili lingekuwa tatizo haswa, ila ni ikiwa tu nisingekuwa mwangalifu. Nikatikisa kichwa tu kuonyesha uelewa.
"Good. Umepita kamtihani kangu. Ngoja tuendelee kuona ya mbele," akasema hivyo.
Nikawa nikimtazama kwa ufikirio sana, nami nikasema, "Bertha... popote pale ambapo me na wewe tutaishia, ninaomba ujue tu kwamba sehemu kubwa ya moyo wangu haitaki kuona unaumia. Hatujaanza vizuri... na... sijui kama tutaishia pazuri, lakini...."
"Shhh..." akaninyamazisha kwa kuweka kidole chake kimoja mdomoni kwangu.
Nikatulia tu.
"Usiwaze negative. Sasa hivi nataka kuhakikisha kila kitu changu na wewe kinajengeka kwa njia positive, tena kuanzia leo leo. Na nitafanikiwa. Utaona tu," akaniambia hivyo kwa uhakika.
Nikashusha macho yangu chini, nikiwa najihisi vibaya kiasi moyoni. Maneno niliyokuwa nataka kumwambia yalikuwa yamebeba maana pana sana, hakujua tu.
Akatoa kidole chake mdomoni kwangu na kusema, "Twend'zetu. Kuna watu muhimu nataka tukakutane nao."
Nikamwangalia na kutikisa kichwa kukubali, naye akanishika mkono na kuanza kuniongoza mpaka tulipoingia kwenye Lexus yake na kuketi siti za nyuma, kisha Dotto akaliwasha na kuanza kuendesha.
Bado tu nikawa nawaza vitu vingi sana, mara kwa mara nikitazamana na Dotto kupitia kile kioo cha mbele pale juu kwa macho yaliyojuana mno, na maswali ya ni wapi haya yote yangekuja kuishia yakaendelea kuisumbua nafsi yangu hasa baada ya Bertha kuonyesha kwamba ni kweli alikuwa ananipenda. Kama tu maneno ya Dotto muda mfupi nyuma, kwa kweli ningetakiwa kufanya uamuzi haraka ikiwa Ramadhan na wenzake wangekawia kuyamaliza haya.
★★
Kulikuwa na mkutano fulani maalumu huko Kinondoni ambao ulibeba matembezi ya wafanyabiashara na viongozi fulani wa juu serikalini, na Bertha alikuwa na lengo la kwenda kumzuzua mfanyabiashara mmoja mkubwa sana awekeze kwenye ishu yake Bertha ambayo bado sikufahamu ni nini. Yaani kuna kitu Bertha alikuwa ameanza kujenga, bila mimi kujua, ila nafikiri kilikuwa pembeni ya ishu zao za madawa ingawa angekijenga kwa kutegemea nguvu ya biashara yake ya madawa.
Sijui alikuwa anataka kufungua kampuni labda? Na ndiyo alitaka kuwa na mtu kama huyo mfanyabiashara mkubwa wa kusaidia kulikuza jambo hilo upesi na kwa njia isiyo haramu, kwa hiyo hii ndiyo ikawa "mission" yetu ya leo. Asingekwenda huko supermarket wala wapi, na alitaka niwe pamoja naye ili nimpe ushirika wangu kama "mpenzi" wake. Kwa hiyo tulipita kwenye duka moja kubwa la nguo, nami nikavalishwa suti na kiatu cheusi bila kupenda. Nilikuwa mwangalifu sana kuhakikisha hawatambui kwamba nilikuwa na bastola, na Bertha akiwa amependeza tayari, tukaelekea huko Kinondoni.
Zilikuwa ni hafla zenye kuboa sana. Tulisubiri kwa muda mrefu, ndani ya ukumbi kwenye jengo kubwa kweli, na ilinikera kutembea kwenye vigae vilivyoteleza na maviatu haya, kila dakika nilihisi ningeweza kuanguka. Lakini hatimaye madam akawa amepata nafasi yake kuongea na jamaa, akitumia ushawishi wake mzuri kwenye maneno na nguvu ya kuwa mwanamke ili kumzuzua kwelikweli jamaa, na jamaa akatoa kadi yake ya mawasiliano na kumuahidi kupanga makutano "binafsi" ili waongee biashara zaidi. Ikawa ni mwanzo mzuri kwa madam.
Kwa hiyo tumekuja kumalizana na hayo jioni kabisa, na baada ya hapo ndiyo tukaelekea sehemu nzuri pamoja na madam kupata msosi. Bertha alikuwa kwenye hali nzuri kihisia, alionyesha furaha yake waziwazi alipoongea, hata akawa ananilisha eti mbele za watu, na mimi nilijitahidi kufanya ionekane nafurahia sana muda huu pamoja naye, lakini kila nilipomwangalia huyo Dotto aliyekuwa amesimama "kibodigadi" huko pembeni, nilihisi hasira tu iliyonifanya nikose amani hata ya kunisaidia kuendelea kuigiza. Lakini ningefanyaje?
Bwana, tumekuja kurudi kwake Bertha saa tatu usiku baada ya mimi kuamua kupita kwenye gym fulani huko Morocco (ya Dar siyo Africa), ili ninyooshe viungo kidogo. Nilifanya hivi kutokana na maumivu niliyokuwa nayo, na Bertha alilazimisha kuja nami ili anitazame eti. Kulikuwa na wanaume vifutu siyo mchezo, waliomtazama madam na kuonyesha ngangali zao, lakini madam wangu alikuwa na mimi tu, hata akipiga makofi ya pongezi alipoona nimetandika push-up mia moja. Yaani mtu mwingine mpaka angehisi raha!
Kwa hiyo nilijisafishia huko huko baada ya tizi, na tulipofika kwake alikuwa ananitaka nilale naye, lakini nikamwambia hata mimi nilitamani sana kubaki hapo ila kwa leo isingewezekana, maana kuna ishu nilitaka kushughulikia huko Mbagala. Nikajitoa akili na kumpetipeti kwa maneno na miguso na nini, naye akalegeza. Alikuwa hadi ameanza kudeka, yaani hakuwa Bertha niliyemfahamu kabisa, dah!
Ila kuna nyakati nilikuwa namwangaliaaa, jinsi ambavyo hakuwa na dokezo lolote la mambo ya mbeleni yaani, lakini sikuwa na jinsi ila kubaki njia kuu mchezoni. Kuna vitu tu ningepaswa kuamua kuacha vitokee, na vingine ningejitahidi kuvizuia visitokee, lakini kwa kweli kuna sehemu zilizokuwa mpaka zinanifanya nihisi kujuta, basi tu, sikuwa na namna tena. Mchezo ungepaswa kuendelea. Kwa hiyo alipokubali kuniachia, nikaondoka hapo upesi sana ili kurudi Mbagala, madam akiwa pia amenikabidhi suti na viatu vipya viwe vyangu kimoja, huyooo nikatembea.
Alikuwa amenipa ofa ya kusindikizwa na Dotto mpaka nyumbani kwa kutumia gari lake, lakini nikaikataa kistaarabu tu. Jamaa asingeweza kumgusa madam hata kama wangeachwa peke yao kwa sababu najua alikuwa akifuata mipango ya Sudi, kwa hiyo na mimi ningeendelea kukausha tu kwa wakati huu mpaka nikiona wazi kwamba hatua waliyotaka kuchukua dhidi ya madam ingechukuliwa. Nikachukua tu usafiri wa umma, nikiwa kwenye umakini wangu kama ilivyotakiwa kwa wakati huu.
★★
Nimekuja kuifikia Mzinga ikiwa imeshaingia saa sita usiku, kama kawaida, usafiri na changamoto zake. Zamu hii hakukuwa na majangili ama akina Pendo walioagizwa kunifatilia, na nilihakikisha bastola ipo mahala pake ili timbwili lolote likizuka basi nitimbwilishane nalo ipasavyo. Mpaka nafika kwa Ankia sikuchokozwa na yeyote yule, walioniona wakiniangalia tu kama vile hawanijui, ila walishawahi kunisikia.
Nilikuwa nimeshamtumia ujumbe Ankia kumjulisha niko njiani kuja huku, na katikati ya safari hiyo nilikuwa nimewasiliana na Adelina pia. Mwanamke yule tayari alikuwa ameondoka kurudi kwao ile mchana, na nilimwomba radhi tu kutokana na kuwahi kuondoka asubuhi bila kuonana naye, lakini akasema haina shida, na alitarajia tungekuja kukutana tena panapo majaaliwa na mambo kwenda vyema zaidi ya jana. Na hiyo jana aisee! Basi tu, ningepaswa kuisahau baada ya muda.
Ile ndiyo nimefika getini kwa Ankia, kama kawaida nikatazama upande wa jirani zetu, na ikiwa kama bahati tu, nikamwona bibie Miryam akiwa amekaa hapo nje; varandani kwake. Kwa kuwa kutembea kwangu kulifanya sauti za hatua zisikike kutoka chini, nikamwona akinyanyua uso wake na kutazama upande wangu, na kwa sekunde chache tukabaki kuangaliana tu bila wonyesho wa hisia yoyote.
Lakini kiukweli mimi bado nilikuwa nikiteseka sana rohoni, hasa tu baada ya kumwona namna hiyo ghafla kukafanya moyo wangu upige ngoma yenye mdundo mzito sana kifuani utadhani nilikuwa nimemwibia kitu. Ila ni yeye ndiye ambaye alikuwa ameiba moyo wangu, na sijui kama angeweza kutambua hilo, yaani ingenibidi tu niache kuwa kama kuku aisee. Nilimwelewa mno, na nilitaka ifike siku ajue hilo japo sikuwa na uhakika kama angelipenda.
Baada ya kuendelea kumwangalia tu kupitia matundu ya ukuta wa uzio, nikanyanyua kiganja changu na kukitikisa kama kumpa salamu, naye akanyanyua chake na kunipa ishara ya "njoo." Ah! Nikageuka fasta, yaani hakukuwa na ubishi wala uchovu tena hapo, malkia aliniita kwa nini nijizungushe? Nikaenda kufungua geti lao na kumfata hapo ubarazani.
Kama kawaida, alivalia kinguo chake cha kulalia huku akijifunika kwa kikoti chepesi cha nguo hiyo, na nywele zake alizosuka zilikuwa zimefichwa kwa kikofia laini cha kusitiri nywele chenye rangi zambarau. Alikaa kitini akiniangalia kwa utulivu, simu ikiwa mkononi, na pia kulikuwa na kiti kingine pembeni yake ambacho hakikuwa na mtu. Hebu ngoja kwanza. Nilikuwa nimewekewa mimi, ama? Alikuwa ananisubiri? Hapana, ilikuwa bado mapema mno kuwaza hivyo, ila hako kawazo kalisisimua!
Nikajisogeza tu hapo, yeye akiwa ananitazama kwa utulivu usoni, nami nikamwambia, "Uko poa?"
Akatikisa kichwa kukubali na kuendelea kunitazama.
"Mbona umekaa kwenye baridi?" nikamuuliza.
Akapandisha mabega kiasi huku akifumba na kufumbua macho yake, kama kusema basi tu amependa.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Wengine watakuwa wameshalala, eh?"
"Yeah, wako vyumbani..."
"Mbona kama haukuwa peke yako hapa?"
"Nilikuwa nimekaa na Tesha. Ndiyo ameingia ndani muda siyo mrefu kuongea na simu, atakuwa ni demu wake," akasema hivyo.
Akanifanya nicheke ghafla kwa sababu ya kutotarajia aseme hivyo.
"Nini?" akaniuliza.
"Hamna. Sikuwahi tu kufikiri na wewe unasemaga maneno kama 'demu,'" nikamwambia.
"Si ndiyo lugha mnayopenda? Nitafanyaje sasa?" akaniuliza hivyo.
"Ni neno la kawaida. Sema tu watu wameshazoea kulitumia kihuni mno," nikamwambia.
"Mhm... kaa basi unipe company kidogo. Au ume...."
Nikakatisha maneno yake kwa kukaa kitini upesi, naye akatabasamu kiasi.
"Inaonekana umetokea pazuri," akasema hivyo.
"Kwa nini?" nikamuuliza.
"Uko na mood nzuri sana," akasema.
"Ah, hamna. Kawaida mbona?"
"Eti eh?"
"Yeah. Hata nikiwa na stress, mood yangu huwa iko juu tu. Hiyo inasaidia stress zinaondoka zenyewe," nikamwambia.
"Naona una balance nzuri kwenye kupunguza stress, ila mtu akikuudhi humwachi salama," akaniambia hivyo.
"Ahahahah... najua unajua. Sipendi wachokozi," nikamwambia hivyo pia.
Sote tukacheka kidogo maana tulikuwa tunakomea njiani kufika kule ambako upana wa maneno yetu ulikuwa unaelekea.
Akauliza, "Ni sawa. Ila ni hasa ulipokuja huku Mbagala, ama ni kutokea zamani ulikuwa hivyo?"
"Nimekuwa hivyo tokea muda. Kama ni kitu ambacho sipendi zaidi maishani... ni uonevu. Mengine tutavumiliana ila... hata wakati nipo shule, yaani mwalimu tu akimwonea mwanafunzi mwenzangu, ama wanafunzi wenzangu kuoneana, nilikuwa najisikia vibaya sana. Nisingeweza kuzuia yote, lakini kila ilipokuja kwangu..."
"Ungewaka!"
"Wee! Hakuna aliyekuwa ananisogelea," nikajitutumua eti.
"Na bila shaka kwenye masomo ulikuwa mkali pia," akaniambia hivyo.
"Yeah, toka nimeanza shule mpaka nimemaliza. Nilijitahidi sana nisianguke hata mara moja," nikamwambia.
"Hukuwahi kurudia darasa hata moja?" akauliza.
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Mambo kwako yalikuwa easy eh?" akauliza.
Nilianza kuona kwamba Miryam alitaka kunielewa zaidi, kwa hiyo nafasi hii ningeitumia vizuri.
Nikamwambia, "Siyo sana. Mungu alinipa tu ubongo mzuri, lakini bidii ilihitajika ili ufanye kazi vizuri. Nilikuwa napenda sana kusoma, na hali za kimaisha hazikuwa rahisi sana wakati nakua, ila... angalau nilifanikiwa kutoka vizuri shuleni," nikamwambia.
"Ulimaliza shule una miaka mingapi?"
"Form four nimemaliza nina miaka 16," nikamwambia hivyo.
"Eh, mdogo!" akasema hivyo huku akitabasamu.
"Ahah... nilianza shule mdogo, na sikurudiaga, kwa hiyo nikamaliza mdogo," nikasema hivyo.
"Baada ya form four?"
"Nikaenda advance, nilichaguliwa kwenye shule moja huku nzuri, nilipata alama nzuri necta. Yeah... kwa hiyo, nikasoma hiyo miaka miwili, nikafaulu vizuri tena, moja kwa moja Muhimbili..."
"Wow... udaktari..."
"Ndiyo. Nikapiga miaka mitano, na ndani ya hiyo miaka tayari nilikuwa nimeshaanza kupelekwa sehemu hizi au zile kusaidia na kazi... mahospitalini kabisa, kwa hiyo nikawa naona mambo mengi yaliyonisaidia niwe na experience zaidi. Lilipokuja suala la masomo, yaani sikutakaga kuwa mtu wa kuanguka kabisa, sometimes hata nilikuwa napewa chaki niwaelekeze wanafunzi wenzangu maana mpaka walimu walielewa nilikuwa genius..."
"Wacha we!"
"Ahahahah... usipime. Nimetoka chuo nimeiva, nikaenda kufanya internship Bugando, kule Mwanza, halafu...." nikajikuta nimeishia hapo baada ya kukumbukia kitu fulani cha zamani.
Miryam akasema, "Halafu..."
Nikamwangalia na kusema, "Yeah, halafu... ilikuwa kwa mwaka mmoja, ndiyo... nikaja sasa Muhimbili."
"Ni Muhimbili ya Mloganzila, au hiyo ya hapo?"
"Kotekote, ila sanasana hii ya huku. Nilikuwa wa kitengo fulani maalumu, na sikuwa daktari mmoja tu kwenye hicho... kwa hiyo ni kama tuseme zamu zinakuwa zinabadilishwa, lakini baada ya muda nikawa nakaa hii Muhimbili ya huku Kariakoo zaidi..."
"Sawa."
"Yeah. Ndiyo hivyo."
"Na hiyo ni... umekaa kwa muda gani yaani?"
"Miaka kama mitatu," nikamwambia.
"Mh? Miaka mitatu?" akaonekana kushaangaa.
"Ee. Michache?"
"Ahah... me nikafikiri labda hata kumi! Asa' unahitaji likizo ya nini, ni kwamba hupendi wagonjwa ama uvivu tu?" akauliza hivyo.
Nikacheka kidogo, kisha nikamwambia, "Kiukweli, sikuwa mtu wa kupumzika sana tokea nimemaliza chuo, mpaka kuingia kazini, mambo yalikuwa mengi. Sometimes nilikuwa silali, unakuta nakaa macho hata saa za kazi zikiisha me nabaki kuangalia mahitaji ya wagonjwa..."
"Hiyo si ni kazi ya wauguzi?"
"Yes, ila siyo wote. Kuna hizi scenario unakuta... wanakuwepo tu kwa ajili ya wagonjwa kuwaangalia, na hata kama madaktari wengine wanakuwa wameshughulika na wagonjwa wao, me napenda tu pia kuwafanyia double checking ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwa sawa," nikamwambia hivyo.
"Si... sijui kama nimeelewa vizuri..." akasema hivyo.
"Iliwahi kutokea... kuna mgonjwa ambaye alikuwa hospitalini amelazwa baada ya msaada wa madaktari, akawa amepoteza maisha baada ya wao kufikiri msaada wanaotoa unatosha. Na inatokea mara nyingi. Najua kazi zinakuwa rundo, ila... me nilishagaona ni muhimu tu kuhakikisha. Naongelea wagonjwa ambao unakuta wanakuwa wamelazwa, na hali zao ni..."
"Ndiyo, ndiyo, naelewa," akanihakikishia.
"Yeah, ndiyo hivyo. Huwa tu sijisikii vizuri mgonjwa akipoteza uhai wakati yuko hapo hapo hospitali. Kuna vingine haviwezi kuzuilika, ila me nikiwepo... nakuwa nataka kuhakikisha usalama unachekiwa mara mbili zaidi ya ile wanayoona inatosha. Kwa hiyo, nilikuwa mtu wa kutaka kusaidia kila mtu... hata kama nisingeweza kuwasaidia wote... popote ambapo ningeweza, hapo hapo. Mpaka ikawa inazidi. Nikachoka kiasi, ndiyo maana nikapewa haka kalikizo," nikamwambia hivyo.
"Kumbe haukuiomba?" akauliza.
"Hamna. Nilipewa kama break, ili nikirudi niwe kwenye game vizuri hata zaidi kupiga miaka mingine vyema," nikamwambia hivyo.
Akatabasamu kiasi na kuniambia, "Ndiyo maana ukamsaidia na Mariam."
Nikatabasamu kiasi.
"Unapenda kusaidia sana watu. Mpaka unajiingiza kwenye vitu hatari sana ili tu uwasaidie wengine," akasema hivyo.
Nikatabasamu zaidi na kusema, "Eeh."
Lakini nilipomwangalia, nikakuta akinitazama kwa hisia makini zaidi usoni, kama vile alikuwa akinitafakari sanaaa, nami nikajikuta nafifisha tabasamu langu na kubaki nimemtazama usoni kwa umakini pia. Akaacha kuniangalia na kushusha pumzi taratibu, na kiukweli hapo niliweza kuona kwamba alikuwa amezama ndani ya fikira fulani kunielekea, na kuwaza ingekuwa ni fikira gani, kulisisimua sana akili yangu.
Nikamwambia, "Ona... Miryam... kuhusu ile jana..."
"It's okay, Jayden. Tuyasahau tu ya jana, sawa? Tusonge mbele," akaniambia hivyo kwa upole.
Nikatabasamu kiasi na kumwambia, "Sawa. Unajisikiaje lakini? Mgongo I mean..."
"Oh, niko sawa kabisa. Ule mkanda ulipiga zaidi nguo ya ndani, na ilikuwa ngumu, kwa hiyo sijaumia sana..."
"Hata kutia alama?"
"Hapana. Niko poa," akanihakikishia.
Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.
"Na wewe? Vipi mgongo?" akauliza.
"Yeah, nimeamka unauma-uma, ila sa'hivi umeachia. Leo imenibidi niingie gym tena," nikamwambia hivyo.
"Ili uongeze maumivu kufanya yaliyokuwepo yapungue?" akauliza.
"Yep. Na kesho nitaamka yamenikaza zaidi, kwa hiyo sitapaswa kuacha," nikamwambia hivyo.
Akatikisa kichwa taratibu na kusema, "Pole lakini."
"Usijali. Halafu... nimewaza kitu..." nikamwambia.
"Mm-hmm..." akatega sikio.
"Vipi tukiwatoa... familia... out ya pamoja yaani, watembee..." nikamwambia hivyo.
"Mh! Wapi?" akauliza pia huku akitabasamu.
"Popote. Iwe sehemu nzuri, halafu iwape kale ka-sense ka ugeni yaani..."
"Yaani iwe kama lunch au dinner hivi?"
"Eeeh. Ila ukisema lunch... ndo' inafaa. Vipi tukiwatoa wote, Mamu, warembo wangu, Tesha, Ankia... twende tukapige kisinia?" nikamuuliza hivyo kwa uchangamfu.
"Ahahah... kisinia! Nina muda sijafanya hiyo kitu..." akasema hivyo.
"Itakuwa poa sana. Najua Mamu atafurahia sana..."
"Na bado hujamsema Tesha..."
"Ahahahah... tufanye hivyo. Tena mapema yaani, iwe kama tunaamshia-amshia na birthday ya cheupe wangu," nikamwambia.
"Ni sawa. Sema, nilikuwa sijajiandaa, kwa hiyo..."
"Usijali Miryam. Zamu hii itakuwa my treat," nikamwambia hivyo.
"Mm? Wewe mwenyewe?" akauliza.
"Mmm. Na tena ikiwa utaona inafaa... kesho," nikamwambia hivyo kwa uhakika.
"Jayden..."
"Usijali Miryam, everithingi niachie mimi, wewe ni kuja tu. Kila kitu kitakuwepo tayari," nikamwambia hivyo.
"Ahah... ni wazo zuri, sema unapeleka mambo fast mno Jayden..." akasema hivyo.
"Mjini kuchangamka Miryam, hujui?"
Akatabasamu na kuangalia pembeni.
"Come on, ni idea nzuri, we' mwenyewe umesema. Tena nimeshafikiria mahala pazuri pa kulia kisinia kesho. Kubali tu," nikamshawishi.
"Wapi?" akauliza.
"Huko kwetu Sinza," nikamwambia.
"Wewe!" akaonekana kushangaa kidogo.
"Eeh, nakwambia ni pazuri kweli. Familia yako itafurahi sa...."
"Jayden, kuwapeleka huko akina mama, me naona ni mbali. Halafu kesho ninaenda kazini. Bora kama ingekuwa...."
"Siyo siku ya kazi, najua utasema hivyo, lakini hiyo wala siyo shida. Wewe nenda dukani, fanya kazi, ukimaliza unamwacha tu Soraya halafu unakuja. Utatukuta. Mimi ndiyo nitawaongoza hawa wote, tutapanda daladala, halafu tukifika huko nakutumia address kabisa ili uje mwenyewe kwa raha zako..." nikamwambia hivyo kwa ushawishi zaidi.
Akacheka kidogo kwa pumzi na kutikisa kichwa chake.
"Eeh, fanya hivyo. Angalau kesho wote watakuwa na mengi ya kuona... na najua wakifurahia, hata wewe utafurahia pia. Unastahili hilo," nikamwambia hivyo kwa sauti tulivu.
Akaniangalia machoni kwa utulivu tu, mimi nikimpa tabasamu hafifu, naye akasema, "Sawa basi... nitawaambia. Na uhakikishe kila kitu una-handle vizuri..."
Nikanyoosha kiganja kimoja juu na kingine nikiweka moyoni, nami nikasema, "I cross my die, and hope to heart. Kila kitu kitakuwa sawa."
Akacheka kidogo na kusema, "We' ni shida Jayden..."
Akanifanya nicheke kidogo kwa furaha, ndiyo nikamwambia, "Asante Miryam. Hautajutia hii."
"Hapana, mimi ndiyo nikwambie asante Jayden. Unaleta vitu vingi vizuri kwenye familia yangu, na hauchoki yaani. Nathamini sana," akaniambia hivyo kwa sauti yake nyorororo.
Mpaka nikajihisi haya, ile ku-blush, na ndiyo hapa bibie akawa amesema ingefaa aelekee ndani ili autafute usingizi sasa. Basi, na mimi nikaona ninyanyuke, nikamsaidia kuingiza kiti ndani na kumuaga vizuri tena, kisha ndiyo nikaelekea kwa Ankia. Mwanamke tayari alikuwa ameingia kulala, kwa hiyo nikaamua kuelekea tu chumbani kwangu moja kwa moja.
Nilifika tu chumbani na kujitupia kitandani, nikijilaza chali huku mkono wangu nikiukunjia nyuma ya kichwa. Nikajikuta tu natabasamu mwenyewe kutokana na kuhisi raha sana. Yaani eti raha tu kukaa vile na Miryam hapo nje, kuongea kidogo, halafu sasa na vile alivyokuwa ananitazama. Dah! Tule tumawazo tulikuwa tunanifanya najihisi kama Cinderella yaani, ningeweza hata kung'ata kidole kimoja mdomoni kwa shau!
Ilikuwa wazi kwangu zaidi na zaidi kwamba nilimpenda sana huyu mwanamke, na ningetakiwa kufikiria wakati sahihi na njia nzuri ya kumweleza hisia zangu bila ya matatizo yoyote kutokea. Sikujua ikiwa angeweza kunichukulia serious, ila ningehakikisha anajua tu. Iwe isiwe. Nikaamua kujiondoa kwenye ulimwengu wangu wa ndoto za mapenzi ya kweli na kwenda kuoga kwanza, kisha nikarejea na kulala hatimaye. Mbu hao!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments