MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI
★★★★★★★★★★★★★★
Jumanne ikakucha. Leo hii sikuamka mapema wala nini, yaani nililala katika maana ya kwamba ilikuwa siku ya mapumziko kwelikweli kwenye hizi siku za likizo, na moja ambayo ingeburudisha. Angalau leo ningetumia muda mwingi pamoja na binti Mariam na familia yake, na tena tungekwenda sehemu nzuri sana pamoja ili kufurahia mlo wa maana, hivyo kusingekuwa na mambo mengi mno ya kunivunja moyo ingawa najua hayakuwa yameisha.
Baada tu ya kumaliza usafi na kunywa chai pamoja na Ankia, nikawa nimeelekea kwa majirani zetu bila kukawia. Nilikuwa nimeshamwambia na Ankia pia kuhusu matembezi yetu ya baadaye niliyokuwa nimepanga kufanya pamoja nao, na yeye bila shaka alikuwa na utayari wa kuja, ila hakujua sana kama angeweza kuwahi kutoka kazini kwake ili ajiunge nasi.
Nikamsihi tu afunge duka lake ikifika mida ya saa saba au nane mchana ili aje tujiandae kwenda, na nikamtania kwa kusema ningelipia gharama yote ya wateja ambao angewakosa leo kwa wakati mzuri ambao angeupata pamoja nasi. Akawa ameridhia maana alikuwa na hamu pia ya kuja kupiga kisinia pamoja nasi, hivyo akaona awahi kuelekea dukani kwake kufungua kidogo mpaka hiyo saa saba, ndiyo angerudi kujiandaa.
Basi, baada ya kuwa nimefika hapo kwa kina Mariam, nikamkuta binti sebuleni, akiwa amekaa chini kabisa na kuonekana akiandika vitu fulani kwenye daftari. Alikuwa amevaa dera zuri lililoufunika mwili wake vyema pamoja na kinguo fulani kidogo cha kichwani kinachofunika nywele, na baada ya kuwa ameniona akaonyesha furaha yake na moja kwa moja kuniita nione alivyokuwa anaandika. Hapo sebuleni hakukuwa na mtu mwingine isipokuwa yeye, kwa hiyo nikamsogelea na kuchuchumaa, nikiangalia alivyokuwa akiandika.
"Dada ameanza kunionyesha... kutumia singyula na pluro..." akasema hivyo.
"Ahaaa... singular and plural?" nikamsemesha huku nikitabasamu.
"Eeeh. Wingii na umoja. Yaani nayaona mepesi sana," akasema hivyo.
"Na ni mepesi sana, safi. Ona... unaandika vizuri sana Mamu, eh! Yaani unanishinda hadi mimi!" nikampa sifa.
Akacheka kwa furaha na kusema, "Tena hapa ni kidogo. Yaani naandika vitu vingi sana. Kila zoezi dada akinipa, napata yote. Kila kitu rahisi yaani... sijui kwa nini zamani nilikuwa naona magumu!"
Nikamwangalia na kutabasamu kwa hisia kiasi, kwa sababu nilitambua kwamba akili yake ilikuwa ikifunguka zaidi, na aliongea kama vile hakujua kabisa kwamba alikuwa na shida kichwani.
"Ya kitoto sana haya, JC. Kiingereza naweza mbona? Uwe unanipa yale magumu ndiyo yenye challenge zaidi... dada ananiona kama yai tu! Nipe magumu magumu nimwonyeshe nayaweza," akasema hivyo.
"Ahah... kumbe unayajua eh?"
"Najua ndiyo!"
"Unasoma sana?"
"Eeh. Nimekuta madaftari huko ndani, kumbe yalikuwaga yangu! Mambo mengi nimeandika, mengine siyaelewi, lakini nimekuta... ma-matiki, matiki, matiki. Tatizo mnanipa marahisi mno, nataka niyajue magumu zaidi na yenyewe yawe marahisi. Sawa JC?" akaongea kwa uhakika kabisa.
Nikatabasamu na kumwambia, "Sawa. Usijali. Kafate na daftari lako moja niyaone yanayokuchanganya."
"Yes!" akasema hivyo kwa sauti ya juu.
Kakanyanyuka kabisa na kukimbilia chumbani huko, na ni hapo ndiyo Bi Zawadi akawa ametoka ndani ya chumba chake. Nikasimama na kutabasamu kwa furaha.
"Mamu? Huyo vipi tena?" Bi Zawadi akanisemesha hivyo huku akija upande wangu.
"Amefurahi, nimemwambia afate daftari lake. Shikamoo?" nikasema hivyo
"Marahaba baba. Basi kanishtua, nikafikiri kuna mtu kavunja mtungi," akasema hivyo.
Nikacheka kidogo kwa pumzi na kusema, "Pole. Ulikuwa umelala?"
"Hapana, nilikuwa tu ndani nakunja nguo. Vipi, JC? Unaendeleaje?"
"Niko poa kabisa cheupe wangu. Jana nilichelewa kurudi nikakuta mmeshasinzia," nikamwambia.
"Kumbe? Basi haina shida. Tesha alituambia yote yaliyotokea ile Jumapili. Aisee, poleni," akasema hivyo.
"Ah, asante... na usijali. Yameshapita."
"Mmm. Niliongea na mzee Hamadi akasema uliwanyoosha waliomwonea Miryam. Hivyo ndiyo inavyotakiwa kijana wangu. Safi sana!" akasema hivyo.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Asante. Vipi hapa? Mnaendeleaje?"
"Tuko salama kabisa. Hofu kwako. Nasikia walikupiga na virungu ulipombutua yule mjinga aliyemchapa Miryam na waya..."
"Eee, yule jamaa si mjinga tu? Akafikiri tutaogopa. Nikampa dozi yake, hatathubutu tena," nikamwambia hivyo.
Bi Zawadi akacheka na kugongesha kiganja chake kwangu, naye akasema, "Ni vizuri sana. Endelea kuwapa dozi zao mbabe wetu."
"Ahahahah... haupingwi mama..."
Bi Zawadi akacheka kidogo.
"Vipi wengine? Wako wapi?" nikamuuliza.
"Tesha ameenda na mama yake mkubwa hapo sokoni Mzinga, na Jamila na yeye ananyoosha miguu kidogo," akasema hivyo.
"Okay, ni vizuri sana. Na Miryam? Kazini mapema?"
"Eeeh. Halafu naona kama vile hayuko sawa," akaniambia hivyo.
"Kwa nini unasema hivyo?" nikawa makini zaidi.
"Sijui tu. Nahisi kama vile anasumbuliwa na ki...."
"JC, hili hapa," Mariam akawa amerejea pamoja na daftari la somo la kiingereza, la kwake wakati yupo kidato cha nne.
"Ooh, safi. Haya... nenda sa' hapo mezani. Chukua na kalamu zako, nakuja unionyeshe, sawa?" nikamwambia hivyo.
Akatikisa kichwa kukubali na kuokota daftari lile lililokuwa chini na kalamu zake, naye akaelekea pale dining.
"Amechangamka sana sasa hivi, JC," Bi Zawadi akaniambia hivyo kwa sauti ya chini.
"Eeh, maendeleo," nikamwambia hivyo.
"Sawa, basi me niwaache mmalize..."
"Aa... ndiyo, ila... niambie... kwa nini umesema unahisi Miryam ana tatizo?" nikamuuliza hivyo kwa sauti ya chini.
"Ahaa... eee, yaani nimemsikia tu hii asubuhi anaongea kwenye simu sijui na nani... ila inaonekana ni kitu kimemshangaza kwa jinsi alivyokuwa anaongea. Ni kama vile nimemsikia anaongelea madeni, halafu... na kwamba haimhusu yeye sijui, yaani sikuelewa sana, alikuwa anaongelea huko chumbani..." akasema hivyo.
Nikaweka uso makini zaidi.
"Sikujua ni nini... alipotoka chumbani nikamuuliza, akasema hamna shida. Ila, ameondoka kama vile hana raha. Itakuwa ni mambo ya kazi. Halafu... ametuambia unatutoa out leo. Ni kweli?" Bi Zawadi akasema hivyo.
Nikamtazama kishauku zaidi na kusema, "Eeeh. Tunaenda kula kisinia."
"Wow! JC wewe! Mamu... umesikia? Tunaenda kula kisinia leo," Bi Zawadi akasema hivyo kwa furaha.
Mariam akamwangalia na kuuliza, "Kwa nini tunaenda kula sinia?"
Mimi na Bi Zawadi tukaangaliana na kujitahidi kubana vicheko vyetu.
"Ni wapi?" Mariam akauliza.
"Usijali Mamu, nitawapeleka, utapaona. Pazuri. Utapenda sana kisinia," nikamwambia hivyo binti.
"Mi' sitaki kutafuna sinia," Mariam akasema hivyo huku akinyanyua bega kama vile mtoto.
Mimi na Bi Zawadi tukacheka kidogo.
"Njoo sasa JC unifundishe," kakaongea kwa msisitizo.
Bi Zawadi akasema, "Haya baba, kazi kwako."
"Ahah... sawa, asante cheupe wangu."
"Tunaanza kujiandaa saa ngapi sasa? Yaani, tuondoke saa ngapi?" Bi Zawadi akauliza.
"Tutaondoka kwenye saa tisa. Kuna usafiri nime..."
"JC!" Mamu akaniita kwa njia fulani ya lazima kwa kudeka.
"Eh, ngoja niwahi. Ila saa tisa tunaondoka..." nikamwambia hivyo Bi Zawadi huku nikimkimbia.
Akacheka kidogo wakati nilipokuwa nimemfikia Mariam hapo dining, nami nikakaa pembeni yake na kuanza kumwelekeza hivi na vile, na mama yake mkubwa akawa amerudi chumbani kwake.
★★
Nimekaa na Mariam hapo nikimfundisha mambo kadhaa kwenye lugha ya kiingereza, na niliona namna ambavyo akili yake ilizidi kuwa nyepesi kila dakika. Alishika vitu upesi, na najua hiyo ilikuwa kwa sababu tayari alikuwa anavijua, sema tu alikuwa amesahau. Sasa ndiyo tulikuwa kwenye daraja la kuvivusha zaidi hivyo vitu ili viingie kwenye ubongo wake kwa mara nyingine tena na kutomwondoka kabisa.
Tesha na Bi Jamila walikuwa wamesharudi kutoka kutembea kidogo, mama huyo akiwa amehitaji zoezi hilo dogo kwa ajili ya maandalizi ya kuondoka baadaye kwenda matembezi huko ambako ningewapeleka. Shadya hangeweza kuja nasi kutokana na kuwa sehemu nyingine kwa leo, ndiyo maana sikumkuta hata na hapa pia. Tesha alikuwa na hamu na haya matembezi maana alielewa ni namna gani Sinza ilivyokuwa na watoto wakali, kama kawaida akili yake ikiwa hapo tu, kwa hiyo eti alikuwa amepanga kupendeza haswa.
Nilikuwa bado nikifikiria kuhusu suala aliloniambia Bi Zawadi kuhusu Miryam. Inaonekana kulikuwa na kitu kipya kilichomsumbua bibie, labda kweli ingekuwa ni masuala ya kazi, lakini kitu tu kujua aliondoka akiwa hana raha kilininyima amani. Nikawa nataka kujua endapo kama ningeweza kusaidia kwa lolote lile, na labda ningempa hiyo ofa baadaye tukishakutana ikiwa bado angekuwa hajapata suluhisho kwa tatizo lake.
Hangekuwa mgumu mno kukubali msaada wangu kama ilivyokuwa kipindi kile, kwa sababu sasa hivi aliniona kama rafiki, na mimi hisia zangu kumwelekea ndiyo zingenifanya nijitoe kwa lolote kwa ajili yake mpaka afanikiwe kutatua shida zake. Kwa hiyo matembezi haya niliyokuwa nimepanga tayari yangeifanya siku yetu iishie pazuri sana, na hivyo mikazo yoyote ambayo malkia wa moyo wangu alikuwa akiipitia ingeweza kupungua uzito kwa furaha ambayo angepata akiwa pamoja nasi. Napenda kumwita hivyo!
Ikiwa ndiyo imeshafika mida ya saa saba mchana, nikawa nimepigiwa simu na rafiki yangu Bobo. Bobo bwana alikuwa anataka kuniona, akisema kuna kitu cha muhimu alihitaji kuzungumza nami maana kilikuwa kinamsumbua, na alikuwa hapo Masai tu ametulia hivyo niende kumwona. Nikaweka wazi kwamba sikuwa na muda mrefu sana maana nilihitaji kuwa sehemu nyingine, na yeye akasema haingechukua muda mrefu; maongezi mafupi tu.
Kwa muda huu, mama wakubwa walikuwa wakijiandaa huko pamoja na Mariam pia, na mimi na Tesha tulikuwa sebuleni tu. Baada ya Bobo kukata simu nikamwambia Tesha kuwa naenda hapo nje kukutana na jamaa maana amesema kuna ishu ya muhimu alitaka kuzungumza pamoja nami, naye akasema haina shida, yeye pia angetumia huo muda kuanza kujiandaa. Nilikuwa nimewaambia kwamba nimekodi usafiri ambao ungetupeleka moja kwa moja mpaka huko Sinza, na ungefika huku kwenye saa tisa, ndiyo sababu wote walikuwa wanachangamka.
Hivyo nikatoka hapo na kwenda mpaka Masai, jua likiwa kali kinoma, na nilipofika, hawakuwa wameanza shughuli zao bado. Hakukuwa na watu zaidi ya wahusika wa kuendesha biashara katika maandalizi yao, na Bobo alikuwa amekaa pale pale ambapo tulikaa ile juzi kwenye mechi ya Simba na Yanga pamoja na wakina Miryam. Alikuwa amevaa T-shirt ya kijivu na suruali nyeusi ya jeans, huku kofia nyeupe ikificha uso wake kiasi.
Nikaenda mpaka hapo na kusalimiana naye kirafiki, kisha nikakaa pembeni yake na kusema, "Uko poa mwanetu?"
"Eeh, kwa nini nisiwe poa?" akauliza pia.
"Simu yako ya ghafla imenifanya nihisi labda umevurugwa, nimekuja nakimbia."
Akacheka na kusema, "Mbona sioni jasho?"
"Ah, sitokagi jasho..."
"Hah... hakuna mtu wa hivyo bana, unazingua."
"Nambie mtu wangu. Mishe niaje?"
"Fresh. Mwanetu na wewe una michongo ya ukweli siku hizi, hutulii sehemu moja..."
"Eeh, michongo lazima. Nitaishije mjini sa' nisipo-hustle, we' vipi?"
"Ahahahah... hata me naona. Bado unamla Bertha?" akauliza.
"Well... sijui hata nikwambiaje. Analika, lakini..."
"Siyo kwamba ni wa kumeza?"
Akanifanya nicheke kidogo na kusema,"Kidogo umeelekea kwenyewe, maana siyo kwamba anatemwa."
"Ahah... sawa. Uko vizuri mwanangu," akasema hivyo kwa njia fulani ya huzuni hivi.
"Vipi wewe? Salome wako amekutema au?" nikamuuliza.
"Aa, kale kademu? Me ndo' nimekatema," akasema hivyo.
"Ih? Lini tena?"
"Hiyo hiyo Jumapili, kabla ya mechi."
"Eh! Yaani umemtambulisha kwangu Jumamosi, halafu Jumapili ukamtema? We' kweli Bobo!" nikamwambia hivyo.
Akacheka sana na kugonga kiganja chake kwenye changu, naye akasema, "Kijinga tu kile. Kilikuwa kinanipotezea time... unajua huwa havitulii."
"We' umetulia kwani?" nikampa suto.
"Ah... ndo' nilichokuitia mwanangu," akasema hivyo.
"Nini? Unataka nikutafutie wa kukutuliza?"
Akasema, "Nimeshampata. Oya, JC... huyu mwanamke nimemwelewa sana. Sana yaani mwanangu."
"Wee! Usiniambie... dem mama, nini?" nikamsemesha kizembe.
"Siyo mchezo kaka, niko serious yaani. Hawa watoto wadogo-wadogo, sitafika popote. Nahitaji mwanamke wa kutulia naye... na ndo' huyu nimeshamwona atakayefaa. Perfect yaani," akaniambia hivyo.
"Okay. Fresh kaka, mawazo kuntu. Na... nadhani unaniambia hivyo kwa sababu huyo mwanamke namjua, si ndiyo?"
"Ee, unamjua. Ndiyo maana nataka tuchonge... maana nakuwa naona kama ashanipiga chini..."
"Ni... ahah, ashakupigaje chini wakati hata hujamtokea? We'... ni nani kwanza?"
"Ankia."
"Wewee! Hahahah..." nikajikuta nacheka tu.
"Si umeona? Lazima ucheke..." akasema hivyo.
"Ahahah... hamna, nimefurahi tu. Yaani... umemwelewa Ankia kihivyo kweli, ama unataka kula tu?"
"Nimempenda, JC. Sikutanii yaani," akaniambia hivyo kwa hisia.
"Dah! Mwambie sasa... mtoe hata anywe bia na nini, mwanamke independent yule, kwa hiyo uongee naye na kumtendea kama mwanaume independent pia."
"Hiyo siyo shida. Nataka tu mwanga halisi..."
"Mwanga wa nini?"
"Uliniambiaga ulishamla," akasema hivyo.
"Eh! Ahee. Well... ile ilikuwa tu... si unajua yaani..."
"Naelewa, ila hiyo ndiyo point yangu. Nataka kujua kama yuko easy kihivyo, kiasi kwamba atatoka na mwanaume yeyote kama JC tu ulivyokuja ukampagawisha, mkalala..."
"Siyo hivyo..."
"... ama kama, yaani anaweza kuwa mwaminifu ama vipi? Maana sikutanii bro, natafuta kutulia sa'hivi," akaniambia hivyo.
Niliona yuko serious, kwa hiyo nikamwambia, "Sawa. Nimekuelewa. Yaani... Ankia ni mwanamke aliyetulia. Sana. Sawa? Anajua kutulia. La muhimu awe amekupenda. Akikupenda, we' mwenyewe utafurahia. Yaani ni kimoja. Mimi nilikuwa yule mtu wa kurukaruka sana, si unajua? Nikaona anataka tuzame, kwa hiyo nikamwambia sipo hivyo, mapema kabisa ili asije kuumia. Yaani ni mwanamke ambaye akikupenda, amekupenda, kamaliza. Kitakachobaki yaani itakuwa labda ni wewe tu ndiyo umuumize..."
"Kumbe?"
"Uhakika. Kwa hiyo Bobo... me sa'hivi nimeshapigilia msumari uhusiano wangu pamoja naye iwe kama kaka na dada yaani, na toka hapo, katulia zake mwenyewe yaani kama hana mpango. Kwa hiyo inabidi uwahi, halafu... uende na swaga za uhakika aone upo serious... kuna majamaa yameshaanza kummendea," nikamwambia hivyo.
"Dah! Basi kaka, me kweli nataka nimsemeshe. Nimefikiria sana yaani..." akaniambia hivyo.
"Jaribu. Ongea naye... bangi weka pembeni yaani, najua atataka mwanaume anayejielewa..."
"Uliniona lini navuta, we' fala nini?" akanisemesha hivyo na kucheka kidogo.
"Ahahahah... haya kazi kwako. Ila... kwanza umeanza kumwangalia kama hivyo kutokea lini?" nikamuuliza.
"Ile siku, juzi, wale wajinga walipotukamata..."
"Aaaa... ile juzi..."
"Eeeh. Alivyokuwa anawatolea mapovu yaani nilimwelewa sana."
"Unapenda hivyo?"
"Eeh, yaani... mwanamke anayejua ku-fight kutetea haki hata kama anapigana na askari... ni mzuri sana. Napenda niwe na mwanamke wa hivyo maana atapambania familia yetu kwa ujasiri kama huo," Bobo akafunguka namna hiyo.
Nikampiga ngumi kiasi begani na kusema, "Hapo ndo' umeondoa bangi sasa. Ongea na Ankia kwa njia hiyo hiyo aone kile unachotaka na unachoweza kumpa pia, na atakachoamua, chochote kile... uwe tayari kukipokea yaani."
"Fact mwanangu," akasema hivyo.
"Na ikitokea akakukubali usije ukafanya ujinga! Kaka zake tuko hapa," nikamtania.
"Eheh... eti kaka yake, 'akati ushamlamba lile shundu!"
"Ahahah... na ni la ukweli!" nikamwambia hivyo.
"Fala wewe!" akasema hivyo.
Sote tukacheka kidogo na utani mwingine kuendeleza, mpaka inaingia saa nane bado nikawa hapo Masai, ndiyo nikamuaga jamaa na kuelekea kwa Ankia sasa ili nijiandae pia. Inaonekana na Ankia angekuwa na jambo jipya la kufikiria kuanzia sasa ikiwa Bobo angemtokea, na nisingemwambia chochote mpaka wakati ambao jamaa angepiga hatua kwake. Kwa hiyo mimi na mwana tukawa kwenye usawa wa kutaka kuwafikishia hisia zetu wanawake tuliowapenda, ilisisimua mno!
★★
Maandalizi yakakamilika bwana. Mzee mzima nikavaa zangu T-shirt jeusi lenye mikono mirefu, lililokuwa jipya na hii ikiwa ndiyo mara ya kwanza kulivaa. Rangi nyeusi iliendana vizuri sana na rangi ya ngozi yangu, kwa hiyo nilihakikisha najiweka fresh zaidi kimwonekano kuanzia utosini mpaka vidoleni. Suruali ya jeans ya samawati pamoja na sneaker nyeupe chini zilikamilisha mwonekano wangu, bila kusahau saa yangu maridadi mkononi. Bastola isingenihusu kwa leo. Nilihisi amani.
Ankia alikuwa amesharejea pia na kwenda kuoga fasta utadhani alikuwa ameambiwa anaachwa na treni. Akavalia nguo nyepesi kwa juu, kama T-shirt ya kijani laini lenye maneno "Supreme" kifuani (zile zinazokuwa ndefu, halafu pembeni kwenye hips zinakuwa kama zimechanwa na kuunganikia kiunoni), suruali nyeusi ya skinny iliyomchora huko nyuma, wee! Akavaa na ndala nyeupe za kike huku akibebelea pochi ndogo mkononi, na nywele zake alikuwa amezichana kabisa na kuwekea tiara yenye rangi ya njano kwa mbele kichwani. Alipendeza.
Tukatoka, tukafunga nyumba, kisha tukaelekea kwa kina Tesha. Tayari jamaa, mama wakubwa, na Mariam walikuwa wameshajivika mavazi mazuri yaliyowapendezesha, mama wakubwa wakivaa kimama zaidi, Tesha kisharobaro zaidi kwa Manga nyeupe na suruali ya jeans iliyo na mtindo wa kuchanika-chanika, huku Mariam akivalia gauni safi na refu la blue mchanganyiko na nyeupe, na nywele zake laini akiwa amesukwa kwa mkono njia tano sijui sita na kuvaa kitambaa mbele ya paji la uso wake mpaka nyuma ya kichwa.
Mariam alionekana kweli kuwa mwanadada zaidi ya jinsi ambavyo alikuwa mtoto kwa ndani, na kutoka kwake leo ingekuwa rudio la kuwafanya wenye kumtazama wamtazame haswa. Alikuwa mzuri kama Miryam yaani, na najua muda si mrefu angeweza tena kuitafuta njia yake katikati ya ulimwengu wa nje uliomzunguka. Matembezi haya yalikuwa sehemu nzuri ya kuanzisha hilo na kuliendeleza zaidi.
Hivyo kila kitu kikiwa kimeachwa kimpangilio hapo, sote kwa pamoja tukaondoka. Ilikuwa rahisi kwa wengi waliofahamiana na akina Bi Zawadi hapo mtaani kuwasemesha na kuwasifia kuwa wamependeza na wao kuwajibu vizuri, lakini mimi na Tesha tulitembea mbele ya wanawake kama vile hatuwajali. Sikutaka niwe na shobo kwa wengi bado hata kama nilikuwa pamoja na hawa marafiki zangu, yaani ndiyo uliokuwa mtindo wangu. Mwendo wa taratibu tu, mpaka tukawa tumefika hapo Mzinga barabarani, na angalau jua lilikuwa limefunikwa kwa mawingu wakati huu.
Gari ambalo nilikuwa nimekodi tayari lilikuwa hapo likitusubiri, na mama wakubwa hawakuwa wametarajia ingekuwa ni Noah nzuri sana, wakiwa wamefikiri nilikodi taxi labda. Kwa hiyo wakaingia, mimi nikikaa na Mariam, mama wakubwa, pamoja na Ankia huku siti za nyuma, naye Tesha akakaa huko mbele na dereva.
Hii ilikuwa kama Uber tu, ingawa niliiagiza kutokea huko huko Sinza maana huyu dereva nilimfahamu, kwa hiyo ilikuwa rahisi kwake kuja mpaka huku kwa kuwa alijua sikuwa mbabaishi; angelipwa vizuri. Mariam alionekana kuwa tayari kutalii mazingira ya sehemu nyingine ya mbali baada ya kipindi kirefu kuwa kimepita akiwa nyumbani tu, na safari ya kuelekea Sinza ikaanza.
★★
Safari ya kuelekea huko Sinza bwana ikawa imetufikisha maeneo hayo kupita hadi Makumbusho na kusonga mbele zaidi. Wapendwa wangu hawa walifurahia sana kuwa nje kama hivi, maeneo yenye majengo maridadi na mifumo iliyoonekana kuwa ya hali ya juu kwa nchi yetu, na Mariam ndiye aliyefurahia zaidi na kuulizia hicho ni nini, kile ni nini, karibia kila mara. Binti hakuwahi kufika huku kabla, ama labda aliwahi lakini hakukumbuka, kwa hiyo ilikuwa nafasi nzuri kumwonyesha vitu vingi na kumwelekeza kwa mengi pia.
Imefika saa kumi dakika za mapema, tukawa tumeingia eneo fulani ukiwa unaelekea Mbezi ama Tegeta hapo kati, wanapaita Mbezi Jogoo, na ndiko kulipokuwa na hiyo sehemu niliyopanga kuwapeleka marafiki zangu. Dereva akaliingiza gari eneo la maegesho nje ya hoteli nzuri ya kitalii (resort), isiyokuwa ghorofa wala nini, kawaida tu ingawa ilisambaa kwa eneo kubwa, nasi ndiyo tukashuka hapo. Nikawa nimemlipa jamaa ya kwanza na kumruhusu aondoke, kisha wakati ambao tungemaliza ishu zetu ningemwita tena. Akasepa.
Hoteli hii iliitwa Viva, ikiwa na mwonekano mzuri kwa kujengewa mbao nene kuizunguka zaidi ya matofali hapa au kule, ikiwa na yale madari ya nyasi ngumu na vijumba vidogo-vidogo vya aina hiyo hiyo kwa ajili ya wageni au wateja, sehemu pana ya ndani yenye meza na viti vingi, bar na kaunta refu huko mbele, sehemu yenye swimming pool mbele zaidi, na ndiyo lingefata jengo lililobeba vyumba vya kulala wageni.
Ilikuwa maridadi, wengi waliofika hapo walikuwa watu wenye pesa, na kwa leo hakukuwa na watu wengi sana kwa muda huo tuliofika kwa hiyo palitulia, na ndiyo maana niliamua kuwaleta hawa huku. Palitulia sana. Tukapata meza ndefu ya kukaa kutoshea "familia" nzima, na hatukusahau kumtunzia siti bibie Miryam pia, kisha nikaagiza visinia viwili kudadeki! Na juisi za kupoza koo kwanza! Tulikuwa tumeshawasiliana na Miryam, nikimtumia anwani na namna ya kufika huku, na yeye akawa ameniambia yuko njiani. Msisimko!
Kwa hiyo zikafata story za hapa na pale, Bi Zawadi na Bi Jamila wakionekana kustareheka, na Mariam akiangalia mazingira ya hapa na kule, kisha ndiyo kisinia namba moja kikawa kimeletwa. We! Msosi kama wote yaani. Masoseji, manyama ya ng'ombe, kuku, pweza, mbuzi, chips yai, matunda yaliyokatwa-katwa, samaki, ubwabwa, michuzi, yaani ujazo! Na matomato na mapilipili pembeni, raa! Bila kusubiri filimbi ipigwe, kandanda ya makamuzi ikaanza.
Tulikula kwa raha zetu yaani, msosi ulikuwa wa maana, mpaka inafika saa kumi na moja na nusu hivi jioni, ndiyo bibie Miryam akawa amefika. Ndugu zake walifurahi kweli, hata Mariam akanyanyuka na kwenda kumkumbatia utadhani alikuwa mama yake mzazi vile. Nilijikuta nikibaki kumtazama tu huyu mwanamke, kwa upendo mwingi sana.
Naona leo alikuwa ameenda kazini kwake akiwa amevalia T-shirt jekundu la mikono mifupi pamoja na suruali nyeusi iliyombana vyema, akionyesha unono wake usiofichika hata kama angekuwa amevaa pana. Nywele zake za kusukwa alikuwa amezibana kisogoni na kuziachia kiasi zimwagikie mgongoni, naye alivaa tabasamu mwanana usoni pia ambalo liliongezea urembo wake urembo maradufu. Hata kama angekuwa na stress za kazini, kweli kuja hapa kungeziondoa.
Kwa hiyo akaketi pamoja nasi, na alikuwa amefika kwenye muda mwafaka ambao kisinia cha pili kikaletwa. Sisi wengine tayari tulikuwa tumeshaanza kushiba, kwa hiyo tukamwambia hilo sinia la pili alipaswa kulimaliza lote. Alifurahia utani mwingi kutoka kwangu, kwa Ankia, na Tesha pia, na aisee kumwangalia huyu mwanamke akitabasamu ama kucheka kulinipa raha ya ndani sana moyoni.
Alipendeza mno kufurahia maisha, basi tu yaani kama ujuavyo maisha hayako kihaki kwa kila mmoja, kwa hiyo changamoto alizokuwa amepitia zilimfanya asiyafurahie kivile na kuwa jinsi alivyokuwa. Nilitamani sana ije siku ambayo mimi ndiyo ningemwondolea mambo yote yaliyokuwa yakimsumbua, hata kama sijui ikiwa kuna mambo yalikuwa yanamsumbua. Nilitaka tu kuwepo kwa ajili yake. Kufanya vitu kama hivi na zaidi ambavyo havingeondoa tabasamu usoni kwake daima. Nilikuwa nimempenda Miryam kweli.
Kisinia cha pili hakikwenda mpaka mwisho, kwa hiyo Tesha na ujanja wake akaona aende kutafuta mfuko ili chochote kile kisibaki. Wakati huo, Miryam pia alikuwa ameshashiba, na Ankia akapendekeza tuanze kupiga picha za pamoja kutunza kumbukumbu nzuri za siku hii. Haikupingwa. Tukasogea sehemu ya nje yenye bustani iliyotunzwa vyema na kuanza kupiga picha kwa pamoja, hadi tukaenda upande uliokuwa na bwawa la kuogelea, na Tesha akawa amerejea na mfuko na kutunza vyakula alivyotaka kwenda kukamulia nyumbani.
Wakati Tesha akiwa amekuja kwetu kupiga picha pia, simu yangu ikaita, mpigaji akiwa ni Bertha, nami nikaona nijitenge kwanza ili nikapokee na kumsikiliza. Ikiwa ni saa kumi na mbili iliyoelekea kulikaribisha giza la saa moja sasa, nikatoka hapo mpaka pale nje usawa wa magari yaliyoegeshwa, pick-up ya Miryam ikionekana kuwepo hapo mbele pia, na hakukuwa na watu huku kwa nje kabisa labda tu walioonekana kwa huko barabarani zaidi.
Ndiyo nikawa nimepokea na nikaongea na madam. Alikuwa tu ameni-miss, na kuniuliza kwa nini sikuwa nimemtafuta leo. Nikamwambia kuna harakati za hapa na pale nilikuwa nikifatilia na nini ndiyo maana, naye akaonyesha uelewa na kuniambia kesho nihakikishe ninaenda kwake nikishatoka kule supermarket, nami nikakubaliana na hilo na kuagana naye haraka baada ya kuona bibie Miryam anakuja upande wangu, ndiyo madam akakata simu. Malkia akawa anakuja kwangu!
Taratibu akaendelea kuja tu mpaka aliponifikia na kusimama pembeni yangu, naye akaachia tabasamu hafifu huku akinitazama kwa macho yake mazuri. "Kwa nini unakata simu kila nikikukuta unaongea na 'baby?'" akauliza hivyo.
Akanifanya nicheke kidogo, naye akacheka pia, kisha nikamwambia, "Miryam unanisoma vibaya bwana."
"Kumbe?"
"Eeeh. Huyo baby unayemsemea hayupo," nikamwambia.
"Mmm... kweli?"
"Kabisa."
"Mbona umekuja huku kote sa' kuongea na simu kama siyo baby?" akauliza kiutani.
"Siyo... ni rafiki tu, siyo baby bwana... ahah..." eti nikahisi haya.
"Mmmm... Jayden, una-blush!" Miryam akasema hivyo kusisitiza zaidi.
Na kweli, nilikuwa nina-"blush" hapa, ila dada wa watu hakujua hiyo ilikuwa kwa sababu yake. Nikabaki kutabasamu tu.
"Gharama ya visinia imetoka ngapi?" akaniuliza.
Nikamwangalia usoni kwa njia ya kuhukumu kiasi.
"Ahah... niambie tu, sitafanya protest yoyote," akasema.
Nikamkazia macho kiasi.
"Kweli. Niambie tu," akasema hivyo.
Nikamwambia, "Laki tatu."
Akapandisha nyusi kama kushangaa kiasi, naye akacheka kidogo kwa pumzi na kuangalia pembeni.
Nikasema, "Okay, nahisi protest inakuja..."
Akasema, "Hamna, wala... hamna shida. Najua umetoa kwa kupenda. Nataka tu kusema asante. Asante sana Jayden. Kwa... kwa kila kitu. Nimefurahia sana kuja hapa, japo nimechelewa lakini... nimefurahia."
Aliongea kwa hisia za shukrani kwelikweli, nami nikamwambia, "Usijali Miryam. Tuko pamoja. Familia yako ni kama yangu pia. Napenda kuwaona wanafurahi."
Akatabasamu kiasi na kusema, "Mara nyingi sana umekuja na familia yako hapa, eti?"
"Ah, siyo mara nyingi... sanasana tu kama dada yangu alikuwa na vi-party na nini, ndiyo tungekuja hapa, au na marafiki... ila sijawahi kuja na mama au mzee hapa..." nikamfahamisha.
"Ahaa... na dada yako, Jasmine, anaonekana mtu wa kupenda party eh?"
"We! Sana! Anapenda sana hayo mambo," nikamwambia.
"Si kama wewe tu? Mtoto wa kishua," akanitania.
"Ahahah... usiniite hivyo bwana..."
"Ahahahah... sawa. Kwa hiyo mna memory nzuri sana hapa eti?" akauliza.
"Eeh. Ahahah... ngoja nikuchekeshe. Kuna rafiki yangu tunamwita Simba, yaani mambo yake, kama Tesha tu..."
Akatabasamu kiasi na kusema, "Enhe..."
"Ilikuwa birthday ya Jasmine. Tukaja hapa. Sasa... alikuwa ameenda uani, amebanwa, kala sanaaa... akawa ameingia kwenye mlango wa choo kilichopigwa marufuku, akashusha haja..."
"Eh!" akasema hivyo kwa sauti ya chini.
"Ahahahah... wasimamizi wakamkuta. Faini ilikuwa elfu hamsini, afu' hakuwa hata na mia. Unajua alichofanya?"
"Akafanyaje?"
"Akaanza kuigiza kwamba ye' kiziwi, hasikii na ni bubu. Akawa anaguna guna tu, anatoa ishara za kuonewa huruma mpaka ikabidi wamwache tu... ahahahah... Miryam, tulicheka! Alikuja kurudi kwetu bado anaendelea kuigiza bubu maana kama wale watu wangemgundua alikuwa amewauza, hela angetoa tu...."
Wakati nikiwa namwelezea bibie hicho kisa, nilikuwa natoa ishara nyingi kwa mikono na mwili kutokana na hisia ya kuchangamka iliyochochewa na kumsikia akicheka kwa furaha sana. Alifurahia sana hicho kisa kiasi kwamba aliendelea kucheka tu, na mimi ndiyo nikaendelea kukielezea kwa njia zilizomfanya afurahie zaidi.
Nikawa nimegeukia upande mwingine nilipokuwa namwonyesha namna ambavyo kipindi hicho huyo Simba aliigiza kutembea kwa njia fulani kama mlemavu ili aonewe huruma zaidi, ndiyo sauti tamu ya Miryam akiwa anacheka ikakoma ghafla. Mimi nikiwa natabasamu, nikageuka kumwangalia usoni na kushtuka kiasi moyoni baada ya kuona jambo fulani ambalo sikuwa nimetarajia kabisa.
"Mambo vipi... JC?"
Swali hilo halikuulizwa na Miryam, bali mtu aliyekuwa amesimama nyuma yake. Tena nikisema nyuma yake, yaani namaanisha alikuwa amegusanisha mwili wake karibu zaidi na mwili wa Miryam kutokea nyuma.
Mtu huyu alikuwa ni mwanaume mrefu, mweusi, ambaye alikuwa mwenye mwili mkubwa kiasi cha kuwa mnene, akivalia sweta zito jeusi lenye kufunika kichwa chake kuniruhusu kuona tu uso wake wenye ndevu nyingi kutokea kwenye timba uliokuwa makini vibaya mno. Kumtazama kwa umakini usoni kukawa kumenifanya nimtambue. Alikuwa ndiyo yule jamaa aliyenifatilia kule Kariakoo ile Ijumaa kabla ya mimi kufanikiwa kumpiga chenga. Ndiyo huyu aliyekuwa amemshika Miryam sasa.
Kuangalia vizuri jinsi jamaa alivyokuwa amekunjia mkono wake mmoja usawa wa kiuno chake Miryam, ndiyo nikawa nimeona kisu kifupi na kinene kiganjani mwake, ambacho alikigusisha kwenye nyonga ya mwanamke huyo! Ai kudadadadadeki!
Pigo moja zito la rohoni likafanya nihisi kama vile mwili wangu wote unarusha damu huku na huko, kwa sababu niliingiwa na hisi kali sana ya hofu. Miryam alikuwa amesimama kwa kutulia, akiniangalia machoni kwa mkazo ulioonyesha hisia kubwa ya hofu iliyokuwa imemwingia, na huyo mwanaume akaweka kiganja chake kingine usawa wa shingo ya Miryam kwa njia ya kuikaba kiasi kutokea nyuma.
"Naona uko una-enjoy kidogo na watu wako... leo akaunti itakuwa imesoma fresh..."
Mwanaume huyo akasema hivyo. Alikuwa anaongea kwa njia fulani kama vile anataka sana nimwogope, besi nzito, akivuta maneno yake na kuniangalia kikatili eti, nami nikaonyesha kutaka kupiga hatua kumfata....
"Aisee! Tulia hapo hapo!" akaniambia hivyo kwa sauti ya chini.
Nikaganda na kuendelea kumwangalia kwa umakini.
"Kama umecheza na wengi, jua kwamba kwangu hautakuwa na hiyo nafasi. Jaribu kupiga hatua uone nitamfanya nini huyu mwanamke!" akaongea hivyo kwa sauti tulivu.
Aliposema hivyo, niliona akizidi kukikandamizia kisu kwenye nyonga ya Miryam huku akiikandamiza shingo yake kwa nguvu na mkono wake mwingine, naye Miryam akapandwa na woga zaidi na kuniangalia kwa hofu huku akipumua haraka-haraka kiasi.
"E e e e e... bro, tulia. Usifike huko," nikamwambia hivyo kwa sauti ya chini kwa njia ya kumtuliza.
Nilikuwa natamani atokee hata mtu mwingine hapo upesi ili nijaribu kufanya jambo fulani haraka, lakini hakuna nafsi yoyote iliyosogea upande huu. Huyu jamaa akawa ananiangalia kwa utulivu, lakini kikatili. Sijui hata alikuwa ametokea wapi ghafla namna hii!
Nikamuuliza, "We' ni nani? Unataka nini... pesa?"
Akachezesha midomo yake taratibu kama kuonyesha amekerwa, naye akasema, "Nataka tuongee."
Nikakunja uso kimaswali kiasi.
"Unaliona lile gari jeusi?" akaniuliza hivyo.
Nikatazama mpaka upande wa barabarani kule na kuona gari jeusi lenye kung'aa upya kwelikweli, aina ya Toyota Vanguard, nami nikamwangalia jamaa.
"Ndani ya dakika tano uwe umefika na kuingia humo..." akasema hivyo.
Nikawa nimeshagundua mwanaume huyu alikuwa ametumwa na nani, nami nikawa namwangalia kwa mkazo tu.
Akalisogelea shavu la Miryam karibu zaidi na kusema, "La sivyo... huyu mwanamke atakufa... na wote uliokuja nao. Usitake kujua ni jinsi gani... jua tu kwamba hilo ni uhakika."
Miryam alikuwa amefumba macho sasa, akijikaza kutokana na kuhisi maumivu sehemu fulani mwilini mwake.
Nikakaza meno yangu kwa nguvu nikihisi hasira sana, nami nikamwambia jamaa, "Sawa. Nakuja."
Mwanaume huyo akatulia kidogo akinitazama kwa utulivu makini, kisha akamwachia Miryam na kumsukuma kiasi mbele. Miryam akakaribia kuangukia upande niliokuwa nimesimama, nami nikamwahi na kuukumbatia mwili wake ili asidondoke, na nilijua huyo jamaa alikuwa ameshaanza kuondoka kuelekea huko ambako gari lile lilikuwa.
Miryam akawa anapumua kwa presha kiasi kifuani kwangu, nami nikamwachia taratibu ili nimtulize kwa maneno. Lakini nilipomwangalia usoni, nikakuta machozi yakimtoka kabisa huku akipumua haraka-haraka kwa hofu, nami nikaingiwa na simanzi na kumkumbatia tena; nikificha kichwa chake kifuani kwangu. Akawa amenikumbatia kwa nguvu pia huku akivuta nguo yangu mgongoni, nami kiukweli nilihangaishwa sana moyoni na hili tukio. Amani ikawa imevurugika tena!
Nikiwa nimeendelea kumshikilia, nikasema, "Samahani Miryam. Naomba nisamehe kwa... hhh... tafadhali naomba unisamehe..."
Nikashindwa hata kuelezea namna ambavyo nilijihisi vibaya sana, nami nikamwachia tena taratibu na kuanza kumfuta machozi.
"Amekuumiza? Umeumia hapa?" nikamuuliza hivyo huku nikimwangalia usawa wa ubavu wake.
Akatikisa kichwa kukanusha hilo huku akitazama chini.
Nikawa bado nimeishika shingo yake huku nikimwangalia kwa hisia sana, nami nikamwambia, "Nahitaji kwenda."
Akaniangalia usoni.
"Utawaambia wengine... nimepatwa na dharura, tutaonana baadaye... sawa?" nikamsemesha kwa sauti ya chini.
Sikujua angesema nini kwa wengine, ila hapa nilitakiwa kujali muda niliopewa, hivyo sikusubiri anijibu, badala yake nikamwachia taratibu shingoni ili niondoke. Lakini akaushika mkono wangu na kuukaza zaidi kama anaurejesha shingoni kwake, nami nikamtazama machoni kwa umakini.
Akaanza kusema, "Huyo mwanaume ni nani? Kwa nini uende hu... usi... usiende huko Jayden. Tuwapigie mapolisi kama hao ndiyo wale watu... mpigie Ramadh...."
Nikaishika tena shingo yake na kusema, "Hapana Miryam, acha niende... usijali, nitakuwa sawa. Najua jinsi ya kushughulika navyo hivi vitu, wala usiwaze. Ondokeni hapa upesi... kwa uangalifu. Nitahakikisha hamna mtu anawasumbua, sawa?"
"Lakini wakikuumiza je?" akauliza hivyo kwa sauti yake yenye kujali.
"Hawana hiyo jeuri. Nitarudi nikiwa sawa Miryam," nikamwambia hivyo.
Akaukaza mkono wangu na kuuliza, "Promise?"
Nikatulia kidogo nikiyaangalia macho yake mazuri kwa hisia sana, nami nikamwambia, "Promise."
Akabaki akinitazama kwa hisia za wasiwasi mwingi, nami nikamwachia na kutoa simu yangu mfukoni, kisha nikampatia kiganjani. Alinitazama kwa kutoelewa kwa nini nilimpa simu yangu, lakini sikubaki kuelezea maana yangu na kuanza tu kuelekea huko juu.
Sijui dakika tano zilikuwa zimeisha? Sikuona shida yoyote kwa sababu nilikuwa naenda, na nilikuwa nina hasira sana. Ile hasira yaani inayokufanya utamani kuuona utumbo wa mtu unatoka ndani ya mwili wake, ndiyo unaridhika sasa. Huyo bwege alitoa wapi jeuri ya kumshika Miryam namna ile? Kutishia maisha yake mbele yangu? Ah, aisee! Hakujua, yaani alikuwa amenichokonolea sehemu mbaya vibaya mno!
Nikaendelea kulifuata gari hilo mpaka nilipolifikia karibu, na usawa wa milango yake mlango wa nyuma ukawa umefunguliwa kutokea ndani. Nikageuka nyuma na kumtazama Miryam, kukuta mwanamke huyo akiwa amesimama pale nilipokuwa nimemwacha, nami nikampa ishara kwa kidole chinichini kuwa awahi kuwaondoa ndugu zake hapo, naye akatikisa kichwa kukubali kisha akarudi kule tulikowaacha wengine.
Nikaushika mlango huo wa gari na kuingia humo, na niliyekuta amekaa hakuwa mwingine ila mheshimiwa Sudi mwenyewe! Kama nilivyopigia picha, ni huyu pimbi ndiyo alikuwa amemwagiza mbwa wake anifatilie siku ile huko Kariakoo, na pia aje hapa na kutishia maisha ya Miryam ili kuipata "attention" yangu, na kweli akawa ameipata.
Nikatazama na mbele ya gari kumwangalia huyo jamaa aliyekuwa ameagizwa kunifata muda mfupi nyuma, akiwa ndiyo dereva wa gari hili pia, nami nikakaa sitini vizuri na kuufunga mlango kwa nguvu. Sudi akatabasamu kiasi na kuangalia mbele, na gari hilo likaondolewa hapo kuelekea safari ya kwenda nisikokujua.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments