MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Ni ukimya tu ndiyo uliofuata kwa muda wa dakika chache ambazo zilipita nikiwa ndani ya gari hili pamoja na Sudi. Sikumwangalia hata mara moja tokea tulipoondoka huko Viva, na hakusema lolote lile wala kutenda chochote kile mpaka tulipofikia maeneo ya Mkwajuni, na hapo gari likawa limesimama kwenye eneo la maegesho ya magari mbele ya jengo moja lenye maduka ya bidhaa.
Saa moja ilikuwa imekwishaingia, na kutokea upande tuliposimamia, jengo la hoteli ya Royal Village ambapo madam Bertha alikuwepo lilionekana vizuri, na jambo hili likavuta umakini wangu na kunifanya nimtazame Sudi. Alikuwa na maana fulani kunisogeza upande huu, huenda alikuwa akitaka nishuhudie jambo fulani ama aniagize kufanya jambo fulani.
Yule mwanaume aliyemtishia Miryam muda ule, akashuka kutoka siti ya dereva na kusimama nje pembeni ya gari. Nikabaki mimi na boss wake tu humu ndani, na alionekana kutulia sana huku akitazama huko nje kuelekea hoteli ya madam. Akiwa ndani ya suti nyeusi na miwani ya macho usoni, alionekana kuwa kama mtu aliyetoka kwenye mkutano fulani rasmi ama ndiyo alikuwa akielekea huko, na ndiyo akawa amenigeukia.
Akanitazama usoni kwa utulivu tu, naye akasema, "We' ni msumbufu sana."
"Me nimekufanyaje?" nikamuuliza hivyo.
"Hupokei simu. Haujibu text. Umenifanya nimekufata mpaka huku..."
"Ulilazimishwa?"
"Usinisemeshe hivyo!" akasema hivyo kiukali.
Nikatulia kidogo nikimtazama kwa hisia kali usoni, nami nikamuuliza, "Wewe unachotaka kutoka kwangu ni nini? Kwa nini umenileta hapa?"
"Nilikupa masaa machache ya kunipa jibu lakini ukakaa kimya..."
"Jibu gani? Kwamba nitajiunga na nyie? Itaweka utofauti upi ule nikikataa ama nikikubali kuwa-support na mipango yenu ya kumwondoa Bertha? Mm? Itawazuia kuifanya hiyo mipango yenu kama nikikataa? Si mtaniua tu?"
"Haujakosea. Ila kama nilivyokwambia... hakuna faida yoyote kukuua kwa sababu we' ni asset nzuri," akaniambia hivyo.
"Kwa hiyo umekosa fundi mwingine, ama hata kufanya utafiti wa jinsi ya kubusti ubora wa madawa yako mpaka unifate mimi na hii scheme... ah, aisee..."
"Nina njia zangu in place... kuhakikisha kwamba naendeleza kile ambacho kilikuwepo, na kukiondoa kilichokuwa juu yake ili mimi nikikalie ni njia ya kwanza kuhakikisha nakiendeleza hivyo..." akaniambia.
Nikamtazama kwa umakini sana, kisha nikasema, "Unataka kuchukua biashara zote za Bertha..."
"Kwa part..." akasema hivyo.
Nikiwa nimemwelewa, nikauliza, "Unataka kuwageuka wenzako wote?"
"Siyo wote. Ila wale ambao hawako na mimi," akaniambia hivyo.
"Ahah... Sudi umekula unga mwingi leo, eti? Yaani... unafikiria kumwangusha Bertha... na Festo? Utaweza?" nikamuuliza.
"Hilo... halikuhusu. Nimekufata mwenyewe kwa mara ya mwisho kukuuliza kama uko on board na mimi, ama... kama bado unataka kubaki kuwa malaya wa huyo mwanamke," akaongea kwa uzito.
"Bertha ningekuelewa, labda hata nafasi unaweza uka.... Festo?! Umechanganyikiwa?"
Sudi akatoa bastola kutoka kiunoni kwake na kuielekezea kwangu, akiikandamizia kwenye ubavu wangu wa kulia. Nikatazama pembeni nikiwa najikaza kihisia maana jamaa alionekana kuwa mbali na mchezo wa kitoto. Neno moja la kipuuzi tena lingenimaliza.
"Nipe jibu. Maneno mengi hayatakusaidia," akaniambia hivyo.
"Jibu kwa swali gani?" nikamuuliza bila kumtazama.
"Utakuwa upande wangu, au la?" akaniuliza hivyo.
Nikabaki kimya tu huku nikiangalia mbele.
Akacheka kidogo kwa pumzi, kisha akasema, "Unajua itakuwa raha sana kukuua we' kijana kwa sababu unajifanya una mdomo mrefu. Nakumbuka hata mara ya kwanza umekuja kule Room ulinitunishia kifua, lakini bado hauna kifua cha kukingia mtu kama mimi mdogo wangu. Ungekuwa umeliwa sana na upuuzi wa Bertha basi ungekuwa umeshamwambia kuhusu mipango yetu, lakini haujafanya hivyo... kumaanisha kwamba hata wewe haumwamini, ila uko pale tu kama njia ya kupata unachopata na unajiaminisha kinatosha... ila moyoni unajua kuwa ni bullshit..."
Nikaendelea kutulia tu huku nikiangalia mbele.
Akaitoa bastola ubavuni kwangu na kusema, "Achana na kiburi, handsome boy. Nakupa masaa 12 ya mwisho. Na nimeshakwambia, yale nayopanga kufanya kumwondoa huyo malaya hayakuhusu. Kinachokuhusu ni wewe kuwa upande wangu kwa ajili ya kazi. Yakipita masaa 12, na uhesabu... yakipita hujanipatia jibu... nitamuua na huyo mwanamke wako mwingine..."
Nikamtazama kwa mkazo sana machoni baada ya yeye kusema hivyo, nikijua alimaanisha Miryam.
"Yeah, umenisikia. Atakufa. Halafu na wewe utafata," akamalizia maneno yake.
Mapigo ya moyo yalikuwa yanakimbia kwa kasi sana, nikihisi hasira na hatia kwa wakati huo huo kujua kwamba nilikuwa nimemwekea Miryam shabaha mbaya kutoka kwa huyu mpuuzi aliyekuwa ananitaka nijiunge kwenye upuuzi wake.
Akauliza, "Simu yako iko wapi?"
Nikatazama pembeni tu na kusema, "Nimeisahau huko tulikotoka."
Akashtua cheko ya pumzi, naye akasema, "Okay. Haina shida. Naona una akili sana. Namba yangu unayo lakini. Nitafute kabla ya mimi kukutafuta JC... usijifanye loyal sana kwa huyo mwanamke, hakupi lolote la maana hata zaidi ya wanawake wengine wote unaoweza kuwa nao. Na ukinifanyia kazi mimi... utapata mengi mazuri zaidi ya uliyonayo sasa."
"Unamaanisha kazi nikiwa kama mfungwa wako..."
"Iite unavyotaka, lakini utapata faida kubwa. Trust me. Ni bora uwe kama mfungwa-rafiki wangu hata kama kwa kutopenda ili unufaike, kuliko nikuone kuwa adui kwa sababu unajifanya loyal kwa mahasimu wangu. Anachokutishia Bertha kwamba atakufanya mimi nimeshafanya mara mia zaidi yake, na ninajua jinsi ya kumwondoa. Kinachobaki ni wewe kuamua utasimama wapi, maana... himaya na upande utakaobaki kusimama utakuwa wangu tu... kwa hiyo kazi kwako," akaniambia hivyo.
Nikaendelea kutulia huku nikikunja ngumi kwa kuhisi hasira kali mno, yaani nilitamani kufanya jambo baya sana ndani ya hili gari! Basi tu.
Akaweka bastola yake pembeni na kuniambia, "Shuka. Nenda kwa mwanamke wako ukitaka, ama nenda nyumbani usipotaka. Niko macho na wewe JC. Lolote utakaloamua, jua tu kwamba litakuathiri aidha kwa ubaya, au uzuri... so, amua kwa busara mdogo wangu."
Sikutaka kabisa kuendelea kukaa humo tena, yaani hapo hapo nikaufungua mlango wa gari hilo na kushuka, kisha nikasogea pembeni na kusimama huku nikijitahidi kupumua kwa utaratibu. Hizi ishu walizofanya hawa watu zilikuwa drama za kijinga sana. Hasira ilikuwa imenikaba, nami nikaligeukia gari hilo na kumwona yule mwanaume aliyemshika Miryam muda ule akiingia humo tena, na alikuwa akinitazama usoni kwa umakini sana, vilevile na mimi nikimwangalia kwa hasira ya wazi.
Gari hilo likawaka na kuondoka eneo la hapo upesi, nikibaki nimesimama kulitazama tu jengo la hoteli ya Royal Village. Nilikuwa nimejiingiza kwenye mambo gani haya jamani, dah! Yaani sikujisikia vizuri kabisa hasa baada ya watu kuanza kutishia maisha ya watu wengine eti kisa tu wanataka niwafanyie kazi, wakati mpango wangu wa mwanzo ulikuwa mimi kutengeneza dawa chache kumzuzua Bertha, kujua njia zao, na kuwaporomosha, lakini ni kama sasa hivi mimi ndiyo nilikuwa naelekea kuporomoka. Na askari Ramadhan, kwa nini alikuwa kimya tu mpaka sasa?
Nilihitaji kujua la kufanya aisee. Mambo yangechacha vibaya kwa sababu mengi yalikuwa yananichanganya, sikujua nifanye kipi ambacho hakingekuja kukoroga kingine vibaya, na hivyo nijikute sehemu mbaya zaidi. Kutulia tu haingekuwa jambo sahihi hasa kutokana na kutojua maaskari wangechukua hatua lini kihususa, kwa hiyo sasa hivi ningedili na hii ishu ya Sudi mimi mwenyewe. Ningesimama pale nilipoona panafaa kusimama, hata kama na penyewe palikuwa pabaya.
Nikaamua kurudi nyuma, nikitembea taratibu tu kuelekea stendi ya Makumbusho ili nikachukue daladala za kunirudisha Mbagala, na nikafanikiwa kupata moja kabla hata ya kufika stendi, ndiyo tukageuka na safari kuanza.
★★
Kutoka huko mpaka Mbagala ilichukua muda usio mrefu sana, yaani saa tatu tu nikawa hayo maeneo, nami nikaamua kwenda pale Zakhem kwanza kwenye gym fulani kupasha viungo na nini ndiyo nielekee kwa Ankia. Kulikuwa tu na ile hisia ya hatia iliyoendelea kuzunguka ndani yangu kila mara nilipokumbukia namna ambavyo Miryam alihatarika leo kwa sababu ya mambo niliyokuwa nimejiingiza kufanya, yaani nilihisi kujichukia kabisa kila mara taswira ile iliponirudia kichwani.
Kwa hiyo nilipoingia kupasha mwili, ikawa zaidi ya mipasho, maana nilishusha na kupandisha chuma nzito haswa ili niutese mwili vilivyo. Sikupumzika hata mara moja kwa saa zima yaani, mpaka wananiambia saa nne ndiyo muda wa kufunga, tayari ilikuwa imeshaingia na kusogeza dakika. Kwa hiyo nikalipia, kisha nikatoka na kutafuta bafu zuri la umma kwa ajili ya kujimwagia kidogo, halafu nikaondoka maeneo hayo. Na bado nilijihisi mchafu mchafu tu hivyo ningeenda kurekebisha hilo zaidi nyumbani kwa Ankia.
Nimekuja kufika hapo kwenye nyumba ya likizo ikiwa inaelekea kuingia saa tano, nami nilipofikia hapo getini kwetu, upande wa pili wa ukuta nikawa nimemwona bibie Miryam akiwa amesimama pale kwenye uvaranda wao. Yaani wakati nimefika hakuwa ameniona, kwa sababu alikuwa kama anatembea kwa kuzunguka-zunguka, akionekana kuwa mbali kimawazo, ndiyo alipotazama huku akawa ameniona.
Niliingiwa na hisia za simanzi na furaha kwa wakati huo huo, nikifurahi moyoni kumwona, lakini nikihisi huzuni kutokana na yaliyotokea huko Sinza. Baada tu ya yeye kuniona, akatoka hapo varandani na kuvaa ndala zake, akisogea taratibu kuelekea gari lake kama kutaka kunifata huku ukutani, nami nikaingiwa na msisimko na kuamua kwenda getini kwao pale. Upesi yaani.
Nikalifungua na kukutana naye akiwa anakuja upande wangu taratibu pia, akivalia dera la kijani wakati huu na nywele zake zikibanwa juu ya kichwa chake, nasi tukasimama mbele ya mmoja na mwenzake huku tukiangaliana machoni kwa subira. Ilikuwa subira ya kutaka mmoja kati yetu aanze kuongea, na yeye Miryam aliniangalia hapa na pale utafikiri alikuwa akitafuta kuona kitu fulani mwilini mwangu, kisha akanitazama tena machoni.
"Jayde..."
"Mirya..."
Sote tukajikuta tunatamka majina kwa pamoja na kuishia njiani, kisha tukaendelea kutazamana machoni kwa utulivu.
Miryam akavunja ukimya tena kwa kuuliza, "Uko sawa Jayden?"
Nikatikisa kichwa kukubali na kusema, "Ndiyo niko sawa. Vipi wewe?"
"Niko poa," akajibu.
Nikaweka viganja vyangu mdomoni kwa pamoja, nikionyesha namna nilivyokuwa nahisi vibaya moyoni, kisha nikamwambia, "Miryam... nakuomba unisamehe sana. Sana yaani. Kwa kilichotokea, yaani... sijui hata niseme vipi..."
"Haina shida, Jayden. Usijali," akaniambia hivyo kwa sauti yake tamu sana.
"No, Miryam yaani... kilichotokea hakikuwa sahihi. Ninaomba sana unisamehe, na... nakuahidi haitatokea tena. Nime... nimefanya maisha yako yakawa kwenye hatari, yaani siwezi kujisamehe kwa kweli..."
"Usiseme hivyo bwana. Haina tatizo, niko sawa. Kilichotokea kimetokea, kwa upande wangu hakuna madhara yoyote yaliyonipata..."
"Wote mmerudi salama?"
"Ndiyo, wote tumerudi vizuri. Usihofu," akanituliza.
Nikaangalia chini kwa huzuni kiasi.
"Ilikuwaje? Uli-ulienda wapi muda ule..." akauliza hivyo kwa kujali.
"Haikuwa mbali sana... niliitwa tu kuongea na hao watu... ndiyo nimerudi," nikamwambia hivyo.
"Mbona nahisi kama vile mambo hayaendi vizuri kwa huo upande Jayden? Ulisema mnaelekea pazuri... wangekamatwa siku mbili tatu, si ndiyo? Mbona... bado wapo, halafu... wanakutishia kwa nini?" akauliza hivyo kwa hisia.
"Kuna vitu wanataka nifanye, wanafikiri niko upande wao. Bado naigiza yaani... mpaka mapolisi wakiwashika... ila ndo' bado hawajawashika. Wana... hawa jamaa wananilazimisha..."
"Wanakulazimisha ufanye kitu fulani kibaya, si ndiyo?" akanikatisha.
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Kwa nini sasa usimwambie Ramadhan... wawahishe kuwakamata?"
"Ndiyo kilichopo Miryam, najua. Ramadhan na wenzake kuna vitu wanaandaa, ndo' maana wanachelewa kwa sababu hawa watu ni wengi. Lakini usijali, watakamatwa tu. Muda si mrefu, najua," nikamwambia hivyo.
"Ah, aisee! Jayden unajiweka kwenye hatari jamani! Hivi hata hauogopi?"
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Siwaogopi wao, Miryam. Ila nisipochukua hizi hatua, naogopa tu yale watakayofanya kwa watu naowapenda."
Akabaki akinitazama usoni kwa utulivu baada ya mimi kumwambia hivyo.
"Mbona uko nje bado? Wengine wameshalala?" nikamuuliza.
"Bado, siyo wote, nilikuwa tu naku...."
Akaishia hapo baada ya kuonekana akitaka kusema kitu fulani kunihusu, nami nikatulia na kuendelea kumwangalia usoni kwa macho yenye subira.
Akaacha kuniangalia na kusema, "Nilikuwa nangoja urudi ili... nikupe simu yako. Kuna watu wamekutafuta."
Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.
"Lakini Jayden... uwe mwangalifu sana, sawa? Hayo mambo siyo mazuri kabisa," akaniambia hivyo.
"Najua. Nitajitahidi sana Miryam. Na inabidi nijitahidi kuwa mbali na nyie kwa muda mfupi mpaka haya yaishe..." nikamwambia hivyo.
"Kwa nini?" akauliza.
"Kama tu ilivyokuwa leo, Miryam. Sitaki... jambo kama hilo litokee tena. Nimejisikia vibaya mno. Siwezi kuelezea yaani," nikamwambia hivyo kwa hisia.
Akakishika kiganja changu kimoja kwa chini na kusema, "Usijali, ninaelewa. Lakini usijiweke mbali na sisi Jayden kwa sababu hiyo, hapa sisi sote ni familia. Na ni vizuri hawa wengine hawajui kuhusu haya, mimi ninaweza kuwa makini, la muhimu tu ni wewe kuwa mwangalifu zaidi maana upo huko muda mwingi. Na tena naona kama Ramadhan anakuhatarisha wewe zaidi Jayden, ni bora uongee naye akwambie wanachukua hatua lini ili yasije kuzuka mengine yasiyotakikana. Nimeshaona hao watu ni hatari kweli, na wewe haufai kabisa kuendelea kujiweka huko..."
Aliongea kwa busara na hisia za kujali waziwazi, na mimi nilikuwa nimetulia tu nikimtazama machoni kwa hisia sana.
"Umeelewa Jayden?" akaniuliza hivyo kwa upole.
Nikatikisa kichwa kukubali maneno yake.
"Fanya hivyo. Hapafai kabisa. Umeshaanza kunifanya niwaze kwamba unaweza... ukaondoka, halafu usirudi tena, jambo lolote baya kukupata inawezekana maana nimeshaona hiyo risk ipo, na kiukweli hiyo itanifanya ni...."
Akaishia hapo tena na kuendelea kunitazama machoni kwa utulivu, nami nikamwangalia usoni kwa matarajio mengi. Ah, alitaka kusema nini? Si angemalizia tu!
Akashusha pumzi na kusema, "Ukipatwa na jambo baya Jayden wote tutaumia sana. Kwa hiyo kuwa care. Ifike mahala uwaachie mapolisi ndiyo wadili na haya mambo, jiweke pembeni kabisa maana imeshakuwa hatari mno. Sawa?"
Miryam alikuwa ameanza kuonyesha kunijali sana, tena sana yaani, jinsi alivyoniangalia na kunisemesha ilionyesha hilo waziwazi.
Nikakikaza kiganja chake zaidi, nami nikamwambia, "Usijali. Nitafanya hivyo. Kila kitu kitakwenda poa, sema napenda kujiona kama Superman sometimes, ahah... kwa hiyo kuiishi hiyo ndoto ni muhimu kama hivi angalau najikuta na me Superman. Ila ndiyo najua sitakiwi kwenda mbali mno... bado kuna mambo mengi mazuri sitaki kuyaacha."
Akatabasamu kiasi kwa hisia, nami nikatabasamu pia. Wonyesho wa hisia za kujaliana ukionekana kwenye nyuso zetu, ikawa wazi kwamba sote tulipenda ukaribu huu uliokuwa ukizidi kuwa na nguvu baina yetu, yaani, kihalisi kwangu mimi zaidi, kwa kuwa sikujua ikiwa yeye alivutwa namna hiyo. Akaacha kuniangalia usoni na kutazama mikono yetu, ambayo haikuonekana kutaka kuachiana viganja, nami nikaitazama pia. Nilipenda sana hii hali mzee!
Nadhani aliona kwamba sikuwa na nia ya kutaka kukiachia kiganja chake kabisaaa, hivyo akakitoa chake kwangu taratibu na kusema, "Twende ndani basi, ukamsalimie mama mkubwa, bado yuko sebuleni..."
"Ah, hapana, ishakuwa usiku, na... nahitaji kuziondoa hizi nguo mwilini maana siko fresh sana... na nahitaji kupumzika pia. Na wewe... najua unahitaji kupumzika. Nitaonana na hao kesho," nikamwambia hivyo huku nikirudi nyuma kidogo.
"Sawa. Wacha nikuletee simu basi," akasema hivyo.
"Haya," nikakubaliana na hilo.
Bibie akaniacha hapo nje nikimtazama tu mpaka alipokwenda ndani na kurudi tena, na sifichi, nilipenda sana miondoko yake. Akiwa amevaa dera, huko nyuma palikuwa panatetemesha bonge la mziki bila spika za sabufa, ilikuwa rahisi kusahau matatizo kabisa! Nikajikuta napata tu amani kiasi baada ya pindi hiyo iliyoonyesha kwamba Miryam alinijali sana, na hata matumaini ya kupata matokeo chanya kwenye jaribio langu la kumwambia hisia zangu kwake baadaye yakawa mazuri.
Akaniletea simu na kunishikisha kiganjani, naye akasema, "Mama yako ndiyo amekupigia zaidi. Hakikisha unaongea naye upesi."
Nikamwangalia na kutabasamu kiasi, kisha nikamwambia, "Sawa. Asante."
"Haya. Usiku mwema. Kesho utakuwepo, au?"
"Nitatoka. Nitaenda kudili na hayo mambo kwanza, nitaongea na Ramadhan pia... halafu ndiyo baadaye nitarudi," nikamwambia.
"Sawa. Uwe makini jayden," akasisitiza.
"Usijali. Superman," nikamwambia hivyo na kukunja mkono kwa juu kumwonyesha nguvu.
Akatabasamu kiasi.
Nikamuuliza, "Na wewe? Kesho kazini eh?"
"Ndiyo, kama kawaida. Leo angalau kulikuwa na excitement na nini, ila kesho naelekea huko tena kudili na mambo mengi... yanaongezeka tu," akasema hivyo kwa njia fulani ya kukwazika.
Jambo hili likanifanya nikumbuke kile ambacho Bi Zawadi aliniambia ile asubuhi kuhusu maongezi ya kwenye simu ya bibie aliyohisi yalihusu tatizo fulani, nami nikamuuliza Miryam, "Kuna shida fulani kazini?"
"Shida? Hapana. Kila kitu kiko sawa," akasema hivyo.
"Mbona nahisi kama kuna tatizo, na hauniambii?"
"Oh... Jayden, usijali. Hakuna ishu yoyo...."
"Miryam, nakujua vizuri. Najua kuna ishu inakusumbua, lakini unataka kuibeba we' mwenyewe. Hakuna tatizo hata na hilo. Ila me si rafiki yako? Unaweza tu kuniambia," nikamshawishi namna hiyo.
Akaangalia pembeni kwa huzuni kiasi.
Nikamsogelea karibu zaidi na kusema, "Niko sahihi. Kuna ishu inakusumbua eti? Niambie tu, labda nikachangia mawazo na nini..."
Akashusha pumzi na kusema, "Well... uko sahihi ndiyo. Kuna... yaani, hata ingawa sasa hivi Joshua amewekwa jela lakini bado ananiumiza sana kichwa."
Nikakunja uso kiumakini zaidi na kuuliza, "Joshua? Amefanyaje?"
"Alikuwa ametoa pledge ya kuuza nyumba yake kulipia pesa za wale watu alizokula kwenye lile sakata la shamba la Mamu... wameiuza, lakini pesa haijatosha. Bado inatakiwa zaidi, na hawa watu wamefanya contact na mimi kuniambia kwamba aidha walichukue shamba la Mamu... ama waiuze na nyumba yangu," akasema hivyo.
Eh!
Alinifanya nishangae mno, nami nikamuuliza, "Nyumba... kwa nini? Yaani... Joshua alipokea kiasi gani kwani?"
"Milioni 23!" akaniambia.
"23?! Joshua alikula milion... alizipeleka wapi hela hizo zote?"
"Sijui kwa kweli," akasema hivyo.
"Ah... aisee! Ina maana, shamba la Mamu ni kubwa kiasi hicho?" nikamuuliza.
"Ni kubwa ndiyo. Joshua kumbe alikuwa amepewa pesa YOTE ya manunuzi, lakini sijui akaipeleka wapi, na inaonekana alikuwa amezipokea hizo pesa muda sana, sijui akaenda kuzitupa wapi na wajinga wenzake. Haya... wameuza nyumba yake, karibia kila kitu chake, bado inahitajika milioni 10. Wanataka kuiuza nyumba yangu, ama walibebe shamba la Mamu. Wana haki zote, na nimepewa masaa 48 tu! Yaani, kesho, kesho-kutwa niwe nimeshalipa. Pesa sasa hivi ilivyo ngumu hivyo, milioni 10... mimi tena ndiyo nilipie huo upuuzi wa Joshua, Jayden! Ah, yaani jamani..." akaongea kwa kutatizika sana.
Aisee! Mpaka nikamwonea huruma zaidi. Kumbe alkuwa na jambo zito namna hiyo la kushughulikia? Ni hapa kweli ndiyo nikawa nimekumbuka maneno ya mzee wangu siku ile nimekwenda kwenye kampuni yake, aliposema kwamba haingekuwa rahisi sana jambo hilo kufumbiwa macho kisa tu Joshua alikuwa amefungwa. Ni lazima kampuni kama kampuni ndiyo ingekuwa imetoa agizo la kurudisha pesa zake hata iweje, kwa hiyo jitihada ya mzee wangu kujaribu kuliondoa hilo suala inaonekana ilishindikana, ama labda alisahau kulishughulikia.
Bado kuna vitu vingi vilikuwa vinanichanganya, yaani haikueleweka vizuri hizo pesa zote zilienda wapi, kwa nini bado Miryam aliendelea kusumbuliwa kwa kuonwa kuwa mbabaishaji ingawa hayakuwa makosa yake, na haya yote yangeishia wapi. Ila najua hata iweje, Miryam asingekubali kuwaachia hao watu hilo shamba, yaani ni lazima angepambana tu hata kama wangekuwa wamempa masaa 10. Ilikuwa ni mtihani mgumu kwa upande wake kwa kweli, lakini nilitaka kuhakikisha anafanikiwa kuupita kwa matokeo mazuri.
Bibie akajipa utulivu na kusema, "Ila ngoja... nitashughulika nalo tu, mambo yatakuwa sawa."
"Una uhakika na hilo?" nikamuuliza hivyo kwa upole.
Akaniangalia usoni kwa umakini.
"Ikipita... tuseme hayo masaa yakipita haujaweza kuwalipa, wanafanyaje?" nikamuuliza hivyo.
Akaacha kuniangalia na kusema, "Nimekwambia nitadili nalo, usijali. Nenda tu kapumzike Jayden."
"Miryam..."
"Tafadhali," akanikatisha kwa kusema hivyo.
Nikaona kuwa bibie hakutaka kuendelea kulizungumzia suala hilo, na ilikuwa wazi kwangu kwamba uzito wa jambo hili ulimtatiza sana, kwa hiyo nikaamua kumwacha tu na kuelekea kwa Ankia.
Mambo yalikuwa yameanza kuwa mengi sana, na yalikuja kwa njia nyingi hasi tu. Maadui walikuwa wanaongezeka na kuongeza matatizo, sikujua hatma yangu na Miryam ingekuwa vipi baada ya leo, na baada ya kuona Kevin mume wa dada yangu akiwa amenitafuta usiku huu pia kwa simu kukanifanya nichoke zaidi. Furushi la kubeba lilikuwa kubwa yaani!
Lakini nikaamua tu kuweka mengine pembeni kwanza na kumpigia mama yangu simu. Nilimkuta Ankia akiwa ndani pamoja na mama Chande shosti yake na mwanaye, wakisimuliana yale ya visinia huko Sinza na Ankia kuuliza nilikimbilia wapi bila kuwaaga, lakini nikaishia kuwapa salamu tu na kuelekea chumbani kuzungumza na mzazi wangu; nikimwambia Ankia tutaongea vizuri baadaye.
Nikaingia chumbani na kuanza kubonga na mama. Alikuwa ananijulia hali, na aliuliza ningetoka huku lini kwenda kuwaona tena maana alinikumbuka sana, na kuna mambo tulipaswa kuzungumzia, nami nikamwahidi kuwa siku siyo nyingi ningekwenda kumsalimu, kwa hiyo aningoje tu. Nikataka kumuulizia na mzee, ila nikaahirisha tu, maana mambo yangekuwa mengi najua na wakati mzuri wa kuyaongelea ungefaa kuwa kesho.
Kwa hiyo nikamuaga mama baada ya maongezi mazuri baina yetu, kisha nikamtumia askari Ramadhan ujumbe mfupi. Najua tulipangana kwamba ningepaswa kusubiri tu, lakini mambo yalikuwa yanabadilika upesi wakati huu tofauti na ile mara ya mwisho nilipokutana naye. Nilihitaji anijibu haraka ili kumwandaa na haya mapya, lakini hakunijibu hata kwa namba ngeni.
Hivyo jambo hili lingekuwa la uhakika: kuanzia sasa ishu hiyo ya Bertha na Sudi ningeshughulika nayo kwa njia YANGU mpaka pale ambapo maaskari wangeacha urembo na kupiga hatua yao. Hali ingebadilika muda wowote ule, kwa hiyo ningefata kile ambacho moyo wangu ungeniambia ni sawa kufata na kufanya, kituo kikuu.
Sikuhisi njaa kabisa, yaani nikavua tu nguo na kwenda kujimwagia tena, viungo bado vikiwa vinauma kiasi, nami nikawaacha wakina Ankia sebuleni wakimalizia mapatano yao. Kesho ikiwa ni Jumatano najua nilitakiwa kuamka mapema kabisa na kwenda huko supermarket na kwake Bertha kama alivyokuwa amenielekeza, kwa hiyo nikajitahidi kuutafuta usingizi mapema ili mwili upumzike vya kutosha.
★★★
Asubuhi ya saa moja nikawa nimeshtuka, na ingawa usingizi bado ulikuwa ukinivuta, nikajitahidi kuamka ili nifanye maandalizi ya kuondoka huku upesi. Jana sikuwa nimehangaika sana kuwatafuta watu wengine walionitafuta kwenye simu isipokuwa mama tu, na hao walikuwa ni pamoja na huyo Kevin, Dina, Soraya, Adelina, Bobo, Tesha, marafiki zangu wengine, pamoja na madam Bertha pia, ingawa tulikuwa tumeshaongea jioni hiyo nilipowatoa wakina Miryam kwa ajili ya kisinia, ikionekana alinitafuta baadaye tena Sudi aliponiteka kidogo.
Kwa hiyo nikaamua kujiondoa kitandani ili niende kufanya usafi wa mwili kwanza, kisha ndiyo nikarudi na kujiandaa vizuri ili nitoke. Lakini, cha kwanza kabisa kufanya kwenye simu yangu ingekuwa ni kumtafuta mzee, yaani Mr. Frank Manyanza, ili niongee naye kuhusiana na ishu iliyokuwa ikimkabili bibie Miryam kwa wakati huu. Najua kwa njia fulani angeweza kusaidia kuitatua maana kutokana na kuwa na mambo mengi inawezekana aliacha kufuatilia hii ishu mpaka ikafika huku kote, kwa hiyo nilitaka kumkumbusha na kumshawishi afanye ipotee.
Nikampigia mara ya kwanza, hakupokea kabisa. Ya pili, kimya. Ya tatu, nikapigwa jembe na demu wa mtandao kuwa 'mtumiaji yuko bize kwa sasa.' Saa mbili tu yaani tayari jamaa alikuwa ameshaanza kazi zake huko zenye kubana kwa hiyo ndiyo, najua ubize ungekuwepo, lakini haikuwa na shida. Nilielewa wakati tu ambao angeona simu zangu basi angenitafuta, kwa hiyo nikaamua kumwacha. Ile tu nataka kuiweka simu mfukoni, ikaanza kuita hapo hapo; Bertha.
Najua tu kalikuwa kanataka kuniambia niwahishe, nami nikapokea huku nikitabasamu na kusema, "Unapenda sana kuwa kama alarm yangu kila siku ya kazi, eh?"
"Umeshaanza kwenda huko?" akauliza hivyo.
"Good morning kwako wewe pia," nikamwambia.
"Agh, acha hizo bwana. Niambie," akaongea kwa kuharakisha.
Nilihisi yuko makini, kwa hiyo nikasema, "Eeh, ndo' naenda. Vipi?"
"Fanya uje huku kwanza, sawa?" akaniambia.
"Sasa hivi? Nije hotelini?"
"A-ah... njoo huku NBC... Victoria ya zamani. Unapafahamu?"
"Ndiyo, napajua. jengo hilo lina polyclinic eh... la pharmacy ya Gina medics?" nikamuuliza.
"Eeeh. Uje hapo. Wahi," akasema hivyo.
"Kuna nini?"
"Kuna kikao kidogo."
"Mbona ghafla?"
"Me mwenyewe nashangaa, ila ndo' nimepewa mwaliko mapema naambiwa ni ya faida, so... uje. We' ndo' mkono wangu muhimu," akaniambia hivyo.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Festus wako anajua kuwapelekesha..."
"Hamna, ni Sudi. Ameona inafaa tukutane hapo, anasema ni muhimu sana," akaniambia hivyo.
Kauli yake ikanifanya niwe makini zaidi, nami nikauliza, "Nini?"
"Nini na wewe?" na yeye akauliza.
"Sudi ndiyo kaitisha hicho kikao?" nikamuuliza.
"Hajaitisha, ana maagizo tu na vitu vya kutupa, ndiyo maana unatakiwa uje mvibebe bwana," akasema hivyo.
"Uko na Dotto?" nikamuuliza hivyo kwa sauti ya chini.
"Eeh, ndo' nakaribia kufika hapo. Wahisha tako lako huku bwana, simu yangu inazima. Baadaye," akaniambia hivyo.
"Ona, ngoja Bertha, subiri kwa...."
Kabla sijamaliza kuzungumza, akawa amekata simu. Khh!
Nikajaribu kumpigia tena, lakni namba yake ikawa bize. Mh! Ilikuwa imeingia akilini kwa utambuzi wa hali ya juu kwamba madam Bertha alikuwa akipelekwa kwenye bonge moja la mtego, mtego ambao ungemwacha sehemu mbaya zaidi ya ile niliyokuwa nikipanga kumwacha abaki. Yaani yangu ingekuwa mbaya pia, sawa, lakini si kwa ubaya kama hawa watu wake waliokuwa wanataka kumwachia.
Bila shaka mpango wa Sudi na Chalii Gonga ulitaka kushika hatamu yake leo leo, na walikuwa na spidi! Najua walitaka kuhakikisha hakuna kitu chochote ambacho kingekwenda mrama mpaka wakamilishe waliyopanga kufanya, na labda ndiyo sababu walimfanya madam afikiri kuwa na mimi nahitajika huko, ili kwa njia fulani za mipango yao na mimi nihusike.
Kwa vyovyote vile, haikuwa nia yangu, ama hata kwa bahati mbaya tu nitake kuruhusu madam Bertha auliwe, sikutaka hilo litokee. Haijalishi alikuwa mbaya kadiri gani. Niliingiwa na hisi ya uharaka kutaka kumwondoa ndani ya mtego huo hao watu waliokuwa wakimwandalia bila kujali hali zetu kihalisi zilikuwaje, yaani hata kama bado nilimwona kuwa mbaya wangu pia, kifo siyo jambo nililohitaji limshukie. Nikajaribu kumpigia askari Ramadhan kabisa, lakini namba yake ikawa haipatikani. Aisee!
Sikuwa na muda wa kufikiri. Nikaifata bastola upesi na kuamua kuvaa viatu na soksi leo, nikizivuta mpaka juu, kisha nikaichomeka ndani ya soksi na kuisitiri kwa suruali niliyovaa. Sikuwa hata na muda wa kusimama kumuaga Ankia, yaani nikatoka hapo kwake kama vile simjui, bila salamu wala nini, nikaingia barabarani na kuanza kuwahisha kwenda kujaribu kumwokoa mtu ambaye mimi pia nilitaka kumwondoa; japo kwa njia tofauti.
Hivi JC nilikuwa nimepatwa na nini? Yaani hata mimi kwa kweli sikuelewa. Damu na joto vilikuwa juu, nikitembea haraka utafikiri nawahi kikombe cha babu wa Loliondo kuponywa UKIMWI, yote hiyo kwenda kumsaidia mtu ambaye ningekuja kumuumiza pia. Ila huu ndiyo uliokuwa uchaguzi wangu, moyo wangu ulitaka nifanye hivi, na niliridhia. Chochote ambacho kingetokea, kingetokea, lakini ningefanya yote niwezayo kuhakikisha damu ya mwanamke huyo haimwagwi.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments