MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Kwa sababu ya kutaka kufika huko upesi sana, nikaamua kuchukua bodaboda mpaka kufikia Rangi Tatu, kisha kutokea hapo nikapanda nyingine na kuomba nipelekwe moja kwa moja hadi Makumbusho huko kwa nauli aliyoona inatosha. Upesi boda ikaanza kupepea, nikiwa bado najaribu kumpigia Bertha na hata kumtumia ujumbe, lakini sikupata itikio lolote. Sijui nini kilikuwa kikiendelea!
Bodaboda ilitembea kwa kasi haswa, yaani maeneo mengi tuliyapita upesi sana. Tukiwa bado mwendoni kuelekea maeneo ya Keko, simu yangu ikaanza kuita, na mpigaji hakuwa mwingine ila mzee wangu, Mr. Frank Manyanza. Oh, inaonekana alikuwa amepata kuziona simu zangu na sasa ndiyo akawa ameweza kunitafuta, kwa hiyo nikaamua kupokea haraka ili tuongee japo kwa ufupi.
"Mzee, halloo..." nikasema hivyo simu ikiwa sikioni.
"Eeh, vipi? Za huko?" akasikika.
"Safi. Pole na kazi..."
"Asante. Hizo ni kelele za nini?"
"Aa... niko kwenye boda, kuna sehemu naelekea hapo mbele..."
"Ahaa... sawa. Niambie, nimepata window ndogo ya kuzungumza," akasema hivyo.
"Yeah. Ni kuhusu ile ishu niliyokuja kuzungumza nawe siku ile ofisini. Unaikumbuka?"
"Ee, nakumbuka... vipi?"
"Nasikia sasa hivi mko... mnataka kutaifisha mali za yule dada, ili mrudishe pesa zenu mzee. Ni kweli?" nikamuuliza.
"Kutaifisha? J unakosea ukisema hivyo. Na nilikwambia umlete huyo mwanamke huku ili nizungumze naye, lakini inaonekana haikuwezekana, na sasa kuna vitu vimetokea vikasababisha iamuliwe hizo pesa zirudi..."
"Lakini mwizi wa hizo hela yuko jela mzee, huyo dada hahusiki..."
"Ndiyo, tatizo ni kwamba jamaa alikuwa ametoa rehani ya nyumba yake na ya huyo mwanamke akisema kwa sababu ndiyo mwenye shamba basi inamhusu pia. Hatutachukua mali zingine na..."
"Mzee ngoja kwanza, nyumba ya huyo mwanamke inatunza familia, sawa? Mkiichukua na kuiuza wataenda wapi? Na siyo fair kwanza kuuza nyumba ile kwa milioni 10 tu, kwa nini wafanye hivyo wakati hana... siyo makosa ya...."
"Nisikilize JC, nisikilize. Hiyo ni mechanism ya kumshawishi atuuzie hilo shamba, kwa sababu sawa, tunaelewa imekwenda vibaya sijui kaka yake alifanya nini, lakini na sisi tumekula hasara nyingi, siyo pesa tu. Muda. Tulikuwa na option nyingi za kuchukua plot zingine lakini sasa hivi zimeshakuwa occupied maana muda umepita tukiamini hilo shamba lake ndiyo tutalichukua. Hakuna plot nzuri zilizo available kwa hilo eneo la mkoa wa Morogoro ambako ndiyo tunataka tujenge tawi ietu, na kama tukilikosa kabisa hilo shamba, basi pesa zinatakiwa ziwe zimerudi haraka ili tubebe kingine sehemu tofauti. Unanielewa?"
"Ndiyo nakuelewa, lakini...."
"Elewa kwamba siyo rahisi kwangu pia, JC. Imagine, kampuni imeshahalalisha haki zote za kuchukua hilo shamba ikiwa pesa haitarudi, sawa? Huyo mwanamke amepewa tu option; aidha akubali kutuachia shamba na tumlipe milioni 15 tena kutoka kwenye mauzo ya nyumba ya kaka yake, au atulipe milioni 10 na hiyo case iende mbali. Imeshasimama namna hiyo mwanangu..." akaniambia hivyo.
"Mliuza mali za Joshua kwa milioni 15?" nikamuuliza.
"Ndiyo. Huoni kwamba ni dili zuri tukimpatia huyo mwanamke hizo pesa akaliachia shamba, kuliko akitoa milioni 10 kwa upuuzi alioufanya ndugu yake?"
"Tatizo HAWEZI kukubali kuwaachia hilo shamba, mzee. Ipo... hhh... ipo tight sana yaani, sijui hata nikuelezeeje..."
Akasema, "JC ikiwa ni hivyo, hakutakuwa na jinsi. Mambo yameshapita hayo, akigoma na asiweze kulipa... tutamnyang'anya shamba kwa force... na hata hiyo nyumba yake pia. Hawa jamaa, wana hiyo nguvu na mahakama itakuwa upande wao, so...."
Nikahisi kuchoka kihisia kabisa.
"Kama huyo mwanamke ni rafiki yako, jaribu kumshawishi aliachie hilo shamba, apate milioni 15 ambazo zitamsaidia kwa mambo mengi. Mwambie asiendekeze kiburi," akasema hivyo.
"Hayuko hivyo mzee..." nikamwambia.
"Well, angalau huo ndiyo msaada naoweza kumpatia, maana nimejitahidi kufanya iwe rahisi hata kwa njia hiyo asije kupoteza kila kitu. Rafiki yako asipotaka kuliachia shamba na asipoweza kulipia hiyo milioni 10 kufikia kesho JC... mambo yatakuwa magumu sana kwake," mzee akasema hivyo.
Dah, aisee! Sijui ndiyo ingekuwaje maana najua kumshawishi Miryam aliachie shamba la Mariam ingekuwa ni utata. Na mzee alikuwa na pointi. Hapo pangekuwa pagumu sana kwa huyo mwanamke endapo kama angebebewa kila kitu chake. Familia yake ingeteseka kwa njia nyingine tena. Joshua alikuwa amemharibia sana huyo dada njia nzuri ya maisha, yaani basi tu. Ilikuwa kama amemwachia mzimu wake umsumbue ingawa hakuwa amekufa!
Baada ya maongezi hayo mafupi, mzee akaona aniage nilipomwonyesha kwamba nimeelewa, na kufikia muda huo tayari tulikuwa tumeingia maeneo ya Makumbusho. Nikamuaga pia na kuweka simu mfukoni, nami nikaanza kumwelekeza boda sehemu ya kupita ili tuelekee huko Victoria ya zamani ambapo hapakuwa mbali sana. Ishu ya Miryam na shamba la Mariam ningekuja kuiangalia tena baadaye, wakati huu nilitaka kwenda kumtoa kwanza Bertha ndani ya pango la nyoka waliotaka kummeza, ikiwa ningekuta bado hawajammeza, na kama mimi pia nisingemezwa.
★★
Bwana, bodaboda akawa amefanikiwa kunifikisha kwenye hilo jengo, eneo na pande moja maridadi zaidi jijini lenye majengo makubwa, barabara safi, harakati na watu walioenda shule yaani, nami nikashuka na kumlipa pesa yake. Akaosha. Nikavuka geti la uzio uliozunguka jengo hili mbele yangu lenye ghorofa ndefu kama nne au tano hivi, na kiuhakika zaidi nikawa nimeliona gari la madam Bertha hapo nje; ile Lexus yake mpya.
Hapa palikuwa kama hospitali, lakini zaidi kliniki kubwa ambayo ndiyo ilikuwa ikianza kukua zaidi. Kulikuwa na pande tatu zilizotengana ingawa kwa jengo moja; ya kwanza mkono wa kushoto ambako ndiyo palikuwa pameshakamilishiwa ujenzi wa kliniki za madaktari waliotoa huduma maalumu kwa wagonjwa binafsi sanasana, ya pili katikati ambayo ilikuwa pana sana ikijengewa zaidi vioo iliyobeba kama duka la madawa ya afya na vifaa maalumu vya hospitali kwa ajili ya wagonjwa, na ya tatu mkono wa kulia, ambako bado hapakuwa pametengenezwa kikamili kuanza kutoa huduma.
Ni upande huo wa tatu ndiyo ambao nilielewa kuwa bila shaka Bertha na wengine wangekuwepo, maana ulikuwa na vyumba vilivyo tupu, vikiwa bado tu havijaanza kutumiwa kwa ajili ya kazi. Yaani hakukuwa na watu. Jengo lote lingeungana baada ya kukamilika kama tu hospitali yoyote ile kubwa ya kibinafsi, na hapo nje kulikuwepo na nyumba ndogo ya wazi kwa ajili ya mlinzi, kukiwepo na mlinzi-askari mmoja ambaye aliniangalia kwa utulivu tu.
Kuona gari la madam Bertha likiwa hapo nje bila lingine kuwepo kukanifanya nitambue kwamba Sudi na ushirika wake haukuwa umefika bado, na sikujua huyo Dotto angekuwa amemweka madam katika hali gani kufikia sasa, kwa hiyo nikampungia tu mkono mlinzi kisalamu nikielewa angekuwa ameshalipwa huyo na kuelekea upande huo wa tatu bila presha, nami nikaanza kuangalia mazingira ya vyumba vya hiyo sehemu ya chini na kukosa nafsi hata moja, kisha nikaanza kupanda ngazi taratibu.
Nikafikia ghorofa ya kwanza, nami nikaingia kwenye vyumba vya huko na kupita kimoja baada ya kingine. Kulikuwa na hali ya ugiza, pakionekana kuwa patupu haswa na papana, milango ya vioo ikiwa imeshawekwa, nami nikamaliza vyumba vyote bila kukutana na nafsi nyingine tena. Kulikuwa na msisimko wa hali ya juu maana nilihisi kama vile naangaliwa yaani, ule utupu si unajua kwa sehemu kama hiyo huku ukielewa kuna baya linaweza kutokea, ulizipaisha kiasi hisia zangu. Nilikuwa jasiri sawa, lakini sikuwa John Wick!
Ngazi za kuelekea ghorofa ya pili zikanihusu, taratibu tu, na sikusikia sauti yoyote ile ya watu hadi nilipofikia ujumba wa huko juu na kuanza kupita chumba kimoja baada ya kingine. Ndiyo nikaanza kusikia sasa sauti kama ya kiatu cha kuchuchumia ikigonga sakafu la vigae kutokea chumba fulani cha mbele, na ilikuwa ngumu kujua kipi maana mwangwi ulisafiri haraka kwa njia iliyochanganya, kwa hiyo nikaitoa bastola yangu mguuni na kuanza kuelekea mbele kwa uangalifu zaidi.
"... ndiyo kama tu kwenye hiyo series, pazuri kweli kutoboa kama hivi... hapa, halafu unayapitisha kwa kutumia hiyo pipe, yenyewe si itakaa... itapita hivi? Eeh... yakiteleza mpaka chini wakati wenyewe wanakuja juu, hakuna nafasi wataweza...."
Nikaanza kuisikia sauti ya madam Bertha akisema maneno hayo, na ikitokea karibu zaidi na nilipokuwa nakaribia kufika, nikajibanza ukutani na kuusogelea muimo wa mlango ambao bado haukuwa umejengewa milango na kuchungulia, ndiyo nikaweza kumwona sasa madam. Alikuwa amesimama mbele zaidi kukaribia ukuta ndani ya chumba hiki kipana, akizungumzia jambo fulani pamoja na Dotto, ambaye alisimama kwa kunipa mgongo usawa huu wa mlangoni nilipokuwa.
Nikajitahidi kuingia taratibu kwa kunyata, na Bertha alipotazama huku na kuniona nikiingia huku bastola ikiwa mikononi, akakunja uso kimaswali, jambo ambalo likafanya Dotto anigeukie. Hapo hapo nikamnyooshea jamaa mguu wa kuku kuelekea kifua chake kwa uhakika wa hali ya juu, naye akashtuka na kurudi nyuma huku akinyanyua mikono yake hewani kiasi.
"HB!" Bertha akaniita hivyo kwa sauti ya chini.
Alikuwa amependeza mwenyewe kama kawaida yake; blauzi nyeupe iliyochanika kimtindo sehemu ya juu kifuani, suruali ngumu nyeusi ya leather iliyombana vyema, na mabuti yake ya kike ya kuchuchumia, nami nikaendelea kumwangalia Dotto kwa umakini bila kushusha mkono wangu wenye bastola kumwelekea.
"Hey... unafanya nini?" Bertha akauliza hivyo.
"Pita huku Dotto! Sogea," nikamwambia hivyo jamaa.
Alikuwa akinitazama kwa macho makini, naye akasogea pembeni huku nikianza kuzunguka kuelekea upande wa madam Bertha, na yeye akasimama usawa wa kona moja kutokea upande wa mlango.
"We' JC... nini hiki unafanya? Mabunduki ya nini asubuhi yote hii?" Bertha akauliza hivyo.
"Madam... najua siyo rahisi kuelewa, lakini naomba uniamini. Hapa umeletwa kwenye mtego. Wanapanga kukuua," nikamwambia hivyo bila kuacha kumtazama Dotto.
"Nini? Nani?" Bertha akauliza.
"Sudi, Dotto, Chalii... madam, unatakiwa kuondoka hapa," nikamwambia.
"We' J... hebu tulia. Nani amekwambia hayo yote? Eh? Are you high?" Bertha akaonekana kutoniamini.
"Sikutanii," nikamwambia hivyo.
"Inaonekana ameonja pafu kumi hii asubuhi..." Dotto akasema hivyo.
"Kaa kimya, mjinga wewe! Nitakupasua, usinichezee!" nikamtishia jamaa.
"Hee, wewe, hebu shusha hiyo! JC? Niangalie. Mbona sikuelewi?" Bertha akauliza hivyo.
Nikamwangalia kwa ufupi na kusema, "Ni mpango wao kukuangusha madam... wanataka kukuua. Hii yote, sijui mkutano... kikao... ni fake. Usipoondoka hapa watakuua. Tena mimi na wewe."
"Haya umeyajuaje?" akauliza.
"Nitakuelezea. Hupaswi kumwamini huyu tena madam, atakusababishia kifo... twende tuondoke," nikamsihi.
"Yaani Dotto... apange na Sudi kuniua mimi?" Bertha akauliza.
"Me mwenyewe namshangaa, huyu mtu wako amekuwaje?" Dotto akajitetea.
"Dotto nitakufumua risasi, hujui tu ni jinsi gani unanikera yaani!" nikamwambia hivyo.
"Nimefanya nini? We' una matatizo? Madam mbona simwelewi huyu..." Dotto akaendelea kunipa kero tu.
"JC, hebu nipe hiyo pistol..." Bertha akaniambia.
"Madam, niamini, naomba tuondoke haraka kabla Sudi hajaja, ni mpango wake na Chalii na Dotto waku...."
"Una ushahidi gani me nataka kumuua madam, eh?"
"Si mlijaribu kunishawishi nijiunge na nyie? Halafu now unajikuta mtakatifu sana?"
"Kama ni hivyo mbona ulikuwa hujamwambia madam..."
"Usinigeuzie tairi na kulizungushia kwangu ukifikiri itakupa...."
"Matairi yanatoka wapi tena? We' umeleweshwa na nani bro? Unakuja na pistol halafu unasema me ndo' nataka kumuua madam? Wakati ni wewe!"
"Dotto usinichefue, nitakuzingua kweli! Ni bora ukae kimya kabla...."
Bertha akayakatisha mabishano kwa kusema, "JC, hebu tulia, nimekwambia nipe hiyo pistol... inaweza ikafyatuka bahati mbaya. Ikitoa kelele hapa itakuwa shida... shusha bastola tuongee vizuri..."
Nikamwangalia madam na kusema, "Hatuna muda wa kuongea madam, ninakuomba... please... naomba tuondoke kabla hao watu hawajaja, nitakuambia, nitakuelezea kila...."
Tatizo moja tu kuendelea kumwangalia Bertha likampa mwanya Dotto kufanya kitu fulani ambacho sikutarajia kabisa baada ya yeye kupiga hatua ndefu kunielekea ghafla. Kabla sijaweza kuitikia vizuri, ile tu macho yangu yametua kwake tayari mwanaume akawa ameikwapua bastola kutoka mkononi mwangu na kurudi nyuma tena huku akiielekeza upande wetu! Aaah... makosa!
Nikawa nimebanwa ukutani na madam Bertha sasa. Aloo! Chuma kikiwa kimetazama upande wetu namna hiyo nilihisi damu ikianza kurukaruka zaidi ya ilivyokuwa inafanya shauri ya ule wasiwasi wa kushika tu bastola, sasa ukawa ni wasiwasi wa kushikiwa bastola. Dotto alikuwa mzoefu inaonekana, maana aliweka uso mtulivu tu na kuikoki bastola vizuri, huku mimi na madam Bertha tukimwangalia kwa umakini sana.
"Dotto... shusha hiyo gun. Kwa nini unaielekeza kwangu? Umekuwaje?" Bertha akamuuliza hivyo.
Dotto akaendelea kutuangalia tu kwa utulivu.
"Nimekwambia madam... hayuko upande wako tena," nikasema hivyo.
"Kumbe ni kweli? Unapanga kuniua... na wakina Sudi?" Bertha akamuuliza jamaa.
Kimya.
"Kwa nini? Nimekufanya nini we' na Sudi? Kwa kipi kilichofanya mpaka uamue kunigeuka?" madam akauliza tena.
Dotto akashika sikio lake kwa kiganja kimoja huku akitunyooshea bastola kwa kingine bado, naye akasema, "Niko nao. Ghorofa ya pili. Njooni."
Inaonekana kulikuwa na kifaa kidogo cha mawasiliano ndani ya sikio lake, na hapo ndiyo alikuwa akiwatumia mawimbi wenzake ili waje huku. Kumbe tayari walikuwepo, ni mimi tu ndiyo nilikuwa nasubiriwa!
"Ndiyo unamwita Sudi? Au Charles?" Bertha akamuuliza.
Dotto akaendelea kubunda tu.
"Ahah... D, hebu acha masihara yako. Shusha hiyo chuma u...."
Bertha akajaribu kupiga hatua huku akisema hivyo, lakini Dotto akaielekeza bastola kwake madam moja kwa moja kwa uhakika na kwa nia isiyo ya utani kuonyesha kwamba angefyatua rusasi. Bertha akarudi nyuma kidogo, na mimi kiukweli nilikuwa nahisi kama vile miguu inataka kumwagika, siyo siri.
Nikamwambia, "Dotto... nisikie. Usifanye hivi... haina maana yoyote kumuua... haitakupa furaha kwa lolote..."
"Mbona yeye imempa furaha sana kuwaua wengine? Kwa nini mimi nisifurahie kumuua yeye?" Dotto akasema hivyo.
"Ahah... kwa hiyo kumbe kweli unataka kuniua? Kwa sababu gani? Niliowaua na we' si nilikuhusisha kuwaua? Sudi amekupa shi'ngapi, eh? Sema! Nitai-double," Bertha akamwambia.
"Hii haihusu pesa mama..." Dotto akasema.
"Ila?" Bertha akauliza.
"Utagundua baada ya sekunde..." Dotto akasema.
"Dotto..."
"Kaa kimya, mbuzi nini! Unajiona mjanja hata pistol huwezi kushika, utakufa tu bwege wewe. Ila nikushukuru kwa kuniletea na hiki chuma, umenirahisishia kazi," akaniambia hivyo.
"Sija... Dotto nakuomba, usifanye hivi... Chalii anakufanyia manipulation tu..." nikamwambia hivyo kwa hisia.
"Agh, na maviingereza yako unanikera!" jamaa akasema hivyo.
"Kwa hiyo ndiyo nini, unamlipizia kisasi ndugu yako? Amekaa huko akakudanganya-danganya kwamba mtaweza kuniua mimi, eh?" Bertha akauliza hivyo kwa kujiamini.
Tukaanza kusikia hatua zikikaribia kufikia chumba hiki, na sauti ya Sudi ikasikika ikiuliza, "Kwa nini tushindwe?"
Mimi na Bertha tukaangalia upande wa mlango, lakini Dotto hakuondoa macho yake kutuelekea, na ndiyo hapo mlangoni jamaa akawa ametokea. Sudi ndani ya suti. Jamaa aliingia kama kibosile yaani, taratibu kwa njia ya kuridhika kabisa, na nyuma yake alifuatwa na wanaume wawili; mmoja ikiwa ni Chalii Gonga mwenyewe, pamoja na yule jamaa mzito ambaye alimshika Miryam ile jana na kutishia kumuua.
Chalii na huyo jamaa walivalia masweta meusi yenye vikofia ambavyo havikufunika vichwa vyao, na Sudi pamoja na Chalii ndiyo waliosogea mbele zaidi kumpita Dotto, na yule jamaa akasimama pembeni mkono wangu wa kushoto huku akishikilia bastola mkononi iliyowekewa kifinya sauti (silencer). Ikawa ni 'four against two,' watu wanne dhidi yetu wawili, na Bertha alionekana kuwaangalia kwa njia isiyo na hofu bali hasira, huku mimi hapa nikihofia usalama wetu kwa pamoja.
"Msengemmoja wewe!" Bertha akamwambia hivyo Sudi kwa sauti ya chini.
Sudi akatabasamu kidogo kwa kiburi, naye akasema, "In the flesh. Happy to see me?"
"Fuck you!" Bertha akamwambia hivyo kwa sauti tulivu.
"Mke wako ameamkia upande wa chaga iliyovunjika leo," Sudi akamwambia Chalii Gonga hivyo.
Chalii akatabasamu kiasi kwa kiburi, naye Dotto akafanya kuiachanisha bastola yangu aliyoshika na kitunzio chake cha risasi, kisha akavitupa pembeni, halafu akavuta bastola nyingine nyeusi kutoka nyuma ya kiuno chake na kuanza kuifungia silencer taratibu, tayari kwa ajili ya mauaji. Aisee! Nilihisi kufa!
Bertha akamtazama mume wake na kusema, "Kwa hiyo ridhaa ya kufanya haya ni ya moyo wako wote kabisa Charles?"
"Kwa asilimia mia. Ulitegemea nini? Kwamba uendelee kunitendea kama mbwa wako kwa maisha yangu yote halafu nitulie tu?" Chalii akamsemesha hivyo.
"Kama mbwa? Ulistahili zaidi ya yale niliyokutendea mshenzi wewe! Wewe ndiyo sababu mwanangu aliuawa!" Bertha akasema hivyo.
"Oh, unaekti kama vile haungeweza kuzaa tena, hujui kifo kipo tu mama? Unashikilia jambo moja tu kunifanya mdoli wa ku-torture utafikiri kuzaa ni mara moja? Ungesema tu kama hukuwa na uwezo wa kuzaa tena, ingeeleweka," Chalii akamwambia hivyo.
"Ulinipima ukaona huo uwezo sina?" Bertha akamuuliza hivyo.
Nikamtazama Chalii kwa mkazo na kumuuliza, "Kwa hiyo kumbe ulikuwa unanidanganya uliponiambia kuhusu jinsi mtoto wenu alivyokufa?"
"Wewe kama nani unaniuliza mimi hivyo?" Chalii akaniuliza.
Bertha akaniangalia na kuuliza, "Unamaanisha nini?"
Nikamtazama na kusema, "Chalii aliniambia wewe ndo' ulisababisha mtoto wenu akafa... ulimpa sumu Giselle... yaani ukiwa unataka kumuua mwanamke wake Chalii."
Bertha akamwangalia Chalii na kusema, "We' ni Shetani Chaz!"
"Ahah, zaidi yako? Hiyo ilikuwa business mpenzi. Tulikuwa tunajaribu kumleta jamaa upande wetu, lakini ni wazi ameona hawezi kutoka kwako maana una k(...) tamu mno eti... najua, inapumbaza mno wapumbavu kama yeye... siyo mimi," Chalii akaongea kwa dharau.
Wenzake wakacheka kidogo, naye Bertha akasema, "Hujisikii vibaya hata kidogo kwamba mwanao alikufa kwa sababu ya upuuzi wako... upuuzi ambao mimi ndiyo nikalipia? Halafu tena unanisingizia?"
"Ooh acha kujifanya victim sana mama G, si ulipata faida lakini? Kunitesa huko kote, kunilisha nyama mbichi, kuniwekea watu wa kunichunga kama ng'ombe... tena hukuchoka, yaani ulitaka tu niendelee kuwa kama mdoli wako...."
"Basi, inatosha," Sudi akamkatisha jamaa.
Mimi na Bertha tukamwangalia Sudi usoni, huku Chalii Gonga akipumua kwa hasira kiasi.
Sudi, akiwa ameweka mikono yake mfukoni, akasema, "Mambo ya familia hayajalishi tena. Tumetoka mbali Bertha, najua... lakini sometimes mwisho wa safari huwa ni lazima ufike, you know that..."
"Safari gani? Me nimeshawahi kufanya venture yoyote na wewe hata mara moja? Kwa nini unaniogopa sana?" Bertha akamuuliza hivyo kwa ujasiri.
"Mimi nikuogope wewe?"
"Kinachofanya utake kuniua ni nini kama siyo woga? Kwamba... unitolee mfano, ili na wakina Farao, Tito, wote wakuogope eh? Umesahau kuhusu Festus? Hujui atakufanya nini akigundua kuhusu...."
"Atagunduaje?" Sudi akamkatisha.
Tukabaki kumwangalia kwa umakini.
"Hawezi kujua, na yeye ana lake linalokuja muda si mrefu..." Sudi akasema.
"Mmm?" Bertha akafanya hivyo kikejeli.
"Eeeh. Kwa hiyo... sitaki tupotezeane muda Bertha. Unajua kinachoenda kutokea now, kinachotakiwa ni uwe tayari kukubaliana nacho. Basi," Sudi akasema hivyo.
"Na baada ya hapo?" Bertha akamuuliza.
"Oh well, yatakayofata hayana faida kwako maana tayari utakuwa six feet underground. Hata kama ukiweza kuyaona wakati upo kuzimu, basi haitakuwa mbaya pia. Lakini hapa sijisumbui kukupa hadithi utamu kolea," Sudi akasema hivyo.
Chalii Gonga akacheka kidogo.
"Unachezea moto Sudi. Wewe na hawa malaya zako," Bertha akasema hivyo.
Yule jamaa mwingine wa Sudi akainyoosha bastola yake kumwelekea madam, nami nikamkinga Bertha kwa mbele.
"Bro... tafadhali, weka chuma pembeni, taf... Sudi... hii siyo fresh aisee, haipasw...." nikajaribu kutuliza hali.
Sudi akacheka na kusema, "Yaani unawaita wanaume wangu wa kazi malaya, wakati malaya wako namba moja huyu hapa! Wewe JC... nilikupa masaa 12 ya kutumia vizuri kabisa lakini ukaamua kuchagua..."
"Sudi tafadhali..."
"... kusimama mbele ya huyu mwanamke, sawa. Nimeelewa. Utakipata kinachokuja kwake pia maana ndiyo umekiomba..." Sudi akamalizia maneno yake.
"Basi sawa, Sudi... nita... nitakufanyia kazi, sawa? Nitakutengenezea madawa... coke nzuri zaidi hata ya nayompa madam, alright? Just please... usimuue... nitakuja upande wako, mwache tu, haina...."
Bertha akaja usawa wangu zaidi na kusema, "Acha kuwa kama pussy, JC! Unaogopa nini?"
Nikamwangalia na kusema, "Sitaki uumie Bertha! Ya nini? Eh? Mwachieni aende... nitawafanyia kazi.... nawaomba..." nikaelekeza maneno hayo kwa maadui.
"Aww... mpaka inagusa sana!" Chalii akaongea kwa dharau.
"Sana! Anampigania mke wako mpaka mwisho, yale ya Kantala na Odemba eh?" Sudi akasema hivyo.
"Odama," yule jambazi wake akamsahihisha.
"Eeeh, Odama. Hahah... lakini huyu mwanamke Shetani hafanani hata kidogo na Odama. Odama alikuwa malaika, yeye Bertha ni roho mchafu sana... pepo yaani... na ni lazima kuwaondoa roho na mapepo wachafu kwa kumwaga damu zao ikiwa maombi yatashindikana," Sudi akasema hivyo.
Chalii akacheka kwa sifa, naye Sudi akatoa ishara kwa upande wa Dotto, na jamaa akawa amenyanyua bastola yake kutuelekea sisi. Niliingiwa na hofu! Yaani kifo hiki hapa nilikuwa nakitazama, bastola mbili zikielekea vichwa vyetu na sijui, yaani sijui ningetokaje!
"Pole JC... umechelewa sana. Masaa 12 yameenda, muda umekwisha," Sudi akaniambia hivyo.
Akarudi nyuma kidogo, nami nikaingiwa na wasiwasi hata zaidi kwa kuwa bastola ndiyo zilikuwa zikielekezwa kwetu zaidi, ikibaki tu amri kwa wanaume waliozishika wavipasue vichwa vyetu, na Bertha alikuwa akiwatazama kwa umakini sana. Kisha, ghafla tu mwanamke huyu akaanza kucheka. Sana. Alicheka kicheko cha kutoka moyoni yaani, kama mtu aliyekuwa amefurahishwa na utani wa hali ya juu, mpaka mimi nikamwangalia kwa mshangao kiasi.
"Aaaa... classic madam Bertha," Sudi akasema hivyo kikejeli.
Bertha akaendelea kucheka zaidi, ikiwa wazi wakati huu kwa sifa.
"Unacheka nini?" Chalii akamuuliza hivyo.
"Oh, mwache. Ni defense mechanism. Kicheko chake cha mwisho lazima kiwe kizuri," Sudi akasema hivyo.
Bertha akamalizia kucheka na kusema, "Haaahh... what drama! Hii imenifurahisha kwa kweli."
"Sehemu ipi zaidi? Kwamba unakufa, ama haufanani na Odama?" Sudi akamuuliza hivyo.
Bertha akasema, "Hivi kwa nini huwa mnajivuta hivyo? Kama kuniua si mgekuwa mmeniua tu tayari? Mnaongeea, mwishowe msababishe mmoja wenu adondoke tu ghafla out of nowhere..."
Ile kamaliza kusema hivyo, damu zikaruka ghafla kutokea upande wangu wa kushoto, nami nikashtuka kiasi na kutazama hapo baada ya mguno usio mzito sana kumponyoka yule jamaa mwingine aliyekuwa ametuelekezea bastola. Kumwangalia, alikuwa amepigiza mwili wake kwa kishindo kikubwa ukutani kisha ukadondoka chini kwa nguvu, na hapo ndiyo nikaona tundu moja la risasi likiwa limetoboa upande mmoja wa kichwa chake, na damu nyingi zikivuja!
Sudi, Chalii, mimi, tulishangazwa sana na hilo, isieleweke imekuwaje, na ile nimeangalia pembeni, nikakuta Dotto akiwa ameelekeza bastola yake yenye kizuio cha sauti kuwaelekea Sudi na Chalii Gonga, moja kwa moja ikionyesha kwamba ni yeye ndiyo alikuwa amemtungua yule jamaa mwingine!
Nini? Nilishindwa kuelewa, kuamini, na kutathmini kilichokuwa kimetokea. Sudi na Chalii Gonga wakamwangalia Dotto kwa taharuki, huku mwili wa jamaa pale chini ukitulia tuli na damu kutokea kwenye tobo la risasi zikiruka kwa kushtua-shtua. Nilichoka!
Uzito wa namna ambavyo hali hiyo ilichanganya ulizidi kupanda tu, nami nikamwangalia madam Bertha pembeni kukuta anaangalia vidole vyake vya mkononi kwa kugeuza-geuza kiganja kama vile hajaona na hajali kilichokuwa kimetokea yaani.
"Madam Bertha will kill you, hiyaa hiyaa oooh..."
Bertha akaimba hivyo kwa sauti ya chini, kisha akaniangalia machoni na kutabasamu. Nikarudi nyuma kidogo huku nikimtazama kwa kutoelewa kabisa kilichokuwa kinaendelea, naye akawaangalia wahasimu wake.
Sudi na Chalii, bado wakiwa wametikiswa pia na jambo alilofanya Dotto, walionekana kuchanganyiwa haswa, naye Chalii akataka kupiga hatua kuelekea mlangoni lakini Dotto akafyatua risasi sakafuni iliyofanya patoboke na kigae kupasuka-pasuka. Jamaa akarudi nyuma kwa hofu.
"Dotto! Unafanya utumbo gani huu?" Sudi akamuuliza hivyo.
Dotto akaendelea kumnyooshea bastola kwa utulivu tu.
"Labda umuulize mmiliki, siyo mmilikiwa," Bertha akasema hivyo.
Sudi na Chalii Gonga wakamwangalia, hata mimi pia nikamtazama huyu mwanamke.
Bertha akasema, "Oooh, the twissst! Imewabamba eh?"
Sote tukabaki kumwangalia kwa umakini.
"Sudi kama uliiangalia hiyo filamu vizuri, utakumbuka kwamba Odama na Kantala waliibuka washindi mwishoni kwa sababu hawakuchoka kupambana. Tena, ni Kantala ndiyo alimpigania Odama na kuwashinda maadui, kama tu JC wangu hapa. Right? Kwa nini tusiibuke washindi?" Bertha akamwambia hivyo.
Nikiwa bado sijaelewa mambo vizuri, nikamuuliza,"Madam, nini kinaendelea?"
Akanishika usoni na kusema, "Usijali, HB wangu. Nilikuwa najua kila kitu. Hii ndiyo intermission."
Nikamwangalia Dotto kwa umakini. Kumbe huu muda wote alikuwa akiigiza? Ai, kubaabake!
Chalii Gonga akamwambia Dotto, "We' mjinga kumbe ulikuwa unatuchezea huu muda wote? Yaani... uko tayari kuendelea kuwa mbwa wa huyu mwanamke badala ya kusimama na mimi kaka yako?"
"Charles, nimeshakwambia tokea muda mrefu sana, huniwezi mimi. Yaani elewa kwamba sikuzote ukifikiri unaijua kesho, Bertha tayari ameiona kama jana. Ulifikiri kweli kabisa mimi... mimi madam Bertha ungeweza kunipangia kifo? Tena yaani unilete tu hapa na kuniua yaani... kihivyo tu? Chaz umesoma kweli wewe?" Bertha akamuuliza hivyo.
Chalii Gonga akaendelea tu kumwangalia usoni.
Bertha akamtazama Sudi na kusema, "Na wewe. Usifikiri nilikuwa sijakuona ukija. Nimekuangalia kwa muda mrefu sana. Una... unatamani kuwa kama mimi, lakini umeshindwa, na unalazimisha kunizidi lakini umeshindwa pia, ndiyo maana ego yako ikakudanganya kufikiri ungeweza kuniondoa kirahisi tu..."
Sudi akawa akimtazama kwa njia ya hasira.
"Ahah... hata katika nyakati hizi unapaswa ujue kuna vitu vikubwa zaidi ya ego, rafiki yangu. Kimoja? Loyalty. Mtu akijitoa kwako kwa moyo mkunjufu Sudi, haijalishi atapewa nini, yaani hawezi kuacha kuendelea kushikamana nawe mpaka mwisho. Move mbaya kwako zaidi kufanya ilikuwa kum-enlist Dotto. Ulifikiri ingekuwa rahisi kumnunua kwa sababu una kaka yake upande wako, lakini huyo hapo. Amekuonyesha nini maana ya loyalty. Loyalty siyo damu tu. Ni RESPECT. Ungekuwa loyal kwa muungano wetu hata kama hunipendi, usingefanya huu upuuzi Sudi. Hata mimi sikupendi, lakini sikukaa kufikiria kukufanyia kitu cha namna hii. Umeharibu palipokuwa pametulia mdogo wangu, na hakuna namna nyingine iliyobaki ila wewe kupatengeneza tena," Bertha akamwambia hivyo kwa sauti tulivu.
"Nani unamwita mdogo wako, malaya wewe?" Sudi akamsemesha hivyo.
Bertha akatabasamu kiasi huku akimtazama kwa hisia kali. Kisha, akarudisha mkono wake mmoja nyuma ya kiuno chake na kuchomoa bastola nyeusi pia, ikiwa ndefu shauri ya kuwekewa silencer, naye akaishikilia kiganjani kwake huku akimtazama Sudi kwa njia ya kawaida. Aisee, huyu mwanamke! Alikuwa anajua kuigiza! Yaani kumbe huu muda wote mchezo ulikuwa ni wake kabisa!
Sudi akatusogelea kidogo bila woga na kusema, "Kwa hiyo unajiona umeshinda? Kwamba una akili sana, unajua yote? Hata kama umeweza haka kamchezo sasa hivi, kumbuka zamu yako itakuja tu..."
"Zamu yangu ya nini? Kufanya upuuzi wa kisenge kama wako ni kitu ambacho siwezi... never, kukifanya. We' ndiyo malaya kwangu kutotambua kwamba me mwanaume wako nilikuwa hatua mbili mbele zaidi yako, na sasa hivi nitahakikisha nayapanua zaidi matundu yote saba ya mwili wako ukiwa kama malaya aliye wewe!" Bertha akamwambia hivyo kwa mkazo.
Dah! Tusi moja baya kinoma lililosemwa kwa ufasaha wa hali ya juu! Unaachaje kumpenda Bertha? Sudi akabaki kimya tu na kuendelea kumwangalia usoni kwa hasira.
Chalii akasema, "Kwa hiyo utatuua? Dotto? Utaniua mimi? Kweli mimi kaka yako? Hm?"
Dotto akamtazama madam.
Bertha akasema, "Unaogopa sana kufa Chaz, eh? Umekuja hapa unajiamiiini, eti 'k(...) yako inapumbaza wapumbavu kama yeye, siyo mimi,' kumbe we' ndo' umejaza mak(...)-uoga tu mishipani mwako. Ilihitajika kibao kukugeukia ili ujionyeshe jinsi ulivyokuwa pussy... na yeah, Dotto atakuua mpumbavu wewe!"
Nikamwambia Bertha, "Madam... haina haja ya kufika huko. Tunaweza tu ku...."
"Nini? Oooh... naelewa JC. Unataka wewe ndo' uvute chuma?" Bertha akaniuliza hivyo.
Nikaweka uso makini na kusema, "Hapana, sijamaanisha..."
"Ahahah... chukua JC. Nataka uutungue ubongo wa huyu mpumbavu hapa hapa," Bertha akaniambia hivyo.
Loh!
Nikaitazama bastola yake, ambayo aliinyanyua kunielekezea ili niichukue, lakini nikashindwa kuipokea. Nikabaki nikimtazama machoni tu kama vile sijaelewa somo, na katika hali hiyo ya kusubiriwa, Chalii Gonga akaona kwamba amepata nafasi ya kujaribu kufanya kitendo fulani cha kibishi kwa kuanza kukimbilia mlangoni, lakini hapo hapo Bertha akaielekeza bastola yake huko na kufyatua risasi mbili zilizomtoboa jamaa mgongoni vibaya mno!
Nilishtuka. Chalii Gonga akaanguka pale pale kwa kishindo kikubwa na kuanza kutoa sauti ya kilio cha chini cha maumivu, nami nilipomwangalia Bertha, nikaona akimtazama Dotto na kutikisa kichwa mara moja kwa uharaka, na ndiyo Dotto akaielekeza bastola yake hapo Chalii alipolala na kufyatua risasi moja kichwani kwa jamaa iliyomfanya akate uhai!
Ilikuwa kama nimeshindwa kuamini jambo hilo kabisa, yaani sikuwa yule mtu wa kuonyesha mshangao sana, lakini nilishangaa yaani. Nilimwangalia Chalii Gonga pale chini kwa njia ambayo mtu angefikiri nilikuwa nimetulia tu, lakini moyo ulikuwa ukifanya riadha ya ajabu ndani yangu. Sikuwahi kufikiri ningeshuhudia kihalisi jambo kama hilo kwa ukaribu tofauti na kuona tu lilivyokuwa likiigizwa kwenye filamu nilizowahi kuona, na kiukweli nilikosa amani sana. Ikiwa mambo yangekuwa yameenda vise versa, mimi ndiyo ningekuwa kwenye hiyo sakafu hapo chini.
Akawa amebaki Sudi na suti yake, tukiwa tumemweka kati, na hakuonekana kama mtu anayeogopa sana ingawa ilikuwa wazi kwamba alishtushwa na kilichompata mwenzake wa pili. Akatuangalia mimi na madam Bertha kwa umakini sana, na mimi pia nikamtazama madam kukuta akitabasamu kwa kiburi huku macho yake yakielekea kwa jamaa. Ilikuwa ile kwamba 'umebaki wewe,' Sudi alilijua hilo, na naelewa alikuwa akijihukumu sana kutengeneza mtego namna hii halafu ukamnasa yeye mwenyewe.
Lakini akajikaza kiume na kumwambia Bertha, "Unasubiri nini? Go ahead."
"Ooh, haraka ya nini Sudi? Hauna maneno ya mwisho unataka tumtumie baby mama wako huko aliko? Na watoto?" Bertha akamuuliza hivyo.
Sudi akaweka uso ulioonyesha wasiwasi.
Bertha akacheka na kusema, "Niambie. Nitawafikishia, personally."
"Mimi ndiyo mbaya wako Bertha, kama kuniua niue, nimeshakubaliana na hilo. Ila familia yangu usiiguse. Hawajui lolote kuhusu haya," Sudi akasema hivyo.
Eti sasa hivi alikuwa anaongea kwa njia fulani kama vile kuonyesha yeye ndiyo mwathirika yaani, kama vile anaonewa hivi, na sijui kwa nini ila nikajikuta nashindwa kujizuia kumwonea huruma kiasi. Bertha asingemwachia, najua, ila kama angeenda kuiharibu na familia ya jamaa, hiyo ingekuwa imekwenda mbali mno. Lakini yalikuwa makosa ya nani?
Mwanamke huyu akiwa anamcheka Sudi kwa furaha baada ya jamaa kuonyesha hofu juu ya familia yake, tukaanza kusikia hatua zikikaribia kufikia chumba hiki kwa mara nyingine tena, naye Dotto akasogea usawa wa mlangoni na kuangalia huko nje. Kisha, akaonekana kutulia tu na kurudi ndani tena, akimtikisia madam Bertha kichwa kama kumpa ishara.
"Finally," Bertha akasema hivyo.
Ikaeleweka kwamba kuna mtu wa upande wake aliyekuwa akija, nami nikaangalia hapo mlangoni mpaka mtu huyo alipofika na kusimama kwanza, akiangalia mazingira ya hapo ndani.
"The fuck?"
Ilikuwa ni Festo. Mwamba akawa ameuliza hivyo baada tu ya kufika na kukuta miili miwili ikiwa imelala chini, damu ikitapakaa hapo mithili ya rangi iliyomwagika, naye akatutazama sisi wote kwa umakini. Alikuwa amevalia kwa njia ya kawaida tu; T-shirt la mikono mifupi lenye rangi mbalimbali alilochomekea kwenye suruali ya kardet pamoja na kiatu rasmi cheusi, huku akishikilia kalamu nzuri kiganjani na funguo nyingi zikiwa zinaning'inia kutokea kwenye mkanda wa suruali yake.
"Festus. Pole nimeanzisha party kabla hujafika, ila bado haijaisha," Bertha akamwambia hivyo huku akitabasamu.
Festo akamwangalia Sudi na kusema, "Kinachofanyika hapa ni nini?"
Sudi akabaki kimya tu huku akiangalia pembeni kwa njia fulani ya jeuri.
Bertha akamwambia Festo, "Njoo nikupe ubuyu."
Festo akaupita mwili wa Chalii Gonga hapo chini na kuja mpaka nilipokuwa nimesimama na madam, naye Bertha akaanza kumwelezea. Akasema namna ambavyo alijua toka mwanzo kuhusu mipango ya wakina Sudi kutaka kunigeuza dhidi yake na kumuua, na aliona aendelee kuigiza kwamba hajui ili aone kama ningemsaliti pia mpaka siku ambayo wote tungejikoroga ili atuondoe.
Lakini alifurahia jinsi nilivyothibitisha kuwa upande wake leo, kwamba upendo wangu kwake ulikuwa halisi, na hapo sasa kilichokuwa kimebaki ni hukumu ya msaliti Sudi, na ndiyo maana alikuwa amemwita Festo mapema ili aje kuhalalisha hukumu hiyo kwa kitendo cha jamaa ambacho kilionyesha hakuwa mmoja wao kwa ajili ya faida yao wote, bali alitaka tu faida za kibinafsi zaidi.
Festo akamwangalia Sudi na kusema, "Sudi haya yote ni kweli? Yaani... ulikuwa unataka kumuua madam kwa sababu tu amekuzidi kimapato? Hujui sokoni ni competition? Kwa nini usingetafuta na wewe mtu mwingine wa kukufanya uwe competitive badala ya kujaribu kufanya cut ya kishenzi namna hii kwa mwenzako? Umechanganyikiwa wewe..."
"Ndiyo nimechanganyikiwa!" Sudi akamwambia hivyo Festo kwa ujasiri.
Festo akamkazia macho kwa umakini.
"Unafikiri sisi wote hatuoni jinsi unavyompendelea huyu? Umempa territory kubwa zaidi yetu sisi wote, hata tukijaribu kuomba utuongezee unatupiga chini tu, eti kuna risk. Mbona kwa Bertha hauoni risk? Kwa sababu yeye ni mwanamke?" Sudi akamuuliza hivyo.
"Ikiwa hauridhishwi na jinsi mtandao unavyofanya kazi, ungejitoa. Suala la territory siyo sababu tosha ya wewe kuchukua maamuzi ya kutaka kumuua mwenzio, nina sababu zangu kugawa nachogawa ninavyokigawa, ukiwa na tatizo na hilo, ondoka," Festo akamwambia.
"Katika maana gani? Mniue? Ahah... me siyo mjinga Festus. Hakuna mtu anaweza akatoka tu mkamwachia hivi hivi, mnaogopa kusnichiwa, kwa hiyo kuondoka unamaanisha nife. Nisingefanya hilo, hakuna choice. Biashara zetu zinaporomoka kwa sababu ya huyu mwanamke, na wewe...."
Bertha akamkatisha jamaa na kusema, "Kwani nimekufunga mikono? Unashindwa kutafuta njia ya kuinua biashara kwa upande wako unakaa kuendekeza upumbavu, eti 'nimuue Bertha, nichukue biashara zake?' Tena hadi alikuwa na mpango wa kukumaliza na wewe Festus, si ndiyo Dotto?"
Dotto akatikisa kichwa kukubali.
"Umeona alivyo mshenzi? Kaja hapa anatamba nakwambia, mpaka movie ya Odama kanisomeshea! Hizo swaga zooote, kiko wapi Sudi? Yaani unapata kingi vizuri tu, lakini ukiona mwanamke karefusha ngazi zake kupanda juu zaidi, hutaki. Eti nakuporomoshea, nimekuporomoshea nini mimi?" Bertha akamuuliza hivyo kwa hasira.
"Unaiba mpaka wateja walio kwenye territory yangu Bertha, usifikiri mimi ni mpumbavu, sioni..."
"Sijakuibia lolote mimi! Una wazimu? Me nikuibie nini, una nini kwanza cha kuibiwa wewe? Hao unaowasema wanakuja kwangu wao wenyewe, sijafunga mtu yeyote kamba shingoni kumburu...."
"Jitetee utakavyo we' mwanamke, lakini nakujua vizu...."
"Ulikuwa unataka kuniua na mimi?" Festo akakatisha hizo kelele kwa kumuuliza Sudi hivyo.
Sudi akatulia na kumwangalia, vilevile na mimi pia, ambaye nilikuwepo hapo kama vile sikuwepo yaani.
"Mwambie. Jitetee," Bertha akamwambia hivyo Sudi.
Kwa ujasiri, Sudi akasema, "Ndiyo. Na wewe ningekuondoa."
Bertha akacheka na kunishika begani, huku mimi na Festo tukimwangalia Sudi kwa umakini. Jamaa alikuwa anajua ameisha, ila alitaka kuonyesha kwamba anaisha kibabe.
Bertha akamwambia Sudi, "Yaani mateso nayotaka upitie wewe kinyang'anyiro wewe! Utajitafuna mwenyewe mpaka ufe!"
"Unaelewa unachokisema, Sudi?" Festo akamuuliza hivyo kwa sauti yake kuu.
Akamwambia Festo, "Vizuri sana. Nyie wote hamna utofauti. Mnajifanya mko upande mmoja sasa hivi, lakini haitachukua muda mrefu kwenu nyote kugeukana. Na unajua sababu itakuwa ni nini? Huyu. Mwanamke. Sisi wote hapa wanaume tunajua vizuri jinsi wanawake wanavyoweza kuvuruga mambo mengi mazuri ndani ya kipindi kifupi, na Festo nakwambia, sasa hivi si una kifua kipana sana na nguvu ulizonazo? Chote kitamomonyoka kwa sababu tu ya mwanamke..."
"Huwa una shida gani na wanawake? Hm? Mama yako hakukupenda sana wakati wa utoto, au... au ndo' na we' walikukuta kwenye shimo la choo? Alikutupa?" Bertha akamuuliza hivyo kwa dharau.
Sudi akaendelea kumtazama Festo na kusema, "Huo ugumu ulionao wote moyoni mwako Festus, uliofanya sisi sote tukuogope, hautaendelea kuwepo tena kwa sababu unajiruhusu kufanya mwanamke awe udhaifu wako. Ahah... tena unajua nini, yaani... sasa hivi hata sikuogopi. Kiukweli mwanangu, yaani nakuona mdogo sana kwa sababu umeshamalizwa na upuuzi wa kufatilia wanawake tu ambao hawakupi faida yoyote, mambo kwenye mtandao yanaharibika, mpaka kufikia hivi... huna habari, wakati mwanzo ulikuwa unajua kila kitu... ni shauri tu ya huyo mwanamke..."
Aliposema hivyo, hakuonekana kama alikuwa akimwongelea Bertha, naye Festo akavuta pumzi ya juu kuonyesha hasira imempanda na kuishusha taratibu huku akimtazama kwa mkazo. Nilielewa kwamba alikuwa akimzungumzia Miryam, na kiukweli sikujua alilitambua jinsi gani suala hilo la Festo kumtaka Miryam. Ila hapo akawa amegusa pabaya.
Sudi akaendelea kusema, "Kuniua mtaniua tu, najua. Lakini hata na nyie mtakufa. Unajitahidi sana kuishi kama... spy mwenye maisha included mno, unafikiri hauna vulnerability kwa sababu hutaki tuzione, lakini najua unazo, na tena kwa huyo mwanamke ndiyo umemalizwa kabisa Festus. Hata sisi usiotaka tujue, tunajua, baba... umekwisha. Hauna lolote tena zaidi ya jina, siyo mimi, wala Farao, wala Tito, na hata huyu Bertha... hakuna yeyote kati yetu atakayeendelea kuogopa pimbi kama wewe kwa sababu tumeshaona madhaifu yako kwa wanawake... na I swear, huyo mwanamke cheupe cheupe huyo unayemfatilia saaana, huyo huyo ndiyo atakuja...."
Kabla Sudi hajamaliza kuongea, Festo akaikwapua bastola ya Bertha na kufyatua risasi tatu moja kwa moja juu ya paji la uso wake Sudi!Ilikuwa ghafla sana, na hapo hapo jamaa akadondoka chini na kupoteza maisha yake!
Nilifumba macho, nikikaza meno, na kuinamisha uso wangu, nikijihisi vibaya sana moyoni. Kifo cha tatu ndani ya chumba kimoja, na kiukweli, najua Sudi alikuwa amefanya maku-Sudi kuongea maneno hayo kumwelekea Festo kwa kujua angekasirika sana, kwa hiyo alionyesha kutaka auliwe upesi badala ya mateso ambayo hawa watu wangempa kwa sababu ya matendo yake. Akawa amekipata.
Nilianza kuhisi tumbo likinivuruga ghafla yaani, siyo labda kinyaa sijui, hapana, maana mimi kama ni damu, nyama, viungo vya mwili vikiwa vimeachanishwa, na mengine ni mambo niliyokuwa nimeshazoea kuyaona mara nyingi mno na ilikuwa kawaida, lakini kuwa hapa kama mhusika wa haya mauaji ilikuwa ishu nyingine kabisa. Sikujiona kuwahi kuja kufika huku, lakini ndiyo nikawa nimefika sasa.
Bertha akasema, "Aww, Festus! Umemuua haraka mno, tulipaswa tumpe vyake vya taratibu kwanza aelewe maumivu ni nini!"
Festo akamrudishia mwanamke huyu bastola yake na kusema, "He wasn't worth it."
Kwamba Sudi hakuwa na umuhimu wowote wa kuanza sijui kumteeesa, yaani hawa watu!
Bertha akamuuliza, "Alikuwa anaongea kuhusu cheupe gani huyu mjinga?"
Festo akamwangalia Dotto na kusema, "Hey, harakisha. Fanya mpango hii sehemu isafishwe."
Dotto akatikisa kichwa kukubali, naye akachomoa simu kutoka mfukoni na kumpigia mtu fulani. Najua Festo aliliepuka swali la Bertha kwa makusudi, na kwa sababu nzuri pia.
Bertha akasema, "This was so fun! Imeuma tu HB wangu hujapata nafasi ya kutia tobo mtu, nilikuwa nina hamu ya kuona unapiga action leo."
Nikamwangalia usoni tu nikiwa nimeishiwa raha.
Akanishika shingoni na kusema, "Aww, mpenzi, mbona hivyo? Haujafurahi maadui zetu wameenda?"
Nikaacha tu kumwangalia na kutazama pembeni.
"Ahahah... najua bado hujawahi. Usijali. Utapata nafasi nyingine real soon," Bertha akaniambia.
Yaani walikuwa wanaona kuua ni jambo la kawaida sana, aisee!
Festo akasema, "Kutakuwa na mabadiliko ya management baada ya huu upumbavu. Jioni tukutane Red Room. Spread the word."
"Sawa. Nitafurahi ukinipa na territory ya huyu mjinga, nguvu yetu itakua," Bertha akamwambia hivyo.
"Yako unamaanisha," Festo akamwambia hivyo.
"Yetu... Festus. Come on, unanijua," Bertha akamsemesha kwa njia fulani ya kumbembeleza.
Nikamwangalia na kukuta amemshika Festo shingoni, na jamaa akaniangalia pia.
Bertha akanigeukia na kusema, "Twende JC. Nasikia njaa."
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Ulikuwa umetokea mbali?" Bertha akamuuliza hivyo Festo.
"Nilikuwa hapo Goba. Nyie nendeni, tutaonana baadaye," Festo akasema hivyo.
Jamaa alionekana kuudhika sana, na alijua naelewa kwa nini aliudhika mno mpaka akamuua Sudi mbele ya macho yangu. Hata jinsi tu alivyokuwa akinitazama ilionyesha wazi namna ambavyo alielewa najua uzito wa maneno ya Sudi ulielekea kwenye suala la Miryam, kitu ambacho kilimtia hasira kugundua kuwa baadhi ya watu wake wengine walitambua hatua zake za kumfatilia yule mwanamke, na walimwona kuwa mdhaifu kwa sababu hiyo. Kwa hiyo alikuwa amekasirika haswa.
Inaonekana Dotto alikuwa amewaita watu fulani waje kusaidiana naye kusafisha hii sehemu kabla haijazua gumzo, watu walio makini, naye akamwambia Festo kwamba wangefika hapo na vifaa baada ya dakika chache. Bertha akanishika mkono na kumwambia Dotto aibebe bastola yangu aliyokuwa ameitupa pembeni muda ule kisha angeileta baadaye huko hotelini, halafu akaanza kunivuta kuelekea mlangoni ili tuondoke.
Ile tumefikia mlangoni hapo, Festo akaniita, nami nikasimama na kumgeukia, huku Bertha akiningoja pia. Jamaa akiwa ananitazama kwa umakini machoni, akaniambia, "Be careful."
Mh!
Sikuelewa maana halisi ya maneno hayo na kuchukulia kwamba alikuwa akinitahadharisha kuhusiana na ishu yake na Miryam. Alikuwa akinitaka niendelee kuwa kimya, nisiseme lolote lile juu ya huyo mwanamke hata kwa Bertha, na jinsi alivyoyawasilisha hayo maneno kwangu yaani hadi ilitisha mzee. Alitoka kunionyesha roho yake ya kikatili inavyokuwa akikasirishwa sana, na kuniangalia kwake kuliionyesha hiyo roho pro max.
Aisee, hii siku ilikuwa imegeuka kuwa mbaya mno zaidi ya siku zingine zilizokuwa mbaya sana maishani mwangu. Nilipata somo kubwa zaidi juu ya Festo wakati huu. Huyu mwamba alikuwa ni hatari sana, sikupaswa kuwa mzembe hata kidogo. Inawezekana labda hata alichukulia suala la Sudi kujua kuhusu nyendo zake kwa Miryam lilisababishwa na mimi, kwa hiyo kweli, nilihitaji kuwa "careful," maana asingechelewa kuniharibu. Alikuwa amekwishaniambia hivyo, kwa hiyo mimi ndiyo ningetakiwa kufanikiwa kumharibu yeye kwanza.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments