Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA TATU

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Baada ya Festo kuniambia niwe makini, Bertha akaonyesha kukerwa naye kiasi na kumwonyesha kidole chake cha kati kwa njia ya utani, kisha akanivuta zaidi ili tuondoke. Hata Dotto, ingawa hakusema lolote, akawa amenionyeshea dole gumba kirafiki, ili kutuliza hali baina yetu, lakini nilikuwa nimeishiwa raha na amani kabisa yaani, siyo siri. Tena sifichi, yaani bado nilihisi adrenaline mwilini ikiwa juu kiasi kwamba miguu ilikuwa ikitetema kiasi, lakini baada ya sekunde chache ikatulia.

Tukashuka ngazi na madam mpaka huko nje kichwa kikiwa na mawazo tu, naye Bertha akaona anipe ruhusa ya kuwa dereva wa gari wakati huu ili nimwendeshe mpaka alipotaka twende akapate kiamsha kinywa, kisha hotelini kwake. Nikawasha tu ndinga, nisiwe na jambo lingine lolote akilini lililopita kuziba taswira ya jinsi wale watu walivyouawa mbele yangu, nami nikaliondoa gari kutoka kwenye jengo hilo upesi.

"Haaahh... what an epic start of a day!" Bertha akasema hivyo kwa furaha tukiwa mwendoni bado.

Nikaendelea tu kuwa makini na uendeshaji.

"JC yaani najihisi kama vile nimetoka kwenye set ya movie, sikutanii! Ile ya Captain America Civil War ile, sema tu hii ikiwa bloody zaidi hahahah..." 

Alionekana kuwa mawinguni yaani, lakini sikujali kabisa maneno yake na kuendelea kuendesha kama vile nimegandishwa.

"Vipi JC? Bado tu una-sulk?" akaniuliza hivyo.

Nikabaki kimya.

"Hey, si naongea na wewe?"

Nikavuta pumzi na kusema, "Niko makini tu na uendeshaji. Kichwa hakipo sawa."

"Kwa nini kisiwe sawa?"

"Mambo mengi tu..."

"Kama?"

"Ah, Bertha..."

"Nini? Ongea. Unataka kusema hao washenzi kufa ndo' imekuuma saaana?"

"Siyo hivyo, sikuwa tu tayari..."

"Tayari na nini? Kwa hiyo haujafurahi kwamba maadui zetu wamekufa?"

"Bertha, sijawahi kufanya kitu kama hicho, sawa? Kuangalia mtu akiuawa mbe...."

"Ulitaka wenyewe ndiyo watuue kwa hiyo?"

"Labda kunge-kungekuwa na njia nyingine ya...."

"Njia gani? Hii ni conscience yako tu inakusuta, si ndiyo? Ulikuwa unataka kujiunga nao at one point kwa kuamini maneno ambayo Chaz alikwambia. Nadanganya?" 

Nikahisi hasira na kuliegesha gari pembeni ya barabara kwa kasi sana, naye Bertha akashtuka na kuniangalia kwa mshangao makini.

Nikamwambia, "I wasn't ready! Bertha... can you imagine, nini kingetokea kama ningefika tu hapo na kum-shoot Dotto nikifikiri kweli alikuwa anataka kukuua? Nini kingefuata baada ya hapo?"

"Well, lucky for us... hiyo haikutokea. Don't be tripping JC. Hiyo imeshaisha, sijui ambacho kinakusumbua ni nini," akaniambia hivyo.

Nikafumba macho huku nikishusha pumzi kutuliza hisia, nami nikamwangalia na kusema, "Sikuwa tayari, Bertha. Leo... ni kitu ambacho sikuwahi kufikiria kingekuja kuwa sehemu ya maisha yangu... lakini sasa hivi nitapaswa kuishi nikijua na mimi nilikuwa na mchango kwa yaliyotokea leo. Naomba uelewe. Bado siko kama wewe."

Akafumba macho pia na kushusha pumzi, huku akitikisa kichwa kwa kukereka kiasi, naye akaniangalia na kusema, "Nataka uiondoe hiyo 'bado' kutoka kinywani mwako, JC. Sitaki kusikia unaitapika tena. Ni part ipi ya hili game iliyokufanya ufikiri hatutakuja kufanya vitu kama hivi? Eh? Na tena hata haujaua mtu leo! Mbona una-trip kihivyo mtu wangu?"

"Inaweza ikawa rahisi kwako, lakini sijawahi kuua mtu, na sidhani... kama nitaweza kuja...."

"Kuua? Kwa nini? Kwa kuwa we' ni daktari?" akaniuliza hivyo.

Nikamtazama kwa umakini sana.

"Hujawahi kuniambia moja kwa moja, lakini najua wewe ni daktari. Hukuniambia pia, ila najua ulienda kwa Festo kutafuta bastola ili ujilinde..." akaniambia hivyo.

Nikatazama pembeni.

"Unaweza usiniambie lolote kukuhusu JC, lakini nakuelewa. Umeacha maisha ya udaktari kwa sababu umeona yanakuboa, si ndiyo? Ukanipata mimi, ukaona hii ndiyo sehemu unayofaa kuwa. Kwa nini unaanza kuogopa tena sasa? Ukiwa ndani ya hili game unapaswa uelewe kuwa kuna kufa ama kupona, and you gotta do everything necessary to survive. Usije kukonyeza hata siku moja mbele ya kifo JC, nakufundisha, nisikilize..."

Nikamwangalia usoni kwa macho makini. 

"Usifikirie mara mbili kabisa. Mtu akikutishia kukuua, unapaswa uwe tayari umeshamuua kwenye akili yako kabla yeye hajaifikia hiyo hatua. Sudi alipokunyooshea bastola siku ile tupo Red Room, kuanzia hapo tayari nilijua angekuja kujaribu kukumaliza, na mimi pia. Sikufumba macho, maana ikiwa ningeyafumba, leo ni mimi na wewe ndiyo tungekuwa tunalamba mchanga. Huu umekuwa kama mfano, ipo siku haya yanaweza yakajirudia maana watu... watu wanapenda rebellion. Wanapenda kutaka kufanya mapinduzi. Sikuzote kuwa mindful, uwe tayari kuchukua hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili ubaki kuwa hai, and on top. Ukiona black mamba anakukaribia utamwangalia tu eti kisa hujawahi kuua?"

Nikatikisa kichwa kukanusha.

"Sasa! Kwa nini mtu atishie kuyaondoa maisha yako halafu umwangalie tu ayaondoe? Huo utakuwa ni ujinga kwako. Narudia tena JC. Umechagua kuwa na mimi ili uje kuwa on top, na kwa sababu unanipenda. Si ndiyo? Basi ukiwa na mimi... uwe tayari kufanya kitu chochote kile kwa ajili yangu. I mean it. Uwe tayari kuua, JC. Hakuna mtu wa kufanya killing test dummy, kwa hiyo ikitokea retaliation, live... uwe tayari kuua. Sijui umenipata?"

Aliongea kwa njia yenye kusihi sana, nami nikaangalia mbele na kutikisa kichwa kukubali kwa shingo upande.

Akanishika shingoni na kusema, "Hey, niangalie."

Nikamtazama.

"Hautakiwi kufanya nini ukiwa mbele ya kifo, JC?" akaniuliza.

"Sitakiwi kukonyeza," nikamjibu.

"Good. So, kione kikiwa kinakuja kwako kutokea mbali, ili kikikufikia uwe tayari kukigeuza kirudi kilipotoka. That's how we survive in this game. Ukiwa mzembe, ukiendelea kuwa soft... utakufa haraka sana, na itakuwa kuchelewa kujutia kuingia kwenye hili game kwa sababu tayari litakuwa limeshakumeza. Sijui unanielewa?" akaniambia hivyo.

Mh! 

Mwana nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa kweli, naye akaiachia shingo yangu na kutazama mbele huku akiegamiza mwili wake vizuri kwenye siti.

"Nitafutie ka-McDonald basi. Nina hamu kali ya kula hamburger," akaniambia hivyo.

Nikarudisha umakini wangu tena kwenye usukani na kuliingiza gari barabarani, nami nikaendesha kuelekea upande ambao ungekuwa na mgahawa mmoja mzuri kama McDonald's kweli ili madam ajilie alivyotaka, na bado rundo la mawazo likiwa limekilemea kichwa changu.

★★

Tukapata mgahawa mmoja mzuri na kujumuika kula hicho cha asubuhi, kwa utulivu tu pamoja tukala hizo baga nzito kwelikweli mpaka kushiba, naye akalipia kisha tukaingia barabarani tena ili kurudi hotelini kwake mara moja. Alihisi uhitaji wa kujisafisha mwili kisha tuondoke tena kwenda kwenye biashara zake kama ilivyokuwa kawaida, na kama vile hakukuwa na lolote zito lililotokea kwa hii asubuhi.

Tumekuja kufika kwenye chumba cha hoteli alipokaa ikiwa imeshaingia saa sita mchana, na huko nje kulikuwa na wingu zito lililoonyesha nia ya kutaka kushusha mvua ya maana, kwa hiyo kulikuwa na hali ya ugiza ndani ya chumba chake iliyofanya awashe taa na kuipa sehemu hii hali ya usiku-usiku yaani. Bado nilikuwa kama sina raha, Bertha ndiye aliyekuwa akizungumza zaidi kuhusu kuliuza lile gari lake lingine la Harrier ili apate pesa ya kuchezea, lakini ni kama nilikuwa simsikii kabisa.

Nikakaa tu sofani na kutulia wakati yeye alipokuwa ameanza kuvua nguo zake, halafu akapokea simu ilipoita na kuzungumza na mtu fulani kuhusiana na masuala ya usambazaji wa madawa na malipo kwa wafanyakazi wao. Nikatoa simu yangu mfukoni kuangalia ujumbe uliokuwa umeingia, na oh ikaja kwa surprise, ilikuwa ni askari Ramadhan. Nikamwangalia Bertha, ambaye alikuwa ametoa nguo zake na kubaki na sidiria na nguo ya ndani nyeupe tu, nami nikaufungua ujumbe huo na kuusoma upesi.

'Tulikuwa kweny mission nyingin huku Ilala. Nisharud, utanipa update mpya. Kesho kesho-kutwa uhakika'

Ukasomeka hivyo. Alikuwa ametumia namba yake ya kisiri, na baada ya kuusoma huo ujumbe nikaufuta upesi Bertha alipokuwa ameanza kuja upande wangu huku bado akizungumza na mtu wake. Akakaa sofani karibu nami kwa kukunjia mguu mmoja juu, akijibinua mgongo kiasi kuelekea mbele ili akikaribishe vyema kifua chake kwangu, nami nikawa namwangalia kwa utulivu tu. Akawa anachezea-chezea ndevu zangu hafifu upande wa shavu, kisha ndiyo akakata simu na kuweka mkono wake mmoja kifuani kwangu.

"Kuna wajinga wanasema nawaonea eti kisa nimechelewa kuwapitishia malipo leo, re-up zenyewe wanazofanya zinayumba, lakini bado wanalalamika. Maneno meengi. Si nimetoka kukwambia? Umeona jinsi watu wanavyopenda rebellion? Basi tu ili tuanze mizozo, halafu tufikie pabaya..." akasema hivyo na kusonya.

Mimi nikaangalia mbele tu kwa utulivu.

Akaonekana kunitathmini kidogo, kisha akasema, "Una uhakika hautaki twende kuoga wote?"

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Mmm... JC! Ndo' kusema bado nyundo ya Thor imekugonga namna hiyo?"

Nikatabasamu kiasi na kusema, "Sijui hata unamaanisha nini."

"Yaani hauna raha kabisa. Unawaza nini bwana?"

"Kuwaza lazima madam. Ah... hivi ikitokea pale pakajulikana? Itakuwaje? Hm?"

"Pajulikaneje?" 

"Inaweza ikatokea... dharula... watu wenu mpaka waje wapasafishe, wenye jengo wanaweza wakafika, au... ile miili tu kwanza wanaitoaje pale huu mchana wote, inawezekana kuna CCTV camera za nje, na... kuna mlinzi pia. Exposure huoni iko high?" 

"Una-panick mno, hakuna vitu vya namna hiyo... we' umeona CCTV wapi?" 

"Sijaona sawa, lakini kuna mlinzi. Hata kama mtamlipa, anaweza akaja akawataja baadaye ikiw...."

"Mlinzi yupi?" akanikatisha kwa kuuliza hivyo. 

Nikaendelea kumwangalia usoni kwa umakini. Akapandisha nyusi kama vile kutaka kunielewesha jambo fulani, nami nikawa nimemwelewa. Aisee! Na mlinzi wangemuua. Dah! Nikatazama pembeni tu nikihisi kuchoka zaidi. 

"Usiwe na presha. Tunajua jinsi ya ku-handle mambo vizuri, so just... tulia. Acha kuwaza mno. Come on, be a man," akaniambia hivyo na kunipiga kidogo shavuni.

Nikamwangalia na kuuliza, "Kwa hiyo una shaka kwamba me siyo mwanaume?"

"Sina shaka, ila ndo' umeanza kunipa mashaka. Ukiiacha hii kitu ikutikise namna hii, kweli utaweza wewe kubeba mengine yanayokuja?" 

"Unamaanisha nini?"

"Charles amekufa. Nataka nikupe hoteli ya Buza na pale Masai, uzi-handle," akaniambia hivyo.

Nikawa makini zaidi na kuuliza, "Nini?"

"Yeah. Tena nakupa zotezote. Lakini utaweza kubeba wewe?" akaniuliza hivyo.

"Ahah... Bertha subiri, usifanye maamuzi haraka-haraka. Me... sidhani kama nitaweza kubeba hizo biashara kweli..."

"Well sina mtu mwingine wa kumpa, awe kichwa huko. Nahitaji mtu ambaye... namwamini," akasema hivyo.

"Kwa hiyo na Chalii ulikuwa unamwamini?" nikamuuliza pia.

Akanikazia macho yake kama kuuliza 'nini?'

"Sorry Bertha, yaani... ni jambo zuri kujua unaniamini, thanks, lakini mimi hayo mambo si...."

"Nakupa hizo sehemu, JC. Utake usitake," akasema hivyo.

Nikabaki nikimtazama machoni kwa umakini.

"And anyway, sina... sina mpango yaani hata wa kuziangalia, maana... nahisi kama vile scent yote ya Charles imetapakaa huko. Nakupa. Handle utakavyoona inafaa. Full stop," akasema hivyo.

"Unamaanisha hazina faida sana kwako?" 

"Yeah. Kwa hiyo, nakupa, yaani kama, nakuachia. Ukiamua kuuza ukanunua gari, sawa tu. Ndo' zawadi zangu kwako, kwa hiyo ukiamua kuzitunza au kuzitupa... ni wewe tu. Zishakuwa zako," akaniambia hivyo.

"Ila Bertha! Unapenda kuchezea vitu wewe..."

"Kuchezea? Si ni vyangu? Najenga vingine bora zaidi, hivyo naona kama vimeshapitwa..."

"Halafu ndo' unaniachia mimi? Kwamba na me nimepitwa sana?"

"Ahahahah... utajiju. We' fanya unaloona kuwa sawa huko, yaani hayo maeneo sa'hivi sitaki kugusa kabisa. Kinachotakiwa nikuhalalishe tu huko, halafu uendeshe mambo unavyoona inafaa. Ila ndo' utumie zawadi zako vizuri. Nimesota sana mpaka zikawa kubwa vile..."

"Halafu sasa hivi unazitupa?"

"Agh... whatever. Don't blow a brain gasket," akaniambia hivyo kwa kutojali.

Alikuwa yuko mawinguni kwelikweli yaani, sidhani hata alikuwa akifikiria upande hasi kwa wakati huu maana alihisi kuwa kila kitu kingekwenda vizuri sana kutokea hapa baada ya kuwaondoa Sudi na Chalii Gonga, lakini ambalo hakulijua ni lile ambalo lingekuja kumpiga vibaya mno kama giza la ghafla pale ambapo umeme wake ungekatwa. 

Ila, kufikiria kwamba nilikuwa nimetoka kujitahidi kumwokoa muda mfupi nyuma ili tena nije kuona anaporomoka kulinipa mvurugo mwingi sana wa kihisia. Yaani moyo wangu haukuwa na msimamo sahihi kujua ulitaka nini kutokea hapa ilipokuja kwenye suala la huyu mwanamke. Mambo yalikuwa yamekwenda mbali sana, na sikuwa na njia ya kuyabadilisha yale yaliyokuwa yakija.

Nikiwa bado natafakari tu, Bertha akaingiza kiganja chake ndani ya T-shirt langu na kunishika tumboni, naye akasema, "Bado tu kale ka-scene pale tulipokuwa kanazunguka kichwani kwako, eh? Ukikumbukia jinsi hao mafala walivyokula chuma... doesn't it turn you on?"

Aliongea kwa njia ya kuamsha hisia za kimahaba huku akiukaribia uso wangu, nami nikamwangalia usoni kwa utulivu.

"Vile nilivyompiga Chaz risasi... tah, tah! Wasn't that fucking hot?" akasema hivyo na kunilamba shavuni.

"Kwa hiyo... hivi tuseme kama ningekuwa nimekugeuka na kukusaliti kiukweli, ungeniua na mimi?" nikamuuliza hivyo.

Mishipa ya shingo yake ikatokeza akiwa ananiangalia kwa utafakari, naye akarudisha uso wake nyuma na kutazama pembeni, kisha akasema, "Acha kuwaza hayo bwana, nimekwambia. Hauwezi kunisaliti, najua hilo. Kwa hiyo kukuua ni kitu ambacho siwezi kufanya."

"Lakini vipi ikitokea, ikitokea tu nikakusaliti Bertha? Utanifanya kama Chalii?" nikamuuliza tena.

Akaniangalia na kusema, "Sitaki kuongelea hayo mambo, JC. Usiharibu mood yangu bwana, niko lifted, unakuwaje?"

Nikashusha pumzi na kukishika kiganja chake taratibu, nami nikamwambia, "Bertha, najua hatujakutana katika mazingira mazuri sana. Mambo ya mbeleni... yanaweza yakabadilika...."

"Unataka kusema nini, JC? Niambie ukweli," akanikatisha kwa kusema hivyo.

Nikabaki nikimtazama machoni kwa utulivu.

"Unahisi utanisaliti? Hm? Kwamba utanichoka na utapata mwanamke mwingine unayeona ni mzuri sana zaidi yangu, si ndiyo? Au tayari una mwanamke mwingine?" akauliza.

Hiyo haikuwa maana yangu, yaani hakuwa hata na wazo kabisa kuhusu uwezekano wa usaliti nilioongelea kuwa wa kumpindua yeye na watu wake kabisa. 

Nikamwambia, "Sijamaanisha hivyo."

"We' nimeshakuelewa JC. Unafikiri nitakufanyia kama nilivyomfanyia Chaz, kwa hiyo unaogopa. Lakini siwezi kukufanyia hivyo. Nakupenda," akaniambia hivyo kwa hisia.

Dah! 

"Na nimekwambia ukiwa na mimi akili yako inapaswa kuwa sehemu moja, usiitangishe sana, utapata ma-stress tu. Sasa hivi wa kutupa hayo mastress nimeshawaondoa, kinachobaki ni mimi na wewe. Angalia hilo. Focus kwenye hilo. Usiwaze sijui unaweza ukanisaliti... we' ni mtu mzima JC, na ni mmoja mwenye msimamo, I know. Kwa nini ufikiri unaweza kunigeuka? Unigeuke kwa kipi labda? Iweke mindset yako inapopaswa kuwa, hautafanya lolote lile baya kwangu. Mimi naamini hilo. Kwa nini we' ushindwe?" akaniambia hayo.

Nikainamisha tu uso wangu.

Akanishika kidevu na kunitazamisha kwake huku akisema, "Usiogope. Wewe ni wangu. Nitafanya kila kitu kukulinda kama wewe ulivyoweza kunilinda. Unajua, nili-imagine ikiwa Dotto angekuwa amenigeuka kiukweli, basi leo... mimi na wewe tungekufa pamoja. Ulikuwa tayari kwa ajili ya hilo, na hiyo ni sababu tosha kwangu kuamini mpaka mwisho kwamba hauwezi kuniumiza. Nimeona upendo wako kwangu JC, kwa hiyo achana na stress kuanzia sasa hivi ili mimi nikuonyeshe wa kwangu. Sawa?"

Nilijikuta hadi napenda ufasaha wake katika kuongea, lakini bado moyo ulikuwa ukiniuma sana. Kujua kwamba alikuwa amenipenda kikweli, lakini mimi nisingeweza kumpenda namna hiyo, na bado ningehitaji kumtupia kwa maaskari ili akutane na mkono wa haki wa sheria. Yote kwa yote, Bertha bado alikuwa mwanamke aliyefanya mambo mengi yasiyofaa, kwa hiyo hata kama roho ingeniuma vipi, ningetakiwa kuacha kile ambacho askari Ramadhan alikuwa amekisema kwenye ujumbe alionitumia kitokee. Hakukuwa na namna.

Baada ya madam kunibembeleza kwa hayo maneno, akanifuata mdomoni na kuanza kunibusu kimahaba sana. Sikuwa katika hali nzuri kihisia kunifanya nisisimke, lakini kadiri alivyoendelea kunionyesha hamu yake kwangu, ndivyo nami nikaanza kupanda taratibu. Akanikalia kabisa na kuendelea kunionyesha upendo wake, nami kiukweli sikuwa nikitaka tena jambo hilo kwa sababu nyingi, lakini kuliacha litokee ikawa ni lazima.

Kwa hiyo nikamruhusu afanye kila alichotaka kwenye mwili wangu ili kunipa mapenzi yake matamu, tukapiga mechi kwa mtindo wa kuendesha farasi akiwa amenikalia hapo hapo sofani, na alikuwa anaruka! Kisha tukaipeleka mpaka bafuni na kuoga pamoja bila kuacha kupeana penzi. Nilihakikisha namridhisha kwa wakati huu kwa sababu nilijua ingekuwa ni mara ya mwisho, kwa hiyo ningekuwa nimemwachiapo kumbukumbu nzuri kiasi kabla ya mbaya ambayo angekuja kubaki nayo wakati ambao angekamatwa. 

Hivyo ndivyo karata dume ilivyopaswa kuchezwa mpaka kufikia mwisho wa mahusiano yangu na huyu mwanamke, na hayangechelewa kufikia tamati, lakini najua kwa njia moja ama nyingine yangeniacha nikiwa nimevurugwa mno. Kutojali sana, ndiyo kitu nilichokuwaga najaribu kukimbia na kujifanya hakipo kabisa kwenye mfumo wangu, lakini hii hali ilikuwa ikithibitisha vingine. Nilimjali Bertha, hata kama alikuwa mbaya, nilikuwa nimemjali. Lakini ndiyo ningetakiwa kumwachia tu, kama msemo wake, nitake nisitake.

★★

Kwa hiyo baada ya mechi tamu iliyomridhisha madam, akawa ameamua kuvaa vizuri tena ili atoke kwenda kushughulikia biashara zake. Ilikuwa twende pamoja, lakini nikasingizia kuwa sikujihisi vizuri, yaani sikuwa na umakini uliofaa kumsindikiza huko na hivyo ingekuwa bora tu kama ningeenda kule Ubungo kwenye supermarket kumalizia nini na nini, maana wenzangu wangekuwa wamelemewa na mengi bila mi' kuwepo.

Lakini Bertha akaona anidekeze kidogo. Akaniambia niende tu kwangu nikapumzike, maana aliona hii siku ilikuwa nzito mno kwa hiyo sabato fupi kutoka kwenye biashara zake ingekuwa bora kuchukua. Na kweli, nilihisi uhitaji wa kupumzika kiakili na kimwili. Akanipa na hela, eti nitakula na kuichezea kidogo kwa kunywa hata bia, nami nikamshukuru na kuamua kuvaa, kisha nikamwacha hapo hotelini kwake ikiwa ni mida ya saa tisa alasiri. Mvua kubwa ilikuwa imenyesha na kukata, kwa hiyo hali ya unyevu ilikuwa imetapakaa kwingi na mawingu kuficha jua bado.

Mpaka napanda daladala kwenda Mbagala na safari kuanza, bado nilikuwa nimetekwa kimawazo sana. Yaani, kuangalia yale mauaji leo, nilijiona kama vile nilitoka kwenye ndoto mbaya tu, na hii sehemu ya maisha yangu haikuwa kweli. Ila, hakuna chochote ambacho ningeweza kubadilisha kuhusu kilichowapata Sudi na Chalii Gonga. Wazia kama kweli Dotto angekuwa pamoja nao, ningekuwa wapi sasa hivi? Kwa hiyo kihalisi nilitakiwa kushukuru Mungu kuendelea kupumua, ingawa yaliyotokea bado hayakuwa yenye kuridhisha.

Sikuwa hata na hamu ya kushika simu, sijui niwasiliane na nani, yaani nilitaka tu kufika kwa Ankia na kulala kabisa. Baga niliyokula saa tano ilinitosha, na nimekuja kufika Mzinga kwenye mida iliyoelekea saa kumi na moja. Hakukuwa na msongamano wala nini. Nikatembea tu mpaka kwa Ankia, nikiwa sina bastola yangu tena, nami kweli nikaingia pale ndani mpaka chumbani na kujitupia tu kitandani kama mzigo.

Mwili ulikuwa umechoka kiasi shauri ya mechi ndefu niliyocheza na Bertha, na bado viungo viliuma-uma kiasi shauri ya kuwa nimeanza kunyanyua chuma, kwa hiyo nikaona nijaribu kuvuta usingizi tu ili nipumzike ipasavyo, lakini ukanigomea. Yaani nilijigeuza na kujigeuza, wapi, mpaka inaingia saa moja yaani bado nilikuwa kitandani tu nalazimisha usingizi, lakini ni mawazo na mawazo tu ndiyo yaliyoendelea kunisumbua.

Nikaona niachane na kitanda na kunyanyuka kwenda kukojoa kwanza, kisha nikawasha taa za ndani na nje na kurudi kitandani tena. Nikachukua simu yangu na kuangalia hili na lile, na bado yule Kevin hakuwa ameacha kunitumia jumbe za kuniuliza kama nilikuwa nimeshaongea na dada yangu kuhusu ugomvi wao. Ndiyo nikaamua kumtumia ujumbe nikisema kuwa ni wiki hii ndiyo ningekwenda kumwona Jasmine, hivyo ningezungumza na dada yangu huyo kwa niaba yake kwa hiyo asiwe na hofu.

Kevin akawa amerudisha jibu la shukrani na kuniambia nimjulishe yatakayojiri, nami nikamkubalia. Kidogo tu, Tesha akawa amenipigia, na nilipopokea akaniuliza ikiwa nilikuwepo hapa nyumbani tayari. Nilipokubali, akasema ndiyo anakaribia kufika huku akiwa anatokea sokoni huko Mzinga, kwa hiyo angekuja hapa kunicheki. Hakukuwa na shida na hilo, na kweli baada ya dakika kadhaa jamaa akaingia hapo kwa Ankia na moja kwa moja kuja mpaka chumbani kwangu. Ankia hakuwa amerejea bado.

Tesha akaja mpaka kitandani na kukaa, akiwa na mwonekano wa kawaida tu wa kinyumbani, nami nikajivuta na kukaa kwa kuegamia mto mwanzoni mwa kitanda. 

"Oya, vipi unaumwa?" akaniuliza hivyo.

"Hamna. Nimechoka tu," nikamwambia hivyo.

"Mizunguko mingi, au siyo?"

"Yeah."

"Kamepiga leo ile mchana!" akasema hivyo.

"Nini, mvua?"

"Eeh. Ilikukuta huku?"

"Hamna, nilikuwa Makumbusho bado. Na wewe? Ilikukutia wapi?"

"Kwa Happy."

"Ooh, kumbe ulienda Tandika?"

"Mm-hmm."

"Sawa. Mzima huyo mke wako?" nikamuuliza.

"Eeh, alikuwa ameni-miss kidogo. Nikaenda kumcheki, amekuja na dada yake pale. Ndiyo nikatambulishwa, eti mashemeji," akasema hivyo na kutabasamu.

"Mhm... na we' utakuja kumtambulisha Happy lini?" nikamuuliza.

"Ah, bado bwana..."

"Anaonekana anakupenda sana. Kwani unaogopa nini?"

"Hizo siyo mambo zangu, kaka. Nitakuja labda kukupeleka wewe kwanza akujue brother wangu, lakini kumleta huku? Hamna."

"Kwa hiyo hutaki kuacha lifestyle ya kurukaruka? Hutaki kutulia na mmoja?" nikamuuliza.

"Muda wa kutulia utafika tu. Sa'hivi naona bado bro. Na sometimes naweza kufikiri nitatulia na huyu afu' tunakuja kutibuana tu. Nishawahi kuleta demu hapo, akatibuana hadi na mama hao... sitaki hayo yajirudie," akasema hivyo.

Nikatabasamu kiasi na kutikisa kichwa taratibu. 

Akasema, "Hata kazi ya maana bado sijapata, nadandia opportunity hapa na pale, hazishiki, natuliaje na mwanamke kama Happy ambaye tayari ana kazi yake. Ye' ndo' anilee?"

"Ee, si anakupenda? Kwani kuna shida gani?" 

"Aa wewe, unazingua. Masuala ya me kuanza kukalia kigoda kumpikia siyawezi," akasema hivyo, nasi tukacheka kidogo.

Nikamwambia, "Uko sahihi. Ni muhimu upate kazi. Huwa unatafuta?" 

"Eeh, kaka. Sema, me JC... kazi sijui za ndoo zege, siwezagi kabisa. Za maofisini ndo' zinanifaa. Natuma maombi kama yote, wengine matapeli tu, si unajua? Huku pakikubali, ukaingia, unalaghaiwa, agh, unarudi mwanzo tena. Yaani... nataka nipate sehemu ya uhakika, bro. Hela nzuri yaani, nitoke nikae na mwanamke wangu," akaniambia hivyo.

"Yeah, ila sa'hivi Bongo kubagua kazi Tesha, unajua jinsi maisha yalivyo magumu. Ni bora uwe na sehemu umeegamia hata kama bado iko chini, ili uende unapanda, kuliko kungoja for the perfect job. Umri unaenda rafiki yangu," nikamwambia.

"Unasema kweli, bro. Ninaelekea 26 sa'hivi, usingekuwa wizi wa Joshua ningekuwa nimetumia mali yangu vizuri sana kuendesha maisha... ila hiyo ishapita. Natakiwa nitafute changu. Da' Mimi mwenyewe analemewa naona, mambo kibunda ananyooshea mkono, lakini sometimes na yeye simwelewi. Sijui anataka nikae nyumbani kimoja?" akaongea hivyo.

"Kwa nini useme hivyo?" nikamuuliza.

Akasema, "Yule jamaa'ake anayemtongozaga, Festo, anayekujaga hapo 'skani..."

Nikawa makini na kuuliza, "Amefanyaje?"

"Alitaka kunipa ofa kufanya kazi... kwenye kampuni yake, anapofanyia. Nikamwambia sister, akanikatalia. Nisikubali eti," akasema hivyo.

Nikatulia kidogo, kisha nikamuuliza, "Kwa nini Miryam alikukatalia?"

"Si hamtaki jamaa? Sasa... anafikiri nikikubali hizo favor na nini, mwamba atakuwa anajirahisishia kuingia pale. Mimi hapendagi watu waingie kwa shortcut, yule jamaa anaonekana ana hela, ashawahi kujaribu kumnunulia mavitu da' Mimi, akayakataa. Huwezi jua, labda hata... unaweza ukakuta ana limke huko mikoani ama hizo hela za utapeli, si unajua?" akasema hayo.

Nikaangalia tu chini na kutikisa kichwa kukubaliana na hilo.

"Da' Mimi hataki kabisa za kupewa na wanaume, naelewa. Ila ndo' sa' me nikikubali kufanya kazi huko, kwani jamaa atambeba kwa lazima? Si ananisaidia tu?" Tesha akaongea hivyo.

"Hapana, dada yako yuko sahihi. Usikubali lolote kutoka kwa huyo mwanaume," nikamwambia.

"Kwa nini?"

"Tumia tu akili ya kuzaliwa Tesha. Kuna wanawake wangapi? Kwa nini anafosi sana kumpata dada yako? Inaweza ikawa siyo kwa nia nzuri, na Miryam anaelewa hilo, ndiyo maana akija hapo anamchekea tu lakini siyo kwamba anamwelewa wala nini... Bongo hii kama unavyojua, ni kuwa makini. So uwe smart pia Tesha. Kama ulivyosema, huwezi jua. Usikubali vyote tu vya kupewa. Pambania unavyotaka kuwa navyo," nikamwambia hivyo.

Akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, naye akasema, "Sawa. Ndo' pambano liendelee."

"Vipi hapo home, wako poa?" nikamuuliza hivyo.

"Eeh. Dah, kaka yaani tulikuwa excited kinyama na birthday ya ma' mkubwa Jumamosi, asikwambie mtu..." akasema hivyo.

"Eee, afu' kweli. Ni Jumamosi! Ah, cheupe wangu atakua. Imewahi kufika eti? Kesho kutwa tu," nikamwambia hivyo kwa shauku kiasi.

"Eeh, ila na matatizo yameitangulia sasa, sijui hata kama tutaisherekea mwanangu," akasema hivyo.

"Kwa nini?" nikauliza.

Akasema, "Kaka... nilipokwambia da' Mimi amelemewa, yaani elewa amelemewa kichizi..." 

Nikiwa nimeshajua ambako angeelekea, nikatazama pembeni tu kwa utulivu.

"Kuna deni nasikia la milioni ngapi sijui anatakiwa alipe, kwa sababu ya yale mautumbo ya Joshua, kaka. Huo mwezi uliopita, ametupa hela nyingi kinoma kwa ajili ya Mamu, huko dukani, ma' mkubwa Jamila, kusapoti ndoa ya Doris, mambo kibunda tu, na sasa hivi hili limekuja tena. Hapo alipo anahaha kuitafuta hiyo hela, sijui wamempa muda gani, ila ni mfupi sana... anakuwa na mawazo huyo... mpaka namwonea huruma," akasema hivyo.

Nikashusha pumzi kiasi na kuuliza, "Amekwambia hayo yeye mwenyewe?"

"Hamna, ma' mkubwa, cheupe wako ameniambia. Waliongea, dada akamwambia, na hataki sisi wengine tujue maana anataka amalizane na hilo kabla ya birthday, ila... nimeshaona kama linampiga vibaya mno. Sijui itakuwaje akishindwa kuwalipa, ndiyo maana nilikuwa natamani hata ningekuwa na kazi tayari mwanangu, kukaa hivi navaa suruali tu halafu sina pepa... ufala tu," akaongea hivyo kwa mkazo.

Jambo hilo likawa limerudi kichwani na kuanza kufanya mizunguko yake kama kawaida, nikiwa nakumbukia maneno ya mzee wangu ile asubuhi wakati nikiwa kwenye boda. Tesha hakujua undani wa kile ambacho Miryam alikabili, lakini mimi nilielewa kwamba kilikuwa kizito sana.

Kwa hiyo tukaendelea kuongea mambo ya hapa na pale kuhusiana na jambo hilo na sherehe ya Bi Zawadi Jumamosi, nikijitahidi kuonekana kuwa sawa kihisia tu hadi Ankia aliporejea hapa tena na kujiunga nasi. Mwanamke alikuwa ameleta chakula kwa ajili ya kupika, yaani unga wa ugali na samaki zilizokaangwa na viungo vyake, na baada ya muda mfupi tu akaenda huko jikoni kwenda kupika. 

Mimi na Tesha tukaendelea kuwa pamoja hapo hadi mida ya saa tatu jamaa alipoaga kurudi kwao, ndiyo nikamtoa mpaka nje na kumwambia awasalimie wa kwao, nisingeweza kwenda leo kuwaona mpaka kesho, kisha baada ya hapo nikaamua kukaa subuleni na mwenye nyumba wangu. 

Sikuwa na uchangamfu yaani, nikiwaza mambo niliyojionea leo, tatizo la Miryam, ishu za familia yangu mwenyewe ambazo mama alitaka sana nije kwenda huko nyumbani ili tuzizungumzie, na kile ambacho kingetokea kwa Bertha baada ya askari Ramadhan kutibua biashara zake. Kichwa kilikuwa kimechemka haswa, hali yangu ya kihisia ikiwa imeshuka bado mpaka na Ankia akauliza ikiwa nilikuwa naumwa. 

Lakini nikamwondolea wasiwasi, na baada ya kuwa amemaliza kupika tukala pamoja, huku tukitazama TV, na tukaendelea kupeana ushirika mpaka kufikia mida ya saa tano kabisa. Ankia alikuwa ameanza kuchat mno kwenye simu yake kwa huo muda, na niligundua kuwa aliyekuwa akichat naye ni Bobo. Inawezekana tayari jamaa alikuwa ameanza kumtokea, lakini mwanamke hakutaka kuweka wazi jambo hilo kwangu kwa hiyo nikaona nijikaushe tu kama vile sikujua.

Akawa ameamua kuelekea chumbani akidai kwamba angelala mapema, wakati naelewa alitaka kupigiana simu na jamaa huko huko! Nikasema sawa tu, yeye aende na mimi ningefanya ufungaji wa hii milango kuanzia huko nje, naye alipoondoka, nikaona nizime tu TV na kubeba funguo ili niende nje kufunga geti, kisha ndiyo ningerudi na kujimwagia kwanza kabla ya kwenda chumbani kupumzika ipasavyo.

Nilipokuwa nimetoka ndani na kuufikia ukuta wa uzio, upande wa nyumba yao Tesha ambao ulikuwa na ile taa iliyoungua haukuwa ukitoa mwanga, kumaanisha hakuwa amebadilisha taa bado, hivyo kulikuwa na giza kuuelekea huu wa kwetu. Nikiwa ndiyo naelekea kuuvuka ili niende huko getini, matobo ya ukutani yakaniruhusu nione upande wao wa varandani hapo nje, na kwa uhakika, bibie Miryam alikuwa amekaa pale kwenye kiti chake kama alivyozoea.

Nikaahirisha kusonga mbele zaidi na kusimama kumwangalia, na kwa sehemu niliyosimama asingeweza kuniona kwa sababu giza lilinificha kiasi, kwa hiyo nikaamua kuegamia ukuta kabisa na kuendelea kumwangalia. Bibie alikuwa amekaa kwa utulivu tu, na urembo wake wote aliojaliwa kuwa nao ukinifanya nimwangalie kwa hisia, akitazama mbele kama mtu aliyezama kwenye mawazo sana, na ninaelewa alikuwa akitafakari vitu vingi mno. 

Labda kama angepewa muda wa kutosha, basi hilo suala la shamba angelitatua vizuri sana, ila yaani ni kesho tu alitakiwa kuamua la kufanya kati ya mambo mawili aliyokuwa amepewa kuchagua, na najua alikuwa akijiuliza ni kipi alichopaswa kuamua ambacho kingekuwa sahihi si kwake tu, bali na kwa mdogo wake Mariam, na familia yote kwa ujumla.

Nikamwona Mariam akitoka huko ndani kwao na kumfata Miryam hapo nje akiwa na shauku ya kumwonyesha dada yake jambo fulani, nami nikatabasamu kiasi baada ya kumwona binti. Miryam pia akatabasamu kwa hisia na kumsikiliza mdogo wake, ambaye alitaka waende ndani pamoja ili amwonyeshe, na bibie akawa amekubali. Mariam akatangulia huku akionekana kufurahi, naye Miryam akaacha kutabasamu na kutazama pembeni kama vile raha imemtoka tena. Alitia huruma! 

Lakini akashusha pumzi tu na kunyanyuka taratibu, naye akajibebea kiti chake na kuelekea ndani bila kutambua kwamba nilikuwa hapo nikimwangalia. Nilitaka sana kumsaidia huyu mwanamke. Sikupenda kumwona hivyo. Na hasa baada ya kuongea na Tesha muda mfupi nyuma kuhusu jinsi dada yake alivyokuwa mkali kwenye masuala ya shortcut, ndiyo nikawa nimeona hakukuwa na njia nyingine ya kumsaidia Miryam isipokuwa kuchukua hatua ambayo najua huenda isingemfurahisha kabisa. Na mimi ndiyo nikaamua kuichukua hiyo hatua sasa, hata kama ingemkwaza.

 

 

★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next