Iliwachukua muda mchache sana kwa Amiri na Hamza kufika mwisho wa safari yao , katika maikazi ambayo anaishi mpenzi wake Amiri afahamikae kwa jina la Mellisa.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Hamza kufika ndani ya hili eneo na lilikuwa likivutia mno kama sifa zake zilivyokuwa zikivuma kwa watu wengi ndani ya jiji la Dar es salaam.
Ni moja wapo ya Apartment ambazo zinamilikiwa na kampuni ya kimataifa ya Dosam Global.
Kwa machache ambayo alikuwa akijua Hamza kuhusu kampuni yaDosam ni kwamba ilikuwa ni kampuni namba moja Afrika ambayo inajihusisha na maswala ya mahoteli na Real estate ambayo makao makuu yake ni hapa nchini.
Dosam ni kampuni namba mbili kwa ukubwa ukiachana na kampuni ya Vexto group ambayo imeweza kuwa na biashara karibia kila kona ya Dunia, ndio kampuni ya Kitanzania ambayo imeorodheshwa katika Nasdaq.
“Bro hii sehemu ni nzuri sijapata ona”Aliongea Hamza mara baada ya kuruhusiwa kuingia na watu wa usalama wa eneo hilo.
“Ni sehemu ya hadhi ya juu hii broo, asilimia kubwa wanao ishi hapa ni aidha michepuko ya vigogo wakubwa serikalini au familia zinazojiweza kiuchumi”Aliongea Amiri huku akiweka tabasamu la kirafiki.
Hamza aliishia kutingisha kichwa huku akizungusha kichwa kulia na kushoto akijaribu kushangaa mazingira.
Ndani ya jiji la Dar es saalam kuna apartment nyingi tu ambazo zina mazingira ya juu lakini ukizungumzia Apartment hii ya Dosam’s Homes sio tu ukubwa wa jengo hilo bali ni uzuri wa jengo lenyewe , usanifu wake ulikuwa ni ule wa ulioendelea na pengine ndio jengo la makazi lenye mvuto mkubwa ndani ya Afrika nzima.
Hamza alijiambiaAmiri alikuwa na haki ya kuwa na wivu na mpenzi wake kama kweli amempangishia hili eneo.
“Bro hapa kwa mwezi malipo yake yakoje?”
“Kwa mwezi hapa ni doller elfu tano”Aliongea Amiri bila wasiwasi lakini bei yake ilimfanya Hamza kushindwa kupumua vizuri maana kwa haraka haraka pesa hio kama ikibadilishwa kwenda hela za kitanzania ni zaidi ya milioni kumi na mbili.
Pesa hio kwake ingeweza kumtosha kutatua changamoto zake zote hata kuanzisha biashara ambayo itaweza kumsaidia kwenye maisha yake ya hapo jijini Dar es salaam.
Dakika ambayo wanasubiria mlango wa lift kuweza kufunguka waliweza kukutana na harufu nzuri ya marashi na Hamza mara baada ya kuangalia mbele aliweza kukutanisha macho yake na mwanamke mmoja mwenye urembo wa ajabu mno ni aina flani ya wanawake ambao ni ngumu sana kuwaona mtaani , aliishia kujisemea Mungu anajua kuumba maana ni kama macho yake yanamdanganya na mwanamke huyo alikuwa akimuona ndotoni.
“Broo !!!, Oya Hamza!!”
“Eeh..!!”Hamza alijikuta akishikwa na mshangao na aliishia kujifikicha macho na kisha akatumbukia kwenye Lift huku yule mwanamke mrembo wa rangi ya chocolate akitoa tabasamu la dhihaka na kumpita Hamza kama kituko.
Alionekana ni wale wanawake ambao washazoea kushangawa na wanaume kutokana na urembo wao.
“Hahaha…. Bro naona mtoto kakuchanganya mpaka ukawa unaota?”Aliongea Amiri huku akishindwa kujizuia kucheka.
“Bro huyo manzi sio wa kawaida, nilidhani naangaliana na jini”
“Hahaha..huyo ni demu wa kawaida mbona , halafu mwanangu usihadaike na huo uzuri ni wa kutengeneza”
“Unamaanisha nini wa kutengeneza?”
“Namaanisha sio wa kuzaliwa nao , huyo manzi uliepishana nao nimemjua vizuri sana kupitia Mellisa, kwa habari za chini nasikia anafanya kazi Binamu Island”Aliongea Amiri kwa sauti ya chini kama vile jambo analoongea ni la usiri na usiriasi.
“Binamu Island !!?”Aliongea Hamza kwa mshangao kidogo na palepale macho yake yaliongezeka ukubwa.
Hamza alikuwa na taarifa chache sana kuhusu Kisiwa cha Binamu(Binamu Island) , taarifa chache alizokuwa nazo kuhusu kisiwa hicho ni kwamba kwanza kabisa ni cha kutengeneza ambacho kinapatikana bahari ya Hindi karibu kabisa na jiji la Dar es salaam.
Kwa fununu ambazo aliweza kusikia ni kwamba kisiwa hicho muda unafanya kazi tofauti na nje ya dunia(Timeless island), ni uzushi ambao kwenye maisha yake hajawahi kukubaliana nao hata mara mara moja.
Siku ambayo aliweza kusikia habari hizo kwanza alicheka na kujiambia waru wanadanganyika kirahisi sana ili tu kuweza kwenda kutembelea katika eneo hilo.
Ukiachana na fununu ambazo anasikia Hamza ukweli ni kwamba Kisiwa hicho kipo kabisa na kimejibebea jina kwa zaidi ya miongo kumi dunia nzima na kimekuwa chanzo cha kuendelea kwa mataifa ya Afrika mashariki kutokana na kutembelewa sana ,kimekuwa kivutio kikubwa sana kwa watalii.
Kwa maelezo machache ni kwamba sio watu wote ambao walikuwa na uwezo wa kufika katika kisiwa hicho kwani ni gharama kubwa sana.
“Nimesikia hivyo bro lakini bado siamini , mimi mwenyewe pamoja na kuwa na hela sijawahi kufika katika hiki kisiwa , lakini kwa upande mwingine naweza kumuamini Mellisa kwani maisha ya Tresha ambayo anayaishi hapa jijini sio ya kawaida”
“Tresha ndio nani?”Aliuliza Hamza muda huo mlango wa Lift ukifunguka na kuwaruhusu kutoka.
“Ni huyo mrembo uliekutana nae kule chini , anafahamika kwa jina la Tresha Noah ni maarufu sana mtandaoni”Aliongea na kumfanya Hamza kutingisha kichwa vhake kumwelewa.
Asilimia kubwa ya wakazi wa hili jengo kwa muda huo wanakuwa kazini na hata wale wachache wanaobaki majumbani ilikuwa ni ngumu sana kuonana nao nyakati za muda huo nadhani ndio maana Amiri akachagua kazi yake kufanyika katika wakati huo.
Baada ya kutembea umbali mfupi walisimama kwenye Apartment namba 103 na Amiri alitumia ‘pasword’ kufungua mlango huo na kisha wote wakaingia.
Hawakuwa wamesahau vifaa vya kazi kwani Amiri alikuwa amebeba begi kubwa wakati huo huku na Hamza mwenyewe akiwa na begi dogo.
Hamza mara baada ya kuingia ndani aliishia kutingicha kichwa na kujiambia kuna watu wanaishi pazuri , ijapokuwa watanzania wengi walikuwa wakidharau kuishi katika nyumba za kupanga aina ya Apartment lakini ufahari uliokuwemo humo ndani ulimpa msukumo na yeye siku moja kuweza kuishi katika mazingira kama hayo.
Hamza kama kawaida yake mara baada ya kuingia eneo la ndani alianza kukagua sebule hio na macho yake yalikuja kutua katika picha mbao yenye kuonyesha sura ya mwanamke mrembo ilioning’inizwa ukutani.
“Oya huyu ndio demu wako?”Aliuliza Hamza.
“Ndio huyo babu , unamuonaje?”
“Aisee ni kisu hata zaidi ya yule Tresha?”
“Hahaha,.. bro sipingani na wewe , Mellisa ni mzuri kuliko unavymuona kwenye hio picha , ukimuona laivu ndio utajua yule Tresha ni wa kawaida sana halafu Mellisa yeye uzuri wake ni wa asili sio wa kutengeneza”Aliongea Amiri kwa kujigamba.
“Ndio maana hujiamini?”
“Hehe ,, bro hata ni wewe ungekosa amani, nina pesa na namtimizia kila kitu lakini bado tu siamini kama ananipenda na hatonisaliti, isitoshe pia aina ya kazi yake inamkutanisha na vibopa zaidi yangu”
“Anafanya kazi gani?”
“Ni meneja wa benki ya Dosam Commercial Bank(DCB) tawi la Ubungo”Aliongea na kumfanya Hamza kushangaa kidogo.
“Anaonekana amepiga hatua katika maendeleo binafsi, naweza kusema haumhudumii kwa kila kitu, maana kwa ninavyojua wafanyakazi wa Dosam sio kama wafanyakazi wa mabenki mengine”
“Hicho ndio kinachonitia wasiwasi bro Mellisa hanitegemei kwa kila kitu hana njaa na mengine namfanyia kwasababu ni mapenzi, ukumbuke pesa ya mwanamke katika mahusiano pia haina thamani na wanajali sana wanachopewa kuliko wanachonunua”
“Haha uko sahihi”Aliongea Hamza huku akimuonea wivu Amiri kuwa na mwanamke mrembo mwenye mafanikio kama Mellisa,alijiambia yeye kama mwanamke wa kawaida kama Anitha amemshindwa ndio atafanikisha kwa Mellisa.
Ijapokuwa maelezo ya Amiri yalimwambia Mellisa ni mzuri zaidi kuliko anavyoonekena kwenye picha lakini kwa haraka haraka alimuona ni mzuri zaidi kuliko Anitha mwanamke ambaye alijaribishia bahati yake na akamdhalilisha mbele za watu kwa kejeli huku akimwambia ananuka umasikini.
Hamza mara baada ya kukumbuka matusi ya Anitha alijikuta akijichekea moyoni na kuachana na mwazo hayo na kisha alianza kufanya uchunguzi wa namna ya kufanya kazi yake.
“Bro unaonaje hapa , nataka picha kwanzia chumbani kwake mpaka hapa eneo la sebuleni , nataka kila kinachofanyika hapa niweze kukiona kupitia simu yangu”Aliongea na kumfanya Hamza sasa kuona kuna kitu hajakifikiri.
“Hizo ni Camera aina gani umenunua?”
“Ni IP Camera , vipi kuna tatizo?”
“Kama ni hizo hakuna tatizo, unachotaka kinawezekana”Aliongea huku akifungua mfuko wa vifaa na kuchunguza kamera hizo za kiuchunguzi na palepale Hamza alianza kufanya vipimo vyake kwa kutumia Angle ,ili kuweza kufunga Camera hizo kwa siri
Hamnza aliomba aonyeshwe na eneo la chumbani ili kuanza kazi yake na Amiri hakupimgas na waliingia wote chumbani na baada ya Hamza kuridhika alianza kazi yake ya ufundi, alifanya kazi kwa spidi kubwa mno huku akimuagiza Amiri kumpatia kila anachohitaji.
Amiri kwa upande wake alijikuta akimshangaa tu Hamza na kujiuliza ujuzi huo Hamza katolea wapi , ijapokuwa alikuwa akijua anaiweza kazi hakutegemea kama anaweza kuwa mtaalamu hivyo kwani ilikuwa ni kama anaangalia filamu za kijasusi, ndani ya dakika ishirini tu kila kitu kipo tayari na Hamza alirudisha mazingira sawa kama yalivyokuwa na kumwambia Amiri akague kama anaweza kugundua na mara baada ya Amrii kuangalia matokeo yake yalizidi matarajio aliokuwa ameyaweka kwa Hamza.
“Bro sijategemea kama kazi ingekuwa nyepesi kwako kiasi hichi , unaonekana ni mtaalamu wa hali ya juu”Aliongea Amiri huku akitoa mwanya wake nje lakini kwa wakati mmoja akimwangalia Hamza kwa wasiwasi na kujiambia pengine bwana huyo anajifanyisha kuishi maisha ya chini tu na ni mtu mwenye historia yake..
“Kaka sisi ambao maisha yetu ni ya chini tunajitahidi kujifunza aina mbalimbali za ujuzi ili tu tusiweze kupitwa na fursa , kwa wewe ambaye maisha yako yana msingi mzuri huwezi kunielewa”Aliongea Hamza na kumfanya Amiri kutoa tabasamu kwani maneno yake hayakuwa mbali na ukweli.
Yeye amezaliwa katika familia ambayo ilikuwa na kipato cha juu , hivyo ni rahisi kusema utajiri ameukuta na hata anachokisomea ni kwa ajili tu ya kuendeleza mali, kwake shida yake kubwa pengine ni maswala ya kimapenzi tu lakini likija swala la pesa alikuwa vizuri.
Baada ya kukamilisha kazi Hamza alimwambia kazi nyingine wanaweza kuifanyia mbali na eneo hilo kumsaidia kuseti kila kitu kuweza kuonekana kwa vifaa vya mbali na Amiri hakuwa na shida.
“Kwahio kwanzia hapa nitaweza kuona kila kitu?”
“Yeah zile ni aina ya Camera ambazo zinatuma teknolojia ya live streaming na zinatuma vidio kwako kwa njia ya internet, ni rahisi kuunganisha kupitia tarakishi kuliko hio simu yako ya Apple, unapaswa kuwa na Android tuweze ku install Apk maalumu ili kufanya configuration ya RTSP”Aliongea Hamza.
“Ninayo hapa hapa simu ya Android”Aliongea na palepale alifungua mkebe wa gari na kutoa simu janja kampuni ya Sumsung tole jipya na kumpatia Hamza.
Hamza alitumia dakika chache tu aliweza kumuunganishia Amiri kila kitu na kumpa aangalie na bwana huyo mara baada ya kuona mitambo imekaa vizuri alijikuta akishindwa kuzuia furaha yake.
“Mellisa japo nakuamini lakini kwa mapenzi yangu kwako nimeona niende mbali hivi , utanisamehe lakini naheshimu hisia zangu, naomba unithibitishie ninachowaza sio cha kweli”AluwazaAmiri huku akiangaalia mazingira ya eneo la Sebuleni kwa Mellisa na ndani chumbani wake.
“Hamza shukrani sana kwa msaada wako mzee , ukiachana na hisia zangu mbaya zidi ya Mellisa lakini kama ni kweli nina shauku ya kutaka kumuona mwanaume anaenisaliti nae”
“Nadhani unajitafutia maumivu ya moyo tu ndugu yangu?”
“Ni kweli unachosema , lakini nimewekeza hisia zangu nyingi kwa yule mtoto nampenda kuliko hata neno lenyewe , najua ninachofanya ni hatari lakini najua nini nitafanya hata kama nnikigundua ananisaliti , ila nikwambie tu Mellisa ni mwanamke ambaye siwezi kumuacha”
“Unaonekana kuwa jasiri , lakini usisahau ni vizuri kupenda na kupendwa pia”
“Haha..hata wewe mwenyewe ni mtu jasiri usisahau nilivutiwa na ujasiri wako ndio maana leo hii sisi ni marafiki , tuna tabia zinazofanana”
“Haha.. sidhani ule ulikuwa ujasiri , pengine wewe unaweza kuona ni ujasiri ila wengine wanaona ni ujinga na wananichukulia kama mwanaume dhaifu”
“Haijalishi wanafikiria nini ili mradi kama mwanaume umeweka wazi hisia zako bila ya kujali mazingira , mengine yapo nje ya uwezo wako”Aliongea na kumfanya Hamza kutabasamu.
*******
Ni masaa kadhaa baada ya Hamza kuachana na Amiri moja kwa moja alichukua daladala kuelekea mahali anapoishi.
Amiri alitaka kumpeleka lakini Hamza alimgomea na kumwambia atapanda daladala na Amiri hakutaka kwenda mbali kwenye kumbembeleza hivyo alikubali aondoke kinyonge.
Amiri alishangazwa na rafiki yake Hamza kwani alionekana kuwa na shida ya pesa lakini alikataa malipo kiasi cha kumfanya kukosa raha lakini kwasababu yalikuwa ni makubaliano hakutaka kulazimisha sana , aliona pengine Hamza amemsaidia kutokana na mara nyngi alikuwa akimsaidia.
Wakati Hamza akiwa kwenye daladala akiwa amepata siti yake kwa kuigombania, alitoa simu yake kwa ajili ya kuingia mtandaoni maana yalikuwa yamepita masaa bila kuingia huko kuona kinachoendelea.
Alikuwa akipenda sana mitandao ya kijamii na alikuwa ni radhi asile chakula ili mradi tu kuwa na bando hiyo yote ni kutokana na kwamba hakuwa na marafiki wengi na mitandao hio lilikuwa sehemu ya kupunguzia mawazo.
“Huu uzi bado tu una trend?”Aliongea Hamza huku akijaribu kuufungua tena na alishangaa kulikuwa na maoni mengi mno, alijaribu kutafuta maoni ya mtoa mada lakini hakuona chochote na kuishia kujawa na shauku zaidi juu ya mtoa mada aliona pengine anamaanisha alichokiandika.
“Kwanzia sasa hivi ngoja nifanyie kazi maneno ya Profesa Stephano nione kama yana uhalisia”Aiongea Hamza akikumbuka somo la Bonus point lililokuwa likizungumziwa na Profesa kuhusu Shauku.
Hamza alijikuta akipotezea makelele ya watu waliokuwa kwenye daladala kushabikia maswala ya uchaguzi na kwenda katika PM ya mtoa mada na kutuma ujumbe.
“Kwa kuzingatia tangazo lako , nipo tayari kwa ajili ya Ajira mawasiliano yangu ni 0656786***** naishi mkoani Dar es salaam”
Ni ujumbe mfupi ambao Hamza aliandika na alijikuta akijicheka mwenyewe , aliona ni kama anajiingiza kwenye mtego wa mtoa mada lakini aliona potelea pote , ngoja ajaribu bahati yake.
Baada ya kutuma ujumbe huo aliamua kuendelea na kutafuta mada nyingine ambazo zilikuwa zikimfurahisha na kupitia mada pamoja na maoni , lakini hata hivyo hakuna kizuri alichoona zaidi ya habari za uchaguzi tu, pengine habari ya ajira ya mahusiano ndio ambacyo ilikuwa ni habari mpya iliopata umaarufu na kutrend katika hizo siku kadhaa..
Usiku wakati Hamza akijiandaa kulala aliingia katika mtandao wa Watsapp na kutafuta jina la Anitha ambalo baada ya kulipata aliweza kuona mrembo huyo yupo Online , Hamza alitoa tabasamu na kisha akatuma ujumbe mfupi wa kumtakia mrembo Anitha usiku mwema huku akimsifia maneno ya hapa na pale kuusifia uzuri wake.
Aliangalia ujumbe huo kusomwa huku akiwa kama mtu mwenye matarajio ya kujibiwa ilihali alijua kwa asilimia tisini na nane Anitha hawezi kujibu ujumbe wake, mara baada ya kusubiria kwa dakika kadhaa alishuhudia tu ujumbe wake kusomwa na kisha palepale DP ya mrembo huyo ikipotea na kuweka kivuli cha sura ya mtu na kwa akili yake ya haraka haraka alishajua ashalambwa tofali.
“Hahaha… maringo ya huyu mwanamke inamfanya kutabirika”Aliongea Hamza huku akitoa kicheko cha uchungu na kujikuta akirusha simu pembeni, alijilaza kwenye gorodo lake la wanafunzi la nchi sita huku akiangalia darini kama kuna kitu anachokiwaza, aligeuza kichwa cheke upande wa kushoto lakini palepale alijikuta akikunja uso mara baada ya kuhisi harufu nziro iliokuwa ikitoka kwapani.
“Hizi ndio sababu ndogo ndogo ambazo zinampelekea Anitha kutonipenda , ngoja nikaoge kwanza”Aliongea Hamza na kisha alipiga teke dumu moja kivivu kuona kama lina maji na alitoa tabasamu mara baada ya kuhisi lilikuwa na maji japo kidogo.
Baada ya kuyamimina yote kwenye ndoo , licha ya kwamba haikujaa mpaka juu lakini hakujali, palepale alipunguza nguo na kisha akachukua taulo lake lililochakaa na kutoka nje kulitafuta bafu la pamoja(public) kuoga.
Ilikuwa usiku hivyo muda kama huo mara nyingi hakukuwa na bughuza upande wa bafuni na ilikuwa ratiba yake mara nyingi kuoga muda huo ili kuepuka kero za wapangaji wengine.
Hamza alitumia dakika chache kuoga pamoja na kukata gogo(Haja kubwa) huko huko na kisha alirudi na kujifuta maji na kisha akavaa bukta yake ya jezi ya Simba na kujitupa kitandani lakini usingizi ulikuwa mbali hivyo alichukua simu yake na kuzama tena JamiiForum.
“Hapa ngoja nitafute bandiko lolote la kizushi refu litanisaidia kupata usingizi”Aliongea huku akifungua mtandao wa JamiiForuma na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye jukwaa la Jamii Intelligence na kutafuta bandiko la kizushi.
‘Wajue Night Shadows , kikundi cha siri kinachotawala Dunia nyuma ya pazia”
Hamza mara baada ya kukutana na uzi huo alijikuta akivutiwa nao mara baada ya kuona una maoni ya watu wengi pamoja na Views , aliufungua kuona kuna kipi ambacho kimewavutia watu.
“Je unawajua Night Shadows ndio wamiliki wa kisiwa cha Binamu?”
Hamza mara baada ya kuona swali hilo ambalo mwandishi alionekana kuliweka makusudi ilimfanya kuvutiwa kwani ni mchana tu aliweza kukutana na mrembo Tresha Noah katika Apartment za Dosam Homes , alijiambia hapo ni mahali pake.
Comments