SEHEMU YA 04
Mwaka 2020 ni mwaka ambao ni wa kukumbukwa dunia nzima, ni mwaka ambao uliandika historia ya aina yake tokea binadamu kuanza kuishi maisha katika dunia akitegemea nishati ya joto na mwanga kutoka kwenye jua.
Kwanini mwaka 2022 ni mwaka wa kihistoria?
Ni kwasababu ya tukio la ajabu sana ambalo liliwahi kutokea , tukio ambalo mpaka leo hii halikutolewa ufumbuzi wa kueleweka kwa wakazi wote wa dunia hii.
Kwa maneno marahisi ni kwamba ni tukio ambalo tumefichwa ukweli wake na watu wanaojiita serikali.
Mwaka huu ndio mwaka ambao kwa mara ya kwanza ndani ya bara la Afrika kupata majira ya theluji(snow).
Linaweza kuwa jambo la kushangaza lakini ni kwa maeneo machache sana pengine hakuna kabisa ndani ya bara la Afrika kihistoria joto kushuka mpaka kufikia hatua ya unyevu nyevu uliopo angani kuganda na kupelekea Theluji.
Kushuka kwa baridi kwa kiwango cha kushangaza haikuwa kwa Afrika tu , tukio hilo linakumbukwa kutokana na kwamba maeneo ambayo yalikuwa yakipata Theluji katika vipindi vya majira, joto lake lilishuka sana kiasi kwamba kuyafanya mazingira hayo kutoweza kusapoti maisha ya binadamu, mimea na wanyama kiasi cha kukimbilia katika bara la Afrika ili kuweza kupata hifadhi ya muda kwa matarajio ya kipindi cha baridi kitakapo pita wangerejea katika makazi yao.
Hili ndio tukio la kwanza kuikumba dunia kiasi cha kufanya Afrika kuonekana mahali salama kwa makazi ya muda ndani ya dunia kwa ajili ya kujikinga na baridi iliokumba mabara mengi..
Ijapokuwa sio watu wote waliokimbia makazi yao na kuja kuishi katika bara la Afrika lakini idadi kubwa ya watu waliokuja kuomba makazi ya muda katika bara la Afrika ilikuwa kubwa mno.
Wanasayansi mbalimbali walishindwa kutolea maelezo mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa hio na kuishia kusema ni tukio la kustaajabisha.
Wapo waumini ambao waliweza kuamini ni siku za mwisho za dunia zilizotabiliwa zimewadia.
Ajabu ni kwamba tukio hilo halikudumu muda mrefu sana mpaka hali ya hewa kurudi katika hali yake ya kawaida na maisha kuendelea,
Baada ya tukio hilo ambalo lilikosa maelezo yakinifu, nadharia za kizushi za aina nyingi ziliibuka na kusema pengine ni onyo kutoka kwa Mungu kwa binadamu kwa matendo yao wanayoyafanya kutokana na anasa mbalimbali zilizokuwa zikifanyika , anasa ambazo zilikuwa zikienda kinyume na mapenzi ya Mungu.
Ukweli ni kwamba kila mtu aliibua kauli yake na wale watu wenye wafuasi wengi kwenye mitandao waliweza kuvumisha kila uzushi uliosemwa na watu wengi kuamini,.(Wakuu nyie ni mashahidi wa tukio hili)
Lakini watu wanasema sikio la kufa halisikii dawa , baada ya tukio hilo la ajabu kuikumba kupita kila mtu alisahau na maisha kuendelea na wale ambao ni watu wa dini walizidi kujikita zaidi na sala wengine wakisema wanaisubiria siku ya kiama na wengine walisema wanasubiria siku ya unyakuzi.
Mara baada ya tukio hilo kupita kulitokea Uzushi maarufu wa kinadharia(Consipiracy theory) iliohusisha uwepo wa watu vivuli(Night Shadows) ambao hutembea usiku.
Zimekuwepo shuhuda mbalimbali kuhusu matukio ya watu kadha wa kadha ambao wameweza kukutana na hawa watu wanaosemekama kuwa ni vivuli na kuwahusisha na viumbe kutoka sayari nyingine(Aliens).
Wakuu mnachokiona chini ni baadhi ya picha za ushahidi ambazo zimepigwa kuhusisha hawa watu wanaojiita Night Shadows.
Je hawa watu ni kweli ni Alien kama watu wanavyosema, je tukio la mwaka 2020 December lilikuwa na uhusiano na hawa watu vivuli , je ni kweli ujenzi wa kisiwa cha Binamu kuna uhusiano na hawa watu.
Kabla ya kuendelea wanabodi nataka kwanza mjiulize kwanini kisiwa cha Binamu kimekuwa maarufu?, kwanini kisiwa hichi ni ghali sana kutembelea lakini bado watu wanaenda.?
Itaendelea hivi punde
********
Ã
Down here in the rain fields
Outside of the Glow
My world is getting Smaller
Oh , oh , oh no
………………..
Ã
Mwito wa simu wa wimbo wa Low Tides kutoka kwa msanii Tom Rhodes ndio uliomuamsha Hamza ambaye hakujua hata amelala saa ngapi na alichokumbuka tu ni kwamba alikuwa akisoma mada ya kizushi kwenye mtandao wa JamiiForums mpaka kupitiwa na usingizi , baada ya kufumbua macho kivivu akiwa bado na usingizi alianza kuitafuta simu yake kwa kupapasa godoro lake lakini hakuiona na iliita mpaka ikakatika na hapo hapo aliendelea kujilaza kivivu, asiangalie hata muda huo ni saa ngapi.
Wakati akibadilisha staili ya kulala palepale simu ilianza kuita tena na awamu hii ilimuamsha kwa kusogea kidogo mpaka kwenye kingo ya Godoro na kuichukua simu hio ikiwa imedondoka chini Sakafuni.
Hakushangaa kwani hata hivyo haikuwa mara yake ya kwanza kupotelea usingizi usiku akiwa anaitumia na kudondokea chini.
“Hello!!”
Hamza hakujisumbua kabisa hata kuangalia aliekuwa akipiga ni nani na yote hio ni kutokana na macho yake kuogopa mwanga wa simu kwani ndio kwanza alikuwa akiamka.
“”Naongea na Ndugu Hamza Mzee?”
Sauti ya kike nzuri iliweza kusikika kwenye ngoma za masikio yake na kumfanya Hamza kushituka na kutoa simu sikioni na kuangalia namba ambayo ameipokea bila ya kuangalia jina la mpigaji lakini alishangaa mara baada ya kugundua ni namba mpya.
“Hello.. Mbona kimya!!”Sauti upande wa pili iliweza kusikika mara ya pili mara baada ya kimya cha Hamza kuwa kirefu.
“Ndio mimi ni Hamza , naongea na nani tafadhari?”
“Unaongea na mwanachama wa JamiiForuma mwenye ID ya Ngwena”Sauti ilisikika na kumfanya Hamza akili yake kufanya kazi kwa haraka na mara baada ya kukumbuka alijikuta akijikalisha kwenye godoro lake.
“Oh! .. wewe ndio ulieotoa tangazo la Ajira la kutafuta boyfriend feki eh?”Aliongea Hamza akiwa sio mwenye kuamini.
“Upo sahihi , je utapenda tuchati kwa meseji au tuongee kwa simu?”Sauti ile nyororo ilianza kumsisimua Hamza.
Katika maisha yake hio ilikuwa ndio mara ya kwanza kuamshwa na simu asubuhi na sauti ya mwanamke mwenye sauti nyororo namna hio , ilikuwa ni kama anaota na muda wowote angeshituka kutoka usingizini.
Ukweli ni kwamba licha ya jana kujaribu kuingia katika PM ya mwanachama huyo wa mtandao wa Jamii Forum hakuwa na uhakika kama anaweza kutafutwa yote hayo ni kutokana na kwamba hakuchukulia swala lenyewe kuwa siriasi kutokana na maoni ya watu , lakini pia asili ya Tangazo lenyewe kwani halikukaa sawa.
Maisha ya watanzania wengi yalikuwa ni ya kimasikini sana na uchumi ulikuwa ni mgumu mno na hata waajiri hawakuajili tena zaidi ya kupunguza wafanyakazi.
Hali hii haikuwa ya kawaida kwa mtu kuweka tangazo mtandaoni la kutafuta mchumba wa maigizo halafu kumlipa , ilikuwa ni swala la kichekesho na ambalo haliwezekani.
“Kwahio unasema kwamba tangazo lile lilikuwa siriasi na umeridhishwa na mimi ndio maana ukanipigia?”Aliuliza Hamza akiwa bado haamini huku akiangalia saa ya simu yake na kulaani kimoyo moyo kwani alikuwa amechelewa kuamka sana, ilikuwa ikikaribia saa moja na nusu na muda huo pengine angetakiwa kuwa kwenye gari kuelekea chuoni.
“Ndio maana nimekupigia Hamza , lakini ili kujua kama unafaa lazima nikuulize maswali kadhaa ndio nikupe muongozo wa kinachofuata”
“Unaweza kuendelea tafadhari?”Aliongea.
“Una ishi mkoa gani Hamza?”
“Naishi hapahapa Dar es salaam kama nilivyoelezea kwenye ujumbe wangu”Alijibu Hamza huku akitoa tabasamu , alijiambia lazima mwanamke huyo atakuwa ni mrembo kutokana na sauti yake.
“Vizuri , je una miaka mingapi?”
“Nina miaka ishirini na saba?”
“Okey! Hamza asante kwa kujibu maswali yote , hatua ya pili inayofuatia kama upo siriasi kufanya kazi ya kuwa boyfriend feki unapaswa kufika katika Dosam V hotel muda ni kesho saa nne asubuhi kwa ajili ya Usaili na kama utafanikiwa kupita basi utasaini mkataba wa ajira”
“Usaili!!, ?Unamaanisha nini kuhusu Usaili , kuna haja juu ya hilo?””
“Hamza nadhani ni utaratibu wa kawaida kufanyiwa Usaili na kama utafaa kivigezo basi utaweza kupewa ajira rasmi kama ilivyotangazwa”
“Aaa..!”
“Kumbuka Hamza ni siku ya kesho saa nne kamili asubuhi heshimu muda”Baada ya mwanamke huyo kuongea maneno hayo palepale simu ilikatwa na kumfanya Hamza kushikwa na bumbuwazi akisahau kwamba anachelewa kwenda chuoni.
******
Maisha ya ajabu ni nini na tunawezaje kuyatumia kufanikiwa?
Maisha ya ajabu ni neno ambalo lina urejeo wa mambo mengi , lakini kwa ujumla linamaanisha mambo ya kuvutia na kushangaza ambayo tunakutana nayo maishani, mambo ya ajabu kama hayo ni kama vile kuangalia maporomoko ya maji ya umbali mrefu , uzuri wa mtoto anapotabasamu na mengine mengi.
Maisha ya ajabu yanaweza kutusaidia kufanikiwa kwa njia nyingi ikiwemo , kutupatia hali ya mshangao na udadisi , kutusaidia kuthamini mambo madogo madogo , kutuhamasisha kuwa wabunifu , kutuunganisha na wengine pamoja na kutupa matumaini mapya.
Zipo njia kadha wa kadha ambazo zinaweza kutusaidia kutumia maisha yetu ambayo yamejazwa na uajabu ili kufanikiwa ikiwemo: kutengeneza orodha ya mambo ya ajabu ambayo ni ya kukushangaza na kukuvutia , jaribu kutafuta uzoefu mpya nje na eneo la faraja(Comfort Zone),Kuwa na shukrani na shirikisha uzoefu wako kwa wengine.
“Haya ndio maneno yangu kwenu ambayo ni kama Bonus Point kwenu , niwatakie siku njema , Mono no aware.
“Paaa.. Paaah!!!
Ilikuwa kama kawaida Hamza aliguswa sana na maneno ya Profesa Singano ukiachana na namna maneno hayo yalivyomwingia na kuyaelewa lakini kwa wakati mmoja ni kama yaligusia kile ambacho amekutana nacho asubuhi ya leo.
Hamza tokea anatoka mahali anapoishi kuja chuoni alikuwa akiikumbka mara mbilimbili kauli ya kuhitajika kwenda kwenye usaili kwa ajili ya kupewa kazi ya kuwa Boyfriend feki.
“Hakika maisha na maajabu yake , lakini leo Profesa maneno yake yamenifanya nichukue maamuzi , lazima kesho niende kwenye huo usaili nikajionee mwenyewe”Aliwaza Hamza.
“Oya Mzee unawaza nini? , huna mpango wa kuondoka nini?”Sauti ilisikika nyuma ya Hamza na kumfanya ageuke na kukutana uso kwa uso na Alex muuza vyungu.
“Hamna ndio najiandaa kutoka hivyo”
“Haha,, Hamza una mawazo mengi sana , kila siku ambayo Profesa akimaliza kipindi chake wewe unaishia kushangaa”
“Mara nyingi namchukulia Profesa kama mchungaji pale anapokuhubiria juu ya jambo la Dhambi ambalo unalifanya, kwa urahisi ni kama Profesa anayagusa sana maisha yangu kwa ujumla”Aliongea Hamza akiwa siriasi na kumfanya Alex kuangua kicheko.
“Unajua nini braza ,Profesa Singano naona muda mwingi anapoteza muda wake tu lakini hakuna cha maana anachoongea na hilo sio kwangu tu nakuhakikishia ni wachache sana ambao wanaguswa na maneno yake , wengine wote wanapenda kumuona anavyoongea ili kucheka basi lakini sio ujumbe”Aliongea Alex na kumfanya Hamza asiweze kuongeza neno.
“Sio kawida yako kunitafuta wakati wa kumaliza kipindi kama huu kwa ninavyokujua sasa hivi ungekuwa na kundi la warembo kwenye gari yako mnaondoka”Aliongea Hamza.
“Upo vizuri mtu wangu , nimekufuata kwasababu nina mishe nataka msaada wako”
“Mishe gani?”
“Ni kazi nyepesi sana yenye malipo mazuri”
“Okey , nipe mchongo”
“Iko hivi leo nina oda za kupeleka vyungu sehemu mbalimbali na wafanyakazi niliokuwa nao ni wachache na hawawezi kumudu oda zote..”
“Nipo tayari, nishakuelewa unachomaanisha , wewe zungumzia kiasi cha pesa ambacho utanilipa “
“Elfu ishirini unaonaje kwa trip moja”Aliongea Alex na Hamza macho yalichanua , aliona ni dili zuri.
“Kama upo siriasi mimi nipo tayari kwa ajili ya kazi”
“Ndio maana nakukubali Mzee , huna tabia za kulemba lemba kwa kuchagua kazi , sasa sikia muda wa jioni jioni saa kumi ndio utaanza , kuna mfanyakazi wangu nitampa namba yako atakupigia na utafika maeneo ya uzalishaji na kisha utachukua mzigo na atakupa na Anuani wapi unapaswa kupeleka”Aliongea na Hamza hakuona tatizo , alikuwa na uhitaji wa pesa na kama kuna mtu alikuwa tayari kumlipa kiasi kidogo cha pesa kwa malipo ya kawaida aliona hana haja ya kukataa dili hilo.
Baada ya kuachana na Alex Hamza yeye hakuona haja ya kwenda nyumbani mapema hivyo , chuoni kulikuwa na Wife ya bure hivyo kutokana na mara nyingi kutokuwa na bando la kuosha aliona atumie muda huo kukaa chuoni hapo kupakua muvi na kwenda kuangalia getoni kwake.
Comments