Reader Settings

SEHEMU YA 05.

Muda wa jioni  Hamza akiwa  chuoni aliweza kupokea  simu kutoka kwa  mtu aliejitambulisha  ni mfanyakazi wa  Alex na  Hamza mara baada ya kusikia utambulisho wake aliweza kumjua mara moja na palepale alipewa maagizo ambayo  Hamza alionekana  kuyaelewa   na kisha   simu ilikatwa.

Dakika chache tu alikuwa tayari ashapata  daladala ambayo  ilimpeleka moja kwa moja mpaka Mwenge  mahali ambapo ndio alielekezwa kushuka.

Kutokana na kuwa mzoefu aliweza kutoka kituoni na kuchukua upande wa kulia kwake  na  kueleka moja  kwa moja mpaka eneo  husika.

Hamza alijikuta akishangaa mara baada ya kugundua   kazi ya Alex haikuwa kazi ndogo , kwani   ilikuwa ni kama Kiwanda.

Jambo hilo lilimshangaza ,  watu walikuwa wakimchukulia Alex wa kawaida  kutokana na kazi yake , lakini Hamza mara baada ya kupita getini na kuingia ndani aligundua    ilikuwa ni zaidi ya alivyofikiria , kwani  kulikuwepo wafanyakazi wengi.

“Wewe ndio Hamza?”Aliuliza jamaa mmoja mwenye nywele ndeefu mara baada ya kumuona Hamza ana shangaa shangaa”

“Ndio Bro”

“Umefanya la maana  kuja haraka maana kidogo tu usingenikuta hapa , nina oda ya kupeleka , njoo nikuonyeshe Mzigo  chapu”Aliongea yule  bwana huku wakipita wamama ambao walikuwa bize kutengeneza  vyungu.

Kulikuwa na utengenezaji wa aina tofauti tofauti , kulikuwa na vyungu ambavyo vilikuwa maalumu kwa ajili ya kuwekea maua   na urembo mwingine ,  kitu kingine ambacho Hamza alikuja kugundua ni kwamba   kilichokuwa kikitengenezwa  hapo sio vyungu  tu.

“Bosi mzigo huu  hapa utaupeleka kwenye hii Anuani”Aliongea yule bwana  huku akimpatia Hamza boksi  ambalo juu lilikuwa na Sticker ambayo mzigo ulipaswa kupelekwa.

“Malipo yanakuwaje  baada ya hapa?”Aliuliza.

“Bosi  hajakuambia?”

“Hamna tumekubaliana ni 20k  ila hajaniambia utaratibu  wa kunilipa upoje?”

“Samahani mkuu,  iko hivi huu  mzigo bado haujalipiwa  ukishafikisha   utakaguliwa na baada ya hapo utalipiwa  bei yake ni laki moja na nusu na gharama ya usafirishaji utapewa hapo hapo”

“Laki moja na nusu!!?”Hamza alijikuta jicho likitoka na kujiuliza ni chungu cha aina gani ambacho kinauzwa laki moja na nusu

Yule bwana alijua mshangao wa Hamza lakini hakutaka kumtolea maelezo  yoyote   na alionekana kuwa na haraka kwani aliingia kwenye gari na kisha akaondoka.

Hamza alitaka kuuliza kuhusu nauli vipi , lakini alikuwa amechelewa na kuishia kuangalia boksi ambalo lipo chini  limefungwa kwa namna ya kipekee..

Alikuwa na shauku ya kujua ni chungu cha aina gani ambayo kinaweza kuwa na bei ghali namna hio   lakini asingeweza kufungua.

Baada ya kusoma Anuani ya mzigo unapopaswa kueleka aligundua ni Madale .

Hamza alijaribu kuchunguza mazingira yaliokuwepo hapo ndani na aliweza kugundua hakuna ambaye alikuwa akimwangalia , kulikuwa na vijana wengi pamoja na wamama  waliokuwa bize kuteneneza vyungu lakini hawakumwangalia usoni , ni kama hawakujali uwepo wake.

Hamza  alinyanyanyua lile boksi  na aliona halikuwa zito sana , alitamani kutafuta mfuko kulifunga lakini  ilikuwa  ngumu kuingia kwenye mfuko wa kawaida  labda   kwenye kiroba  lingefiti lakini  kiroba chenyewe hakuwa nacho hivyo aliamua kubeba hivyohivyo na kutoka   ndani ya eneo hilo na kwenda kusimama kituoni.

Kama kawaida watu wa jiji la Dar hawakuwa na habari na mtu  kila mtu  alikuwa bize na mambo yake na Hamza na yeye hakujali watu na kuendelea kusubiri usafiri.

Hamza wakati akiwa kituoni  hapo aliona ndio maana  Alex alimtajia pesa kubwa kwa ajili ya kusafirisha kwa awamu moja  kumbe  gharama ya chungu kimoja ilikuwa kubwa hivyo.

Dakika kadhaa tu akiwa amesimama kituoni gari iliweza kusimama na Hamza licha ya kuona gari hio ilikuwa imejaa  sana  aliingia moja kwa moja na kisha akaweka mzigo wake sehemu husika na kisha akasimama  na safari ikaanza.

Muda wa saa kumi  foleni ilikuwa kubwa mno kutokana na watu wengi ndio kwanza wanatoka kazini , hivyo ilimchukua dakika nyingi sana kusimama mpaka kufika eneo husika.

Jiji la Dar lilikuwa limeboresheka sana katika maswala ya anuani za nyumba , ilikuwa ukiingia mtandao kwenye  ramani  unaweza kuona kila nyumba  hivyo haikumpa  Hamza shida kutafuta nyumba  ya mzigo unapopaswa kufikishiwa.

Baada ya kushuka  katika kituo husika alianza kutembea kwa kufuatisha Ramani na  alitembea kwa dakika  kama kumi tu  alikuja kusimama kwenye  nyumba kubwa  iliokuwa na geti  rangi nyeusi ambalo lilikuwa limenakshiwa na  madini ya shaba.

Hamza aliangalia kulia na kushoto katika maeneo hayo na alionyesha kuridhika , ijapokuwa kulikuwa na nyumba za kawaida ndani ya hilo eneo lakini  nyumba nyingi zilionekana ni zile za kifahari  na zenye  bustani za kuvutia nje.

“Ngoo… ngooo , ngooo!!!”

Hamza aligonga  mara   tatu na kisha akasubiria   kwa dakika  nzima  lakini hakukuwa na  dalili yoyote ya kufunguliwa, na alijikuta akigonga tena  kwa dakika nyingine  lakini bado mlango  haujafunguliwa na  aliamua awamu hio kugonga kwa nguvu lakini kabla  hata  mkono wake haujagusana na geti kijimlango kidogo cha nyumba hio kilifunguliwa.

“Una shida gani?”

Sauti iliokuwa   ya kibabe  iliweza kusikika  na Hamza kwa ufahamu wake wa haraka haraka alijua mtu huyo atakuwa mlinzi  kwani hata rafudhi yake haikuwa  ile  ilionyooka katika kiswahili chake.

“Nimeleta Mzigo”Aliongea Hamza.

“Mzigo gani?”

“Chungu”

“Hapo pembeni yako unaona nini?”

“Pembeni wapi tena?”

“Kushoto kwako?”

“Sioni  kitu?”Aliongea  Hamza.

Ukweli ni kwamba  wakati alipofika hapo aliweza kuona kitufe cha kengele lakini hakutaka kukigusa  na aliamua kugonga geti na  mlinzi huyo alivyokuwa akimuuliza alikuwa akijua alichokuwa akimaanisha.

“Acha ushamba  basi , angalia pembeni yako hapo kuna  kengele na Camera , bonyeza hiyo  na kisha  utasema shida yako”Aliongea kwa hasira na kisha alifunga kijidilisha  na kumuacha Hamza kutoa tabasamu la uchungu

Hamza alijiamulia kubonyeza ile kengele mara mbili na palepale aliweza kusikia sauti kutoa ndani”

“Delivery!!”Aliongea

“Ok”

Sauti ya kike iliweza kusikika kutoka ndani   na  mara baada ya kusubiria kwa dakika kama  mbili hivi mlango wa geti ulifunguliwa.

“Kijana unaweza kuingia”Aliongea Mlinzi  na  sasa Hamza aliweza kumuona yule mlinzi.

Ijapokuwa sauti yake haikuwa imekaa vizuri  lakini kimuonekano alikuwa vizuri sana kuliko hata yeye  kwa upande wa mavazi.

Hamza mara baada ya kuingia ndani alijikuta akishangazwa na mandhari nzuri pamoja na ufahari wa jengo ambalo lilikuwa mbele yake.

Mlinzi alimuonyeshea ishara  Hamza kutembea kueleka upande wa kushoto  na Hamza mara baada ya kuangalia upande ambao anaelekezwa ni  kando ya  bwana la kuogelea sehemu ambayo imejengwa kwa ajili ya mapumziko.

Hamza kila hatua aliokuwa akipiga kueleka hilo eneo mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda  mno mpaka mwenyewe kujishangaa , ijapokuwa kiumbe alichokuwa akikiangalia mbele yake kilikuwa  kimempa mgongo lakini   utashi wake ulimwambia huyo mwanamke alikuwa mzuri  sio  kawaida.

Hamza alijiambia pengine  anachanganyikiwa sana kila anapowaona wanawake warembo kwasababu ni muda mrefu hajakutana na mwanamke kimwili.

Ilikuwa ni kama akili yake ilivyomwambia kwani mara baada ya kufika katika hilo eneo aliweza kukutana na mwanamke ambaye alikuwa nusu uchi , ilionekana kabisa alikuwa akiogelea kwenye hilo bwawa na muda huo  alikuwa amepumzika kwani hata mwili wake haukuwa umekauka maji.

Hamza kwa akili yae palepale alijua  huyo sio mtu ambaye alimwitikia  baada ya kubonyeza kitufe.

Hamza mara baada ya kufika mbele ya mwanamke yule akiwa ameshikilia boksi lake  mapigo yake ya moyo yalionekana kudunda sana.

Alikuwa  ni msichana mweupe mwembamba kiasi ambaye alikuwa na ngozi laini mno na nywele zake ndefu, alikuwa na macho madogo ambayo yaliendana na  namna uso wake ulivyoumbwa.

Ijapokuwa mrembo huyo hakuwa akimfikia yule msichana aliefahamika kwa jina la Tresha Noah ambaye alikutana nae kule kwenye  jengo la Apartment  la Dosam Homes lakini itoshe kusema  huyo alikuwa mrembo na wakuvutia zaidi.

Katika maisha ya Hamza alishakutana na wanawake wa aina nyingi , kuna wanawake ambao  alikutana nao licha ya kwamba walikuwa na uzuri wa aina yake lakini hawakuwa wakivutia kingono , kuna wanawake wengine ambao alikutana nao licha ya kwamba hawakuwa na muonekanno wa kirembo lakini walikuwa wakivutia mno kingono(Sexy), hizo ni aina mbili ambazo  alikutana nazo Hamza , ijapokuwa  mrembo huyo  hakuwa mzuri sana lakini alikuwa na  umbo ambalo linavutia kingono  sana, yaani  ni  aina ya wanawake ambao ukimuona tu  unawaza  kufanya mapenzi.

“You are Hamza right?”Aliuliza yule mwanamke  na sauti yake ilimuacha Hamza hoi.

“Yes.,.. yess”Alijibu kwa kubabaika.

“Okey  nimepewa taarifa zako  na Alex ,unaweza kufungua nithibitishe mzigo”Aliongea yule mwanamke , hakuwa na sura ya dharau   wala  ya ukarimu yaani alikuwa katikati huku akionekana  kumkagua Hamza.

Hamza  hicho ndio kitu pekee ambacho alikuwa akitaka kufanya , alikuwa na shauku ya kutaka kujua kwanini chungu hicho kilikuwa kikiuzwa pesa nyingi  sana kuliko uhalisia.

Ilimchukua dakika chache  sana kwa Hamza kufungua ndani , ijapokuwa kwa mtu wa kawaida angehitaji  kisu kukata hizo gundi lakini Hamza hakuhitaji kisu na  namna ambavyo alifungua ilimshangaza kudogo yule mwanadada  lakini  hakuongea chochote zaidi ya kubakia kimya.

Hamza mara baada ya kufungua lile boksi  macho yake  ni kama yamesaliti matarajio yake , ukiachana na namna  ufungashaji wa chungu hicho ulivyo lakini hakikuwa na muonekano ule wa  kimaajabu , kilikuwa chungu kama chungu ambacho  muonekano wake ulikuwa wa kawaida sana , vilikuwa vyungu kama vile vya  kitamaduni ambavyo wamama wengi  hupikia.

Jambo hili lilimfanya Hamza kushangaa na kujiuliza nini kinaendelea , alijaribu kuangalia  ndani yake  kwani mwanzo alijua pengine kuna madawa ya kulevya  kwenye hilo boksi lakini hakukuwa na kitu chochote  cha kushangaza zaidi ya chungu.

“Kaka , inaonekana hii ni mara yako ya kwanza kufanya Delivery”

“Kwanini?”

“Unashangaa sana”Aliongea yule msichana  huku akisimama na kumpokea  Hamza kile chungu na kuanza kukichunguza kwa dakika kadhaa na mara baada ya kuridhika alitoa tabasamu na kumpatia Hamza kukirudisha kwenye boksi.

“Wait here”

Aliongea  huku akibeba kile chungu na kutembea kuelekea upande mbele wa jengo  hilo sehemu ambayo kuna mlango wa kuingilia ndani.

Hamza macho yake yalikuwa yakiangalia  mpwito wa makalio ya mrembo huyo ambaye hakuwa akijali kama amevalia kijichupi tu  na kuingia  hadi ndani.

“Kuna watu  wanafaidi aisee”Alijiwazia   Hamza  mara baada ya mrembo yule kutokomea kwenye  jumba hilo ambalo lilikuwa na  ghorofa  mbili kwenda juu.

Hamza alitumia dakika hio kujaribu kukagua mazingira kwa haraka haraka  na ile anagueza sura yake macho yake yalikutana na mlinzi aliekuwa akimwangalia  na baada ya kukutanisha nae macho alionekana kama mtu ambaye alikuwa akimwangalia kwa macho yasiokuwa ya kawaida  na Hamza  alishindwa kuelewa lakini aliamua kupotezea na kugeuza macho yake sehemu nyingine.

Baada ya dakika  kama sita hivi  mwanamke yule alirudi   huku awamu hio akiwa   tofauti na alivyokuwa , alikuwa amejisitiri kwa kuvalia  vazi  refu  la  kitambaa cha hariri(Silk Duster) ambalo lilikuwa na vishikizo huku  kichwani akiwa  amevaa Bonnet.

Alikuwa hajalifunga vishikizo vyake na kumfanya  bado nguo yake  ya ndani kuonekana.

“Hesabu hizi?”Aliongea  yule mwanamke huku awamu hii akiweka tabasamu  na kumfanya Hamza kushangaa kidogo na kujiuliza mwanzoni hakuwa na mwonekano wa kusomeka lakini sasa hivi alikuwa akitabasamu.

Hamza alihesabu  kwa haraka sana zile hela   na  baada ya kumaliza aligundua ni  Shilingi laki moja na tisini.

“Hela iliozidi  ni kama ofa Hamza , naamini utakuwa mwaminifu kuniletea  mzigo wangu mwingine kila nitakapohitaji”Aliongea   huku akiweka tabasamu na kuufanya uzuri wake kuzidi kuongezeka.

“Asante sana”Aliongea Hamza , ijapokua  hakuelewa mwanamke huyo anamaanisha nini kumwambia  anategemea  kuletewa mzigo mwingine na yeye lakini  hakutaka kuuliza.

Hamza mara baada ya kuaga aliweza kutoka nje ya geti huku  bado akiwa na maswali mengi sana , swali lake kubwa ni kwanini chungu cha kawaida kama kile mwanamke huyo akakinunua kwa bei ghali,

Ilikuwa ni ajabu ambayo chungu cha  kawaida ambacho kilikuwa kikiuzwa sokoni  kwa shilingi elfu tatu kununuliwa   kwa  zaidi ya laki  mbili.

Hamza alijiambia hata kama watu hao ni matajiri  lakini bei hio ni kubwa sana kiasi kwamba haina uhalisia , akili yake palepale ilimwambia pengine  kuna kitu cha ziada kwenye kile chungu lakini hakujua, kwani kila kitu hakikumwingia akilini.

Ijapokuwa alikuwa akijua   madawa ya kulevya yalikuwa  yakisafirishwa kwa mbinu nyingi lakini ilikuwa ngumu madawa kusafirishwa kwenye kile chungu, lakini hata hivyo hivyo hakutaka kufikiria zaidi.

Wakati akianza kutembea kukisogelea kituo cha  daladala simu yake ilianza kuita  na alipoangalia jina la mpigaji  alikuwa ni Alex na palepale alipokea.

“Hahaha..  Bro kazi nzuri”Sauti ya Alex ilisikika bila hata ya salamu.

“Nimeleta mzigo tu sehemu husika , ni swala ambalo mtu yoyote anaweza kufanya”

“Hapana Bro , ni kweli linaweza kuonekana swala la kawaida lakini sio la kawaida  kama unavyoona wewe”

“Unamaanisha nini?”

“Tutaongea  usijali , ila  nikuambie mwanangu sijui  niseme una bahati au kuna siri  kuhusu inayoendelea ,ila  kwanzia sasa hivi  utahusika na kumpelekea huyo demu  kila atakapohitaji mzigo , amenipigia simu na kusema lazima iwe wewe”Aliongea Alex  na kumfanya Hamza kusimama kwanza.

“Alex  unajua  mambo mengi  umeniacha hewani ,  nina maswali mengi sana , itoshe kusema leo ni siku ambayo imenifanya kushangaa sana”

“Najua bro  lazima utakuwa  na maswali ila  utajua , kwasasa  elewa kwamba utakuwa unampelekea huyo  manzi  mzigo wake  na  malipo yatakuwa mazuri”Aliongea Alex na kumfanya Hamza kufikiria kidogo.

“Tunakutana wapi nikupe  hela ya  mzigo”

“Haina haja mzee unaweza  kwenda nayo, hio chukulia kama pesa ya kujikimu kwa  mwanzo wa kazi  yako”Aliongea na  palepale simu ilikatwa na kumfanya Hamza kuzidi kuchanganyikiwa

Kitu kingine kilichomfanya kuchanganyikiwa ni kama  Alex alikuwa akiongea kinafiki ila hakutaka kuwaza sana kuhusu Alex bali  aliwazia vyungu.

“Kuna siri gani   juu ya hivi vyungu..?”

Ndio swali ambalo liliibuka kwenye kichwa chake  na hali ya kutaka kuanza udadisi  ilimvaa palepale ,  Hamza alijikuta akitengeneza Scenerio mbalimbali kwenye kichwa chake kuhusu vyungu ambavyo anatengeneza Alex.

Ukweli ni kwamba hata yeye aliona kuna kitu ambacho sio cha kawaida tokea dakika ambayo aliingiza mguu katika kiwanda cha  Alex  cha utengenezaji vyungu.

Hamza alianza kufikiria  mbali zaidi na kujiambia hili swala halikuwa la kawaida tokea siku ambayo anaisikia   Alex alikuwa muuza vyungu , kulikuwa na wafanyabiashara wengi nchini ambao wanatengeneza vyungu iweje Alex biashara hio imtoe na kuwa na maisha mazuri namna hio.

Safari yake ya kupata majibu ni kama ndio imeanza rasmi ,  kwanza kabisa alishajua aina ya   vyungu ambavyo  vilikuwa vikitengenezwa  lakini pia alijua uthamani wa vyungu vingine , kilichokuwa kimebakia  ni kujua nini siri iliokuwemo kwenye  vyungu hivyo.

Swali  tu la kumshangaza Hamza ni  kwamba kwanini  maisha yake yamejaa mshangao tokea siku anajitambua.

******

Saa  kumi na mbili kamili za jioni Hamza alikuwa  eneo la Mwenge , ijapokuwa haikuwa mwisho wa safari yake lakini aliamua kushukia hapo huku akiwa na wazo moja akilini na hio yote ni kutokana na kuwa na pesa nyingi mfukoni.

Hamza mara baada ya  kushuka kituoni alivuka  barabara upande mwingine na kisha akaingia kwenye maduka ya nguo, alikuwa na wazo  la kununua  nguo kwa ajili ya kwenda kwenye usaili siku ya kesho.

Ijapokuwa  kwake ilikuwa kichekesho  kwenda kwenye usaili huo kutokana na aina ya kazi yenyewe lakini   hakutaka kudharau hata kidogo , kitendo cha kupigiwa simu asubuhi kilimwaminisha yoyote ambaye alituma lile tangazo  alikuwa siriasi , lakini  shauku yake nyingine ni kwamba kama mtu huyo alikuwa siriasi na  kuamua kumlipa mtu zaidi ya laki saba wa ajili ya magizo tu basi ilimaanisha kwamba   ni mwanamke mwenye pesa , lakini vilevile huenda kuna  sababu ya ziada.

Hamza  moja kwa moja aliingia kwenye  jengo la  Dosam Shopping Mall . hili  ni jengo ambalo alikuwa akitamani sana kuingia siku moja kwa ajili ya kununua nguo , lakini kutokana na kukosa pesa  kila siku alikuwa akiliogopa kama ukoma,lakini siku hio alikuwa na zaidi ya laki na nusu mfukoni hivyo aliamua kuzitumia katika  manunuzi ya nguo  kadhaa  na kisha baada ya hapo angeenda saluni kuweka muonekano wake vizuri.

Sifa kubwa ya maduka  ya Dosam ambayo yametapakaa nchi nzima ni  nguo zake kuwa bora lakini kwa bei nafuu kabisa , ilikuwa ni tofati  kabisa na madumka ambayo yalikuuwa yakipantikana mlimani City  na kwingineko.

Kwa mfano Mlimani unaweza kukuta nguo inauzwa bei lakini ubora wake ukafanana na nguo ambayo inauzwa katika maduka ya Dosam,  na inasemekana tokea kampuni ya Dosam kufungua maduka ya nguo biashara nyingi zimefirisika sana   kutokana na mauzo kupungua.

Sifa nyingine katika maduka  haya ni huduma ya viwango vya  juu sana , yaani  hawakujali muonekano wa mteja ambaye alikuwa akifika kufanya manunuzi katika maduka yao,  wao walimjali kila aina ya  mteja   na kuwakwa  daraja sawa  na muda wote walikuwa ni  watu wenye tabasamu usoni  na wangekusaidia katika machaguzi ya nguo mpaka pale utakaporidhika.

Jambo hili lilimfanya Hamza  kukubali sana mmiliki wa kampuni ya Dosam Global,

Ukweli ni kwamba  inasemekana kampuni ya Dosam mmiliki wake ni mwanamke   tena  pengine ni kosa kusema mwanamke bali   ikawa sahihi kusema ni Msichana ndio mmiliki.

Mwanzoni kampuni hii ilimilikiwa na Mzee Lasuli Dosam mwenywe na mara baada ya kufariki inasemekana  usimamizi na urithi wa  makampuni yote ulienda kwa  mjukuu  wake kike.

Uzushi unaenda mbali zaidi na kusema kwamba  msichana huyo  ambaye ni mmiliki alikuwa ni mrembo haswa , pengine zaidi ya neno lenyewe la Urembo  lakini  pia kwa wakati mmoja alionekana kuwa ni  mwenye akili nyingi , baadhi ya watu walikuwa wakimtaja kama kiumbe kutoka sayari nyingine.

Jina hilo liliibka kutokana na kwamba aliweza kufanya biashara nyingi katika mataifa mbalimbali kupata hasara kubwa kutokana na mbinu zake za kibiashara tokea kupewa uongozi wa kampuni , vyombo  mbalimbali vya habari vishawahi kumwandika  kuhusu   mwanamke  huyo.

Hamza yote hayo alikuwa akiyajua , isitoshe alikuwa ni mtu  mpenda  mitandao ya kijamii hivyo ilikuwa ni rahisi kwake kukutana na taarifa ambazo zinamzungumzia , ukweli ni kwamba kukutana na taarifa hizo kwenye mitandao  sio jambo la bahati mbaya , ukweli ni kwamba  kuna taarufa zake nyingi , kwa mfano tu  katika mtandao wa kijamii wa JamiiForum  umejaa mada zinazomzunguzia mmiliki wa kampuni ya Dosam Global mara  mia nne tokea kupewa uongozi , sio hivyo tu majarida makubwa  duniani na yenywe yamemzungumzia mara nyingi sana  na kufanya mahojiano nae.

Ajabu ni kwamba  katika kila mahojiano ambayo yalifanyika inasemekana mwanamke huyo alikataa kupigwa picha.

Kuna wengine wanasema  mrembo huyo alikuwa mbaya wa sura ndio maana hakutaka kuonekana lakini wale ambao wameenda kumfanyia  mahojiano walisema alikuwa mrembo wa sura  na hata wale ambao walikuwa wakifanya kazi katika kampuni hio walikuwa wakisema ni mrembo wa sura.

Hamza alijikuta akiwaza kila aina ya mada ambazo alizisoma mtandaoni  kuhusu  mmiliki wa kampuni ya Dosam  na kilichomfanya kukumbuka  taarifa hizo ni siku hio mara baada ya kuingia kwenye duka hilo.

“Kaka hii  itakufaa sana , kwanza kabisa inaendana  na mwonekano wako wa mwili  kwanzia rangi yako  mpaka urefu na unene wako ,  kitu kimoja ambacho kitakufanya upendeze zaidi ni kunyoa  nwele kwa mtindo  huu”Aliongea mwanamke mrembo sana   huku akimuonyesha Hamza vazi maalumu ambalo amechagua.

Hamza aliweza kushika  kishikwambi  huku akiangalia mtindo wa nywele ambao mfanyakazi wa  eneo hilo amependekeza  na aliishia kutoa tabasamu.

“Sijazoea kunyoa hivi  dada”AliuongeaHamza.

Mtindo  wa nywele ambao aliokuwa akiangalia kwake ni kama haukukaa kimaadili, pengine sio kwamba mtindo wenyewe haukukaa kimadili lakini kutokana na sheria zake  au pengine   aina ya maisha aliokulia  ndio maana aliona ni mtindo ambao  haukukaa kimaadili.

Ilikuwa ni kama vile   wale wazee waliozaliwa miaka ya  sitini na sabini  uwaambie wanyoe kiduku ukweli ni kwamba hawatokuelewa, lakini sasa kidogo ilishangaza kwa Hamza kwani alionekana ni kijana  kabisa ambaye hata miaka therathini hajafikisha.

Yule mfanyakazi wa kike mrembo aliishia  kushangaa kidogo lakini aliubadilisha mshangao wake na tabasamu.

“Kaka niamini  , huu  ni mtindo ambao utamfanya mwanamke  yoyote  yule kukupenda , kwanza wewe ni handsome na kwa muonekano wako ni kama vile  Justin Timberlake,  hivyo staili yako ya nwele inakupasa kufanana…..”

Hamza  kwa namna  ambavyo mwanamke huyu alivyokuwa akiongea ungeweza kuamini na kujisikia vizuri lakini kilichomfanya kutokuamini maneno yake ni kwamba pembeni yake kulikuwa na bwana ambaye  alikuwa ni mweusi sana na kichwa kama kibuyu  aliekuwa pia akihudumiwa , ukweli katika maisha yake hakupenda kujifanananisha lakini alisema ijapokuwa yeye hakuwa akijiona Handsome lakini  huyo bwana  aliekuwa pembeni yake alikuwa  na sura ngumu mno, ndio mwanaume hasifiwi  kuwa na sura nzuri lakini  kilichompa mshangao ni namna ambavyo  mfanyakazi alivyokuwa akimpamba kwa kumwambia alikuwa na sura nzuri na kichwa kizuri, hivyo ilikuwa ni ‘redflag’ ya kuona hata yeye alikuwa akipambwa tu kinafiki  nje  ya uhalisia wa muonekano wake.

Iliimchukua kama nusu saa kuhudumiwa   na kisha alipewa nguo zake na kutoka, alikuwa amenunua  suruali mpya , Jeans pamoja na  viatu  na ajabu  ni kwamba hakuwa amelipa pesa nyingi,  kilichokuwa  kimebakia ni  kwenda Saluni na kuweka   nywele zake sawa kwa ajili   ya maandalizi ya kesho.

Hamza wakati akitoka kwenye Lift alijikuta akijichekea , yaani kwa namna ambavyo alikuwa akijiandaa ni kama vile anakwenda kukutana na mchumba au anaenda kwenye ‘Blind date’,   alicheka kutokana na kwamba  siku kadhaa zilizopita wakati wa kumtongoza mwanamke mrembo kama Anitha hakujali kabisa muonekano wake zaidi ya hisia zake, tena anakumbuka ile siku shati lake lilikuwa limechafuliwa na juisi  ya matunda wakati akiwa kwenye daladala na kutengeneza doa..

Hamza alitamani kughairisha   kwenda saluni lakini kuna  roho ilikuwa ikimwambia ‘ingia saluni bro upendeze acha uchafu’, pengine  mwanamke  unaekwenda kukutana nae ni zaidi ya Anitha.

Hamza mwenyewe alishangaa na kujiuliza hio sauti inatoka wapi , lakini aliamua  kuitii na kujiambia pengine  ni roho mtakatifu , lakini mara baada ya kuingiwa na neno  Roho mtakafitu alipotezea na kujiambia   kwanza hakuelewa yeye   ni dini gani  hivyo aliamua kupotezea  kile anachofikiria na kuamua kufuata utashi wake unakomwelekeza.

“Bro  unanyoa staili gani?”Aliuliza kinyozi mara baada ya  Hamza kukalishwa kwenye kiti  na kinyozi kumaliza maandalizi yake.

Hamza alifikiria ni staili gani anyoe , au apige  para..”Alijikuta akikosa majibu  na palepale macho yake yalitua  kwenye picha ambazo zilikuwa na  vichwa ambavyo vimenyolewa kwa staili tofauti tofauti.

Baada ya kuangalia ni staili gani ingemfaaa palepale alijikuta akiishia kwenye  staili ambayo alionyeshwa  muda mchache uliopita  na   yule muuza nguo,.

“Bro hio staili ni nzuri  na inaendana na nywele zako  lakini kidogo itakugharimu, kwani ili upendeze utahitajika na kuosha pia  na kupakwa dawa”Aliongea kinyozi akiwa na wasiwasi Hamza asingeweza kumdumu  bei.

“Ni shilingi ngapi  jumla?”

“Kwa kila kitu nilichokutajia   jumla yake ni  elfu  kumi na tano tu?”Aliongea .

“Ni bei kubwa ndio ila nitalipia”Aliongea Hamza na yule bwana alimwangalia kidogo na kisha akaanza kupiga kazi,

Hamza  hakuwa mwafrika orijinal bali alikuwa ni chotara , mchanganyiko wa Mwafrika na mzungu hivyo nywele zake zilikuwa zimekaa kizungu pia japo rangi yake ilikuwa imefubaa kidogo  kupoteza ile  hali ya  uzungu  yaani kwa maneno marahisi ni kwamba uzungu wake umeathiriwa na  rangi   ya kiafrika.

Zilipita dakika chache tu kama nusu saa hivi kinyozi alikuwa ashamaliza kumuweka Hamza sawa upande  wa nwele na alitakiwa kuweka dawa pamoja na kuoshwa  na kukaushwa  na  hakuwa na hiyana kufuata maelekezo kutokana na kwamba ndio   mwenyewe aliamua kuyavulia maji  nguo hivyo hakuwa na   budi kuyaoga.

Baada ya    lisaa lizima   aliweza kusafishwa  vizuri  na alipewa na ofa ya kusafishewa uso na Scrub .

“Edmund  naelekea nyumbani , bado  hujamaliza tu?”Sauti  ya kike iliweza kusikika katika Saluni ambayo  Hamza  anapunguza nywele.

“Leila nisuburi   kuna  bwana anamalizia kukaushwa  nataka nione kama hana kasoro  tuondoke”Aliongea  kijana huyo na kumfanya Leila kuvuta pumzi na kisha kwenda kukaa kwenye sofa.

“Zamu yako ishaisha , leo  mapema sana mpenzi”Aliongea Edmund.

“Bosi  katoa maagizo kila mfanyakazi anaefikia malengo ya mauzo kwa siku anaweza kuondoka hata kama ni mchana”Alijibu   na kumfanya Edmund  kutingisha kichwa huku akichomoa  simu yake chaji.

Dakika ileile  mlango wa chumba cha  wanaooshwa kwenye saluni hio  kilifunguliwa  na Hamza aliweza kutoka akiwa  anawaka hatari na kumfanya yule mdada aliekuwa ameketi kwenye Sofa kupigwa  na mshangao.

“Kaka  nilikuambia hio staili ya nywele itakufaa , jamani  hebu muone alivyopendeza”

Msichana Leila alikuwa ndio aliemhudumia Hamza katika  kununua mavazi  na  aliweza kumtambua Hamza mara baada ya kumuona.

“Leila unamjua?”

“Yeah mimi ndio nilimuelekeza kuja hapa”Aliongea huku akimwangalia Hamza kwa macho ya kurembua  na kumfanya Edmund  kuona wivu.

Ukweli hata Hamza mara baada ya kujiangalia kwenye kioo alijiona kabisa amebadilika , ijapokuwa bado alikuwa na mavazi yake yaleyale lakini aliamini kama atavaa alionunua  basi atakuwa ni mtu mwingine kabisa, aliishia kutoa tabasamu  kwa kujikubali na kujiambia yeye  kumbe ni  Hamdsome aliekosea matunzo.

“Bro  naona umekaa  sawa sasa , unaweza kulipa sasa , nilikuwa nikikusubiria wewe tu”Aliongea Edmund huku akimkatisha Hamza ambaye alikuwa akijiangalia kwenye kioo pasipo ya kuridhika.

“Okey  ngoja nilipe”Aliongea na palepale aliingiza mkono mfukoni na kutoa pesa  nyekundu mbili na kisha kumpatia”

“Sister  asante kwa kupendekeza hii staili ya kunyoa ,  chenchi inayobakia  ni shukrani  yangu kwako”Aliongea Hamza huku akitoa tabasamu na palepale alimkonyeza Leila  na kuchukua  mifuko yake na kutoka.

“Broo….!!”Edmund alitaka kuongea neno lakini  palepale Leila aliekuwa  akimwangalia Hamza kwa macho ya  kurembua alimpa ishara ya kufunga mdomo wake.

Siku iliofuata Hamza hakuwa na ratiba za chuo  kabisa  mpaka  jumatatu, yaani siku hio ilikuwa ni  Ijumaa na kwa kozi aliokuwa akisomea ni kama wikiendi ndio imeanza rasmi.

Usiku  hakuwa amelala kabisa , alikuwa  na mawazo mengii, kwanza aliwaza sana kuhusu mtu anaefahamika kwa jina la Mzee mtu ambaye hakuwa akimjua licha ya kwamba amehusika katika maisha yake kwa kiasi kikubwa , aliwaza namna ya  kumfahamu Mzee  ni nani  na kwanini alikuwa akimtafuta nyakati za usiku , aliwaza mambo mengi  kuhusu mzee na kujijengea picha katika akili yake na kujiambia pengine Mzee ni mtu mzito serikalini .

Mawazo ya  namna hio yalimjia kutokana na maisha ambayo amekulia  kulingana na maagizo  ambayo Mzee alitaka  awe.

Yaani kwa maneno marahisi ni kwamba mpaka wakati huo Hamza hakuwa ameyaishi maisha yake , ni kama maisha aliokuwa akiishi  ni kwa ajili ya Mzee kwani ndio aliekuwa akimwambia afanye hivi na vile na yeye kutii.

Alikumbuka    siku ambayo hakutii maagizo ya Mzee na kilichomkuta mpaka siku hio na  umri wake huo  hajawahi kusahau , sasa  kutokana na tukio  hilo ambalo lilimtokea ilimfanya  kuamini pengine   mzee ni mtu mkubwa sana serikalini , ukweli ni kwamba alikuwa na mawazo mengi kuhusu Mzee.

“Kama mzee hataki kujitokeza kwangu mimi nitajitokeza mbele yake uwezo huo ninao”

Aliongea Hamza  baada ya kuwaza  , alionekana ameamua  mwenyewe katika kichwa chake   na kujiambia kama  mtu huyo anaemtambua kwa jina  moja tu la Mzee asipojitokeza kwake basi yeye atajitokeza kwake ,. Hakujua ni kwa namna gani ambavyo angemfahamu Mzee lakini alijiambia   kutokana na uwezo wake basi lazima amfahamu mzee .

Hamza hakuwaza tu kuhusu Mzee pia aliwaza kazi ya Alex ya utengenezaji  vyungu namna ambavyo ilionekana kumtajirisha  nje ya uhalisia wa biashara wenyewe , alikuwa  na   shauku ya kutaka  kujua kilichopo  nyuma ya vyungu vile ni  nini, kuna hali ilikuwa ikimwambia pengine ni njia nyingine ya usafirishaji madawa lakini alipingana na mawazo yake na  akili yake ilimwambia kabisa pengine ni kitu kingine kabisa ambacho hajawahi kukifikiria kwenye maisha yake, kutokana  na mawazo mengi alijiambia pia hilo ni swala ambalo atalitafutia ukweli.

Baada ya kuoga vizuri na kujiandaa  kwa kuvaa mavazi yake mapya na viatu, licha ya kwamba hakuwa na kioo lakini aliamini alikuwa amependeza haswa.

Usaili kwa maelekezo ya mwanamke kwenye simu alimwambia ni  saa nne  asubuhi katika hoteli ya Dosam V

Hamza alikuwa akijua hoteli hio vizuri kwani ilikuwa ni  hoteli  maarufu  na yenye jengo refu kwenda  juu ndani ya jiji lote la Dar es salaam , pengine asilimia hamsini ya watanzania wote walikuwa wakiijua hoteli hio kwani matamasha mengi hufanyikia hapo,  hata vikao vya  waandishi wa habari hufanyikia ndani ya  hoteli hio.

Siku hio  pengine ndio inakuwa mara yake  ya kwanza kuingia katika hio  hoteli,lakini licha ya hivyo hakuonekana na wasiwasi kabisa.

Hakutaka hata kujihangaisha na maswala ya nchi asubuhi hio na alijiambia atajua mbele kwa mbele.

Mara baada ya kutoka nje ya   eneo hilo la uswahilini wanawake  na wanaume walikuwa wakimkodolea  macho kwa mshangao mkubwa.

Ukweli ni kwamba muoenknao wa Hamza  ulikuwa   hauendani  kabisa na maeneo   hayo ya uswahilini , kitendo cha kuchanganya rangi ya mzungu na mwafrika  ilikua  ni kama sababu kubwa ya kumuona Hamza sio wa kawaida.

Hata asubuhi hio  watu wengi   sio kama walikuwa wakimwangalia kutokana na kupendeza kwake bali ni kwamba walikuwa wakimwangalia huku wakijiambia moyoni Hamza  amerudi katika uhalisia wake na maisha ambayo alikuwa akiyaishi  hapo na familia hizo ni ya magizo tu.

“Niliwaambia mimi ,  hakuna mtu mzungu akawa masikini hivi”Aliongea mmoja ya viijana walioamkia kucheza pooltable.

“Juma uko sahihi , hata mimi kwasasa nakuunga mkono , jamaa hakuwa mwenzetu kabisa, ule upole wake ulikuwa ukificha mambo mengi”Alichangia mwingine. Na stori juu ya Hamza hazikuishia kwa  wacheza pooltable tu  hata wanawake waliokuwa wakiuza vitafunwa  nje ya vibaraza vya nyumba zao walikuwa wakimzungumzia Hamza.

Hamza  kutokana na watu wengi kumshangaa  kwake ilitosha kumwambia kwamba alikuwa amependeza.

Naam  ni saa tatu  na nusu Hamza aliweza kufika kandokando ya bahari ya Hindi  nje ya geti la kuingilia katika hoteli ya Dosam.

Tofauti  ya Hamza na wageni ambao walikuwa wakiingia ndani ya hoteli hio ni kwamba yeye alishuka na basi la  mwendokasi lakini wageni wengine wote aidha walifika wakiwa kwenye gari binafsi au  waliletwa hapo na Uber , Bolt na magari mengine yanayofanya huduma ya Taxing,

Licha ya hivyo  swala hilo halikumpa unyonge sana Hamza ,  pengine kwa watu waliokuwa wakimwangalia wangesema labda Hamza alikuwa amejipa uzoefu mwingine  wa kupanda magari ya  abiria.

Mwonekano wake ulimbeba,alikuwa ni mtanashati mno, Hamza alikuwa ni  mwanaume mrefu kwenda hewani , mwenye mwili ambao umejengeka kimazoezi  akiwa na weupe wa kuchanganya rangi na macho yake ambayo  yana kiini ambacho hakikuwa cheusi sana kama waafrika wengi , pengine  uzungu wake  ulionekana zaidi machoni kuliko sehemu yoyote ya mwili lakini hata hivyo ilikuwa kosa kumuita Mzungu.

Katika mavazi yake aliovaa kitu pekee alichokosa ilikuwa ni saa tu mkononi  , pengine ingemfanya kuonekana Handsome zaidi lakini hata hivyo  bado alionekana kupendeza.

Hamza alitembea kwa kujiamini kana kwamba alikuwa ni mzoefu kabisa wa eneo hilo.

“Ni muda mrefu sana nimejitenga na   maeneo ya namna hii , nadhani ni mwanzo wa  mimi kurudi kwenye maisha yangu”Alijiwazia Hamza huku  akiongea kauli  ambayo kidogo  inachanganya.

“Hello!, nina miadi na mtu ndani ya hii hoteli?”Aliongea Hamza mara baada ya kufika katika Front desk.

“Karibu sana kaka   , nitajie  jina la mgeni unaetaka  kukutana katika hoteli yetu  tafadhari”Aliongea yule mwanadada na kumfanya Hamza kuwaza kidogo  , ukweli ni kwamba hakuwa akijua jina lake kamili na   aliambiwa tu kufika  ndani ya hoteli hio muda wa saa nne.

Wakati akijiuliza   ni jina gani anapaswa  kutaja palepale simu yake ilianza kuita  na aliitoa haraka haraka  na kuangalia  jina la mpigaji na alitoa tabasmau na kumwangalia yule  mrembo  wa mapokezi akimpa ishara  kwamba anapiga.

Hamza aligeukia upande mwingine ili kuongea na simu  lakini   macho yake yalitua  kwa mwanamke mrembo sana ambaye alikuwa akisogea  katika  dawati  la eneo la mapokezi.

“Hello  Mr , uko wapi unakumbuka  miadi ni saa nne kamili?”Sauti ilisikika upande wa pili lakini wakati huo macho ya Hamza yalikuwa kwa mwanamke aliekuwa akitembea kimadaha kusogelea upande wake.

“Nipo eneo la mapokezi ndani ya hoteli ya Dosam”Aliongea  Hamza na palepale yule mwanamke alisimama  huku akitoa simu yake sikioni na kuangalia  mbele yake na  palepale alionekana kugundua kitu na haikuwa kwake tu hata kwa Hamza mwenyewe alionekana kugundua mtu aliekuwa akiongea nae kwa simu ni mwanamke aliekuwa mbele yake.

Sasa tofatui ni kwamba Hamza mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda mno  kutokana na kushangaa urembo wa mwanamke ambaye alikuwa akimsogelea huku akiwa na uso uliopambwa tabasamu.

Hamza  ni kama hakuamini kama  huyo ndio mwanamke ambaye alikuwa akienda kuonana nae.

Kuhusu yule mwanamke hakuonyesha mshangao wowote wa Hamza , yaani  ni kama Hamza alionekana wa kawaida sana na mara baada ya kumfikia alinyoosha mkono  kwa ishara ya kusalimia.

 

Previoua Next