Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

FOR YOU

Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa 

R-rated 18+


★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA TANO

★★★★★★★★★★★★★★★★


MWANZA


Safari ya haraka kwa kutumia magari mawili maalum ya kijeshi yaliyokuwa na chuma ngumu iliwafikisha ndani ya mkoa huo ambao mwanaume huyo waliyekuwa wakimfatilia alikuwa. Luteni Michael aliambatana na ACP Nora, Mario, Hussein, Alex na Mishashi ili kumkamata mwanaume yule, huku wachache wa timu yake Luteni wakibaki kule walikotoka. Mishashi alikuwa mwanajeshi mahiri mwenye ustadi katika suala la kutungua watu kwa silaha za shabaha ya mbali (sniper), hivyo wakati ambao wangefika eneo ambalo walijua mwanaume yule alikuwa, walimhitaji Mishashi awe sehemu za pembeni akiwa chonjo kuangalia kama kulikuwa na maadui wengine pia. 

Basi, ikiwa ni mida ya jioni, Luteni Michael na wenzake wakawa wamefika eneo moja lililokuwa na soko kubwa kiasi la biashara. Mario na Hussein ndiyo kati ya wale wanajeshi ambao angalau walijua kuongea kwa uchangamfu, na mara kadhaa walitania kuhusu kuondoka na samaki nyingi baada ya kumkamata mhalifu wao. Kwa kuongozwa na Bobby kwa vifaa maalumu masikioni, waliweza kumwona mwanaume huyo, Kevin Dass, akiwa eneo hilo la soko, lakini siyo kama vile akitaka kununua kitu chochote, bali alikuwa akitembea tu kuelekea upande mwingine uliokuwa na barabara ya lami. 

Wanajeshi hawa na ACP Nora walikuwa wamevalia kwa njia ya kawaida tu ili wasitambulike kirahisi kuepuka kushtua mtu yeyote, kwa hiyo wakawa wanamfatilia kwa umakini. Waliokuwa nyuma yake kwa umbali mfupi ilikuwa ni Mario, Hussein na Alex, huku Luteni Michael, ACP Nora na Mishashi wakiwa pande zingine lakini siyo mbali sana na hapo. 

Kupitia kifaa cha masikioni Mishashi aliwajulisha wenzake kwamba haikuonekana kama kuna nuksi za pembeni eneo hilo, kwamba Kevin Dass alikuwa peke yake kabisa, hivyo Luteni Michael akawaamuru wanaume hao wamfate tu Kevin na kumshika, kisha kumpeleka kwenye moja ya gari zao. Lakini wakati Mario, Hussein na Alex walipokuwa wameanza tu kumwelekea moja kwa moja, Kevin Dass akaanza kutembea kwa kasi sana kama vile anajaribu kuwaepuka. Mario akamjulisha Luteni Michael kwamba inaonekana Kevin alikuwa ametambua anafatiliwa na hivyo alikuwa akijaribu kuwaponyoka. 

Ghafla jamaa huyo akaanza kukimbia kwa kasi kabisa! Ilibidi Mario, Hussein na Alex walianzishe na wenyewe, wakipamiana na watu wengi njiani eneo hilo. Mishashi alikuwa anamwambia Luteni Michael kwamba aliona kule Kevin Dass alipokuwa anaelekea, na ni upande huo huo ambao yeye Luteni Michael alikuwepo.

Kevin Dass akafika sehemu ya barabara ya lami ambayo magari yalipita kwa kasi sana, naye alitaka kuvuka. Kivuko kilichokuwepo kwa mbele ilikuwa ni kama daraja dogo kutokea pande moja ya barabara kufikia nyingine, kilichokuwa kama na ngazi ndefu kuelekea juu kisha zinashukia upande mwingine wa barabara hiyo. Akazielekea upesi na kuanza kupanda, huku nyuma wanajeshi wale watatu wakiendelea kumfukuzia sana, na watu wengi wakishangaa kuona jambo hilo. 

Kevin Dass alipofika sehemu ya juu ya kivuko hicho, akasita na kusimama baada ya kuona watu wengine wawili wakiwa wanamfata pia, mmoja akiwa ni Luteni Michael na mwingine ACP Nora mwenyewe. Akabaki kutaharuki asijue aende wapi, na ile amegeuka nyuma akawaona wale watatu wakiwa wamefika nyuma yake. Akawa anababaika kwa kukosa sehemu ya kukimbilia huku akiwa amejishika sikio la kushoto, kisha akaona kuruka kutokea juu hapo mpaka kule chini ndiyo lingekuwa suluhisho ili aendelee kuwakimbia. 

Lakini wanajeshi hawa na ACP Nora hawakujisumbua kumkimbiza tena na kubaki kumwangalia tu, na ile aliporuka kule chini na kujitahidi kusimama, akapigwa na chuma ya bunduki nyuma ya kichwa chake na kufanya adondoke chini na kupoteza fahamu. Aliyekuwa hapo chini na kumpiga hivyo ni Mishashi, ambaye tayari alikuwa amefika mapema. Watu eneo hilo walikusanyika haswa wakishuhudia mambo hayo. Luteni Michael na wenzake wakashuka kutoka huko juu na kumnyanyua mwanaume huyu, kisha wakampeleka kwenye gari lao moja na kumfunga kwa pingu mikononi na miguuni, nao wakayaondoa magari yao maeneo hayo. Waliacha gumzo kubwa sana mitaa ile. 

Luteni Michael akawaambia wengine kwamba walipaswa kumhoji kwanza mwanaume huyu kabla ya kumpeleka mkoani kwao kule, kwa sababu huenda hata na wenzake walikuwa huku. Akasema sehemu ya kumpeleka aliijua, kwamba ingekuwa kwenye nyumba fulani ndogo tu iliyoachwa maeneo ya huko huko walikotoka muda mfupi nyuma, kwa hiyo hapa walikuwa tu wanafanya kama kuzunguka ili kuondoa kelele za watu wengi. 


★★


Walitoka kwenye lami na kutumia barabara za ndani-ndani ambazo zilikuwa na mawe-mawe mengi, lakini kwa sababu gari zao zilikuwa imara waliweza kufika pale Luteni Michael alipodhamiria. Bado Kevin Dass hakuwa ameamka mpaka walipoifikia hiyo nyumba, hivyo Alex, Mario na Hussein wakambeba na kumwingiza kwenye nyumba hiyo. 

Ilikuwa pana kiasi, lakini ndani yake hakukuwa na vitu vingi zaidi ya mbao chakavu, viti vya chuma vyenye vumbi na kinara cha mbao kwa ajili ya masuala ya hotuba. Wakachukua kiti kimoja na kumkalisha jamaa hapo, kisha wakafungua pingu zake mikononi, wakairudisha mikono yake kwa nyuma na kumfunga tena kwa pingu. Alikuwa bado kapoteza fahamu, na giza lilikuwa limeshaingia.

Alex akawasha taa iliyokuwa hapo ndani, nayo ikawaka.

"Mh... nani analipia umeme kwenye hii nyumba?" akauliza Mario.

"Haijaachwa muda mrefu sana," akajibu Luteni Michael.

"Ulipajuaje hapa?" akauliza ACP Nora.

"Kuna... rafiki ambaye alikuwa anafanya ibada ya kidini na wenzake hapa," akajibu Luteni Michael.

"Dah! Nyumba ndogo kishenzi, walikuwa wanatoshaje humu?" akauliza Hussein.

"Hawakuwa wengi kihivyo," akasema Luteni Michael.

"Mungu yupo popote, haijalishi ni jumba kubwa, dogo, au jalalani. Point ni kwamba aabudiwe," akasema Mario.

"Wewee... fala gani atakubali awekewe na kula chakula kwenye sahani iliyotoka chooni eti kwa sababu tu ni chakula?" akauliza Hussein.

"Kwo' Mungu ni fala?" akauliza Mario.

Nora akacheka kidogo. 

Luteni Michael alikuwa anamtazama kwa makini Kevin Dass. Mishashi yeye alikuwa anapitia kwa makini vitu kadhaa ambavyo vilikuwa ndani ya wallet ya Kevin Dass.

"Vipi ACP, na wewe huwa unaenda kuabudu?" Hussein akamuuliza Nora.

"Ndiyo. Lakini nina muda mrefu kidogo sijakanyaga kanisani," Nora akajibu.

"Mimi hata sijui kama bado yule jamaa waliyemtundika pale juu bado yupo! Hivi hachokagi tu kukaa namna ile?" Hussein akatania.

"Pumbavu, we' si mwislamu wewe!" akasema Mario.

Hussein akacheka.

"Kwa nini uliacha kwenda?" Alex akamuuliza Nora.

"Oh... mambo mengi tu," Nora akajibu kwa ufupi.

"Me mwenyewe nilishindwaga kuendelea kwenda aisee. Kwa dini yetu niliona ni kama maigizo tu every weekend. Simama, kaa, piga magoti, kaa, simama, simama, kaa, magoti, magoti, kaa, simama... ahahahah..." akasema Mario kiutani.

"Na wanachoangalia siku hizi ni money tu... bila hiyo ufalme wa juu huupati," akasema Alex.

"Ahahahah... vipi Luteni, wewe na Mungu bado zinapanda fresh?" Hussein akamuuliza Michael.

"Siku akinipa sababu muhimu ni kwa nini anataka tumpende halafu anawachoma watu moto, ndiyo zitapanda fresh," akasema Luteni Michael.

"Dah Luteni! Mbinguni hufiki wewe!" akasema Hussein.

Wote wakacheka.

"Kwa hiyo tunakaa kumsubiri huyu bwege aamke, ama?" Mishashi akauliza.

"Una haraka kwani? Kuna msosi tumebeba kwenye gari, kama vipi tupige kwanza kabla hajajiunga nasi," Mario akasema.

"Kweli idea nzuri. Halafu tukimaliza tukazurure jijini na kuogelea ziwani, au siyo?" akasema Mishashi kwa kejeli.

"Aagh... usiwe na presha bwana. Sa'hivi tuna ACP Nora hapa kwo' hawa jamaa ni mabegini ndani ya muda mfupi tu. Huyu mpumbavu tunaye leo, kesho tutakuwa na wengine. Makofi kwa ACP Nora," akasema Mario huku akimpigia makofi Nora.

"Oh subiri... amekusikia unamwita mpumbavu, huyo hapo kaamka... jiandae," Alex akamwambia Mario.

Kevin Dass alikuwa ameanza kufumbua macho yake na kunyanyua kichwa taratibu. Alionyesha dhahiri kwamba kichwa kilikuwa kinamuuma sana, lakini akajikaza na kuwaangalia watu waliokuwa mbele yake. Alipomaliza kuwaangalia wote, akainamisha kichwa chake tena.

"Oya vipi... hujambo?" Luteni Michael akamwambia Kevin.

"Sijambo, sh'kamoo?" Kevin Dass akasema bila kunyanyua kichwa.

"Mhm... nisikilize mvulana. Sijali wewe ni nani au ni nini. Unajua ni kwa nini uko hapa. Tusipotezeane muda sasa. Ninataka unijibu kila swali nitakalokuuliza," akasema Luteni Michael.

"Nikujibu wewe kama nani?" Kevin Dass akauliza na kumwangalia usoni.

"Naitwa Michael. Mimi ni mtu ambaye naweza kuamua ikiwa utaondoka hapa na p**** moja au bila hata moja kabisa. Kwa hiyo kitu cha muhimu ambacho nataka kutoka kwako ni ushirikiano tu, la sivyo mambo mengine nitakayokufanya hutapenda kabisa. Unaponiona mimi unaliona Jeshi la Nchi pia, kwa hiyo tenda kwa busara ili utoke hapa ukiwa salama," Luteni Michael akamwambia.

"Umekosea kaka. Mimi siyo unayenifikiria kuwa," Kevin akamwambia.

"Kilichokufanya ukimbie ilikuwa ni nini?" Luteni Michael akauliza.

"Miguu," Kevin akajibu.

"Kuwa makini na unachoniambia. Nikikasirika utabaki kukimbilia matako," Luteni Michael akamwambia.

Mario na Hussein wakacheka.

"Mbona unaongea sana kama demu? Shimo lako la nyuma linawasha sana unataka nikupe msaada, au?" Kevin akasema kwa dharau.

"Najua wewe ni mmoja wao... mnajiita Mess Makers. Nachotaka kwanza uniambie wenzako wako wapi, pili nani ni kiongozi wenu, maana kwa akili yako yenye makunyanzi sidhani wewe ndo' ulipanga wizi ule. Na tatu, pesa zote mlizoiba ziko wapi. Harakisha, vijana wangu wana njaa," Luteni Michael akamwambia.

"Oya, hivi huyu bwege anaongea nini? Yaani hata wenzako wanakushangaa," Kevin akasema.

"Ninakupa sekunde kumi uanze kujibu maswali yangu yote," Luteni Michael akamwambia.

"Mmetoka kilabuni nyie wahuni? Mko high? Ey mrembo mwambie boo wako huyu sielewi lugha ya vichaa, maana naona bangi zimempanda kichw...."

Kabla Kevin hajamaliza kusema maneno yake ya dharau, Luteni Michael akamshika chini ya mikono yake na kumnyanyua juu kwa nguvu sana, kisha akamwachia. Kiti alichokuwa amekalia Kevin kiliruka hewani huku mwili wa jamaa ukiangukia sakafuni kwa nguvu sana. Luteni Michael akamfata hapo chini na kumsimamisha, akiwa bado amefungwa kwa pingu miguuni na mikononi, kisha akaanza kumcharaza makofi mazito usoni yaliyomtia maumivu makali. Wenzake na Luteni walikuwa wakiangalia huku wanacheka, lakini ACP Nora akawa anatazama mambo hayo yote kwa umakini tu.

Luteni Michael alimpatia Kevin kipondo cha nguvu siyo mchezo. Alimfumua mpaka jamaa akajaa damu usoni, kisha akamshika usoni akiwa amekaa chini na kumtazama kwa ukaribu.

"Hapo nilikuwa nakuonja tu. Kwa usalama wako niambie kila kitu nachotaka kujua, kwa sababu kitakachofuata kitakuwa kibaya zaidi," Luteni Michael akamwambia.

Kevin Dass akatema damu chini na kusema kwa ubabe, "Kama wewe mwanaume kweli kwa nini unapigana na mwanaume mwenzako akiwa amefungwa mikono?"

Luteni Michael akamwangalia kwa ufupi, kisha akamwachia na kuanza kurudi upande waliposimama wengine.

"Mfungulie," Luteni Michael akamwambia Alex.

Alex akatii na kwenda kuzifungua pingu kwenye mikono na miguu ya Kevin.

"Lieutenant..." ACP Nora akamsemesha Luteni Michael.

"Mm..." Michael akaitika bila kumwangalia.

"Samahani, lakini... hii kweli ni njia sahihi ya kushughulika naye?" Nora akamuuliza.

"Mtoto akiomba nyoka?" Luteni Michael akamuuliza pia.

"Mpe," Mario akajibu, naye pamoja na Hussein wakaanza kucheka.

Nora akabaki tu kimya. 

Alex akawa amemaliza kumfungua Kevin na kumnyanyua juu ili asimame tayari kwa pambano, kisha akarudi kwa wenzake. Kwa uwazi ambao walikuwa wameuacha katikati baina ya wawili hawa, Kevin alikuwa anaangalia kama kuna njia ya kutorokea, lakini mlango ulikuwa nyuma ya waliposimama adui zake, na madirisha yalikuwa yamejengewa nondo ambazo haingekuwa rahisi kuzikunja kwa mikono. Hivyo akakunja tu ngumi na kujiandaa kupigana. Luteni Michael akaanza kumfata Kevin bila kusita hata kidogo.

"Huyu fala atajuta sana," Mishashi akamwambia Nora.

Kevin akamfata Luteni Michael na ngumi zikaanza. Jamaa alikuwa anamrushia ngumi kwa ustadi sana, na ijapokuwa kadhaa zilimpata Luteni Michael, lakini naye pia alimtandika haswa. Kevin alijitahidi kuonyesha anajua kupigana lakini kwa Michael hakuweza kushinda. Luteni alimpiga sana mpaka Nora akawa anamwonea huruma Kevin. Mwanaume huyu alikuwa anajaribu kunyanyuka lakini akawa anashindwa; kwa kuanguka-anguka kila alipojaribu. 

Luteni Michael akaona aache tu kumpiga na kumsogelea tena usoni, huku Kevin akiwa anapumua kwa uzito na akihisi maumivu makali mwilini.

"Vipi... bado unafikiri mimi siyo mwanaume?" Luteni Michael akamuuliza.

"Hhh... hiyo ni kwa sababu tu ulikuwa umeshaanza kunipiga mwanzoni," Kevin akasema.

Luteni Michael akatabasamu na kumpiga kofi laini la kirafiki kwenye shavu.

"Nafikiri uko tayari sasa kuongea," Luteni Michael akamwambia.

"Hhh... sawa. Lakini... kwanza nahitaji maji ya kunywa... tafadhali," Kevin akasema.

Luteni Michael akakerwa sana. 

"Kaka, huyu anataka kutuchezea. Mpatie phase nyingine ya maumivu, ataropoka tu," akasema Mishashi.

"Hauko chini ya hali yoyote ile kuniomba jambo lolote lile. Ninaweza kuutoa ukweli wote kwako na kukuua bila kukonyeza. Kwa mara ya mwisho... nijibu maswali yangu yote niliyokuuliza," akasema Luteni Michael kwa mkazo.

"Nitawezaje kujibu ikiwa... sijisikii vizuri... natakiwa niwaambie mambo kwa mapana na marefu ili mwelewe... mambo siyo simple... kaka..." Kevin akaendelea kukwepa kijanja.

Nora akawa ametambua kuwa mwanaume huyu alikuwa anawapotezea muda kwa makusudi. Kwa kipigo alichopokea, kwa mtu yeyote angekuwa radhi kuanza kuongea kwa sababu maisha yake yalikuwa kwenye hatari, lakini yeye bado alionyesha ukaidi. Hii ikamwambia kuwa kuna kitu ambacho kilikuwa kinampa mwanaume huyu kiburi, kama vile alikuwa anajiamini sana kwamba hii haikuwa shida kubwa kwake.

"Usijali kwa kuwa nitakufanya ujisikie vibaya hata zaidi na bado utasema tu kila kitu, mpumbavu wewe!" Luteni Michael akamwambia.

Akamshika shingoni akitaka kumwanzishia kipigo kingine. 

"Ngoja kwanza!" ACP Nora akamzuia.

Luteni Michael akamgeukia Nora. 

"Mario, Hussein, njooni nami," Nora akawaambia.

Kisha akaanza kwenda pale alipokuwa Luteni Michael na Kevin. Mario na Hussein wakamfata tu wakiwa hawaelewi alitaka nini. Akafika karibu ya Luteni Michael, ambaye bado alikuwa ameishika shingo ya Kevin kwa nguvu.

"Luteni... huyu mwanaume kuna kitu anaficha. Tafuteni kifaa chochote cha kielekroni kwenye mwili wake," Nora akasema.

"Lakini tumemtolea kila kitu... hana chochote tena. Kila kitu anacho pale Mishashi, simu, nini..." akasema Hussein.

Nora akamsogelea karibu Kevin na kuanza kumkagua-kagua. 

Luteni Michael akamwachia mwanaume huyu na kubaki anamtazama tu Nora. "Kwa nini unafanya hivi?" akamuuliza.

Nora hakujibu ila akaendelea tu kumkagua.

"Mrembo amenikubali," Kevin akasema.

"Funga domo lako, panya wewe!" Luteni Michael akamfokea.

Nora akiwa anaendelea kumkagua jamaa, macho yake yakatulia kwenye sikio la kushoto la Kevin. Kwa haraka ungesema alikuwa amevaa tu hereni kwenye sikio hilo, lakini Nora akalivuta na kuiangalia hereni hiyo kwa umakini. Ilikuwa ikitoa mwanga mwekundu kwa mbali sana ulioshtua-shtua. Kevin akawa anajaribu kugeuza kichwa chake upande mwingine lakini Nora akang'ang'aniza kulishika sikio hilo.

"ACP unafanya nini?" Mario akamuuliza.

"We' mwanamke huna hereni au? Unaitaka hii ya buku?" Kevin akasema kwa hasira.

"Luteni... hii hereni ni tracking device!" akasema Nora.

"Nini?" Luteni Michael akauliza kwa mshangao.

Akasogea karibu na kuangalia kwa makini, naye akawa amejihakikishia.

"Tracking device? Kwa ajili ya nini?" Mario akauliza.

"Tracking device huwa ni kwa ajili ya nini Mario?" Hussein akamuuliza.

Alimuuliza swali hilo kumfanya Mario aone alichouliza kilikuwa kitu cha kijinga. Mishashi na Alex wakaona wasogee hapo pia. Luteni Michael akamwasha kofi zito Kevin usoni lililofanya aangukie kichwa vibaya. Nora akashtuka na kusogea nyuma.

"Pumbavu wewe! Huu muda wote umekuwa ukicheza na mimi kumbe unawaita wenzako hapa? Ili wakuokoe? Sasa nisikilize... hapa ndiyo mmefeli. Si wanakuja eeh? Tuko tayari kwa ajili yao, kwa hiyo ni vizuri kwamba umewaalik...." 

Kabla Luteni Michael hajamaliza kuongea, kishindo kikubwa kikapiga bati na kufanya wote washtuke na kutazama juu. Hiyo ilikuwa ni mzubaisho kwa kuwa papo hapo taa ikazimwa, na wanajeshi hawa pamoja na ACP Nora wakachanganywa sana kwa sababu giza lilikuwa zito ndani hapo. Luteni Michael aliweza kusikia wenzake walipoanza kuzikoki bastola zao tayari kwa kujihami, lakini hakuweza kuwaona vizuri. 

Ghafla wakasikia sauti ya kilio cha maumivu kutoka kwa Alex na kishindo kuashiria ameanguka chini. Kwa kuanza kuzoea giza kiasi, Nora aliweza kumwona Mario akielekeza bastola upande aliosimama Mishashi, ikiwa wazi hakuweza kuona vizuri.

"Subiri! Msipige risasi tutapigana wenyewe kwa wenyewe!" Nora akaonya.

Vishindo vingine vikaanza kusikika na sauti za mapigano pia. Luteni Michael akashtukia anapigwa kwa nguvu sehemu mbalimbali mwilini bila kumwona adui. Ilikuwa ni kwa kasi sana, naye bila kutarajia akaangushwa chini na kupigwa vibaya sehemu ya kichwa chake na kupoteza fahamu. Nora alipigwa nyuma ya shingo na kusababisha mwili wake ufe ganzi na kudondoka chini, lakini hakupoteza fahamu. Wengine pia walikuwa wanadundwa haswa mpaka kupoteza fahamu zao, naye Kevin akanyanyuliwa na mmoja wa watu hawa waliofika "kumwokoa."

"Hhh... mbona mmechelewa hivyo?" Kevin akauliza.

"Asante kushukuru," akajibu aliyekuwa akimsaidia, ikiwa ni sauti ya mwanamke.

Kisha Kevin akajitoa mikononi mwake na kwa hasira akaanza kumfata Luteni Michael pale chini. Akamfikia na kuanza kumpiga ngumi nyingi sana usoni. Lakini mmoja kati ya waliokuja kumwokoa akamfata na kumsukuma kwa nguvu. Hakuongea lakini akatoa ishara kuwa waondoke. Kevin Dass akawa kama anabisha na kumsogelea karibu kibabe, lakini yule mwanamke ambaye alimnyanyua muda ule akaingia kati yao na kutoa ishara kuwa WAONDOKE. Kevin, akiwa amejishika tumboni kwa kuhisi maumivu, akarudi nyuma na kuanza kuelekea sehemu ya mlangoni.

Yote haya Nora alikuwa akiyaona, kwa kuwa sasa alizoesha macho yake kwenye giza hilo. Ijapokuwa hakuweza kuwaona vizuri usoni, kwa haraka aliweza kuwahesabu na kutambua walikuwa 6, ukijumuisha na Kevin, naye akawaona wote walipoanza kutoka ndani hapo. Wanajeshi wote walikuwa wamepoteza fahamu sasa, naye Nora akajiburuza taratibu upande mmoja. Kwa tukio zuri mkono wake uligusa kitu kigumu ambacho kwa haraka alitambua ilikuwa ni bastola, naye akaona ni bora awakomeshe watu hao, kwa kuwa alifikiri labda wamewaua wenzake.

Hakuwa na nguvu za kutosha, lakini akainyanyua bastola na kuielekeza mlangoni, ambapo wale watu walikuwa wameshaanza kutoka upesi, lakini wa mwisho akiwa bado sehemu ya ndani. Akafyatua risasi nne zilizompata mtu huyo mgongoni. Lakini mtu huyu akasimama tu, kisha akageuza kichwa chake na kumwangalia Nora. Nora aligundua kuwa mtu huyu alivaa kiziba uso (mask) kilichofunika macho yake kufikia puani, lakini sehemu ya mdomo ilikuwa wazi. 

Wale waliokuwa wametangulia nje kutia ndani na yule Kevin waligeuka nyuma na kumwona mwenzao akiwa amesimama tu hapo bado, wakitambua alikuwa amepigwa risasi kwa nyuma. Wakataka kurudi ndani ili wamshughulikie Nora, lakini mtu huyo aliyepigwa kwa risasi mgongoni akawazuia. 

Nora akawa ametambua kuwa nguo alizovaa mtu huyo, au labda kwa ndani kulikuwa na 'bulletproof,' aina ya nguo inayozuia risasi. Kwa vile nguo hiyo nyeusi ilionekana mwilini kwake pote, Nora alijua kumpiga risasi kusingekuwa na matokeo yoyote yale. Akabaki kuangaliana naye kwa sekunde chache, kisha mtu huyo akageukia mbele na kutokomea.

Nora alibaki akipumua kichovu. Alihisi sehemu za mwili wake zilizoishiwa nguvu zikianza kuirudisha, naye akajinyanyua polepole na kujitahidi kusimama.

"Aahhh... Mario... Hussein..."

Nora akasikia sauti hiyo ya Luteni Michael ikiita, naye akahisi kufarijika kujua kwamba alikuwa hai. Akamfata taratibu pale chini na kumshika. Lakini Luteni Michael akifikiri ni adui, akamvuta kwa nguvu na kumkaba shingoni. 

"Ah! Ni mimi... ni mimi..." Nora akaongea.

Luteni Michael akamwachia, huku mwili wa Nora ukiwa juu yake.

"ACP... nini kinaendelea?" Luteni Michael akauliza.

"Wameondoka... wame... wameondoka na Kevin," Nora akamjibu huku akijitoa mwilini kwake.

"Damn it! Agh... ninawezaje kuonyesha ujinga mwingi kiasi hiki!" Luteni Michael akasema kwa hasira.

"Luteni... tuangalie kama... wengine wako sawa," Nora akasema.

Luteni Michael akajinyanyua, huku akihisi maumivu makali ya kichwa, lakini akajikaza na kuanza kumsaidia Nora kuwatafuta wenzao pale chini. Nora akaona aelekee upande ambao angeweza kuwasha taa, na baada ya kuiwasha, wakawaona wanajeshi wale wengine wakiwa wamelala chini tu. Luteni Michael akaanza kuwafata akiangalia hali zao, naye akaridhika baada ya kuona kwamba kila mmoja wao alikuwa hai. Wakaanza kusaidiana kuwaamsha na kufanikiwa. Wote walikuwa wakihisi maumivu vichwani, na hasira ziliwajaa sana.

"Hao ndiyo Mess Makers eti... dah... tumekalishwa chini kama vyura yaani," akasema Hussein.

"Oya jitahidi ku-improve slang zako," Mario akamwambia Hussein.

"Aliyekwambia hiyo ni slang nani?" Hussein akamuuliza.

"Basi chura ni wewe peke yako," akasema Mario.

Hussein akamwonyesha kidole cha kati.

"Ni bora tu tungempeleka huyo mshenzi jengoni... haya yote yasingetokea Luteni," akasema Mishashi.

"Unataka kusema kwamba ni makosa yangu haya yote kutokea?" Luteni Michael akauliza kwa kuudhika.

"Hamaanishi hivyo... Mishashi tuliza boli," Alex akaongea.

"Hapana, nasema tu kama tungempeleka sehemu secure zaidi basi hii yote isingetokea. Kuja hapa haikuwa busara. Samahani Luteni, lakini lazima niseme ukweli," Mishashi akasema.

"Kwa hiyo ukikaa kunilaumu ndo' watarudi, au?" Luteni Michael akauliza kiukali.

"Basi inatosha! Kilichotokea kimetokea, hakuna njia ya kubadili zaidi ya kuendelea na kazi," Nora akawaambia kwa uthabiti.

"Yaani huo muda wote alikuwa ametuzidi akili kweli! Kwa hiyo kama tungekuwa tumeanza kumpeleka kule je?" akauliza Alex.

"Wangekuja. Inaonekana timu yao hii ina muungano wa karibu sana. Tunahitaji kujua muungano wao chanzo chake ni nini na kuusambaratisha kama tukitaka kuwamaliza wote," akasema Luteni Michael.

"Hawa jamaa wako makini. Luteni... tumempoteza mmoja wao ambaye labda angekuwa ndiyo njia ya pekee ya kutusaidia kuwasambaratisha kama usemavyo. Sasa sa'hivi itakuwa ngumu maana watakuwa makini zaidi," akasema Mishashi.

Luteni Michael akapiga ngumi chini kwa hasira.

"Bado inashangaza kwamba hawakutuua. Hata nimempiga risasi mmoja wao, lakini... akaniacha tu," Nora akasema.

"Na kwa hilo watajuta. Ni lazima tuwashike tu kwa hali na mali zote. Alex tukitoka tu hapa tuma taarifa kwa Bobby aisambaze picha ya Kevin Dass haraka iwezekanavyo kwa vyombo vyote nchini, kwa matangazo, kila kona. Nataka awe wanted upesi na sum up a hefty price kwa yeyote atakayemwona," Luteni Michael akasema.

"Uhakika Luteni," Alex akamwambia.

"Hii ni nchi yetu, na tumeapa kutekeleza haki pale ambapo watu kama wao wanaivunja. Hatutakata tamaa mpaka tuhakikishe tunashinda. Vijana wangu... tutashinda tu," Luteni Michael akasema kwa uhakika.

Wanajeshi wengine wakatikisa vichwa kuonyesha wameyatilia maanani maneno ya Luteni Michael. ACP Nora alikuwa bado na maswali mengi kichwani. Lakini kwa wakati huu, wote wangehitaji kutoka hapo ili kurudi mkoani kwao kuendelea na msako huo, kwa kuwa huku walijua tayari walimpoteza ndege wao angani. Wote wakatoka na kuelekea kwenye magari yao, kisha wakaondoka kuelekea kwenye hoteli ambayo walikuwa wamechukua vyumba kwa muda mfupi.

Nora akiwa kwenye chumba chake, alimtafakari sana mtu yule aliyempiga risasi mgongoni. Kila mara alipokumbukia tukio la muda mfupi nyuma alitulizia akili yake hapo tu; jinsi mtu huyo alivyomgeukia na kumwangalia sana. Alijiuliza ni kwa nini hata baada ya kumfanyia vile, yaani kumpiga kwa risasi nne, mtu huyo hakuchukua hatua yoyote na kuondoka tu. 

Akaona aende tu kujimwagia maji kisha aingie kulala, kwa kuwa hakuhisi tena hamu ya kula.

★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next