Reader Settings

Wasichana  wawili ambao walikuwa eneo la mapokezi kidogo walionyesha kukosa utulivu mara baada ya kumuona mwanamke alievalia suti  akisogea upande wao na walijua pengine  alikuwa  akiwasogelea  lakini walijikuta wakishangaa mara baada ya kumuona  mwanamke yule akisimama mbele ya  Hamza na kunyoosha mkono.

“I Suppose wewe ndio Hamza right!!?”Aliuliza  yule mwanamke akiwa  na tabasamu usoni.

“Yes ndio mimi Hamza Mzee”Aliongea Hamza huku  akionyesha kukosa utulivu kiasi   na kunyoosha mkono wake kusalimiana nae.

Wakati wa kushikana mkono na yule mwanamke alihisi   ni kama kuna shoti za umeme zinampiga kwani zilianzia mkononi  na kwenda kichwani kutoa mawasiliano kama ameshikana na kitu kisichokuwa cha kawaida na baada ya pale  taarifa zilitumwa   kwenye moyo kwa ajili ya kuongeza msukumo wa damu kuelekea kiwiliwili  cha chini  na ghafla tu  kiungo cha uzazi cha Hamza kilianza kusisimka.

Muunganiko wa mwili   ulikuwa ni wa ajabu sana  na  pengine Mungu  katika kazi aliopatia  ni kuumba kiumbe binadamu.

Mwanamke aliekuwa mbele yake alikuwa  ni  mweupe wa  wastani, mrefu  kiasi  mwenye  mwili uliojipanga huku ngozi yake ikiwa ni kama vile imetengenezwa ,  itoshe kusema katika wanawake ambao Hamza alishawaona tokea  afike jijini  Dar es salaam huyo  ndio mwanamke wa  kwanza kwa uzuri , Melissa mpenzi  wake Amiri alijiambia tupilia kule , Tresha Noah  msichana alieambiwa  alikuwa ametengenezwa muonekano wake  tupilia  kule , Anitha  hakutaka hata  kuongea  zaidi ya kutamani kusonya.

“Mr Hamza!, naitwa Prisila Singano Afisa mkuu wa idara ya Rasilimali  watu  kampuni  ya Dosam, mimi ndio niliekupigia simu nadhani sauti yangu hujaisahau”Aliongea  kwa mapozi na kumfanya  Hamza kuzidi kupagawa , hakuamini huyu ndio mwanamke ambaye alikuwa akitafuta mchumba wa maigizo.

‘Nimefurahi kukufahamu  mrembo Prisila Singano , lakini  naomba kuuliza una undugu na  Profesa Stephano Singano?”Alongea Hamza huku akiwa  anajiamini kiasi kwamba kama  unamjua ungesema hio hali ya kujiamini kaitolea wapi, maana Hamza tunaemjua sisi ni yule Mzembe aliepigwa cha mbavu na mrembo Anitha.

Wale wafanyakazi wa mapokezi walikuwa na maswali kibao , walikuwa wakimfahamu  Prisila sio mtu wa mchezo mchezo ijapokuwa alikuwa mdogo ki umri lakini  alikuwa ni mkali mno  kazini  na hakupenda uzembe  lakini sio hivyo cheo chake kilikuwa kikubwa mno   ndio aliekuwa ni CHRO  wa  kampuni ya Dosam Global.

Kila  mwanadada ndani ya jiji la Dar es salaam  ambaye alikuwa ni mtaaluma alikuwa akimchukulia Prisila kama  ‘role model’  wao  kutokana   na mafanikio  yake ya haraka haraka na kuongoza kampuni kubwa  Afrika na duniani.

Yaani kwa maneno marahisi yeye ndio alikuwa mwajiri  mkuu wa kampuni ya Dosam hivyo watu wengi wanaotafuta ajira walikuwa lazima wapitie kwa huyu mwanamke, kutokana na  watu wengi kutaka kufanyia kazi katika kampuni ya Dosam wale ambao walipata nafasi   hawakutaka kuzembea kazini na kutolewa , kwani kudumu ndani ya kampuni ya Dosam ilihitajika  zaidi  utendaji mzuri na  ujuzi  na sio maswala ya GPA au ufaulu  mkubwa unaonekana katika cheti chako.

Hivyo  ilimfanya  Prisila kuogopeka sana kwani alikuwa ni mwanamke aliekuwa  akienda na falsafa yake ya 4E katika eneo la kazi ambayo   ilisimama kama mbadala wa Effort(juhudi), Excellence(Ubora), Embodiment(Mfano halisi) na Environment(Mazingira).

Yaani kama mfanyakazi akikosa vigezo  katika hio  falsafa ya 4E basi  kama  ni mfanyakazi atafukuzwa au kama  ndio anaomba   hawezi kupatiwa kazi, ukikidhi vigezo hivyo  hata kama cheti chako hakina  maksi kubwa basi  jihesabie  unafanya kazi katika kampuni kubwa  Afrika ya Dosam Global.

Prisila alicheka  kwanza , hakuamini Hamza  angekuwa ni mwanaume wa kujiamini namna hio tena na kwenda mbali  na kumtania kama mrembo , asilimia kubwa ya wanaume  wa  rika la Hamza aliokutana nao  wengi walionekana  ni wenye kukosa hali ya kujiamini.

“Mzee Stephano ni  baba yangu, sijui umefahamiana nae vipi lakini sina muda wa kuukuliza sasa hivi kwani unapaswa kukutana   na bosi  mwenyewe ambaye anataka kukuajiri , naomba nifuate Hamza”Aliongea na kauli yake ilimfanya  Hamza kutoa macho.

Inamaana huyu mwanamke sio ambaye alikuwa akihitaji   mtu wa kufanya nae maigizo ya boyfriend, alijiuliza Hamza na aliona ilikuwa ikileta maana , mwanamke mrembo kama huyo anahitaji vipi   boyfriend wa maigizo kwa mfano , ilikuwa kichekesho.

Hamza alijiambia  alikuwa akijidanganya tu , pengine  matumaini yake ya kukutana na mwanamke mrembo yalikuwa yakienda kusambaratikika  kabisa..

“Kwanini isingekuwa ni wewe , pumbavu kabisa yaani nimejitutumua vyote hivi kupendeza  na kuwa jasiri mbele yako…”

“Mr Hamza come on,.. muda unaenda?”Aliongea Prisila mara baada ya kumuona Hamza amesimama tu na kumfanya bwana huyo kushitika kutoka kwenye   mawazo na kuanza kutembea.

Wale  wafanyakazi wa mapokezi waliishia kuangaliana kwa ishara  kama vile wanajiuliza huyo mtu ni nani , kwanini  bosi  Prisila ndio kaja  mpaka hapo kumchuka.

Asilimia kubwa ya  watu ambao aliweza kuwaona  ndani ya jengo hilo ni wazungu na wahindi  na waliochanganya rangi kama yeye ,  watu weusi walikuwa ni wa kuhesabu sana , pengine ni  kutokana na eneo lenyewe kuwa ghali sana , hii ilimfanya  Hamza kujiambia kwamba hata kama  mtu anaekutana nae  kuwa mbaya lakin angalau anaonekana kuwa na pesa na kama angepita katika usaili huo ilimaanisha kwamba  moja kwa moja  angepata Exposire ya maeneo ya watu wazito wazito.

“Hata kama ni mbaya  nnitaenda nae hivyo hivyo kibishi, pengine inaweza kuniweka na watu wazito wazito na ikawa safari ya kumjua Mzee”Aliwaza  Hamza wakati akiwa kwenye lift.

Ijapokuwa alikuwa katika hali ya mawazo lakini bado  hakuchoka kutazama umbo  la mwanamke mrembo Prisila, alitamani kuuliza swali  lakini  alishindwa mara baada ya lift kufunguka na kuruhusu mtu mwingine kuingia.

Dakika chache tu  walienda kutokezea katika floor ya juu kabisa  na mara baada ya Hamza kutoka kwenye lift  hiyo  alijikuta akishangaa  baada ya kuona uzuri wake lakini macho yake yalichanua mara baada ya kugundua eneo hilo lilikuwa  likihudumia watu wa hadhi ya juu  yaani  VVIP.

Ijapokuwa  alikuwa akijiamini kama vile amekunywa kiroba  lakini  bado mapigo yake ya moyo hayakuacha kudunda kwa kasi na kujiuliza ni mtu gani ambaye anaenda kufanya nae usaili tena eneo la VVIP katika hoteli kubwa  ya hadhi kama hio.

Prisila alionyesha kutembea kama vile anafanya makusudi , pengine  amevutiwa na  sura ya Hamza maana  bwana huyo alikuwa amependeza kweli ukijumlisha na  muonekano wake wa ngozi ilimfanya  kuwa   wa kuvutia kwa kila mwanamke  yoyote yule , lakini licha ya hivyo  hali ya kimasikini ya Hamza haikujificha kwenye uso wake.

Kuonekana tajiri ni tofauti na  uvaaji wa mavazi ,  unaweza kuwa tajiri  lakini ukaamua kuishi maisha ya kawaida lakini siku zote huwezi kuonekana masikini , masikini siku zote ataonekana kwa umasikini wake na tajiri ataonekana kwa utajiri wake, kuna vitu vingi sana vya kumtofautisha tajiri na masikini  au mtu aliefanikiwa na ambaye hajafanikiwa  na hio inaenda kabisa  kwanzia katika  namna mtu unavyoongea ,wajihi  , namna unavyotembea na  ujengaji wa hoja wakati wa kuchangia mambo.

Tajiri anaweza akajificha katika kundi  la watu masikini lakini siku zote hawezi kufanana na masikini.

Masikini na tajiri wote wanaweza kuwa na njaa kutokana na kutokula lakini kama utaamua kuwatofautisha  na njaa zao utagundua masikini ndio anaeteseka zaidi na njaa kuliko yule tajiri, maana njaa ya tajiri ni ya kuchelewa kula wakati njaa ya masikini ni ya kukosa chakula.

Kwa upande wa Hamza ukweli ni kwamba  ilikuwa ngumu kumtofautisha  na masikini , kwa haraka haraka unaweza kusema kwamba  Hamza ni mtoto wa tajiri ambaye ameamua kuishi maisha ya kimasikini.

Prisila alienda kusimama katika  mlango namba 402  na kisha aligonga mlango   kwa dakika kadhaa na palepale  mlango ulifunguliwa na  mwanadada  mwenye sura iliokakamaa  alievalia suti kama vile ni afisa usalama au  bodigadi.

Mwanamke yule alimruhusu  Prisila kuingia lakini alimwashiria Hamza kusimama nje  kabla ya kuingia.

“Kijaji  mruhusu,  ndio mgeni anaepaswa kuonana na bosi”Aliongea Prisila lakini  mtu alieitwa Kijaji  bado  alimwangalia  Hamza kwa macho ya tahadhari na palepale alimsogelea na kuanza kumpapasa kama hana siraha ya aina yoyote  na aliporidhika alimpiga jicho kali la tahadhari na kisha akamruhusu kuingia.

Hamza alijiambia huyu mwanamke ni mrembo sana lakini  tabia yake ya ukakamavu inamfanya kuwa na sura  ngumu.

Hata hivyo hakutaka kumfikiria sana , yeye  hofu yake ni mtu ambaye anakwenda kuonana nae.

Hamza alikaribishwa na mandhari ya kuvutia ya chumba cha  hadhi ya raisi(Presidential suite), haikuwa chumba cha kawaida  kwa mtu wa kawaida kuingia na ilimfanya  Hamza macho yake kuangalia  vitu vilivyokuwemo pamoja na uzuri wake kwa haraka haraka.

Mbele yake kabisa upande wa dirisha kubwa  ambalo linaangaliana na bahari ya Hindi  kulikuwa na eneo la sebuleni na sofa kubwa ambalo lilikuwa imekaliwa na mtu alievalia kofia ya  hat kichwani.,

“Huyo ndio  bosi , nadhani mawazo yangu yapo sahihi   nakwenda kukutana na mtu mbaya  ambaye amekataliwa na wanaume mpaka kuamua kutafuta  boyfriend feki , aisee hata hivyo maji nimeyavulia nguo sharti ni yaoge”Alijiongelesha katika mawazo yake akimwangalia  yule mwanamke aliempa  mgongo akisubiria  surprise  ya  kuona sura  ya mwanamke mbaya,

“Bosi , Mr  Hamza kashafika kwa ajili ya usaili?”Aliongea  Prisila huku akionyesha hali ya heshima.

“Okey  mnaweza kuondoka , nitawaita baada ya  usaili”

“Boss!!’Aliongea Kijaji kwa tahadhari.

“Hakuna kibaya kinachoweza kunitokea , mnaweza kuondoka”Aliongea  bila ya kugeuka .

Upande wa Hamza sauti hio ilimsababishia mshituko wa aina yake , ilikuwa ni sauti nyororo  lakini yenye madaraka  ndani yake, ilikuwa ni kama wimbo  wa kubembeleza unaozigonga ngoma za masikio yake.

Ilikuwa ni sauti nzuri  mno  na Hamza alijiuliza au mawazo yake ni tofauti na  uhalisia , kwanini mwanamke anaemdhania kuwa ni mbaya wa sura kuwa  na sauti nyororo hivyo , alijiambia pengine sio mbaya kila kitu , isitoshe  kuna msemo  wa kwamba Mungu hakupi vyote , anaweza akakupa sauti  nzuri  lakini akakupa sura mbovu, anaweza akakupa mguu ila akakupa Komwe kubwa.

Licha  ya Prisila Singano kusita sita  pamoja na mlinzi wa bosi huyo lakini waliishia kutii maagizo yake.

“Ukifanya chochote kibaya kitakachomdhuru bosi basi jua ndio kifo chako”Aliongea  Kijaji  kwa tahadhari na kumfanya Hamza kutoa tabasamu na kuzidi kumkera  mlinzi wa watu,

Baada ya  kila mtu  kuondoka  ndani ya  hiko chumba yule mwanamke  palepale  aliinua mkono wake na  kuitoa ile Hat.

Ilikuwa ni hat aina ya Beekeeping Veil,  yaani  hat ambazo  huunganishwa na kitambaa cheusi ili kuzuia sura ya mtu kutokuoenekana

Hamza mara baada ya kuona  mkono wa yule mwanamke ukiondoa ile hat taratibu mapigo yake yalianza kuongezeka spidi spidi , ilikuwa ni hisia ambazo kwenye maisha yake hakuwahi kuzisikia hata  siku moja,  kadri  ile Veil ilivyokuwa ikiiacha sura wazi alizidi kujawa na hofu  pamoja na mshituko wa aina yake,

Mwanamke yule   baada ya kuivua alisimama  na sasa  namna ambavyo alikuwa akisimama ni kama vile  yupo kwenye mwendo wa slow motion , ni kama vile malaika  anaibukia  kutoka ardhini.

Yalikuwa ni matarajio tofauti kabisa na kile alichokuwa akikiwazia   Hamza , mwanamke aliekuwa mbele yake  akili yake ilimwambia kabisa ni mwanamke ambaye anapaswa kusujudiwa kwa kupaza  sauti.

******

MIEZI  KADHAA  ILIOPITA.

Ni miezi kadhaa iliopita   ndani ya eneo la maegesho ya magari katika hospitali   ya  chuo ya Mayaya Clinic  iliingia gari ya kifahari  aina ya  Porsche Gayenne  G Coupe .

Baada ya gari hii kusimama  palepale mlango wa dereva ulifunguliwa  na mwanaume  mtanashati alievalia suti  na kwa haraka haraka alizunguka upande wa kushoto  na kisha akafungua mlango wa abiria.

Mwanamke mrembo sana  alievalia gauni lenye mkanda kiunoni na Blazer ya rangi  ya ugoro alishuka kwenye gari lile huku yule mwanaume akionyesha heshima mbele yake.

Kwa haraka haraka  anaeangalia  tukio lile angeelewa kwamba yule mwanaume ni dereva wa yule mwanamke.

“Utanisubiria hapa mpaka nitakapomaliza”.

“Sawa madam”

Alijibu yule bwana kwa  heshima  kubwa tu   mbele ya yule mwanamke , alikuwa  ni msichana mrembo haswa pengine  zaidi ya neno urembo , alikuwa ni msichana mdogo  pia  kimuonekano  makadirio ya miaka kama  ishirini na nne hivi  , alikuwa ni mweupe wa  wastani mrefu  na aliejaaliwa umbo  zuri.

Kitu kimoja tu ambacho pengine ambacho kinapunguza asilimia mbili ya uzuri wake ni muonekano wa yule mrembo , alikuwa ni kauzu mnno  lakini hata hivo bado alikuwa amependeza.

Aliweza mkoba wake kwapani vizuri na kisha alizipiga hatua kuingia ndani ya hospitali hio  kubwa.

Mayaya Clinic ni moja ya hospitali kubwa  sana ndani ya ukanda wa Afrika mashariki na kati yote , ilikuwa ni  hospitali ya  binafsi  ambayo ipo chini ya   kampuni ya Vexto Group kampuni  namba moja  kwa ukubwa  Afrika na  namba kumi  kwa  Dunia nzima.

Yule mwanamke mrembo alitembea kwa mwendo wa kujiamini  mpaka kwenye lift  huku akionyesha sio mwenye kujali  macho ya wanaume na  wanawake  wanaomwangalia.

Ukweli ni kwamba ilionekana ni kawaida kwake kuangaliwa hivyo kutokana na yeye mwenyewe alivyo , alikuwa mzuri hivyo  ilileta maana kuangaliwa na kila  mtu , wengine walimwangalia kwa matamanio na wengine walimwangalia kwa maswali  kwa Mungu kwa kuweza kuumba   mwanamke wa aina hio.

Wahenga wanasema Mungu hakupi vyote  na kauli hii ilithibitishika kwa  mrembo huyu ndio maana siku hio ya asubuhi alikuwa ndani ya hospitali hio

Dakika chache mbele  mwanamke yule alikuja kutokezea katika floor namba  saba ambayo  ni idara ya  Saikolojia(Psychiatric Department).

Idara ya saikolojia  mara nyingi huhusiika na tiba ya magonjwa mbalimbali ya  yanahusiana na akili.

“Miss Regina karibu sana , Dr  Shukuru   anakusubiria”Aliongea  mwanadada wa mapokezi.

Kwa  haraka haraka ilionekana mrembo huyu ambaye sasa anafamamika kwa jina la Regina   alikuwa  ni  mgonjwa wa mara kwa mara  kufika ndani ya hospitali hio kutokana na  nesi wa mapokezi alivyompokea.

Mrembo Regina  aliishia kutingisha kichwa  na kisha alitembea kuelekea upande wa kulia akipita mapokezi na alisimama mbele ya mlango uliokuwa na   kibao  juu  ofisi ya daktari au chumba cha daktari  namba 01.

Mazingira ya hospitali katika idara hio ya magonjwa ya akili  ilikuwa tulivu mno, pengine  unaweza kusema wagonjwa wanaofika katika hospitali hio ni wachache lakini huo sio ukweli hospitali hio   ina floor mbili ambazo zote hutumika kama  idara ya magonjwa  ya akili lakini floor ya sita  ni yale magonjwa ya akili ambayo  ni  very comnon yaani yanayoeleweka na floor namba sita ni ya  magonjwa ya akili ambayo ni special zaidi.

Unaweza ukashangaa mgawanyo huu  lakini ukweli ni kwamba  zama za miaka ilipita na zama za  wakati huo zilikuwa zimebadilika sana tena sana , ni miaka ya hivi  karibuni kulibuka wimbi la magonywa ya akili ya kipekee ambayo  yamekuwa  ni  magumu sana kueleweka wa wataaluma na mpaka wakati huo  chanzo cha magonjwa hayo hakijafahamika bado na wanasayansi wanapambana  kujua chanzo chake.

Hii yote inasemekana ni mara baada ya  tukio la mwaka 2020 , tukio la mwaka 2020  halikuwa  na athari moja tu  bali lilikuwa ni tukio ambalo  lilibeba athari nyingi na moja ambazo  ya athari ambazo zinahusishwa  ni kuibuka kwa magonjwa ya akili  ambayo sio ya kawaida.

Sasa ukiona mtu  ambaye sio mfanyakazi wa hospitali ya Mayaya anaingia  floor namba  saba basi jua ni mwasilika wa tukio  la mwaka 2020.

“Miss Regina  karibu sana”

Mwanaume mmoja mtanashati wa makamo  alievalia koti  la udaktari  alisimama mara baada ya mango kufunguliwa na mrembo  Reginai.

Kwa muonekano wa daktari huyo ilionekana Regina  ukiachana na uzuri wake ambao sio wa kawaida lakini  kuna sababu nyingine ambayo inambeba kwani  daktari aliefahamika kwa jina la  Shukuru alionyesha unyenyekevu mkubwa.

“Thanks , I can see that you’re still a little nervous around me , please relax , I am regular patient remember”Aliongea yule mwanamke akitoa tabasamu hafifu  kidogo akimwambia yule  daktari kuacha wasiwasi  akiwa nae  na atulie kwani yeye  ni mgonjwa  wa mara  kwa mara.

“Bila shaka .. ni kwamba tu wewe ni mgonjwa wangu muhimu”Aliongea Dr Shukuru  huku akikaa kwenye kiti chake”

“Najua lakini mimi ni kama wagonjwa wengine tu  na isitoshe  bado natakiwa kuonana na daktari  wakati kwa wakati”

“Ni kweli kabisa Ms Regina  ,  umuhimu wako katika jamii unanifanya niwe makini na kutotaka kufanya makosa”

“Oh..  nashukuru  naamini utafanya vizuri , isitoshe  wewe ndio daktari  bingwa  ninaekuamini na tatizo  langu , ni miaka  mingi sana  tokea nianze kupata matibabu kutoka kwako, ni mwaka wa tatu  huu unaingia kama sikosei”

“Upo sahihi   na imekuwa heshima kwangu muda wote kukusaidia   kwa kila namna kuweza kupona ..”Aliongea na kisha palepale aliwasha tarakishi yake na kuandika jina la Regina kutafuta taarifa zake.

Kwa haraka  haraka ilionekana mrembo huyo anaefahamika kwa jina la Regina sio mara yake ya kwanza kufika ndani ya hospitali hio.

“Awamu hii umechukua muda mfupi sana  tokea appointment ya mwisho , nilikutegemea mwezi ujao , vipi kuna mabadiliko yoyote?”Aliuliza Dokta na kumfanya Regina uso wake kidogo kukosa utulivu.

“Siwezi kusema  kuna mabadiliko  makubwa  na leo  nilitaka kuonana na wewe kwa ajili ya ushauri zaidi”

“Ushauri , unaweza kuendelea nipo tayari  kukupatia ushauri wowote kama ni swala linalogusa shida yako maana ndio taaluma yangu”

“Dr  kwa  miezi  kadhaa mpaka sasa   familia  yangu  wanalazimisha  niolewe na mwanaume ambaye   wamemchagua , nilikataa pendekezo lao lakini  wameenda mbali na kuanza kufanya vikao kushawishi  Shareholders wa kampuni ili  kunilazimisha , wanasema  nisipokidhi vigezo  basi natakuwa kuachia nafasi  yangu kwenye kampuni kama CEO na mwenyekiti wa bodi”Aliongea na kumfanya Dr  kuwaza kidogo.

“Nadhani nimekuelewa  unachotaka kumaanisha .. lakini ili  niwe  more specific kwenye ushauri wangu , hebu  elezea  unachukuliaje swala hili?”

“Dokta  ninachofuata ni ushauri wako wa kitabibu kuhusiana na ugonjwa wangu wa ukichaa…”

“Miss  Reginai   naomba nikurekebishe, wewe  huna tatizo la ukichaa bali una shida ya  ugonjwa wa DID, nadhani nimekuambia ili  matibabu yako kufanya kazi vizuri lazima utambue ugonjwa wako kwa jina hilo na sio  ukichaa”

“Nimezoea  kwa muda kuiita ugonjwa wa  ukichaa, tukiachana na hilo nadhani  katika ushauri wako wa kitabibu  ulisema   ugonjwa wangu unaweza kumalizwa  na mapenzi?”

“Ndio nilimaanisha   kutokana na shida yako kuwa ya kisaikolojia zaidi itakuhitaji kuwa na high self willing ya  kuchagua ni  namna gani unataka kuishi na kuishinda nafsi yako  nyingine   na hili litawezekana ukiwa na msaada wa nje wa kisaikolojia , kama vile  kushare  hisia zinazofanana na mtu mwingine , hii ni moja wapi ya njia ambazo nilipendekeza lakini  haikuwa lazima sana lakini  kwa  wagonjwa wengi ambao nimekutana nao  njia  hio imeonyesha mafanikio , njia ya pili  ni kuzipatanisha  nafsi zako  zote mbili  tofauti na kuzikataa na  njia hii ili kuweza kufanikiwa nilikuelezea kwamba  unatakiwa ujue  chanzo cha kila nafsi na pengine kujua  kumbukumbu za maisha ya nyuma ambazo umepoteza”Alielezea Dokta Shukuru kwa kirefu.

DID  ni kifupi  cha neno la Kingereza yaani Dissociative  identity Disorder ni ugonjwa  wa akili ambao  ulikuwa ukifahamika kwa jina la Multiple personality disorder , ugonjwa ambao unamfanya mtu kuwa na Utu wa aina mbili au nafsi mbili  ambapo  humvaa mtu kwa nyakati  tofauti  tofauti na kudhibiti tabia.

Yaani kwa mfano  unaweza ukajitambbua kama  John  na  watu  pia wakakutambua kama John  na tabia zako lakini muda mwingine unabadilika na kuwa  Ayubu  na tabia zako zinakuwa ni kama Ayubu bila ya kufanana kabisa na John.

Huo ndio ugonjwa ambao mrembo Regina   alikuwa nao , yaani  anatawaliwa na ugonjwa wa akili ambao unamfanya kuwa na  nafsi  mbili zenye tabia tofauti tofauti.

 Ni ugonjwa ambao huwapa changamoto  sana   madaktari kuutibu  lakini  unatibika kupitia njia za kiushauri zaidi.

“Kwahio  kulingana na  tatizo langu   na mipango ya familia  yangu , unanipa ushauri gani?”

“Njia ambayo ni rahisi zaidi ambayo tokea mwanzo nilisisitiza ni kuishirkisha familia yako juu ya tatizo uliokuwa nalo ,lakini sio wewe tu ambaye ulikataa juu ya hili lakini babu yako  pia  alikataa  swala ambalo  naelewa kulingana na haki za mgonjwa wangu, nasema hivi kwasababu  pengine   kama mama yako wa kambo  anajua  una tatizo la namna hii asingefanya  maamuzi ya kutaka kukutafutia  mume wa  kuolewa nae  kwani  haitokusaidia kupona tatizo lako , nikizingatia msingi wa matibabu  nikiri kwamba  familia yako maamuzi  ambayo imeamua  ni  hatari kwa maendeleo ya  shida yako, lakini naelewa pengine ni kutokana na kutokuwa na uelewa, pia najua  kwa upande wako unachukua tahadhari”

“Asante Dokta  kwa kuwa muwazi ,  ukweli tokea nafike hapa nishafanya maamuzi na nilitaka  kusikia maoni yako  juu ya hili”

“Ndio nipo  tayari kusikia maamuzi yako”

“Napanga  kuajiri mwanaume yoyote  aigize kuwa boyfriend  wangu  ili kuzuia mpango wa wazazi  wangu  zidi ya kampuni”Aliongea na kumfanya  Dokta  Shukuru kushangaa kidogo  lakini  alipotezea mshangao wake.

“Kuna haja ya kwenda mbali hivyo , Ms Regina  najua  unalichukulia  tatizo lako kwa ukubwa lakini ni tatizo la kawaida na  kwa muonekano wako  na mafanikio yako sidhani  kama kuna haja ya kuwa na mwanaume  wa maigizo , wapo wanaume wengi ambao wanaweza kukupenda na wewe  kuwapenda  ni swala  la kutoa  nafasi tu”

“Dokta  kwa  maelezo yako unahisi  ni rahisi kupata mtu kunipenda , ushasema  kwa muonekano wangu na mafanikio hivyo sidhani kuna  mwanaume ambaye  anaweza kunipenda kwa dhati tofauti  na kutanguliza nilichokuwa nacho ,  nimeona wakati nikiendelea kumtafauta huyo mwanaume  nitakaempenda na  ambaye atanipenda kwa dhati  nitafute mbadala maana mapenzi pia ni swala  la mchakato na kama  hili  swala likishindikana  nitaenda na  plan B  kupatanisha nafsi zangu”

“Unafikiri unaweza kupata mwanaume ambaye anaweza   kukubali kuajiriwa  kuigiza kuwa mchumba?”

“Naamini  nguvu ya pesa ndio itafanya kazi, itakuwa ni kama ajira tu  na ni swala ambalo  nataka kulifanya  ili kujipatia muda nikiendelea kufuatlia  namna ya kumaliza  tatizo langu , huenda pengine ni kapata mwanaume  ninaempenda na ikawa rahisi  tatizo langu kumalizika”Aliongea  na kumfanya  Dokra Shukuru kuwaza kwa muda.

“Nadhani  sio wazo baya kulingana na hali yako ,  umesema pengine unaweza kupata mwanaume unaempenda  wakati ukiwa na  mchumba wa maigizo , hoja yangu ni kwamba  pengine   mchumba wa maigizo  akawa ndio mtu uliepangiwa kuwa nae na mkapendana hivyo nipo tayari  pia kubeti , nilisha fikiria  kwa kina nitakuja kufanya chochote kwa ajili ya kuhakikisha hali ya mgonjwa wangu inaisha  , kwasasa tujaribu na hiki ulichoamua” Aliongea Dr Shukuru na kumfanya Regina   kutoa tabasamu.

Ugonjwa wa DID ulikuwa  mgumu kudili nao ndio maana inashauriwa na daktari kuwa flexible wakati  wa kushughulika na mgonjwa na hicho ndio ambacho alikifanya Dr Shukuru.

Dr Shukuru  Omari ni  daktari mbobezi ambaye amepitia  mafunzo  makubwa ya kudili na wagonjwa  wa  akili na haikuwa mara yake  ya kwanza kudili na mgonjwa mwenye nafsi mbili.

 

 

Previoua Next