Mkataba wa Mpenzi wa Kukodi.
“Kifungu cha kwanza cha mkataba wa kukodisha mpenzi ,Mhusika A ana haki ya kumtafuta mhusika B wakati wowote ndani ya masaa 24, Mhusika B ana wajibu wa kuhakikisha simu yake muda wote ipo wazi , pili muhusika B ana wajibu wa kushirikiana kikamilifu na maombi yote ya Mhusika A maadamu maombi hayo hayavunji sheria za nchi au mkataba , tatu Mguso wowote wa kimwili lazima uruhusiwe na Mhusika A kabla ya kufanyika… nne ,,, tano …”
Ndani ya chumba cha kifahari cha hoteli ya Dosam V alionekana mwanamke mrembo akiwa amekaa kwenye sofa upande wa dirishani . alikuwa mrembo mno na siku hio mavazi yake yalizidi kumfanya kuwa mrembo zaidi.
Alikuwa amevalia mwenyewe gauni la light blue huku akiwa nywele zake amezirudisha nyuma mara baada ya kutoa ile kofia ya Hat na mkononi alikuwa ameshikilia karatasi ya mkataba akimsomea Hamza.
Macho ya mwanamke huyo yalikuwa mazuri na angavu kama vile ni maji ya vuli , nyusi zilizopindwa , kope zake ndefu na midomo yake myekundu na minene vilimfanya kuvutia zaidi ,bila kusahau uumbwaji wa uso wake ulioendana na haiba yake , alikuwa kama vile ni mchoro wa sanaa uliotoka kwa mchoraji maridadi.
Hamza alikuwa ameketi mbele ya mwanamke huyo mrembo akimwangalia na kumsikiliza kwa umakini mkubwa.
Ki ufupi umakini wake haukuwa kwenye mkataba bali ulikuwa kwenye uzuri wa huyo mwanamke , kwake ni kama vile yupo ndotoni.
Kusomewa mkataba huo ilikuwa ikimaanisha alikuwa amepita kwenye usaili na sasa alikuwa akipewa mashari ya kuanza kazi.
Ukweli ni kwamba huyo mwanamke baada ya kumwangalia Hamza kwa sekunde kadhaa alionekana kuridhika nae na alienda moja kwa moja kwenye mkataba.
Upande wa Hamza kwa namna ambavyo alikuwa akitingisha kichwa kila mara baada ya mwanamke huyo alipokuwa akisoma ni kama vile aliogopa mwanamke huyo angebadilisha mawazo na kushindwa kusaini mkataba wa kazi.
Alijiambia ni kheri hata kuigiza kuwa mpezi tu wa kukodi na hio yenyewe ingetosha kumletea heshima.
“Sahihi ya mkataba kipengele A , Regina Wilson Dosam., kipengele B Hamza Mzee.. ni muda wa kusaini…”Aliongea mwanadada mrembo ambae anafahamika kwa jina la Regina na kuweka mkataba ule juu ya meza kwa ajili ya kusaini mara baada ya kusoma vipengele.
Regina alijikuta akivuta pumzi ya ahueni huku akimwangalia Hamza ambaye ndio amekutana nae kwa mara ya kwanza siku hio na alionekana kuridhika nae.
Alikuwa na uhakika kuhusu macho yake kulingana na muonekano wa Hamza na taarifa ambazo amempatia alikuwa na uwezo wa kuona kwamba alikuwa ni mtu muamiifu na muwazi.
Zaidi ya yote mrembo Regina aliona muonekano wa Hamza sio mbaya sana , ijapokuwa mavazi yake hayajamkaa vizuri lakini kama atamvalisha na kupata matunzo kidogo atafanikisha kuwadanganya watu kuwa ni mpenzi wake halisi kumbe ni feki.
Wasiwasi wake kwa muda huo ni ugonjwa wake tu, lakini kulingana na vipengele vya mkataba huo aliamini Hamza kila atakachokiona kwake kwa bahati mbaya basi itakuwa ni siri.
“The contract is roughly like this , first I’ll rent it for three months, then we‘ll see how it goes , do you have any objections?”Aliongea kwa kingereza kitamu makusudi kabisa akitaka kumpima Hamza uwezo wake wa kuongea kingereza.
Hamza alitoa tabasamu , kadri mrembo huyo anavyoongea ndio alivyokuwa akipata hali ya kujiamini na kumzoea na palepale alishika mkataba ule na kupitia kwa haraka haraka kabla ya kusaini.
“Miss Regina , I have a few questions that I need to confirm first”Aliongea akimaanisha kwamba anayo maswali kadhaa ya kuuliza kujihakikishia kwanza.
“Unaweza kuuliza?”
“Vipi kama itatokea nipo kwenye kipindi na siwezi kuja kwako mara baada ya kunipigia simu na nikapoteza muda?”
“Upo makini , inaonekana pia ni mwanafunzi mtiifu”
“Nishatoa ada hivyo nataka kuitumia vizuri”Aliongea na kumfanya Regina kuonyesha ishara ya kuridhika, hakujali kuhusu Hamza bado kuendelea na masomo , alichojali alionekana kuwa siriasi, na yeye alikuwa akitafuta mtu siriasi.
“Usijali siwezi kukusumbua wakati wa masomo yako , utanipa ratiba ya vipindi na kama kuna dharula utaniambia”
“Hapo vizuri , naona na wewe pia ni mtu muwajibikaji” Aliongea huku akiwa na tabasamu na muda uleule simu yake ilianza kuita na kujikuta akilaani kimoyo moyo , Regina s alimpa ishara ya kuipokea na Hamza mara baada ya kuangalia jina la mtu anaepiga ni Iryn.
“Huyu ni mwanafunzi wangu namfundisha masomo ya jioni twisheni , yupo form six anapiga maana jioni ya leo nina kipindi nae”aliongea Hamza.
“Hakuna shida unaweza kupokea na kumsikiliza sina haraka” Aliongea Regina na palepale Hamza alipokea.
“Ticha nadhani hujasahau leo tuna kipindi?”
“Najua lakini si niliwasiliana na mama yako na kumwambia tutaanza wiki ijayo?, kwasasa nina kazi nyingine hivyo nitakuwa bize tutaanza wiki inayokuja kulingana na nilivyokubaliana na mzazi wako”
“Oh! , Mama hajaniambia kuhusu hili”Sauti nzuri ya kike ilisikika.
“Unaweza kumuuliza tu “
“Basi sawa nadhani tutaonana wiki ijayo”Aliongea huyo mwanamke na palepale simu ilikatwa na kwa sauti ya Iryn alijua tu lazima amekasirika.
Ukweli ni kwamba Hamza katika kujitafutia kipato alikuwa akifanya kazi za aina mbalimbali ,miezi kadhaa iliopita wakati akifanya kazi ya kibarua chini ya kampuni ya mazingira ya Tata ndio aliweza kukutana na Mama Iryn nyumbani kwake kwa mara ya kwanza na hapo ndio mwanamama huyo alimfahamu Hamza ni mwanachuo kutoka FEMU ,
Sasa katika kuongea ndio mama huyo alisema ana binti yake kutoka shule ya sekondari ya Alpha na anachukua masomo ya EGM na alimuomba kama ingewezekana kwa Hamza kumfundisha twisheni kwa malipo na Hamza alikuwa na uhitaji wa pesa hivyo hakukataa.
Tatizo lilianza mara baada ya kufanya vipindi kadhaa na Iryn alianza kumtega Hamza na kumtaka kimapenzi,, Hamza alikuwa hana mwanamke ndio lakini hakuwa tayari kutoka na mwanafunzi na hio yote ni kutokana na mama yake Iryn kuweka imani kubwa kwake hivyo kutokana na dalili hizo Hamza alikuwa akimkwepa Iryn kiaina.
Ki ufupi Hamza ni mtu wa harakati na aliishi kwa kuchakalika , hakuchagua kazi ili mradi ilikuwa na pesa, lakini kwa Iryn ilikuwa ngumu licha ya kazi hio ilikuwa na malipo mazuri kutokana na mama yake Iryn kutokea kumpenda Hamza.
Kitu kingine sio kwamba Hamza alishindwa kumuonya lakini ukweli ni kwamba Iryn alikuwa binti mrembo sana ambaye kwa mwanaume rijali yoyote yule ni rahisi kuingia kwenye mtego wake ndio maana alikuwa akiona ugumu.
“Samahani Miss Regina kwa kukuchelewesha wakati naongea na simu”Aliijibu Hamza.
“Hakuna shida , kama huna pingamizi lolote unaweza kusaini mkataba”Aliongea.
Ijapokuwa sauti yake ilikuwa ya kirafiki lakini alionekana kuwa kauzu mno na hata Hamza mwenyewe alijiambia hajawahi kuona mwanamke Kauzu kama huyo halafu mrembo , lakini alichopenda ni kwamba hakuona aina yoyote ya Dharau,
Hamza alitia sahihi yake kama vile ana saini mkataba wa mabilioni kwa niaba ya nchi , sahihi yake ilikuwa nzuri mno na kumfanya hata Regina kushangaa kidogo, ilionekana Hamza alikuwa na mwandiko mzuri sana kwa kuangalia sahihi yake tu.
Baada ya kutia sahihi yake na Reginai kutia sahihi yake palepale alifungua mkoba wake na kutoa bahasha na kumpatia.
“Haya ni malipo ya utangulizi kama mkataba unavyosema ni milioni tano , unaweza kuhesabu kujihakikishia, lakini hela zipo katika mfumo wa dollar hivyo utazibadili”Aliongea na Hamza alipokea ile bahasha .
“Haina haja ya kuhesabu uzito wa bill ya dollar mia ni sawa na gramu 1.51 na humu ndani kuna dollar elfu mbili hivyo uzito wake ni sawa na gramu 30.2, hivyo kwa kuzingatia uzito huu basi hesabu zipo sawa”
Reginai macho yake mazuri yalichanua , hakuamini kama mtu anaweza kuhesabu hela kwa kuzingatia uzito wake tu , moja kwa moja ilimwambia mtu ambaye yupo mbele yake anapenda sana hela na hilo lilimuongezea pointi.
Upande wa Hamza alifanya makusudi tokea jana yake alikuwa akipanga namna ya kukubalika na kushinda usaili na alikuwa na mbinu nyingi lakini hata hivyo mbinu zake hakuwa ameziandaa na kutokana na kuamini kichwa chake kilivyo chepesi basi angetunga hapo hapo.
Sasa mara baada ya kupewa kibunda alitaka kumhakikishia Regina kwamba yeye anajali sana pesa kuliko kitu chochote kile.
Unajua bwana watu wanaopenda hela ni rahisi kuwakontrol na kuwaambia hiki na kile na wakatii kuliko watu ambao hawapendi sana hela mara nyingi wanakuwa sio watiifu hio ni kanuni ambayo Hamza aliizingatia.
Regina aliona na hicho ni kigezo pia ambacho alikuwa akitafuta , alitaka pia mtu ambaye anakwenda kuigiza kama mpenzi wake awe anapenda pesa ili iwe rahisi kumuendesha.
Regina mara baada ya kuzuia mshangao wake aliingiza mkono wake kwenye mkoba na kisha akaibuka na bahasha nyingine na kumpatia Hamza.
“Katika hii nyaraka kuna taarifa ambazo zinahusiana kuhusu wewe na mimi namna ambavyo tumekutana na tulivyoanza kuwa pamoja , nenda nayo na ukaisome uilewe lakini hakikisha hakuna mtu ambaye ataiona.”
Hamza hakuamini mwanamke huyo kuwa profesheno kwenye kazi yake namna hio na alitoa tabasamu na kuchukua ile bahasha.
“Nitaisoma kwa umakini nikisharudi”
“Kesho asubuhi saa nne kamili tukutane Dosam Tower kwenye parking B2, hakikisha hauchelewi”Baada ya kuongea kauli hio alisimama akitaka kuondoka.
“Ms Regina usiwe na wasiwasi , mimi najali sana muda”
“That is for the best”Aliongea na Hamza aliangalia glasi ya juisi ambayo ilikuwa mbele ya mwanamke huyo , alichukua ya kwake kwanza na kuinywa na kisha akamwangalia.
“Ms Regina bado umebakisha nusu ya juisi yako”
“Siitaki tena”Aliongea.
“Utakuwa ni uharibifu sana kwa alieitengeneza”Aliongea Hamza na palepale aliinua ile glasi na kisha akainywa yote kwa mkupuo mmoja.
Mrembo Regina alitaka kumzuia lakini aliona aibu kwa kitendo chake na mawazo yake ya kijinga yalimwambia anachokifanya Hamza ni kubusiana nae kwa njia isio ya moja kwa moja.
Hamza na Regina walitoka pamoja na sasa rasmi Hamza alikuwa ni mpenzi feki wa mrembo Regina , Hamza ijapokuwa alikuwa hapo kwa kazi lakini alijiambia atahakikisha huyo mrembo anampenda mwenyewe.
Baada ya kutoka nje ya mlango alimwambia mlinzi wake kwenda nyumbani na kuanzia hapo ataendesha gari yake mwenyewe , mwanadada yule mlinzi alitaka kugoma lakini alikubali na aliishia kumwangalia bosi wake na Hamza wakitokomea kwenye lift akiwa katika hali ya wasiwasi.
Haikueleweka Prisila alikuwa ameenda wapi na Hamza alitamani kumuona mara ya mwisho , kwake ni kama alikuwa ameokota embe kwenye mnazi.
Baada ya kutoka kwenye lift watu waliokuwa eneo la mapokezi walikuwa wakimwangalia mrembo Regina kwa macho ya mshangao na matamanio lakini alionyesha kutojali na moja kwa moja alitoka nje na kwenda upande wa magari yalipoegeshwa na kusogelea gari moja ya kifaharai aina ya Maserati Gran Gabrio.
Uzuri wa lile gari ulimfanya Hamza kumwangalia kwa macho yaliokuwa na matamanio ilikuwa ni gari ambayo inaendana na muonekano wake,
“Hivi ulisema upo mwaka wa ingapi chuo?”
“Nipo mwaka wa tatu , kuna tatizo?”Aliuliza Hamza kiwasiwasi.
“Hakuna”
Aliongea na palepale kimadaha aliingia upande wa mbele ya gari na kuliwasha.
Regina alijihisi kujiamini na kuona sio mbaya mwanafunzi wa digrii ya uchumi mwaka wa tatu anamfaa sana.
Comments