Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

CHANGE

Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI NA MOJA

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Namouih alianza kupumua kwa kasi kiasi, huku mapigo yake ya moyo yakiongeza midundo ndani ya kifua chake. Draxton yeye akaifikia ndoo yake na kuendelea kufua, asitake kumtazama tena Namouih ili aondoke tu yeye mwenyewe, lakini mwanamke huyu ndiyo akawa kama amegundishwa hapo hapo aliposimama baada ya kuona alichokiona. Akawa anamwangalia Draxton kimaswali mno, asielewe ni nini kilichokuwa kinaendelea. Alipotoka tu kufikiri kwamba labda alimhukumu vibaya, jambo hilo lingine likazuka.

Draxton alikuwa ametambua kwamba bado Namouih aliendelea kusimama hapo, hivyo akaamua tu asimame vizuri ili amwambie aondoke kwa ustaarabu. Lakini alipomwangalia usoni, akakuta Namouih anamtazama kwa njia fulani mpya, siyo udadisi tena, bali kama hofu. Akabaki tu kumtazama na yeye, hivyo Namouih akaangalia chini kidogo na kugeuka ili aanze kuondoka. Akafikia mwisho wa ukuta wa nyumba kutokea hapo na kugeuka tena kumwangalia Draxton, naye akakuta mwanaume huyo anamwangalia kwa yale macho yake makali fulani hivi, kama tu siku ya juzi walipokutana mahakamani kwa mara ya kwanza. Namouih akaacha kumwangalia na kuondoka hapo upesi sana, mpaka akalifikia gari lake na kukaa ndani; akitulia kwanza ili kurudia jambo lile vizuri kwenye akili yake.

Haingewezekana kufikiri labda macho yake yaliona mambo vibaya. Alichokiona kilikuwa sahihi kabisa kupatana na kile alichokiona usiku ule. Ile tattoo, jinsi maneno yale yalivyokuwa yamechorwa kwenye mwili wa yule "mtu" waliyemgonga, ndiyo namna hiyo hiyo yalivyokuwa yamechorwa mgongoni kwa Draxton. Lakini alikumbuka mambo ya usiku ule vizuri sana ambayo yalimchanganya. Yule mtu waliyemwona, alikuwa na ngozi nyeupe kama mzungu, lakini Draxton hakuwa mweupe namna hiyo, yaani hata chembe ya weupe aliokuwa nao Namouih, Draxton hakuwa ameifikia. Pia yule mtu alikuwa na nywele nyingi na nyeupe sana kichwani ilhali Draxton alikuwa na nywele fupi sana zilizonyolewa kwa ukawaida kichwa chake chote, na nyeusi.

Ikiwa hakuwa yule waliyemgonga siku ile, basi inawezekana walikuwa wawili, au walikuwa na kundi la watu wa namna hiyo. Alihofia sana kuhusu usalama wa Blandina hata zaidi wakati huu, lakini angemwambia kwa njia gani suala hili bila kumkwaza, hasa baada ya yeye kuwa amemwahidi kwamba angeacha kumhukumu vibaya Draxton? Alichokuwa amekosa tu ni ushahidi wa uhakika, lakini alijua isingekuwa ngumu kwa Blandina kumwamini endapo kama angeupata, kwa sababu rafiki yake huyo alikuwepo pia usiku ule. Namouih alichanganyikiwa sana. Akabaki hapo hapo kwenye gari lake kwa dakika zaidi ya 20 akiwaza vitu vingi, kisha hatimaye akaondoka tu ili kuelekea nyumbani.


★★★


"Aaaaaah!"

Hiyo ilikuwa ni sauti ya juu sana ya kelele kutoka kwa Namouih. Alikuwa ameamka kutoka usingizini, naye akawa ameketi kitandani huku akipumua kwa presha sana. Mwili wake ukashtuka kiasi baada ya kuhisi mguso begani, naye akageuka na kukuta ni mume wake ndiye aliyemshika hivyo.

"Namouih... nini?"

Efraim Donald akauliza hivyo huku akionyesha uso wenye kujali sana. Namouih akaanza kuangalia mazingira waliyokuwepo. Ndiyo, walikuwa kwenye chumba chao. Ilikuwa asubuhi sasa. Siku hii ilikuwa mpya, jana ilipita. Akafumba macho na kuinamisha uso wake kwa mfadhaiko kiasi, naye Efraim akamshika mabega yake yote.

"Ni nini Namouih? Ndoto mbaya?* akamuuliza.

Namouih akatikisa kichwa kukubali.

"Umeota nini?" Efraim Donald akauliza.

"Hhh... ni ndoto mbaya sana, inatisha, sitaki hata kuizungumzia," Namouih akasema.

Efraim Donald akamwambia pole, kisha akachukua simu yake iliyokuwa pembeni.

"Saa ngapi?" Namouih akauliza.

"Saa moja," Efraim akasema.

"Nisamehe kwa kukuamsha," Namouih akamwambia.

"Usiwaze. Rudi tu kulala..."

"Sidhani kama nitaweza. We' ndiyo urudi kulala, me ngoja nikajimwagie tu..."

"Unaelekea ofisini baada ya hapo?"

"Hamna... nitatulia tu kwanza... nicheze na Angelo kidogo ndiyo... niende na msibani..."

"Ni lazima sana uende huko msibani? Si umeshawapa salamu za rambirambi jana?"

"Ndiyo, ila nitaenda tu kwa muda mfupi... nilikuwa namsimamia yule msichana unajua hilo..."

"Haya, sawa. Pole ya ndoto tena," Efraim Donald akamwambia huku akijilaza upande mwingine.

Namouih akamwangalia kwa kitambo kifupi, kisha akanyanyuka na kuelekea bafuni. Ndoto mbaya aliyokuwa ameona usingizini ilikuwa imemkosesha amani kabisa, na fikira ya kwanza kwake ikawa kwamba huenda jambo hilo lilihusiana moja kwa moja na mambo aliyotoka kuona jana. Kwa nini? Alikumbuka kabisa namna ambavyo aliota ndoto mbaya sana usiku ule alipomwona yule kiumbe mwenye tattoo aliyokuja kuiona tena jana kwa Draxton, halafu na leo akawa ameota ndoto mbaya. Hapo kulikuwa na uhusiano kabisa, naye akawa ameingia bafuni na kujimwagia maji huku akitafakari nini afanye ili kufichua kilichofichika juu ya Draxton.

★★

Muda mfupi baadaye, Namouih akawa ameondoka nyumbani na kuelekea ofisini kwake, akiwa na mwonekano nadhifu wa kiofisi uliompendezea sana. Alimkuta Blandina huko tayari, nao wakaanza kushughulika na mambo fulani ya kikazi. Namouih alikuwa amemuuliza Blandina kama jana alikutana tena na Draxton baada ya wawili hawa kuachana, akiwa anataka kujua kama mwanaume yule alimwambia kuhusu yeye kwenda pale alipoishi. Lakini Blandina akasema tu kwamba ndiyo, Draxton alikutana naye mida ya saa moja, nao wakaenda sehemu nzuri sana kupata chakula, kisha wakaenda na kwake kutulia kidogo kabla ya jamaa kuondoka kurudi kule alikoishi.

Kwa hiyo Blandina kutosema lolote kuhusiana na ishu hiyo kukamfanya Namouih atambue kuwa mwanaume yule hakumwambia lolote, hivyo naye akaona akae kimya tu. Rafiki yake huyo akasema kwamba baadaye wakienda msibani, yeye alikuwa anatoka pamoja na Draxton kuelekea huko kisha ndiyo mambo yao mengine yangefuata. Blandina alionekana kufurahia sana uhusiano wake na mwanaume huyo mpaka Namouih akashindwa kujua aanzie wapi kumwambia kuhusu mambo aliyofikiria. Akaona tu aache kwanza, naye akaamua kumtafuta yule kijana kwa jina la Japheth Warioba ili amuulize mambo machache kuhusiana na kile ambacho Draxton alimwambia jana.

Baada ya kuongea naye, kweli Japheth alimweleza kwamba Agnes alimtafuta muda fulani kabla ya kuja kusikia kuhusu taarifa ya kifo chake. Akamwambia kuwa mwanzoni hakutaka kumjibu baada ya binti huyo kutoka kudanganya kuhusu yeye kumbaka, lakini akapokea simu yake tu ili asikie alitaka kusema nini, na ndipo akaanza kumsikia akiongea kwa hofu sana na kuomba msaada wake. Namouih akamuuliza ni nini ambacho Agnes alikuwa anaombea msaada, lakini Japheth akasema hakujua kwa sababu simu ilikata ghafla, na ndiyo yeye akampigia mwanasheria Draxton ili kumwambia hayo kabla ya maafa yale kumkuta binti.

Namouih akamshukuru na kumwambia yeye pia ajitahidi kuwa mwangalifu, na kama kuna jambo lolote ambalo lingezuka basi amtaarifu endapo kama msaada wake ungehitajika, naye Japheth akakubali na kuagana naye. Ingawa hii ilikuwa nija moja ya kuthibitisha kwamba Draxton hakuhusika na kifo cha Agnes, bado haikuelezea uajabu wa hali alizokuwa nazo kabisa. Mambo kama ile tattoo, mara yeye kutoweza kufanya mapenzi, jinsi alivyokuwa akimtazama kwa macho fulani makali, na namna alivyoongea kwa upole ambao Namouih aliuona kuwa wa kinafiki ni vitu ambavyo viliisumbua sana akili yake.

Ni wakati alipokuwa akiendelea kuwaza na kuwazua ofisini kwake pale Blandina alipoingia tena na kusema ndiyo alitaka kuondoka kwa sababu Draxton alikuwa anamsubiri nje. Namouih alibaki kumtazama tu rafiki yake kama vile hajasikia kilichosemwa, naye Blandina akamshtua kidogo na kurudia maneno yake. Namouih alikuwa amemsikia, ila tu kuna wazo lililokuwa limemwingia wakati huo baada ya kujua Draxton yupo huko nje, naye akamkubalia Blandina na kumwambia kwamba wenyewe watangulie, naye angeenda muda si mrefu. Kwa hiyo Blandina akamuaga na kuondoka hapo.

★★

Hazikupita dakika nyingi, Namouih akachukua mkoba wake pia na kuondoka kutoka kwenye kampuni yao. Lengo lake lilikuwa Blandina na Draxton wakishaondoka tu, na yeye pia atoke, kwa sababu alitaka kwenda pale mwanaume huyo alipoishi. Kwa nini? Kama msemo mmoja wa waswahili unavyokwenda, ikiwa haujui mambo mengi kumhusu mtu, ongea na majirani zake, watakwambia. Mwanamke alikuwa ameamua kwenda huko ili aweze kupata chochote kile chenye nuksi ambacho bila shaka hata majirani wa mwanaume huyo pale alipoishi wangekuwa wamejionea.

Akafika na kugonga geti la nyumba hiyo, nalo likafunguliwa, zamu hii ikiwa ni mwanamke mwingine ambaye bila shaka aliishi hapo. Namouih akamsalimu na kujitambulisha, kisha akaomba kuingia ndani na kumwambia kwamba alihitaji kuzungumza pamoja naye na wakubwa wengine waliokuwepo. Mwanamke huyu akamkaribisha mpaka ndani ya chumba ambacho yeye na wengine walikaa, kisha akaja mwanamke mwingine pia pamoja na yule msichana wa rika kama la Agnes. Ni hawa tu ndiyo waliokuwepo kwa wakati huu, nao wakajitambulisha kwa majina ya Salhat, Rehema, na Kuluthum.

"Asanteni sana, mimi naitwa Namouih. Najua hamjatarajia ujio wangu hapa, na sitachukua muda wenu mwingi sana," Namouih akasema.

Wote wakamwambia haikuwa na shida, nao wakaweka umakini wao ili kumsikiliza.

"Sawa. Mimi ni mwanasheria, na ninafanya kazi sambamba na huyu kijana anayeishi hapa... Draxton. Hatujajuana kwa muda mrefu hivyo nilikuwa nahitaji kujua mambo machache tu kumhusu ili kufanya naye kazi vizuri zaidi. Sijui ameishi hapa kwa muda gani?" Namouih akauliza.

"Mh... yaani me ndo' leo nalisikia jina lake kwako. Huwa sijui hata anaitwa nani... ila ana muda sana hapa, sisi tumehamia tumemkuta..." Rehema akasema.

"Kumbe?" Namouih akauliza.

"Ndiyo. Huwa hata hatusemeshi, yuko kivyake mno yaani, zaidi ya salamu hakuna kingine," akasema Rehema.

"Kumbe ni mwanasheria?" Kuluthum akauliza.

"Ndiyo..." Namouih akajibu.

"Hmm... yaani dada, me mpaka nikafikiriaga labda ana matatizo ya akili, ila kuona mpaka ana gari sisi tukajua lazima awe anafanya kazi nzuri, au labda tapeli," Salhat akasema na kufanya wenzake wacheke kidogo.

"Kwa hiyo hajihusishi na nyie hata kidogo? Hata kwenye maongezi na waume zenu, au labda mwenye nyumba..." Namouih akauliza.

"Mwenye nyumba anampendaga kweli, anasema huyu kijana ni mpole, mstaarabu, na amekaa hapa kwake kwa muda mrefu bila kuleta zengwe kabisa..." akasema Rehema.

"Haletagi hata marafiki hapa..." Kuluthum akaongea.

"Sijawahi hata kuona analeta demu au mshakji yeyote," akasema Rehema.

"Ila kuna kale kadada nimeona ameanza kukaleta hapa ile juzi..." Salhat akasema.

"Kakoje?" Rehema akauliza.

"Kapo tu hivi... Kuluthum si ulikaona?" Salhat akasema.

"Ee nilikaona. Kana shepu-shepu hivi na tako kubwa, alikaleta juzi juzi tu hapo... yaani ndiyo mara ya kwanza kumwona analeta mtu hapa..." akasema Kuluthum.

Namouih akawa amebaki kimya, akielewa kwamba waliyemzungumzia ni Blandina.

"Mambo ya sijui kuongea na waume zetu hanaga. Akiambiwa kuna jambo linahitajika, huwa anatenda tu upesi bila shida yoyote. Sema hana urafiki yaani. Huko kazini kwenu huwa ana marafiki hata?" Salhat akamuuliza Namouih.

"Hapana. Ni mtu fulani ambaye... amejichimbia sana kama anaficha kitu fulani hivi..." Namouih akasema.

Wanawake hao wakaanza kukubaliana na kauli hiyo, wakisema ni kweli kabisa.

"Eee... si mliniona ile juzi nipolikuja hapa?" Namouih akauliza.

"Ndiyo..." Salhat akajibu.

"Yeah, yaani nilikuja kumuuliza jambo fulani muhimu sana lakini akawa ananipa majibu kwa njia kama vile yeye mtakatifu hivi... halafu anavyoangalia machoni yaani mpaka unaogopa..." Namouih akasema na kuwafanya wacheke.

"Sasa huwa anafanyaje hizo kazi? Watu huwa wanamwelewa?" akauliza Kuluthum.

"Kikazi yuko vizuri sana, ila ndiyo kama hivyo yaani... haeleweki. Kwa hiyo ni kawaida yake kuja hapa kila siku, kazini, anatoka, kazini, anarudi, hivyo yaani?" Namouih akauliza.

Salhat akasema, "Kama hivyo dada, kabisa. Sema wakati mwingine huwa harudi kulala kwake. Anaweza kupitisha usiku mmoja au siku chache hajaja... inakuwa labda yuko safarini sijui...."

Wanawake hao wakaendelea kuzungumza mambo mengi, na Namouih akawa amepata mwanga kiasi kuhusiana na tabia za Draxton. Ikawa wazi kwake kuwa mwanaume yule aliishi maisha ya maigizo, yaani alijifanya mtu mwema, wa kivyake, na asiye na makuu ili kuficha maovu aliyokuwa anafanya. Alikuwa anaamini kabisa moyoni mwake kwamba mwanaume yule alikuwa mwovu, na kwa njia moja ama nyingine angemfunua mbele ya Blandina.

Baada ya kuwa amemaliza maongezi hayo na mashoga zake wapya, akawaaga na kuondoka hapo hatimaye. Safari yake ilikuwa kuelekea kule msibani ambako mwanaume huyo angekuwepo pia, naye akajiweka sawa kiakili zaidi ili aje kufanya jambo ambalo lingemlazimu tu Draxton afichuke kutoka kwenye kichaka cha maovu aliyokuwa akitenda.


★★★★


Ilipita wiki nzima kabisa baada ya matukio hayo yote bila ya Namouih kuwa amepata uthibitisho mzuri wa matendo ya Draxton yaliyofichika. Alijitahidi sana kwa kila nafasi aliyopata kuchunguza mienendo ya yule kaka, lakini ikawa kama kazi bure. Upande wa Felix wa upelelezi haukuwa umepata matokeo yoyote mazuri katika uchunguzi wa kifo cha Agnes, na ikawa kama vile suala hilo limeacha kukaziwa sana fikira ingawa lilikuwa jambo zito mno. Ni kutokana tu na matukio kuwa mengi sehemu mbalimbali za maisha ya watu, lakini la Agnes angalau lilizunguka sana mpaka kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa hiyo wakati huu Namouih alikuwa akiendelea na masuala ya kazi, lakini bado hakuwa amesahau kuhusu utata wa tattoo ile mgongoni kwa Draxton, ikiwa ndiyo moja kati ya manbo makuu yaliyomshawishi kuamini kuwa mwanaume yule si mtu mzuri. Na tokea siku ile alipoota ndoto mbaya sana baada ya kuiona tattoo ile, hakuwa amesumbuliwa na ndoto nyingine mbaya tena. Ikiwa ni siku ya ijumaa sasa, alikuwa ofisini kwake tu ametulia, naye akawa anajibu simu za "wateja" wao ambao walikuwa wanampigia simu kumjulisha mambo kadha wa kadha au kutoa shukrani kwake kwa msaada wake katika kesi zao. Ndipo Blandina akaingia ofisini hapo na kukaa kwenye sehemu iliyokuwa na sofa, akimwangalia Namouih kwa njia fulani ya kuudhika-kudeka.

Namouih akatabasamu na kumalizia maongezi yake kwenye simu, kisha akanyanyuka kutoka kwenye kiti chake na kwenda kukaa na rafiki yake. "Vipi na wewe, mbona umeweka sura utadhani mtoto aliyenyimwa ubwabwa?" akamuuliza kiutani.

"Si napendezea lakini?" Blandina akauliza kiutani.

"Yeah, ni mashavu yako tu ndiyo yanakuwa yanaonekana kama umeyajazia vyura," Namouih akasema.

Blandina akacheka kidogo, kisha akashusha pumzi na kusema, "Vitu vingi."

"Nini, wimbo wa Young Lunya au?"

"Ahahahaa... acha zako bwana..."

"Kama sikosei shida iliyopo inaanziwa na herufi D..."

Blandina akamwangalia na kutikisa kichwa kukubali.

"Mhmhm... nini kimetokea sa'hivi?"

"Siyo jambo kubwa wala...."

"We' niambie tu. Sita-judge," Namouih akasema kwa ustaarabu.

"Okay. Mambo yamekuwa yanaenda fresh sana, Drax ananitendea vizuri mno, every time tukiwa pamoja... ni raha," akasema Blandina.

"Naona hadi sa'hivi ameshakuwa 'Drax,'" Namouih akasema kiutani.

"Ahah... yeah. Ila hiyo jana tena, mambo yamevurugika kidogo..."

Namouih akamshika kiganjani na kuuliza, "What happened?"

"Mara kwa mara nilikuwa namkumbusha kwenda kumwona daktari kuhusu lile suala, lakini kila mara ambayo nililigusia angekwepa au kusema tungetafuta wakati mwingine. Sasa jana usiku nilikuwa kwake, na tulikuwa tumepanga nilale pale. Katika michezo yetu na utani na nini, hamu ikawa imenizidia, nikaanza kumbusu... na kumshika. Mwanzoni alijaribu kunikumbusha kwamba hangeweza kuendelea na jambo hilo, lakini nikaona nijaribu kulazimisha, kistaarabu tu... ila Draxton akaanza tena kuchemka na kunisukuma kwa nguvu..." Blandina akaeleza.

"Wewe! Haukuumia?" Namouih akauliza kwa mshangao kiasi.

"Hapana tulikuwa kitandani... alinisukumia tu pembeni. Nilishtuka sana yaani," Blandina akasema.

"Nini kikaendelea?"

"Akaanza kuniomba samahani akidhani nimeumia sana... na bado alikuwa anaonekana kuumwa. Ikanibidi nimwambie kwa ukali kabisa ni lazima twende kuonana na daktari kwa sababu hiyo haikuonekana kuwa shida ndogo... lakini ndiyo akasema hangeweza kwenda. Nilipomuuliza kwa nini, hakunijibu, ila akasema tu kuwa jambo hilo halikuwa ndani ya uwezo wake... na eti kama Blandina nahisi kutoweza kuendelea naye, basi tungepaswa tu kukomesha mapenzi yetu...."

"Ah-ah!" Namouih akashangaa.

"Yaani Nam, sijui nakosea wapi. Atakuwa anatafuta kigezo tu cha kutaka tuachane... yaani... ah..." Blandina akaongea kwa mfadhaiko.

Namouih akatikisa kichwa kwa kumwonea huruma rafiki yake. Hilo lilikuwa jambo zito, kwa sababu alielewa namna ambavyo Blandina alimpenda yule kijana. Hakutaka kumwona rafiki yake akiendelea kuugua moyoni namna hii juu ya mtu aliyeonekana kutojali hisia zake kwa asilimia zote, na ingawa ilikuwa inaonekana ni kama upuuzi wa Blandina kuendelea kulazimisha mapenzi kwa jamaa, bado Namouih alimwona Draxton kuwa ndiyo mbaya.

Akamuuliza hivi, "Blandina... baada ya kitendo hicho... wewe unataka kuachana na huyo mwanaume?"

Blandina akatikisa kichwa kukanusha na kusema, "Bado nampenda mno kuwaza masuala ya kuachana Namouih. Hajanifanya chochote lakini nampenda sana, hajui tu. Ni kwamba... nakuwa nataka kumwelewa, lakini yeye... ni kama ananisukuma mbali inapokuja kwenye suala hilo, ila bado hisia zangu kwake zina nguvu nyingi sana..."

"Kwa hiyo una mpango gani?" Namouih akauliza kwa upole.

"Nimeamua kumwacha tu mpaka akinitafuta yeye mwenyewe. Leo niliamkia kwake nikakuta ameshaondoka, na hatujatumiana hata jumbe za salamu...." Blandina akasema.

"Oh, kwa hiyo ulilala kwake, ukaamka asubuhi ukakuta hayupo, halafu hajasema lolote mpaka sasa hivi?" Namouih akauliza.

"Aina hiyo," Blandina akasema.

Namouih akatikisa kichwa kwa kusikitika, kisha akasema, "Pole Blandina."

"Mhm... asante. Hhaaa.... angalau nimelitoa jambo hilo kifuani, ndiyo maana nilikuja kuongea nawe, nashukuru kwa kunisikiliza," Blandina akamwambia.

Namouih akamwambia, "Usijali, unajua niko hapa kwa ajili yako. Ukihitaji msaada kwa lolote, we' niambie tu, sawa? Ninataka sana kukusaidia darling."

"Asante love. Asante," Blandina akasema na kukumbatiana naye kwa kuhisi faraja.

Basi, baada ya hapo Blandina akamwacha ili akashughulikie masuala mengine ya kazi, na Namouih akabaki kwenye sofa akimtafakari rafiki yake. Jitihada yoyote aliyoweka katika kumchunguza Draxton haikuwa imefanikiwa, na bado alikuwa anahofia kwamba huenda siku moja mwanaume yule angekuja kumuumiza vibaya sana rafiki yake, lakini ni kama Blandina alikuwa amepofushwa na upendo aliokuwa nao kumwelekea kuona hilo.

Kwa hiyo sasa akawa ameamua jambo moja tu; kuupata ukweli kutoka kwa Draxton kwa njia ya lazima. Yaani angemfata na kutumia njia fulani ambayo ingemlazimu mwanaume yule aseme kila kitu yeye mwenyewe. Alikuwa ameshahisi kuchoshwa sana na jinsi ambavyo kila mara jina la mwanaume yule lingetajwa ingempa hisia mbaya, na sasa alikuwa ameazimia kwenda kukomesha hilo. Akanyanyuka na kuzifunga kazi zake zote, kisha akabeba mkoba wake na kuondoka kwenye jengo hilo la ofisi yake.

★★

Namouih alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwake. Esma hakuwa ametarajia rejeo hilo la mapema kutoka kwa Namouih, naye akawa anamuuliza ikiwa alikuwa anaumwa. Namouih akakanusha na kusema hakuwa amerudi ili kukaa, alitaka kutoka tena, ila kuna kitu fulani alikuwa amepitia hapo nyumbani. Akaelekea mpaka chumbani kwake, naye akaenda kabatini na kuifungua. Akachuchumaa na kuingiza mkono wake chini kabisa, akiusukumia ndani zaidi upande wa nyuma ili kutoa kitu fulani alichokuwa anatafuta, naye akautoa baada ya kukipata, na sasa akawa ameishikilia bastola ndogo kwenye kiganja chake huku akiitazama kwa umakini.

Huu ndiyo uliokuwa mpango wake. Alitaka kuona mwanaume yule angetenda vipi pale ambapo angefatwa na kuulizwa kuhusu mambo yake ya siri, yaliyokuwa ya ajabu pia, na kama angeleta fujo, basi Namouih angehakikisha anamtandika hata risasi ya mguuni. Lakini siyo kwamba alikuwa anamfata bila kuhakikisha anatoka na kitu chenye kuthibitisha kuwa mwanaume yule alitenda mabaya. Alikuwa amenunua kifaa kidogo cha mfumo wa kurekodi sauti, ili kama ni maongezi au jambo lolote ambalo lingetokea akiwa pamoja naye basi kungekuwa na kitu kilichobaki cha kuthibitishia, na angekificha kifaa hiki kwa umakini sana. Akaondoka hatimaye baada ya kuificha bastola nyuma ya kiuno chake.

Bastola hii ilikuwa ya Efraim Donald, ambaye aliitumia kipindi cha nyuma sana kwenye masuala ya uwindaji, na sasa ilikuwa imekaa tu ndani hapo kwa muda mrefu bila matumizi. Namouih alikuwa amefundishwa kutumia bastola na mume wake kwenye zile shule za mafunzo ya shabaha, hivyo alielewa vizuri kile alichokuwa anakwenda kufanya. Akaingia kwenye gari lake na kuanza kuelekea kule ambako Draxton aliishi. Hakujali endapo kama angekwenda huko na kukuta hayupo; angemsubiri tu. Yaani alikuwa ameazimia kabisa kwamba leo ingekuwa leo, na angekomesha mchezo wa mwanaume yule uliokuwa unamwathiri vibaya rafiki yake ingawa mwanaume mwenyewe alionekana kutojali hilo. Kujiingiza kwake sana kwenye suala hili kulionyesha namna gani alimpenda Blandina, na angehakikisha anafanikiwa katika jambo hili ili amsaidie rafiki yake.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, akawa anakaribia kuingia mitaa ya eneo aliloishi Draxton, lakini wakati akiwa barabarani bado akaona jambo fulani. Sehemu ya barabara iliyoingia upande huo kuelekea alikoishi jamaa, yaani barabara iliyoiacha lami kuu, aliweza kuliona gari aina ya Forester nyeusi likitokea huko, na kwa haraka akawa ametambua ni gari la Draxton. Ikambidi apunguze mwendo ili kuona lingeelekea wapi, nalo likaingia lami kuu na kuanza kuelekea upande mwingine wa barabara, yaani mbele ya Namouih. Mwanamke huyu akaanza kulifuatilia gari hilo taratibu, akihakikisha hajiweki sehemu za karibu ili mwanaume yule asije kutambua alikuwa na kupe kwenye mkia wake.

Kufatilia gari la Draxton kulimfikisha Namouih kwenye maeneo ambayo hayakuwa na makazi mengi ya watu, na gari la Draxton lilitumia njia mbalimbali zenye kuchanganya kiasi kulifikia eneo la huku lakini Namouih alitambua kwamba bado mwanaume huyo hakuwa amejua kama anafatiliwa. Akaendelea kulifuatilia gari hilo mpaka lilipofika eneo lenye miti mingi kama mapori vile, na gari la Draxton likaiacha barabara ya lami na kuingia barabara ya changarawe kuelekea upande wa mapori hayo. Namouih akaongeza kasi ili aliwahi, akiingia barabara hiyo pia na kuendelea kulifuatilia. Yaani alihisi kama siku hii ilikuwa ya bahati kwake kwa sababu mwanaume huyu alimleta sehemu ya mbali alikokuwa na jambo fulani la siri, na Namouih angeweza kujua ni nini hasa kilichofanya aje huku.

Akafika sehemu fulani ndani ya eneo hilo na kuona gari la Draxton likiwa limeegeshwa tu karibu na miti, na kwa sababu hakujua ikiwa tayari jamaa alishuka au la, akasimama kwa umbali aliokuwa na kuamua kusubiri kwanza. Sekunde tano kupita akaona mlango wa gari la Draxton ukifunguka, na mwanaume mwenyewe akitoka, kisha akaanza tu kutembea kuelekea upande wenye miti mingi zaidi. Namouih hangeweza kuona nyumba yoyote aehemu hiyo, na hivyo akawa anajiuliza ni nini ambacho kingempeleka mwanaume huyo sehemu hizo zilizojificha sana.

Hangekaa kukisia jibu la swali lake, lakini akiwa anakumbuka vyema kwamba jamaa alikuwa na tattoo kama ya yule kiumbe waliyemgonga usiku ule, akaikoki vizuri bastola yake na kulisogeza gari lake mpaka karibu kabisa na gari la Draxton. Akashuka. Akalisogelea na kuanza kuchungulia kwa ndani, kisha akajaribu kuufungua mlango upande wa usukani, nao ukafunguka. Akatazama kule Draxton alikoelekea lakini hakuweza kumwona, hivyo akajiingiza ndani hapo na kuanza kukagua vitu vilivyokuwepo ili kuona kama angepata jambo lolote lenye kuthibitisha masuala yenye utata kumhusu mwanaume huyo. Akaangalia makaratasi mengi yaliyotunzwa humo, akapekua upande wa nyuma wa gari, akanyanyua siti ili kuchunguza kwa chini, yaani chochote kile ili tu apate lolote, lakini hakupata jambo lenye kuridhisha haja zake.

Akajitoa hapo na kuangalia huku na kule kuona kama Draxton alikuwa anarudi lakini hakumwona. Wazo la kwamba ingefaa zaidi kama angemfatilia jamaa huko huko alikoenda alikuwa nalo, lakini isingekuwa rahisi kumpata sasa hivi maana alikoelekea hakukujulikana. Akawaza tu kuondoka hapo upesi kisha angetumia fursa nyingine kumfatilia jamaa moja kwa moja, au aje huku wakati mwingine ili atafiti eneo hili yeye mwenyewe. Akarudi usawa wa gari la Draxton na kuufunga mlango wake, na hapo akashtuka sana baada ya kumwona mwanaume huyo akiwa amesimama nyuma yake! Yaani kupitia kioo cheusi cha mlangoni aliweza kumwona kwa nyuma, na kwa haraka akageuka na kumtazama pia.


★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next