DOSARI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Uhalifu, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA PILI
★★★★★★★★★★★★★
Tunakuja upande mwingine wa jiji analoishi bwana Reuben, ikiwa ni katikati ya usiku uitwao wa manane. Pande nyingi za jiji hilo tayari hekaheka na shughuli nyingi kubwa zilikuwa zimepumzishwa kwa muda huo, na kwa huku kulikuwa na duka moja kubwa la vifaa vingi maalumu vya kielektoni kwa manunuzi ya wateja kama vile runinga maridadi, sabuba, ving'amuzi vya michezo (game), na hata vifaa kama friji, majiko ya umeme, oveni, mashine za kufua, na kadhalika. Likiwa moja kati ya sehemu nyingi ambazo zimefungwa kwa wakati huu, linapewa ulinzi na wanausalama wawili maalumu, kwa kuwa siyo kama maduka mengine kwenye eneo hilo. Ni kubwa sana, wakibeba bunduki za ulinzi, na wanalinda kwa mzunguko kuangalia usalama na sehemu zingine za karibu na hapo.
Kama ilivyo kawaida, kazi yao mara nyingi inakuwa yenye kuboa kwa sababu hakuna mtu anayethubutu kusogea eneo hilo kwa wakati huo, yaani ni utaratibu usiokwepeka kwa mtu yeyote kutoonekana katikati ya usiku akitembea karibu na hapo, isipokuwa gari moja-moja huko barabarani, na kwa wachache ambao wangepita ingekuwa kufatwa na kuombwa watoe sababu zilizonyooka kuhusu ni kwa nini wanatembea usiku sana. Basi, ikiwa ni mida ya saa nane usiku, walinzi hawa wakawa wameketi pamoja kwenye benchi fupi chini ya mti mdogo karibu na jengo hilo, na ili kupisha muda wakawa wakishushia kahawa ambayo sikuzote walitunza kwenye chupa zao ili kusaidia umakini wao mpaka kukucha.
Wakiwa wanaongelea mambo ya hapa na pale, kutokea kwenye kona ya jengo hilo kuelekea upande uliokuwa na ukuta uliokinza eneo lao na mnara mrefu wa mtandao, likarushwa kopo dogo la soda, lililopiga ardhi kwa kishindo kilichotoa sauti yenye kushtua kiasi. Mshtuko sanasana kutokana na kutojulikana kimerushwa na nani ndiyo jambo lililowatia hisi ya tahadhari walinzi hao na upesi kunyanyuka huku wakielekeza bunduki zao kuelekea upande huo. Wakiwa makini, kwa pamoja wakaanza kuelekea sehemu ambayo kikopo hicho kilitokea, na mmoja akamtangulia mwenzake ili mwingine awe nyuma kuangalia dukuduku lolote na huku walikopaacha, ingawa walienda sambamba.
Kukaribia sehemu hiyo kikopo hicho kilipokuwa, kikarushwa kingine tena kutokea upande wa pili wa ukuta ule, na ikawa wazi kwa walinzi hawa kwamba kuna mtu alikuwa akiwaletea mzaha. Wote wakafikia sehemu hiyo na kupeana ishara ya kwamba mmoja azunguke kwenda upande huo wa mnara kuona nani anawaletea zengwe, na mwingine abaki kulinda jengo lao, na baada tu ya kukubaliana, ghafla sana mlinzi aliyekuwa akitaka kwenda huko akashtukia anarukiwa na kitu kizito kilichomwangusha chini kwa nguvu!
Ile mwenzake ameshtuka pia na kutazama kilichotokea, akaona kwamba ni mtu mwingine alikuwa amemrukia mwenziye, bila shaka akitokea ukutani pale. Alionekana kuvaa nguo nyeusi karibia mwili wake wote mpaka kichwani, yaani akikiziba kwa kificha uso, na yeye mlinzi upesi akapiga hatua ili amsaidie mwenzake pale aliposhtukia anakabwa kutokea nyuma na kupigwa ngeta kali miguuni iliyomwangusha chini sambamba na aliyemkaba.
Vishindo vikazidi kuongezeka baada ya walinzi hao kuvamiwa na watu wengine zaidi, waliojiunga na wakabaji hao na kuwashushia vipondo vya nguvu kwa ngumi na mateke, nao wakanyang'anywa bunduki zao haraka huku wakikandamizwa chini. Ardhi ilikuwa ya kokoto ngumu zilizogandishwa kwa pamoja, hivyo walinzi walihisi maumivu makali na kutoa sauti zilizoonyesha hilo.
"Fasta, kafungue!"
Sauti ya mmoja wa wakabaji hao ikaamuru hivyo, na baadhi yao wakaondoka hapo kulielekea jengo la duka haraka.
"Wanyanyue."
Sauti hiyo ikaamuru tena. Walinzi kwa pamoja wakavutwa kwa nguvu na kuwekwa katika hali ya kupigishwa magoti, na sasa waliweza kuwaona wahasimu wao waliokuwa wamekuja kufanya uhalifu huo. Haikuwa kuwaona nyusoni kabisa, kwa sababu wote walizificha kwa vificha uso vyeusi vilivyofunika vichwa vyao vyote kuacha uwazi mdogo machoni na midomoni. Ikawa wazi hao hawakuwa wakabaji tu, bali walikuwa majambazi. Waliosimama hapo walikuwa wanne, na wawili wakiwa karibu na walinzi wakawaambia waweke mikono yao vichwani na watulie hivyo hivyo. Wakatii. Wengine wawili walishikilia bunduki pia ambazo hazikuwa za wale walinzi, wakiwaelekezea ili wasifanye ujanja wowote, na kweli hawakuwa na ujanja wowote tena.
Ikionekana wazi kwamba majambazi wengine walikuwa wamevunja na kuingia dukani kule, sauti ya mngurumo wa gari ikaanza kukaribia sehemu hiyo, na walinzi wakaona gari la pick-up jeusi likija kwa kasi na kisha kwenda kuegeshwa karibu na milango ya duka. Gari lingine jeusi pia kama hiace likafuata, lenyewe likisimama huko mbele zaidi kuelekea barabara, na kwenye ile pick-up akashuka mwanaume mmoja, akificha uso pia, naye akaelekea kule ndani.
Kutokea dukani, majambazi watatu wakaanza kutoka na vitu vingi na kuviweka kwenye gari, TV, ving'amuzi, sabufa, vyombo vingi vya umeme vyenye thamani ghali, yote hayo walinzi wakijionea tu, lakini hawakubeba vitu vizito kama friji kubwa. Walihakikisha wanasomba kila kitu kilichotoshea garini, na baada ya kujaza, mmoja wao akachukua dumu moja lenye mafuta ya petroli kutoka garini na kuanza kulimwagia duka hilo kutokea kule ndani kuja hadi nje.
Wakati mafuta yakiwa yanamwagwa, mmoja wa majambazi hao akaanza kuelekea karibu na sehemu ambayo walinzi walipigishwa magoti, akiwa na mwili mpana na mrefu, naye akasimama karibu nao zaidi akiwaangalia kwa umakini.
"Dakika kumi na tano, over. Twendeni," jambazi mtoa amri akasema.
"Na hawa?" mwingine akauliza.
"Waacheni. Walaze hapo tuondoke," jambazi mtoa amri akamjibu.
"What's the fun in that? (Kuna burudisho gani kwenye hilo?)"
Kauli hiyo ikatoka kwa yule jambazi aliyekuwa amewasogelea walinzi, akiwa na sauti nzito lakini tulivu, na akiongea taratibu lakini kwa njia iliyotikisa hisia upesi mno. Jambazi aliyewaongoza alikuwa tayari kuondoka hapo baada ya kuwaambia wenzake wawaache tu walinzi hao, lakini akaishia kumtazama huyo mmoja kwa umakini baada ya kumsikia anauliza hivyo. Akawaangalia walinzi na kuona namna ambavyo waliwatazama majambazi kwa maumivu, naye akarudi kumtazama tena mwenziye.
"Nimesema waachwe. Una tatizo na hilo?" jambazi aliyewaongoza akamuuliza hivyo.
Mwenzake, bila kumtazama, akauliza, "Kwa nini?"
"Hakuna lolote wameona as far as we're concerned, hiyo ndiyo sababu. Narudia tena, una tatizo na hilo?" aliyewaongoza akamuuliza.
Huyu mwenziye akamgeukia hatimaye na kutazamana naye kwa njia iliyoonyesha damu inapanda moto, kisha akavuta kificha uso chake mwenyewe na kuiacha sura yake wazi kwa makusudi. Wenzake walimshangaa!
"Unafanya nini?!" jambazi aliyewaongoza akamuuliza kwa mkazo.
Mwanaume huyu aliyevua kificha uso chake akatabasamu kiasi, naye akasema, "Wameuona uso wangu sasa... so hatuwezi kuwaacha."
Aliongea huku akitoa tabasamu lenye hila sana, naye akawaangalia walinzi tena. Mwanaume huyu alikuwa mwenye rasi nene na ndefu sana kichwani, mweusi, na sura yake yenye ukomavu ilitoa taswira moja ambayo yeyote yule aitazamaye angeipata upesi; ukatili. Alikuwa na mwili mpana na uliojengeka vyema sana kiume, mikono yake yote ikikolezwa rangi nyeusi kwa michoro ya tattoo aliyoijaza mpaka ndani ya torso. Macho yake yalikuwa na rangi ya udhahabu kwenye lenzi na hivyo kuonekana kung'aa hasa ilipokuwa giza, jambo lililotoa taswira ajabu ya mwanzo kumwelekea mwanaume huyu. Kitendo chake hapo kilionyesha kwamba nia yake ilikuwa kuwaondoa kabisa walinzi hao ingawa wenzake hawakuona uhitaji wa kufanya jambo hilo, na hilo likamtia hasira sana aliyewaongoza kwenye uhalifu wakati huu.
Aliyekuwa anamwagia jengo mafuta akafika pembeni ya wawili hawa, akiwa amelitegesha dumu la mafuta karibu na duka lile, naye akamwambia aliyewaongoza, "Tayari, tusepe. Muda umeisha."
"Ona jamaa alichofanya!" mwingine akamwambia hivyo, kumaanisha ishu ya mwenzao kuondoa kificha uso.
Aliyeendesha ile hiace nyeusi akafika hapo pia baada ya kuona kama kuna mvurugo baina ya wenzake. Sasa majambazi wote wakakutana hapo katikati, wakiwa nane.
Aliyewaongoza akamshika mkononi mwanaume huyo aliyevua kificha uso na kumwambia, "Mbona unaleta ufala mwana? Unajua hatuna muda wa kupoteza halafu una...."
Mwanaume huyo akauvuta mkono wake kwa nguvu na kumnyooshea kidole usoni kiukali, naye akasema, "Usije rudia nigusa tena!"
"Au utafanya nini?" aliyewaongoza akamuuliza kibabe na kumsogelea usoni zaidi.
Ikaonekana kwamba wanataka kupigana, na wenzao wakaingilia kati kuwaachanisha kwa kuwasukuma.
"Aisee, muda!" mmoja wao akasema.
"Hii haikuwa order ya boss... anataka tuwaue hawa kwa basi tu..." aliyewaongoza akasema hivyo.
"Fuck off! I'm dealing with this myself (Toka! Ninashughulika nalo hili mwenyewe)," mwanaume huyo mwenye rasi akasema.
"Utajua mwenyewe. Tuondokeni," aliyewaongoza akasema hivyo.
"Tunapaswa kuondoka pamoja, hiyo ndo' code," mwingine akamwambia.
"Waue basi faster, uridhike, tuondoke," mmojawapo akamwambia rasi.
Jamaa akatabasamu.
"Msi... msitufanye lolote joh... sisi hatutasema lolote, hatujaona chochote..." mmoja wa walinzi akasema hivyo kwa hofu.
Aliyekuwa akiwaongoza majambazi wenziye akatikisa kichwa kwa kuudhiwa sana na jambo hili, na huyo mwanaume mwenye rasi akachukua bunduki kutoka kwa mwenziye huku akitabasamu kwa hila. Walinzi waliogopa sana. Wakawa wanaongea na kujongea kwa kujirudi-rudi nyuma, na huyo mwanaume mwenye rasi akamtandika mmojawapo kwa uchuma wa bunduki kichwani kwake. Alimpiga vibaya sana mpaka damu zikafurumka kama bomba lililopasuka kwa pigo hilo moja tu, naye akadondokea pembeni huku akishtuka mwilini.
Huku akiwa anatabasamu, mwanaume huyu akamwangalia mlinzi wa pembeni, ambaye alipumua kwa hofu kiasi, lakini akajitia ujasiri na kunyanyuka upesi. Akamfuata mwanaume huyo na kumpamia kwa nguvu ili ajaribu pambano pamoja naye, lakini jamaa akarudi nyuma kidogo tu bila kuweweseka wala nini. Alikuwa na nguvu sana. Mlinzi akabaki kusimama huku akimwangalia kwa wasiwasi mwingi, hapo akiwa kama amezungukwa na majambazi wote, na hapo hapo mwanaume mwenye rasi akampamia kwa nguvu na kumdondosha chini. Akaanza kumpiga kwa uchuma wa bunduki kichwani mara nyingi sana na kukipasua vibaya mno, na hata ilipokuwa wazi kwamba mlinzi amepoteza maisha, bado mwanaume huyu akaendelea tu kukitoboa kichwa hicho hadi kukizagaza kwa njia isiyotamanika hata kidogo.
Majambazi wengine walimwangalia mwanaume huyo kwa ukakasi alipokuwa akifanya hivyo, mwenyewe akifurahia kweli kufanya ukatili huo, na aliporidhika, akajilamba damu zilizomrukia midomoni na kufumba macho huku anatabasamu. Wenzake wakaangaliana mmoja na mwenzake na hata kutikisiana vichwa kwa kutopendezwa na roho hiyo mbaya kupitiliza ya mwenzao aliyependa kumwaga damu, nao wakaanza kusambaa na kuyarudia magari upesi ili waondoke; akibaki yule aliyewaongoza hapo, na rasi mwenyewe. Huyu mwanaume mwenye rasi akasimama, akiwa amerukiwa na damu nyingi sana usoni, kisha akamtazama mwenzake pembeni.
Akamwambia, "Now that... that was fun (Sasa hiyo... hiyo ndiyo imeburudisha)."
Jambazi mwongozaji akasema, "We' ni psycho mmoja mbovu sana. Unahitaji msaada."
"Yeah, yeah. Fuck you too," mwanaume mwenye rasi akasema hivyo kizembe.
Mwenzake akaondoka na kuelekea garini upesi, na mwanaume huyu akaendelea kusimama hapo hapo mpaka pick-up ilipokaribia upande wake na kusimama. Akiwa ameishikilia bunduki mkononi, mwanaume huyu akaielekeza upande wa duka lile na kufyatua risasi moja kulielekea dumu la mafuta, kitu ambacho kikafanya moto uanze kuwaka kwa kasi sana kuelekea huko ndani. Akafungua mlango wa gari na kuingia haraka, ile hiace nyingine ikiwa imeshatangulia kuondoka, nao wakafata pia na kutokomea pasipojulikana huku eneo hilo likiachwa ndani ya moto mkali uliozidi kuongezeka. Kazi yao ikawa imekamilika.
★★★
Jumatatu ikakucha hatimaye. Ikiwa ndiyo jambo lililoshika kasi zaidi kujulikana, tukio hilo la duka kuungua kwa moto lilienea sehemu nyingi za jiji na nchi nzima kiujumla baada ya vyombo vya habari kusambaza taarifa. Moto huo ulifanikiwa kuzimwa baada ya magari ya zima-moto kufika eneo la tukio, na maaskari walipofanya uchunguzi wakagundua kuwa duka hilo liliunguzwa kwa makusudi na wahalifu waliofika kuiba na kuwaua walinzi wa hapo, huku wakitoa ahadi kuwatafuta na kuwakamata watu hao ili waadhibiwe. Ilionekana wazi kwamba duka hilo lilikuwa limelengwa shabaha ya moja kwa moja, kama vile kuna mtu alitaka kumkomoa mwenye nalo, hivyo maaskari walihitaji kuanza kuchunguza upande wa mmiliki kuona kama angefahamu mtu yeyote aliyetaka kumfanyia kitendo kama hicho kwa sababu za uadui.
Hayo yakiwa yanaendelea, upande wa bwana Reuben siku hii ilianza kwa ukawaida wake wa kuelekea kazini, kwenye kampuni yaani, na hata yeye pia alikuwa amepata taarifa za tukio hilo la moto. Kwake yeye lilikuwa na umuhimu wa kadiri kubwa kwa kuwa mwenye duka lile alifahamiana naye, akiwa kama rafiki wa karibu sana, hivyo alifanya kuwasiliana naye ili kumpa pole na kuchanganua namna ambavyo mambo yangekwenda kutokea hapo. Huyo mtu alikuwa mbaba mwenye umri mkubwa kumpita Reuben, aliyeitwa Stanslaus Mwita, ambaye alikuwa na maisha mazuri pia na mfanyabiashara mwenye maduka kadhaa makubwa ya vitu mbalimbali yaliyomwingizia pesa nyingi. Hilo moja ndiyo likawa limeenda.
Baada ya kuongea naye kwa kina, Reuben akajua maoni ya Stanslaus kuwa kwamba kuna watu walimlenga yeye moja kwa moja ndiyo, wakitaka kumwangusha, ndiyo sababu wakamfanyia hivyo kwenye moja ya maduka yake makubwa zaidi. Hakujua nani kihususa, lakini kwa aliokuwa amewafikiria, aliwapa majina kwa maaskari, hivyo wangemsaidia kuwatafuta watu hao na kufanikisha kuwakamata baadaye. Reuben akamuunga mkono kwa hilo na kusema ikiwa angehitaji wasaidiane kwa lolote lile, basi asisite kumwambia, nao wakaagana vizuri.
Akaendelea kuwa ofisini kwake hadi mida ya mchana, akipokea, kushughulikia, na kutuma kazi zilizohusika kwa siku hii, huku akiwa na hamu kubwa kupisha wakati ili ufike muda ambao mke wake angefika jijini hatimaye. Lydia alikuwa anarudi siku hii, na bila shaka Reuben angekwenda kumpokea stendi baadaye. Akiwa ndiyo anafikiria kutoka mara moja ili akapate chakula, akapigiwa simu na yule rafiki yake ambaye walikutana jana asubuhi mgahawani kwa mkewe, Francis. Akakumbuka kuwa, jana jioni wakati yupo nyumbani, rafiki yake huyu aliwasiliana naye, nao wakakubaliana kukutana leo hapa hapa ofisini kwake. Kumtembelea, apajue yaani.
Ah, kutokana na mambo kuwa mengi yaani jambo hili lingetoweka kabisa akilini kwa Reuben, hivyo akapokea na kuzungumza naye wapangane vizuri hata zaidi. Francis akamwambia kwamba kwa muda huo tayari alikuwa ameshafika nje ya jengo la kampuni yao Reuben, hivyo alihitaji tu mwongozo ili afike ofisini kwake waweze kuonana. Reuben hakutarajia Francis awe ameshafika eneo hilo, lakini kwake hiki kikawa kitu kizuri, angalau Francis hakusahau ahadi kama yeye alivyokuwa mbali na hilo wazo tayari. Hivyo, akamwelekeza vyema kabisa, naye Francis akapanda mpaka kwenye ghorofa iliyobeba ofisi ya bwana Reuben.
Francis akafika ofisini kwake Reuben kwa kukaribishwa na msaidizi wa hapo, mwanamke kijana mwenye mwonekano mzuri, naye akaelekea hadi mezani kwa "bosi" mwenyewe na kuunganisha naye viganja kisalamu, wote wakipeana tabasamu kwa furaha.
"Ah, mkubwa uko penyewe hapa," Francis akasema hivyo kabla ya kukaa kitini.
"Yeah, karibu sana bro," Reuben akamwambia hivyo kwa utulivu.
"Aisee, nilifikiri ningepotea huku bwana, hizi kona za haya majengo zinachanganya kweli..."
"Hahah... haujatembelea hizi pande sana?"
"Siyo sana. Yaani... mara nyingi napapita tu kama nikiwa kwenye usafiri. Kutembea si sana," Francis akasema.
"Ndiyo tuko hapa bwana, karibu sana," Reuben akamwambia.
"Nimekaribia kaka. Mambo mazuri sana haya..."
"Yeah, ila yana ugumu wake. Angalau lakini tunapata, tunasonga mbele. Vipi wewe? Familia?"
"Ah, me nipo tu kaka. Kama nilivyokwambia jana, yaani ndiyo nimeingia kwenye harakati za spare juzi kati hapo, biashara imeanza kukua kidogo, so now napangilia hilo suala la familia..."
"Hahah... ndoa iko njiani..."
"Eeh, na me nitulie kama we' mkurugenzi."
"Hongera sana."
"Asante. Vipi na wewe? Ulisema bi mkubwa yuko safarini eh?"
"Eeh, yuko njiani kurudi. Nilikuwa ndo' nataka nikapate lunch McDonald hapo nje, nimalizie ishu kadhaa hapa ndiyo nielekee huko stendi..."
"Ooh, ataingia mapema tu?"
"Saa kumi na mbili sanasana..."
"Okay. Kumbe hujapata msosi bado?"
"Toka asubuhi."
"Aah..."
"Hahahah... kazi hizo ndugu yangu. We' ushapata?"
"Yeah, saa tisa sa'hivi, tumbo lisharidhika hili. We' kama vipi, fanya twende upate msosi, halafu nitapitilizia huko huko..." Francis akasema.
"Okay. Kuna sehemu nyingine ulikuwa unaenda?" Reuben akauliza.
"Eeeh, napita kwanza maeneo... then narudi dukani kwangu. Tutapanga na we' uje upaone," Francis akamwambia.
Reuben akasimama huku akisema, "Fresh, suala ni muda kubana, ila Jumapili tutafanya jambo."
Simu yake ikaanza kuita, wakati huo Francis amesimama pia huku akisema, "Eeh, Jumapili ndo' imetulia zaidi kwenda kupiga mbili tatu na nini..."
Reuben akacheka kidogo huku akitoa simu mfukoni, kukuta namba ngeni, naye akapokea na kuchukua funguo mezani huku akianza kumwelekea Francis ili waondoke. Akaanza kuongea na mtu aliyempigia, mwanaume, akiwa mgeni kwake, naye alipomwambia yeye ni nani na dhumuni la kumpigia, Reuben akakatisha hatua zake na kubaki ameangalia chini kwa mkazo sana. Francis alikuwa ametangulia mbele kidogo na kugeuka nyuma baada ya kuona mwenzake amesimama, na kwa jinsi ambavyo sura ya Reuben ilionyesha mkazo, akahisi kwamba kulikuwa na tatizo. Reuben hakusema lolote tena kumwelekea mtu aliyempigia, naye akashusha simu kutoka sikioni huku sura yake ikianza kuonyesha wasiwasi.
Francis akamsogelea na kuuliza, "Vipi kaka?"
Reuben akamwangalia usoni rafikiye, lakini akaishia tu kushusha pumzi kali kama vile mtu aliyechoka.
"Reuben?" Francis akamwita.
Reuben akafumba macho na kusema, "Nime... gari alilopanda mke wangu...."
Francis akaingiwa na utambuzi wa maana ya maneno ya rafiki yake kabla hata hajamaliza kuongea, na Reuben akamwangalia usoni huku akianza kupumua kwa hofu kiasi.
"Imekuwaje? Yaani... nini kimetokea?" Francis akauliza.
"Sijui, anasema... limepinduka... kuna... aisee!" Reuben akaongea kwa sauti ya chini, lakini hofu yake ilionekana vyema.
"Alikuwa nani huyo?" Francis akauliza.
"Askari... sijui... daktari, I don't know. Francis, nahitaji kwenda," Reuben akaongea kwa uharakishi.
"Ninakuja nawe bro. Twende," Francis akamwambia hivyo.
Kwa pamoja wakaondoka upesi sana ofisini hapo, hali ikiwa imegeuka kuwa nzito ghafla kwa njia ambayo haikutarajiwa kabisa, na Reuben akaondoka jengoni hapo pamoja na rafikiye bila kukawia ili aende kujua mke wake alikuwa kwenye hali gani huko ambako ajali hiyo ilitokea. Yaani hakutaka kuambiwa lolote lile na yeyote ambaye angetaka kumwambia kwa njia ya simu, alihitaji kwenda kuthibitisha yeye mwenyewe ukweli wa kile alichokuwa ametaarifiwa, na aliomba kwa Mungu mke wake asiwe amepatwa na maafa ambayo yangemwacha na huzuni isiyopimika moyoni mwake.
★★
Ajali iliyotokea ilihusisha magari matatu, ambalo alisafiria mke wa mwanaume huyo likigongana na lori la mizigo baada ya gari dogo kuchanganya njia na kuingiliana na magari hayo makubwa. Watu kadhaa walikufa eneo la tukio na wengine kufia hospitali, wengi wakijeruhiwa, na Lydia alikuwa miongoni mwa wale waliopoteza maisha pale pale ajali ilipotokea. Reuben alikumbwa na jambo zito mno ambalo hakuwahi kukaa kufikiria lingempata katika kipindi hiki, ama kingine kabisa. Sehemu kuu ya furaha katika maisha yake sasa ilikuwa imetoweka baada ya safari ya kumrudisha mke wake nyumbani kugeuka kuwa sababu kuu ya majonzi kwake. Hakuamini kabisa kwamba hili lilitokea, akiwa ameuona mwili wa mkewe uliohamishwa na kupelekwa mochwari, alihisi ni kama ndoto mbaya sana ilikuwa ikimpata.
Aliuacha mwili wa mkewe na kurudi kwenye gari, Francis akiwa pamoja naye, naye Reuben alikaa humo kwa saa zima akilia kwa kuuinamia usukani kana kwamba alikuwa mtoto mdogo. Alihisi uchungu mwingi kumpoteza mke wake kwa namna mbaya sana, na rafiki yake aliendelea kujitahidi kumtia moyo na kukaa kando yake katika wakati huu mgumu mno kwenye maisha yake. Huzuni ya Reuben ilizidishwa uzito hasa kila mara alipomfikiria binti yake kule nyumbani. Angemwambia vipi yule mtoto kuhusu jambo hili, na ingekuwaje kwake yeye na mtoto wake kutokea hapa bila ya Lydia kuwa nao tena? Mwanaume aliugua sana moyoni, hakujua ingekuwaje.
Francis akamsemesha Reuben baada ya mwanaume huyo kutuliza kilio chake cha chini na kumwambia wangetakiwa kuanza kufanya maandalizi ya msiba, lakini kwa yeye Reuben sasa alipaswa tu kwenda nyumbani na kuacha mipango hiyo chini ya uangalizi wa mtu ili kuweza kumuaga mke wake kwa njia iliyostahili. Akamtia moyo zaidi kwa kumwambia anaelewa namna anavyohisi, ila huu ndiyo ungetakiwa kuwa wakati wa yeye kuonyesha nguvu kama mwanaume na baba, ahakikishe anasimama kwa uimara licha ya jambo hilo kuwa baya sana; kwa ajili ya binti yake na familia yake yote kwa ujumla.
Reuben aliyasikia vyema maneno ya rafiki yake, na hakusema chochote. Bado alihisi kudhoofika sana kihisia lakini alielewa Francis alikuwa sahihi, hivyo alichofanya ikawa ni kuweka mwongozo wa ramani ndani ya gari wa njia ya kufika nyumbani kisha akajitoa kwenye siti ya usukani na kukaa siti za nyuma ndani ya gari, akiwa amemwachia rafiki yake amwendeshe kuelekea huko. Francis aliuelewa vizuri mkazo wa rafiki yake, kwa hiyo kweli akafanya alichoombwa afanye ingawa hakuambiwa kwa maneno. Alitambua sasa angehitaji kuwa na Reuben bega kwa bega kumsaidia apambane na huzuni yake. Akawasha gari na kuanzisha safari.
★★
Mwendo wa kuwarudisha jijini zaidi ulichukua karibia masaa mawili, shauri ya mvua kubwa kunyesha na misongamano ya magari kukawiza, na hatimaye Francis akafanikiwa kuifikia nyumba yake Reuben kwenye mida ya saa mbili usiku. Ilimbidi Reuben aanze kushuka ili kumdhibiti kwanza mbwa wake mkali kwa wageni, na baada ya kwenda kumfungia akarejea upande wa mbele wa nyumba na kukutana na rafiki yake hapo. Alisimama kwa ufupi akiitazama nyumba yake, manyunyu ya mvua bado yakidondoka, na Francis akamshika begani kumtia moyo kuwa waelekee ndani ili aweze kuongea na bintiye mpendwa. Wakaanza kwenda.
Hatua chache kuelekea mlango wa kuingilia ndani na Reuben akashindwa kusonga mbele baada ya msisimko wa huzuni kumwingia hata zaidi. Francis, akiwa pembeni yake, akamshika begani tena na kumtia nguvu bila maneno, na Reuben akatulia kwa sekunde chache kutuliza hisia zake vyema zaidi ili aende kushughulika na binti yake huko ndani. Lilikuwa jukumu lake pekee kwa sasa kufikisha taarifa yenye kuchoma sana kwa mtoto wake mpendwa, na hakujua ingemwachaje binti kihisia lakini ilihitajika kumwambia Larissa kilichotokea, na baada ya hapo Reuben angepaswa kuhakikisha anamlinda zaidi binti yake.
Akaendelea kusonga na rafikiye hadi kuufikia mlango, na alipoufungua tu kuingia ndani tayari aliweza kumwona mtoto akiwa ameketi sofani huko mbele, na akionekana kuchora jambo fulani kwenye karatasi. Kwa sekunde chache Reuben tena akabaki kusimama hapo hapo mlangoni akimtazama mtoto huyo, huzuni ikianza kumvaa tena kutokana na kumwangalia Larissa lakini taswira aliyoiona ikawa ni ya Lydia, mke wake marehemu.
Kutokea mbele zaidi akaanza kuja msaidizi wa kazi, na alipomwona bosi wake akatuma salamu ya upesi na kuelekea upande wake Reuben kumpokea; ingawa hata hakubeba chochote. Larissa aliponyanyua uso pia, akamwona baba yake, naye akaacha kuchora na kunyanyuka, upesi akikimbia na kumpita msaidizi ili yeye ndiyo awe wa kwanza kumpokea baba. Reuben akabaki kumtazama bintiye hadi alipomfikia na kumkumbatia kwa shauku, na hata hapo akashindwa kurudisha kumbatio hilo na kubaki ameangalia tu mbele kama kazubaa.
"Shikamoo baba?" Larissa akamwamkia huku akimtazama kwa kuegamiza kidevu chake tumboni.
Reuben akamwangalia na kusema, "Marahaba," kwa sauti ya chini sana.
"Shikamoo," msaidizi, aliyeitwa Amina, akamwamkia Francis.
"Marahaba," Francis akamwitikia.
"Uncle shikamoo?" Larissa akasema hivyo kumwelekea Francis pia.
"Marahaba mtoto mzuri. Hujambo?" Francis akamwitikia vyema.
"Sijambo. Baba umekuja na uncle na mama? Kama vile tutafanya party leo..." Larissa akaongea kwa shauku.
Reuben akamwangalia Francis, ambaye akamtikisia kichwa mara moja kama kumpa ishara.
"Nataka niwachekeshe... yaani leo shule ahahahah... nimemuuza mwalimu..." Larissa akasema hivyo na kumwachia baba yake.
Reuben akasema, "Larissa..."
"Mama bado yuko nje?" Amina akauliza, akiashiria kutaka kuwapita wanaume.
Francis akatikisia kichwa kukanusha na kumshika mkono Amina kumzuia.
"Ngoja niwaambie kwanza nyie halafu na yeye aje acheke..." Larissa akasema hivyo.
Reuben akachuchumaa kwa kupiga goti moja na kusema, "Larissa... baby, kuna... nataka nikwambie..."
"Ngoja kwanza me ndo' nikwambiee!" Larissa akasisitiza.
Reuben akabaki kumtazama kwa hisia.
"So, mwalimu aliuliza swali, sawa? Hivi... yaani, tuseme umri wa wazazi wetu. Alikuwa anataka kuonyesha kwamba mara nyingi watoto hatujui wazazi wetu wana umri gani, which is truuue... kwa hiyo akawa anafanya ku-clarify point yake mwenyewe. Kamuuliza Thomas, Anita, Loveness, wote hawajui... halafu akaja kwangu..." Larissa akaanza kusimulia.
Reuben, akiwa anakaza hisia zake, akatikisa kichwa chake kumruhusu mtoto aendelee.
Larissa akasema, "Akauliza eti 'how old is your mother?' Nikamwangaliaaa... halafu nikamwambia 'my mother is eight years old.' Mh? Wenzangu wakaanza kunishangaa, na teacher akaniuliza eti nina matatizo ya akili? Mama yangu iweje awe na miaka nane? Nikamwambia teacher sina matatizo ya akili, ila huo ndiyo ukweli. Mama yangu ana miaka nane, kwa sababu hakuwa mama wakati sijazaliwa, alianza kuitwa mama alipomzaa baby Larissa. Kwa hiyo umri wa mama yangu ni miaka nane kwa sababu ndiyo miaka yangu mimi mtoto wake..."
Francis akatabasamu kiasi kwa kutambua jinsi binti huyo alivyokuwa mwerevu. Reuben akaendelea tu kumwangalia mtoto.
"Nikamwambia 'when you want proper answers for your questions, be specific with what you're asking.' Angeuliza Lydia ana miaka mingapi, ndiyo ningesema sijui. Lakini mama yangu ana umri mwingine. Uwongo? Hapo nani utasema ni mwenye matatizo ya akili?" Larissa akaongea kwa kujinadi.
Amina akashindwa kujizuia kucheka kidogo, naye akasema, "Ila Larissa! Ungechapwa..."
"Shubutuu!" Larissa akasema hivyo.
Reuben akatazama chini tu kwa huzuni.
"Anaanzia wapi? Ndiyo wametambua leo wasicheze na mimi. Hiki kichwa ni genius. Uwongo uncle?" Larissa akasema hivyo.
Francis akalazimisha tu tabasamu na kutikisa kichwa kukubaliana naye.
"Sa' mbona hata hamcheki?" Larissa akauliza.
Reuben akamwangalia.
"Mm, nyie old school sana. Ngoja nimwambie mama, najua ata...."
Larissa alikuwa akitaka kumpita baba yake alipoanza kusema hivyo, lakini Reuben akamshika kumzuia.
"Daddy, naenda kumpokea mama, na ye' nimsimulie. Anachelewa kuingia..." Larissa akasema.
Amina sasa alikuwa ameshaanza kuhisi kwamba kuna tatizo baada ya kumwangalia Francis na kuona hakuwa na raha kabisa kama tu bosi wake.
"Lari... ona... mama hajaweza kufika..." Reuben akamwambia hivyo.
"Hamjaja naye?" Larissa akauliza.
Reuben akashindwa kutoa jibu.
"Basi limechelewa kufika baba? Au... haji leo?" Amina akauliza.
"Aah baba! Mama si alisema anakuja leoo?" Larissa akauliza kwa kuudhika.
Reuben akachomwa na hisia kali sana iliyosababisha machozi yaanze kumjaa, naye akainamisha uso wake na kufumba macho.
Larissa kuona hivyo, akauliza, "Baba... nini?"
Reuben akabaki namna hiyo hiyo.
Larissa akamshika usoni na kuunyanyua ili baba yake amtazame, naye akasema, "Basi baba, usihuzunike. Kama haji leo basi. Labda atakuja kesho. Tutamsubiri. Eti?"
Aisee!
Reuben akatikiswa moyoni hata zaidi kutokana na jinsi binti yake alivyoongea, naye akamshika mabegani na kusema, "Larissa I'm sorry. Mama... hatawhh... hataweza kuja tena nyumbani, maana...."
Akaishia hapo, Larissa akibaki kumtazama tu kwa umakini kwa sababu ya kutoelewa.
Francis akamshika Reuben begani na kusema, "Mwambie."
Reuben akajikaza na kusema, "Larissa... unakumbuka kipindi kile bibi Rose yuko hospitali... alikuwa anaumwa sana... tukaenda kumwona, kumtembelea, halafu...."
"Halafu akafariki?" Larissa akamkatisha kwa kuuliza hivyo.
Reuben akabaki kimya.
Larissa akamwangalia Francis kwa njia yenye kuchanganywa, hata mwanaume huyu hakutarajia mtoto aende moja kwa moja kwenye pointi hiyo, na binti akarudi kumtazama baba yake na kuuliza, "Baba, unataka kuniambia nini?"
Amina naye akawa ameshaelewa na kubaki amemwangalia bosi wake kwa mshangao makini, na Reuben akasema, "Mama... alikuwa amepanda gari leo, na... kwa bahati mbaya likafika sehemu fulani lika... oh God, I don't know how to do this Francis!"
Mwanaume huyo alishindwa kabisa kwenda moja kwa moja kwenye pointi, na Francis akachuchumaa pembeni yake pia na kumshika mtoto.
Francis akamwambia, "Larissa... ni kwamba mama alikuwa kwenye basi anakuja, ila likawa limeanguka. Limeanguka... na mama akawa ameumia, kwa hiyo yaani..."
"Na yeye amekuwa kama bibi Rose?" Larissa akauliza kwa sauti ya chini, machozi yakianza kumjaa machoni.
Reuben akabaki kumtazama kwa hisia za uchungu mwingi sana. Mtoto alikuwa na uelewa mpana!
Larissa akamwangalia baba yake, machozi yakianza kumtoka na pumzi zake kushtua, naye akaanza kusema, "Baba... baba..."
Sauti yake ilionyesha maumivu sana, na jambo hili likafanya Reuben aumie pia na kushindwa kuzuia machozi yake kumwagika pia.
"Baba... hh.. ba... mama... mama aa... ma..." binti akaanza kulia na kushindwa kuzungumza vizuri.
"Larissa..." Reuben akajaribu kumshika.
Kifua cha mtoto kikaanza kushtua kwa kilio chenye uchungu mwingi huku akisema, "Baba me sitaaki.. hh.. mwambie mama arudi... hh... nilikuwa nimemcho... nimemchorea welcome sign.. ile kuule... nimwhh... nim hhh... nimwoneshee..."
Francis akasema, "Larissa..."
Reuben naye akasema, "Baby, sikia..."
"Sitaki... bab.. hh.. sitaki aende kwa bibi Rose babaa... mwambie arudii... mamaa..." Larissa akaongea kwa hisia huku akinyoosha kidole mlangoni.
Iliumiza sana. Reuben akamsogelea karibu zaidi na kumkumbatia, huku mtoto akiendelea kuita "mamaaaa" kwa sauti yenye uchungu mwingi sana. Amina alikuwa pembeni akilia kwa huzuni pia, huku Francis sasa akisimama na kumwangalia rafiki yake na bintiye kwa huruma nyingi. Larissa akaendelea kulia na kulia akiwa mikononi mwa Reuben, ambaye sasa aliachwa kuwa mzazi pekee kwenye maisha yake. Reuben aliumia sana kuliko namna ambavyo hakuwahi kudhani angewahi kuumia. Huzuni ya binti yake ilikuwa kama kioo cha ile iliyokuwa ndani yake, ingawa alijitahidi kujizuia lakini moyo wake ulichoma sana, sana, sana. Akaendelea tu kumshikilia mtoto wake kwa upendo akijaribu kumpa kitulizo ndani ya kumbatio lake, huku yeye akijihisi haba moyoni kutokana na kumpoteza mwenzi wa maisha yake.
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Comments