SEHEMU YA 08.
Hamza alihisi siku hio ni kama vile muda wowote ataamka kutoka ndondoni , ndoto ambayo ilianzia tokea siku ambayo aliweza kusoma Tangazo la ajira ya mchumba feki katika mtandao wa JamiiForum mpaka siku hio ambayo ameweza kupata kazi hio.
Wakati anatoka katika hoteli ya Dosam V alitamani kuonana na mrembo Prisca lakini kwa bahati mbaya hakumuona na alijua pengine amekwisha kuondoka hivyo hakutaka hata kujisumbua kumtafuta na kutoka zake katika hio hoteli na kuelekea nje.
Alikuja kwa usafiri wa mwendokasi hivyo kama ni kurudi nyumbani alipaswa kuondoka kwa mwendokasi.
Wakati akiwa anapita eneo la Posta ya Zamani akitembea huku kichwa chake kikiwa katika mawazo mbalimbali alijikuta akisimama kwa muda na palepale ilionekan kuna wazo lilimuingia , wazo hilo lilimwambia huo sio wakati wa kurudi moja kwa moja geto kwake bali anapaswa kutafuta mahali kukaa na kupunga upepo na mahali alipoona panamfaa ni maeneo ya Kivukoni.
Ukweli ni kwamba wazo hilo lilimjia kutokana na kutaka kukaa chini na kuanza kutafakari mambo ya kimaajabu ambayo yamemtokea siku hio ndio maana.
Hamza maisha yake yalikuwa ni yenye maajabu tokea alivyokuwa mdogo mpaka kufikia wakati huo na msururu wa maajabu huo ulionekana kutokukoma katika maisha yake.
Maisha ni msururu wa mshangao , mzuri na mbaya na hatujui ni kipi kipo katika dakika nne zinazofuatia na hichi ndio kinafanya maisha yawe ni yenye msisimko mkubwa na muda ambao maisha yanapokutupia mshangao chukua muda wako kutathimini yale ambayo hayakuwa ndani ya matarajo na hicho ndio ambacho aliona.
Hamza alitumia zaidi ya lisaa kufikiria kile ambacho kimetokea siku hio , licha ya kwamba alikuwa na mambo mengi ya kuwazia lakini ambalo limetokea siku hio alilipa kipaumbele.
Ukweli ni kwamba hakujua kitakacho kwenda kutokea kwanzia siku zitakazofuatia lakini aliamini chochote kile ambacho kitamtokea kitakuwa ni jambo lenye msisimko mkubwa.
Alikuja kushitushwa na simu yake ambayo ilianza kuita mfululizo na mara baada ya kuotoa na kuangalia aliekuwa akimpigia ni Mama mmoja ambaye alishawahi kwenda kufanya kazi kwake kwa kutengeneza AC(Air Conditioner) yake ilipoharibika na alishangaa mama huyo kumpigia lakini moja kwa moja alijua lazima atakuwa na kazi hivyo alipokea kwa furaha zote.
Ijapokuwa alikuwa na pesa nyingi mfukoni ambazo zingemtosha katika matumizi ya takribani mwezi mmoja kabla ya kupokea mshahara wake wa kwanza lakini bado hakutaka kudharau kazi ambazo zimemsukuma na kumfikisha leo hio.
“Kijana habari yako?”
Sauti ya mwanamama mtu mzima iliweza kusikika upande wa pili ya simu.
“Salama mama habari za masiku?”
“Ni nzuri tu , bado unapatikana hapa Dar sik hizi?”
“Ndio Mama nipo”
“Oh! basi vizuri, kuna jirani yangu nae kapatwa na shida kama ileile ya kwangu , je unaweza kufiika kumsaidia kumtengenezea?”
“Mama mimi kama malipo yapo ninaweza kuja hata muda huu?”
“Asante sana baba yangu , mimi nipo kazini kwasasa lakini yeye pia atakuwa ndio anatoka kazini nitakupatia namba yake uwasiliane nae ukifika”
“Sawa mama Asante kwa kuniunganisha na hii kazi?”Aliongea Hamza na mara baada ya simu kukatwa alitoa tabasamu na kuangalia saa yake na kuona ilikuwa imetimu saa tisa hivi.
Ukweli muda huo alikuwa akijichukulia kama mwajiriwa lakini kwasababu kwake pesa ilikuwa kipaumbele hakuona haja ya kukataa kazi , hata hivyo licha ya kwamba chuoni alikuwa akisomea maswala ya uhumi na uhasibu lakini ukweli alikuwa akipendasana kazi ya ufundi , ni kama alikuwa na kipaji hicho kwani kazi ambazo nyingi alikuwa akifanya zilikuwa ni za ufundi, kusoma uhasibu ilikuwa ni sehemu ya maagizo ya Mzee.
Shukrani kwa mtandao wa The Job uliweza kumuunganisha na watu wengi ndani ya jiji la Dar es salaam ambao wana shida na maswala ya ufundi na ndio katika mtandao huo ambapo aliweza kupata kazi kwa mama huyo.
Eneo la kazi ilikuwa ni Kigamboni na kwasababu alikuwa kivukoni ilikuwa rahisi kusafiri kutoka hapo kuelekea huko lakini alikuja kugundua kwamba hakuwa na vitu muhimu vya kumsaidia kutengeneza lakini kutokana na kuwa na hela kidogo mfukoni aliona atapitia dukani na kununua vifaa.
Kazi yenyewe ilikuwa ni kurekebisha AC hivyo licha ya kwamba mama huyo kamwambia tatizo lilikuwa kama la kwake matatizo ya AC hayafanani hivyo kwanza alipaswa kuona tatizo na hapo ndio atajua namna ya kudili na tatizo.
Dakika chache Hamza alikuwa ashafika katika Apartment za Lotus , jambo moja ambalo Hamza alipenda kwenye hizo Apartment ni kwamba zilikuwa zikikaa wanawake tupu tena wale ambao hawajaolewa.
Unaweza ukashangaa lakini inasemekeana ndio utaratibu uliowekwa na mmiliki wa Apartment hizo ambazo asilimia kubwa ya wanaoshi hapo ni wafanyakazi a kampuni ya Dosam Global.
Sio kwamba kampuni hio ilikuwa ikipendelea wanawake, hapana bali ukweli ni kwamba ilikuwa imejenga majengo hayo kwa kulingana na stutus, yaani kama mwanamke ameolewa basi haruhusiwi kukaa ndani ya Apartment hizo.
Ni sehemu maarufu sana ndani ya jiji la Dar es salaam kwa kuwa na warembo wa viwango , yaani hakuna pisi mbovu ambazo zilikuwa zikishi ndani ya jengo hilo na hio yote ni kutokana na aina yao ya kazi , asilimia kubwa ya wafanyakazi wa Dosam wa kike aidha ni wafanyakazi ndani ya hoteli, Shopping Mall, Wahudumu wa ndege na Benki.
Yaani kwa haraka sana ni kwamba kampuni ya Dosam inajihusisha na biashara za miamala(Dosam Bank ) , Usafiri wa Anga (Dosam Air) ,Mahoteli(Dosam hotels and hospitality) na maduka(Dosam Distributions&Department store).
Sasa aina ya kampuni hizo ni kwamba zinahitaji sana wafanyakazi ambao wana mvuto wa kipekee kimuonekano iwe ni mwaname au mwanamke , kwa mfano mhudumu wa Hoteli hawezi kuwa na sura ngumu lazima awe na sura ambayo akitabasamu mgeni palepale anavutik, bila shaka hicho sio kigezo pekee cha kuajiriwa ndani ya kampuni hio kikubwa ni ujuzi na taaluma, moenekano ni sifa ya ziada tu.
Sasa asilimia kubwa ya wafanyakazi wa Dosam walikuwa wakiishi katika Apartment za kampuni kwa wale ambao hawana makazi ,sio sheria kuishi katika Apartment hizo lakini asilimia kubwa ya wafanyakazi walikuwa wakiishi katika Apartment hizo kutokana na kwamba walikuwa wakilipia gharama nusu halafu mazingira ni Premium.
Yaani kama nyumba kwa mwezi ni milioni moja basi mfanyakazi hulipia laki tano, huo ni mfano tu na sio gharama husika..
Sasa nyumba hizo mara nyingi ni kama zimetengwa japo si sheria, kuna Apartment ambayo inachukua tu wanaume ambao ni mabachela na kuna Apartment ambayo ilikuwa ikichukua wanawake ambao ni mabachela na kuna nyingine ambayo ilikuwa ikipangisha wale ambao wameoa au kuolewa , yaani familia.
Sasa katika Apartment zote ambazo zinakaliwa na wafanyakazi wa kampuni ni hio ya Lotus Flower Apartment, hio Apartent ilikuwa na warembo sio mchezo , ilikwa ikiendana na jina lake, wanaume wengi mabachela walikuwa wakitembelea hapo kujaribu bahati zao.
Ukitaka kuthibitisha hilo ni nje ya eneo la apartment hio kulikuwa na Dustibin kubwa ambayo ilikuwa na maua mengi sana pamoja na kadi , yote hayo ni wanaume ambao walikuwa wakitembelea mji huo kwa ajili ya kujaribu bahati zao na pale ambapo wanakataliwa wanaishia kutupa maua yao pamoja na kadi zao kwenye Dustibin hizo na kuondoka.
Hamza alikuwa akisikia habari za Apartment hii lakini ukweli ni kwamba siku ambayo alikuja kufanya kazi ilikuwa ni muda wa mchana muda wa kazi hivyo hakukutana na warembo wengi.
Ilikuwa ni muda ambao Hamza anakaribia kufika ndani ya Aparttn hizo , mita kadhaa kabla ya lilipo geti aliweza kuona gari mbili zilikiwa zimesimama, moja ilikuwa ni gari aina ya Aud na nyingine ilikuwa ni gari aina ya Noah.
Kwa macho yake ambayo yanaona mbali aliweza kushuhudia mwanamke ambaye alikuwa amezingirwa na wanaume na ilionekana ni kama vile wanaume wale walikuwa wakibishana hivi na yule msichana kwa kumzonga zonga.
Hamza jambo lile lilimtia shauku na kuongeza mwendo ili kujua kililichokuwa kikiendelea , ukweli ni kwamba hata kama asingetaka kujua angejua tu kwani watu hao walikuwa wamesimama njiani kuingia katika Apartment hizo.
“Eliza nimechoshwa na majibu yako ya kis**nge , ninachotaka leo hii ni pesa zangu na si vinginevyo”Mzee mmoja mwenye mwili ambao ulikuwa umetuna kidogo aliongea.
“Mzee Amosi nilishakuambia nivumilie , hela unayonidai ni nyingi na sasa hivi sina uwezo wa kupata mkopo tena, unafikiri kiasi chote hicho nitatoa wapi , isitoshe hela ambazo nimekupatia ni kiasi kikubwa mno kuliko hata ulichonikopesha, unachonidai hapa ni riba”
“Sitaki maelezo yako Eliza yashanichosha na kila siku unatoa kauli zinazofanana , hivyo leo una chaguzi mbili aidha ukubaliane na sharti ambalo nakuambia kila siku na tuondoke pamoja urudi kesho au unipate pesa yangu leo hii, kama hela huna na sharti langu hukubaliani nalo basi vijana niliokuja nao watafanya kazi yao”Aliongea kwa kufoka.
Hamza ambaye ndio sasa amekaribia karibu alikuwa akisikia kila kitu na kwa haraka haraka aliweza kuelewa kinachoendelea, kwanza ilionekana watu hao walimkinga mwanadada huyo kupitisha gari kuingia ndani na ilionekana walikuwa wakimdai pesa.
Kadri mzozo huo ulivyokuwa ukiongezeka wanawake baadhi ambao walikuwa wakiishi ndani ya hilo eneo walikuwa wanajikusanya huku wakionyesha hofu ya kuamulia ule ugomvi , ni kama walikuwa wakimjua huyo mzee ambaye anaonyesha yupo kifujo fujo hata kama anadai pesa yake.
“Mzee Amosi naomba usinifanyie hivyo , kwanini unakosa utu?”
“Haha,… leo ndio unasema sina utu , wakati nakupatia pesa yangu nani alimbembeleza mwenzake, kama nisingekuwa na utu nisingekupatia kiasi chote kile cha pesa , sasa mama yako amekwisha kupona lakini unashindwa kulipa pesa yangu , kingine unasema unalipa riba kwani makubaliano yetu yapoje wakati unachukua mkopo?, hebu acha kupoteza muda , nimekupa njia nyepesi kabisa lakini unaleta maringo , kwani mimi ni mbaya sana mpaka ushindwe kutii sharti langu dogo namna hio?”
Hamza ambaye mara baada ya kusikia kauli hio alijua kabisa hapo huyo mwanaume sio kama alikuwa na shida sana ya pesa au huyo mwanadada mrembo alikuwa ameshindwa kulipa ila ilionekana analazimisha kulipwa pesa yake hapo hapo akijua huyo mwanadada atashindwa kuitoa ili akubaliane na sharti lingine ambalo kwa haraka haraka alijua ni ngono.
Hamza alifikiria kidogo mwanamke aliekuwa akizongwa alionekana kuwa mrembo mno, lakini kwasababu watu walikuwa wakiongezeka kukusanyika ndani ya eneo hilo hakuona haja ya kuendelea kusimama kwani muda ulikuwa ukisogea kwa kasi hivyo palepale alitoa simu yake na kutafuta namba ambayo alitumiwa na kisha akaipiga.
Akiwa amesogea pembeni ya barabara aliweza kusikia simu ile ilikuwa ikiita pasipo ya kupokelewa na iliita mpaka ikakatika , akarudia kupiga na ikaita mpaka ikakatika mara baada ya kurudia mara ya nne akijiambia isipopokelewa anaondoka palepale simu ilipokelewa.
“Sikia Eliza sitaki kukudhalilisha na isitoshe mimi na wewe tumetoka mbali , kama huna hela kwanini tusiwe wote wastaarabu,ongozana na mimi na kuondoka mbele ya macho haya ya watu?”
“Helloo..!!!”
Hamza alianza kuongea lakini sauti ambayo ameweza kusikia ni ya mwanaume ambae anamdai Eliza , palepale aligeuza sura yake na kuangalia upande wa ugomvi unapoendelea na alikuwa haoni vizuri kutokana na kuzibiwa na watu na ilimfanya kusogea karibu zaidi.
“Boss amepokea simu..?”
“Kijana ambaye alikuwa karibu na yule mzee alieitwa Amosi aliongea na kauli ile ilimfanya Amosi kumwangalia Eliza mkononni mwake na palepale alimpokonya ile simu.
“Umetutegeshea simu sio , Eliza kwanini unaenda mbali hivi?”Aliongea huku hasira zikionekana zaidi na zaidi katika macho yake huku akiwa tayari ashakata ile simu.
Upande wa Hamza mara baada ya simu ile kukatwa palepale alijua mtu ambaye anapaswa kuja kumfanyia kazi ni huyo mrembo ambaye anadhalilishwa na wadeni wake.
“Nakuuliza ulikuwa ukiongea na nani?”Amosi alipatwa na mashaka na palepale alimshikilia mkono na kummnya Eliza kwenye gari.
“Puuh!!!”
Haikueleweka imekuwaje lakini Amosi alijikuta akidondoka kurudi nyuma kwa kasi ya ajabu kama vile amevutwa.
Kitendo kile kilishangaza waliokuwa wakiangaliana na hapo hapo ndipo sasa waligundua Amosi alikuwa amevutwa kurudi nyuma na kijana ambaye alikuwa amefika hapo muda huo.
Hata Eliza hakujua namna ambavyo Amosi alitoka mbele yake na alijikuta akiinua uso wake ambao alikuwa amefumba macho kwa kile ambacho alitegemea kufanyiwa na hapo ndipo alipoweza kushuhudia sura ya kijana ambaye amesimama mbele yake.
“Dogo unakitafuta kifo sio?”Mzee Amosi mara baada ya akili yake kufanya kazi alionyesha kukasirika mno kwa kile alichofanyiwa.
“Mzee hebu tuliza kwanza jazba najua una shida na huyu mwanadada lakini vilevile na mimi nina shida nae”Aliongea Hamza kwa sauti iliojaa upole , ni kama alikuwa akitania hivi na kufanya watu kumshangaa , hata Eliza mwenyewe alionekana kushangaa na kujiuliza huyo kijana ni nani kwanini anajiingiza kwenye mgogoro wake na kusababisha matatizo zaidi.
“Chongolo mnashangaa nini , hebu mshikisheni kwanza adabu ndio tuongee nae vizuri na kumjua ni nani”Aliongea Amosi kwa hasira , hakutaka kusikia ngonjera za kijana huyo.
Chongolo mara baada ya akili yake kurudishwa kwenye uhalisia ni kama alishituka na palepale pamoja na wenzake wawili walimsogelea Hamza kwa ajili ya kumdhibiti.
“Mamaa…!!!”
Kijana mmoja ambae alikuwa kimbelembele mara baada ya kumsogelea Hamza alijikuta akipigwa teke la kigoti na kumfanya atoe ukulele huku akichuchumaa chini kutokana na maumivu.
Kitendo kile kilishangazwa wengi kwani kilitokea kwa spidi ya hali ya juu sana kutoka kwa Hamza , ilikuwa ni kama vile alikuwa na uzoefu wa hali ya juu kwenye kudili na watu wa namna hio.
Wale wengine mara baada ya kuona kiilichomtokea wenzao ni kama hawakuaini amini kama shamblizi hilo lilitoka kwa kijana wasiemjua na moja kwa moja hasira zao ziliongezeka mara mbili na kusogelea Hamza kwa kasi.
Puuh! , Bam!!!”
Chongolo mara baada ya kumsogelea Hamza kwa ajili ya kurusha ngumi mkono wake ulidakwa ukiwa hewani na kuvutwa mbele , wakati huo huo yule mwenzake aliekuwa nyuma akipigwa teke la makagari na kumfanya adondoke kama furushi huku Chongolo akisukumiziwa kwenye kiooo cha mbele cha gari ya Noah kiasi cha kutengeneza ufa.
“Sikutaka kwenda mbali hivi ila nachukia kupotezewa muda, Mzee unaonaje ukirudi siku nyingine kudai pesa yako, nahitaji kumalizana na huyu mrembo mapema nirudi kwenye shughuli zangu nyingine”Aliongea Hamza huku akimwangalia Mzee Amosi ambae alionekana kuwa katika kiwewe asiamini vijana wake watatu aliokuwa akiwaamini kupambana na watu ndani ya dakika moja tu wamedhibitiwa na wote wanaugulia maumivu.
Alimwangalia Hamza kwa macho yasiokuwa ya kawaida kama kwamba alikuwa akimtathimini.
Mzee Amosi alionekana kutafakari kwa muda , kwa jinsi alivyomuona Hamza akifanya mashambulizi na kupitia uzoefu wake wa miaka mingi kuna kitu alikiona haraka haraka na hakutaka kuendelea kuuliza ni nani.
“Chongolo tuondokeni tutarudi , Eliza jiandae siku nitakayorudi sitokuwa na huruma tena , ni kheri upige simu mapema kabla ya kukutafuta”Aliongea Mzee yule huku akimwangalia Eliza kwa macho makali na kisha alipangua watu na kuingia ndani ya gari.
Hamza mara baada ya kuona mzee huyo amekuwa mtiifu kwake alijikuta akivuta pumzi za ahueni maana hakutaka kwenda mbali sana.
Wakati akiona amefanya jambo la kawaida upande wa watu waliokuwa ndani ya eneo hilo walionekana kuwa katika mshangao, kila mtu alikuwa na lake kichwani na kuna wale walioamini huenda Hamza ni mwanajeshi licha ya kwamba muonekano wake haukuwa ukisanifu kile alichokifanya.
Mrembo Eliza alikuwa ni kama haamini alikuwa amesalimika na aliemsaidia ni kijana aliekuwa mbele yake ambaye ndio mara yake ya kwanza kukutana nae, maswali kibao yalichipua katika akili yake lakini alishindwa kuuliza zaidi ya kumwangalia Hamza bila ya neno.
Hamza ni kama sasa alikuwa akimthaminisha mrembo huyo , wakati anafanya maamuzi ya kumsaidia mwanamke huyo hakufikiria sana kwa sababau aliamini akifukuza watu wale kazi yake iliomleta hapo itaisha haraka na kupata ujira wake , lakini mara baada ya kukutanisha macho na msichana huyo aliekuwa katika hali ya mshangao ni kama sasa alikuwa akipata wazo la pili.
“Kwanini ndani ya hizi siku chache nimekuwa nikikutana na wanawake warembo namna hii , hii ni ishara nzuri kwangu au mbaya?”Hamza alijiuliza swali hilo.
Alikumbuka wakati alipokuwa katika Apartment za Dosam Homes alikutana na mwanamke aliefahamika kwa jina la Tresha Noah, akaja kukutana na mrembo aliempelekea chungu , hatimae Prisca , Mrembo Regita ambae ndio alimshangaza zaidi na hatimae leo hio anakutana na msichana aliefahamika kwa jina la Eliza.
Kama angewapangilia warembo hao kulingana na uzuri wao basi Regina angeshika namba moja , Prisca namba mbili , huyo Eliza namba tatu , Anitha namba nne na kisha Tresha Noah namba tano.
Ukweli Tresha Noah alikuwa akifikiana uzuri na huyo Eliza lakini alikosa vigezo katika macho ya Hamza mara baada ya Amiri kumwambia uzuri wake ni wa kutengeneza.
“Kaka upo vizuri kwa kweli , ni mara ya kwanza kuona mtu mwenye uwezo wa kuwashinda wale Vibaka ,Wewe ni mwanajeshi au polisi , Vipi Eliza ni mpenzi wako?”Kundi lile la wanawake waliokuwa wakiangalia tukio hilo walimzunguka Hamza wakitaka kusikia neno kutoka kwake.
“Eliza kumbe una mpenzi mwanajeshi na husemi jirani?”Aliongea wanamama mwingine na kumfanya Eliza kushangazwa na swali hilo na kuishia kumwangalia Hamza.
“Jamani mimi sina mahusiano na huyu dada , mimi ni fundi na nimekuja kutengeneza AC , kama kuna yoyote mwenye shida inayohitaji fundi nipo hapa natengeneza kila kitu”
Kauli ya Hamza iliwashangaza wanawake waliokuwa wamemsikia , ila kauli ile ni kama haijamfurahisha Eliza ni kama vile alitamani Hamza akubali na aseme niwapenzi hata yeye mwenyewe alijishangaa kuwa na mawazo ya namna hio , pengine ni kutokana na kuwa single kwa muda mrefu..
“Handsome , upo siriasi unatengeneza kila kitu?, unaonaje ukatengeneza na moyo wangu ulioumizwa”Aliongea mrembo mmoja ambae alikuwa ametumia Make up nyingi mno huku akiwa na kikuku mguuni.
“Recho..!!!”Aliongea Eliza ambae ni kama vile ameamka sasa kutoka kwenye mshangao na kumsogelea Hamza.
“Kaka tunaweza kwenda ukaanganlie shida ya Ac yangu”Aliongea Eliza na kwasababu alikuwa na aibu za kutosha kuendelea kukaa katika eneo hilo kwa yale yaliomsibu alimchukua Hamza na wakaingia ndani huku wakimwacha mwanadada aliefahamika kwa jina la Recho akivuta mdomo.
Hamza alikuwa kimya kimya na mwanamke huyo mpaka wanaingia kwenye lift, ilikuwa ni kama vile amerudi kwenye upole wake.
Ukweli ni kwamba Hamza kimuonekano alikuwa mpole sana lakini matendo yake yalikuwa tofauti na yeye alivyo , haikueleweka ana historia gani ya maisha yake ya yuma lakini ni rahisi kuotea maisha yake hayakuwa ya kawaida.
Eliza na yeye ilikuwa mara yake ya kwanza kusaidiwa na mwanaume , tena mbele ya wale waliokuwa wakimdai.
“Asante kaka kwa kunisaidia”Aliongea Eliza kwa kukosa kujiamini na kumshitua Hamza aliekuwa akijiwazia mambo ya ajabu na yote hayo ni kutokana na kumtamani mrembo huyo Eliza.
“Hii tabia ya kuwazia kile mwanamke inatokana na kukosa mchezo muda mrefu nini?”Alijiwazia Hamza.
“Hakuna shida ya kunishukuru Eliza , kama nilivyosema nimekusaidia ili kumaliza kazi yangu kwa haraka”Aliongea Hamza huku akijiona kidume na kauli ile ilimfanya Eliza kumwangalia Hamza kwa macho ya kidadisi, ni kama vile alikuwa amejawa na hamu ya kumjua vizuri Hamza.
Kwa mtu yoyote pengine siku hio angevutiwa na Hamza hususani kwa muonekao wake na kwa kile abacho amefanya dakika chache zilizopita.
Hamza hakuwa amebadili mavazi yake ambayo yalikuwa mapya na mtindo wa nywele ulikuwa umempendeza sasa ukijumlisha na ngozi yake yenye mchanganyo wa kizungu ilimfanya kuwa mtanashati kupindukia na hakika mwanamke yoyote angempenda na kuvutiwa nae , siku hio hakuwa akionekana kama fundi kabisa , kwa kumlinganisha na mrembo Eliza moja kwa moja kwa tu asie na uelewa atasema wawili hao ni wapenzi kwa namna wanavyoendana.
“Ding..!!!”
Lift ilifunguka katika Ghorofa ya kumi na tano ambayo ndio mwisho kabisa , mazingira ya Jengo hilo yalikuwa yakvutia mno , yamejaa ufahari wa macho , Ijapokuwa haikuwa kama apartment za Dosam Homes lakini ni mazingira ambayo yanatosha kuhifadhi watu wa vipato vya kati na juu.
“Karibu kaka”
“Asante , unaweza kuniita Hamza”Aliongea Hamza huku akijitahidi kuonekana mpole mbele ya mwanamke huyo , ni kama alikuwa akijitahidi kumpangawisha Eliza.
“Oh karibu sana Hamza fundi”Aliongea na kumfanya Hamza kutabasamu, alitamani aendelee kuisikia sauti ya Eliza kwani ni kama ilikuwa ikibembeleza.
Kama alivyotegemea nyumba hio ilikuwa safi mno na mpangilio wake ulikuwa ni wa kiwango cha juu , kulingana na uzoefu wa Hamza hata apartment ya Mellisa mwanamke wa Amiri haikuwa na mpangilio safi kama huo , ijapokuwa hakuona chumbani kulivyo lakini eneo la sebuleni lilimpa picha.
Wazungu wanasema ‘A house is a mirror to its owner’ hivyo mazingira ya eneo hilo yalimpa picha kamili Eliza ni mwanamke wa namna gani.
“Hamza sijui nikukaribishe kwanza kinywaji au uanze kazi moja kwa moja nikikuandalia chochote”Aliongea Eliza ambae alionekana kukosa kujiamini kwa namna flani hivi , pengine ilikuwa ni kwasababu ya kile kilichomtokea dakika kadhaa ilizopita mpaka Hamza kuingilia kati.
“Kwa leo naomba niende moja kwa moja kwenye ufundi , itakuwa vizuri baada ya ufundi kupata hata juisi tu itatosha kutia baraka”Aliongea Hamza akijiamini .
*****
Upande mwingine ikiwa ni dakika kadhaa tokea kuondoka kwa Amosi na kundi lake , ikiwa ni kilomita kadhaa kutoka eneo hilo la Apartment walienda kusimamisha gari katika moja ya mgahawa na kabla ya Amosi kushuka aliwaangalia vijana wake waliokuwa hawajiamini kwa kile kilichotokea na kisha akavuta pumzi.
“Chongolo nadhani unajua hii kazi hainihusu mimi moja kwa moja bali ni bosi, kama atasikie kile ambacho kimetokea leo hii nadhani kuna swala lolote ambalo litatokea , nani anajua anachokiwaza bosi sasa hivi?”Aliongea Amosi.
“Mkuu tunapaswa kufanya nini?”
“Inamaana bado tu hamjaelewa ninachomaanisha , mbona mnakuwa na vichwa vidogo namna hii”Aliongea Amosi huku akionyesha kukasirika , ni kama aliongea kauli tatanishi ili mradi wasielewe ili tu awafokee kupunguza hasira zake.
“Sikieni kuhusu Eliza hili swala nitaongea na bosi mwenyewe , ninachotaka ni kumfatilia yule mpuuzi alievuruga mipango yetu, kazi hii inaanza sasa hivi mtaondoka na gari”Aliongea Amosi na palepale akashuka kwenye gari na kisha akaingia katika Mgahawa huo.
Hazikupita dakika kadhaa Chongolo na wenzake waliondosha gari hio ya Noah na kutokomea upande waliotokea.
Amosi alitembea kiwasiwasi kuingia ndani ya Mgahawa huo wa kisasa , kulikuwa na watu wachache sana lakini hao wachache walionyesha ni wale wenye uwezo mkubwa wa kifedha.
“Unavyonifanyia sio vizuri , unajua kabisa nakupenda lakini kwanini leo unataka kukatisha mahusiano yetu , kwanini unanifanyia hivi Chriss”
“Anitha unaenda mbali na nadhani akili yako haifanyi kazi vizuri , mimi na wewe nani alitaka mahusiano , ulinifuata mwenyewe ukitaka niwe Boyfriend wako kwa muda kuwaringishia wenzako lakini kwa huruma zangu tumefikisha mwezi huu , unataka nini kutoka kwangu , leo ndio mwisho maana nina mtu tayari ninaempenda , naomba uondoke nina mazungumzo muhimu na Amosi”Aliongea mwanaume mmoja mtanashati sana aliekuwa amekaa kwenye Kona ya mgahawa huo huku mbele yake akiwa ni msichana mrembo ambae alionyesha hali ya kutaka kulia katika macho yake,
Kwa kauli mbili tu ambazo Amosi aliweza kusikia alijua fika kile kinachoendelea , ila hakutaka kuongea neno kwanza bosi wake amalizane na mlimbwende huyo.
Mwanamke huyo aliefahamika kwa jina la Anitha alionekana kuwa na hasira mno na mwanaume aliefahamika kwa jina la Chriss , kwa kile kilichokuwa kikionekana hapo ni kama msichana huyo anafosi penzi kwa kijana huyo.
“Anitha nimesema naomba uondoke , mkataba wangu na wewe umeisha leo hii”Alirudia Chriss kuongea na msichana mrembo wa haja alimwangalia mwanaume huyo kwa macho yaliojaa hasira na kisha akasimama na kuchukua mkoba wake.
“Siku moja utakuja kujua mimi ndio mtu ninaekupenda kwa dhati na sio pesa zako Chriss na utakuwa umechelewa”Aliongea na kisha palepale akageuka na kuondoka.
Amosi ambae alikuwa amesimama pembeni ya meza hio aliishia kugeuza shingo kumtathimini mwanamke ambae analilia penzi , na aliishia kuona wivu kwani msichana huyo alikuwa amebarikiwa kila kitu , alikuwa ni mrembo haswa kuliko maelezo , pengine katika maisha yake na uzee huo hajawahi kuwa na mwanamke wa urembo huo , hata kuota kuwa na mwanamke wa namna hio hajawahi , sasa kijana aliekuwa mbele yake alikuwa na uwezo wa kuacha mwanamke mrembo huyo ambae analilia penzi , aliona wivu na kujiambia katika maisha pengine sio pesa tu na muonekano pia huvutia zaidi wanawake.
“Chriss huyu binti ni mrembo sana , lakini kuna haja gani ya kumuacha namna hii ni bora ungemdanganya na kuendelea nae pale unapomhitaji”AliongeaAmosi huku akikaa kwenye kile kiti.
“Nina sababu za kuachana nae ambazo hata wewe ukizijua hutonilaumu”Aliongea na kumfanya Amosi kutabasamu..
“Wewe na mzee wako mna tabia zinazofanana , tatizo mnapenda sana wanawake lakini kudumu nao hamuwezi”
“Haha .. Siwezi kufanana na yule mzee mimi , ni muhuni kupindukia, sidhani kuna mwanamke mrembo ambae ashawahi kumvutia akashindwa kumpata”Aliongea Chriss na kumfanya Amosi kutabasamu na kujiambia kwa wakati mmoja Chriss hakuwa akimfahammu baba yake vizuri , sio kila mwanamke anaemtaka ashawahi kumpata, kwani ni mwaka wa pili huo alikuwa akihaha kutaka kumuweka Eliza kwenye himaya yake lakini imeshindikana.
“Nimeitikia wito bosi wangu , simu kama hizi hunipa hamasa kwani naamini kuna malipo”Aliongea Amosi huku akiweka tabasamu.
“Haha.. Amosi mimi napenda watu wanaopenda pesa kama wewe , ndio maana kila inapokuja swala linalohitaji juhudi na uharaka wa utimilifu jina lako hujitokeza”
“Hii ndio kazi inayoniweka mjini , ijapokuwa pesa ni kipaumbele lakini matokeo mazuri nazingatia sana , kuna wanaopenda pesa zaidi kiasi cha kutumbukia kwenye utapeli, matokeo ndio kila kitu baada ya malipo”
“Haha.. Ijapokuwa unaniita bosi lakini wewe ni mtu mzima sana kwangu , si shaka kuwa na busara na nidhamu katika kazi yako , anyway tokea nikujue kupitia baba nimekuwa na shauku sana kuyajua maisha yako lakini maswali hayo nitayaweka kapuni kwa leo na niende moja kwa moja kwa kilichonifanya nikutafute”Aliongea lakini kwa sauti yake ilimfanya Amosi kuona hali ya kusita sita katika macho ya Chriss.
“Kuna mwanamke nataka unisaidie kumtafuta”Hatimae Chriss aliongea na kumfanya Amosi kushangaa kidogo.
“Mwanamke!!!?”
“Ndio mwanamke , kuhusu taarifa zake faili lake utaletewa kesho ofisini kwako, Mzee Amosi nimekuita tuongee swala hili ili kuonyesha ni kwa namna gani ni swala muhimu, hii inaweza kuwa kazi kubwa kuwahi kuipata tokea kuanza kwako kazi ya maswala ya kijasusi..”Alisita kidogo na kisha akaendelea kuongea.
“Kuna watu nyuma yangu juu ya hii kazi , mimi ni kama Freelancer , ijapokuwa sitowataja ni wakina nani kwa ajili ya usalama wako na wangu lakini wapo tayari kulipa kiasi chochote cha pesa , cha msingi ni matokeo ya kuridhisha”Aliongea na kwa namna Amosi alivyokuwa akimuona Chriss alihisi uzito wa kazi yenyewe maana bwana huyo mara nyingi alionekana kutokuwa siriasi lakini kwa namna flani ni kama hofu ilianza kumvaa.
“Kwa muonekano inaonekana sio kazi ya kawaida na inahitaji rasilimali za ki uwezeshaji?”
“Haha.. Amosi unaonekana kuwa na uelewa wa haraka , ndio maana Mzee anakuita jasusi nje ya mfumo,, kama ulivyosema mimi ni kama Freelancer katika hii kazi hivyo nipo tayari kuwekeza kiasi cha pesa kwako kwa ajili ya uwezeshaji wa ukamilishaji wa hii kazi, tutaanza na milioni mia moja”Aliongea Chriss.
“Milioni mia moja!!?”Amosi alishangaa mno.
“Kama ni milioni mia moja kama rasilimali uwezeshaji inamaana…..”
“Ndio Amosi , kazi hii ni ya mabilioni ya pesa , wenye uhitaji wa kukamilisha kazi hii wanataka ifanikiwe kwa haraka na kwa ufanisi lakini wapo Desparate, ukubwa wa pesa unaendana na ukubwa wa kazi yenyewe hivyo usishangae”Aliongea Chirss na kumfanya Amosi kumeza mate mengi.
“Nipo tayari juu ya kazi hii”Aliongea Amosi bila ya kufikiria , ukweli kilichomfanya kutoa jibu la haraka haraka sio ukubwa wa kiasi cha pesa bali ni shauku juu ya kazi yenyewe , kama anataka matokeo ya kazi hio anataka kutoa mapesa mengi kiasi hicho basi jambo hilo linaweza kumshangaza.
“Safi Amosi, unaonekana kuwa na shauku , hata mimi nilipokea kazi hii kutokana na shauku, nadhani tutazungumza zaidi baada ya kupokea faili, kumbuka usiri mkubwa unahitajika katika kazi hii na tahadhari zote zimechukuliwa, katika faili kutaambatana na fomu ya makubalianao ya kufanya jambo hili kuwa siri”Aliongea na Amosi alitingisha kichwa.
****
Dakika chache mbele mara baada ya Hamza kuelezewa tatizo la AC aliweza kuijua shida yake kabla hata hajafanya uchunguzi , ilionekana kulikuwa na shida ya kipima joto cha AC hivyo kufanya Ac kushindwa kukadiria kiwango flani cha ubaridi ndani ya nyumba hio.
Hamza hilo halikuwa tatizo kubwa kwake na aliweza kurekebisha haraka haraka na kumaliza lakini hakuishia hapo tu alijaribbu kuagalia na shida nyingine na aligundua kulikuwa na vumbi jingi upande wa Evaporator Coill hivyo alijaribub kurekebisha, mpaka anakuja kumaliza kazi yake ni kama nusu saa imepita na alijihisi njaa.
Kilichomfanya kuhisi njaa ni harufu ya chakula iliokuwa ikisambaa ndani ya nyumba hio ikimaanisha mrembo Eliza alikuwa jikoni.
“Inaonekana huyu mwanamke amekamilika kila idara , sio kwa kunukiza huku”Alijiwazia Hamza huku akijifuta vumbi kwenye mikono yake na Hangerchief , shati ambalo alikuwa amevaa lilikuwa limechafuka kutokana na kuparamia ukuta wakati wakusafisha Ac hio.
Inaweza ikawa kazi nyepesi kwa Hamza kutokana na uzoefu lakini kwa mtu mwingine ingekuwa kazi ngumu mno , kwani kwanza ilimhitaji kuchungulia upande wa nje wa jengo hilo , jambo ambalo lilikuwa likiogopesha kutokana na urefu wa jengo.
“Nishamaliza kazi yako , kulikuwa na shida ya setting tu na nimerekebisha”Aliogea Hamza huku akimwangalia Eliza ambae alionekana kutokea upande wa jikoni kuja eneo la sebulenni, alikuwa amependeza kwa mavazi ya kinyumbani zaidi na kumfanya kuonekana wife material.
“Oh!, Asante kaka yangu , naona pia namna ulivyochafuka”
“Yeah, wakati mama ananipigia kuja nnilikuwa nimetoka mahali na kuona nisiende nyumbani moja kwa moja”
“Na maamuzi yako yemeishia kuniokoa siku ya leo , nashindwa hata kuelezea tukio hili , linanifanya niwe na aibu mbele yako”Aliongea Eliza huku sauti yake ikionekana ni ya kusita sita na hakukutanisha macho kumwangalia Hamza .
“Ni swala la kawaida ambalo linaweza kumtokea yoyote , watu wa aina ile hawana mipaka na ni vizuri kutojihusisha nao”
“Asante sana , Hamza sijui nakushukuru vipi lakini naamini kile ulichokifanya ni kwa ajili ya kuninsaidia , kila mtu alikuwa akifurahia kudhalilika kwangu, ni swala la kawaida kwa binadamu , nadhani dunia sio mbaya kama nilivokuwa nikifiiria , umekuwa mtu wa kwanza kusimama upande wangu..”Aliongea Eliza huku hali yake ya kihisia ilionekana kubadilika mara moja jambo ambalo lilimshangaza Hamza , ilikuwa ni kama ashasoma Eliza ni mwanamke ambae alikuwa amepitia changamoto za kimaisha na kutokana hali ile ya kubadilika alishindwa kujua ni hatua gani achukue.
“Eh! , jamani naunguza..!!!”Aliongea Eliza akiwa kama ameshituka na kukimbilia jikoni na kumfanya Hamza atabasamu na kukaa kwenye sofa akimsubiria achukue pesa yake na aondoke maana muda ulikuwa umeenda.
“Samahani kwa kukuchelewesha mwaya , naandaa chakula cha kupeleka hospitalini , muda naona umeenda , unaonaje ukipata kabisa chakula cha usiku?”Aliongea Eliza huku akionekana kutokujiamini.
“Pole kwa kuuguza”
“Asante , nimeshapoa”Aliongea.
“Sasa mimi nisikucheleweshe , kwasababu kazi ilionileta ni ufundi na nishaimaliza ngoja nikuache uendelee na ratiba zingine”
“Malipo yatakuwa kiasi gani?”
“Nipatie elfu kumi tu inatosha “Aliongea Hamza , ijapokuwa mwanamke huyo alikuwa akimfanya amwambe nimetengeneza bure lakini aliona ni udhaifu hivyo anapaswa kuchukua chake.
Eliza palepale aliingia chumbani na kutoka na noti mbili za elfu kumi na kisha kumpatia Hamza.
“Sidhani ni sawa nikikuita fundi au Hamza wewe ni mwokozi wangu leo hii na angalau nilipaswa kukupa chochote kuweka baraka zaidi ya hii juisi, hii ya ufundi na hii naomba utumie kama nauli”
“Wewe unaweza kuniita fundi , namba yangu inayo ukiwa na tatizo unaweza kuniambia muda wowote nitafika”Aliongea Hamza na kupokea ile hela , hakutaka kukataa malipo ya elfu ishirini , ijapokuwa alijua mwanamke huyo alikuwa na matatizo lakini kama atakataa angeonekana kama alikuwa na ajenda zaidi ya moja.
Baada ya hela kama kawaida alipewa juisi na Korosho lakini Hamza kutokana na haraka na kutomfanya mwanamke huyo kuwa na wasiwasi ,korosho aliweka kwenye koti na juisi akainywa kama maji na kisha akaaga na kuondoka.
*******
Saa mbili kamili za usiku ndani ya mgahawa wa Golden Fork mbezi Beach ilisimama gari nzuri ya thamani aina ya BMW 14Oi ya rangi ya blue metallic.
Ilikuwa gari nzuri kweli iliofanya watu baadhi waliokwa wamekaa upande wa madirisha yanayoangaliana na maegesho kukaza macho kwa mtu anaeshuka katika gari hio.
Dakika kama moja kupita aliweza kutoka mtu katika gari hio ,ijapokuwa ilikuwa usiku na taa hazikuwa kali sana lakini ilitosha kuwafanya watu kukaza macho zaidi, kwani mwanamke alietoka katika gari hio hakuwa wa kawaida,alikuwa mrembo haswa japo kwa macho ya Hamza ambae ameshakutana na mrembo Regina angemuweka pengine nafasi ya tatu au ya pili mwanamke huyo.
Akiwa si mwenye kujali macho yanayomwangalia alizipiga hatua kuingia ndani ya mgahawa huo huku waliokuwa wakimtathimini wakitaka kujua yupo peke yake au kuna mtu amefika hapo kwa ajili ya kukutana nae.
Mwanamke huyo alievalia suruali ya rangi nyeupe na blazia ya rangi ya bluu alitembea kwa kuchezesha miguu yake na viatu vyake vya high heels mpaka upande wa kulia wa mgahawa huo huku nyuma akiacha usumbufu wa marashi yake.
“Alex!, umefika muda mrefu sana?”Aliongea yule mwanamke baada ya kumfikia mwanaume aliekuwa ameketi kwenye meza peke yake upande wa kulia wa mgahawa huo ,sehemu ambayo ni kama imejitenga.
“Wakati na kutumia meseji ndio nilikuwa nikikaribia , ni kama dakika ishirini zilizopita, kwanza sijategemea kama ungewahi maana najua wanawake na tabia zenu”Aliongea Alex kwa namna flani hivi ya kukosa amani kutokana na uzuri wa mwanamke huyo.
“Wewe mwenyewe ndio ulitaka usumbufu wa kukutana , malipo yangeweza kufanyika kwa njia ya mtandao kwanini unataka Cash?”
“Nadhani ushajua sababu ya mimi kutaka Cash Frida , nataka kuongea na wewe maana kuna mambo mengi bado sijayaelewa , mimi ndio ambae nilikuwa nikikuletea mzigo na hakuna kosa la aina yoyote limetokea , Frida kama ni lile swala la kuzielezea hisia zangu kwako naomba usahau , chukulia kama halijatokea na kazi iendelee”Aliongea Alex akiwa katika hali ya kulalamika hivi mbele ya mwanamke huyo , kwa macho ya haraka ilikuwa ni sawa na kusema alikuwa akimpenda huyo mwanamke lakini ilionekana mwanamke alikuwa amemkataa.
Mwanamke aliefahamika kwa jina la Frida alitoa tabasamu huku akimwangalia Hamza bila ya kujibu akimpa nafasi muhudumu kuweka juisi alioagiza kisha aendelee kuongea.
“Tatizo lako Alex unakosa focus, wewe ni mfanyabiashara lakini unakuwa kama vile ni mwajiriwa”
“Unamaanisha nini kusema hivyo??”
“Namaanisha utaendelea kutii kile ambacho ninahitaji kama mteja wako na si vingineyvyo,kuhusu sababu ulizoelezea kwangu huwa sizipi kipaummbele sana, wewe sio wa kwanza hata hivyo,anyway nimekuja hapa kwa maswala mawili tu, la kwanza ni kukupatia mzigo wako na hii ni mara ya mwisho sisi kuonana moja kwa moja , malipo yote yatafanyika kwa njia za kawaida , pili Alex acha kuuliza maswali mengi , wewe fanya biashara na kidhi mahitaji ya mteja wako , maswali mengi huua uaminifu, Nadhani kuna sheria na vigezo umepatiwa na Binamu mpaka kukidhi kuendesha biashara zao”Aliongea Frida huku akinywa juisi ile kimapozi.
“Lazima awe Hamza , Frida kuna ajenda gani, yeye ana nini mpaka ndio awe mwenye kukuletea mzigo?”
“Lazima awe Hamza ndio na si vingineyo , nadhani unashindwa kuelewa nilichokuambia , hizi ni hela zako natumaini mahitaji yangu katika mtazamo wa kibiashara yatashughulikiwa ipasavyo , Alex nakuambia mara nyingine acha kuuliza sana maswali , fanya biashara”Aliongea Frida na kisha alitoa bahasha na kuiweka mezani na kisha akamwinamia Alex na kumbusu shavuni la kwaheri ya kuoanana.
Busu lile lilimfanya Alex mwili wake wote kusisimka lakini kwa Frida ilionekana ni kitendo cha kuficha kile kilichokuwa kikiendele kati yao , ijapokuwa walikuwa wamejitenga lakini eneo hilo lilikuwa wazi kufanya watu wawaone.
Alex aliishia kumwangalia mrembo Frida akitokomea kwenye macho yake , hata ile hamu ya kuendelea kukaa hapo ilikuwa imempotea , mwanamke huyo alikuwa akimvutia kimapenzi mno.
Alex kama mfanyabiashara maarufu wa vyungu jijini Dar es salaam alikuwa akifanya biashara na wateja wengi ambao sio wa kutafuta bali ni wale wa oda , yaani ki ufupi ni kwamba biashara yake haikuwa ya kujitangaza kama zilivyo biashara nyingi , alikuwa kama mfanyabiashara ambae ameridhika na wateja aliokuwa nao lakni ukweli ni kwamba sio kama kile kilichokuwa kikionekana , wateja wake alikuwa akiwatafuta kwa namna za upekee sana na mathalani sio yeye ambae anawatafuta , wapo watu wa kazi hio.
Sasa kati ya wateja ambao anafanya nao kazi ni mwanamke mrembo , Frida , ijapokuwa mwanamke huyu hakuwa mrembo sana kuliko wanawake wote aliokuwa akifanya nao biashara lakini Frida ni aina ya wanawake ambao walianza kumvutia kingono kwa mara ya kwanza tu kuonana nae , pengine ni ile tabia ya mwanamke huyo ya kizungu ndio iliomfanya kumvutia kingono , mwanzoni ulikuwa ni mvuto wa kupenda kufanya nae ngono na Alex aliamini kwa namna yoyote ile lazima mwanamke huyo angeingia kwenye kumi na nane zake kama wanawake wengi ambao amepita nao , ‘hakuna mkate mgumu mbele ya chai’ ndio falsafa yake ya siku zote kila anapomtongoza mwanamke , hivyo aliamini falsafa hio hio ingefanya kazi kwa Frida lakini kinyume chake mwanamke huyo mlimbwende wa haja hakuwa na haraka nae , ki ufupi licha ya kwamba alikuwa mwanamke wa kujiachia achia lakini alionekana ni wanawake ambao si rahisi kumvua nguo moja tu ambayo mara nyingi Alex ndio humkuta nayo kila alipokuwa akipeleka mzigo wa chungu.
Mara nyingi mwanamke huyo angemkuta akiwa na nguo za kuogelea tu akipunga upepo na kusitiri manyonyo na kitumbua pekee huku akiacha kila kitu wazi , tabia ambayo ilizidi kumpagawisha mno Alex , ule ugumu wa mwanamke huyo ulimfanya kuanza kutengeneza chembechembe za kihisia na hapo ndipo ambao alipojihisi kupenda.
Kitu pekee ambacho kilianza kumchanganya Alex ni siku kadhaa nyuma mara baada ya Frida kumwambia anahitaji mwanaume aliefahamika kwa jina la Hamza Mzee kumletea mzigo wake kila siku.
Alex alishangaa , ndio alishangaa kwani Hamza alikuwa ni mtu wa kawaida mno kufahamika kwa Frida na hata yeye aliona pengine Frida anamaanisha Hamza mwingine , lakini kwa msisitizo Frida alimwambia ni Hamza huyo huyo anaemfikiria.
Japo swala hili lilimshangaza lakini lilimpa shauku na maswali mengi kichwani, akijiuliza inakuwaje Frida mwanamke mrembo anaemsumbua kumfahamu Hamza na kwanini anataka yeye ndio amletee delivery.
Kama kawaida ya Frida alikuwa ni mtu wa kuongea mara moja na atakachotaka ni vitendo ndio ambavyo alimpa Alex namna ya kupinga maamuzi yake.
Alex alikuwa na maswali , lakini biashara yake ilipaswa kuendelea na tokea amekabidhiwa biashara hio kulikuwa na misingi ya sheria ambayo alitakiwa kuifuata , kwanza hakupaswa kuwa na maswali mengi kwa wateja na anapaswa kuwasikiliza kwa chochote wanachohitaji na ikitokea amevunja kanuni hizo basi ilitosha kuhamishwa kikazi au kuachishwa kabisa.
Hivyo akiwa na wasiwasi wake na shauku aliamua kutii takwa la mteja wake na kumfuata Hamza kwa ajili ya kazi hio , bila shaka alikuwa na matumaini makubwa Hamza hawezi kukataa kazi ya donge nono hilo ,alijiambia ni rahisi kumchimba Hamza zaidi kuliko ilivyo kwa Frida ambae alionekana kama mwanamke msiri.
Dakika chache mara baada ya kupokea simu kutoka kwa Frida juu ya mzigo kufika , huku mwanamke huyo akionyesha furaha yake ya kuletewa na mzigo na Hamza ilimfanya Alex kutaka kumhoji Frida ana kwa ana ndio maana akawekeana miadi nae kwa kisingizo kwamba anahitaji pesa yake cash, wazo zima ilikuwa ni kutaka kujua au Frida alikuwa na hisia za kimapenzi na Hamza ,au Hamza alishawahi kufahamiana na Frida lakini kulingana na Hamza ilionekana ni kama wawili hao hawafahamiani kabisa.
Sasa anapata nafasi ya kumhoji Frida mrembo lakini bado anashindwa kupata majibu anayotaka.
“Kuna kitu kinaendelea kuhusu huyu Frida , nina uhakika sio swala la kimapenzi , Hamza ni nani kwanini mwanamke kama huyu mrembo mwenye pesa anataka kuweka ukaribu na Hamza kupitia delivery ya vyungu”Kichwa cha Alex kilicheza , alijua lazima Frida alikuwa akilenga kujenga ukaribu na Hamza.
Zikiwa ni dakika chache baada ya Frida kutoa gari yake katika mgahawa wa Golden Fork , akiwa anaendesha katika barabara ya Bagamoyo uelekeo wa Jogoo, heads up display(HUD) ya gari yake ilionyesha ujumbe ambao ulikuwa kama vile ni kodi.
“Board to Alamos!!
Ujumbe huo ulisomeka hivyo na Frida bila ya kubadili uelekeo alikanyaga pedeli zaidi akiongeza spidi.
Comments