CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Draxton alikuwa amesimama huku akimwangalia mwanamke huyu kwa umakini uliopitiliza, naye Namouih akavikaza viganja vyake vilivyoshikilia bastola kwa chini, akiwa ameingiwa na hofu kiasi lakini akijitahidi kuonyesha ujasiri. Ni suala la ni jinsi gani mtu huyo alifika nyuma yake ghafla namna hiyo wakati hakuonekana sehemu yoyote ile sekunde chache nyuma.
"Unafanya nini?" Draxton akauliza kwa umakini.
"Naonekana kama nafanya nini?" Namouih akajibu lakini kwa swali.
Draxton akaiangalia bastola aliyoishika mwanamke huyo, naye Namouih akaikaza vizuri zaidi na kujiweka tayari kumshambulia nayo endapo kama angejaribu kuleta mzaha mbaya, akiwa hajasahau pia kwamba kifaa chake kidogo cha kurekodi sauti kilikuwa kinafanya kazi yake.
"Hii itakuwa ni mara ya kwanza na ya mwisho kukwambia hivi. Achana na mimi," Draxton akamwambia kiutulivu.
"Nimekushika wapi?" Namouih akauliza kwa ujasiri.
"Kaa mbali na mimi wewe mwanamke..." Draxton akasema kwa uthabiti.
"Kwani tatizo ni nini attorney? Unaficha nini huku? Huwa unakuja kuzika wafu au?"
"Haikuhusu. Ninakuomba uingie kwenye gari lako uondoke."
"Ah-ah subiri. Tuongee kidogo. Sisi... mimi na wewe... we're cut out from the same cloth... kwa hiyo kama kuna siri, basi naweza kukusaidia kuitunza..." Namouih akaongea kikejeli.
Draxton akainamisha uso wake kuonyesha amekerwa.
"Niambie kama una tatizo lolote tusaidiane," Namouih akasema.
"Utanipatia msaada gani? Kunipiga kwa risasi?"
"Oh, kwa hiyo unasema kwamba ndiyo, una tatizo..."
"What's it to you? Kwani we' unataka nini?"
"Nataka tu nikusaidie...."
"Sihitaji msaada wako!" Draxton akamkatisha kwa ukali.
Namouih akabaki kumtazama.
"Nenda. Nakuomba uende," Draxton akamwambia kiutulivu.
"Hapana. Siondoki. Siondoki mpaka uniambie wewe ni nani..."
"Nini?"
"Wewe ni nani? Wewe ni mtu wa aina gani? Unagongwa kwa gari haufi? Unaingia kwenye kesi siku moja tu tayari umeshajua fact zote za mambo ambayo hata mtuhumiwa wako unayemsimamia hajui?"
"Kwani... unaongelea nini, sikuelewi...."
"Ukiguswa tu kidogo na mwanamke unachemka kama pasi na kukimbia, ni kwa nini?"
Draxton akakaza sura na macho yake kimaswali.
"Na unakuja huku msituni kufanya nini? For a guy anayejifanya kuwa mnyoofu sana una mambo mengi yanayokutia mashakani..." Namouih akamwambia.
"Why are you so obsessed with me?"
"Sina muda wa kuwa obsessed nawe. Umeingia kwenye maisha ya rafiki yangu na kuanza kuyarusha danadana kama vile hayana thamani, na hilo linaniathiri mimi pia. Ukiingia mahakamani unajifanya unajua sana kutetea haki, lakini kila kitu kukuhusu ni question mark inayotakiwa kutafutiwa majibu haraka sana, la sivyo utayaharibu maisha ya...."
"Mimi siyo mmiliki wa maisha ya mtu! Huyo rafiki yako nimemfunga mikono? Wanaume wameisha duniani au? Na kwani maisha yake binafsi yanakuchoma vipi wewe mpaka unakosa kutumia busara na kunifatilia mimi? Inakupa faida gani?" Draxton akaongea kwa ukali.
"Siyo kuhusu rafiki yangu tu...."
"Nimekwambia ondoka. Ondoka sasa hivi..."
"Au utanifanya nini? Na mimi utanikata tumbo kama hao wasichana unaowapoteza na kuwaua?"
Draxton akakaza macho yake na kuishika shingo ya Namouih ghafla sana! Namouih alitaka kutenda kwa uharaka ili amfyatulie risasi mguuni, lakini mkono mmoja wa Draxton ukaishika mikono yake iliyoshikilia bastola na kuikandamiza kwa nguvu, hivyo Namouih akashindwa kuielekeza kwa jamaa. Draxton akamsukuma na kumkandamiza kwenye gari lake, huku akimwangalia kwa hasira sana, naye Namouih akawa anapumua kwa kasi lakini kwa shida.
"Niachie.... niache...."
Namouih akajaribu kutoa sauti lakini ikawa kavu mno kutokana na jinsi alivyokazwa shingoni. Draxton akaubamiza mkono mmoja wa mwanamke huyu kwenye gari uliokuwa umeshikilia bastola, na Namouih akaidondosha chini. Kisha jamaa akaacha kumkaba na kubaki amemwangalia tu, naye Namouih akaanza kukohoa sana.
"Kalia kimya kile usichokijua. Narudia tena, hii iwe mara ya mwisho unanifatilia. Ninakuomba uondoke," Draxton akamwambia kwa mkazo.
Namouih alikuwa amejishika shingoni sasa huku akimtazama, na kwa hasira akampiga Draxton sehemu za siri kwa goti lake ili amuumize kutokana na jinsi alivyomtendea. Lakini akashangaa sana baada ya kufanya hivyo na mwanaume huyu kutoonyesha dalili yoyote ya maumivu. Ikamwingia akilini kuwa inawezekana kweli jamaa hakuhisi maumivu kwa kukumbukia usiku ule walipomgonga mtu mwenye tattoo kama yake, na huenda ilikuwa ni huyu huyu ingawa walitofautiana kwa kadiri fulani.
Mwanamke akataka kuiokota bastola yake upesi ili aitumie tena, lakini Draxton akaushika mkono wake huo, sehemu ya chini ya kiganja (wrist), akiukaza kwa nguvu sana. Namouih akawa anajaribu kuutoa mkono wa Draxton lakini akashindwa. Draxton ni kama alikuwa anaongeza nguvu ya kuukaza mkono wa mwanamke huyu ingawa hakuonyesha jitihada yoyote hata usoni kwake, akimtazama Namouih kwa njia ya kawaida tu. Kadiri alivyoendelea kuukaza ndivyo jinsi Namouih alivyohisi kudhoofika, naye akalegea na kupiga magoti huku sura yake ikionyeaha namna alivyohisi maumivu.
"Aaih... mamaa... unaniumiza...."
Namouih akanena hivyo kwa sauti kama ya msichana anayelia, naye Draxton akawa anamwangalia kutokea juu kwa njia fulani yenye huruma kiasi. Akaulegeza mkono wake uliomkaza mwanamke, naye Namouih akautoa wake na kumsukuma kidogo kwa mwingine, akionyesha kukasirika bado. Akawa amejishika mkono wake wenye maumivu huku akimtazama kwa mkazo, naye Draxton akajishika kichwani kwa kiganja chake kama vile kuonyesha kinamuuma. Akakaza meno yake kwa nguvu, kisha akaichukua bastola ya Namouih na kumnyanyua kwa nguvu mpaka akasimama.
Mwanaume huyo akaanza kumvuta kwa lazima kuelekea gari lake (Namouih), halafu akamwingiza na kumfungia mlango kwa nguvu baada ya kuirushia bastola yake siti za nyuma. Namouih akawa anamwangalia tu kwa hasira mpaka jamaa alipoanza kuondoka na kulifata gari lake, kisha akaligeuza na kuondoka eneo hilo. Namouih akiwa amebaki hapo, ndani ya gari lake, alikuwa akiangalia sehemu ile ya mkono Draxton aliyomkaza kwa nguvu. Ilikuwa nyekundu hasa kutokana na ngozi yake nyeupe kuwa laini, na bado msuguo aliohisi uliendelea kumpa maumivu kiasi.
Pamoja na kwamba alijitahidi kuonyesha ushupavu wake mbele ya mwanaume huyo, hakupata chochote cha maana katika uchunguzi wake huu zaidi ya kuambulia maumivu tu. Lakini alikasirishwa sana na kitendo ambacho Draxton alikuwa amemfanyia, na hiyo ikafanya aazimie hata zaidi kufichua yale yaliyokuwa yamefichwa na mwanaume huyo mwenye uajabu wa hali ya juu. Akawasha gari lake na kuondoka huko pia.
★★
Alifika nyumbani kwake tena kwenye mida ya saa kumi na mbili na nusu jioni. Alikuta gari la mume wake likiwa hapo tayari, na hicho ni kitu ambacho hakutarajia, yaani Efraim Donald kurudi mapema bila kumwambia. Akaelekea ndani na kumkuta sehemu ya sebule ya chini, akiwa amekaa kwenye sofa huku akitazama mechi kwenye TV yao kubwa sana ukutani, naye akaelekea usawa wake na kumsalimu. Alikuwa amejishika sehemu ile ya mkono wake ili Efraim asione ulivyotiwa alama nyekundu.
"Ulifika saa ngapi?" Namouih akamuuliza.
"Muda siyo mrefu sana. Nilikuwa tu nimewahi mechi hii kuiangalizia huku," Efraim Donald akamwambia.
"Oooh... kombe la dunia kweli. Sawa. Ngoja nikajimwagie halafu nishuke..."
"Ulikuwa wapi?" Efraim akauliza.
Namouih akamtazama kimaswali, kisha akasema, "Nilikuwa ofisini, unauliza nilikuwa wapi tena?"
"Nimepita kwa Edward wakati nakuja, nikakucheki hukuwepo. Na Esma ameniambia ulifika hapa kwanza halafu ukaondoka. Ulikuwa ofisi gani?"
"Ahah... Efraim ngoja kwanza nikaoge, nitakwambia. Nimechoka...."
"Umechoshwa na nini?" Efraim akauliza.
Namouih akaangalia pembeni.
"Namouih... njoo ukae hapa," Efraim akamwambia.
"Efraim... siko fresh... nahitaji..."
"Nimesema njoo ukae hapa," Efraim Donald akamwambia kwa utulivu.
Namouih, akionekana kutoridhia, akaelekea alipoketi mume wake na kukaa pia. Efraim Donald alikuwa anamtazama kwa umakini sana, na Namouih akawa ameangalia chini tu huku amejishika mkono wake.
"Umefanyaje mkono?" Efraim akauliza.
"Sijafanya kitu," Namouih akajibu kama ameudhika.
Mume wake akauchukua mkono huo kwa lazima na kuutazama, naye Namouih akakunja uso kuonyesha anaumia kiasi.
"Hii alama imetoka wapi?" Efraim akauliza.
Namouih akabaki kimya tu.
"Sema Namouih," Efraim Donald akaongea kwa uthabiti.
Namouih akautoa mkono wake kwake na kusema, "Kuna mtu tu nimekorofishana naye, ndiyo aka...."
Kabla hajamaliza maneno yake, Efraim akasimama na kuifata rimoti mezani, kisha akazima kabisa runinga kuonyesha kwamba alitaka umakini wake wote uwe kwa mke wake. Akarudi kwake akiwa amevuta kiti kidogo cha sofa cha kuwekea miguu kilichokuwa pembezoni mwa meza hiyo, naye akakikalia; sasa akiwa anatazamana uso kwa uso na mke wake.
"Nataka uniambie ni nani amekufanya hivi, na kwa nini," Efraim Donald akasema kwa utulivu.
Namouih akatulia kidogo, kisha akasema, "Ni Draxton."
Efraim akarudisha uso wake nyuma kidogo, akiwa ameshangaa kiasi. "Attorney Draxton?" akauliza.
Namouih akatikisa kichwa kukubali.
"Kwa nini akufanye hivi?"
"Ni kuhusu ile ishu nilivyokwambia. Yule kaka hajakaa sawa, ni wa ajabu sana. Ninahisi anahusika kabisa na mambo ambayo Felix amekuwa akichunguza kuhusiana na vifo vya wasichana wengi kwa muda mrefu, na ninahofia anaweza kumuumiza Blandina. Lakini naye hasikii, amemng'ang'ania tu wakati mtu hata haonyeshi kumpenda... leo alikuwa ameenda msituni huko, sijui kufanya nini. Ana pigo za kichawi yule siyo wa kumwamini... ni kama...."
Namouih akaishia hapo baada ya kutambua kwamba mume wake alikuwa anamwangalia tu, kwa njia iliyoonyesha haamini mashaka ya mke wake.
"Mbona unaniangalia hivyo?" Namouih akauliza.
Efraim Donald akashusha pumzi, kisha akauliza, "Kwa hiyo... umemfatilia leo... mpaka huko msituni... kumuuliza ikiwa ni yeye ndiyo anawaua hao wasichana, au... ikiwa yeye ni mchawi?"
"Unataka ku-imply nini Efraim?"
"No, no, usiniulize swali, nipe jibu. Umeenda ukamhoji... ndiyo akakufanyaje... akakupiga?"
"Hapana hajanipiga. Nilikuwa namuuliza anieleze ni kwa nini anafanya vitu ambavyo.... akakasirika, ndiyo akanikandamiza mkono..."
"Yaani akukandamize mkono kwa sababu tu umemuuliza? Namouih nakujua, umefanya nini kingine?"
Namouih akatulia kidogo, kisha akasema, "Nili... nilimtishia kumpiga kwa bastola."
Efraim akashangaa. "Bastola? Umetoa wapi bastola?"
Namouih akabaki tu kumtazama machoni.
"Oh my God... Namouih!" Efraim Donald akasema hivyo baada ya kuwa ametambua kwamba mke wake alimaanisha bastola yake yeye Efraim.
"Efraim nisikilize. Instinct zangu zinaniambia kabisa kwamba huyo kaka ni mtu mbaya. Siku ile tulipomgonga yule mtu sijui kiumbe gani, niliona tattoo ambayo...."
"Halafu mje kusema wanaume hatuwakililizi, lakini mkiongea ni vitu pointless," Efraim akamkatisha.
Namouih akamkazia macho na kuuliza, "Unamaanisha nini? Unasema kwamba nakudanganya?"
"Namouih nilikwambia hayo masuala achana nayo. Unamsumbua kaka wa watu kwa sababu tu umeota ndoto za kutisha?"
"Efraim...."
"Siyo watu wote watakuwa jinsi unavyotaka Namouih, na kama haufurahishwi na mtu fulani achana naye... siyo kuanza kumsakama. Hii yote kwa sababu ulipoteza kesi dhidi yake? Na tena na hapo ni yeye ndiyo alikuwa sahihi. Haya masuala ya wasichana kuuawa, Namouih, waachie maaskari. Usijiingize huko. Hata kama mimi ndiyo ningekuwa Draxton ningekasirika maana umeanza kumsakama kijana wa watu tokea mara ya kwanza alipofika hapa, na hata hajawahi kuonyesha ubaya. Kuna watu wangapi kwenye hii nchi wa kushuku kwa sababu ya hayo mauaji unayoongelea halafu wewe umemkazania Draxton tu?"
Efraim Donald aliongea hayo kwa uthabiti kabisa, naye Namouih akainamisha uso wake kidogo. Alionekana kuhuzunika sana mpaka machozi yakaanza kumlenga, naye Efraim akaketi kwenye sofa tena na kupitisha mkono wake begani kwa mke wake ili ambembeleze kidogo.
"Sikia Namouih. Mimi sitaki uingie matatizoni kwa sababu ya vitu kama hivi. Wewe ni muhimu sana hapa. Mambo yaliyo nje ya kazi yako yasikuumize kichwa, na usikazane kuchunguza maisha ya watu mpaka kufikia hatua za namna hii. Leo umekwanguliwa mkono, kesho ukinyofolewa kichwa je? Umeshafikiria mama, Sasha, na Nasma watasonga vipi bila wewe?" Efraim akamwambia kwa upole.
Namouih akajitahidi kuikaza midomo yake ili asilie. Efraim Donald akakilaza kichwa cha mke wake usawa wa kifua chake, akimpa kumbatio hilo ili kumtuliza. Alimdekeza sana.
"Niambie hautafanya jambo kama hili tena honey," Efraim akasema.
Namouih akatikisa kichwa kukubali, kisha akakinyanyua kichwa chake kutoka kifuani kwa mumewe na kuketi sawa.
"Nitaongea na Draxton kuhusu suala la yeye kukukaza mkono..." Efraim akamwambia.
"Hapana, haina shida. Uko sahihi. Sikuwa nimetambua kwamba nimevuka mipaka. Sitarudia," Namouih akasema.
"Oh honey, sipendi kukuona namna hii. Okay, you know what? Nenda kajisafishe, vaa vizuri halafu tutoke, sawa? Twende uagize chochote unachotaka," Efraim akamwambia ili kumchangamsha.
Namouih akatabasamu kidogo na kutikisa kichwa kukubali, kisha Efraim Donald akambusu shavuni na kumwambia airudishe bastola kule kule alikoitoa maana ingeweza kuwa hatari kwake, na Namouih akaanza kuzifata ngazi ili apande kuelekea juu. Dada wa watu akaenda mpaka chumbani na kuingia bafuni bila kukawia ili kutoa uchovu mwingi na kuweza kujiandaa kutoka na mumewe. Bado tukio la awali kule msituni liliendelea kuzunguka kichwani kwake, lakini akajitahidi kutoliacha limharibie "mood" yake aliyotaka kuifanya iwe nzuri kwa ajili ya mume wake. Hii haingemaanisha kwamba suala hilo angelipuuzia kabisa, kwa kuwa tayari alikuwa ameshafikiria njia mbadala ya kujua ukweli kumhusu Draxton.
★★★
Tunaelekea mpaka upande mwingine wa jiji ambako kuna mtu muhimu sana kwa Namouih. Huyu si mwingine ila mdogo wake kipenzi, binti mpole na mrembo sana aitwaye Sasha. Huku ndiko alikokuwa anaendelea na masomo yake ya vidato, na kwa wakati huu ndiyo alikuwa anatarajia kuingia kidato cha sita. Tokea alipojiunga na shule yake kuendelea na masomo, aliishi bwenini, yale mabweni ya shule yanayokuwa yamejengwa eneo tofauti na shule yenyewe, lakini si mbali sana. Kwa vipindi ambavyo wangekuwa na likizo, Sasha hakurudi nyumbani kwao kabisa, bali angekaa kwenye chumba cha kupanga pamoja na rafiki yake aliyesoma pamoja naye, lakini yeye akiwa siyo wa bweni. Rafiki yake aliitwa Sabrina, aliyekuwa na miaka 20.
Wakati huu Sasha alikuwa pamoja naye, zikiwa zimebaki wiki kadhaa kabla ya masomo kuanza rasmi, naye alikuwa amepatwa na shida fulani iliyomkosesha amani sana, tena sana. Alikuwa na mawazo mengi mno. Kila mara ambapo kungekuwa na likizo, angetumia muda mwingi pamoja na Sabrina kutembelea maeneo mbalimbali, kujifurahisha kwa njia nyingi pamoja na rafiki zao wengine waliokuwa huku, na kuwa pamoja na mpenzi wake aliyeitwa Shomari, mwanaume kijana aliyefanya shughuli ndogo tu ya uuzaji wa bidhaa mbalimbali za madukani na za kisasa. Alianza mahusiano na kijana huyo mwenye sura nzuri mwanzoni kabisa alipofika jijini kuanza kidato cha tano, na alimpenda sana kwa sababu alikuwa mtaratibu na mchapakazi.
Lakini kilichokuwa kimemkosesha amani Sasha kwa wakati huu ilikuwa ni huyo huyo Shomari, na sababu ilikuwa ni kubwa sana. Kwa wiki mbili mfululizo, Sasha alionekana kukosa raha kabisa, na kila mara ambayo Sabrina alimuuliza tatizo lilikuwa nini, binti aligoma kusema. Mwishowe, jioni ya siku hii baada ya Sabrina kutoka mizunguko na kurudi ndani ya chumba walichopanga, alimkuta Sasha akilia kabisa kitandani, na hilo likamtatiza sana. Alitaka kujua nini hasa kilichomsumbua mwenzake, hivyo akalazimisha sana kumfanya aseme mpaka Sasha alipolegeza na kufunguka hatimaye.
Akiwa anajikaza kulia, Sasha akasema, "Ni Shomari."
Sabrina alikuwa ameketi naye kitandani huku akimwangalia kwa umakini, naye akauliza, "Shomari amekufanya nini?"
Sasha akabaki kimya kwa ufupi.
"Niambie Sasha, amekufanyaje? Ameku-cheat? Au amekupakazia maushenzi?" Sabrina akauliza tena.
Sasha akatikisa kichwa kukanusha. Sabrina akaendelea kumtazama akisubiri jibu.
"Nilimpa Shomari hela... nilimkopesha. Lakini sasa hivi kila nikimtafuta simpati... sijui ameenda wapi?" Sasha akasema huku machozi yakitiririka.
"Umempa hela? Umempa shi'ngapi?"
"Laki tisa..."
"Laki tisa? Sasha umempa mwanaume laki tisa?!" Sabrina akashangaa.
Sasha akatikisa kichwa kukubali huku akijifuta machozi na mengine yakiendelea kumtoka.
"Kwa nini umempa laki.... umezitoa wapi?"
"Hhh... alinipa dada..."
"Za nini?"
"Ada."
"Eh Mungu wangu!" Sabrina akashangaa zaidi na kujishika shavu.
Sasha akaendelea kulia bila kutoa sauti ya juu.
"Sasha jamani! Kweli unampa mtu hela ya ada, aifanyie nini?"
"Alisema angeirudisha. Mara zote huwa anarudisha... hata hii nilijua... ahhh...." Sasha akashindwa kuendelea.
"Mara zote? Unamaanisha huwa una kawaida ya kumpa hela?"
"Akiwa anahitaji ya haraka kama ninayo nampa... hhh... halafu anairudisha kila tarehe aliyo-promise..."
"Ndiyo umpe laki tisa? Kwanza... dada yako si huwa analipia ada moja kwa moja kwa akaunti ya shule? Imekuwaje akakupa wewe?"
"Zamu hii alinipa nije kulipia ya mwaka mzima mpaka tukimaliza cha sita... na ya matumizi yangu pia. Sasa... ahh... me... aliponitumia niliona nisubirie mpaka tukikaribia kuanza Ili ndiyo nikalipie. Lakini Shomari aliniomba nimsaidie, halafu angeirudisha... ndiyo nikatoa hicho kiasi kwenye ya ada. Ni kawaida... tumeshafanya hivyo sana nyuma nilipokuwa natoa kwenye za matumizi ila sa'hivi kwa kuwa aliomba kubwa kidogo ndiyo nikatoa kwenye ya ada. Sijui tu sasa hivi ime..imekuwaje... labda amepatwa na matatizo huko aliko...."
"Acha kuwa mjinga Sasha. Huyo amekuibia. Amekuibia, kakutapeli, mwanaume tapeli tu huyo!" Sabrina akasema kwa uthabiti.
"Lakini mbona..."
"Hakuna cha lakini Sasha, tumia akili. Hizo mara... hicho kipindi cha nyuma ulikuwaga unampa laki tisa?"
"Hapana. Nimempa laki, tisini, hamsini, laki mbili, na zote angerudisha...."
"Oooh... yuko wapi sasa sasa hivi umempa laki tisa? Alikwambia angeirudisha lini?"
"Tarehe ya wiki iliyopita..."
"Ai jamani! Sasha..." Sabrina akasikitika.
Sasha akaendelea kulia.
"Siku hizi mambo ya kuaminiana kwenye mapenzi mpaka unampa mtu hela ndefu namna hiyo hayapo. Hayapo Sasha. Watu... ah... watu siyo jinsi wanavyoonekana rafiki yangu, siyo kabisa. Ameshakutia hasara sasa. Laki tisa... dada yako alikupa shi'ngapi?"
"Hhh... milioni moja na nusu..."
"Jamani!"
"Yaani sijui nitafanyaje Sabrina... Namouih ataniua mimi..."
Sabrina akamwangalia kwa huruma sana. "Umemtafuta huyo mbwa kila sehemu hujampata?" akamuuliza.
"Hayupo. Pale alipopanga hayupo, dukani hayupo, kwa simu simpati, yaani aah... nahisi dunia imenilemea jamani... sijui nifanyeje..." Sasha akasema kwa huzuni.
"Sasha... futa machozi. Futa machozi, twende polisi sasa hivi!" Sabrina akamwambia.
"Hapana Sabrina!" Sasha akakataa.
"Hapana nini?"
"Nikienda polisi Namouih... Namouih... Namouih ataniua Sabrina..."
"Kwa hiyo ukiendelea kukaa hapa kulia hizo pesa ndiyo zitarudi? Unajua usipofanya lolote dada yako ndiyo atakuua vizuri zaidi? Twende polisi, waambie hiyo hela huyo mshenzi amekuibia... hata dada yako akijua ataona kweli umeibiwa... Sasha..."
"Hapana Sabrina. Namouih ana akili sana. Atajua tu nilimpa me mwenyewe, na atajua alikuwa mpenzi wangu wakati ni kati ya vitu alivyoniambia niepuke kwanza kwa wakati huu. Ni ujinga wangu tu mimi. Kujaribu kuonyesha nampenda mtu halafu nimeangukia pua... oh Allah... nitafanya nini?"
Sasha aliongea kwa majonzi sana mpaka Sabrina akaingiwa na simanzi.
"Sasha... nisikilize. Ni lazima kuwe na kitu cha kufanya. Hauwezi kukaa tu kusubiri muujiza, na ninaelewa jinsi dada yako alivyo mkali. Hiyo ni hela nyingi sana, na sasa hivi maisha ni magumu kucheza na pesa na kuiacha ipotee tu hivyo," Sabrina akasema ukweli.
"Najua. Uko sahihi. Yaani natamani muda ungerudi nyuma... sijui itakuwaje. Namouih... amenipigania kwa vitu vingi sana... ataumia mno akijua nimeivunja trust aliyonayo kwangu. Sikutegemea yaani Sabrina... kumuumiza dada yangu ni kitu ambacho sitaki, na sijawahi taka kitokee kabisa... lakini ndiyo nilichokifanya... aahh... labda itakuwa bora tu kama akiniua kabisa...."
"Hawezi kufanya hivyo bwana..."
"Ndiyo najua... najua. Sabrina ni kujua kwamba hataniua kihalisi ndiyo kutafanya nihisi kama ameniua... kwa sababu atanichukia sana," Sasha akaongea kwa uchungu.
"Hatakuchukia... wewe bado ni mdogo wake. Dada yako anakupenda sana..." Sabrina akajaribu kumtia moyo.
"Atanichukia Sabrina... sana... amefanya mengi... atachoka... aahh..." Sasha akasema hivyo na kuufunika uso wake kwa viganja huku akilia kwa huzuni.
Sabrina alimtazama rafiki yake sana, akitafakari kuhusu nini afanye ili kumsaidia. Hangeweza kujizuia kuwaza kwamba haya yote yalikuwa ni makosa ya Sasha mwenyewe, na malipo ndiyo yalikuwa hayo. Ila kumsaidia lilikuwa jambo la muhimu sana hasa kwa sababu alimpenda kama dada yake wa damu. Akakaa kutafakari kwa kina kuhusu njia mbalimbali za kumsaidia rafiki yake, na hatimaye, wazo fulani likamjia. Hakuwa na uhakika ikiwa Sasha angekubaliana na hilo wazo, lakini akaona ajaribu kumwambia kwa sababu lilionekana kuwa suluhisho la haraka na pekee ambalo halingemtia matatani, endapo tu kama angekubali kulifanya, na kulifanya kwa umakini.
Akamshika rafiki yake kwa upendo na kuulaza mwili wake kwake, kisha akamwambia amepata wazo mbadala kumsaidia apate pesa za kufidishia kile alichoiba Shomari. Sasha akajifuta machozi na kuweka umakini wake kwa Sabrina, akisikiliza kile ambacho angesema, na rafiki yake akaanza kumpanga kuhusu ni nini afanye ili kuliondoa tatizo hilo bila Namouih kujua. Lilikuwa ni jambo zito kiasi kwa Sasha kuafiki, lakini alijua pia kwamba hakukuwa na njia zingine za haraka za kusuluhisha tatizo lake, hivyo akakubali kulifanyia kazi, na ambacho kingebaki ingekuwa kulitekeleza, kumwachia Mungu, na kusubiri matokeo.
★★★
Wanandoa Efraim Donald na Namouih walirejea nyumbani usiku baada ya kutoka matembezi yao jijini. Angalau wakati huu Namouih alikuwa akijihisi uchangamfu kwa kuwa Efraim alimfanyia mambo mengi yenye kufurahisha na kumnunulia vitu vingi sana. Kwa hiyo walipofika, mwanaume akaona aingie bafuni kujimwagia ili akilala alale vizuri, naye Namouih akamwambia kuna kazi fulani alitaka kwenda kuiweka kwenye laptop yake, iiyokuwa ndani ya ofisi yake ndogo kule chini. Efraim akamwambia asichukue muda mrefu maana bibie alipenda mno kazi, naye Namouih akatoka na kuelekea chini baada ya kuvaa nguo ya kulalia.
Ilikuwa ni mida ya saa sita na nusu usiku sasa. Taa za ndani ya nyumba nzima zilikuwa zimezimwa, isipokuwa ndani ya chumba cha ofisi alichokwenda Namouih. Alikuwa akihamishia ile rekodi ya sauti yake na Draxton aliyorekodi leo kutoka kwenye kile kifaa kidogo na kuiweka kwenye laptop yake ili kuitunza humo, na karibu na miguu yake chini ya meza alilala Angelo. Palikuwa kimya sana, kama vile kuna mtu alibonyeza kitufe cha "mute" kwenye rimoti iliyoendesha sauti zozote ndani ya nyumba hii.
Akiwa anaendelea kubofya kwenye laptop yake, taswira fulani ndani ya akili yake ikamwingia kumfanya atambue kwamba Angelo hakuwa amelala. Alipomtazama chini hapo, akamwona sasa akiwa amesimama, masikio yake yakiwa yamelala nyuma ya kichwa chake, na hata sauti ya mbali ya kuunguruma ilisikika kutoka kwake. Umakini wake ulielekea sehemu ya mlango wa kuingilia ndani ya ofisi hiyo, naye Namouih akatazama huko pia.
Ilimshangaza kiasi kuona kwamba mlango ulikuwa umeacha uwazi mdogo, ingawa alikumbuka kwamba alikuwa ameufunga alipoingia humo muda si mrefu. Hata kama ungekuwa umefunguliwa tena angesikia, lakini kwa kufikiria ni Esma labda, akaona aite.
"Esma... Esma..."
Kimya. Alikuwa ameita kwa sauti isiyo kubwa sana lakini kama kungekuwa na mtu mlangoni basi angesikia, lakini hakupata jibu lolote.
"Efraim..."
Akajaribu kuita na jina la mume wake, lakini hakupata jibu. Alipomwangalia Angelo tena, bado alikuwa ameweka mkao wake ule ule wenye kuonyesha ukali, kisha ghafla paka huyu akaingia zaidi katikati ya miguu ya Namouih kama anajificha. Namouih alipotazama tena mlangoni, akaanza kuona kitu kama kivuli kidogo kikitokea nje ya mlango na kuingia ndani humo taratibu kwenye sakafu. Kilikuwa na umbo dogo, kama vile kidole mwanzoni, lakini kadiri kilivyoingia kiliongezeka upana na kuchukua umbo kama pembe tatu, lenye ufanano na sikio la paka.
Msisimko mkubwa sana ukamwingia mwanamke huyu, ambaye alihisi mwili wake ukianza kutetemeka, hofu ikiwa inajijenga ndani yake, lakini akaendelea tu kutazama jambo hilo. Kadiri kivuli cha "sikio" hilo kilivyozidi kuingia, ndiyo na mlango ukawa unafunguka taratibu, kama vile unasukumwa kwa upepo, au kitu fulani.
Namouih akaifunga laptop yake na kusimama taratibu, kisha akajaribu tena kuita "Efraim" bila kupata itikio lolote. Ilikuwa ni kama "kivuli" hicho kwenye sakafu "kilisikia" alipoita hivyo, kwa kuwa hapo hapo kikaanza kupungua, yaani kikiishia na kutoka ndani ya ofisi hiyo. Ilimfanya Namouih awaze kwamba kulikuwa na kitu fulani kimesimama hapo na kuondoka, na hii haikuwa kwamba labda ni akili yake tu ndiyo inayomchanganya kwa sababu hata Angelo alikiona na kuonyesha kuogopa.
Namouih hakujua ni jinsi gani alipata ujasiri wa kuibeba laptop yake na kutoka ndani ya chumba hiki cha ofisi. Sehemu yote kuanzia hapo ilikuwa na giza, la kawaida tu kwa sababu mambo mengi yalionekana kiasi kutokana na mwangaza wa taa za nje pia, lakini kuvuka hapo na kuanza kupanda ngazi bila kugeuka nyuma ilikuwa ni jambo lililohitaji ujasiri wa hali ya juu. Mapigo ya moyo wake yalidunda kwa nguvu sana kila hatua aliyopiga kuelekea juu zaidi, akihisi ni kama yuko kwenye nyumba ngeni kabisa kwa sababu hakutaka hata kugeuka nyuma kwa jinsi alivyoogopa.
Akafanikiwa kukifikia chumba chake, naye akawasha taa na kuufunga mlango kwa funguo upesi sana huku mikono yake ikitetemeka. Ni hapa ndiyo alihisi kama moyo wake unataka kupasua kifua kwa hofu iliyomwingia baada ya kuhisi kitu fulani kikiugusa mguu wake kwa chini, naye akarusha mguu wake kwa nguvu na kujibamiza mlangoni. Alipoangalia vizuri sasa akawa amemwona Angelo, paka wake, akiwa amerukia upande mwingine, naye akaelewa kuwa mnyama huyo alipanda kuja huku pamoja naye bila yeye kutambua. Alikuwa anapumua kwa kasi kiasi kutokana na woga uliomwingia, lakini akaingiwa pia na huruma baada ya kutambua alikuwa amempiga Angelo kwa nguvu.
Paka wake akamfata tu tena miguuni na kuanza kujisugua taratibu, naye Namouih akatembea haraka kukielekea kitanda huku akimwita. Akaweka laptop yake pembeni na kupanda kitandani, naye Angelo akalalia kigodoro chake kidogo kwa chini. Hakuwaza hata kumshika Efraim na kumsemesha, kwa sababu ilionekana tayari mume wake huyo alikuwa ameshapitiwa na usingizi. Namouih akajifunika kwa blanketi na kulala huku taa ikiwaka. Hakujua ikiwa hata angeweza kupata usingizi, lakini mwishowe akasinzia.
Mwanamke huyu hakuwahi kuogopa giza kabla, lakini baada ya hiki kitu kilichokuwa kimetokea muda mfupi nyuma, alihisi ni kama asingeweza kuja kutazama tena gizani, kwa sababu sasa alitambua kwamba giza lilikuwa linamtazama yeye.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments