CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA TATU
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Kukucha kukakucha. Ikiwa imetimia saa tatu asubuhi siku hii ya Jumamosi, Efraim Donald akaamka na kujigeuza kitandani hapo taratibu ili amwangalie mke wake. Akakuta Namouih akiwa amelalia ubavu wake huku amejifunika kwa blanketi mpaka kichwani, akiacha sehemu ndogo ya uwazi kwenye uso wake. Alikuwa ameikunjia mikono yake kufikia usawa wa shavu, na macho yake yalikuwa yamefunguka huku yakiangalia chini tu kwa njia fulani yenye huzuni. Efraim akajigeuza vizuri na kulalia ubavu wake pia, sasa akiwa anatazamana uso kwa uso na mke wake kwa ukaribu, naye akapitisha mkono wake ndani ya blanketi hilo na kuanza kuzishika nywele laini za mke wake kwa njia ya kuzichezea.
"Good morning," Efraim akasema.
Namouih akamtazama tu machoni.
"Vipi... unajisikiaje sa'hivi?" Efraim akauliza tena.
Lakini Namouih akaendelea kumwangalia kwa njia iliyoonyesha mfadhaiko mwingi, na hilo likafanya Efraim Donald atambue kwamba mke wake hakuamka vizuri.
"Namouih what's wrong?" Efraim akauliza kwa kujali.
Tena, na hapa Namouih akashindwa kusema lolote na kubaki ametulia tu, naye Efraim Donald akamshika kwenye paji la uso kuona kama alikuwa anaumwa, ila akakuta joto lake liko kawaida tu. Akajinyanyua na kuketi, kisha akatumia nguvu kiasi kumvuta Namouih ili naye akae pia, na akafanikiwa kwa hilo. Namouih alionekana kuchoka yaani, uso wake haukuonyesha hisia yoyote ya furaha kama alivyokuwa jana usiku walipotoka kwenda matembezi, naye Efraim akataka kujua ni nini tena kilikuwa kinamsumbua.
Akamshika shingoni na kumtazama kwa ukaribu, kisha akauliza, "Umeota ndoto mbaya tena?"
Namouih akatikisa kichwa kukanusha.
"Tell me honey. Nini tatizo?" Efraim akauliza tena kwa kubembeleza.
"Yaani sielewi kwa kweli. Nahisi kuchanganyikiwa Efraim..."
"Shida ni nini? Ni haya mambo yaliyotokea jana au?"
"Yaani sijui. Sijui ikiwa mambo yaliyotokea jana ndiyo yanasababisha nakuwa naona hivi vitu, au ni nini yaani...."
"Vitu gani?"
Namouih akafumba macho yake.
"Namouih nielezee..." Efraim akamwambia.
"Jana... kabla sijapanda kuja kulala, nilikuwa huko na Angelo... tukaanza kuona kama kivuli Efraim... kilikuwa kama kinaufungua mlango kabisa... niliogopa sana yaani sijui tu ni nini kilichonisaidia nikaweza kufika huku lakini... hii hali inanitisha mno..." Namouih akaongea kwa hisia.
"Kivuli?"
"Ndiyo. Mara nyingi nikiota ndoto za kutisha huwa naona vitu kama vivuli... ila jana haikuwa ndoto Efraim. Sikutanii... kuna kitu hakiko sawa..."
"Usijali Namouih, nakuamini. Pole sana. Ungeniambia hiyo jana, labda kuna mtu alikuwa ameingia hapa..."
"Hamna, hakukuwa na mtu kabisa. Ahh... nakwambia kila mara nikifanya tu interaction na Draxton ni lazima nitaota ndoto mbaya au kuanza kuona vitu vya ajabu. Ni kama kipindi kile ambacho unanichumbia unakumbuka nilikwambiaga kuna wakati nilikuwa naona mtu fulani wa ajabu, mara ananifatilia, mara anitokee dirishani...."
"Ndiyo, nakumbuka Namouih, nakumbuka..."
"Ni kama hivyo yaani. Hayo yaliacha lakini ni kama tena na sasa hivi yameanza... I don't know... sijui tu Efraim nimefanya nini kustahili kupatwa na haya yote..." Namouih akasema kwa huzuni.
"Namouih... naelewa unakuwa na mambo mengi akilini, na inaonekana ndiyo kati ya mambo ambayo...."
"Hapana Efraim, nina uhakika hii siyo tu kwa sababu ya kuwa na mambo mengi akilini..."
"Sasa inaweza kuwa nini? Kuna mwanaume yeyote ambaye labda... anakuchokoza-chokoza labda kimapenzi au...."
"Nini?"
"Yaani, labda kuna mtu anayekuchokonoa vibaya ndiyo maana...."
"Efraim nakwambia kuhusu mkazo naopata kwa sababu ya haya mambo ya ajabu halafu wewe unaniambia masuala gani tena hayo?"
"I'm sorry... nilikuwa tu najaribu kuangalia labda kuna shida hapo. Mtu anaweza hata akakutupia madude mabaya kwa mambo kama hizo, ni muhimu sana kuwa mwangalifu, ndiyo nachosema tu..."
"Agh, me kiukweli ninachoshwa sana na haya mambo. Itabidi nikaonane na shehe..." Namouih akasema.
"Au labda tukupeleke kwa Mwamposa?" Efraim Donald akasema kiutani.
Namouih akamwangalia na kushindwa kujizuia kutoa tabasamu ingawa kweli alikuwa amefadhaika.
"Ahahah... pole honey, pole. Jitahidi tu kufanya vitu hivi. Achana na masuala yale tuliyozungumzia jana, ni moja kati ya mambo yanayokupa huo mkazo. Halafu... labda itakuwa vyema kama usipoenda kazini leo maana hata hivyo ni Jumamosi..." Efraim akamwambia.
"No, kwenda ni muhimu. Nitakuwa sawa. Hili jambo lilinitikisa sana jana lakini... nitakuwa sawa," Namouih akasema.
"Una uhakika?" Efraim akamuuliza.
Namouih akatikisa kichwa kukubali.
Basi, Efraim Donald akambusu mke wake kwenye paji la uso wake na kumwambia yeye anaingia bafuni kuoga, naye akamwacha kitandani hapo akiwa bado na mawazo mengi. Kulikuwa na hilo suala la Draxton, ambalo akili yake ilimwambia kuwa lilihusiana kwa njia fulani na hili suala la mambo yenye kuhofisha yaliyokuwa yakimpata. Usiku waliomgonga yule kiumbe na yeye kuiona ile tattoo, aliota ndoto mbaya. Siku aliyoona tattoo ile mgongoni kwa Draxton, akaota ndoto mbaya. Jana ndiyo alimfata Draxton na kumuuliza kwa ujasiri kabisa kuhusu mambo yote ya ajabu kumhusu, halafu usiku akaona kitu kile chenye kutisha. Sasa kilikuwa kimebaki nini?
Alielewa kwamba wengine wangeona maoni yake kuwa kama ya mtu aliyepandwa tu na jazba, lakini bado hakutaka kukata tamaa ya kujua na kufichua mabaya ya mwanaume yule. Akajiondoa kitandani hapo na kwenda kuoga pia baada ya Efraim kutoka bafuni ili naye ajiandae kwenda kazini.
★★
Muda mfupi baadaye, Namouih akawa ofisini kwake akishughulika na mambo machache kwa siku hii. Kwa sababu ilikuwa Jumamosi kweli hakukuwa na mambo mengi, hata mume wake alikuwa amekwenda kazini lakini hakungekuwa na mambo mengi sana labda tu kwa sababu yalikuwa ya lazima kufanywa. Mpaka inafika saa tano, Namouih hakuwa ametoka kwenye kiti chake wala kupata kiamsha kinywa, na ndipo rafiki yake kipenzi akaingia muda huo kwa kuwa hawakuonana tokea alipofika.
Blandina aliingia akiwa na shauku yake ya kama kawaida, jambo lililoonyesha kuwa sasa alikuwa sawa kihisia, lakini Namouih akawa wa baridi tu, akionekana kuwa makini na kile alichoandika kwenye kompyuta yake.
"Steplar yako ina pini?" Blandina akauliza.
"Ndiyo, yako haina?" Namouih akamuuliza pia bila kumwangalia.
"Imeishiwa, nipe yako nikaitumie..."
"Chukua."
Blandina akasogea karibu na meza ya Namouih ili kuichukua, kisha akauliza, "Umeshapiga breakfast?"
Namouih akatikisa kichwa kukataa.
"Well, mambo kati yangu na Draxton yako vizuri sa'hivi, ali-apologize jana, tuka-spend muda pamoja," Blandina akasema huku akitabasamu.
"Okay. Hongera Blandina," Namouih akasema hivyo bila hata kumwangalia usoni.
"Niliona picha uliyopost Insta uko na Donald jana usiku. Mlienda wapi?"
"Kuzurura."
"Mmm... si useme wapi kabisa, short answer za nini sasa?"
Namouih akamwangalia, kisha akasema, "Tulienda kutembea town, tukatembea kuzungukia sehemu mbalimbali, tukala dinner, tukaingia mall, tukanunua vitu kama saa, cheni, mikufu, mkaa, pemba, vijola... tukatoka hapo tukaenda park ile yenye rollercoaster, tukanunua ice cream, akanilisha, akaniambia mimi ni mrembo sana, nikacheka, akanibusu, tukabembea, akanibeba, tukarudi nyumbani baada ya kupiga picha, ndo' nikapost... halafu tukalala."
Blandina akabaki kumtazama tu, kisha akasema, "Una makusudi sana."
"Nini sasa, si ndiyo jibu refu ulilokuwa unataka?"
"Yeah, lakini hujagusia na ile part ya lala nikupandilie."
Namouih akairudia kompyuta yake na kusema, "Tulikuwa tumechoka, kwa hiyo... hiyo haikutokea."
"Aisee! Unatia huruma sana best..."
"Na mimi nisemeje kuhusu wewe?"
"Angalau kuna sababu upande wangu, wewe mommy hupewi sababu yoyote... no offence," Blandina akasema.
Namouih akabaki kimya tu, akionekana makini sana.
"Umefanyaje mkononi, mbona umeweka plasta?" Blandina akauliza.
"Mtu wako ndiyo amenifanya hivi" ni jibu ambalo lilitaka kumtoka Namouih, tena kwa hasira, lakini akaishia tu kumwangalia rafiki yake usoni.
"Nini sasa?" Blandina akauliza.
"Niliumia tu kidogo, siyo kitu kubwa," Namouih akaficha ukweli.
"Okay, inaonekana unahitaji kuachwa kwanza la sivyo utameza mtu..."
"Hey... kila kitu kiko fine kati ya me na wewe, usifikiri labda...."
"Usiwaze honey, nakujua vyema. Chochote unachopitia jua kwamba itakuwa rahisi zaidi kukishinda ukishusha chai kidogo na kaushauri kutoka kwa rafiki... ukikahitaji unajua pa kunipata," Blandina akamwambia.
Namouih akatabasamu kidogo na kutikisa kichwa kukubali.
"Okay, baadaye," Blandina akaaga na kuanza kuondoka.
Namouih akawa anamtazama tu rafiki yake, akihisi ni kama hakutenda haki kutomwambia alichofanya jana, lakini ikiwa angesababisha audhike tena isingekuwa jambo zuri, hivyo kutomwambia ikaonekana kuwa kitu cha busara. Blandina ndiyo alikuwa ameukaribia tu mlango ili atoke pale ulipofunguliwa na msaidizi mwingine wa kampuni hiyo. Akasimama tu na kumwambia Blandina kwamba mwanasheria Namouih alikuwa na mgeni, naye Blandina akasema amruhusu kuingia. Msaidizi huyo akapisha kidogo, na mgeni huyo akaingia hapo.
Blandina akaachia tabasamu la furaha baada ya kumwona Draxton, akiwa amefika bila kutarajiwa. Alikuwa amevalia koti lenye rangi ya blue-nyeusi juu ya T-shirt nyeupe, suruali nyeusi, na viatu vyeusi vya kisasa vyenye muundo kama raba. Baada ya Namouih kumwona, akaacha alichokuwa anafanya kwenye kompyuta yake na kubaki amemtazama tu, kwa sababu uwepo wake wa ghafla hapo ulimaanisha bila shaka kuna jambo halikuwa sawa. Hangeweza kujizuia kumtazama kwa hisia kali, lakini akajitahidi kutofanya hilo lipite kiasi.
"Draxton!" Blandina akaita kwa shauku.
Draxton akasimama mbele yake, kisha akamtazama Namouih pale alipoketi. Namouih akarudi tu kuitazama kompyuta yake. Msaidizi yule akaondoka.
"Hukuniambia kama unakuja babe," Blandina akasema.
"Aa... nimekuja kumwona Namouih," Draxton akamwambia.
"Okay. Si umeshamwona sasa?"
Draxton akatabasamu kwa mbali, kisha akasema, "Nina mazungumzo naye kidogo. Nitaku-check tukimaliza."
"Okay, utanikuta kwa ofisi yangu..."
"Poa."
Blandina akamgeukia Namouih, na sasa mwanamke huyo alikuwa anamwangalia pia hivyo akampungia vidole kwa njia ya kusema kwa heri, halafu akatoka hapo. Mwanaume akaanza kuelekea mpaka kufika usawa wa meza ya Namouih na kusimama tu mbele yake. Namouih hata kumwangalia hakumwangalia, akiendelea kuonyesha yuko bize na kazi.
"Habari yako Namouih?"
"Unataka nini?"
"Nimekuja kuzungumza nawe kuhusu jana. Nina... ninahitaji kuomba samahani kwa... kukutendea bila..." Draxton akaishia tu hapo.
Namouih akamwangalia na kuuliza, "Bila nini, heshima? Utaweza vipi kutenda kwa heshima wakati ni kitu ambacho huna?"
"Ndiyo maana nakuomba samahani. Nimekuja tu kuomba samahani..."
"Halafu?"
"Sitarajii chochote. Nilichokufanyia hakikuwa sawa... nilijutia. Hakuna kitu cha namna hiyo kitatokea tena ikiwa sote tutaheshimu mipaka yetu dada."
"Kwa hiyo huwa una kawaida ya kuwasukuma au kuwaumiza wanawake wakivuka mipaka yao kwako eh?" Namouih akauliza.
Draxton akaangalia pembeni.
"Unafikiri Blandina atakuona vipi nikimwambia jinsi ulivyonifanyia jana?" Namouih akamuuliza.
"Itakuwa jambo zuri ukimwambia. Kwa sababu nimeshajionyesha kuwa mbaya kwako, ninaweza kuja kuwa mbaya hata kwake pia. Kwa hiyo ni bora ajue nilikuumiza ili naye akae mbali nami... asije kuumia," Draxton akamwambia.
Namouih akamkazia macho yake, akiwa ameshangazwa kiasi na kauli hiyo.
"Ona... ifike tu mahali ambapo muda utapita na sote tutasahau kwamba hii iliwahi kutokea. Ningesema hauna sababu yoyote ya kuwa na mashaka juu yangu lakini sitakulazimisha unione kwa njia yoyote ile. Hayo yatabaki kuwa mawazo yako. Narudia tena kuomba samahani kwa kilichotokea jana," Draxton akasema.
Mwanaume huyu aliyasema maneno hayo kwa njia iliyoonyesha kwamba aliyaamini kabisa, yaani yalikuwa yanatoka moyoni, na Namouih akawa anamtazama tu kama vile anamtathmini.
"Uwe na kazi njema," Draxton akamwambia hivyo, kisha akaanza kuondoka ofisini hapo.
Namouih akamwangalia tu mpaka alipokuwa ameufikia mlango, kisha akasema, "Subiri."
Draxton ndiyo alikuwa ameshika kivutio cha mlango, lakini akageuka kumwangalia baada ya kuambiwa hivyo.
Namouih akanyanyuka kutoka kwenye kiti chake, naye akaanza kutembea taratibu kumwelekea jamaa. Kuna kitu kuhusu mwonekano mzuri sana wa mwanamke huyu kilichofanya Draxton abaki kumtazama tu kama amezubaa, lakini hakuwa na wazo lolote la uvutio kumwelekea. Namouih akamfikia karibu zaidi, na kama ile kawaida, Draxton akafumba macho taratibu na kuinamisha uso wake. Bado jambo hilo lilikuwa moja kati ya mambo yaliyomfanya Namouih aone uajabu ndani ya mwanaume huyu, lakini kwa sasa akaamua tu kulipuuzia. Draxton akanyanyua tena uso wake na kumwangalia machoni, na wote wakawa wakitazamana sawia.
"Unaujua ule msemo wa nimekusamehe ila sitakusahau?" Namouih akamuuliza.
"Ndiyo," Draxton akajibu.
"Well, mimi nimekusamehe kwa kilichotokea jana, na nitasahau kabisa mambo hayo ikiwa tu utaniahidi jambo moja..."
Draxton akabaki tu kumwangalia, kama kumwambia anamsikiliza.
"Usimwambie Blandina. Haitakuwa na faida yoyote nyie mkikatisha mahusiano yenu eti kisa tu ulinikaza mkono," Namouih akasema.
"Si ni wewe ndiye uliyesema utamwambia?"
"Ndiyo, nilikuwa nakujaribu. Nataka tu kuhakikisha kwamba wewe hautamwambia lolote."
Draxton akatazama pembeni.
"Nisikilize. Mimi pia nahitaji kukuomba samahani kwa kila kitu nilichofanya, nili-panick tu. Blandina anafurahia sana kuwa nawe na mimi sitopenda kuona chochote kinamnyang'anya hilo. Nakuomba tu pia usahau mambo yote niliyosema jana. Ninatumaini next time tunakutana itakuwa ni companionship nzuri... ikiwezekana hata tuwe marafiki. Unaonaje?"
Namouih aliyasema maneno hayo kwa uhakika kabisa, naye Draxton akawa anamwangalia tu kama vile bado anataka kuendelea kumsikiliza.
"Vipi... litakuwa jambo zuri au halitafaa?" Namouih akauliza.
"Hapana, ni wazo zuri. Nashukuru kwa kunionyesha msamaha," Draxton akajibu kikawaida tu.
Namouih akatabasamu, kisha akasema, "Sawa. Cheer up. Mimi siyo mbaya sana kama navyoonekana."
"Yeah, wewe siyo mbaya. Unataka tu kuhakikisha kwamba kila kitu na watu unaowapenda wanakuwa sawa, na hilo linakufanya unakuwa imara unapohitaji kusimama kwa ajili yao," Draxton akamwambia.
Namouih akatulia kidogo, kisha akasema, "Asante. Basi... tutaonana nafikiri. Acha niendelee na kazi."
"Yeah, sawa."
"Kaonane na huyo dogo asije kunitafuna kwa kukuchelewesha," Namouih akatania.
"Okay. Jitahidi kula pia. Tumbo lako linaunguruma kama trekta," Draxton akatania pia.
Namouih akapandisha nyusi kuonyesha mshangao, naye Draxton akatoa tabasamu hafifu na kisha kuuvuta mlango na kuondoka.
Mwanamke huyu akavuta pumzi ndefu na kuishusha huku akiwa amefumba macho yake, akijipa utulivu baada ya pindi hiyo iliyokuwa imemfanya ajione kuwa mnafiki wa hali ya juu. Kwa nini? Kwa sababu ni kweli alikuwa akifanya unafiki. Akarudi mezani kwake na kupiga simu kwa mtu muhimu sana, ambaye hakuwa mwingine ila rafiki yake mpelelezi Felix Haule mwenyewe. Akamwambia kuna jambo la muhimu sana alitaka wazungumzie, hivyo wakutane ana kwa ana ili ampe taarifa zote mubashara.
Felix kama Felix hakukwaza, akimwambia rafiki yake kwamba hata akipenda basi wakutane mida hiyo hiyo, naye Namouih akasema wakutane saa saba mchana sehemu isiyo maalumu kikazi. Baada ya hapo, mwanamke huyu akakata simu na kuendelea na mambo mengine kwanza, akiwa ameshauweka tayari mpango wake wa kumhusisha Felix kwenye utata kumwelekea Draxton, ili mpelelezi huyo amsaidie kumnasa jamaa katika maovu ambayo Namouih aliamini ni Draxton ndiye aliyehusika kuyatenda.
★★★
Upande wa bwana Efraim Donald. Mzee wa kazi tu alikuwa ofisini kwake siku hii, kama kawaida akifanya mambo ya kiofisi. Ubize mwingi ni kitu ambacho kilikuwa cha kawaida sana kwake kila siku ambayo aliingia ofisini au kutoka kushughulika na mambo ya kikazi, hivyo kwa leo pia alijikuta amemezwa na kazi nyingi ingawa ilikuwa Jumamosi.
Lakini mwanaume huyu alikuwa amekusudia kuwahi kumaliza mambo yake ili ampitie na mke wake, waende sehemu fulani pamoja kisha waelekee nyumbani, au kama Namouih angehitaji kuendelea na kazi basi yeye Efraim atangulie nyumbani. Aliona ingefaa kufanya hivyo hasa kutokana na jinsi mambo mengi yalivyoonekana kumchanganya sana mke wake siku za hivi karibuni, naye akajitahidi kuzihimilisha kazi vizuri ili kufikia saa saba mchana asiwe na mambo ya lazima ya kufanya kisha ndiyo amtafute mke wake.
Ilipofika mida ya saa sita hivi, akapigiwa simu na rafiki yake wa karibu zaidi, aliyeitwa Mr. Godwin Shigela. Huyu kwa Efraim Donald ndiyo alikuwa "best friend," kwa sababu walijuana kwa muda mrefu na walisaidiana kwa mambo mengi. Mwanaume huyo alikuwa mtu mwenye pesa nyingi na mafanikio mengi pia, hivyo yeye na Efraim Donald walikuwa kama timu ya mapedeshee wawili tu. Efraim akaipokea simu huku akitabasamu kwa kuwa alifurahi sana kuipata simu ya rafiki yake.
"Kaka kaka," Efraim Donald akasema.
"Vipi kijana wangu?" Godwin akauliza kutokea upande wa pili.
"Ah ujana ushapita, naelekea ukongwe sasa..."
"Hahahaha... za huko?"
"Nzuri tu. Uko wapi sasa hivi?"
"Nimeingia Nairobi juzi kati hapo."
"Mh... wewe si ulisema ukitoka kisiwani unakuja moja kwa moja huku?"
"Yeah, change of plans. Kama ujuavyo mambo yetu bwana, kidogo tu uko hapa au pale, hupumziki yaani..."
"Dah, fanya utoke sasa huko brother, mwezi wa saba huu sijaliona lisura lako..."
"Haaaahahah... nishakuwa babu mandevu. Nitakuja tu... ndiyo nilikuwa nimekupigia kukujulisha niko huku kwa hiyo kama ulikuwa umeniandalia party itabidi mgeni rasmi abadilishwe..."
"Ahahah... pesa za mgomo, party wapi kaka?"
"Aa kwenda zako."
Simu ya mezani ofisini kwake Efraim ikaanza kuita, lakini akaipuuzia.
"Huko mshiko unakamatika eh?" Efraim akaendelea kuongea na Godwin.
"Kama vumbi la mpunga..."
"Usinambie! Dah, kweli maisha mazuri sana usipokuwa loser..."
"Hahahaha... wazogaji watuachie sisi tufurahie pepo ndani ya hii dunia iliyo kama jehanamu," Godwin akasema.
Efraim akacheka kidogo.
"Vipi bi mkubwa yuko poa?" Godwin akauliza.
"Yuko poa. Umri unaenda lakini hazeeki," Efraim akamwambia.
"Hah... je mrembo wetu?"
"Nani, shemeji yako?"
"Kwani kuna mwingine?"
"Ahahahah... yupo poa tu. Bado hakuna anayeufikia utajiri wa sura nzuri kwake..."
"Hahahaha... unapenda kumringia sana bwege wewe. Vipi lakini lile suala la ndoto? Bado zinamsumbua?"
"Yeah, nilikwambia imekuwa ikiendelea kutokea, sa'hivi ameanza hadi kuona mambo ya vivuli yaani... ila anasema atakuwa sawa."
"Well, unajua itakuwa problem kama akiendelea hivyo. Mlete kwangu basi..."
"Hahahah... kichwa chako! Ila hapana, haitakuwa na shida wala usijali..."
"Una uhakika? Uchizi ndiyo unaanzaga hivyo hivyo, anapiga kelele, anakimbia kimbia, mwisho wa siku hauko naye tena. Na we' ni kama umepuuzia hilo rafiki yangu, ile mali siyo ya luiacha iteseke namna ile..."
"Ahah... brother, inaonekana unatamani sana kuja kuupeleka moto kwa mke wangu siku moja eeh?"
"Ahahahah... kweli umeoa mwanamke anayejielewa. Ungechelewa kidogo tu...."
"Ungefanyaje? Unajua kwamba nina pistol ndani?"
Godwin akacheka na kusema, "Huko sitafika, we' enjoy tu hilo kombe. Piga hadi na watoto sita kabisa."
Simu ya mezani ikawa imeacha kutoa mwito baada ya kuita kwa muda mrefu.
Efraim akaendelea kuongea, "Heheheh... bwege wewe. Anita hajambo kwanza?"
"Anita yupi tena? Yule tuliyekutana naye kwenye boti?"
"Hamna, yule kibibi mweupe anayependa cocktail sana..."
"Unaongelea yule anayevaa vimini zaidi, jicho la kusinzia?"
"Achana na hilo jimama. Aisee, kaka umewapanga kama ndoo za maji hahahah..." Efraim akasema huku akicheka.
"Aaa... kama ujuavyo, hakuna kuremba. Wakijileta ni kuwafumua tu..."
Efraim Donald akiwa anaendelea kuongea na rafiki yake, msaidizi wake akaingia ofisini humo na kumfata kisha kusimama mbele ya meza yake.
"Hey kaka, subiri mara moja..." Efraim akamwambia hivyo Godwin, kisha akaishusha simu kwa ufupi. "Vipi Lucy?" akamuuliza msaidizi wake.
Msaidizi huyo, mwanamke mzuri na mweupe aliyevalia kwa unadhifu wa kiofisi, akasema, "Una mgeni."
"Nani? Sina mipango ya kukutana na mtu yeyote leo hapa," Efraim akasema.
"Anasema ni mdogo wako," Lucy akamwambia.
"Mdogo wangu? Nani?"
"Anaitwa Sasha."
"Sa.... oooh Sasha! Mdogo mdogo, mweupe?"
"Ndiyo."
"Okay. Mwambie aje. Mwambie aje ndani."
Lucy akatikisa kichwa kukubali, kisha akaondoka ofisini hapo taratibu.
"Hey Godwin..." Efraim akairudia simu.
"Nilikuwa namsikia hawala yako hapo anaongea," Godwin akasema.
Efraim akacheka kidogo, kisha akasema, "Acha zako. Nina mgeni asiye rasmi hapa, nitakucheki mida baadaye."
"Wala hata usijisumbue, we' piga tu mambo yako hayo yasiyo rasmi," Godwin akamwambia kiutani.
Efraim Donald akatabasamu na kuagana naye, kisha akaketi sawa akisubiri ujio wa dada mdogo wa mke wake.
Mlango wa kuingilia hapo ukafunguliwa tena, naye Lucy akaonekana kusimama hapo kama anapisha mtu, na hatimaye binti Sasha akaingia. Alikuwa amevalia shati jeupe la kike lenye mikono mirefu, sketi iliyoishia magotini yenye rangi fulani ya kijivu hivi, na viatu "simple" vilivyokuwa rahisi kutembelea. Alisuka mtindo wa rasta nene zilizolazwa kuelekea nyuma ya kichwa chake lakini zikiishia shingoni tu, fupi yaani, naye alibeba kimkoba cha rangi nyeusi mkononi. Alionekana kama mtu wa ofisini zaidi kuliko mwanafunzi, hasa kutokana na kuwa mrefu karibu na urefu wa dada yake. Lucy akaufunga mlango na kutoka, akimwacha Sasha amesimama huku anamwangalia kaka-mkwe wake usoni.
Efraim akaachia tabasamu lililoonyesha jinsi alivyofurahi sana kumwona, kisha akasema, "Sasha. Karibu. Karibu sana."
"Asante kaka," Sasha akajibu kwa sauti yake nyororo.
"Njoo... njoo ukae," Efraim akamwambia.
Sasha akatembea taratibu kuielekea meza ya Efraim, kisha akaketi kwenye kiti cha upande wa kushoto kutokea pale alipotazamana naye mezani.
"Aisee... karibu sana mdogo wangu. Yaani umeni-surprise," Efraim Donald akasema.
Sasha akatabasamu na kuendelea tu kumwangalia.
"Habari za shule?"
"Nzuri tu kaka."
"Ndiyo unaingia form six eh?"
"Ndiyo."
"Hongera sana. Masomo vipi?"
"Safi tu."
"Ulichukua combi gani?"
"PCB."
"Wow! Unaenda kuwa daktari kumbe!"
Sasha akatabasamu tu.
"Safi. Safi sana. Komaa haswa..."
"Ndiyo, nitakomaa..."
"Very good. Ila... niseme pole kidogo Sasha. Mimi na wewe hatujawahi kukaa kuzungumza mengi. Mambo yanakuwa tight sana..."
"Usijali kaka, ninaelewa. Una majukumu mengi."
"Yaani! Kazi mpaka basi. Ila nashukuru umekuja kunitembelea. Ni kitambo eeh... tokea mara ya kwanza tumekuja huku na Namouih, sikudhani hata kama ungepakumbuka..."
"Siwezi kupasahau. Kampuni yako ni kubwa yaani hata siyo rahisi kupotea."
"Ahahah... nafurahi sana. Karibu. Sijui... kuna jambo fulani umekuja kuzungumzia au ni ili kunipa hi tu?" Efraim akauliza.
"Aa... vyote. Kwanza samahani kaka kwa kuja bila kutoa taarifa..."
"Ondoa shaka mdogo wangu. Unakaribishwa muda wowote, ila ni kama tu ukinikuta maana mara nyingi sikai tu hapa..."
Sasha akatabasamu tu tena na kuangalia chini.
"Mambo yanasemaje?" Efraim Donald akamuuliza.
"Nilikuwa nimekuja kuongea nawe kuhusu jambo fulani. Yaani tu... sijui hata nianzie wapi..."
"Usijali Sasha. Unaweza kuniambia chochote. Jisikie huru kabisa."
"Okay. You see... nina rafiki yangu ambaye... ana tatizo fulani baya sana. Limekuwa likimsumbua kwa muda mrefu, na... linatakiwa kutafutiwa suluhu haraka la sivyo... atakufa," Sasha akasema.
"Oh Sasha, hiyo ni mbaya. Pole. Pole kwa rafiki yako pia..."
"Asante."
"Anasumbuliwa na nini?"
"Saratani."
"Aaa... sawa. Unasoma naye?"
"Hapana. Yeye hasomi. Alikuwa tu anafanya biashara ndogo ndogo, lakini sasa hivi yuko hospitali. Alikuwa ameanza kupata matibabu... ila kuna njia nzuri zaidi zinazohitajika kufanywa ili wamsaidie kuiondoa..."
"Kuiondoa kabisa?"
"Ndiyo... a... apone kabisa."
"Okay... sawa. Ungependa nikusaidie vipi mdogo wangu?" Efraim akauliza.
"Wangemfanyia... yaani... wangempa hiyo tiba ila sema, gharama yake ni kubwa na... alikuwa amebakiza kiasi fulani kumalizia lakini kufikia sasa bado hajapata. Anahitaji, ametafuta na kutafutiwa za kuongezea lakini hajapata. Nataka sana kumsaidia ila nashindwa," Sasha akaeleza.
"Amebakiza kiasi gani?" Efraim akauliza.
"Laki tisa," Sasha akajibu.
"Oh sawa. Umejaribu kuongea na Namo...."
"Hapana!" Sasha akamkatisha upesi.
Efraim Donald akaendelea tu kumwangalia kwa utulivu.
"Na..namaanisha... dada ndiyo... ndiyo alikuwa ametoka kunilipia ada ya mwaka mzima, na... najua kuna mambo mengi anashughulikia... nahisi kumwomba anisaidie kwa hili itakuwa kama... yaani kama mzigo kwake... halafu..."
"Okay Sasha, usihofu. Nimekuelewa. Usijali," Efraim akamtuliza.
Sasha akaangalia chini tu, akionekana kuwa na wasiwasi kiasi.
"Usijali Sasha nitakusaidia. Utampatia rafiki yako kiasi kilichobaki ili atibiwe, sawa?" Efraim akasema.
Sasha akamwangalia, kisha akasema, "Nashukuru sana kaka. Yaani... sijui niseme nini tu..."
"Nashukuru uliyosema inatosha," Efraim akamwambia.
"Hapana, naona kama haitoshi. Kaka nikija kuanza kazi nitahakikisha nakulipa kwa sababu ya msaada unaonipa... namaanisha... kwa ajili ya rafiki yangu..."
"Ondoa shaka Sasha. Usiwaze kabisa. Subiri..."
Efraim Donald akamwambia hivyo na kuchukua kijitabu fulani kidogo, kisha akaanza kuandika juu ya kikaratasi kimoja ndani yake.
"Unajua kutoa pesa kwa mfumo wa cheque?"
"Ndiyo," Sasha akajibu.
"Okay."
Efraim Donald akamaliza kuiandikia karatasi hiyo na kuichana kwa uangalifu kutoka kwenye kitabu hicho, kisha akampatia binti, ambaye aliipokea kwa mikono miwili. Sura ya Sasha ikakunjamana kimaswali baada ya kusoma kilichoandikwa, naye akamwangalia kaka-mkwe wake kwa mshangao.
"Kaka... mbona... mbona umeandika milioni mbili?" Sasha akauliza.
"Ndiyo ni milioni mbili. Au ulikuwa hujui kwamba we' ni wa gharama?" Efraim akamwambia.
Sasha akaganda kwa kumtazama kama vile hamwelewi kabisa.
Efraim Donald akacheka kidogo na kusema, "Nakutania tu. Unaweza kufanya unayohitaji sasa. Msaidie rafiki yako, na we' jihudumie kwa chochote unachotaka."
"Lakini kaka, hiki ni kiasi kikubwa... siwezi kukubali hii yote..."
"Sasha take it easy. Relax. Unaniheshimu kama kaka, si ndiyo? Nakuomba uichukue tafadhali. Sitamwambia Namouih lolote. Nimefurahi sana kwamba umekuja kwangu badala ya kuamua kutafuta njia za mbali au kulibeba hili mwenyewe. Kwa hiyo... uwe na amani. Muda wowote ukihitaji nikusaidie usisite kuniambia, umeelewa mdogo wangu?" Efraim akamwambia kwa upole.
Sasha akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa. "Asante sana kaka Donald," akasema.
"Karibu."
"Yaani... ahah... sikutegemea kabisa kama..."
"Usiwaze... hapa ni anytime. Be free."
Efraim akamwambia hivyo, kisha akakunja kiganja chake na kumnyooshea mkono. Sasha akatabasamu na kufanya hivyo hivyo pia, nao wakagonga tano kirafiki.
"Umekuja huku kwa usafiri gani?" Efraim Donald akauliza.
"Kutokea kule karibu na hostel nilichukua mwendokasi. Nilipofika maeneo ya huku nikachukua gari za abiria mpaka hapa."
"Mmm... na foleni?"
"Haikuwa kubwa... ahah..."
"Umejitahidi. Piga picha kama ungekuta sipo sasa," Efraim akasema.
Sasha akacheka kidogo.
"Unatakiwa urudi mapema? Au... unapanga kuonana na dada?"
"Ninataka kuwahi. Sikuwa nimepanga kuonana na Namouih... sikutaka hata ajue nipo huku," Sasha akasema kwa sauti ya chini kidogo.
"Aaaa sawa. I got you," Efraim akamwambia na kumkonyeza kirafiki.
Sasha akatabasamu na kusema, "Shukrani sana kaka Donald. Sana."
"You're welcome. Sana. Ukipenda naweza kukufanyia mpango wa usafiri ukupeleke hadi kule hostel moja kwa moja," Efraim akamwambia.
"Aa, hapana, haina shida. Nitachukua tu usafiri kama nilivyokuja. Msaada ulionipatia ni mkubwa sana kaka kukuomba mwingine..."
Efraim Donald akatabasamu na kutikisa kichwa kuonyesha ameelewa.
"Basi, ngoja me nikuache uendelee na kazi kaka. Na sijasahau kuhusu kuja kukulipa. Nitakulipa tu, upende usipende," Sasha akasema na kumfanya Efraim acheke kidogo.
Baada ya hapo, binti akanyanyuka na kumuaga tena kaka-mkwe wake, ambaye naye akamuaga kwa kusema wangeonana tena. Efraim alikuwa anataka kunyanyuka ili amsindikize Sasha nje, lakini binti huyu akasisitiza kwamba haikuwa na shida; yeye angeondoka tu upesi kwa hiyo kaka mkubwa aendelee na kazi zake. Akaanza kuondoka huku akihisi furaha kiasi moyoni, hasa kwa kupewa kile ambacho kilipita matarajio yake, na jinsi Efraim alivyomtendea kwa heshima na ukarimu. Akawa anaiingiza karatasi ile ya cheki kwenye mkoba wake mdogo huku akitembea kuelekea mlangoni, nayo ikadondoka chini kabisa. Aliiona, na katika tendo la haraka la mwili wake, akachuchumaa ili aikote upesi. Alipoifikia tu chini, akawa ametambua jambo fulani lililotokea bila yeye kutazamia.
Kuchuchumaa kwake kulifanya shati lake lijivute kiasi kwa kupanda juu kutokea nyuma, na hivyo sehemu ya kiuno kwa nyuma ikafunuka. Sketi yake ilikuwa kwa usawa huo huo pia, lakini nguo yake ya ndani, chupi nyepesi ya rangi ya pink, ilikuwa imepita kwa juu kiasi kutokea kwenye mstari uliotenganisha mashavu ya kalio lake, hivyo kwa uwazi huo ikawa wazi kwake kwamba ilionekana vizuri kwa nyuma. Akaiokota karatasi upesi na kusimama, akilivuta shati lake chini kujisitiri, naye akageukia nyuma yake kuangalia kama Efraim aliona jambo hilo lililomtamausha binti huyu kwa kadiri fulani. Lakini ndiyo kwanza Efraim Donald alikuwa bize na kompyuta yake, akionekana makini kuandika mambo fulani, naye Sasha akashusha pumzi ya utulivu na kuufikia mlango, kisha akatoka hapo hatimaye.
Mwanadada huyu alihisi furaha sana. Kutoka na milioni mbili halikuwa jambo alilotazamia kabisa. Kwa upande mwingine, alijihisi vibaya kwa kadiri fulani, kwa sababu ingawa alikuwa anaihitaji pesa hiyo, aliipata kwa njia ya uwongo. Huu ndiyo uliokuwa ushauri ambao rafiki yake, Sabrina, alikuwa amempatia baada ya Sasha kumwelezea kisa chake cha jinsi mpenzi wake alivyotoweka na kiasi cha laki tisa alizompa. Kwa kuwa Sasha aliogopa kusema lolote kwa Namouih, Sabrina alimpa ushauri wa kumwomba shemeji yake amsaidie bila kumjulisha dada yake, kwa sababu alijua kuhusu namna ambavyo mwanaume huyo mkarimu alijitoa kusaidia kuokoa maisha ya baba yao kipindi cha nyuma, yaani mzee Masoud, ingawa baadaye alikufa.
Kwa hiyo Sabrina alimsaidia rafiki yake kubuni hadithi hii ya rafiki kuumwa saratani, ili Sasha apate pesa ya kufidishia kile ambacho mpenzi wake mshenzi aliiba. Mpaka wakati huu, bado huyo Shomari hakuwa amepatikana. Kiukweli, haikuwa jambo rahisi kwa binti huyu kumdanganya shemeji yake, lakini mwisho wa siku akawa amefanikiwa, na ambacho kingebaki tu kwa sasa ilikuwa ni Namouih kutokujua lolote, maana aliuelewa moto wa dada yake vizuri.
★★★
Muda wa saa saba ulipofika, Namouih akaondoka ofisini kwake ili kwenda kukutana na Felix hatimaye. Walikuwa wameshapanga kukutana kwenye mgahawa fulani wa kisasa, na mpaka kufikia muda huu Namouih hakuwa ameweka chochote tumboni mwake, hivyo angeitumia nafasi hiyo kupata chakula pia. Akaelekea huko baada ya kuagana na Blandina, aliyemwambia kwamba alikuwa na mipango na Draxton pia jioni ya siku hii, bila kujua kwamba rafiki yake alikuwa na mpango wa kumweka mpenzi wake huyo shabaha ya kumfatilia kisiri, na ndiyo alikuwa anaenda kuiweka sawa mipango hiyo.
Namouih akafika kwenye mgahawa huo na kumkuta rafiki yake mpelelezi akiwa hapo tayari. Wakasalimiana kwa kukumbatiana, kisha Felix akamwongoza bibie mpaka kwenye meza aliyokuwa amekwishachukua mapema. Ilikuwa kwa sehemu ya nje ya jengo la mgahawa huo maridadi, kukiwa na meza kadhaa hapo zenye watu pia waliopata milo na maongezi. Namouih akaketi, naye Felix akamwita mhudumu aliyekuwa karibu ili waagize msosi na vinywaji. Kila mmoja akaagiza chakula chepesi tu na sharubati za maembe, kisha wakaanza kuzungumzia mambo mbalimbali ya kirafiki mpaka Felix alipogusia kile ambacho Namouih alisema angemwambia.
"Yeah, nilikuwa nataka kushiba kwanza ndo' nikurushie mzigo sasa," Namouih akamwambia.
"We' urushe tu. Unaweza ukasubiria tushibe, ukaurusha, njaa ikarudi tena," Felix akasema.
"Mhm... kweli Felix ni jambo zito kiasi nalotaka kukuomba..."
"Nini, mechi au?"
"Ahahah... acha mambo yako..."
"Kama kuna boya amekuzingua vibaya jua hii ndiyo sehemu sahihi ya kufikia," Felix akasema.
"Asante, lakini... si kihivyo. Kuna mtu... Felix kuna mtu nahisi ana-connect na vifo vya hao wasichana uliokuwa ukifanyia upelelezi."
"Come again?"
"Ni instinct tu, sina uhakika sa...."
"Nani?" Felix akamkatisha.
"Draxton."
"Ndiyo nani?"
"Boyfriend wake Blandina..."
"Acha masihara basi!"
"Kweli. Unamfahamu?"
"Namsikia. Si ndiyo yule aliyekufanya ukaipoteza kesi ya Agnes?"
"Ndiyo, na tena na hapo najua alitumia uchawi... hata kama Agnes ndiyo alikuwa na hatia..."
Felix akacheka kidogo.
"Ninahisi kabisa kuna kitu anaficha."
"Kweli?"
"Kweli. Hayuko poa yule mwanaume... na Felix, mimi nahofia...."
"Usalama wa Blandina," Felix akamalizia maneno yake.
"Ndiyo."
"Nini kimekufanya ufikiri ni yeye, au ana-connect vipi na hii ishu?" Felix akauliza.
Vyakula vikawa vimeletwa, nao wakasubiri mpaka mhudumu alipomaliza kuwawekea kwa sehemu zao na kuondoka, kisha wakaanza kula taratibu huku Namouih akimwelezea Felix mambo aliyofikiria. Akamwambia kuhusu usiku ule walipomgonga mtu fulani wa ajabu aliyekuwa na mchoro wa tattoo mgongoni ambayo alikuja kuiona mgongoni kwa Draxton pia; ikiwa ni maneno yale yale. Akamwambia kuhusu usiku ule Agnes aliouawa, jinsi ambavyo alimwona Draxton hapo na gari lake kisha akaondoka upesi kabla ya maaskari kufika, na namna ambavyo mwanaume huyo alimtendea siku ya jana alipomfata na kumuuliza ikiwa alihusika na vitu vibaya vilivyokuwa vinaendelea.
"Mambo unayosema yana-make sense, lakini bado najiuliza ni kwa nini alikuacha tu hiyo jana. Ikiwa yeye ni serial killer usingekuwepo hapa sasa hivi," Felix akasema.
"Na leo kanifata ofisini eti kuniomba samahani kwa kilichotokea. Ni huyu huyu ambaye jana niliposema tu kuhusu kuwaua wasichana alinikaba nusu kuniua, halafu leo anajifanya malaika. Sijui anataka kuthibitisha nini?" Namouih akaongea kwa kuudhika.
"Labda atakuwa mgonjwa wa akili. Ninajua watu ambao huwa wanaonekana kuwa sawa kwa nje lakini vitu wanavyofanya gizani ni vibaya mno," Felix akasema.
"Na jinsi alivyo vizuri kwenye kazi zake unadhani kuna mtu ataamini hilo? Nimemwambia Efraim jana lakini hakuniamini..."
"Ahahah... bwana mkubwa akakuona kama wacko..."
"We' acha tu," Namouih akasema hivyo na kuendelea kula taratibu.
"Hmm... okay. Nitamchunguza huyu jamaa. Ikiwa anahusika kweli nitahakikisha anakuja kupata adhabu ambayo hakuna mtu aliwahi kupata kabla," Felix akaongea kwa uhakika.
"Unaweza ukakuta anashirikiana na watu wengine."
"Nikigundua anahusika kweli nitamtumia atuongoze kwa wenzake. Natakiwa nianze ku-monitor nyendo zake haraka, na wewe pia jitahidi kuigiza kwamba kila kitu kiko normal ili asishtukie lolote. Blandi ndo' hana clue kabisa?"
"Yaani utafikiri amerogwa! Hatanisikiliza kabisa na anaweza akawa anajiweka hatarini," Namouih akasema.
Simu yake Namouih ikaanza kuita.
"Nitaharakisha uchunguzi. Umefanya vizuri kuniambia, utapaswa tu kusubiri sasa," Felix akasema.
Namouih akaangalia simu yake na kukuta ni mume wake ndiyo anapiga, akamwonyesha Felix kwamba mwenye mali ndiyo alikuwa anapiga, naye Felix akatabasamu na kuendelea kula. Efraim Donald alikuwa anamuuliza mke wake ikiwa alikuwa ofisini muda huo ili ampitie na labda waende kupata chakula sehemu fulani kisha waelekee nyumbani, lakini Namouih akamwambia alikuwa ameshakula na alitoka ofisini kwenda sehemu nyingine kukutana na mtu ili azungumze naye mambo ya kikazi, hivyo yeye Efraim atangulie tu. Efraim hakuwa na neno, naye akaagana naye vizuri kisha simu zikakatwa.
"Bwana mkubwa anaku-mind sana," Felix akasema.
"Kivipi?"
"Ahah... una gari lako mwenyewe lakini bado anataka kukupitia ili mwende wote home..."
"Aaa... anapenda kunipeti, si unajua me kwake 10 ya 10?"
Felix akacheka.
"Mara nyingi akinipitiaga gari huwa naliacha tu kazini, then siku inayofuata ananipeleka kwa lake," Namouih akamwambia.
"Mmm... una raha sana. Kila ndoa ina matatizo lakini we' ni kama hayakupatagi kabisa. Siwezi kusema ulimnywea dawa maana sura tu hiyo ni mwisho...."
Namouih akacheka, akiwa amewaza namna ambavyo Felix hakujua kihalisi kwamba hata yeye alikuwa na mikazo kwenye ndoa yake, na marafiki hawa wakaendelea kuzungumza huku wakimalizia vinywaji na chakula. Walipomaliza, Felix akalipia ingawa Namouih alitaka kufanya hivyo badala yake kwa kuwa mkutano huu aliuitisha yeye. Wakatoka hapo, Felix akitembea kwa ukaribu na Namouih mpaka walipolifikia gari la bibie na kusimama wakimalizia maongezi, kisha wakakumbatiana na kuagana. Namouih akaingia ndani ya gari lake baada ya Felix kumfungulia mlango kiutani wa kirafiki, naye mrembo akaliwasha na kuondoka eneo hilo.
Hakungekuwa na yeyote kati yao ambaye angetambua kwamba tokea Namouih alipofika hapo kukutana na Felix, walikuwa wakitazamwa. Mwanzo mpaka mwisho. Na tena siyo kuangaliwa tu kwa kawaida ile ya watu kumtazama sana Namouih kwa sababu ya urembo wake, bali walikuwa wakiangaliwa kwa hila kabisa. Felix akaanza kulielekea gari lake pia, huku aliyekuwa anawatazama akiendelea kumwangalia mpaka alipoingia ndani ya gari lake na kuondoka, na mtu huyu akaondoka eneo hilo pia.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments