Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

FOR YOU

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa 

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA SITA

★★★★★★★★★★★★★★★★

 
Wataalamu wa kazi ya wizi wa Trilioni 20 kwenye majengo ya benki kuu walifanikiwa kumpeleka Kevin sehemu ambayo ilikuwa salama kwa usiku huo. Walifika kwa pamoja kwa kutumia gari lao kwenye nyumba ndogo maeneo ya ziwani, ambayo ilikuwa imejitenga mbali sana na makazi ya watu wengine. Nyumba hii ilijengwa kwa mabati makuukuu tu na hivyo kuonekana kama ya hali ya chini, lakini kwa ndani watu hawa walikuwa wameweka vitu vyao kadhaa vya kitaalamu sana, na kwa huku ilikuwa ni sehemu nzuri ya kujifichia.

Kevin Dass alikuwa amepewa egamio na mwenzake ili aweze kutembea vizuri, kwa kuwa alihisi maumivu mengi mwilini. Walipofika ndani akakalishwa na kuvulishwa T-shirt lake, kisha wenzake, mmoja baada ya mwingine, wakaanza kuvua viziba uso vilivyoficha sura zao. Kati ya wenzake waliomwokoa, watatu walikuwa wanaume, na wawili wanawake.

"Aahh... haki ya mungu nitamuua huyo mpumbavu! Nitampa kifo ambacho hatakaa kusahau!" Kevin akasema kwa hasira.

"Atakikumbukaje akiwa ameshakufa sasa?" akauliza mmoja wao, mwanaume aliyeitwa Victor.

"Anajishaua eti atamuua wakati jamaa amemponda ka' kiazi hahahah..." akatania mwanaume kijana aliyeitwa Oscar.

"Shut up! Kilichowachelewesha ilikuwa nini wakati nilikuwa nimewapa signal tokea kitambo?" Kevin akauliza kwa ukali.

"Okay first, hatukufanyii kazi wewe. Second, unapaswa ku-respect chain ya command. Unawezaje kujiachia namna hiyo wakati unajua jinsi ilivyo hatari kwetu?" Victor akamuuliza Kevin.

Mwanamke mmojawapo akawa ametoa vifaa vichache kwa ajili ya kutumia kumponya Kevin sehemu alizoumia; kama dawa za kunywa, kuchua, na sindano. Akamsogelea na kuchuchumaa kisha kuanza kumpaka dawa.

"Hatari kivipi? Siyo kwamba hata nyie mlijua hawa wajinga wangenifikia mimi... je kama wangekufikia wewe ukiwa chooni, tungesema hau-respect chain of command? Aagh... taratibu bwana!" Kevin akasema na kumwambia hivyo mwanamke huyu aliyekuwa anamchua.

"Hey tulia, haunilipi!" mwanamke huyu aliyekuwa anamchua akamwambia hivyo. Jina lake lilikuwa LaKeisha.

"Ulikuwa wapi walipokukamata?" akauliza mwanaume mwingine aliyeitwa Mensah.

"Sokoni," akajibu Kevin.

"Maeneo gani?" Mensah akauliza tena.

"Wanapaita Mabatini..." akasema Kevin.

"Ulikuwa umeenda kutafuta mabati ya nini?" Oscar akamuuliza kiutani.

"Ili nije niya-shove in your ass," Kevin akasema kwa kukerwa.

"Unajua kabisa huku kilichotuleta haikuwa kuzurura. Ulitakiwa kufata Buzuruga ulichoambiwa na kugeuka, wewe ukaona free time una yote duniani mizunguko yako kufanya, nini unategemea? Ni lazima tu wangekukamata!" Mensah akasema kwa ukali.

Kevin akanyanyuka na kumfata Mensah mpaka karibu, akionyesha ubabe. Mensah naye akamsogelea karibu zaidi usoni, nao wakawa wanaangaliana kwa hisia kali.

"Here we go (haya sasa)," Victor akasema.

LaKeisha akasonya na kusema, "Mkimaliza utumbo wenu chuaneni wenyewe." 

Kisha akaelekea upande mwingine akiviacha vifaa vile chini.

"Unanifokea namna hiyo wewe kama nani?" Kevin akamuuliza Mensah kwa sauti ya chini.

"Kama mtu ambaye anaweza kukutandika ukawa mpaka mwekundu zaidi ya nyanya!" Mensah akajibu kiutulivu pia.

"Usijipaishe kwa kuwa niko weak kidogo sa'hivi. Nitakuonyesha ngozi yako yote ya ndani inafananaje siku moja hadi uweze kuongea Kiswahili vizuri," Kevin akamwambia.

"Ulishawahi kuliona fuvu lako wewe mwenyewe? Nitakuonyesha hiyo siku ikifika," Mensah akasema.

Midomo yao ikakaribiana zaidi wakiwa wanaangaliana kwa hasira sana.

"Busu hiyo inakuja, busu hiyo inakuja, busu hiyo inakuja..." Oscar akawa anasema huku anampiga-piga Victor mgongoni.

"Kawasaidie kugonganisha vichwa basi," Victor akamwambia Oscar.

"Usijifanye wewe ndiyo mwenye neno hapa, hauko karibu na hilo hata kidogo," Kevin akamwambia Mensah.

"Nikija kumalizana na wewe kuutumia ulimi wako hautaweza tena, ndiyo utajua nani amebaki na neno," Mensah akasema.

"Enough!" 

Mwanamke yule mwingine aliyekuwa anawatazama tu muda wote huu akasema hivyo kiukali. Wawili hawa wakaendelea tu kutazamana kibabe.

"Kevin... back off! (Kevin..rudi nyuma)," mwanamke huyu akamwambia.

Kevin akaendelea kumwangalia Mensah kwa sekunde chache, kisha akaanza kurudi nyuma taratibu. Mensah akatabasamu kwa kejeli. Mwanamke huyo akaanza kumfata Kevin mpaka aliposimama. Akaanza kumshika polepole sehemu za mwili wake zilizoumia, naye Kevin akawa anamwangalia kwa hisia.

"Utahitaji uangalizi wa kina Kevin... umeumia sana," mwanamke huyu akasema.

"No biggie wala, niko sawa," Kevin akasema.

"Ndiyo, kwa nje. Lakini kwa ndani unavuja damu. Torres atahitaji kukupa attention," mwanamke huyu akamwambia.

"Siyo kama vile yuko hapa," Kevin akasema.

Mwanamke huyo akampatia Kevin kifaa fulani mkononi. 

"Utamfikishia Torres," mwanamke huyu akasema.

Kevin akashangaa. "Unamanisha nini?" akauliza.

"Unaenda chini," mwanamke huyu akamwambia.

"Nini? Lakini... subiri, kwa muda gani?" Kevin akauliza.

"Mpaka nitakaposema utoke," mwanamke huyu akamwambia.

"Why?" Kevin akauliza kimshangao.

"Wanajua wewe ni nani sasa hivi, utasakwa kila kona. Kwa hiyo hauna jinsi tena... ltttaah... CHINI... hahahaah..." Oscar akamtania Kevin.

"Lakini Lexi..." Kevin akawa anataka kupinga.

"Oscar yuko sahihi. Silaha yetu kubwa ni kutojulikana, na unajua hii ni lazima ili uwe salama," mwanamke huyo akasema.

"Usingefanya uzururaji isingekuwa hivi. Sasa hautazurura tena," Mensah akamwambia.

"Hapana Mensah, hiyo siyo sababu iliyofanya akamatwe. Kevin, nahitaji uniambie wale watu walikuwa wakina nani," mwanamke huyu akasema.

"Sijui sana, ila nadhani ni wanajeshi," Kevin akasema.

LaKeisha akawa amefika usawa wa mwanamke huyu mwingine, ambaye jina lake lilikuwa ni Lexi, na kusimama karibu yake akiwa amezungushia mkono wake mmoja begani kwake.

"Tunajua walikuwa wanajeshi. Anamaanisha ni nani hasa. Kichwa chako kina nini, au bado kipigo kimekukolea?" LaKeisha akamuuliza Kevin.

Kevin akamwangalia LaKeisha kwa kuudhika, kisha akasema, "Walikuwa wanamwita jamaa Luteni. Aliniambia anaitwa Michael."

"Luteni Michael? Boom! Kazi imeanza hahah..." Oscar akasema.

"Na yule mwanamke... alikuwa nani?" Lexi akauliza.

"Walimwita ACP, lakini sijapata jina lake. Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kujua hereni niliyovaa ni TD," Kevin akasema.

Mwanamke huyu, Lexi, akaangalia pembeni kwa umakini.

"Lexi... tufanye nini sasa?" LaKeisha akamuuliza mwanamke huyu.

"Kwani ni lazima nikae kule chini kuanzia sasa? Si tunaweza tu kuendelea na..."

"Hatuwezi, boya wewe. Kwa kuwa wamekujua utapaswa kulay low, na hata kama ni mission tukifanya now utatakiwa uwe unagusa mara moja tu. Boss atakutafuna," Mensah akamwambia Kevin.

"Hivi sababu ilikuwa ni nini mkamwingiza huyu kunguni kwenye hii mission, mbona ananichokonoa vibaya sana?" Kevin akauliza kwa hasira.

Oscar na Victor wakacheka.

"Victor, Oscar, LaKeish... nendeni pamoja na Kevin chini upesi, mmpatie Torres info za leo, kisha mmwambie anitumie majibu. Mensah uko nami, tunaenda Dar," Lexi akatoa amri.

"Yes ma'am," akasema Oscar.

"Dar kufanyaje sa'hivi? Na pia Lexi... kwa nini Mensah asiende na hawa wengine halafu mimi niende nawe huko?" LaKeisha akamuuliza.

"Usijali, mtakuja tu. Ila nataka kuhakikisha Kevin mnamfikisha salama," Lexi akajibu.

"Kama litoto lililopotea," Victor akatania.

"F*** you," Kevin akamwambia.

Victor akacheka.

"Jiandae kuhusu ni hotuba gani utatoa ukifika kwa boss," Mensah akamwambia Kevin.

Kevin akamwangalia kwa kuudhika na kurudi taratibu pale alipokuwa amekaa.

Lexi akamwangalia LaKeisha, kisha akasema, "Chukueni gari mwondoke now, kabla ya saa sita mchana kesho muwe mmeshafika chini."

"Aagh... yaani hatuna hata muda wa kupumzika," LaKeisha akasema kwa maringo.

Lexi akamwangalia Oscar, naye jamaa akamrushia funguo kwa ajili ya gari lingine tofauti na lile walilokuja nalo. 

"Mkitoka choma kila kitu," Lexi akasema.

Oscar akampigia saluti kuonyesha ameelewa. 

LaKeisha akawa anachezea-chezea nywele za kichwa cha Lexi huku akimwangalia kwa hisia, naye Victor pamoja na Oscar wakaangaliana na kuchekea kwa chini bila kutoa sauti. Kisha LaKeisha akambusu Lexi kwenye shavu, naye Lexi na Mensah wakatoka ndani hapo na kuelekea nje.

"Hivi we' hauachagi tu?" Oscar akamuuliza LaKeisha.

"Kuacha nini?" LaKeisha akauliza.

"Hayo mambo yako," Oscar akasema.

"Kwa Lexi? Sahau," LaKeisha akasema kwa uhakika.

"Okay, mtoto wa mama kama umemaliza kulialia hapo chini vaa shati tuondoke. Haraka!" Victor akamwarisha hivyo Kevin kikejeli na kutoka akiwa anacheka. 

Oscar alikuwa anacheka pia huku akimnyooshea Kevin kidole, ambaye alikuwa amenuna na kuvimba nusura ya kupasuka.

"Ooouh... mbona mnamwandama hivi baby wangu? Eti sugar wanakuonea kwa kuwa umebamizwa leo? Usijali wasikuonee hawa, sawa? I'm here for you," LaKeisha akamwambia Kevin kimadoido lakini kwa kejeli.

Kevin alikuwa amekasirika kwelikweli, na sababu ilikuwa ni kilichompata muda mfupi nyuma, na kile ambacho kingefuata. Sehemu ile ambayo Lexi aliiita "chini," ilikuwa ni sehemu yao ya mwisho kwa ajili ya maficho; yaani ikiwa jambo kama hili lililompata Kevin lingempata yeyote kati yao, basi walipaswa kwenda sehemu hiyo na kutulia huko mpaka wakiambiwa vinginevyo na "boss" wao, kwa kuwa tayari wangekuwa wamejulikana. 

Hawa walikuwa ni vijana kutoka kwenye kundi la watu wale waliofanya wizi kwenye Benki Kuu, lililofahamika kama Mess Makers. Walikuwa ni wataalamu katika mambo yote waliyofanya, na waliyokuwa wamejiweka tayari kufanya. Kwa ujumla, kundi hili la "Mess Makers" lilikuwa na watu nane; nane tu! Lakini mambo waliyokuwa wamefanya mpaka sasa na ambayo walikuwa wameazimia kufanya yalikuwa makubwa kupita maelezo. Kama Lexi alivyosema, nguvu yao kubwa ilikuwa ni kutojulikana wao walikuwa akina nani, kwa hiyo kwa jambo kama lililompata Kevin, nguvu yao ingepungua kwa kadiri fulani. Kwa hiyo kuanzia wakati huu wangejitahidi kuweka umakini wa hali ya juu. 

Kevin Dass alikuwa mwanaume mwenye nguvu, mwenye kujiamini sana, na mwenye ustadi mwingi katika masuala yote yaliyohusisha ujenzi wa majengo ya aina zote. Hivyo kwa kundi hili yeye alikuwa muhimu sana ilipokuja kwenye masuala yaliyohusisha michoro ya majengo, maeneo mbalimbali, na kujua ni vifaa vipi vingehitajika sehemu mbalimbali walizotaka kuingia. Alikuwa na miaka 34, naye alikuwa mweusi, mwenye mwili mpana wenye nguvu, na mrefu kiasi. Lakini alikuwa mtu mwenye kukasirika upesi sana pia. Mara kwa mara alikosa subira kwa mambo mengi waliyofanya, hivyo ilikuwa jambo la kawaida kwa wenzake kumsahihisha endapo angejaribu kufanya mambo kwa njia ambayo haikupatana na mipango yao wakiwa kama timu. 

Oscar Amari alikuwa ndiye kijana mdogo zaidi kwenye kundi hili; akiwa na miaka 26 tu. Alikuwa kijana mwenye mwili usio mpana sana lakini uliojengeka vizuri kimazoezi. Alikuwa mcheshi, mtundu, mwepesi kuongea, na utaalamu wake ulikuwa ni ujuzi mwingi wa mitambo ya aina zote za kielektroni. Angeweza hata kutengeneza bomu dogo kwa kutumia betri za simu na kulitumia kushtua watu ili kujifurahisha alipokuwa na miaka 14 tu. Alikuwa muhimu sana ilipokuja kwenye masuala ya kukorofisha mitambo mingi ya ulinzi, CCTV camera, kuondoa password ngumu kwenye vyumba au mashine kubwa kubwa za kielektroni, na hata kutengeneza mabomu yenye nguvu kubwa sana. Ni huyu ndiye aliyetengeneza mabomu yaliyotumiwa kulipua majengo ya Benki Kuu, hivyo pamoja na kwamba alikuwa "mdogo," mambo yake yalikuwa makubwa sana.

Victor Quawey alikuwa mwanaume mwenye miaka 44, mweusi, mnene wa kadiri na mrefu kiasi. Alikuwa mtaratibu, msikivu, na mwenye utulivu pia. Lakini chonde! Huyu alikuwa mtu mwenye hila balaa! Alikuwa na ustadi mzuri wa kutengeneza vitu bandia ambavyo vilifanana kabisa na vile vilivyokuwa halali. Hii ilimruhusu kutengeneza pesa, vitambulisho, vito, ngozi kama za watu, na hata sura za watu ambazo zilikuwa za bandia. Alikuwa mtaalamu sana kwenye jambo hili, lakini pia alijua mambo mengi kuhusiana na siasa na biashara. Hivyo alikuwa na umuhimu wa pekee kwenye kundi hili la Mess Makers.

Halafu kuna LaKeisha Uatu, ama kwa jina walilozoea kumwita wenzake, LaKeish. Huyu alikuwa mwanadada mwenye miaka 28, mwenye ngozi isiyo nyeusi sana wala nyeupe sana; maji ya kunde. Alikuwa na sura nzuri, mwenye mwili mwembamba kiasi lakini hips zake zilikuwa nene na kufanya achoreke vizuri sana kutokea kiunoni. Alikuwa mwepesi kuongea, mjeuri, na mwenye kujiamini kupita maelezo. Ustadi wake muhimu zaidi ilikuwa ni kuiba kwa njia isiyoonekana wazi. Yaani kama vile mtu unayepishana naye halafu mkapamiana akakuomba samahani, kisha ukifika mbele unakuta kwenye pochi au wallet yako hakuna kitu, ndiyo alikuwa LaKeisha sasa. Alipenda sana kukwapua vitu vya watu kwa kuwa alikuwa na mikono yenye kasi sana, naye alijua kuchora pia. Kwa kundi hili, yeye ndiye aliyekuwa "kipenzi" cha wote kutokana na njia yake ya kufanya mambo kimadoido, lakini kwenye kazi alikuwa makini sana.

Mensah Dodzi alikuwa mwanaume mwenye miaka 41. Alikuwa mrefu kiasi, mwenye mwili mkubwa wa mazoezi na mweusi pia. Alifuga rasi kichwani na ndevu nyingi, naye alikuwa na uzoefu katika kutumia silaha za kila aina. Aliwahi kuwa kwenye moja ya makundi yaliyofanya ujambazi tokea alipokuwa na miaka 21 mpaka 30 kwenye nchi aliyotokea. Aliwekwa gerezani mara kadhaa, lakini hakuacha tabia zake za kikorofi mpaka baadae alipopatwa na msiba wa familia yake; iliyouliwa kikatili na watu wengine wabaya waliotaka kumkomoa. Kwa hiyo baada ya hayo, akiwa anataka kujijengea maisha mengine sehemu nyingine, alijiunga na kundi hili. Huyu alikuwa mwanaume aliye makini sana. Hakupenda mchezo na kazi, naye angefuata kile alichoongozwa kufanya bila kujali nani wala nini kingekuwa mbele yake. Ni moja ya wale watu wanaoitwa "damu baridi," kwa sababu ilipokuja kwenye suala la kuua asingesita hata kidogo.

Kijana mwingine wa kundi hili aliitwa Torres Dela Robia. Huyu ndiyo yule mtu unayeweza kusema ni "ubongo" wa timu. Jamaa alikuwa na ustadi mmoja ambao ulimfanya awe wa muhimu sana kwenye timu hii, na ustadi huo ulikuwa ni kwamba alijua mambo mengi. Yaani huyu ndiyo alikuwa "genius" kwenye kundi la Mess Makers, kwa sababu alikuwa na ubongo mwepesi sana wa kuchanganua mambo mengi kwa wakati mmoja. Alijua kila aina ya somo. Alijua sayansi, alijua biashara, alijua teknolojia, alijua siasa, alijua falsafa, alijua sheria, alijua kila aina ya mazingira, yaani alijua vitu vingi sana, hivyo ili mipango mingi ya kundi hili ifanikiwe, alihitajika sana kuipangilia kwa njia ambayo mwisho wa siku ingefanikiwa tu. Kwa kuwa na umuhimu huu, yeye alikaa sehemu moja ambayo angeitumia kwa ajili ya kuwaongoza wenzake endapo wangekuwa kwenye "mission" fulani; kule kule walikopaita "chini." Alikuwa na miaka 37, lakini mwonekano wake ulimfanya aonekane kuwa mdogo sana. Alikuwa na mwili wa wastani tu, mrefu pia, mwenye rasi fupi kichwani, naye alipendelea kuvaa miwani yenye kuonyesha macho lakini isiyo ya dawa. 

Kisha kuna Lexi, aliyekuwa na miaka 29. Mwanamke huyu ndiyo alikuwa kama roho ya kundi, iliyowaunganisha kwa pamoja licha ya wao kutofautiana kwa mambo mengi. Alikuwa mtu mwenye akili kwelikweli, na ustadi wake ilikuwa ni werevu wa kuchukua maamuzi ya haraka ambayo yaliwasaidia wanakundi kutenda upesi chini ya hali mbalimbali. Yaani sikuzote kulikuwa na mipango ambayo tayari iliwekwa, lakini siyo sikuzote matokeo yangekuwa kwa njia ambayo kila mmoja alitarajia. Hivyo mtu kama Lexi alikuwa wa muhimu sana katika kutokeza njia mpya za kushughulika na mambo kwa vitendo zaidi, na kama kungetokea tatizo kwenye mfumo wao mzima, basi angetokeza njia ili mambo yakae sawa. Tofauti na Torres ambaye alitoa suluhisho kwa njia ya mawazo, Lexi alikuwa mtu wa kuyaangalia mawazo hayo na kutafuta njia za kuyatekeleza kwa vitendo kulingana na hali walizonazo na kile ambacho Torres angekuwa ameshauri. Hivyo wawili hawa walikuwa na ushirikiano wa karibu sana katika kufanya maamuzi ambayo yangeiletea timu yao hii manufaa. 

Lexi pia alikuwa mtaalamu wa kupigana. Alijua kupigana kwa mitindo mingi, naye alikuwa na mwili ulioimarika ijapokuwa kwa njia ya kike, wenye ngozi nyeupe, na nywele zake laini (zenye mwonekano kama wa manyoya yenye kuchoma) alikuwa amezipunguza kuzungukia pande za kichwa chake na kuziacha nyingi upande wa juu. Kutokana na njia yake ya kushughulika na mambo kwa umakini, wenzake walimheshimu sana kutokana na busara zake katika mipango na maamuzi, hivyo kwa hawa wengine alikuwa kama kiongozi. Ikiwa angesema kitu, basi wenzake wangefuata. 

Lakini mtu wa mwisho kwenye kundi hili ndiye aliyekuwa kama mkuu wao, kwa sababu wengine walimwona kama "boss." Yeye ndiyo aliwapa kila kitu walichohitaji ili kutekeleza mipango yao, kutokana na kuwa na pesa nyingi sana, na pia yeye kuwa mwanzilishi wa kundi hili. 

Hawa ndiyo walikuwa "Mess Makers." Wote walikuwa na nia zao za kufanya haya yote waliyokuwa wamejiingiza kuyafanya. Baada sasa ya Lexi na Mensah kuwa wameondoka, waliobaki kwenye nyumba ile pia wakabadili mavazi na kuvaa ya kawaida tu, kisha wakaenda kwenye gari wakiwa wameacha vitu kadhaa kwenye nyumba ile na kubeba vichache kwenye mabegi ya mgongoni. 

Walipoanza kuliondoa gari sehemu hiyo, Oscar akatumia kifaa kidogo kama rimoti na kubonyeza, na ndani ya nyumba ile waliyoiacha likalipuka bomu dogo tu ambalo jamaa alikuwa ameliweka. Hivyo nyumba hiyo na kila kitu kilichokuwa ndani yake kikateketea kwa moto. Oscar alipenda sana kufanya mambo kama vile yuko kwenye filamu za kuigiza, na kwa kuwa wenzake walikuwa wameshamzoea kwa njia hiyo walimwacha tu awaburudishe kwa lolote lile alilofanya. 

Safari ya kumpeleka Kevin kule "chini" ikaendelea usiku huo huo uliokuwa umetokeza mambo mazito ambayo yangezidi kuufanya mchezo huu wa paka na panya uwe mtata zaidi.


★★★


Siku iliyofuata, Luteni Michael pamoja na wenzake waliamkia kwenye safari ya kurudi Dar es Salaam. Walikuwa wamechukua helicopter ili kuweza kufika kule haraka iwezekanavyo. Kufikia wakati ambao walikuwa wamefika Dar es Salaam, tayari vyombo vya habari nchini vilikuwa vimeshaanza kusambaza taarifa muhimu kuhusu Kevin Dass kuwa mmoja wa watu walioshiriki katika wizi uliofanyika benki kuu. Wananchi waliombwa ushirikiano kutoa taarifa haraka ikiwa wangemwona mtu huyo sehemu yoyote ile. IGP Donald Ngassa ndiye aliyetoa tamko kupitia vyombo vya habari na kusema kwa kutoa taarifa haraka, wananchi wangekuwa msaada mkubwa sana katika kuwakamata wahalifu wote waliohusika na wizi huo. 

Luteni Michael, ACP Nora, Mishashi, Hussein, Mario, pamoja na Alex walielekea kwenye jengo lile ambalo kikosi kilichobaki cha timu ya Luteni Michael kilikuwepo. Waliwakuta akina Bobby, Omari na Vedastus wakiwa hapo, na wanajeshi hawa wakawapokea vizuri na kuwapa pole kwa kilichowapata kule Mwanza. Bila kukawia, Luteni Michael akamuuliza Vedastus ikiwa kazi ambayo alikuwa amemwachia yeye na Omari wafanye waliitekeleza.

"Ndiyo Luteni. Tumefatilia makazi ya huyo Kevin na sehemu ambazo amefanyia kazi, lakini hatujapata mtu yeyote ambaye anaweza kuwa wa familia au rafiki wa karibu," Vedastus akasema.

"Na watu ambao amefanya nao kazi wanasema wanamjua tu kikazi, lakini hata kutoka naye kupata kinywaji hawajawahi. Majirani wa sehemu anayokaa wanasema hana urafiki na mtu yeyote, na hawajawahi kumwona akipeleka mtu pale," akasema Omari.

"Unataka kusema hana historia yoyote? Vipi kuhusu address za zamani, shule alizosomea, vyeti vya masomo, vyeti vya kuzaliwa?" akauliza Luteni Michael.

"Wazazi wake wote wameshafariki. Record zake za zamani za masomo na maeneo aliyoishi ziko blank. Hakuna uhusiano wowote wa kiukoo alionao na yeyote huku. Yaani ni kama jamaa amesafisha maisha yake ya zamani ili kuwa na maisha mengine kabisa," akasema Vedastus.

"Dah! Kwo' ndiyo tumempoteza yaani! Hawa watu wanafanyaje hivi?" akauliza Hussein.

"Hatujawapoteza. Kuna njia nyingine tu itakayosaidia kuwakamata haraka. ACP Nora... una jambo lolote?" Luteni Michael akasema.

"Ndiyo... aam... kuna jambo nimefikiria, lakini nahitaji kufanya uchunguzi kwanza," akasema Nora.

"Umefikiria jambo gani?" Alex akamuuliza Nora.

"Nilipompiga risasi nne yule jamaa, zote zilidunda na hata nikaona cheche. Nataka kujua ni aina gani ya fabric iliyotumiwa kwenye nguo yake maana kwa bulletproof za kawaida risasi zingeingia ndani na kuganda," Nora akasema.

"Lakini zake kudunda inamaanisha ilikuwa ngumu sana. Kevlar labda..." akasema Omari.

"Labda. Tukishajua ni aina gani zilizo ngumu sana namna hiyo kuagizwa nchini ndani ya miezi michache iliyopita na kwenda sehemu tofauti na vyombo vya usalama, basi huenda tukapata clue yoyote ya mtu aliyetumika kuzitengeneza ziwe nguo overall... na kama ziliuzwa..."

"Basi ziliuzwa kwa nani," Luteni Michael akamalizia maneno ya Nora.

"Ndiyo," Nora akasema.

Luteni Michael akatabasamu na kuwaambia wenzake, "Mmeona? Hii ndiyo sababu tunaye huyu dada hapa. Bobby, fuata kila kitu atakachoomba ufanye kwa masuala ya utafiti."

"Sure boss," Bobby akasema.

"Alex, Mishashi, nifuateni. Tunaenda kuonana na watu fulani. Wengine, mpeni hospitality nzuri dada yetu," Luteni Michael akawaambia.

"Ah... usijali boss. ACP Nora ndiyo malkia hapa," akasema Mario na kugongesha kiganja chake kwa kiganja cha Nora.

"Una akili nzuri sana dada," Omari akamwambia Nora.

"Asante. Lakini... sina uhakika sana kama hii ita..."

"Usijali. Instinct zako zina nguvu sana, ninajua tutapata jambo fulani tu. Na... usijikakamue mno, we' ukimaliza kuwaelekeza hawa mbwa toka ukapate chips mayai u-relax kidogo, sawa?" Luteni Michael akamwambia.

Nora akacheka kidogo.

"Dah! Kwo' sisi wengine ndo' tukae kupiga kazi mpaka basi?" akauliza Mario.

"Ndiyo maana yake," Luteni Michael akasema.

Kisha akamwangalia Nora na kutabasamu kirafiki, naye Nora akatabasamu pia. 

Baada ya hapo, Luteni na wanajeshi wake wawili wakaondoka wakimwacha ACP Nora na wengine kwenye utafiti huu mpya.


★★★


LaKeisha, Victor, Oscar, na Kevin walifanikiwa kufika salama sehemu yao muhimu ya maficho kwenye mida ya saa 4 asubuhi. Ilikuwa ni kwenye mkoa mwingine sasa, na baada ya wao kufika huko "chini," walimkuta Torres Dela Robia akiwa ametulia tu akisoma mambo fulani kwenye kitabu. Alipowaona tu, alitambua kuwa Kevin alikuwa ameumia, naye akamwambia aketi ili amchunguze vizuri na kumpatia tiba sahihi. 

Kevin akakaa, akiwa bado ameudhika sana kwa mambo yote yaliyotokea, na akiwa anahisi maumivu mwilini mwake. Wengine wakawa wameelekea kufata vyakula upande mwingine wa sehemu hiyo na kuvileta ili wale. Akiwa anamchunguza Kevin, Torres aliuliza yaliyotokea Mwanza, naye Oscar akaanza kumsimulia lakini kwa kutia chumvi nyingi sana kwamba Kevin alipigwa na mwanamke mwembamba tu na mfupi mno.

"Hivi Torres, hakuna dawa yoyote hapa ya kukata maumivu yangu haraka ili niyahamishie kwa bwege mmoja hapa?" Kevin akasema kwa kuudhika.

Torres akatabasamu na kusema, "Hapana."

"Hey, umeshampatia?" LaKeisha akamuuliza Kevin.

"Kunipatia nini?" Torres akauliza.

Kevin akatoa kifaa kile ambacho Lexi alimpa na kumwambia Torres kwamba Lexi alisema ampe.

"Halafu anataka uchunguze kuhusu watu waliomw-attack Kev, umwambie unafikiri nini kuwahusu maana anahofia njia waliyotumia kumfikia inaweza kutuletea shida," Victor akamwambia.

"Mmm... okay. Twendeni," Torres akasema.

Akawa amemaliza kumfungia bendeji Kevin na kuanza kuelekea upande mwingine wa sehemu hiyo. Walifikia chumba ambacho kilikuwa na mitambo mingi pamoja na "screen" kadhaa zilizounganishwa kupitia kompyuta zake maalumu kwa ajili ya mambo mengi aliyofanyia utafiti. Chumba hiki kilijaa makolokolo ya kiteknolojia ya kila aina, naye Torres bila kukawia akaketi na kuanza kupekua taarifa kuhusu watu ambao walimkamata Kevin. 

"Kwa hiyo tokea walipokushika mpaka wakati ambao wakina Oscar walikufata, hakuna aliyetambua una tracking device, isipokuwa huyo mwanamke?" Torres akamuuliza Kevin.

"Ndiyo. Sijui hata alitambuaje yaani, ka' mchawi vile," Kevin akasema.

"Eeh, inaonekana ndiyo mchawi wao. Luteni Michael nilitegemea angehusishwa na hili sakata, lakini huyu... ACP... inabidi nisake picha za ma-ACP wa kike kwa mikoa yote unionyeshe ni yupi," Torres akasema.

Kisha akaanza kubofya haraka-haraka sana 'keyboard' yake hapo, akitafuta mafaili ya haraka ya picha za Makamishna wasaidizi wa polisi nchini.

"Bado huwa sielewi unafanyaje hayo madude yako haraka haraka hivyo bila hata kuangalia, halafu...." Oscar akawa anaongea.

"Hizi hapa, njoo unionyeshe ni yupi," Torres akamwambia Kevin.

"... boom! Tayari unapata unachotaka," Oscar akamalizia alichokuwa anasema.

Kevin akasogea karibu zaidi na kuanza kuziangalia picha hizo, naye akamwonyesha picha ya Nora baada ya kumwona.

"Well, well, well... ACP Nora Lois Nahaman," Torres akasema.

"Ndiyo nani?" LaKeisha akamuuliza.

"Ni Kamishna Msaidizi wa Polisi Dodoma. Lakini jina la cheo hiki lisiwadanganye. Huyu mwanamke ana level za hali ya juu sana kwenye masuala ya upelelezi, na mara nyingi wahuni wanapofanya uhalifu halafu wakashindwa kupatikana, huyu ndiyo huwa anaitwa kuwachokonoa huko waliko mpaka wanawapata," Torres akawafahamisha.

"Mbona anaonekana kama contestor wa Miss Tanzania, siyo kwa uzuri huo! Ameolewa? Kuna namba zake hapo chini?" Oscar akauliza kimasihara.

"Hivi hauwezi ku-focus kwa dakika moja tu?" Kevin akamuuliza Oscar kwa kukereka.

"Kinachofanya awe na huo uwezo ni nini? Maana haonekani kuwa mtata kihivyo," Victor akamwambia Torres.

"Looks huh? Hapana. Nora unaweza kumchukulia kama FBI agent Victor. Amesomea Marekani, na hata kuna wakati alialikwa kwenye darasa muhimu la wapelelezi vijana na General wa Ufaransa... tena Ministère De La Défense! Ame-specialize kwenye masuala yote ya decisive action, offensive, defensive, stability, forms of maneuver, reconnaissance, infiltration... yaani ni mtu ambaye sikuzote atakuwa na tentative plan ikiwa moja haitafanikiwa ili kufanya mbili ifaniki...."

Torres akaendelea kumwelezea ACP Nora kwa njia yake yenye ujuzi mwingi. Oscar, Victor, Kevin na LaKeisha walikuwa wanaangaliana tu wasielewe alikuwa anabwabwaja hayo yote kwa ajili gani. Ikabidi Victor aingilie kati.

"Okay, okay, kaka... slow down. Siyo wote humu tunaelewa lugha yako," Victor akasema.

"Na Kevin kuielewa ni mpaka Nora amshushie kipigo kingine," Oscar akasema.

"Sekunde tano zitakazofuata ukitaja jina langu, nakushona mdomo," Kevin akamwambia Oscar.

Oscar akacheka.

"Mtu wa hivyo anawezaje kuwa na cheo cha kifala namna hiyo?" akauliza LaKeisha.

"Well... kwa ninavyojua, Nora mwenyewe ndiyo alichagua hiyo position. Ni mtu fulani asiyependa makuu sana, na sijui ni kwa nini ila ni kama huwa hataki vyeo vya juu kwa sababu fulani. Labda baba yake ndiyo sababu," akasema Torres.

"Baba yake ni nani?" akauliza Victor.

"You'll never guess. Baba yake ni...."

"Vijana..." 

Torres alikatishwa na sauti hiyo, na wote wakageuka na kumwona mwanaume waliyemfahamu vizuri sana.

"Boss!" Oscar akaita kwa shauku.

LaKeisha akatabasamu na kumfata Boss wao huyu, kisha akamkumbatia na kusimama karibu yake. 

Kevin akawa anamwangalia kwa wasiwasi kiasi.

"Boss... uhali gani?" Victor akamsalimu.

"Niko poa. Naona mmerudi," Boss akasema.

"Yaani! Isingekuwa ya huyu mpaka sasa ningekuwa Gold Crest napigwa sunscreen... angalau pale ndiyo pamekaa vizuri Mwanza nzima," LaKeisha akasema, akimaanisha Kevin.

"Boss... ishu yote haikuwa jinsi ambavyo unadhani kwamba...."

Kevin alikuwa ameanza kujitetea, lakini Boss wao akanyanyua kiganja chake juu kumzuia asiendelee.

"Ajali huwa zinatokea, hatuzipangii. Imeshapita hiyo, kilichopo sasa ni stage inayofuata. Torres?" Boss akaongea.

"Yes boss. Lexi ameituma tayari. Kevin ndiyo amekuja na kunipatia, kwa hiyo nitaangalia ni jinsi gani watayaingiza nchini na wakati gani ili tufanye interception haraka," Torres akamwambia.

"Good," Boss akasema.

"Sa'hivi tumeshaanza kupigana hadi na wajeshi. Boss... its so cool," Oscar akamwambia.

Boss wao akamwangalia Kevin, kisha akauliza, "Lexi yuko wapi?"

"Dar. Ameenda na Mensah," Kevin akajibu.

"Amekwenda huko bila sisi boss, naona kama siyo fair. Kwanza ameenda kufanya nini? Maana hata wewe inaonekana hukujua angeenda huko," LaKeisha akauliza.

"Hajaenda kuzurura LaKeish, anafatilia ishu ya Kevin kukamatwa, ndiyo maana anataka nimtumie taarifa juu ya ACP Nora. Sasa hivi mambo yatakuwa complicated kiasi maana Nora ni kichwa. Itatubidi tuwe makini zaidi," Torres akasema.

"ACP Nora?" Boss akauliza.

"Ndiyo boss... huyo huyo," Torres akasema.

"Yeye pia alikuwepo wakati umeshikwa?" Boss akamuuliza Kevin.

Kevin akatikisa kichwa kukubali.

"Ulikuwa unasema ni mtoto wa nani?" Victor akamuuliza Torres.

Torres akanyoosha kiganja chake kumwelekea boss wao ili atoe jibu. Wote wakamwangalia na kuona uso wake ukigeuka na kuwa makini zaidi.

"Nora ni binti ya Jacob," Boss wao akawaambia.

"Jacob as in...." Oscar akauliza.

"General Jacob Rweyemamu?" Victor akauliza kimshangao.

"Yeah," Torres akajibu. 

"Umesema anaitwa Nora Lois Namahan, inawezekanaje awe mtoto wa Jacob?" Victor akauliza.

"Anatumia jina la pili la mama yake, siyo baba yake. Na... ni Nahaman, siyo Namahan," Torres akamwambia.

"Kumbe! Kwa hiyo kumbe ndani ya huu mzunguko kuna father-daughter love wanayotaka ituandame? Haitakuwa na shida tena lakini. Lexi ana akili, ndiyo maana ameenda na Mensah ili autungue ubongo wa huyo malaya. Problem solved," LaKeisha akasema.

"Sidhani sana kama anapanga hivyo, itabidi nimtumie info zote then tusikie atasemaje. Bado hajaongea nawe kabisa?" Torres akamuuliza Boss.

"Fanya tu alivyokwambia. Kevin...." Boss akasema.

"Ndiyo boss..." Kevin akaitika.

"Ukimaliza kula, msafishe Zelda," Boss akasema, kisha akawaacha wote.

Kevin akabaki amesimama huku pozi likiwa limemwisha. 

Oscar akaigiza kama anataka kucheka lakini akaziba mdomo; makusudi tu ili Kevin akasirike. 

"Bro, una mikosi. Maliza kula kamwoshe mbwa huyo. Ila angalia asikung'ate," Victor akasema, naye Oscar akaangua kicheko cha kukera sana.

"Usimwite Zelda mbwa bwana," LaKeisha akasema.

"Agh... whatever," Victor akasema na kuondoka hapo.

Kisha LaKeisha na Oscar wakaendelea na mambo yao mengine, wakimwacha Torres anafanya vitu vingi kwenye kompyuta yake kutia ndani kumtumia Lexi taarifa alizohitaji, na Kevin bado akiwa na hasira sana moyoni kwa kuhisi ni kama anadharauliwa. Akaamua tu kuondoka hapo pia na kwenda kufanya kazi ambayo boss wao alikuwa amempa, akitambua ilikuwa ni kama adhabu isiyo ya moja kwa moja.

★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next