SEHEMU YA 09.
Saa mbili za usiku Hamza alionekana katika pikipiki ambayo ilienda kusimama kando kando ya barabara ndani ya Kijichi.
Hamza mara baada ya kushuka katika bodaboda hio aliangaza kulia na kushoto na kisha alianza kupiga hatua kwa kuvuka barabara upande wa pili akiachana na ile iliokuwa ikinyoosha moja kwa moja kuelekea uelekeo wa Vikunai kwenda Kibada.
Mtaa huo ulikuwa ndio mtaa wa kifahari kwa wilaya ya Temeke ndani ya jiji la Dar es salaam , kulikuwa na utulivu wa hali ya juu na mazingira yake yalikuwa safi na hata Hamza aliyapenda.
Baada ya kutembea umbali mfupi alikuja kukunja kulia kwake na kuingia katika moja ya mgahawa mkubwa uliokuwa ukipatikana ndani ya eneo hilo , uliofahamika kwa jina la Dina Tea House & Restaurant.
Ulikuwa ni mgahawa wa kifahari mno na wa kipekee ambao unapatikana ndani ya jiji la Dar e salaam , upekee wake ulitokana na kwamba ndio mgahawa pekee ambao umejipambanua kwa kuuza vinywaji aina ya chai pekee na chakula cha aina zote ambacho kinaendana na aina ya chai husika.
Kwa mfano chai aina ya Kombucha lazima iendane na chakula chake na aina hii ya huduma iliufanya mgahawa huo kuwa maarufu kati ya watu matajiri..
Ndio ulikuwa ni mgahawa wa kifahari kwani unaambiwa kikombe kimoja cha chai kinaweza kuuzwa si chini ya thamani za shilingi elfu kumi za kitanzania na kuna zaidi ya hapo, kwa mfano chai ya Gisaeng kutoka Korea tu ilikuwa ikiuzwa zaidi ya shilingi laki moja.
Ndani ya maegesho kulikuwa na magari mengi ya kifahari , hakukwa na gari la chini ya milioni therathini ndani ya magahawa huo.
Hamza alishazoea na alijua aina ya wateja ambao huhudumiwa na mgahawa huo lakini siku hio kidogo magari yalikuwa mengi kuliko siku zote ambazo alikuwa amefika ndani ya eneo hilo.
Hamza alijiambia pengine kutofika kwake hapo zaidi ya mwezi mmoja kunamfanya kuona mabadiliko makubwa.
“Bro Hamza leo naona umefika , karibu sana Madam anakusubiria ndani”Aliongea kijana mmoja huku akitoa tabasamu akimkaribisha Hamza.
“Lau nishakuambia mara nyingi haina haja ya kutoka kunipokea kama hivi”Aliongea Hamza akiwa na muonekano ambao haukuwa umebadilika sana.
“Bro unakuja mara chache sana hili eneo , hivyo sidhani kama nitapata usumbufu wa kutoka mara kwa mara na kuja kukupokea kila ninapokuona”Aliongea na kumfanya Hamza kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha.
“Naona hali ya hewa siku hizi ni ya joto sana ndani ya hili jiji , kazi zimekuwa nyingi kwangu na kunifanya kuwa bize ndio maana sikupata muda wa kufika kuwasalimia”
“Ndio ndio , nakujua wewe ni mtu ambae upo bize sana”.
“Naona baisikeli yangu hamjaitoa bado ipo palepale”Aliongea Hamza huku akishangaa kidogo na kutaka kucheka kwa wakati mmoja baada kati ya usafiri wa hali ya chini uliokuwa ndani ya maegesho hayo ilikuwa baiskeli yake ambayo mara ya mwisho alifika nayo hapo na aliiacha kwasababu iliharibika mara ya mwisho.
“Nimeitoa na kuirudisha , madam alinipa kazi ya kuipeleka kwa fundi na imetengenezwa , si unaona sasa hivi inamuonekao mzuri”Aliongea na kumfanya Hamza kutingisha kichwa kidogo kwa kukubali na kisha kuanza kuzipiga hatua kuelekea mlango wa nyuma.
“Bro naomba usitumie mlango wa nyuma , Madam akijua hili ataniletea shida”Aliongea kwa kubembeleza bwana aliefahamika kwa jina la Lawrence au Lau wengi wanavyomuita.
“Hebu kwanza angalia nguo zangu namna zilivyochafuka , sidhani hao mabosi waliopo hapa ndani wataniangalia vizuri nikipita mlango wa mbele, nashusha hadhi ya huu mgahawa pia”
“Braza haina haja ya kuongea hivyo , Madam sio mtu wa namna hio , hawezi kujali na ititoshe unadhani kuna yoyote ndani ya hili eneo mwenye kutosha umuhimu wako kwa Madam?”
Hamza mara baada ya kuona Lau yupo ni mwenye kubembeleza sana aliona asikatae ukarimu huo hivyo aliamua kupita mlango wa mbele na kwa bahati nzuri katika Korido ya mgahawa huo hakukuwa na watu wengi , staili ya mgahawa huo ilijengwa kwa namna ya vyumba kama Kabini tokea mwanzo , ijapokuwa kulikuwa na sehemu ambayo ni kama watu wote waliweza kukaa lakini kwa wale ambao walikuwa wakihitaji kufanya maongezi ya muhimu walikuwa wakitumia vyumba hivyo kukutania , hii ni moja wapo ya faida ya mgahawa huo.,
Hamza alinyoosha mpaka katika moja ya chumba cha mwisho kabisa binafsi ambacho aliekuja kumsalimia ilikuwa ni kama ofisi yake na kisha alishika komeo na kusukuma mlango.
Sekunde ambayo mlango alifungua visu vitatu vilirushwa kuelekea alipo vikilenga eneo la moyo na tumbo kwa spidi ya mwanga.
“Damn!!”
Hamza alijikuta akimaka kwa mshangao lakini wepesi wake ulimfanya kusogea pembeni na visu hivyo vilipita inchi chache sana kutoka kwenye mwili wake .
“Tuk ! , Tuk , tuk!!!”
Vile visu vitatu vilikuwa vimefungwa na vishada(Tassels) vya rangi ya Violet , vilikuwa vyembamba mno na vyenye makali kama viwembe na viligonga katika ukuta na kudondoka chini.
Hamza mwanzoni alidhani huo ndio mwisho lakini dakika ileile ilitokea mianga kama flash aina tatu na kumsogelea kwa kasi kubwa.
Lakini Hamza alionekana kuwa mwepesi na shambulizi hilo lingine na palepale aliinua mkono wake juu na vile visu vyote vitatu vilinasa katiki ya vidole vyake, ilikuwa ni utaalamu wa hali ya juu mno.
“Dina , kuna haja ya haya mambo , kwani lazima uone utumbo wangu ndio uridhike?”Aliongea Hamza huku akitoa kicheko.
“Nilitaka kuona kama uwezo wako umeusahau kama ulivyonisahau na mimi, miezi miwili inapita bila ya kunitembelea”Aliongea mwanamke mrembo .
Alikuwa ni mrembo haswa , akiwa amevalia gauni jeupe lenye maua maua ya rangi nyekundu ambalo limefungwa na mkanda kiunoni na kuufanya mwili wake kugawanyika vizuri kati ya kiuno na juu , alikuwa na sura ya kuchongoka kama yai na lips pana ambazo zimepakwa rangi nyekundu.
Muonekano wake ulikuwa sio wa kawaida kabisa , pengine licha ya kwamba alikuwa akivutia sana lakini ni ngumu sana kwa mwanamke wa kawaida kuwa na mapozi ya aina hio.
“Sio muda mrefu sana tokea nifike , mimi naona ni juzi tu”Aliongea Hamza huku akiokota vile visu vilivyokuwa vimedondoka chini na kuweka mezani.
“Miezi miwili bado tu unasema sio muda mrefu , wanaume wengi wenye pesa zao na maarufu hufika hapa kila siku kwa ajili ya kuniona mimi Dina , kiasi cha kunifanya kushindwa kutoka lakini wewe mkorofi umekosa hata nafasi moja katika mwezi kuja kunitembelea?”
“Distance makes the heart grow fonder , Kama tukionana kila siku haitaleta raha tena , kwangu mimi naona ni vizuri zaidi kukuona mara moja kwa uda mrefu , inannifanya nikuone kama malaika alieshushwa kutokana na urembo wako”Aliongea Hamza.
Kwa namna ambavyo alikuwa akiongea ni kama vile amebadilika mbele ya mwanamke huyo , hakuwa na muonekano wa kipole bali ulikuwa ni muonekano wa kicheshi uliojaa utu uzima.
“Eti malaika alieshushwa , kwaho mimi ni mzuri sana mpaka kuitwa malaika?”
“Nadhani unanijua vizuri mimi ni msema kweli “Aliongea Hamza , lakini ukweli ni kwamba katika moyo wake mwanamke ambae amekutana nae muda wa mchana hakuwa wa kawaida kabisa , mrembo Regina kwake alikuwa mzuri zaidi ya Dina , faida kubwa ya Dina ni mvuto aliokuwa nao kutokana na mapozi yake ya kike na mazoezi.
Upande wa mrembo huyo aliefahamika kwa jina la Dina , ambae hatujui wanafahamiana vipi na Hamza mpaka kuanza kurushiana visu alionyesha tabasamu katika uso wake lililomfanya kuvutia zaidi na yote hayo ni ile raha ya kusifiwa kama mwanamke mzuri.
“Nimekusamehe siku ya leo , nina njaa ya usiku , hebu kaa na wewe ule , vyakula vyote unavyopenda vipo hapa”Aliongea.
Hamza alikuwa na njaa mno na harufu ya chakula hicho tokea anaingia ilimfanya njaa izidi kuuma , alisogea na kisha alivuta kiti na kukaa na mara baada ya kufunua chakula ambacho kilikuwa kimefunikwa alijikuta akivuta pumzi nyingi.
“Unasemaje hiki ni chakula ninachokipenda ilihali siwezi kabisa kukilipia .. ugali wa hizi Abaloni za ki’Australia nadhani nikianza kula nitatokwa na damu puani”Aliongea Hamza na kisha alisogelea bakuli ambao lilikuwa na pilau ndani yake na kisha alijisevia kwenye sahani na akachukua na nyama wa kukaanga pamoja na mchuzi wa samaki na kuweka kwenye sahani yake na kuanza kula chapu chapu , ndani ya dakika chache tu asilimia sabini ya pilau yote ilikuwa imeisha.
“Dina dada yangu mbona umeacha kula?”Aliuliza Hamza mara baada ya kuona Dina hakuwa akifanya chochote zaidi ya kumwangalia tu .
“Nishamaliza kula tayari , pili nnimeanza diet hivi karibuni,nakula kidogo sana”
“Kuna haja gani ya kufanya diet ilihali mwili wako huo huo unakupendeza?”
“Wewe ni mwanaume na huwezi kuelewa , ‘diet’ ni ‘life carear’ ya mwanamke , sitaki kuongeza uzito mimi .. kwanza hebu niambie, unapendelea mwanamke wa aina gani , mwembamba mwenye nyama au mnene?”
“Napenda wale wanawake ambao ni wembamba na wana kalio lainiii ukiliminya”Aiongea Hamza huku akitabasamu kifedhuli , alikuwa mtu mwingine kabisa kwa kile alichokuwa akikifanya.
“Wewe muhuni , yaani huna hata aibu nitakukata mimi?”Aliongea Dina na palepale kutaka kumrushia tena Hamza vile visu.
“Dina inatosha bwana , haina haja ya kutaka kunitumia kama kifaa cha majaribio ya mbinu zako za kininja””Aliongea na kumfanya Dina kutulia.
“Hamza hebu niambie kwanza ukweli , unadhani nitachukua miaka mingapi ya mazoezi mpaka kufanikiwa kukupiga na mashambulizi yangu?”
“Miaka..!, hehe , labda arobaini au hamsini hivi”
“Kwanini usiseme tu maisha yangu yote”Aliongea huku akiwa siriasi.
“Haha.,. haina haja ya kuwa siriasi hivyo , ukiachana na mbinu za mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi, siku zote mtu anapaswa kuangalia kipaji chake kwanza kabla ya bidii, ule msemo wa kusema Bidii hushinda kipaji ni uongo, ni msemo ambao watu hutumia kujifariji tu”Aliongea Hamza.
“Halafu Dina hii supu ya kuku ina radha flani hivi, ni kama kuna chembe chembe za vinyama nyama ,umeweka Sea Cucumber nini?”
“Oh! , kumbe umeona, kuhusu hilo ni nyama ya kusaga ya mkia wa Kangaruu , nimenunua bei sana na ni kwa ajili yako kukupa virutubisho”Aliongea Dina huku akiwa na tabasamu flani la kichokozi.
“Mkia wa Kangaruu!!!”
“Unaonaje? , imekuwaje kwanza ukagundua utofauti wa harufu maana unasagwa na kuwa kama vumbi la nyama na kisha huweka kama viungo kwenye supu na harufu yake hupotea kabisa, inafanyika hivyo ili iwe rahisi kufanya kazi mwilini”Aliongea.
Mkia wa Kangaruu ni sawa na mtu anapotumia Viagra au Mkongo , mara nyingi hutumiwa sana na matajiri tena kwa siri kuwekwa kwenye vinywaji kama Mvinyo na baadhi ya dawa za kuongeza hamu ya tendo.
“Dah , sasa kwanini ukanifanya ninywe supu yenye huu mchanganyiko ,unataka nitokwe na damu puani?”Aliongea Hamza mara baada ya kuhisi presha ya damu kuongezeka kwa kasi.
Unaambiwa vumbi la vinyama vya mkia wa Kangaruu kidogo tu inaweza kumfanya mwanaume kupatwa na uchizi na ni ngumu sana kuepuka mtego wa mwanamke ukiwa katika athari ya dawa hio.,
“Unadhani kwanini nimefanya hivi?” Aliongea Dina na alisimama kutoka alipokuwa amekaa na kumsogelea Hamza na kisha alimwinamia shingoni na kufanya marashi yake yaliochanganyika na pumzi kumsisimua Hamza shingoni.
Kutokana na Athari ya dawa hio , mwanamke ambae alikuwa mbele yake urembo wake ni kama umeongezeka mara kumi , lakini kwa uwezo wake wote alijizuia kutoruhusu akili kumpotea na kumgusa kwa namna yoyote ile.
Alikuwa akijua kabisa kufanya mapenzi na Dina kila kitu kisingekuwa sawa tena , tokea arudi nchini Tanzania na kuanza chuo huku akiishi maisha ya kawaida ni kama ilimfanya kupata amani ambayo alikuwa akiiota hivyo hakutaka hali hio kubadilika.
Dakika ileile muonekano wa Hamza ulianza kubadilika na chumba kilizidi kuwa cha baridi huku msisimko ndani ya eneo hilo ukiwa ni ule wa kuogofya,Hamza alikuwa ni mtu mwingine kabisa na hakuwa na ishara yoyote ya utani katika macho yake.
“Dina usiendelee..!”Aliongea Hamza kwa sauti iliokuwa na mikwaruzo lakini kwa namna flani ya kuhamasisha.
Mabadiliko ya Hamza yalimfanya mwanamke huyo kushikwa na hali ya uchungu mno kwenye macho yake na ishara za hasira lakini dakika hio hio alibadilisha muonekano wake na tabasamu bandia na kujiondoa kwake.
“Hebu muone sasa uoga ulivyokushika , unadhani mimi Dina nataka kukumeza mpaka kunibadilikia hivyo , haya sitaki tena hata kuchokozana na wewe mimi”Aliongea akijitahidi kurudisha hali ya utani ili kuonoa hali hio isiokuwa ya kawaida katika uso wa Hamza.
“Tena umekuja wakati muafaka , nimepokea mzigo wangu wa majani ya chai kutoka nje ambayo nahitaji ujuzi wako kuyachunguza, nione kama sijapigwa maana ni hela nyingi nimetumia”Aliongea.
Dakika hio Hamza hatimae alikuwa amerudi katika ule muonekano wake wa kizembe na kuangalia chai ambayo ilikuwa ikimiminwa kutoka kwenye jagi.
“Hakuna shaka , ni wakati wa kufurahia chai ya kimatawi ya mrembo Dina kwamara nyingine”Aliongea Hamza akiwa na tabasamu , spidi yao ya kubadilika haikuwa ya kawaida kabisa , pengine watu wa kawaida kwa kile kilichotokea dakika chache zilizopita wasingerudi katika hali hio.
Dina kama bosi wa mgahawa huo ambao umaarufu wake ni kutokana na kuhudumia aina mbalimbali ya ‘premium tea’ alikuwa makini sana kwa kila mzigo ambao anaagiza.
Dina upande wake alionekana kuwa siriasi na hakutaka kuendelea kuongea matani na alianza kuonyesha umahili wake katika kufanya mchanganyiko wa viungo vya chai , pamoja na kuweka majani flani katika kikombe na kuyaloanisha na maji ya moto. Na baada ya hapo ndipo alipompatia kikombe Hamza ajaribu.
“Hii ni chai ya mmea wa jamii ya Camellia Sinensis , ambayo hutengeneza chai maarufu ya Hui , majani haya yamefika jana kutoka China, hebu jaribu kuonja na uniambie ni gredi ya ngapi?”Aliongea Dina kwa kirefu wakati wa kumpatia kikombe Hamza.
Hamza kabla ya kunywa kwanza aliangalia majani hayo , yalikuwa majaini kama majani ambayo hayajasagwa na ilishangaza kwa namna ambavyo yalionekana mabichi licha ya kusafirishwa umbali mrefu.
“Hili jani limenyooka na ni zito , ukiangalia veini zake kidogo ni nyeusi kuliko jani , hii ni jamii moja ya majani ya Camellia kama ulivyosema , mmea wa chai ya kijani , unaofahamika kwa jina maarufu la kichina, Taipeng”
“Sio mbaya hebu jaribu radha yake kwanza”Aliongea na Hamza alionja pamoja na kunusa harufu ya chai ile.
“Mh! , hii ni chai nzuri sana , radha yake unaipata baada ya kumeza , sio chungu hata kidogo”
“Hio ndio maana yake , la sivyo isingenigharimu zaidi ya kiasi cha shilingi laki moja kwa kilo tu , ninachouliza ni gredi ya ngapi?”Aliongea na kumfanya Hamza kunywa tena na alionekana ni kama alikuwa akiichezesha kwenye ulimi na kisha akameza.
“Harufu na ‘Aftertaste’ inatosha kusema imeingia gredi namba tatu , lakini kuhusu utamu usioisha haraka naweza kusema hii ni Grade A”Aliongea Hamza.
“Kwa maneno yako , ni sahihi kusema kwamba Lawrence bado hana uelewa wa kutosha kuhusu sayansi ya chai, licha ya kusoma food science”Aliongea.
“Uzoefu unahitajika sana likija swala la chai za tamaduni mbalimbali , ni rahisi kufanya makosa kwa mtu ambae hajatembea sana na kuonja kila aina ya chai”Aliongea Hamza.
“Unaonaje ukifanya kazi hapa , utapata faida ya sehemu ya kuishi na chakula, lakini pia malipo mazuri, kuliko kule uswahilii unakoiishi”Aliongea.
“Ah! Hapana, napenda aina ya maisha yangu bwana , yananitosheleza”Aliongea Hamza huku akijiambia wakati huo hakuhitaji kazi nyingine kabisa ya uboifried wa maigizo inamtosha.
“Unaongea kama vile nitakuingilia kwenye mambo yako, nataka kukuona mara kwa mara ndio nia yangu”
Mara baada ya mwanamke huyo kuongea kwa sauti hio ya kubembeleza ilimfanya Hamza moyo wake kulainika na kwa mvuto wa huyo mwanamke alijiambia anapaswa kuondoka la sivyo anaweza kushindwa kuvumilia.
“Dina muda umeenda , ngoja niondoke”
“Mbona haraka , hivyo kwanini usikae kidogo tukipiga stori , inachosha sana kukaa mwenyewe”
“Hahaha… kaa na Lawrence mpige stori , kwaheri , haina haja ya kunisindikiza”Aliongea Hamza na kisha alitoka.
“Mjinga sana wewe, mpuuzi sana wewe Hamza, unanuka, umeniona sivutii ndio maana unanikwepa kila siku?”Mrembo huyo alilaani huku macho yake yakitawaliwa na upweke.
Upande wa Hamza mara baada ya kutoka nje ya mgahawa huo alijikuta akipatwa na ahueni kwa kupumua kwa nguvu , maana alikuwa akijitahidi kujizuia mno na alikosa amani kwa kuona kwamba ataishia kufanya kitu ambacho hakikuwa kwenye mpango wake , ukweli ni kwamba ijapokuwa alikuwa akimkwepa huyo mwanamke lakini alifika hapo kutokana na kwamba alikuwa amemmisi.
“Bro vipi unaondoka na baiskeli yako?”Aliuliza Lau.
“Nitaiacha usiku mkubwa huu nitaondoka na pikipiki, ihifadhi vizuri”
“Sawa broo”
“Halafu hivi unamjua mtu mmoja anaefahamika kwa jina la Amosi , mzee flani hivi ambae ni kama mkopeshaji?”
“Unamzungumia Jasusi mstaafu , ni maarufu sana katika maeneo haya mpaka Kigamboni yote , yupo chini ya tajiri Hamdu mfadhili mkuu wa mgombea wa uraisi kupitia chama tawala.. anajitapa sana kwa kuamini jeshi lote la polisi lipo mikonoi mwake , anaweza kufungwa leo kwa uhalifu na kesho asubuhi ashatoka … vipi amekuletea tatizo lolote?, kwanini unamuulizia?, kama unataka nikamshikishe adabu niambie , nitahakikisha asubuhi anaitwsa hayati”
“Ah! , sijamaanisha hivyo , huyo bwana kuna mwanamke anamdai na anatumia deni kumtaka kingono , nataka angalau apatiwe vitisho ila usiende mbali”Aiongea Hamza.
“Nimekuelewa braza”Aliongea na kisha Hamza alimshika Lau Bega na kisha alizichapa raba kuelekea barabarani kutafuta bajaji au boda kwenda nyumbani , alitaka akakae chini kwanza asome karatasi ambayo alipewa na mrembo Regina kwa ajili ya kujiandaa na ajira yake kuanzia siku inayofuata.
“Madam !!”Aliita Lau mara baada ya kumuona bosi wake amesimama mlangoni akimwangalia Hamza akitokomea.
“Alikuwa akikuambia nini?”
“Inaonekana Braza Hamza amekosana na Amosi , Jasusi mstaafu , vipi tumuue?”Aliuliza Lau huku akiwa na muonekano tofauti na ambao alikuwa nao wakati wa kuongea na Hamza, alikuwa siriasi mno kama vile ni ninja.
“Haina haja tutaamsha matatizo mengine tu , hakikisha mnampa vitisho na onyo , pia fuatilia umfahamu mwanamke ambae Hamza anajaribu kumlinda , nataka kuona picha yake”
“Sawa Madam , halafu Zedi , Mbunge wa Ukonga amepiga simu ,anaulizia kama upo free kesho kwa ajili ya chakula cha usiku?”
“Mwambie siko free”Aliongea Dina kikauzu na Lau alitingisha kichwa na kutoka.
Comments