Reader Settings

SEHEMU YA 10.

Hamza mara baada ya kurudi  katika chumba chake alichopangisha maeneo ya uswahilini  Gongo la mboto  alikimbilia bafuni kuoga , maana  muda huo  wapangaji wote walikuwa washalala  na kumaliza kuoga hivyo   alikuwa huru kutumia bafu  na choo.

Mara baada ya kumaliza kuoga moja kwa moja alijitupa kwenye godoro  lake huku akiangalia juu kwenye ceiling board  akionekana kuwaza kitu  lakini ni dakika ileile  alikumbuka  alikuwa  na  karatasi ya kusoma ili kufanya vizuri katika ajira yake mpya.

Lakini kabla ya hapo aliingia katika mtandao na kutafuta jina lake  na ndani ya sekunde lilionekana.

“Regina Wilson, Eldest daughter   of the prestigious Dosam family in  Tanzania , CEO  of Dosam  Group , intelligent  and talented enterprenuer , the most beutifull  businesswoman of the year ….”

“Kwahio kumbe huyu ndio  mrembo  ambae ni CEO wa makampuni ya Dosam, naona hata hii picha ni kama  sio yake”Aliongea mwenyewe  Hamza wakati akipitia taarifa hizo.

Ukweli  ni kwamba kampuni ya Dosam ilikuwa ni maarufu sana nchini , na umaarufu wake unatokana na Brand yake , kila mahali ilikuwa ipo sio kwenye usafiri wa anga, maduka na mahoteli , hata Hamza jana  yake aliweza kupendeza kutoka katika moja ya duka la  Dosam.

Sasa ilimshangaza mwanamke mrembo namna ile ndio ambae alikuwa akivuma sana kwa kuwa mrembo asietaka kujionyesha lakini ambae alikuwa na akili nyingi kiasi kwamba ameiwezesha kampuni ya Dosam kutambulika kimataifa.

Hamza aliishia kupitia nyaraka ambayo alikuwa amepewa na  mrembo huyo   na kuanza kuisoma kwa umakini  lakini  ndani ya dakika tano tu alikuwa tayari ashapitiwa na usingizi.

Siku iliofuata Hamza alionekana katika moja ya mgahawa ambao alipendelea kula  na alijipatia chapati zake tatu , maharage pamoja na  juisi  na mara baada ya kumaliza  alianza safari ya  kuelekea  kwenye ajira yake  kwa mara ya kwanza.

Hakuwa na mavazi yale ya jana ,  jana aliyachafua na hakufua hivyo  hakujisumbua kubadilisha , mavazi yake  ambayo yamemkaa vizuri lakini yamechakaa ndio aliamua kuvaa.

Kwa kutumia mwendokasi aliweza kufanikiwa kufika kituo kilichokuwa kikipakana na  jengo la Dosam Tower  sehemu ambayo alikuwa na miadi na mrembo Regina.

Katika jengo hilo ukiachana na  kuwa   na makao makuu ya baadhi ya kampuni katika floor za chini lakini chini kulikuwa na maduka makubwa ya  luxury brand  kama vile Chanell , Luis Vuiton  na zaidi, juu kabisa kulikuwa na migahawa ya kimataifa kama vile Italian Restaurant , French Restaurant  na Chiniese , ni sehemu ambazo Hamza asingeweza kutia mguu.

Saa nne kamili juu ya  alama  simu ya  Hamza iliita na aliekuwa akipiga ni Regina na mara baada ya kumsikia  Hamza amefika tayari  alijikuta akipata  ahueni.

Katika maegesho ya magari  B2 , Hamza hakuweza kuona  ile gari ya Maserati ambayo mrembo Regina  alitumia jana bali kulikuwa na gari  aina ya Lexus SUV.

Kama bosi wa kampuni hio kubwa sio swala la kushangaa kubadilisha  badilisha magari  hivyo haikumfanya  Hamza kushangaa.

Mara baada ya kukaribia gari ile ,  kioo cha mbele kilishushwa  na mwanamke mrembo sana alievalia  gauni  lenye  kola ya bluu alionekana , gauni lililoacha mikono yake milaini  wazi, huku akizidi kupendeza kwa mkufu wa madini ya dhahabu  uliokuwa shingoni kwake., muonekano wake ulikuwa ni wa kitulivu mno  kuliko ule wa jana.

“Goodmorning Madam, wapi  tunaelekea?”Alisalimia   Hamza huku  akiwa na muonekano wa kizembe lakini hata hivyo hakuacha kutoa tabasamu.

“Ingia kwenye  gari kwanza”Aliongea.

“Oh! , sawa boss”

Mara baada ya Hamza kuingia,  Regina alimchunguza kwa dakika kadhaa , huku akijiambia huyu  jana alifika akiwa amependeza lakini  leo anaonekana  wa kawaida , kuizoea kazi kabla hata ya kuanza.

“Vua nguo  zako”

Kauli ile  ilimshitua  Hamza na kumwangalia mwanamke huyo kama anamaanisha , lakini  hakukuonekana na utani.

“Madam!, ijapokuwa urembo wako ni wa viwango  vya juu na pia  tuna mahusiano ya kikazi , siwezi kuwa mrahisi namna hio , naomba ufikirie mara mbili , siamini kama wewe ni mtu mwepesi hivyo pia”Aliongea Hamza.

“Unaongea ujinga  gani?” Mwanamke huyo alionekana kukunja sura  na kujiambia mbona   anakuwa na mawazo ya aina hio  , lakini hata hivyo hakujali  na alipitisha mkono nyuma ya gari na kutoa   mfuko na kumpatia  Hamza.

“Ninachomaanisha ni wewe kubadilisha ,  ndani ya hili jengo huwezi kuingia ukiwa na  hayo mavazi”

“Ah , sasa si ungeongea hivyo   mapema , angalau nimepata ahueni …”Aliongea  Hamza huku akijifanyisha  kupumua  kwa nguvu , alijua  sasa  ndio maana  alikuwa amebadilisha  gari na kuja na kubwa kumbe malengo ilikuwa ni kumpa nafasi    ya kubadili mavazi yake.

“Unamaanisha nini kuongea hivyo?”Aliuliza Regina  huku akionekana kukosa utulivu , hata kama kitu kitatokea ndani ya hilo gari  yeye ndio ambae  atapata zaidi hasara kuliko  Hamza , maana alijua kama mwanamke mrembo  hakuna wa kumkataa , lakini ajabu yake  Hamza ndio anajiona  atapata hasara.

“Hamna tu  , nilikuwa natania,  nitabadilisha”Aliongea Hamza huku akicheka.

Hamza sio kama hakuwa  akielewa  ni kwamba tu alikuwa akitafuta  nafasi ya kumfanya  bosi wake amzoee haraka ili asiwe na wasiwasi na maigizo yao  yasigundulike , hivyo kuwa mcheshi kama hivyo ilikuwa ni  mbinu ya kuweka sawa mazingira yake ya kazi.

Sasa cha ajabu Hamza alivua shati lake palepale  na  mara baada ya Regina kuona tukio hilo aligeuka haraka kuangalia pembeni  huku wakati huo akipata hisia mbaya   kwa kujiambia mbona ni kama  huyu mwanaume  sio  muwazi kama ilivyokuwa jana kwenye usaili.

Yaani Hamza wa jana alikuwa mpole na muwazi na ndio kilichomvutia , lakini wa  muda huo aliionekana kama muhini fani hivi.

Lakini hata hivyo asingeweza  kubadilisha mawazo , kwani kama ni mkataba umekwisha kusaini  na pili hata kama atafute mtu  wa kufanya maigizo asingepata  mtu mwenye muonekano kama wa  Hamza , muonekano wa kitanashati , alipenda sana namna ambavyo  Hamza alichanganya rangi na kuona ingefaa sana  kufanya maigizo.

Ndani ya dakika chache  tu Hamza aliweza  kumaliza kubadili mavazi yake yote  ikiwemo shati na suruali ,  alikuwa amevalia shati la  brand ya Givenchy  na suruali yake , Mkanda  wa  ngozi brand ya Mont Blanc ulioendana na viatu  vya ngozi ya Brown brand ya Ferragamo.

Mavazi yote kuanzia viatu mpaka juu iligharimu zaidi ya  milioni therathini  na  kwa jinsi alivyokuwa amependeza  iliendana vyema na ule msemo wa kizungu wa ‘Clothes make the man’  maana ndani ya dakika chache  tu Hamza alikuwa ni mtu mwingine kabisa.

“Looks fine”Aliongea  Regina kwa kingereza  huku akijivunia kwa namna  anavyojua  kuchagua.

Hamza aliweka nguo zake alizokuja nazo kwenye  ule mfuko  na kisha akatupia nyuma.

“Miss  wapi tunaelekea sasa?”

“Kukutana  na wazazi wangu”Aliongea  kikawaida kabisa lakini kwa Hamza  alibung’aa akiwa  ni kama hajasikia vizuri.

“Aisee naona mambo yanaenda haraka haraka sana , vipi  napaswa kubeba zawadi   au kitu chochote , naona sio vizuri kwenda  kukutana na wazazi wako mikono mitupu”

“Haina haja ,,, hata hivyo  unakutana nao leo  tu  na  haijalishi kama utakutana nao  siku za mbeleni , ninachotaka   ni wao kujua nimepata boyfriend basi”Aliongea na Hamza alitingisha kichwa kumuelewa.

“Halafu  usiniite madam , unaweza kuniita kivingine”

“Kama   ni hivyo unaonaje nikikuita , Babe Regi , au Darling Regina , Mrs Hamza, Sweatheart..”Aliongea Hamza huku akicheka.

“Hey! Inatosha”Alibweka  huku  mrembo huyo  akizidi  kuona  Hamza  jana alikuwa  akijifanyisha  muigizaji  na sio kama alivyokuwa akimdhania.

“Huyu mtu huu  ni ucheshi  au  ni kukosa aibu , mbona jana hakuwa hivi?”Aliwaza Regina.

“Niite Regina tu  inatosha”Aliongea  na kisha palepale akatoka nje ya gari na kuongoza njia  kuzielekea lift.

Mara baada ya kuingia kwenye lift  Hamza palepale alimshika mkono  Regina.

“Unafanya nini?”

Regina alionekana kutetemeka ni kama vile  amepigwa na shoti , alitaka kuvuta mkono wake lakini  Hamza alionekana kuushika vizuri.

“Regi nipo  kazini ,  unadhani tutaweza kuwadanganya wazazi wako kama tusipoonyesha  vitendo”

“Sawa lakini , Mkataba  unakutaka kuomba  ruhusa kwanza”Aliongea huku akizidi kuwa kauzu.

“Kama ni  hivyo unadhani ni sawa tukiachiana?”Swali hilo lilimfanya  Regina kukosa neno , alijua fika kama kweli kusipokuwa na kitendo  hata cha kushikana mikono mbele ya wazazi wake itaibua wasiwasi.

“Okey , tunaweza kushikana mikono lakini…”

“Haha… Regii   unaona sasa … hii ni kama  unavyoingia  kwenye  basi  kwanza na baada ya hapo ndio unapewa tiketi ..”

“Nimekuambia uniite  Regina , acha kufupisha”

“Oh  sawa  Regi”Aliongea  Hamza na dakika ambayo  mrembo huyo alitaka kuongea alikosa neno.

Ndani   ya lift hio walikuwa wawili tu na kumfanya Hamza kuweza kunusa harufu nzuri ya marashi.

Katika kazi ambazo  amefanya  hio ni moja ya Ajira ambayo aliona   ni nzuri na ya kuburudisha.

“Endelea  kusogeza pua  zako  karibu , utashitukia ngumi”Aliongea Regina mara baada ya kuona  Hamza ni kama anasogeza uso wake  karibu zaidi  na  alikosa uvumilivu.

“Regi , haina  haja ya kukasirika , hii  ni kazi kama kazi zingine  na ili ifanyike kitaalamu  unapaswa kutoa ushirikiano , hivyo kukusogelea karibu ni sehemu ya kazi , wewe unaonaje?”Aliongea  Hamza , ule muonekano wa kizembe hakuwa nao tena.

“Niseme kweli  tu , jana nadhani   sikuwa  na umakini , sikuwaza kama utaweza kubadilika ndani ya muda mfupi na kuwa   mwanaume  mwenye  aina hii ya tabia ,  nikutahadharishe tu usije ukaona  una uwezo wa kufanya chochote ukisingizia kazi ,  leo sijaja tu na bodigadi wangu  la sivyo  ungejutia”Mara baada ya kauli   Hamza alisogea mbali kidogo.

******

Jasusi mstaafu  Amosi Masekela  aliingia ofisini saa nne na nusu  huku akionekana ni mwenye uchomvu mkubwa  huku usoni akiwa na viashiria vya michubuko  na  kuvimba  uso.

Kwa jinsi ambavyo alikuwa akijisikia  asingeweza kufika ofisini kwa namna yoyote ile , ila  ilimradhimu kufika kutokana na Chriss kumsisitizia kuwepo  ofisini saa tano kamili wakati bahasha ikiletwa ofisini kwake , nguvu ya pesa na shauku ya kazi ambayo anakwenda kufanya ndio ilimpa hamasa ya kujitahidi kuamka.

Wakati anaingia vijana wake walikuwa  tayari wapo ndani ya  eneo la  kazi  na hata wao pia walishangaa kumuona bosi wao akiwa na michubuko  pamoja na  nundu usoni.

Amosi  baada ya kupita mapokezi aliwapa ishara  wale vijana kumfuata  kwenye ofisi  yake na kisha akapita.

Amosi Masekela  alikuwa  akifanya kazi kama mkopeshaji , alikuwa akikopesha  watu kiasi flani cha pesa na kisha  kurudisha  kwa riba flani ndani ya muda  anaokubaliana na wateja wake ,  ofisi yake ilikuwa ni kama benki  isio rasmi lakini iliosajiliwa kufanya biashara hio.

Alikuwa na uwezo wa kukopesha mpaka bilioni moja ndani ya ofisi hio  kwa masharti nafuu kabisa.

Lakini yote hayo yanawezekana kwa kuaminika kwamba  alikuwa akifanya kazi chini ya bosi mwingine , yaani ofisi hio  haikuwa  ya kwake kabisa  bali yeye ni kama msimamizi mkuu.

Sasa aina yake ya ukopeshaji kwasababu ilikuwa  ikitofautiana na wakopeshaji wengine kwa mfano kuweka  dhamana ya kitu fulani alijikuta akifanya kazi ya ziada kudai pesa kwa nguvu kwa wale ambao hawakuwa wakilipa ndio maana akaajili  watu wa kumsaidia kazi hio  na sasa ndio vijana   kama Chongolo  na wenzake.

Kabla ya Masekela kuanza kazi hio iliaminika alikuwa ni mwana kitengo  ambae  aliachana na kazi hio na kuamua kujitegemea ndio maana  alivuma sana kwa jina la Jasusi mstaafu.

Sasa iwe kweli alikuwa ni mstaafu au  kuna kilichotokea  mpaka kuamka kwa uvumi huo lakini ukweli ambao upo  ni kwamba  Amosi alikuwa akiaminiwa na watu wazito wazito serikalini katika kazi ambazo zilihitaji akili ya utafiti   na ujasusi zaidi   na ndio kazi ambayo ilikuwa ikimlipa kwa  kiasi kikubwa na  angalau kuwa na maisha mazuri,vigogo wengi walikuwa wakimwita Hunting dog.

“Bosi  nini kimetokea , kwanini una michubuko na nundu usoni , tuambie ni fala gani kakufanyia hivyo tutaenda kumshikisha adabu”Aliongea Chongolo.

“Bosi  tupo  tayari kwenda kupambana wewe tutajie jina , ni radhi tufe  tukipambana kuliko  bosi wetu kuumia”Aliongea mwingine.

“Bosii…”Kijana wa tatu wa kundi hilo alitaka kuongea lakini  Amosi aliinua mkono kumzuia  na kisha aliangalia saa ukutani.

“Kazi niliowapa jana mmeishia wapi Chongolo?”Aliuliza  huku akiwa ameegeamia kiti chake   lakini swali lake  ni kama liliwafanya Chongolo kuanza kukosa kujiamini.

“Bosi  yule mtu  ni jini , sio wa kawaida mbele  ya macho yetu alitoweka”Aliongea  na kumfanya Amosi kukunja sura.

“Ndio maana mshaanza kuwa chawa asubuhi asubuhi , kumbe kazi hamkumfanya inavyostahili?”

“Bosi sio hivyo ,  alikaa sana ndani kwa yule demu  lakini wakati wa kutoka tulimuona  na tulianza kumfuatilia ,  wakati  tunafika  kwa Mzee Mashimo  hatukuweza kumuona tena mbele yetu”Aliongea Chongolo.

“Alikuwa akitembea?”

“Ndio bosi , alikuwa akitembea  na hiki ndio kilitufanya tuchanganyikiwe  na kuona ni  jini , anapotea vipi mbele yetu?”Aliongea  Kihedu na kumfanya Amosi kutafakari.

“Endeleeni kumfatilia  Eliza  kwa siri kama kawaida , picha  za kila siku zinahitajika juu ya kila kitu anachokifanya”

“Lakini bosi vipi kuhusu yule jamaa?”.

“Chongolo una akili  kweli wewe , kama mtu amewapotea mbele yenu mtaanzia wapi kumtafuta , kama atakuwa na mahusiano  na Eliza  ndio  namna nyepesi ya kumuona ,hakikisheni mnafanya hili kwa siri, hakikisheni  hamjitokezi mbele ya Eliza , sitaki kilichonitokea jana kijirudie  sawa?”

“Ah!, Nimekuelewa bosi , lakini unamaanisha nini kilichokutokea jana?”

“Kafanyeni kazi, muda wa kuongea na nyie umeisha”Aliongea  na kisha palepale alitoa bahasha kwenye  mfuko wa koti lake na kurushia mezani.

Chongolo alitabasamu na kisha kwa heshima aliinua bahasha ile na kisha akaaga  na wenzake wakaondoka.

Hio ndio kazi ya vijana hao, hawakuwa waajiriwa  wa Masekela Credit  and Loans bali walikuwa na kazi moja tu kudili  na watu ambao walikuwa wagumu kulipa pamoja na  baadhi ya kazi chafu ambazo Amosi hakutaka kujihusisha yeye mwenyewe kama bosi, ki ufupi Amosi kwa namna nyingine unaweza kumchukulia kama Loan Shark.

Baada ya Vijana hao kutoka ,  alionekana kukosa utulivu  mno na kila saa alikuwa akisubiria  muda  ufike ili kupokea bahasha alioahidiwa  na  Chriss.

“Bosi kuna mzigo umefika?”

“Ulete ofisini kwangu Bertha”

“Anasema anataka upokee mwenyewe  na kutia saini”Aliongea  mwanamke  wa mapokezi kupitia  simu ya meza.

Amosi mara baada ya kuambiwa hivyo hakutaka kuchelewa , kwa taratibi hizo alijua ni kile ambacho alikuwa akisubiria hivyo kwa haraka haraka aliienda mapekezi kupokea mzigo wake.

Aliekuwa ameleta mzigo huo alikuwa  ni kijana  mdogo   wa miaka kama ishirini na nne hivi ambae ni mfanyakazi wa Swift  Courier , kampuni ambayo ilikuwa chini ya  Chriss.

“Bosi nimepewa maelekezo kukufikishia huu mzigo wewe mwenyewe na kuupokea, niwe radhi kama nimekusumbua”

“Unatii maagizo , haina haja ya  kukakamaa hivyo”Aliongea Amosi huku akilazimisha tabasamu na kupokea mzigo  ule na kisha akasaini.

“Chriss anaonekana  kuwa makini  mno , sio kwa ufungashaji huu”Aliwaza  Amosi wakati akiondoka mapokezi akiwa na mzigo wake.

Mara baada ya kukaa kwenye kiti  , ujumbe  wa meseji uliingia  na aliona  ni kutoka kwa Chriss  na kumfanya aufungue haraka.

“Napiga baada ya dakika kumi”Meseji iliingia na Amosi alielewa alichokuwa akimaanisha Chriss.

Mzigo uliofika ulikuwa ni Limu A4  na mara baada ya kuuweka mezani alitoa ile  katarasi ya juu na kisha akaanza kuchangua karatasi moja baada ya nyingine na ile anafika katikati aliweza kukutana na  karatasi ambayo imechapishwa.

Amosi  alikuwa na shauku ,  usiri wa kazi hio  ulimfanya kuzidi kujawa  na shauku ya kutaka kujua ni  kipi ambacho Chriss anahitaji  kifanyiwe kazi ambacho kina malipo makubwa hivyo.

 Kabla ya kusoma karatasi ile aliendelea kuangalia vitu vingine na aliweza kuona  picha   ya mwanamke mrembo , ijapokuwa picha hio ilionekana kuchakaa lakini bado  mwanamke  aliekuwa katika picha hio alikuwa akionekana vizuri.

Picha hio  ilimfanya Amosi kuiangalia kwa muda mrefu , ni kama alikuwa akijaribu kukumbuka ni mahali gani aliweza kuiona   lakini licha ya kusumbua akili yake  hakuweza kukumbuka mara moja.

Alihamia kwenye  ile karatasi  na kuanza kusoma  na sasa anafahamu  mtu aliekuwa kwenye picha  jina  lake ni Naomi Lindsey mmarekani mweusi, mwimbaji  maarufu wa nyimbo za injili ambae  alifariki dunia  mwaka 1999 kwa mshituko wa Moyo wakati akiwa  katika tamasha  huko jijini Milani Italia.

Mwanzo  mwa  taarifa hio   inamshangaza Amosi na kumfanya  azidi kusoma mbele , lakini anajikuta akipagawa zaidi mara baada ya kugundua  ambae yupo  kwenye picha anafahamika kwa majina mawili , anafahamika kwa jina  la Naomi Lindsey kutoka Marekani  lakini vilevile anafahamika kwa jina la  Rosemary Macha  raia wa Tanzania.

Amosi  kabla ya kuendelea  kusoma  anajiuliza inamaana Rosemary na Naomi ni watu wawili wanaofanana au ni mtu mmoja mwenye majina mawili tofauti.

Amosi aliendelea kusoma karatasi ile  kwa umakini mkubwa ili kujua ni kipi ambacho anapaswa kufanya  na anakuja kugundua  kazi iliokuwa ikihitajika ni kuunganisha historia  ya Rosemary Macha na  Naomi Lindsey.

“Krii.. Krii..!!”

Simu yake iliita  na kwa namna ambavyo alikuwa ameweka  mwito wenye nguvu ni kama alikuwa na ugonjwa wa masikio , ila  mwenyewe ukimuuliza kwanini mwito wa simu wa namna hio atakwambia mwito wa simu yake  ni  wa fursa na kwasababu  hataki kukosa fursa anakaa kimachale.

“Jasusi  nadhani umesoma bahasha?”

“Ndio lakini mbona  kuna  mkanganyiko wa hii kazi?”

“Ndio maana nimepiga simu Jasusi , siwezi kuweka wazi kwa kila kitu lakini kazi  unayotakiwa kufanya ni kumtafuta huyo Mtanzania kwanza na baada ya hapo  tafuta  uhusiano  na Mmarekani”

“Hii taarifa haina mwelekeo wowote , kama nitaanza kutafuta  tanzania nzima itachukua muda , nahitaji  angalu mwanga wa  uelekeo kuanza kazi yangu”Aliongea Amosi.

“Jasusi kazi hio  umepewa wewe kwasababu ndio mtu  pekee ambae unajua pa kuanzia , ‘hebu angalia hio picha vizuri na vuta kumbukumbu’ hio ndio kauli ambayo nimeambiwa  nikufikishie kama ilivyo”

“Kwahio kazi yangu ni kumtafuta tu huyu mwannamke?”Aliongea Amosi  ambae kwa namna moja hata yeye mwenyewe ni kama  alikuwa katika hali ya kujiuliza ,  kuna kitu kilikuwa kikimwambia kabisa picha hio alishawahi kuiona mahali kama sio mtu  kabisa wa kwenye picha.

Lakini kwa wakati mmoja anashanga  kuona kwamba waliompatia kazi Chriss ni kama pia wanamfahamu na yeye , hali ya shauku ilizidi kuongezeka.

“Jasusi najua una maswali mengi , mimi pia nina maswali mengi lakini kwasasa ninachojali ni pesa itakayopatikana  juu ya  kukamilika kwa kazi hio, Narudia ninachojali ni pesa, hivyo  maswali uliokuwa nayo  mimi sijauliza”Aliongea  Chriss  na kisha simu ikakatwa.

Amosi  alifikiria kidogo akiwa amekaa kwenye  meza  na kisha  aliinua ile picha kwa mara nyingine na kuiangalia.

“Huyu mwanamke kwenye picha nishawahi kumuona , lakini ni wapi na lini?”Aliendelea kujiuliza swali hilo  na  kuendelea kutafakari lakini kumbukumbu zake hazikumps bahati..

Dakika chache mbele Amosi alikata shauri , hakutaka tena kuendeea kukaa ofisini  na alitoka  isieleweke anaelekea wapi lakini kwa muonekano wake ni lazima hakuwa akielekea nyumbani, alikuwa na karatasi zile mkononi  lakini zikiwa zimehifadhiwa katika bahasha ya kaki.

 

Previoua Next