“Uimara ni kuyashinda yale ambayo hujayatarajia , uendelevu ni kuishi , lengo la kuwa imara ni kufanikiwa”-Jamais Cascio
SEHEMU YA 12.
Amosi alitaka kazi mpya ambayo amepatiwa kuifanyia kazi kwenda sawia bila ya kuwa na dosari, na ili hilo kufanikiwa hakutaka kuwa na watu ambao wanaweza kuhatarisha usalama wake.
Siku ya jana alichokipata akiwa nyumbani kwake hakikuwa kitu cha kawaida kabisa , watu waliokuja kumvamia na kumpa sulubu ya kipigo hawakuwa na huruma hata kidogo , kama sio kuomba sana kutojeruhiwa zaidi pengine siku hio asingeweza kuamka kabisa na kufika ofisini.
Mara baada ya kutoka katika ofisi yake baada ya kupokea bahasha katika akili yake kitu pekee kilichomjia ni kwenda kumalizana na Eliza mwanamke ambae ndio aliekuwa chanzo cha kupigika kwake na kumfanya kuonekana na nundu asubuhi hio.
Ijapokuwa kazi ya kumsumbua Eliza haikuwa matakwa yake bali ya bosi wake , lakini hakutaka hata kushauriana nae.
Alienda kusimamisha gari yake katika jengo la makao makuu ya kampuni ya Dosam na kisha kuelekea eneo la mapokezi na kueleza shida yake, lakini kwa kile ambacho kimetokea kwenye mitandao ilimfanya watu wa usalama wa eneo la mapokezi kutomruhusu moja kwa moja na aliitwa mkuu wa kitengo cha ulinzi.
Yonesi mwanamke mrembo na mkakamavu ndio aliekuwa kiongozi wa kitengo cha ulinzi wa kampuni ya Dosam lakini vilevile alikuwa mlinzi binafsi kwa bosi wa kampuni hio ya Dosam , yaani Regina Wilson.
“Mzee Amosi unafanya nini hapa baada ya kumdhalilisha mfanyakazi wa Dosam?”Aliuliza
Yones kikauzu mara baada ya kumfikia Mzee Amosi , kwa jinsi aivyotaja jina lake ni kama alikuwa akifahamiana nae.
“Mdogo wangu Yonesi bora umekuja wewe , nadhani tutaelewana kulingana na historia yetu”Aliongea Amosi na kumfanya Yonesi kumwangalia Amosi kwa macho yasiokuwa na hisia za aina yoyote , huku wakati mmoja akijiuliza nani kamshikisha adabu mpaka kuwa na manundu hayo usoni.
“Kitendo cha kufika hapa na kinachoendelea mitandaoni ni kuibua taharuki , umemdhalilisha Eliza na watu wakarekodi na kutuma mtandaoni , unadhani Eliza anajisikiaje , Mzee wewe ni mtu mzima na Eliza ni kama mwanao kwanini kwenda mbali vile?”Aliongea Yonesi huku akionyesha hasira.
Amosi na yeye alionekana kushangaa , hakuwa na habari ya tukio la jana kufahamika kwa watu wengi na kwa kauli ya Yonesi alijua lazima kuna mtu alirekodi, aliishia kutoa tusi la ndani akiwalaani Chongolo na wenzake kwa kutokuwa makini.
“Sio kama unavyofikiria Yonesi, ila unachoongea ni sahihi jana nilivuka mpaka na ndio maana nipo hapa , kumuomba Eliza msamaha kwa tukio la jana”
“Kwa kauli yako sidhani hata huo msamaha ni wa dhati , unaongea kwa namna ya amri ukitarajia kusamehwa mara moja , sitaki kumsemea Eliza juu ya kilichomtokea na kama atakuwa tayari kuonana na wewe nitaruhusu vinginevyo utaondoka”Aliongea kibabe na kumfanya Mzee Amosi kutabasamu.
“Nilidhani kufanya kazi chini ya watu wazito kutakubadilisha Yonesi , lakini naona upo vilevile , msichana wa shoka ambae huna utani hata kidogo , ukiendelea hivyo utakosa mume maisha yako yote, jilegeze kidogo mimba iingie”
“Ni kheri mimi ambae sijabadilika kuliko wewe ambae umegeuka kuwa mbwa usie na mmiliki , yoyote mwenye pesa unawinda kwa ajili yake, kwa tabia yako utazeeka ukiwa huna familia”Amosi hakuwa na familia , aliishi peke yake na alikuwa tayari ni mtu mzima na kauli ya Yonesi ilimgusa.
“Wote tuna malengo yanayofanana Yonesi , njia tu ndio tofauti, juu ya yote kuwa na familia na kutokuwa na familia sio sheria ni aina ya maisha ambayo mtu anachagua hivyo sioni tatizo, ushauri wangu ni wewe kubadilika kidogo au kutafuta mwanaume , jilegeze hata akupe mimba tu”Aliongea Amosi kwa kejeli.
Maneno yale yalimfanya hata yule mwanadada wa mapokezi kumfanya kukosa amani , maneno hayo yalionekana kuwa na ukweli , tabia ya ukakamavu ya Yonesi ilimfanya kuogopwa na wanaume wengi licha ya kwamba alikuwa mrembo.
Yonesi licha ya kauli ya Amosi kupiga kwenye mshono hakutaka kuruhusu hasira zake zimtawale na hakutaka kujibishana nae maana hata hivyo Amosi alikuwa mtu mzima kwake , hivyo alimpa ishara mtu wa dawati la mapokezi kuwasiliana na Eliza.
Yule mwanadada wa mapokezi mara baada ya kuongea kwa dakika kadhaa alirudisha jibu, Eliza hakuwa tayari kuonana na Amosi.
“Hey , mwambie sipo hapa kwa ubaya nataka kuomba msamaha”Aliongea .
“Samahani baba , nimemwambia hivyo?”Aliongea yule mwanadada kwa kipole lakini kwa chuki kidogo.
“Nadhani ushasikia jibu wewe baba, hapa ni eneo la kazi na sio sehemu ya kuomba msamaha hivyo unapaswa uondoke , aliekuadabisha jana na kukufanya uje kuomba msamaha amefanya vizuri , pengine akili ya ki utu uzima imekurudia”Aliongea Yonesi kwa chuki.
“Yonesi, ijapokuwa nishatoka jeshi la polisi muda mrefu haimaanishi cheo changu cha usenior kimekoma , unapaswa kuniheshimu pia”
“Heshima haiombwi , kama kweli unataka nikutambue kama mkubwa wangu basi ishi kama mkubwa wangu , acha kuwa mfano mbaya kwa jamii, hata kama umeamua kuwa mbwa wa wakubwa , jiwekee sheria zako za ki uwindaji”
“Asante kwa ushauri wako binti”Aliongea Amosi huku akikunja sura na palepale aligeuka na kuanza safari ya kutoka katika jengo hilo , alijua hakuwa na haja ya kulazimisha , isitoshe alikuja kuomba msamaha kwa ajili ya kujiepusha na marudio ya tukio la jana.
Amosi mara baada ya kutoka nje aliangalia upande wa kulia , ilikuwa ni kama alihakiksiha sura yake ikionekana katika moja ya gari iliokuwa imepaki mita kadhaa kutoka alipo na alitingisha kichwa na kisha akaingia ndani ya gari yake.
“Damn! Hisia zangu ziliniambia vizuri , yule kijana hakuwa wa kawaida , lakini inafikirisha kuwa na ukaribu na Eliza wa ghafla tu , hatujawahi kumuona wakiwa pamoja , jana ni siku ya kwanza, lakini imekuwaje akawahusisha Chatu kuja kunipa onyo?”Aliwaza Amosi kabla ya kuwasha gari, mtu aliekuwa akimzungumzia ni Hamza ambae aliwavurugia jana katika mpango wa kumlazimisha Eliza kulipa deni kupitia mwili wake.
Amosi alisifika kwa ubishi na ukiburi , kitendo cha kufika kwenye kampuni na kuomba msamaha ni dhahiri maji yalikuwa yamemfika shingoni , sio kwamba watu waliomshambulia jana hakuwa akiwajua , alikuwa akiwajua fika ndio maana hakuaka kuleta ubishi wa aina yoyote na kutii maagizo yao , Chatu ni kundi la wahalifu ambalo siku zote alihakikisha hatengenezi nalo uhasama, lakini jana ikawa siku yake ya kwanza kujiingiza katika uhasama na ili kuondoa uhasama huo alilazimika kuja kuomba msamaha mbele ya Eliza.
Uwepo wa kundi la kihalifu la Chatu katika nchi yenye ulinzi mkali wa kipolisi katiika kupambana na uhalifu kama Tanzania ilikuwa ni swala la kushangaza(mystery).
Baadhi ya watu wanasema kundi la chatu ni jina jipya la kundi la kihalifu ambalo lilikuwa likisumbua sana taifa kwa muda wa miaka mingi , kundi ambalo lilifahamika kwa jina la Panya Road.
Wengine wanasema kundi la Chatu linaendelea kushamiri ndani ya Tanzania kwasababu ya baraka zote kutoka serikalini.
Ki ufupi ni kwamba uwepo wa kundi la Chatu ndani ya Tanzania ni moja wapo ya habari za kusisimua mno na habari zilizidi kusisimua mara baada ya moja ya mgombea wa uraisi kupitia chama cha wanaopinga kusema kwamba hatua ya kwanza akiingia madarakani ni kutokomeza kundi hilo la kihalifu ambalo linafadhiliwa na serikali.
Mgombea huyo wa uchaguzi anaenda mbali kwa kuliunganisha kundi hilo na vijana watekaji na wezi waliokuwa wakijiita Panya Road.
Ki ufupi ni kwamba katika kipindi hiki ambacho ni cha uchagunzi nchini Tanzania kila mgombea alitafuta namna ya kujipatia pointi za kujinadi mbele ya wananchi.
“Bosi tuendelee kumfuatilia?”Aliuliza kijana aliekuwa ameshikilia usukani , huku pembeni yake kukiwa na kijana mwingine ambae alikuwa amevaa hat pamoja na miwanin ya jua.
“Kazi yetu ilikuwa ni kuhakikisha kama amefika na kuomba msamaha , lakini ngoja niongee na bosi Lau kama ana maagizo mengine”Aliongea yule bwana na palepale alipangusa simu yake , alikuwa amevalia glovusi nyeusi.
“Mkuu Lau , Jasusi mstaafu ameonekana akiingia ndani ya jengo la makao makuu ya kampuni ya Dosama , amekaa kwa dakika therathini na kutoka , inaonekana onyo limefanya kazi , kuna maagizo mengine tunapaswa kufuata?”
“Kazi nzuri Bwalia , mnaweza kurudi chimbo”
“Sawa mkuu”Aliongea Bwalia na palepale simu ilikatwa na akampa ishara dereva wa forester hio kuondoa gari maeneo hayo kuelekea Chimbo.
Upande wa Kijichi , mrembo Dina aliekuwa amvalia suti ya rangi nyeupe alikuwa amekaa kwenye sofa akiwa amekunja nne akipata mvinyo wake taratibu huku akifurahia kiyoyozi kinachomwepushia na adha ya joto la jiji la Dar.
Macho yake yote yalikuwa katika runinga akiangalia kampeni za mgombea kiti cha uraisi kupitia chama cha wanaopinga.
“Hatuwezi kukubali kabisa nchi hii kuendeshwa kihuni , tunapaswa kukemea hili kwa nguvu zote , njia sahihi ya sauti zetu kusikika ni kupitia kura zetu
, sisi ndio waamuzi wa mwisho wa namna tunavyotaka nchi hii iendeshwe , haiwezekani Wapenda madaraka wafadhili kundi la Panya Road na sisi tuone ni sawa , haiwezekani kabisa wahalifu waliotuulia ndugu zetu waishi chini ya mwamvuli ya viongozi wa chama cha wapenda madaraka tofauti na kuwaadhibu kwa makosa yao , hii ni dharau kwa sisi wananchi , na dharau hizi zimefika mwisho , iwe ni Chatu , Cobra au panya Road lao ni moja , hao ni wahalifu ambao wanapaswa kuwajibishwa mbele ya sheria na hakuna namna ya hili kuwezekana bila ya nyie wenye nchi kutukabidhi dhamana hii , nipatieni kura muone ni kwa namna gani nitawajibisha kundi lote la wahalifu hapa nchini , haitakuwa kwa machatu tu , kunguni wote wanyonya haki zetu watawajibishwa, huu ni wakati wa maamuzi makubwa… na Mimi Msemakweli nitumieni kama siraha…”
“Bosi..!!!”
Sauti ya Lau ndio iliomgutusha mrembo Dina ambae alionekana kusikiliza kampeni ya mgombea wa chama cha Wakosa madaraka , licha ya kwamba alionekana kusikiliza kwa umakini lakini moyoni mwake ni kama alikuwa akidharau kile ambacho Msemakweli alikuwa akizungumza.
“Msemakweli , unaweza ukawa wewe raisi lakini huwezi kuiondoa Chatu katika mfumo , hujasoma faili letu bado ndio maaa, ni haki yako kuongea chochote kujipatia kura”Hayo ndio yalikuwa mawazo ya Dina.
“Boss kazi ulionipatia imekamilika , hizi ndio taarifa za mwanamke ambae Bro Hamza anamlinda”Aliongea Lawrence na kukabidhi kishikwambi kwa mrembo Dina.
Picha mbalimbali za mrembo Eliza zilionekana katika skrini ya kishikwambi hicho na zilimfanya Eliza kukunja sura kiasi sana na kurudi katika hali yake ya kawaida.
Kwa namna moja alionyesha kukasirika na kushukuru kwa wakati mmoja
“Kuna taarifa nyigine tofauti na hizi picha?”
“Ndio bosi , huyu msichana ni Katibu muhtasi na msaidizi binafsi wa bosi wa kampuni ya Dosam , anaitwa Eliza Msuya”
“Imekuwaje mpaka akajiingiza katika mgogoro na Amosi?”
“Alikopa kiasi cha pesa kutoka kwa Amosi kwa ajili ya matibabu ya mama yake ambae alikuwa na shida ya moyo, aliweza kulipa kiasi chote pamoja na nusu ya riba , lakini nusu iliobaki hakushindwa kuilipa ndani ya muda hivyo deni lake kuongezeka ndio maana Amosi alikuwa akimlazimisha kulipa riba iliobaki”Aliongea Lawrence na kumfanya mrembo Dina kufikiria kwa dakika kadhaa.
“Vipi kuhusu yeye na Hamza walivyokutana?”
“Bosi sijajua walivokutana , lakini kwa maelezo ya taarifa vijana waliyokusanya Bro jana alienda Lotus apartment kwa ajili ya kazi yake ya ufundi na hapo ndipo alipotokea kumsaidia Eliza kutoka katika mikono ya Amosi , kulingana na mashuhuda wa tukio wanasema ni mara yao ya kwanza kumuona akiwa na Eliza , kwa mtazamo wangu kuna uwezekano Bro aliamua kumsaidia tu”Aliongea na kumfanya Dina kutafakari.
“Madam sidhani kuna haja ya kuwa na wasiwasi , huyu ni wa kawaida sana kwa Bro kulingananisha na wewe”
“Unaongea ambacho sijataka kusikia Lau, ila asante , unaweza kwenda sasa , hakikisha vijana hawasababishi matatizo, wala kufanya vitu bila maagizo yangu”
“Sawa bosi , najua hiki ni kipindi muhimu kwetu, nitakuwa makini”Aliongea na kisha alimuacha Dina akiwa peke yake.
Dina alikuwa na wivu kwa kitendo cha Hamza kuonyesha kumsaidia mwanamke Eliza, katika hali kama hio aliona pengine ni bora kutokuwa na uwezo wa kujilinda pengine Hamza angeongeza umakini wake juu yake.
Lakini licha ya hivyo hakuwa na hofu , baada ya kumuona Eliza hali yake ilitulia na kujiambia nafasi bado anayo.
*****
Sehemu ambayo Hamza alikuwa akiishi haikuwa na uwezo wa kufika gari , mara baada ya kufika barabarani ilibidi asimamishe na yeye pamoja na Yonesi walianza kutembea kuingia katika uchochoro.
Yonesi licha ya kazi yake ya ulinzi kuonekana sio ya hadhi kubwa lakini ukweli ni kwamba alikuwa ni mwanumke ambae familia yake haikuwa vibaya ki uchumi, hivyo mazingira ya maeneo kama hayo ambayo Hamza alikuwa akiishi hajawahi fika kabisa licha ya kuishi mjini Dar Es salaam.
Sio kwamba hakuwahi kuingia ktika uchochoro kabisa , lakini mazingira ya anapo ishi Hamza yalikuwa mabaya mno , kulikuwa na harufu kali ya maji machafu mtaroni.
Hamza aliweza kuona mabadliko ya Yonesi lakini hakutaka kutia neno ,isitoshe alijua mazingira hayo yalikuwa ya kimasikini mno na kwa mwanamke wa aina yake lazima akose utulivu.
Kitu kumoja pekee ambacho kilimfanya Hamza kutokumzingaria Yonesi ni namna watu wa eneo hilo walivyokuwa wakimwangalia , mwanzoni alijua pengine ni kwasababu ya kuja na Yonesi mwanamke mrembo na mkakamavu lakini baadae aligundua hio sio sababu.
Baada ya kutembea kwa umbali wa kilomita moja hatimae aliweza kufika katika sehemu ambayo amepanga.
“Huku mbali hivi , mizigo yako tunabeba vipi?”Aliuliza Yonesi ambae alionekana kabisa kukosa utulivu , macho ya watu yalivyokuwa yakimwangalia ni kama alielewa ni kipi ambacho walikuwa wakifikiria , ilionekana ni kama mwanamke wa kishua ambae ameletwa geto uswahilini, mambo ambayo yanaonekana sana kwenye simulizi au filamu huku kwenye uhalisia yakiwa ni nadra.
“Sina mizigo mingi ya kubeba , nachukua begi langu tu , vingine nitamwachia mwenye nyumba”Aliongea Hamza huku akiongeza umakini wa mazingira.
Eneo ambalo alikuwa akiishi halikuwa na watu wengi sana , ni kwasababu lilikuwa ndani ndani na baadhi ya watu wanaoishi huko wapo katika kazi zao za kujitafutia kipato , walikuwa watu wachache sana ambao walikuwa wakionekana kupita pita.
“Afande Chumba changu ni kile pale , shika ufunguo huu hapa nakuja”Aliongea Hamza huku akinyooshea mlango wa chumba chake cha uwani.
“Unanipa ufunguo wa nini , katoe nguo zako tuondoke”Aliongea huku akionyesha kukasirika.
“Tutapoteza muda sasa , wewe tangulia ndani , mimi naenda kumuaga mama mwenye nyumba”Aliongea Hamza na hakusubiri jibu alimkabidhi mkononi Yonesi ule ufunguo na kisha alikimbia kuelekea upande mwingine huku akiwa na tabasamu usoni.
Yonesi aliishia kuangalia ile ufunguo na kisha akageuza macho yake kwa Hamza ambae alikuwa akitokomea upande wa pili na aliishia kutingisha kichwa, alijishauri kutokwenda kufungua kile chumba lakini kwa namna flani alionekana hakutaka kuendelea kusimama hapo hata kwa sekunde kutokana na kukosa utulivu.
“Kuna watu wanaishi kwenye mazingira magumu sana”Alijiongelesha kisha alipiga hatua kusogelea chumba cha Hamza.
Wakati huo kuna watu kutoka nyumba za majirani ambao walikuwa wakimwangalia Yonesi kwa macho ya kumshangaa.
Yonesi alijua alikuwa akiangaliwa kwasababu alikuwa mgeni , lakini haikuwa hivyo na alifahamu hivyo mara baada ya kusogelea mlango wa chumba cha Hamza , mlango wa chumba hicho ulionekana ulikuwa wazi na umerudishiwa tu kidogo.
Kilichomfanya kujua mlango ulikuwa wazi ni ile kunesa nesa kwake , ikiwa ni kama vile ulikuwa ukipeperushwa na upepo na kwasababu alikuwa na ufunguo wa Hamza mkononi na aina ya kitasa cha mlango alijua lazima kuna watu waliokuwa ndani na hio ni kutokana na watu walivyokuwa wakimwangalia kwa wasiwasi, ni kama walikuwa wakitaka kumwambia asiingie.
Yonesi aliongeza umakini , akili yake ilikuwa ikifanya kazi kwa spidi kubwa mno na kwa haraka haraka alishainusa hatari.
“Mshenzi sana , alijua kuna hatari nini ndio maana akaniachia huu msala?”Aliwaza Yonesi na kitendo cha kuushika mlango tu kuusukuma ulifunguliwa kwa ndani na alichomoka mtu kama mshale akitanguliza mguu wa kulia kumlenga Yonesi , lakini ilikuwa ni kama kitendo kile Yonesi alikuwa amekitegemea kwani alisogea pembeni kidogo na mara baada ya mtu yule kumfikia usawa wake alizungusha mguu wa kushoto na kumgonga eneo la kigoti.
“Puuh!!”
Yule mtu alidondoka chini kama furushi huku akigugumia maumivu, lakini hakupoa kwani palepale alichomoka mtu mwingine akiwa ameshikilia rungu na kutaka kumlenga nalo Yonesi, lakini muda ule Yonesi alionyesha kwanini alikuwa mlinzi ambae aliaminiwa mpaka kumlinda mtu mzito kama Regina.
Kijana yule kitendo cha kumsogelea na ile rungu ni kama Yonesi aliitega na kuifanya ipite kwapani na kisha alimvuta yule mtu kwake na ilikuwa pigo moja la karate lililopiga shingoni na kuwafanya watu wote wawili kuwa chini, mmoja akiwa hajitambui mwingine akiwa anaungulia maumivu.
Yonesi alimtaka yule ambae alikuwa akiugulia maumivu ili kumhoji, watu wote wawili walionekana kuwa vijana katika sare za jeshi la polisi , lakini kwa uzoefu wake alijua hao sio polisi hata kidogo.
“Nyie ni nani , nani kawatuma?”Aliongea Yonesi kibabe mara baada ya kumsimamisha yule ambae alikuwa akijitahidi kusimama baada ya kutenguliwa mguu.
“Sisi ni…. Sisi niii..”Kabla hata hajamaliza kuongea alikuwa tayari ashapoteza fahamu, jambo ambalo lilimshangaza Yonesi , hakuwa amempiga kiasi cha kupoteza fahamu.
Muda uleule Hamza aliweza kurudi na mara baada ya kukutana na Yonesi kumaliza kazi yake alitoa tabasamu huku akitafuna karanga.
“Upewe maua yako mwanajeshi”Aliongea Hamza mara baada ya kumfikia Yonesi.
“Wewe mwanaume muoga sana , ulishajua kuna hatari ndio maana ukaniachia ufunguo”Aliongea Yonesi huku akimwangalia Hamza kwa macho makali.
“Me najuaje , nimekuaga naenda kuongea na mama mwenye nyumba na ndio nimerudi”Aliongea na kumfanya Yonesi kukunja sura na kisha alimwachia yule kijana aliepoteza fahamu kwa kumuweka chini na kuanza kuangalia baadhi ya watu wachache waliokuwa waishangaa.
“Una wafahamu?”
“Siwafahamu , nadhani ndio hatari aliokuwa akizungumia Regina , mtu kama mimi masikini sinaga maadui”Aliongea Hamza.
Kauli yake ilikuwa sahihi,watu hao waliokuja kuvamia walionekana kutokuwa na mafunzo yoyote ya kivamizi ni kama vibaka tu ambao wameagizwa kuja kumshambulia , lakini hata hivyo aliona hakuna uwezekano wa James mchumba wa Regina kutuma watu hao , maana ndio kwanza amefahamiana nae leo.
“Kwahio tunawafanyaje , tupigie polisi waje wawachukue?”
“Haina haja ya polisi , ni kujiingiza matatizoni tu na maswali mengi”
“Sema unaogopa polisi , huna lolote”
“Hey , kwanini niogope polisi wakati sina kosa , sitaki kupoteza muda mwingi hapa”Aliongea Hamza na kisha aliingia ndani kwake na kuanza kutafuta kitu cha kubeba na vingine vya kuacha.
Upande wa Yonesi aliishia kuzungusha macho katika chumba cha Hamza na kutokana na namna maisha yake yalivyokuwa ya kimasikini aliishia kumuonea huruma.
“Hatimae naona kitu cha thamani”Aliongea Yonesi mara baada ya Hamza kuchoropoa kiboksi kidogo ambacho mara baada ya kukifungua I kulionekana kitu kama mkufu wa dhahabu uliofungwa na medali ya Dhahabu , pamoja na mchoro usioelezeka.
“Upo sahihi , hiki ndio kitu cha thamani nilichokuwa nacho”Aliongea Hamza na kisha alirudisha medali ile kwenye kiboksi na kutumbukiza kwenye begi.
“Unatabasamu nini sasa , malizia tuondoke”
“Sawa sawa Kapteni”
Mara baada ya kufungasha kila kitu chake na kuacha alivyotaka kuacha hatimae walitoka na Hamza aliwamwagia wale wavamizi na maji ili wazinduke na kisha wakaondoka zao huku wakiacha watu nyuma wakiongea kila neno na kumshangaa Yonesi.
Egret ni mtaa uliokuwa ukipatikana kilomita kumi kutoka feri kigamboni , ndani ya mtaa huo ni majumba makubwa ya kifahari tu ndio yalikuwa yamejengwa , ulikuwa ni mtaa tulivu ambao wanaoishia hapo ni wale wenye ukwasi mkubwa wa pesa.
Kilichopendezesha zaidi mtaa huo ni mazingira yake ya kijani kibichi na upepo mwingi kutoka baharini.
Sasa Regina alikuwa akiishi ndani ya mtaa huuu katika nyumba au kasri namba saba , na kuishi katika namba hio ilikuwa ikioneisha ni kwa namna gani utajiri wake ulikuwa mkubwa.
Mara baada ya gari kuruhusiwa kuingia ndani ya geti Yonesi aliendesha na kwenda kupaki katika nyumba anaoyoishi Regina , nyumba yao haikuwa imezungukwa na geti , ndani ya eneo lote la Egret kilichoteganisha nyumba na nyumba ni uzio na sio ukuta na hiii imefanya eneo hilo liwe la kupendeza mno , ilikuwa ni kama vile ni Ulaya.
Mara baada ya kusimamihsa gari mwanamke mama hivi mwenye umri wa miaka kama arobaini kwenda hamsini hivi alitoka, licha ya kuvaa kikawaida sana lakini afya yake ilikuwa nzuri.
“Kapteni Yonesi , karibu ndani hata upate maji tu”Aliongea yule mama mara baada ya Yonesi kusalimia.
“Aunt Mari , kwa leo sitokunywa maji , napaswa kurudi haraka kazini”Aliongea Yonesi huku akitabasamu.
“Kama kawaida yako,mtu mwenye haraka zako”Aliongea huku akiweka tabasamu lakini alionekana kumwelewa Yonesi na muda uleule ndio sasa alimgeukia Hamza.
“Nadhani wewe ndio Mr Hamza kama sikosei , Regina amenitaarifu ujio wako kwamba utaishi na sisi kwanzia leo, karibu sana nyumbani”Aliongea yule mama lakini Hamza muda wote alionekana kumshngaa na aliishia kujiambia huyu mama sio wa kawaida kuna msisimko ambao alikuwa akiupata ila hakujua unahusiana na nini.
“Wewe mkorofi, Aunt Mari anakuoangelesha unakaa kimya , usije kumletea ukorofi, ni shangazi yake Regina lakini ni kama mama kwake”Aliongea Yonesi kwa kuamrisha.
“Sio hivyo , nilikuwa nikishangaa , sikutegemea Aunr Mari kuwa kijana hivi?”Aliongea Hamza akijitetea.
“Haha.. Mr Hamza nadhani utakuwa ni mtu unaependa utani , mimi na ujana vipi wakati bado miaka miwili tu kutimiza miaka sabini”Aliongea na kauli ile ilimfanya Hamza kuthibitisha hisia zae, miaka sabini lakini anaonekana kuwa kijana.
“Aunt Mari, akikuletea ukorofi usisite kuniambia , nitafika mara moja kumshikisha adabu”AliongeaYonesi kibabe.
“Hapana , sidhani yupo hivyo , isitoshe naamini maamuzi ya Regina”
Kapteni Yonesi alionyesha kuwa na wasiwasi na Hamza na aliongea maneno kadhaa na mwanamama huyo na kisha aliondoka.
Sasa akabakia Shangazi Mariposa na Hamza peke yao , wote waliangaliana kwa dakika kadhaa na Shangazi Mariposa alivunja ukimya.
“Mr Hamza ngoja nikuonyeshe mazingira ya nyumba”Aliongea
“Shangazi niite tu Hamza , ninaona vibaya ukiniita Mr”
“Nitakuita basi Hamza , Mr ni jina la heshima kwasababu umeshakuwa boyfriend wa Regina”Aliongea na Hamza alitingisha kichwa kukubali.
Mara baada ya kuingia ndani ya kasri hilo , Hamza alivutiwa sana na usanifu wa ndani na mapambo yake, ulikuwa usanifu mwepesi lakini wa kisasa zaidi , nyumba ilikuwa na mwanga flani hivi wa rangi ya majivu na bluu na muonekano huo uliendana sawa kabisa na tabia ya Regina.
Vifaa vya umeme vyote vilikuwa ni vile va bei ya juu na vya teknolojia kubwa , hakukuwa hata na ishara ya vumbi kwenye sakafu , kulikuwa na michoro ya thamani iliokuwa imening’inizwa ukutani. Ijapokuwa uzuri wake ulikuwa ukifurahisha macho lakini pia kulikuwa na ile hali ya flani ya kujisikia kinyumbani.
Sehemu pekee ambayo ilikuwa na vitu vingi ni jikoni pekee , kulikuwa na chillers tatu na friji moja na kumfanya Hamza kuwaza ni kiasi gani cha chakula huhifadhiwa kwenye hizo chillers maana ni kubwa mno.
“Shangazi hii ndio sehemu ambayo wewe na Regina mnaishi siku zote?”
“Ndio , Mzee Wilson na mke wake hawaishi hapa , tokea Regina aondoke nyumbani aliishi na mimi hapa , hii sehemu ipo kimya sana miaka yote tokea tuhamie”
“Aisee , nadhani inachosha sana kuishi kwenye mjumba wote huu watu wawili pekee”
“Labda kwangu lakini kwa Regina anaona sawa , anapenda sana ukimya , akirudi nyumbani ni kula na kulala au afanye kazi katika chumba chake cha kujisomea , sio mtu wa kujichanganya changanya na nimeshamzoea hivyo hivyo”Aliongea Shangazi Mariposa.
“Tena vipi wewe , familia yenu ni ya watu wa ngapi?, wazazi wako wanajua umehamia hapa?”
“Mama yangu alifariki , kuhusu baba sikumbuki sana , nimeishi peke yangu tokea mdogo”
“Ah!, Jamani , pole sana na samehe huu mdomo wangu wa kiropo ropo , sikupaswa kuuliza”
“Haha..Shangazi usiwe na wasiwasi kabisa , nishazoea , hebu niangalie nipo vyema licha ya kwamba nimeishi mwenyewe maisha yangu yote, sina utofauti wowote”
Bi mkubwa huyo hakuongea zaidi na alimchukua Hamza na kwenda kumuonyesha chumba chake.
“Hamza utakuwa unalala kwenye hiki chumba kwanzia leo na kuendelea , chumba kinachofuatia ni cha Regina cha kusomea na mbele yake ni chumbani kwake, nimekuweka karibu karibu na yeye ili angalau mapenzi yenu yashamiri, hii ndio mara ya kwanza kwa Regina kuwa katika mahusiano hivyo juhudi ya ziada inahitajika , nadhani ni Mungu amewakutanisha hivyo hakikisha unatimiza wosia wa babu yake”Aliongea Shangazi.
“Nini , hii ni mara ya kwanza kwa Regina kuwa na mpenzi?”
Hamza alishangaa , ijapokuwa yule mwanamke alikuwa kauzu na ngumu sana kuwa na ukaribu nae , lakini alikuwa mrembo mno na haijalishi juu ya tabia zake lazima kuna wanaume ambao walikuwa wakitaka kutoka nae kimapenzi , labda kama tu walikuwa wamefeli kumshawishi mrembo huyo au kuna sababu nyingine inayomfanya Regina kutojihusisha kimapenzi.
“Hakuna anaemini ila huo ndio ukweli , ijapokuwa mimi ni shangazi yake lakini ni mlezi wake vilevile , nilimuona tokea akikuwa mpaka kusoma kwake na kuhitimu , ni kweli vijana mbalimbali wa tabia zote walikuwa wakimfuatilia lakini hakuonekana kupenda kabisa kujihusisha kimapenzi…hii ilimpa wasiwasi hata babu yake.
Mwanzoni nilijua ataendelea tabia yake hii mpaka akipita kipindi cha kubeba ujauzito , lakini imekuwa bahati nzuri umetokea, Hamza hakikisha unajitahidi , ninasubiri kwa hamu siku ambayo mtaoana na kukuitana mke na mume na mimi kukuita mkwe”
Hamza aliishia kujiuliza na kujiambia kuoa tena na kuitwa mke , mbona kwake ni kama haiwezekani.
Ukweli hakujua acheke au anune , aliona ni kama Shangazi Mari alikuwa akienda mbali sana kimawazo na kuona kwamba jambo hilo haliwezi kutokea , isitoshe amesaini mkataba wa miezi mitatu tu kwa maana hio ataishi hapo kwa miezi hio mitatu.
Lakini kwa namna ambavyo Shangazi huyo alivyokuwa akionekana , ilikuwa ni kama Regina hakumweleza kila kitu kama mahusiano yao yalikuwa ya mkataba.
Upande mwingine ilionekana Shangazi alikuwa akiishi na Regina kwasababu ya babu yake Regina pekee.
Hamza aliweka nguo zake katika chumba chake na kisha akashuka chini na aliweza kumuona Shangazi Mari akiwa amebadili mavazi na ilionekana ni kama alikuwa akijiandaa kutoka.
“Shangazi unaelekea wapi ?”
“Oh , kuna samaki tu ndio wamebaki kwenye mafriji , hivyo naenda angalau kununua mbonga za majini na vitu vingine , nataka kuandaa chakula cha kukukaribisha usiku , wewe bakia tu hapa , unaweza kuangalia Tv au kwenda nje kuogelea”Aliongea. “Lakini si unaendesha kwenda huko sokoni”
“Na umri huu , najulia wapi kuendesha gari , natembea mpaka nje huko kisha nichukue daladala au bajaji”Aliongea huku akicheka.
“Twende wote , nadhani kutakuwa na gari nyingine hapa nyumbani , nitakupeleka”Aliongea Hamza mara baada ya kukumbuka Regina alikuwa na gari aina ya Maserati.
“Hakuna shida , kama hujali kuongozana na mzee kama mimi kwenda Supermarket”
“Hehe , kwanini nijali , nataka kuhakikisha safari haikuchosi ili chakula kiwe kitamu usiku”Aliongea Hamza bila ya wasiwasi na kumfanya Shangazi kutoa tabasamu , hata yeye alikuwa amechoka kupanda vibajaji.
“Tuingie kwenye lift kwenda Gereji ya magari”Aliongea na kumfanya Hamza kushangaa , nakujiambia inamaana utajiri wa Regina ulimpa hadi nafasi ya kumiliki gereji ya magari.
Hamzamara baada ya kuingia katika lift ndipo alipojua hili jengo licha ya kuonekana kuwa na ghorofa tatu kwenda juu lakini ni kama lina ghorofa tano kwani kulikuwa na floor mbili kwenda chini ambazo zote ni gereji, yaani B1 na B2 ,
“Hamnza utapendelea kuendesha lipi hapa , chagua moja mwenyewe , Regina anaendesha magari ambayo yapo B1 pekee na B2 yote hayaendeshi na analetaga fundi tu kuyashitua shitua”
Hamza aliingia katika magesho ya B1 na aliweza kuona magari kumi na yote alikuwa ya kifahari , gari pekee ambayo ilikuwa ya bei rahisi ilikuwa ni BMW Z4, halafu inafuatia Mercedenz Benz ML 400 , kisha BMW X6 na kuendelea , ikiwemo Porsche 911 latest model na pia hata ile Maserati ambayo Regina alitumia mara ya mwisho ilikuwepo..
Comments