Hamza mara baada ya kumaliza kudili na nguo zake moja kwa moja alienda katika chumba cha kusomea cha Regina.
Chumba hicho kilikuwa kidogo sio kikubwa sana na kulikuwa na shelfu mbili tu za vitabu ambazo zimejaa na vyote vilikuwa vimepangiliwa kulingana na Genre zao.
Alikuwa mwanamke msafi mno , hakukuwa hata na ishara ya vumbi na mpangiio wa kila kitu ulikuwa ni wa kuvutia .
Mtu yoyote akiambiwa amwelezee Regina moja kwa moja angekuambia ni mwanamke ambae anajitahidi kuwa perfect katika maeneo mengi na vilevile alionekana alikuwa akipenda kile alichokuwa akifanya.
Katika meza alikuwa amekaa huku akisoma nyaraka iliokuwa mikononi mwake kwa usiriasi wa hali ya juu mno.
Hamza mara baada ya kuingia ndani ya chumba hicho , mwanamke huyo hakuongea chochote kabisa ni kama alitaka kumalizia alichokuwa akifanya kwanza ndio aanze maongezi.
Hamza alichukua kitabu kioja kutoka kwenye shelf na aliweza kuona vyote vilikuwa vikihusiana na maswala ya management na finance na kuendelea hivyo havikumvutia licha ya kwamba na yeye pia alikuwa mwanachuo.
“Unapenda aina hio ya vitabu?”
“Japo naenda chuo na kusomea maswala ya uchumi lakini sio mpenzi wa kusoma sana vitabu vya aina hii , anyway nimekuja kuitikia wito”Aliongea kisha akarudisha kile kitabu.
Regina hakuwa na mabadiliko ya muoekano lakini kuna ishara za usiriasi katika macho yake , ilikuwa ni kama vile yupo ofisini na mfanyakazi yupo mbele yake, ki ufupi kwa mtu ambae hajiamini mbele ya Regina angeomba muda wowote maongezi yaishe aondoke.
“Mr Hamza kuna kitu natumaini unapaswa kuzingatia…”
“Eh , nini hiko?”
Aliongea lakini Hamza muda huo aliweza kuhisi namna ambavyo kuna umbali kati ya Regina na yeye , licha ya kwamba umbali wao ulikuwa kama futi mbili tu lakini ni kama vile mmoja alikuwa ncha ya kaskazini mwingine akiwa ncha ya kusini.
“Kwanza kabisa sisi hatuna mahusiano yoyote wewe ni mwajiriwa wangu wa mkataba , hivyo ikiwa hakuna mtu yoyote usiniite Regi , Unaweza kuniita Boss au CEO , lakini sio kufupisha fupisha kama Regi ,liweke hilo kichwani maana hatuna undugu wowote na hakuna anaemjua mwenzake.
Pili , unaishi hapa kwangu kwasababu za ki usalama peke lakini vile kuendelea kuigiza kama mkataba unnavyokutaka ufanye , sijakuleta hapa kwasababu labda unadhani nataka kuwa na mahusiano na wewe , lazima uheshimu utofauti wa jinsia kati ya mwanaume na mwanamke , huwezi kukaa au kuvua nguo unavyojisikia kama ulivyofanya leo
Tatu , mkataba wetu utaisha ndani ya miezi mitatu tu pengine hata hivo miezi mitatu isifike , usidhani labda nitabadilisha mawazo kwa namna unavyokuza mazoea yako na shangazi na kumfanya awe na furaha kwa kumpeti peti , tabia yako katika nyumba yangu leo hii tayari imevuka mpaka , matumaini yangu utajua nafasi yako..”
Hamza mara baada ya kusikia hayo alishangaa mno lakini kwa wakati mmoja alijisikia vibaya.
“Kwahio unadhani nilikuwa nikimfanya Shangazi kunizoea kwa haraka , kama ndio unachowaza usiwe na wasiwasi , mimi sipo hivyo, sijawaza kama ulivyonidhania , najua vizuri kabisa mimi na wewe haiwezekani kabisa , sisi ni watu wa ulimwengu tofuati”
Regina alikunja ndita kidogo mara baada ya kusikia kauli hivo ya neno haiwezekani kati yao ni kama kuna kitu alijisikia.
“Ni vizuri umelitambua hilo , natumaiini utaijua nafasi yako na usiende mbali na kumfanya Shangazi kuwa na huzuni siku utakayo ondoka hapa”
Hamza alitingisha kichwa na kisha aliweka mikono yake mfukoni , alionekana kusita kidogo lakini akaamua kuongea.
“Regin.. Bosi sijui navuka mpaka ila nadhani kuna kitu unapaswa uzingatie”
“Nini?”
“Naona kabisa ni namna gani baba yako anavyokujali , ila inaonekana mambo mengi hayajui badala..”
“Shut up!!”Aliongea kwa nguvu kumzuia Hamza asiendelee na palepale alibadilika na kuwa mtu mwingine kabisa na kumwangalia Hamza kwa chuki kubwa.
“Wewe ni nani unaetaka kuongelea maswala yangu binafsi , sitaki mtu wa nje kutoa maoni yoyote kuhusu familia yangu, ondoka nyumbani kwangu sitaki kukuona”Aliongea huku akinyoosha mkono kama ishara ya kumfukuza Hamza.
Muda huo huo ndio Shangazi alionekana kufika na alishangaa mara baada ya kuona namna ambavyo Regina alibadilika na wasiwasi ulionekana katika macho yake.
“Nata.. Regina nini kinaendelea , mbona mnagombana”Aliuliza lakini kuchanganya kwake jina kulimfanya kidogo Hamza kushangaa.
“Shangazi usiwe na wasiwasi kuhusu huyu mtu , mpe mizigo yake aondoke nyumbani kwangu” Hamza hakutegmeea Regina kuwa hivyo mara baada ya kutaka kuongea kuhusu baba yake lakini hata hivyo hakutaka kuendelea kubakia hapo na kugombana na mwanake aliona ni kama kujidhalilisha.
Alishia kutoka huku akitoa tabasamu la aibu mbele ya shangazi na dakika chache aliweza kutoka kabisa nje ya nyumba hio na kuondoka.
Asingeweza kubeba chochote kwani nguo zilikuwa zimeloa baada ya kuzifua na nyingine zilikuwa kwenye mashine.
Kwake hakujali sana , hakutaka kujishusha mbele ya mwanamke huyo na kuomba msamaha , alijiambia tena ana bahati sana siku hizi ni mwenye kujizuia la sivyo angemshikisha adabu palepale na kisha kuondoka.
Hamza mara baada ya kutoka alitembea mpaka nje ya geti la mji huo na kisha alipanda daladala , hakuwa na pakuelekea na alitafuta eneo lililochangamka ili kupoteza muda na sehemu pekee ni Bar.
Hakuwahi kwenda kumbi za starehe muda mrefu ili kuokoa hela na kilichomfanya kuwa bize ni kufaya kazi za kifundi.
Lakini siku hio alijiambia anapaswa kunywa japo kidogo , kama angepata na mtoto mzuri usiku huo ingefaa kabisa.
Mwembeni Bar ndio sehemu ambayo aliona itamfaa , ni moja ya Bar ambayo ina utulivu sana na ambayo ni ya viwango ki huduma.
Mara baada ya Hamza kuingia ndani ya Bar hio alienda moja kwa moja mpaka Counter na kisha aliomba apewe Whiskey.
Kwa namna ambavyo aliagiza usingedhania ni yule
Hamza mzembe , hapo alikuwa mzoefu lakini kabla hata hajapewa kinywaji chake alisikia jina lake likiitwa na sauti ya kike kutoka nyuma.
******
Saa nne kamili Amosi alionekana akitembea katika mtaa wa Sinza, muda huo alikuwa amevalia shati la mikono mifupi , alionekana katika mavazi ya ujana zaidi.
Baada ya kutembea kwa miguu kwa dakika kadhaa aliweza kusimama katika moja ya mgahawa maarufu unaosifika kwa nyama choma, mgahawa huo ulikuwa umegawanyika mara mbili kulikuwa na Bar na upande mwingine ulikuwa ni mgahawa bila Bar.
Amosi aliingia moja kwa moja upande wa Bar na aliagiza nyama choma nusu na kisha alisogea na kisha akaenda kukaa katika kitu ambacho kilikuwa na mtu mmoja aliekuwa bize kula nyama na bia, kulikuwa na chupa kadhaa za Windhoek ikionyesha amefika muda mrefu.
Amosi alianza kueletewa chupa yake ya bia K- vant na kumimina kiasi kwenye glasi.
“Taarifa!!”
Sauti ya chini ilimtoka yule mwanaume wa makamo aliekuwa bize kutafuna na kushushia na kinywaji, kwa kumwangalia tu alikuwa na kitambi, lakini vilevile alikuwa mtu mzima kuliko hata Amosi.
“Nimepata dili jipya”Aliongea Amosi huku akipeleka Glasi mdomoni na kupiga pafu.
“Dili gani?”
“Kuna mwanamke nimepewa kazi ya kumtafuta , malipo ni makubwa sana , ndio kazi yangu ya kwanza kupata malipo makubwa hivi”
“Kuna muunganiko wowote na kazi yako?, Mwanamke huyo ni nani? Na vipi kuhusu waliokupatia kazi”
“Sijaweza kufanya muunganiko bado , lakini mwanamke ni kama sura yake nishawahi kuiona , lakini nimeshindwa pa kuanzia , waliotoa kazi sijawajua bado ,Chriss ndio mtu wa kati alienikonekti na hili dili”
Kwa jinsi walivyokuwa wakiongea usingeweza kusikia , lakini vilevile usingejua kama wanaongeleshana.
“Chriss ameingia kwenye rada za MALIBU tokea mwezi uliopita , ukaribu wake na wabrazili umeongezeka na kuibua wasiwasi kwa kitengo , kuna uwezekano kazi hio ikawa ni kutoka kwa Wabrazili ,
kama ni kweli muunganiko na kazi yako utakuwa mkubwa”
“Nahisi hivyo pia , kwa maelezo ya Chriss wanasema ni kazi ambayo najua pa kuanzia , inaonekana wananijua vizuri , nadhai hatua yangu ya kwanza ni kujua nilimuona wapi mwanamke katika picha alionipa.
“Una hio picha”
“Ndio”Aliongea na palepale alipitisha picha ile kwa chini na bwana yule asiefahamika jina alipokea.
Baada ya kutumia mwanga hafifu aliweza kuangalia picha ile na palepale sura yake ilionekana kujikunja.
“Unamjua?”Aliuliza lakini kabla ya kupokea jibu lake mhudumu alifika alipo Hamza na kupokea alichoagiza hivyo ukimya ulitawala.
“Ndio maana wamekupatia hii kesi , inaonekana waliokupatia wapo ndani ya mfumo wa intelijensia yetu”
“Nini!!?”
“Rejea kesi ya radi ya mwaka 2002, iliomfanya Kanali Sedekia kupotea”Aliongea na hapo hapo sasa akili ya Amosi ilipata network.
“Nilidhani nilikutana nae ana kwa ana huyu mwanamke , lakini kumbe niliona picha yake pia”Aliongea huku akiwa ni mwenye wasiwasi kwenye macho yake.
“Kama ni hivi kwanini Wabrazili kumtafuta huyu mwanamke , si faili la kesi lilishafungwa mara kuthibitishwa yule mama alifariki?”Aliongea Amosi.
“Sidhani kama ipo hivyo , uchunguzi wa kesi ile walipewa wanausalama wa serikali wafanye kazi , lakini yalikuwa maagizo kutoka Jesuit , mpaka sasa kuna uwezekano Sedekia kuna kitu alichofahamu ndio maana akapotea”
Jasho lilimtoka Amosi na sasa alijua ni kwanini kazi hio ilikuwa na malipo makubwa sana , inaonekana ni kazi ya hatari mno.
“Kwahio ni dhahiri uchunguzi unaendelea nje ya kitengo cha usalama wa taifa”
“Hilo linawezekana , ni swala ambalo hata mimi mpaka leo hii linanifikirisha , nani aliondoka na maiti ya mtoto mmoja?, shauku yangu imeongezeka baada ya kuona kuna siri kubwa iliojificha kama si hivyo kwanini kanisa la Wabrazili wamekupa kazi umtafute mwanamke ambae amekwisha kufariki , nadhani kuna kitu wanataka kujua”Aliongea yule bwana na kisha alisimama akionyesha ishara anataka kuondoka.
“Kuwa makini na hii kazi , la sivyo kilichomtokea Sedekia kinaweza kutokea kwako pia, ukifanikiwa umepata taarifa muhimu kwa kitengo chetu pia, fanya hii kazi ukiwa na uzalendo kwenye moyo wako”Aliongea na kisha aliondoka.
Comments