CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA NNE
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Baada ya Namouih kuwa ameachana na Felix muda mfupi nyuma, sasa mwanamke huyu alikuwa mwendoni kuelekea nyumbani, na leo ingekuwa ni mapema tu anarudi nyumbani hasa kwa kuwa alijua mume wake angekuwa ameshafika huko. Alihisi kujiamini zaidi wakati huu kwa sababu alijua baada ya maongezi yake na rafiki yake mpelelezi, Felix hangemwangusha hata kidogo katika kumchunguza Draxton na hatimaye angeweza kufichua mabaya ya mwanaume yule na kumpa alichostahili.
Akafika nyumbani ikiwa ni saa tisa alasiri, naye akamkuta Efraim Donald akiwa zake chumbani amejipumzisha kwa kusinzia kabisa kitandani. Akaweka mkoba wake pembeni na kuanza kubadili
mavazi, kisha akaingia bafuni kujimwagia maji kwanza. Akiwa bafuni, taswira ya tukio la jana usiku ikaanza kumwingia akilini tena, akikumbukia jinsi kivuli kile kilivyokuwa kinapenya kuingia ndani ya ofisi yao ya hapo nyumbani na mlango ukifunguka taratibu, kisha kilivyoondoka ghafla tena. Akafumba macho yake na kuendelea kuruhusu maji yaumwagikie mwili wake kwa muda mrefu, kisha akatoka humo na kurudi chumbani.
Kwa kuwa Namouih alikuwa ameshakula, akavaa tu nguo za kawaida na kwenda chini kuonana na Esma, akaongea naye mambo kadha wa kadha yaliyohitajika hapo nyumbani na kucheza na Angelo
kidogo, kisha naye akapanda juu tena na kwenda kitandani kulala. Akawa amewasiliana na mama
yake mzazi, Zakia, kumjulia hali yeye na mdogo wake, yaani Nasma, kisha ndiyo akautafuta usingizi wa mchana. Hakupata shida kusinzia mpaka alipokuja kuamka na kukuta Efraim akiwa ameketi tu kitandani kwa kumpa mgongo huku akisoma vitu fulani kwa simu yake, naye akamgusa mgongoni ili kumjulisha kwamba alikuwa ameamka.
Efraim Donald akageuka na kusema, "Vipi?"
"Safi," Namouih akajibu.
"Unalala kama umekufa yaani..."
"Kwa nini?"
"Hakuna hata sauti ya mkoromo."
"Mhmhm... me huwa sikoromi. Wewe sasa..."
"Ahah... unakuwa uchovu. Ulikula?"
"Ndiyo, si nilikwambia nilitoka kukutana na mtu? Nilikula huko."
"Sawa."
"Saa ngapi?"
"Saa kumi na moja. Ona, kuna sendoff leo ya rafiki yangu wa kazini... tutaenda saa mbili," Efraim
akamwambia.
"Iih! Yaani hata nilikuwa sijajiandaa Efraim..."
"Kwani unahitaji nini, nguo si zipo? We' twende bwana... nimeshalipia double."
Namouih akatabasamu tu, naye akauliza rafiki yake huyo alikuwa nani na alimuoa nani. Efraim Donald akaanza kumwelezea kuhusu sherehe hiyo ambayo alipokea mwaliko wake mapema leo na kufikiria kwenda pamoja na mke wake huko, hivyo kama ni kuanza kujiandaa wangetakiwa waanze mapema maana Efraim alitaka mke wake amsaidie kumtengeneza vizuri kwa ajili ya hafla hiyo. Kweli Namouih akamchagulia mume wake mavazi mazuri na kumnyooshea, naye pia akatafuta vazi zuri sana lenye rangi ya maziwa (cream) ambalo angelivalia na kinguo chepesi kama ushungi wa kichwani lakini kisichofunika kichwa chake chote, yaani kingening'inia kutokea
nyuma ya nywele zake alizozibana. Efraim hakusema lolote kwa mke wake kuhusu ujio wa Sasha
ofisini kwake mapema ya leo.
Walikuja kukamilisha mitoko yao na kuendelea kukaa hapo nyumbani mpaka inafika jioni, kisha
wakaondoka kuelekea huko kwenye sherehe. Ilikuwa ni mwendo mrefu kiasi kufika huko lakini walitumia dakika chache tu hasa kwa kuwa dereva wake Efraim, yule Suleiman, ndiyo alikuwa anawaendesha kwa ustadi wake mwingi kwa hivyo hawakukawia. Walipofika wakaelekea moja kwa moja ndani ya ukumbi, uliokuwa mkubwa na uliopambwa vyema. Walipoingia ndani, baadhi ya watu waliofahamiana na Efraim Donald wakawa wanasalimiana naye na kupata kumjua mke wake
pia, na kama kawaida Namouih alisifiwa kwa urembo wake na kupendeza. Wakaelekea kukaa kwenye meza ambayo ilizungukwa na viti kadhaa, nao wakaletewa vinywaji. Hapo kulikuwa na wanawake wengine wawili na mwanaume mmoja, nao wakawa wanaongea pamoja na wanandoa hawa kwa njia ya kirafiki.
Namouih aliweza kutambua kwamba kuna baadhi ya watu kuzunguka sehemu ya ukumbi huo walioongea kwa njia ya umbea kumwelekea, tena waziwazi kabisa, lakini akajitahidi kuwapuuzia tu. Muda haukupita sana na bibi harusi akafika hapo. Kama kawaida ya taratibu za sendoff MC akawa anafanya yake ili sherehe isonge mbele, naye Efraim Donald akawa amepigiwa simu na kwenda nje kuzungumza kwanza. Mwanamke mmoja kati ya wale wawili waliokuwa wamekaa meza moja na Namouih akawa ametambua kwamba mwanamke huyu aliishiwa pozi kwa sababu fulani, na tayari alikuwa ameshajua kwa nini. Akakishika kiganja cha Namouih, naye Namouih akamwangalia machoni.
"Hao wanaokuongelea sana ni washakunaku tu, hawakujui, huwajui, kwa hiyo wasikuvurugie usiku wako kabisa sawa mpenzi?" mwanamke huyo akamwambia kwa sauti ya chini lakini iliyosikika
vyema kwa Namouih.
Namouih akatabasamu tu kwa mbali na kutikisa kichwa chake kukubali.
Mwanamke huyo alikuwa
na umri mkubwa kiasi kumzidi, kwa hiyo kulikuwa na heshima ya mwanzo kumwelekea kutoka kwa
Namouih. Ni wakati huu ndipo Efraim Donald akawa amerejea na kuketi pembeni ya mke wake.
"Namouih... kuna suala limezuka. Ninahitaji kwenda kukutana na kiongozi wa Cargo, ameniita mara
moja," Efraim akamwambia.
"Sasa hivi?" Namouih akasema.
"Ndiyo, yaani kuna mkataba mpya nilikuwa mbioni kusaini pamoja na kampuni yao, sasa hajapata muda na nini lakini sasa hivi ndiyo anataka tukutane ili tuongee vizuri... honey, sitachelewa. Tukimaliza tu narudi, okay?" Efraim akasema.
"Je ikitokea ukachelewa?"
"Hapana, sitachelewa. Na ikiwa kama dharura ya kunichelewesha sana itatokea basi nitamwambia
Suleiman aje akuchukue," Efraim akamwambia.
Namouih akaangalia pembeni.
Efraim Donald akambusu kwenye shavu mara mbili na kukishika kiganja chake, kisha akaondoka
hapo haraka ili awahi huko.
"Ni jambo zuri sana kwamba mume wako anakupenda... anaonyesha hilo waziwazi," yule mwanamke akamwambia Namouih.
Namouih akamtazama na kusema, "Ndiyo. Ni jambo zuri lakini sijui kwa nini kwa wengine huwa ni
dhambi."
"Agh, achana nao. Hakuna hata mmoja kati yao anayejua maisha yako kwa hiyo maneno yao
yasikubabaishe kabisa," mwanamke huyo akamwambia.
"Asante. Naitwa Namouih..."
"Naitwa Salome. Nakufahamu dada. Wewe ni mwanasheria mzuri sana, na kinachowafanya hao pakashumi wapige domo mno ni kuwa umewazidi kwa mambo mengi mno, na bado unazidi
kung'ara..."
Namouih akatabasamu na kusema, "Maneno ya watu hayajawahi kunipa shida. Sema, sipendi tu
hivyo wanavyoninyooshea-nyooshea vidole makusudi tu ili nijue wananisema. Inakera. Lakini
nikinyanyuka kuwafata me ndiyo nitaonekana mpuuzi... haina faida yoyote."
"Ni kweli. Mimi nilijifungua mtoto mlemavu miaka mingi nyuma, na nilisontewa vidole sana na watu... wakaongea mengi mno yaliyonikosesha amani. Lakini nilikuja kujua ukiwaonyesha kwamba haujali wanachosema, wanakuacha, ila ukiwaonyesha kwamba unajali ndiyo wanakuwa kama wameshinda. Ni kupuuzia tu, maana ukibishana na chizi...."
"Na wewe utaonekana chizi," Namouih akamalizia maneno ya Salome.
"Ndiyo hivyo," Salome akasema.
"Unasema kweli. Pole pia kwa...."
"Aa... usijali. Mwanangu hakuwa mkamilifu kwenye kutokukamilika lakini nilimzaa mwenyewe.
Hakuna aliyenisaidia kumzaa... alikuwa wangu. Hilo lilitosha," Salome akasema.
"Alikuwa?" Namouih akauliza.
"Alikufa miaka mitatu iliyopita. Na wale wale waliokuwa wananisema vibaya ndiyo wakaja kulia pamoja nami. Ahah... dunia hii..."
"Masikini... pole sana Salome..."
"Nilishapoa. Wewe una mambo mengi mazuri, na umesaidia wengi, kwa hiyo hao watu wasikukoseshe raha kabisa..."
"Hivi unafikiri hata nawajali? Ni basi tu yaani hizi siku chache kumekuwa na mambo mengi yenye kukwaza halafu na hawa mbwa hata hawanijui wanakaa kunisontea tu vidole," Namouih akasema
na kusonya.
Salome akacheka kidogo.
"Umeshasikia maneno wanayosema kunihusu?" Namouih akauliza.
"Ndiyo. Huwa nasikia wanakuongelea sana kwamba unaringa mno kwa sababu ya sura yako... una pesa lakini mchoyo sana, ndiyo maana eti Mungu amekufungla usiweze kuzaa," Salome akasema.
Namouih akacheka kidogo kwa mshangao.
"Na hasa ile juzi maneno yalikuwa mengi ulipopoteza kesi ya yule msichana aliyekufa... mara sijui
ulimwahidi kushinda ndiyo maana aliposhindwa akajikuta anabebwa na malaika wa kifo.... yaani dada, we' acha tu," Salome akasema.
"Ahah... ina... inahuzunisha na inakera sana. Lakini angalau inafariji kujua kwamba kuna watu kama
wewe wanaonielewa vizuri," Namouih akasema.
"Kabisa, tena wako wengi tu. Usifikiri vitu vinavyokuzunguka vinakuwa mbali nawe, unakuta viko hapo hapo ulipo. Cha muhimu ni kujua tu jinsi ya kuishi vizuri ndani ya duara la dunia yako mwenyewe hata kama wanaokuzunguka wanataka kuiporomosha, na unafanikiwa katika hilo kwa kuishi namna uishivyo siyo kwa kuridhisha mtu, ila kwa kuridhika wewe mwenyewe," Salome
akamwambia.
Namouih alipendezwa sana na maneno ya mwanamke huyu, naye akasema, "Asante Salome.
Nampa Mungu marks za asilimia mia kunikutanisha nawe leo."
Salome akacheka kidogo na kusema, "Asante."
"Wewe ni..."
"Ni daktari... nimebobea sanasana kwenye mambo ya ushauri na saha," Salome akamwambia.
"Ooh... sawa. Ndiyo maana una maneno mazuri."
Namouih akaendelea kukaa hapo na rafiki yake mpya wakiongelea mambo ya hapa na pale huku
sherehe ikiendelea taratibu, naye kiukweli alikuwa amejihisi vibaya moyoni baada ya kujua kwamba
watu walizungumzia suala lake la kutokuwa na watoto kwa njia mbaya sana. Hakuwahi kukazia fikira sana suala la kuwa na watoto, lakini kisa cha Salome cha kumpoteza mtoto wake aliyekuwa mlemavu kilimgusa sana kiasi kwamba akaanza kutamani kuijua furaha iliyopo ya kuwa mama. Akaendelea kutulia tu akimsubiri mume wake arejee kwa sababu tayari sehemu kubwa ya sherehe hiyo iliyomboa sana ilikuwa imekwisha.
★★
Upande wa Blandina. Mwanamke huyu alikuwa ametoka pamoja na mpenzi wake kwenda matembezi kama walivyokuwa wameahidiana kufanya baada ya Draxton kukutana na Namouih mapema ya leo, na wapendanao hawa walikuwa wametumia muda mrefu wakiwa pamoja. Walitembelea sehemu nyingi na kufurahia maongezi na vitumbuizo, ndipo mida ya saa nne wakaelekea kwenye kumbi moja ya starehe ili kupata chakula na vinywaji. Yaani Blandina aliagiza chakula nje ya kumbi hiyo, kisha ndiyo wakaingia kule ndani na kuketi kwenye meza yenye viti virefu na kuletewa vinywaji. Blandina yeye akachukua vileo vinne na Draxton viwili tu, kwa sababu mwanaume huyu hakunywa sana vilevi.
Blandina alikuwa ameketi karibu sana na Draxton kwa kupitisha mkono wake ndani ya mkunjo wa
kiwiko cha mpenzi wake, mara kwa mara akimnong'oneza maneno mazuri sikioni, naye Draxton
angemwambia vitu vilivyomfanya mrembo acheke sana. Kulikuwa na watu wengi kiasi, wengine
wakicheza muziki na wengine wakitazama runinga za hapo, bila kukosekana walevi walioongea
kwa sauti kubwa sana. Blandina akawa anamwangalia Draxton na kuona jinsi ambavyo alitazama
watu kwa njia ya kutojali, na hilo likamfanya atambue kuwa mwanaume huyu hakupendelea sana sehemu kama hizi. Kulikuwa na wanawake ambao walimtazama sana Draxton lakini yeye hakuwa
na muda nao kabisa, vile vile na Blandina aliyeangaliwa sana na wanaume kadhaa.
"Panakuboa hapa?" Blandina akamuuliza Draxton kwa kunong'oneza.
"Mm?"
"Pamekuboa? Tutafute sehemu nyingine?"
"La... haina haja. Si tumeshaingia?"
"Yeah, ila naona kama hujapapenda..."
"No, pamechangamka. Besides, umeshaagiza na chakula so...."
"Lile pale lidada linakuangalia sana natamani nilifate nikalikoe!" Blandina akasema.
Draxton akatabasamu na kunywa tu kinywaji chake.
"Ah... sss!" Blandina akatoa sauti hiyo kama ameumia na kuutoa mkono wake kwa Draxton.
"Vipi?" Draxton akauliza.
"Sijui... kuna mbu amening'ata," Blandina akasema huku akijiangalia mkononi.
"Pole..."
"Yaani midude mingine mpaka unajiuliza sijui kwa nini iliumbwa tu..."
"Ahah... unajua kuna mtu anaweza kusema umekufuru."
"Hata kama bwana, yanakera. Halafu midude yenyewe huwa inaishi kwa siku moja na nusu tu... yaani inasumbua, mikelele nyooo... afu' inakaa siku moja tu," Blandina akaongea na kusonya.
Draxton akacheka kidogo na kumwangalia sehemu hiyo iliyong'atwa.
Blandina akahisi bega lake likishikwa kutokea nyuma, naye akageuka upesi kumwangalia aliyemshika. Tabasamu la furaha likamtoka baada ya kumtambua haraka.
"Hee... Felix!" Blandina akasema.
"Vipi wewe panya buku, upo?" Felix akamwambia kiutani.
"Sura kama kiroboto wewe!" Blandina akamwambia kiutani pia.
Wawili hawa wakakumbatiana kwa furaha, Blandina akiwa bado amekaa, lakini kuna jambo likawa
limemkera Draxton haraka. Felix alikuwa ameshika sigara katikati ya vidole vyake, hivyo alipomkumbatia Blandina hakuushikisha mkono ulioishika sigara mgongoni kwa Blandina, kwa hiyo ukawa hewani, lakini kwa kuwa Draxton alikuwa karibu sana na Blandina hiyo ikafanya sigara hiyo iguse T-shirt aliyokuwa amevaa. Draxton akaitazama sigara hiyo na kumwangalia Felix, ambaye alikuwa anamtazama pia huku akitabasamu kwa furaha, na ikawa wazi kwa Draxton kwamba mwanaume huyo alifanya hivi makusudi kabisa.
Kisha....
"Oh, samahani, so sorry bro..." Felix akasema hivyo na kumwachia Blandina.
Blandina alipomwangalia Draxton akakuta anajiangalia kwenye T-shirt yake, ambayo sasa ilikuwa imebakiza alama ya majivu kiasi kutokana na sigara kuigusa, lakini haikuwa imechoma kabisa.
"Aaa... Felix mambo gani? Unaniharibia moment bwana..." Blandina akamwambia.
"Pole kaka, excitement ya kukutana na huyu nikajisahau. Pole sana," Felix akamwambia Draxton.
Draxton akatikisa kichwa chake tu kuonyesha haikuwa na tatizo, naye Blandina akawa anampangusa kwenye T-shirt yake.
"Haujaachaga tu kuvuta hayo madude?" Blandina akamuuliza Felix.
"Nina muda. Ila sema leo niliona tu haitakuwa mbaya kupiga pafu moja hahahah..." Felix akasema.
"Uko poa babe?" Blandina akamuuliza Draxton.
"Yeah," Draxton akajibu.
"Huyu ni rafiki yangu, anaitwa Felix, tumesoma wote. Felix, huyu ni Draxton. DRA-X-TON," Blandina
akasema.
"Nimesoma bwana, we' naye vipi? Hahah... nashukuru kukufahamu kaka. Pole tena kwa hiyo ajali ndogo," Felix akamwambia Draxton.
"Haina shida. Ni vizuri kukufahamu pia," Draxton akamwambia kikawaida tu.
"Za siku?" Blandina akamuuliza Felix.
"Aah mambo mengi... unyama mwingi. Tokea kwa Mwantum mpaka now hatujaongea eti?" Felix akasema.
"Eee we' si uko bize sana... lazima unyama uwe mwingi," Blandina akasema, naye Felix akacheka.
Ni wakati huu ndiyo vyakula ambavyo Blandina alikuwa ameagiza vikaletwa, na vilikuwa vyakula
vizuri sana vyenye kutamanisha mdomo mpaka kuijaza mate.
"Dah, safi sana. Mambo ya makamuzi hayo..." Felix akasema.
"Karibu. Kaa basi," Blandina akasema.
"Oh, no, nilikuwa napiga mbili tatu tu hapo ndo' nataka kukimbia sasa hivi... nyie mji-excuse tu. Aa...
mnafanya kazi pamoja?" Felix akaongea hivyo.
Blandina akamlalia Draxton begani na kusema, "My only one love."
Felix akacheka kidogo na kusema, "Sawa kabisa. Mko vizuri pamoja. Hivi ndiyo Draxton huyu
aliyempiga chini Namouih kwenye kesi eeh?"
Draxton akamtazama kwa macho yake makini.
"Ndiyo huyu. Habari zinasambaa haraka kumbe... hahahah..." Blandina akasema hivyo na kucheka.
"Dah, hongera sana kaka. Yule alikuwa hakamatiki kwenye kesi ila ukamweka sehemu yake, vizuri
sana. We' ni mtu wa wapi?" Felix akauliza.
Draxton akaacha kumwangalia na kubaki kimya tu.
"We' si ungekaa bwana, umeanza na upelelezi wako sasa... kaa ndiyo tuongee vizuri Ili uju...."
"We' ni mpelelezi?" Draxton akamkatisha Blandina kwa kumuuliza Felix swali hilo.
"Ndiyo. Rank za juu mpelelezi. Kwa kuwa sisi ni marafiki na Blandina ingekuwa poa mimi nawe
tukijuana vizuri zaidi au siyo?" Felix akasema.
"Yeah," Draxton akajibu huku akimtazama kwa umakini.
Blandina alikuwa ameshaanza kula, naye akasema, "Vipi tukipanga kesho tukutane sehemu nzuri?
Ni Jumapili. Sisi wote na Namouih, na Donald, na Oprah? Kwanza mke wako huyo hajambo?"
"Ahahahah... yuko poa. Itakuwa jambo zuri, au siyo... Draxton?" Felix akaongea hivyo huku anamwangalia usoni kwa umakini.
Draxton akamtazama kwa ufupi, kisha akatikisa kichwa kukubali.
"Haya, tutaongea badae'... nyie wawili mw-enjoy... kaka tutaonana," Felix akawaaga na kuondoka.
Blandina alikuwa anatabasamu, naye akamwangalia Draxton na kusema, "Ni rafiki yetu sana huyo me na Namouih. Tunao wengi lakini, Felix yuko tight sana. Tumetoka mbali."
"Anaonekana yuko rafu," Draxton akamwambia.
Blandina akacheka kidogo, kisha akaanza kuongelea mambo mengi kuhusiana na maisha yake ya
zamani pamoja na hao rafiki zake, bila ya mwanamke huyu kutambua kwamba lengo la Felix kufika hapo lilikuwa kumchunguza mpenzi wake kwa kadiri fulani. Akaendelea tu kuzungumza kuhusu namna alivyotaka kuanza mazoezi ya viungo ili kuupa mwili wake umbo zuri zaidi kwa wakati huu kama jinsi Namouih alivyokuwa. Draxton akawa anamwambia kwamba umbo lake lilikuwa zuri na hakutakiwa kujilinganisha na mtu yeyote yule, lakini Blandina aliona bado alihitaji kuuchangamsha mwili wake ili asijikute anafikia manyama uzembe. Ni kati ya mambo yaliyofanya Draxton amfurahie sana mwanamke huyu kwa kuwa Blandina alikuwa mtu mwenye kujiachia sana akiwa pamoja naye. Wawili hawa wakaendelea kupata chakula na vinywaji taratibu huku wakifurahia maongezi.
★★
Upande wa wanandoa Efraim Donald na Namouih. Mambo ya chereko yaliendelea vyema ndani ya sendoff ya rafiki yake Efraim ambapo mwanaume huyo alikuwa ametoka kidogo baada ya kupigiwa simu kwa dharura fulani ya kikazi, na sasa ikiwa imeingia saa sita usiku ndiyo mwanaume huyo akawa amerejea. Alimkuta Namouih akiwa pamoja na Salome; wawili hawa wakiwa wamepatana sana hadi ikawa ni kama Namouih amemsahau kabisa mume wake ingawa alichelewa. Efraim akafurahi kukuta Namouih yupo kwenye hali ya uchangamfu, naye akasema kama ikiwezekana waendelee kukaa ili wazungumze zaidi na kupata vinywaji. Lakini tayari maharusi walikuwa wameondoka, na Salome alisema alihitaji kufika nyumbani haraka pia. Efraim Donald alikuwa ametoa kama ofa ya kumpa lifti Salome lakini mwanamke huyu alikuwa na gari pia, kwa hiyo wakaachana baada ya Namouih kumpa mwanamke huyo namba za simu ili waendelee
kuwasiliana.
Wanandoa hawa wakaelekea nyumbani huku Efraim akiomba radhi kwa kumwacha Namouih mwenyewe, lakini mke wake hakuona shida sana kwa kuwa alipata rafiki mpya aliyepatana naye vizuri sana kimawazo. Wakafika nyumbani hatimaye, na baada ya Suleiman kuingiza na kuegesha gari ndani, geti likafungwa na mlinzi, yule Alfani, ambaye alikuwa macho muda wote kulinda sehemu hiyo.
Namouih na Efraim Donald wakashuka huku mwanamke huyu akimwambia mume wake kwamba
ingependeza sana kama wangebadili geti la nyumba hii liwe la mfumo wa kuendeshwa kwa rimoti, naye Efraim akasema angelifanyia kazi suala hilo. Walipofika ndani walimkuta Esma akiwa amesimama karibu na mlango wa kuingilia kama anawasubiri, naye akawasalimu vyema na kusema kweli alikuwa anangoja warejee. Namouih akamwambia hakupaswa kufanya hivyo hasa kwa kuwa muda ulisonga sana, naye akamwambia aende tu kupumzika.
Ikiwa ni mida ya saa saba ya saa nane usiku sasa, wanandoa hawa wakaingia chumbani na kuanza
kuondoa mavazi yao mwilini ili wavae mepesi kwa ajili ya kupumzikia. Namouih alikuwa
anamwangalia sana mume wake aliyekuwa kimya tu mpaka alipomaliza kuvua nguo zake na
kubaki na boksa, naye akaanza kumfata na kumkumbatia kutokea nyuma; yaani Efraim akiwa amempa mgongo. Mwanamke akawa anavitembeza taratibu viganja vyake kwenye kifua cha mume wake huku kucha ndefu kiasi kwenye vidole vyake laini zikimtekenya kwa mbali, na akimbusu shingoni, naye Efraim akawa ametulia tu. Kisha Namouih akaushusha mkono wake
kufikia sehemu ya siri ya Efraim na kupagusa, na hapo akasisimka baada ya kuhisi namna
palivyovimba sana, kuonyesha kwamba alifanikiwa kumpandishia mume wake hamu ya kimahaba.
Lakini mara Efraim akaushika mkono wa Namouih na kuushikilia kwa pembeni, ikiwa kama ameutoa hapo kwa kusudi, naye akamgeukia na kumtazama machoni. Namouih sasa alikuwa amebaki na sidiria nyeupe na chupi laini nyeupe pia, mwili wake mzuri uliotamanisha sana ukiwa wazi mbele ya mume wake, naye akawa anamtazama tu Efraim Donald kwa hamu na matumaini.
"Namouih..." Efraim akaita.
"Bee..." Namouih akaitika kwa sauti ya chini.
"Tungelala tu mpenzi... ni saa nane sasa hivi..."
"Me sina usingizi... we' una usingizi? Si tulilala wote mchana?"
"Yeah, but ni uchovu tu. Kulikuwa na mambo mengi huko nilikoenda kwa hiyo...."
Namouih akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa, kisha akatoka mbele ya mume wake na kuelekea kabatini. Efraim Donald akabaki kumtazama tu jinsi alivyoanza kuzitoa nguo za kulalia na kuzirusha kitandani kwa njia iliyoonyesha hasira, naye Namouih akavaa nguo yake nyepesi ya kulalia na kubana nywele zake nyuma ya kichwa, kisha akachukua mto na kuanza kuelekea mlangoni. Efraim akakunja uso kimaswali na kumfata upesi, kisha akamzuia kutembea kwa kumshika mkono na kusimama mbele yake ili asiufikie mlango.
"Unaenda wapi?" Efraim Donald akauliza.
"Guest room," Namouih akajibu.
"Unaenda chumba cha wageni kufanya nini?"
"Kulala."
"Kwa nini?"
"Kwa sababu sihitajiki humu."
"Namouih em' acha basi. Sa'hivi ni usiku, hakuna muda wa kuanza maigizo...."
"Maigizo? Anayefanya maigizo ni mimi au wewe?"
"Unamaanisha nini?"
"La 'usadiq hadha!" Namouih akaongea kwa kiarabu akiwa amekerwa sana.
Efraim akabaki kumtazama tu.
"Yaani Efraim... umekuwaje sijui... hii ni ndoa au maigizo?"
"Namouih..."
"Nini?"
Efraim akabaki kimya.
"Naomba unipishe," Namouih akasema.
"Hauwezi kwenda kulala huko... kitanda chako hicho hapo..."
"Kitanda gani? Hilo ni pambo tu Efraim. Unanisifia sana, unanitendea vizuri, unaniambia mimi ni wa
muhimu hapa, lakini kwa lipi? Nimekaa kuwa kama mdoli tu hapa..."
"Namouih ni kwa nini unaongea hivyo? Kila kitu unacho Namouih. Unataka nifanye nini... unataka
nikupe nini zaidi ili kukuonyesha kwamba nakupenda?"
"Ah! Are you seriously asking that? Nachokitaka ni wewe Efraim!" Namouih akasema hivyo na
kumpiga kifuani na mto.
Efraim Donald akatazama chini.
"Kuna mambo mengi yametokea... na kwa muda fulani, ndiyo... nilihitaji wakati upite. Lakini inaonekana kama unafanya hivi kunikomoa. Yaani unanifanyia hivi ili sijui nikome au.... au labda
unaishi kwa masharti Efraim?"
Efraim akamwangalia na kusema, "Namouih ni maneno gani hayo unaongea?"
"Unataka nifikiri nini sasa? Efraim... unajua watu wanasema nini kutuhusu? Kwamba sisi tunaringa
sana na tunaishi kwa masharti ndiyo maana bado uko nami ingawa eti siwezi kuzaa. Hawana uhakika kuhusu hilo lakini kwa jinsi mambo yalivyo inaanza kuonekana kuwa kweli," Namouih akaongea kwa hisia.
"Toka lini umeanza kujali yale watu wanayosema?"
"Agh, this is not about them! Hii ni kuhusu sisi Efraim! Hatujawahi hata kukaa kuzungumza ikiwa tunataka kuwa na watoto. Ni kazi, visingizio, kazi, visingizio, mpaka lini? Au unataka nije nitoke huko nje nikutane na limtu litakalotimiza haja zangu?"
"Usije kuthubutu tena kuongea hivyo Namouih!" Efraim akasema kwa hisia kali.
"Kwa hiyo unataka nifanye nini ikiwa wewe kama mume wangu mwenye haki zote unashindwa
kunipa nachohitaji? Niendelee kuwa pambo lako tu humu ndani si ndiyo? Una nguvu nzuri, una mke
mzuri, unapendwa, una... unahitajika Efraim... kwa nini huoni hilo? Kwa nini... just... kwa nini?" Namouih akasema kwa hisia mpaka machozi yakaanza kumtoka.
Efraim akataka kumfuta machozi lakini Namouih akarudisha uso wake nyuma.
"Namouih nisikilize..."
"Ndiyo nakusikiliza..."
"Nakuahidi... nitarekebisha hili. Nipe muda kidogo tu..."
"Ohoh... crap..." Namouih akasema hivyo kuonyesha hamwamini.
Efraim Donald akawa anataka kumshika mabegani, lakini Namouih akamfata mdomoni na moja
kwa moja kuanza kumbusu kimahaba. Alikuwa akimpa huba kwa kasi na kushika sehemu yake ya
siri lakini Efraim akamshika kwa nguvu kiasi na kumzuia, jambo lililofanya Namouih abaki
kumwangalia tu huku akitikisa kichwa kwa kufadhaika.
"Namouih..."
Namouih akanyanyua kiganja chake juu kumzuia asiendelee kuongea, naye Efraim akabaki kimya.
"Huo muda kidogo ukiisha, ndiyo nitarudi kulala humu. Keep me posted," Namouih akamwambia.
Efraim Donald akabaki tu kimya na kuendelea kumtazama mke wake usoni. Namouih akajifuta machozi na kuuokota mto wake ili atoke, lakini simu yake ikaanza kutoa mlio wake wa kuita. Akawa amekumbuka hakuwa ameichukua, hivyo akaifata ili atoke pamoja nayo, na Efraim akabaki kumtazama tu. Alipoishika simu yake, Namouih akaona kwamba aliyekuwa akipiga ni Blandina, naye akajipa utulivu na kuipokea huku akianza tena kuondoka.
"Hallo Blandi..." Namouih akasema.
"Namouih...."
Mwanamke huyu akasimama baada ya kusikia sauti ya rafiki yake ikitaja jina lake kwa njia iliyomwambia kwamba Blandina alikuwa analia. Uso wa Namouih ukakunjamana kwa njia ya kuonyesha maswali, naye Efraim akamsogelea karibu.
"Blandina... nini tatizo? Mbona unalia?" Namouih akauliza.
"Hhh... Namoouih... kuna... tumefiwa Namooouih...."
"Nani? Nani ame...."
"Felix ameuawa Namouih!" Blandina akaongea hivyo.
Namouih alihisi mtetemo ukipita ghafla kwenye mkono wake uliosababisha aidondoshe simu yake kutoka sikioni!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments