SEHEMU YA 19.
Kitendo cha Linda kumwelezea namna utaratibu wa CEO unavyokuwa kila akifika kazini , hatimae lift iliweza kufnguka katika floor ya saba na ndio sehemu ambapo idara ya uwekezaji inapatikana na meneja wa idara hio alikuwa tayari ameshaandaa nyaraka nje ya lift na kumpatia Regina.
“Mkurugenzi malighafi mpya ambazo zinatengenezwa na Taita Chemical, zinaenda kubadilisha kabisa teknolojia ya utengenezaji wa raba na kuzima teknolojia ya zamani katika maeneo mengi , hii itapelekea kupunguza gharama za udhalishaji wa bidhaa zote zinazotumia raba kwa zaidi ya asilimia arobaini na tano, tulikubaliana katika kikao kuongeza hisa zetu ndani ya kampuni ya Taita kwa asilimia 4.3%”Meneja wa idara ya uwekezaji alisoma ripoti kwa haraka.
Regina alipitia nyaraka ambayo alikuwa amekabidhiwa haraka haraka na baada ya pale aliitupia kwenye lift na ukauzu ukamvaa.
“Uza hisa zote tunazomiliki ndanni ya kampuni ya Taita”Aliongea na kauli ile ilimfanya meneja kushangaa , kana kwamba amesikia vibaya.
“Mkurugenzi kwanini kuuza katika wakati muhimu kama huu?”
“Bidhaa zao zinaenda kupoteza thamani muda si mrefu na kudorora sokoni hivyo hisa zao kushuka”Aliongea na kauli ile ilimchanganya meneja.
“Umeshindwa kuona mabadiliko ya wafanyakazi ndani ya kampuni ya Taita , unadhani ni kwanini idara ya usafirishaji imeongeza wafanyakazi katika maghala yao?”
“Kwasababu uwezo wao wa kudhalisha umefika mwisho , hivyo presha ya bidhaa kuwa kubwa kuliko uwezo wao.., kwanini sikulifikiria hili”Aliongea yule Meneja huku akijiona mzembe .
Meneja yule kabla hata hajaanza kutaka kumsifia Regina kwa uwezo wake wa kuona mbali Linda alikuwa ashabonyeza kitufe tayari na lift ilijifunga.
Ilienda kufunguka tena katika floor nyingine na Regina hakutoa kwenye lift lakini mbele yake kulikuwa na mwanamama wa makamo na alimkabidhi Linda nyaraka ambazo alimpatia Regina.
“Mkurugenzi!, Farida Group hawapo tayari kuhamisha umiliki wa ardhi kwetu, wanasema wanataka ongezeko la milioni mia mbili , tuchukue hatua gani?”
Regina palepale alichukua karamu ya rangi nyekundu na aliandika maandishi makubwa kwa lugha ya kingereza
“Waambie tutawaongezea mpaka milioni mia tano’
Mwanamama yule mara baada ya kuona maandishi yale alishangaa na aliona pengine Boss wake amekosea.
“Mkurugenzi wanataka ongezeko la thamani la milioni mia mbili tu”
“Fanya kama nilivyokuambia , kisha subiri mpaka wafanye maamuzi na kuja kwangu kwa ajili ya kusaini”
Mwanamama yule aliishia kutoa mdomo tu lakini aliishia kutingisha kichwa asijue bosi wake anachopanga ni nini.
Lift ilijifunga tena na Hamza ambae alikuwa amesimama nyuma ya Regina alikuwa kwenye dumbuwazi na alishikwa na shauku ya kutaka kujua kauli ile ilimaanisha nini.
“Mkurugenzi au nimesikia vibaya , kama wanahitaji ongezeko la thamani ya milioni mia mbili kwanini uwaongezee mpaka milioni mia tano , inamaana unatoa milioni miatatu ya bure?”
Regina hakujibu swali lile kwani Lift ilikuwa ishafunguka tayari na kwa mara nyingine kulikuwa tayari na mtu aliekuwa akisubiri na alikabidhi nyaraka ambazo zilisainiwa na Regina.
Floor kwa floor mwanamke huyo alipita na kila floor alikuwa akifanya maamuzi na kuweka sahihi baadhi ya mambo kwa umakini mkubwa na mengi ya maamuzi yalikuwa kinyume na meneja wa idara husika lakini licha ya hivyo hakuna ambae alipinga maamuzi yake , ilikuwa ni kama vile walijua maamuzi yake yapo sahihi zaidi kuliko ya kwao waliokubaliana.
Kilichomshangaza zaidi Hamza ni namna
walivyofika katika floor ya juu zaidi baada ya kukutana na mama mtu mzima alieonekana kuwa na uzoefu wa muda mrefu lakini alitii kauli ya Regina bila ya kuuliza kabisa.
Baada ya kumaliza floor zote za jengo hilo , hatimae walifika floor ya juu kabisa ambapo ndio ofisi ya mrembo huyo hupatikana , ilikuwa ni ofisi kubwa mno yenye vioo vikubwa ambavyo havipitishi risasi
Kupitia madirisha hayo ya vioo alikuwa na uwezo wa kuona hadi maeneo ambayo yapo nje ya jiji la Dar es salaam.
Hakukuwa na mapambo mengi ukiachana na vyungu vya maua na shelf kadhaa za mafaili , yaani ilikuwa ofisi kubwa lakini vitu vichache na rangi yake iliendana na wajihi wa Regina kabisa.
Regina alikaa katika kiti chake cha kibosi huku kulia akiwepo Hamza na kushoto akiwepo Linda ambae alimkabidhi Regina nyaraka nyingine kuzipitia.
Regina alitumia muda mrefu kidogo kupitia zile nyaraka na Hamza alionyesha kuchoka hivyo alijikalia zake kwenye sofa huku akicheza game la pooltable kwenye simu yake lakini muda uleule Regina aliinua macho yake na kumwangalia.
“Linda mpatie nyaraka za Farida Group”Aliongea Regina na Linda alifungua faili kupitia kishikwambi na kumpatia Hamza ambae alianza kusoma mara moja
“Hii inahusu nini?”
“Si uliuliza swali kwanini nimeongeza pesa zaidi licha ya ongezeko la thamani waliloomba katika kipande cha ardhi nilichotaka kununua?”Aliuliza Regina na Hamza alitingisha kichwa.
“Sasa nakupa nusu saa unitafutie sababu kwanini nimefanya maamuzi hayo kupitia hizo taarifa za kiuchunguzi za kampuni ya Farida Group , ukifanikiwa utapatiwa ofisi ya kwako peke yako”
“Ofisi ya kwangu , unamaanisha itakuwa na tarakishi kabisa?”Hamza alikuwa na mpango wake , alijua ofisi kubwa kama hizo zina mtandao wa internet wenye spidi hivyo atatumia muda huo kutengeneza pesa online.
“Ndio, kila kitendea kazi”Aliongea na Hamza aliona vizuri na kwa haraka sana alianza kusoma taarifa hio.
Regina hakumjali tena , alichokifanya ni kwa ajili ya kumzuia Hamza kuwa bize kwa muda , akijua fika hawezi kupata sababu ndani ya muda wa dakika ishirini ,hata Linda mwenyewe alijua kabisa Hamza hawezi kutoboa na kujua sababu , lakini baada ya dakika tano Hamza alipumua kwa nguvu huku akijinyoosha.
“Nini tatizo?”Aliuliza Regina.
“Acha kumsumbua Mkurugenzi na sauti zako za ajabu”Aliongea Linda kwa kuonya
“Sio kama namsumbua , nishaona sababu tayari”
“Mh , nakupa nafasi nyingine tafuta kwa umakini”Aliongea Regina , hata Linda mwenyewe alijua haiwezekani kwa muda mchache hivyo , ukweli ni kwamba alijua Hamza hata hakumaliza kabisa kusoma taarifa yote maana ilikuwa na kurasa za kutosha.
“Farida ni kampuni ambayo ineonekana imara kwa nje lakini kwa ndani wapo katika hatari ya mlolongo wao wa kimapato . kama hii ardhi hawatoiuza mapema ili kupata pesa , kuna uwezekano wakafirisika”Aliongea Hamza na kauli ile ilimfanya Regina kumkazia Hamza macho
Katika akili yake alikuwa akishangaa na kujiambia yaani ndani ya dakika tano tu alikuwa ashaona taarifa iliojificha ya namna hio katika nyaraka hio , spidi yake ya kusoma aliona ni ya kutisha mno.
Linda hata yeye alikuwa kwenye mshangao , hakuamini kama Hamza aliweza kumaliza kusoma tayari hio nyaraka ndani ya dakika chache.
“Murugenzi niseme tu mbinu yako ni kuntu sana , kama ungeongeza milioni mia mbili kama walivyohitaji wangekuuzia haraka , lakini kitendo cha kuongeza milioni mia tano zaidi watapatwa na mashaka na kujiuliza kwanini unataka kununua ardhi yote kwa gharama kubwa kiasi hicho , watajiuliza au kuna kitu ambacho hawakuzingatia kuhusu hio ardhi ambacho kinaweza kukupa faida kubwa , kwa mbinu hio watasita kwanza kuuza ili wajue sababu ya wewe kutaka kununua kwa gharama kubwa , lakini wakati huo hakuna kampuni ambayo itakuwa tayari kununua ardhi kwa bei kichaa kama hio , hivyo wasiwasi wao utawafanya kupitisha siku muhimu ya kuuza na siku watakayo ona wakuuzie kwa ongezeko la milioni mia tano , unachofanya ni kuwakataa tu kiana na hawatakuwa na jinsi tena , mwishowe watakuuzia kwa thamani ya mwanzo kabisa, hawatokuwa hata na ubavu wa kuomba kuongezewa milionni mia mbili nyingine kwasababu hawana muda wa kutafuta mnunuzi mwingine”
Baada ya Hamza kumaliza kuongea Regina macho yake yalionyesha ishara ya kuridhika na jibu lake , aliona hakuwa amekosea tokea mwanzo , ijapokuwa Hamza anaonekana kama mwanaume muhuni muhuni mwenye tamaa na mbahili lakini akili yake ilikuwa ikifanya kazi vizuri , anao uwezo wa kujifunza na kuelewa kitu kwa haraka na kwa tabia hio ana uwezo wa kufanya jambo kubwa baadae. Hayo ndio yalikuwa mawazo ya Regina kwenda kwa Hamza.
Linda ambae alikuwa pembeni ya Regina alijikuta akishagnaa pia , aliona alikuwa amemchukulia poa huyo msaidizi mpya wa bosi wake lakini aliona yeye ndio alikuwa na makosa , inakuwaje bosi wake mwenye akili kubwa kutafuta mtu ambae hana uwezo , hivyo hakumpa sifa Hamza kwa kuwa na akili bali sifa alizielekeza kwa bosi wake kwa kuwa na jicho la ziada katika kujua uwezo wa mtu.
“Murugenzi, kama hii mbinu ikifanikiwa , nakuambia watu wa kampuni ya Farida watakuchukia kufa , watapata athari kubwa za mzunguko wa pesa ndani ya kampuni yao”Aliongea Hamza.
“Ukiwa mfanyabiashara , soko unalichukulia kama uwanja wa vita , kwasababu wao wenyewe ndio wameonyesha tamaa na kwenda kinyume na bei ya mwanzo , sidhani wanahaki ya kunilaumu kwa kutokuwa na huruma, pili kama wana akili ni kheri wakanifuata na kuniuzia ikiwa mapema , wakichelewa watakuwa wanajiingiza wenyewe katika mtego wangu kwa tamaa zao”
“Bosi , una akili sana , mtu wa kawaida hawezi kufikiria kwa namna yako”Hamza alimsifia.
“Hata wewe upo vizuri , sio mbaya umeweza kujua sababu ndani ya dakika tano tu”
Hamza mara baada ya kusifiwa kwa mara ya kwanza aliachia cheko lakini ambalo lilikuwa la kistaarabu kidogo
“Hamna , unajua nini bosi , mimi ni wa kawaida sana, akili yangu ipo ndani ya wastani wa kila mtu”
“Don’t be too arrogant , our CEO is a member of Pars Society , don’t think that just because you’re a little smart, you’re that great”Aliongea Linda kwa kujiamini kwa kingereza akimaanisha kwamba aache majigambo kwani bosi wake ni mwanachama wa Pars , hivyo kwa viakili vyake vidogo asijione mkubwa na kuanza kupandisha mabega.
Upande wa Hamza alishangaa mara baada ya kusikia Regina ni mwanachama wa Pars.
“Kwahio Boss wetu ni moja ya wanachama wa jamii za watu wenye IQ kubwa?”
“Unaonekana kujua mengi kama umeelewa sentensi
yangu , ndio bosi wetu ana IQ 180 hivyo huhesabika kama Genius , kama sio hivyo unadhani kwanini kila mtu ndani ya kampni anaamini maamuzi yake na kuyafauta?”
The Standard wisdom societies ni umoja ambao wanachama wake wana IQ kubwa, inasemekana ili kujiunga katika umoja huo mtu anapaswa kufikia angalau vipimo vya IQ kuanzia 175 na kuendelea , sio umoja ambao unaweza kujiunga kwa pesa na hadhi.
Kwa kadri ambavyo alikuwa akielewa watu ambao huhesabika kama Genius ambao IQ zao ni kuanzia 180 wana uwezo wa juu sana katika maswala ya kitafiti , ubunifu na biashara , lakini wakati huo huo wakiwa vibaya sana katika baadhi ya sehemu kiasi kwamba wanaonekana kama watu dhaifu.
Kwa lugha nyepesi ni kwamba majiniasi wanaweza kuwa juu ki uwezo aidha iwe katika maswala ya kitafiti au biashara lakini likija sehemu nyingine wanafanya vibaya sana , na hili linaweza kukushangaza, ki ufupi ni kwamba wanaonekana sio wa kawaida na maamuzi yao yanaweza kuwa ajabu mno.
Hamza aliweza kuliona hilo , hasa ukizingatia na tabia ya Regina mbele ya familia yake, alikuwa na mahusiano mabaya sana na baba yake.
“Huruhusiwi kuongea kuhusu jamii hio tena siku nyingine”Aliongea Regina na kumfanya Linda kufubaa kwa kuona alifanya kosa, lakini aliitikia kwa adabu.
Hio ndio moja ya sifa nyingine ya Regina , wafanyakazi wa kampuni hio walikuwa wakijua taarifa hio nyeti juu ya kuwa mmoja ya mwanachama wa jamii ya watu wenye busara na hawakuwa wakizungumzia hilo hadharani.
Sasa hata wakurugenzi wa bodi walielewa kwanini Mkurugenzi wa Zamani yaani babu yake Regina aliweka ngumu kumfanya msichana mdogo aliekulia katika kituo cha kulelea Yatima kuwa kichwa cha kampuni , kwa taarifa walizokuwa nazo alionyesha kuwa na akili isiokuwa ya kawaida tokea akiwa mdogo, kitu pekee ambacho wakurugenzi wa bodi hawakuwa wakifahamu ni ukichaa wa Regina, kutokana na Regina kuwa na akili nyingi ndio moja ya sababu ambayo ilimpelekea kuwa na ugonjwa wa nafsi mbili.
“Mnaweza kuondoka sasa, Linda muonyeshe Hamza ofisi yake”Aliongea Regina.
Hamza alikuwa na hamu ya kuona ofisi yake hivyo hakuwa na pingamizi na mkufuata Linda kwa haraka.
“Linda ,vipi kama nisingeweza kujibu , ni ofisi gani ningepelekwa?”Aliuliza Hamza mara baada ya kufikishwa katika ofisi ndani ya floor hio hio ambayo ilikuwa haina vitu vingi zaidi ya tarakishi ya thamni ya kampuni ya Apple na printer
“Haijalishi ungejibu kwa kukosea au kupatia , hii ofisi ndio niliandaa tokea juzi kwa maelekezo ya boss”
Hamza aliona kabisa Regina alikuwa akimchora tu , aliona kabisa Regia anatumia akili yake vibaya kumchezea akili.
Hamza mara baada ya kuchunguza tarakishi hio alitoa tabasamu , ilikuwa na sifa zote za kuitwa tarakishi yenye uwezo wa juu na kwa kuliona hilo alijua kabisa mpango wake wa kuvuna Bitcoin ungeenda vizuri sana. Mara baada ya kujinyoosha kwa kuanza kazi yake ya kutengeneza pesa, Linda aliingia akiwa na rundo la nyaraka na kuzitua mezani.
“Boss amesema unajua kuongea kifaransa kwa ufasaha , anataka utafsiri nyaraka zote kuwa katika lugha ya kingereza , ndio kazi yako utakayofanya kwanzia leo mpaka Ijumaa, ukimaliza print na niletee ofisini kwangu mlango unaofuatia”Aliongea katika sauti ya kiheshima.
Hamza alipitia nyaraka hizo kwa haraka haraka na aligundua ni taarifa za moja ya kampuni ya kifaransa na ilionekana ni nyaraka ambazo hazikupatikana kirahisi ndio maana hawakutaka mtu wa nje ya kampuni kuzitafsiri kutokana na unyeti wake.
“Huyu mwanamke , inaonekana alikuwa amepanga kunipa kazi tokea muda mrefu na sio kwasababu ya kumdanganya Eliza”Aliwaza Hamza mara baada ya kuona kazi ya kwanza ni kutafsiri kifaransa. “Naona sasa nina kazi ya kufanya”
“Hakikisha unafanya kazi na huleti uzembe , kampuni yetu inajali sana watu wachapakazi na sio watu wazembewazembe kazini”
“Sawa”
Alijibu Hamza lakini mara baada ya Linda kutoka Hamza alikimbilia mlango na kuufunga kwa ndani na kisha alirudi kwenye tarakishi yake na kuanza kazi ya kutengeneza mzingira ya kuvuna sarafu.
“Kama nilivyotarajia spidi ya hii internet ni kiboko”Alijiongelesha Hamza , lakini alishituliwa na simu yake ilioanza kuita , aliitoa mfukoni na mara baada ya kuangalia jina la anaepiga ni mama Iryn.
Hamza alishasahau kama alikuwa na mwanafunzi na ni kama simu hio ilimkumbusha alikuwa na miadi ya kumfundisha Iryn wiki hio.
“Habari za uzima mwanangu?”Sauti iliita , Mama Iryn alikuwa akipendelea kumuita Hamza mwanae.
“Salama kabisa mama , habari za nyumbani?”Hamza aliongea alikuwa na upole kabisa.
“Salama kabisa , wiki hii mwanafunzi wako alikungojea hujatokea , kanikumbusha nikupigie simu”Hamza mara baada ya kusikia kauli ile alishindwa kujua afanyaje , kama ingekuwa siku kadhaa nyuma asingekuwa na shida ya kujibu lakini muda huo ni mwajiriwa wa milioni kadhaa hakuona haja ya kwenda kufundisha.
“Naomba unisamehe sana mama , ila nipo field kwasasa , muda wa masomo unanibana sana , semister yetu hii ya mwisho mwisho”Hamza alijitetea , ndio namna pekee alivyoona ajibu. “Oh! , ndio nilichomwambia Iryn lakini hanielewi , mimi naelewa upo mwaka wa mwisho na unahitaji muda mwingi kujiandaa”
“Ni kweli kabisa mama , nahitaji muda wa kujiandaa”Aliongea Hamza , ukweli ni kwamba hajawahi hata kufanya discussion na wenzake , maisha yake ya chuo yeye ni kama vile anafanya utani , lakini likija test hajawahi kufeli.
“Basi hakuna shida baba yangu , nikutakie masomo mema na kujiandaa kwema”
“Asante mama nikutakie na wewe afya njema na masomo mema kwa Iryn”
Baada ya kuongea hivyo mama Iryn aliaga na kukata simu na kumfanya Hamza avute pumzi na kujiambia ni bora kukiepuka kikombe hicho,alijua kwenda kwa Iryn kwa vyvoyte vile ni kujiingiza kwenye majaribu ya mwanafunzi huyo wa Advance.
Hamza hakutaka kuwaza sana na alirudi kwenye kazi aliokuwa akitaka kuendelea nayo.
Baada ya kupoteza lisaa lizima kwenye mtandao wa Blockchain alirudi katika kazi ya kutafsiri , Hamza aliangalia nyaraka alizokuwa amepewa na aliona haikuwa kifaransa kigumu, ni kile cha kibiashara hivyo alikaa vizuri kwenye tarakishi na kuanza kuchapa kwa spidi kubwa , alikuwa na spidi sio ya kawaida na ndani ya masaa matatu bila ya kupumzika alikuwa amemaliza kila kitu na alipoangalia saa ilikuwa ni saa saba kasoro mchana, hivyo alimalizia kuprint kabisa.
Baada ya kumaliza alisimama na kuanza kujivuta vuta lakini ni dakika hio hio sauti kutoka nje pamoja na kugongwa kwa mlango ilisikika , alikuwa ni Linda aliekuwa akimtaka kufungua.
“Kwanini umejifungia?”
“Ofisi ni yangu ni maamuzi yangu kufunga na kufungua”Aliongea na kumfanya Linda amwangalie kwa kejeli huku akimpita na kusogelea tarakishi. “Ulichokuwa ukifanya umeficha wapi?”Aliuliza
“Nliichokuwa nikifanya, unamaanisha nini?”
“Ulikuwa ukicheza michezo yako ya Blockchain”
“Umejuaje nilikuwa nikifanya hivyo?”
“Unadhani idara ya IT inafanya kazi gani ,spidi ya Internet ilipungua kwa kiasi kikubwa na kufanya uanze kufuatiliwa unachofanya”
Hamza mara baada ya kusikia hivyo alijikuta akianza kujikuna kichwa na kuona ni ukatili kwa kampuni kufatilia kile wanachokifanya wafanyakazi ndani ya ofisi zao.
“Nimepewa maagizo nikakuripoti kwa Mkurugenzi na kulingana na sheria mshahara wako unakatwa asilimia ishirini”Mara baada ya kuongea kauli hio Linda aligeuza kutaka kuondoka.
“Hebu subiri kwanza , kazi ulionipatia nishaimaliza , kwanini mnikate mshahara , sikuwa na chakufanya ndio maana nikaingia kwenye vitu vingine”
“Unaongea nini wewe , yaani umemaliza kazi ya siku tatu ndani ya masaa machache?”
“Ndio , kama huamini angalia , sikupata muda tu wa kukukabidhi kazi”Aliongea Hamza huku akimpatia Linda katarasi ambazo ashamaliza kuziprint.
Linda alijikuta akishangaa mara baada ya kukagua karatasi hizo , zilikuwa zimeandikwa kwa usanifu mzuri sana tena kwa kingereza rasmi cha kikazi kabisa, lakini hata hivyo hakutaka kumuamini , aliingia kwenye mtandao na kujaribu kukopi na kupaste baadhi ya maneno ya kifaransa katika programu ya kutafsiria ili kuhakiki na kweli ilikuwa sahihi kabisa na aliishia kumwangalia Hamza kwa maswali mengi.
“Umewezaje kukamilisha kazi hii kwa muda mfupi tu?”Aliuliza na Hamza alitingisha mabega.
“Halafu kuna baadhi ya maneno yalikosewa kuandikwa , nimeyawekea alama na kisha nikayabadilisha wakati wa kutafsiri unaweza hakiki pia”Aliongea Hamza huku akimkabidhi Linda zile karatasi nyingine.
Linda aliishia kumwangalia Hamza kwa sekunde kadhaa na kisha akageuka.
“Ni muda wa lunch unaweza kwenda kula , nitampatia hizi nyaraka mkurugenzi”
“Subiri kwanza ,vipi kuhusu mshahara wangu sasa?”
“Kwa leo nitaacha hili lipite , ukirudia tena kufanya mambo nje ya utaratibu wa kazi kwa tarakishi za kampuni sitolifumbia macho”Aliongea na kisha alifungua mlango kutoka nje.
“Vipi wewe huendi kula , Mkurugenzi yeye anakula wapi?”
“Nipo kwenye diet , kuhusu mkurugenzi hali chakula mchana , hivyo jali mambo yako”Aliongea na hakutaka tena kuendelea kuongea na Hamza hivyo aliondoka.
Hamza licha ya kwamba alikuwa feki mbele ya Regina lakini kusikia kwamba hakuwa akila chakula cha mchana aliona mwanamke huyo anatia huruma na pengine jambo hilo hata Shangazi hakuwa akilijua la sivyo angekuwa mkali, lakini kwasababu hakuwa na chakufanya aliamua kupotezea na kutoka ndani ya ofisi yake na kwenda chini kabisa mgahawani .
Kampuni kubwa kama hio hakukuwa na haja ya kuongelea maswala ya maisha mazuri ya wafanyakazi wakiwa kazini , mgahawa wa kampuni ulikuwa mzuri mno na kulikuwa na kila aina ya chakula kizuri
Kila mtu alikuwa bize na chakula , wafanyakazi walikuwa wengi na baadhi yao walikuwa makundi makundi , kwasababu Hamza alikuwa mgeni yeye alienda zake kuchukua chakula na kisha kutafuta pakukaa.
Kampuni hio ni kama ilikuwa na upendeleo na wanawake kwani walikuwa wengi mno kuliko wanaume , Hamza licha ya kwamba alikuwa mgeni hakutaka kujitenga hivyo aliona sehemu sahihi ni mahali ambapo kuna watu ili kujenga kidogo mazoea.
Lakini kabla hata hajapata sehemu , aliitwa na kumfanya ageuke na hapo ndio aliweza kumuona Asha pamoja na msichana mwingine aliemfahamu kwa jina la Mirium , walikuwa ni wasichana ambao aliwakuta pamoja na Eliza wakiwa mwembeni Bar.
“Hello, nakuona Asha ulivyopendeza”Aliongea Hamza.
“Kwahio umemuona Asha tu , mimi hujaniona?”Aliongea Mirium huku akijifanyisha mwanamke mwenye wivu.
“Ndio”Alijibu Hamza akiwa siriasi na kufanya warembo wale kumshangaa kidogo na kisha waliangua kicheko.
“Eliza hajarudi kutoka safarini bado , lakini alituambia umepata kazi hapa makao makuu kama msaidizi namba mbili wa bosi , Hamza usitusahau kwenye ufalme wako”Aliongea Asha kwa tabasamu.
“Ah! , msinitegemee sana , mwenyewe sijui ni kwa muda gani nitafanya kazi , pengine ninaweza kufukuzwa ndani ya miezi mitatu tu”
“Sio kirahisi hivyo , kama umemfanya bosi kukupa kazi muhimu kama hio basi ni wazi upo vizuri
upstairs “
“Hebu acheni soga bwana , tutafuteni pakukaa kwanza muda unaenda”Aliingilia Mirium ambae alionekana kuchoka kusimama na kuachwa kwenye mazungumzo.
Baada ya kusogea upande wa kushoto mwa mgahawa huo Hamza aliweza kuona nafasi za wazi na kulikuwa na mwanamke mmoja tu aliekuwa akila peke yake na alimfahamu , alikuwa ni Kapteni Yonesi mkuu wa idara ya usalama wa kampuni.
“Twendeni pale”Aliongea Hamza, alitokea kumkubali Yonesi , ijapokuwa alikuwa na tofauti sana na wanawake wengi waliokuwa hapo ndani lakini ukauzu wake ulimfanya kuvutia , isitoshe alikuwa mrembo
“Unamaanisha tutakae na Kapteni Yonesi, Akha hatuendi pale sie”Aliongea Asha.
“Kwanini sasa , yule si mtu kwanini kama mnamnyapaa?”
“Ana sheria ngumu sana ukikaa nae kwenye meza , hataki muongee ongee wakati wa kula, hasa umbea umbea , yaani ukikaa nae Mjeda yule hakuna amani na chakula ni kama unakula sumu”Aliongea Mirium.
“Halafu ukimchokoza kidogo tu atakasirika , lazima akushikishe adabu , ni mkali mno mbele ya wafanyakazi , na hakuna wa kumfanya lolote maana anaaminiwa sana na Mkurugenzi”
“Hamza usije kujaribu bahati yako pale , kuna wenzako waliowahi kufika hapa na wakajifanya wana swaga na kuanza kutupia maneno pale , kilichowakuta ni udhalilishaji”Asha naMirium walikuwa wakipokezana kumjadili Yonesi na washasahau walikuwa wameshikilia vyakula mkononi.
“Kama nyie hamtaki kukaa pale , tafuteni eneo lingine mimi nitakaa”Aliongea Hamza na hakusubiri hata majibu yao na alitembea mpaka katika meza aliokaa Kapteni Yonesi.
Wafanyakazi waliokuwa ndani ya mgahawa huo waliona kitendo kile na kwasababu walishamjua Hamza ni mgeni , walitaka kuona kile kitakachotokea.
Yonesi alikuwa zake bize na chakula na mara baada ya kuhisi mtu kuongezeka katika meza yake ndio aliinua uso wake na alishangaa kumuona ni Hamza.
“Ni wewe?”
“Niambie Kapteni naona tunakutana tena”Aliongea Hamza akiwa na tabasamu na kukaa mkao wa kula.
“Kakae kwenye meza nyingine”Aliongea Yonesi , kibabe.
Comments