Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

CHANGE

A Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI NA TANO

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Efraim Donald akashangazwa na jambo hilo na kumshika Namouih mabegani, aliyekuwa ameachama huku pumzi zake zikiongezeka kasi zaidi.

"Nini Namouih?" Efraim akamuuliza.

"Ahh... a... aahaaaaah!" Namouih akaanza kulia kwa sauti ya juu sana.

Efraim Donald akamwahi kumshikilia kwa kuwa mwili wake ulishuka chini kwa njia iliyoonyesha ameishiwa nguvu. Mwanamke huyu akaendelea tu kulia kwa uchungu, na Efraim akiwa haelewi sababu, ikabidi aivute simu yake hapo chini na kuangalia kama aliyepiga bado alikuwepo, naye akaiweka sikioni baada ya kuona bado Blandina alikuwa hewani. Akamuuliza tatizo lilikuwa nini, naye Blandina akasema ndiyo alikuwa amepata taarifa za mauaji ya rafiki yao wa karibu sana, yule mpelelezi aliyeitwa Felix Haule. Efraim Donald alimfahamu pia, na alijua Felix alikuwa mtu muhimu sana kwa mke wake kama ilivyo Blandina tu, naye akampa Blandina pole na kusema angehitaji kumtuliza mke wake kwanza maana alikuwa ameishiwa nguvu kwa sababu ya taarifa hiyo.

Jambo jipya likawa limezuka. Felix Haule alikuwa ameuawa, na zilikuwa ni taarifa zilizomshtua sana Namouih hasa ukitegemea na ukweli kwamba walikuwa wametoka tu kuonana siku hiyo hiyo iliyopita, maana hii tayari ilikuwa ni siku mpya. Efraim Donald akamkumbatia mke wake wakiwa hapo chini, akimbembeleza kwa upendo na kumwambia aendelee tu kulia ili autoe uchungu wake wote, na ndipo hodi ikasikika nje kwenye mlango wa chumba chao. Efraim tayari akiwa anajua ni Esma, akamwambia aingie tu, na mwanadada huyo akaingia na kuwasogelea huku akiwa na sura iliyoonyesha kujali sana. Efraim Donald akamwambia kwamba Namouih amefiwa na rafiki yake wa karibu sana, naye Esma akashuka hapo chini na kumshika Namouih begani kwa huruma.

Baada ya dakika chache Efraim akajitahidi kumnyanyua mke wake na kumpeleka kitandani, akiwa anamtia moyo na kumbembeleza, na Namouih alikuwa analia bado huku amemlalia Efraim kifuani. Esma akawa ameondoka baada ya Efraim kumwambia akapumzike tu ili asubuhi waanze kufanya mipango ya kwenda kukutana na familia ya Felix. Namouih akawa analia kwa sauti ya chini kadiri muda ulivyoendelea kusonga, mume wake akiwa amemkumbatia kitandani na kumpa faraja kwa kutembeza kiganja chake kwenye nywele zake taratibu mpaka Namouih alipobebwa na usingizi
ilipofika saa kumi usiku. 

Yaani mwanamke huyu alikuwa amelia kwa masaa mawili mfululizo, kwa sababu jambo lililokuwa limetokea lilimtia huzuni kuu moyoni kwa kuwa tayari alikuwa ameshapigia picha ni nini kilichomsibu Felix ingawa hakuwa na taarifa kamili. Ingetakiwa kusubiri kukuche ili kujua mwanaume yule alipatwa na masaibu gani, na baada sasa ya Namouih kusinzia, Efraim Donald akautafuta usingizi pia.


★★★


Siku ikakucha zaidi. Hii ikiwa ni Jumapili, Efraim Donald na Namouih waliamka na kuanza kujiandaa ili kwenda nyumbani kwa Felix pamoja na Esma pia. Namouih alikuwa ameamka saa mbili tu, na kwa sababu ya huzuni alishindwa kuhisi lepe lingine la usingizi ingawa alilala kwa masaa machache. Efraim akawa amemtia moyo tena kwa kuwa alifahamu jinsi mambo haya yalivyomtikisa sana mke wake, na Namouih kiukweli alikuwa ameishiwa raha kabisa. Efraim Donald akawa amewasiliana na Blandina, ambaye alimjulisha kwamba yeye pia alikuwa anaelekea kule, hivyo wangeona jinsi mambo yalivyokuwa mpaka kupelekea kifo cha rafiki yao. Safari nzima ya kuelekea huko Namouih hakusema lolote lile ingawa Efraim alijaribu kumsemesha. Suleiman ndiye aliyewaendesha wote kwa gari la Efraim Donald na kuwafikisha mpaka upande wa mji ambako familia ya Felix iliishi kwenye mida ya saa sita mchana.

Walikuta watu wengi wakiwa wamekusanyika hapo nyumbani kwake na kufanya mambo kama jinsi taratibu za msiba zinavyokwenda, na baadhi ya marafiki na ndugu zao waliowafahamu Efraim na Namouih
waliwappkea na kuanza kufarijiana. Namouih akaelekea ndani ya nyumba pamoja na Esma, na huko alimkuta Blandina akiwa pembeni ya mke wake Felix, aliyeitwa Oprah. Mwanamke huyo alikuwa analia tu kwa sauti ya chini huku akiwa ameketi kwa kuishiwa nguvu, na
binti zake wawili walikuwa karibu wakimpa faraja kwa kulia pamoja naye. Alikuwa na watoto watatu pamoja na mume wake marehemu; wa kiume mwenye miaka 14, na hao wasichana wawili mapacha wenye miaka 10. 

Mama yake mzazi na ndugu wa kiukoo walikuwepo hapo pia, na baada ya Namouih kumfikia akamkumbatia na kumfanya Oprah aanze kulia kwa uchungu zaidi. Walikuwa wanafahamiana na kupendana sana, naye Namouih akawa anamwambia maneno yenye kufariji huku naye akidondosha machozi, kisha akawakumbatia na binti zake Oprah. Mwana wake alikuwa mkoa wa mbali kimasomo na ndiyo alikuwa safarini wakati huu pamoja na mjomba wake kuja huku baada ya kupata taarifa za kifo cha baba yake, kwa hiyo alikuwa akisubiriwa pia.

Muda mfupi baadaye, Mwantum, yule mwanamke ambaye mume wake na mwana wake waliokoka ajali ya barabarani, akawa amefika hapo pia kutoa faraja kwa Oprah. Efraim Donald, Namouih na Blandina wakawa wametoka nje ili kuzungumza kidogo, kwa sababu Namouih alitaka kujua undani
wa kifo cha Felix kutokana na Blandina kusema kwamba "aliuawa." Taarifa alizokuwa amezipata ni kwamba Felix aliuliwa usiku wa kuamkia leo, na mwili wake ulikuwa umepatikana ndani ya choo cha kulipia ambapo ulikuwa umekatwa tumboni na kunyofolewa ulimi. Namouih na Blandina walielewa wazi kwamba huo ndiyo mtindo ambao muuaji au wauaji wa wasichana wale wadogo walitumia, na Namouih akawaza kuwa kwa sababu Felix alikuwa anapeleleza jambo hilo inawezekana alikuwa amekaribia sana kupata ukweli ndiyo maana akauawa namna hiyo.

Blandina alikuwa anaongea kwa huzuni sana, akisema anahisi hii kuwa ni ndoto kwa maana walikuwa wametoka kumwona tu saa chache walipokutana naye kwenye kumbi moja ya starehe kisha ndiyo akaja kupewa taarifa hizo baadaye usiku zilizomshtua sana. Namouih akamuuliza alikuwa na nani wakati alipomwona Felix, naye Blandina akajibu ni Draxton. Namouih akakunja ngumi kwa nguvu sana, akiwa ameingiwa na hasira nyingi kwa sababu alielewa kabisa kitu hicho kilihusiana moja kwa moja na kifo cha rafiki yake. Yaani, alijua na alijua kwamba ni Draxton ndiye aliyemuua rafiki yake, na kutambua jambo hilo kukamfanya aanze kulia tena, lakini zamu hii kwa hasira. Efraim akajaribu kumbembeleza na kumwambia atulize hisia, lakini Namouih akaondoka tu hapo walipokuwa na kwenda kujifungia ndani ya gari lao.

Aliwaza mengi sana mwanamke huyu. Aliendelea kulia kwa uchungu mwingi sana kwa sababu ya kuhisi kwamba ni yeye ndiye aliyemsababishia Felix maafa hayo ambayo yalikuwa na athari mbaya sana kwa familia yake aliyoiacha. Lakini kwa jambo hili asingekaa tu na kuendelea kulia, alitaka afanye yote kuhakikisha muuaji wa Felix analipia kwa ubaya huu alioufanya. Jinsi alivyowaona wengine wakiwa bila wazo lolote kumhusu mtu aliyehusika kulimuumiza sana, hasa Blandina, ambaye alimwona kuwa kipofu kwa kumwamini mwanaume yule mwenye roho ya kikatili. Hivyo ndivyo Namouih alivyohisi, na sasa akawa amejiamulia kuwa ni lazima tu haki ingetendeka wakati huu tofauti na ilivyokuwa kwa Agnes.

★★

Shughuli za msiba ziliendelea siku hii, na Namouih pamoja na wapendwa wake waliendelea kuwa hapo mpaka usiku, kisha Efraim Donald akarudi nyumbani pamoja na Namouih. Mwili wa Felix ulikuwa mochwari, na ulifanyiwa uchunguzi na wengi wa wapelelezi waliofahamiana naye kubaini kile kilichompata, yaani muuaji alikuwa nani, lakini hakukuwa na jambo lolote lililowaongoza kwa muuaji huyo. Walijaribu kuchunguza eneo lile la choo cha kulipia, wakamuuliza aliyefanya kazi pale kuhusu watu walioingia na kutoka wakati ambao mwanaume huyo aliingia ndani ya choo hicho, lakini haingekuwa rahisi kwa mhudumu huyo kujua na kukumbuka watu walioingia na kutoka, kwa kusema kwa usiku ule watu walikuwa wengi, labda kama angewaona tena.

Hakukuwa na viambishi vyovyote kumhusu muuaji vilivyopatikana mwilini mwake Felix, lakini ilieleweka kwamba muuaji wake ndiyo yule yule aliyemuua Agnes pia, kwa kupenda kuwakata watu ulimi na tumbo. Ilikuwa inashangaza sana kwamba matukio haya yaliendelea kwa muda huu wote bila kubaini mhusika ni nani, kwa hivyo bidii ingehitajika zaidi ili kuzuia maafa hayo, na Namouih alikuwa ameazimia kuukomesha mchezo huu kwa sababu yeye tayari alimjua mlengwa wake.


★★★


Jumatatu ikafika. Namouih na Blandina wasingekwenda kazini siku hii, hata Efraim Donald pia. Walikwenda msibani tena, na wakati huu watu waliokwenda kutoa pole zao walikuwa ni wengi sana, kwa sababu Felix alijulikana kwa idadi kubwa ya watu. Mwanaye wa kiume alikuwa amekwishafika pia, na tayari matayarisho ya mwili wa marehemu yalikuwa yamemalizika kufikia muda wa saa tisa alasiri kule hospitalini, ukiwekwa ndani ya jeneza maridadi, kisha ungepelekwa hapo nyumbani, halafu ungelala ili kesho ndiyo usafirishwe kupelekwa mkoa aliozaliwa Felix ili kuzika. Familia yake ingekwenda huko, na walikuwa wameamua tu kumzika Felix mapema na kuendelea kusubiri matokeo ya uchunguzi wa kifo chake.

Mwili ulipofikishwa nyumbani tena vilio vya huzuni vilitawala kutoka kwa familia ya mwanaume huyo, na ilimchoma sana Namouih kwa sababu ya hatia aliyohisi moyoni mwake. Aliona ni kama hakustahili kabisa kuwa hapo kwa sababu ya kuchangia kifo cha Felix, lakini hakuwa na namna ila kuwepo na kutoa mchango wake wa faraja kwa familia hii ya rafiki yake. Inafika saa kumi hivi jioni baada ya mwili kuingia nyumbani hapo ndiyo Namouih akapata kuliona gari lisilokuwa geni sana machoni mwake likifika maeneo hayo ya nje. Hisia kali zilianza kumwingia mwanamke huyu baada ya kumwona Draxton akitoka ndani ya gari hilo na kusimama karibu nalo, naye Namouih akasimama huku akimtazama kwa mkazo mkali.

Blandina alikuwa ameshamwona Draxton kule alikosimama, hivyo akamfata haraka na kumkumbatia huku baadhi ya watu wakiwatazama sana. Wawili hao wakaonekana wakiongea, naye Namouih akaanza kuelekea hapo walipokuwa akiwa anatembea kama mtu anayehisi baridi kali. Efraim Donald alikuwa anamwangalia mke wake na kuona jinsi alivyotembea, na kwa haraka akawa ametambua kwamba kuna jambo halikuwa sawa. Akatoka sehemu aliyokuwa na kuanza kumfata pia. Namouih akawa amefika mbele ya Blandina na Draxton, naye Blandina akamgeukia na kumwangalia kwa njia ya kirafiki usoni, lakini Namouih akawa anamtazama Draxton kwa mkazo
sana mpaka Blandina na Draxton wakatazamana kama kuulizana 'vipi?'

Blandina akamwangalia tena rafiki yake na kumuuliza, "Vipi Nam?"

Draxton akawa anamwangalia Namouih kwa umakini.

Kuna kitu fulani kuhusu namna Draxton alivyomwangalia Namouih kilichomtia hasira sana mwanamke huyu na kumfanya amsogelee karibu na kumwasha kofi zito usoni!

"Namouih!"

Blandina akaita hivyo akiwa ameshtushwa sana na kitendo hicho cha rafiki yake, na ni hapo ndiyo Efraim Donald akawa amewahi na kumvuta mke wake nyuma kidogo. Blandina akamwangalia Draxton na kumwona akiwa ameinamisha uso wake kidogo tu, akitazama chini kwa njia ya kawaida, naye akamwangalia Namouih tena.

"Unafanya nini Namouih?" Blandina akauliza.

"Muuaji mkubwa wewe!" Namouih akamwambia Draxton kwa hisia.

Watu walioona jambo hilo wakaanza kusogea upande huu waliokuwepo.

Draxton akamtazama tena Namouih kwa umakini.

"Yaani wewe ni mfano halisi wa Shetani! Imekupa faida gani kumuua?" Namouih akasema huku akijitahidi kujitoa kwenye mikono ya Efraim.

"Namouih... unatengeneza scene hapa... naomba tuondoke," Efraim Donald akamwambia hivyo mke wake kwa kung'ata meno.

"Halafu unakuja kabisa hapa ili kuthibitisha nini? Kwamba hauhusiki au?" Namouih akasema kwa hasira.

"Namouih..."

Akawa amefika mama yake Oprah hapo na kumwita hivyo, naye Namouih akamtazama.

"Nini kinaendelea hapa?" mama yake Oprah akauliza.

"Aa, samahani mama. Namouih hajisikii vizuri... Namouih, naomba tuondoke," Efraim Donald akaongea.

Namouih akajitoa mikononi mwa Efraim kwa nguvu na kusema,

"Mama, unamwona huyu mwanaume? Usimwamini... yaani hapaswi kuaminiwa... ni huyu ndiyo amemuu...."

Kabla Namouih hajamaliza maneno yake, akashikwa mkono na Blandina kwa kugeuzwa, na alipomwangalia tu, Blandina akamtandika kofi usoni pia!

"Blandina..." Efraim akaita hivyo na kumshika tena Namouih.

Draxton akamsogelea Blandina na kumshikilia mikono pia kutokea nyuma.

Namouih akamwangalia rafiki yake kwa mkazo huku akiwa amejishika shavuni, naye Blandina alikuwa anadondosha machozi huku akipumua kwa hasira, na akimtazama Namouih kwa hisia kali sana. Watu walikuwa wameanza kukusanyika zaidi hapo wasielewe kilichokuwa kinaendelea, naye Efraim Donald akamtoa Namouih hapo kwa nguvu na kumpeleka garini kwao. Mama yake Oprah alikuwa anamtazama sana Draxton, na wakati huu mwanaume huyu alikuwa anamfuta machozi Blandina, kisha kwa kumkumbatia akaanza kuondoka naye kuelekea mpaka kwenye gari lake Blandina, akamsisitiza aingie tu na kuliwasha, halafu yeye Draxton angerudi kwenye lake ili waondoke hapo wakifuatana.

Baada ya Efraim Donald kumwingiza Namouih kwenye gari akampigia simu Esma, ambaye alikuwa ndani kule kwenye nyumba ya Felix, na kumwambia arejee kwenye gari ili waondoke. Efraim akawa amejishika kichwani huku amefumba macho yake kutokana na kutoamini kioja kilichokuwa kimetokea, kisha akamtazama mke wake na kumwona ameangalia upande wa kioo cha mlango wa gari huku analia kwa kwikwi. Alikuwa ameshindwa kuzizuia hisia zake pale na kusababisha picha mbaya sehemu ya msiba, lakini kiukweli roho ilikuwa inamuuma sana. Alikuwa amechoshwa na unafiki mwingi uliomzunguka, na tena na hapo alijua mwisho wa siku ni yeye ndiyo angeonekana mbaya. Blandina kumpiga kofi ilithibitisha hilo.

Safari ya kuanza kurejea makwao ikaanza baada ya Esma kufika ndani ya gari. Efraim Donald akamtazama mke wake kwa hisia, kisha akakishika kiganja chake kwa ustaarabu, naye Namouih akamwangalia. Mwanamke huyu alikuwa anamtazama mume wake kwa huzuni sana, naye Efraim akamvuta kwake, akimlaza kifuani na kuanza kumbembeleza taratibu. Akawa anamwambia kwamba ingawa kitendo kile hakikuwa sahihi lakini alimwelewa vizuri, na zile zilikuwa ni hisia tu zilizopaswa kuongozwa vizuri kwa sababu zikizidi sana matokeo yake ndiyo yanakuwa hayo. Akamwambia aache kumlaumu Draxton hata kama alihisi vipi kwamba ni yeye ndiyo msababishi wa haya yote, kwa sababu hakuwa na ushahidi wa kuonyesha madai yake kuwa kweli. Hicho tu.

Wakaendelea tu na safari yao huku bibie akiendelea kubembelezwa mpaka walipofika nyumbani, naye Esma akaanza kuandaa masuala ya chakula kwa kuwa hawakula kule walikotoka. Lakini Namouih yeye akaamua kwenda kulala tu kwa kukosa hamu ya kula, na mume wake akamsindikiza chumbani mpaka mwanamke alipojilaza na kuanza kuutafuta usingizi ili ayakimbie kwa kitambo kifupi mambo yaliyotokea awali nyumbani kwa Felix.


★★


Blandina na Draxton walielekea mpaka pale alipoishi mwanamke huyu baada ya kuondoka kule msibani kwa mtindo wa ukweli! Blandina alikuwa na huzuni sana, akihisi kama vile kilichotokea pale msibani ilikuwa ni ndoto, kwa sababu hakufikiri kwamba Namouih angeweza kufanya jambo ile lililosababisha na yeye Blandina afanye jambo ambalo hakutaka kufanya. Draxton akaenda pamoja naye ndani, na alipotaka waingie sebuleni, Blandina akasema angependelea zaidi kulala chumbani, hivyo wakaenda wote, naye Draxton akajilaza kwa njia iliyomruhusu Blandina amlalie kifuani, na mwanaume huyu akawa anapitisha kiganja chake mkononi kwa mpenzi wake taratibu.

"Utakuwa sawa?" Draxton akavunja ukimya.

"Ndiyo... nafikiri nitakuwa sawa," Blandina akajibu kwa sauti ya chini.

"Samahani Blandina..."

"Samahani ya nini?"

"Kwa kilichotokea. Labda ingekuwa bora kama nisingekwenda pale."

"Hivi, Namouih ana tatizo gani na wewe? Jana... umeondoka, ukasema... mlivyoonana si yalikuwa maongezi mazuri? Hayo anayoyasema yametoka wapi? Yaani me simwelewi Draxton kwa kweli. Amenifanya nimefikia yaani...."

"Usiwaze sana Blandina... ni huzuni yake tu ndiyo...."

"Kwani sisi wengine hatuna huzuni Draxton? Lakini umeona mimi namfata mume wake na kusema ndiyo amemuua Felix? Yaani yeye... anachofikiri ndiyo ukweli ndiyo hicho hicho, anataka sikuzote judgement yake ndiyo iwe sahihi tu... si vinginevyo. Isingekuwa ya wewe yule Japheth tungemfunga wakati hakuwa na hatia, na hapo Namouih bado angejiona kuwa sahihi kabisa. Ndiyo anachotaka kufanya na sasa hivi... kila kitu Draxton, kila kitu Draxton, sijui huwa anataka nini...."

"Basi, Blandina please... usi... anaumia tu. Unajua huzuni ya kufiwa huwa ina-impact watu kwa njia tofauti..."

Blandina akanyanyua uso wake na kumwangalia machoni. "Kwa hiyo unataka kusema alichofanya ni sawa kabisa?"

"Si hivyo..."

"Ila nini sasa? Acha kujifanya una huruma sana Draxton, amekuaibisha mbele ya wengi wasiotufahamu. Siku moja ukipita mbele za watu wanaanza kukunyooshea vidole, yule pale alifanya hivi, yule pale alifanya hivi, kwa sababu tu ya mtu kusema vitu asivyokuwa na uhakika navyo kukuhusu wewe... na vya uwongo," Blandina akaongea kwa mkazo.

Draxton akajiketisha vizuri na kumshika Blandina kiunoni taratibu ili amnyanyue na kumfanya aketi pia, nao wakawa wanatazama kwa ukaribu sana.

"Kuna mambo mengi yanayomchanganya yule mwanamke... anajikuta katikati ya eneo ambalo kila mara akitazama upande fulani na kufikiri ndiyo barabara sahihi ya kuondoka, barabara zingine zinatokea... na hivyo anashindwa kujua ipi ndiyo sahihi zaidi. Anapopita kwenye ile anayodhani ni sahihi, anapotea, lakini anaona kurudi nyuma ni ngumu mno... kwa hiyo anakazana kuipita hiyo hiyo tu akijiaminisha kwamba bado yuko njia sahihi. Wewe Blandina... unaijuia njia sahihi, unaujua ukweli, Namouih haujui. Unajua kwamba usiku huo wote mimi na wewe tulikuwa pamoja, tukalala pamoja, tukaamka pamoja... Namouih halijui hilo. Anadhani yuko sahihi kuona mambo namna
yoyote anayoyaona, lakini wewe unatakiwa kumfanya auone ukweli ili... asipotee," Draxton akamwambia kwa hisia.

"Lakini tayari ameshapotea Draxton...."

"La... hajapotea. Kama navyokwambia, anakazana kupita huko anakodhani ni sahihi, ila wewe ndiyo wa kumshika mkono na kumvuta atoke huko. Nachojaribu kusema ni kwamba... anakuhitaji. Jaribu tu kumwelewa. Wewe kuliko mtu yeyote unajua kwamba Namouih amepitia mengi, ndiyo maana
yuko kama alivyo..."

"Nakuelewa Draxton. Lakini amevuka mipaka. Mtu unafika tu, anaanza kukurushia maneno, tena hadi anataka kumwambia mama ya mfiwa kwamba wewe ndiyo umemuua mume wa mtoto wake kweli? Ah-ah..." Blandina akaongea kwa kuudhika.

Draxton akaushika uso wake na kumwangalia machoni kwa upendo. "Zile zilikuwa ni hisia Blandina. Anaumia. Nimefurahi tu kujua kwamba unaniamini ingawa... mambo mengi kuhusu mimi... ni fumbo. Lakini maneno ya watu yasikusumbue. Wewe na Namouih ni kama dada, najua unampenda sana. Mfanye auone ukweli hata kama akisisitiza vipi kwamba tayari anaujua... you are
good at that. Kwa hiyo nakuomba uniahidi kwamba utajaribu kuyanyoosha mambo kati yako na yeye kesho... tafadhali. Hiyo haitamsaidia Namouih na wewe pekee kuwa na amani... bali na Felix pia."

Blandina alijawa na faraja yenye simanzi sana kwa sababu ya maneno hayo yenye kugusa moyo kutoka kwa Draxton, naye akaulaza uso wake kwenye shingo ya mpenzi wake huyo. Draxton akawa anatembeza kiganja chake taratibu kwenye kiuno cha Blandina, na kwa kadiri kubwa hii ikafanya mwanamke apandwe na hisia za kimahaba. Akaunyanyua uso wake na kuigusisha midomo yake sikioni kwa Draxton, halafu akabusu sehemu ya chini ya sikio hilo kwa hisia sana. Draxton akaushika ubavu wake, akiwa na lengo la kumvuta kidogo ili amkumbushe kwamba hawangepaswa kupitiliza, lakini alimshika na kumbinya kwa njia iliyofanya Blandina asisimke sana, na mwanamke huyu akaanza kumbusu shingoni, shavuni, na kumfata midomoni akidhani Draxton alikuwa anamwamshia hisia zake pia.

Kutokana na uzito wa hisia aliokuwa nao, Blandina akaendelea kumbusu Draxton kimahaba sana mdomoni mwake, naye Draxton akawa anambusu kwa upendo pia. Blandina alipoanza kuongeza kasi, Draxton akajitoa mdomoni mwake na kumwangalia machoni. Mwanamke alikuwa anamwangalia kwa hamu sana, na hii ikamfanya Draxton aone kweli alihitaji kujaribu tena kwa
wakati huu kumpa kile alichohitaji.

"Taratibu..."

Draxton akamwambia hivyo kwa sauti ya chini, naye Blandina akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa. Wakarudia tena penzi lao la mdomo, huku sasa mambo yakienda taratibu kweli, naye Blandina akapitisha miguu yake pande za mapaja ya Draxton ili awe kama amemkalia katikati, huku akiendelea kumpiga busu. Wakati huu ilionekana kweli Draxton alitaka sana kumpa penzi mwanamke huyu, na tayari Blandina alikuwa anafurahia mno hatua hii waliyofikia. Wakiwa wanaendelea kupiga busu Blandina akaanza kuufungua mkanda wa suruali ya Draxton kwa kupitisha mikono yake kwa chini, huku mwanaume akiwa amekishikilia kiuno cha mrembo na kulichezea kalio lake kubwa kwa viganja vyake. Blandina akawa amefanikiwa kuingiza kiganja chake ndani ya suruali ya Draxton na kuishika sehemu yake ya siri, lakini hapo hapo akautoa mkono
wake upesi.

Draxton alikuwa ameanza kuchemka tena, na hapa ndiyo wakaivunja busu yao, Blandina akimwangalia usoni kwa kujali, na Draxton akitazama chini huku akipumua na kukaza macho kama vile kuonyesha anaumia. Blandina alimtazama kwa huruma sana asielewe ni kwa nini jambo hili lilikuwa linampata mpenzi wake kila mara walipojaribu kuonyeshana upendo, na alipokuwa
anataka tu kusema kitu, Draxton akajivuta nyuma na kufanya Blandina ajitoe hapo alipokuwa amemkalia na kujiweka pembeni. Draxton akawa amefumba macho yake huku akipumua kwa nguvu kiasi, naye Blandina akamsogelea mgongoni na kupitisha mikono yake kiunoni kwa jamaa.

"Samahani Blandina.... nahitaji kwenda..."

Draxton akasema hivyo kwa sauti tetemeshi kiasi, na kiukweli Blandina alikosa hata cha kusema na kuitoa mikono yake kiunoni kwa mpenzi wake huyo. Mwanaume akajitoa kitandani hapo na kusimama kwa ufupi, akiwa amempa mgongo Blandina kama anafikiria jambo fulani, na mwanamke huyu akawa anataka kusikia atakachosema.

"Nitakupigia."

Draxton akaongea tu hivyo bila kumwangalia na kuondoka ndani ya chumba hicho.

Blandina akainamisha uso wake kidogo, kisha akajitupia kitandani hapo na kutazama juu akiwa anatafakari vitu vingi. Kuwa na mtu kama Draxton kulimridhisha sana kihisia kwa kuwa alionekana kuwa na moyo mzuri mno, lakini tena kila mara alipotaka kufurahia zaidi upendo wake kwake kwa njia hii jambo hilo lingezuka, na mwanaume mwenyewe alionyesha kutotaka kutafuta suluhisho. Hali hii ingeendelea hivi mpaka lini? Blandina akajiahidi kufanya yote yaliyokuwa ndani ya uwezo wake kujua na kusaidia kusuluhisha kile kilichomtatiza mpenzi wake, lakini kwa sasa, angehitaji kujitahidi kurudisha hali ya amani baina yake na Namouih kama tu Draxton alivyokuwa amemshauri.


★★★


Namouih anafumbua macho yake na kujikuta akiwa ndani ya kitu kilichoonekana kama sanduku la chuma, akiwa amelala chali na mwili wake ukihisi baridi sana. Yaani alikuwa amenyooka, na alipojaribu kunyanyuka akatambua kwamba ilikuwa ni ndani ya chumba kidogo sana sehemu hiyo aliyolala iliyoubana mno mwili wake, naye asingeweza kunyanyuka hata kidogo. Alihisi ni kama vile amelala ndani ya jeneza, na jambo hilo likamfanya aingiwe na hofu kubwa. Akaanza kupiga kelele na kilio cha kuomba msaada, ndipo akahisi kifaa hicho kinavutwa kwa nyuma, na mwili wake ukarudi nyuma pia.

Kifaa hicho kiliposimama, yeye akiwa amelala vile vile chali, akaanza kuona namna ambavyo sehemu hiyo ilikuwa na umaridadi wa kiasi fulani, na kwa haraka akajinyanyua kwa kujivuta nyuma ili apatazame vizuri zaidi. Kwa macho ya haraka akawa ametambua kwamba alikuwa ndani ya chumba cha kutunzia maiti, yaani mochwari, na alipoangalia sehemu aliyokuwa akatambua ilikuwa ni kwenye masanduku ya kutunzia miili ya maiti yaliyokuwa kama majokofu ili miili isiharibike, naye akajitoa hapo haraka na kuanguka chini. Kweli kulikuwa na sehemu zenye meza za matairi ambazo angeweza kuona miili mibichi ya watu waliokufa ikiwa imelazwa hapo, mingine ikiwa imekatika katika viungo na hata mifupa ya viunzi, naye akaanza kutembea kuelekea pale alipouona mlango huku akijitahidi kutoangalia mambo yote hayo yaliyohofisha.

Alipoufikia mlango akaufungua upesi na kutoka nje ili aondoke ndani ya mochwari hiyo, lakini akajikuta anakanyaga sehemu yenye majani kwenye eneo lenye giza sana, naye alipogeuka nyuma akashangaa sana baada ya kukuta chumba kile cha mochwari kimetoweka kabisa; kana kwamba hakuwa ametoka huko muda mfupi tu. Akaingiwa na hofu zaidi, lakini akajiimarisha kwa kutoa sala kimoyomoyo, kisha akaanza kujipapasa mwilini ili kuona kama alikuwa na simu yake hapo, awashetochi, lakini hakuwa nayo. Ni katika kujipapasa huko ndiyo akawa ametambua kwamba mwili wake haukuwa na nguo hata moja, naye akaanza kuwaza kwamba huenda na hapa alikuwa akiota.

Eneo hilo lilikuwa na giza zito na kimya kikali sana, naye akaanza kupiga hatua kwenda mbele huku akiyashika manyasi marefu kujipa mhimili mzuri, akijiambia moyoni mwake kwamba alikuwa anaota na asingechukua muda mrefu kuamka, lakini ni hapa ndiyo akaanza kusikia sauti ya popo ikilia kuzungukia sehemu alipokuwepo. Akasimama kwanza na kutulia. Sauti hii ikaendelea kusikika kwa njia fulani kama vile inasema "njoo," "njoo," "njoo," naye Namouih akageuka huku na kule kuangaza chochote kile, na ndipo akaona kitu kama mwangaza wa mbali ukitembea hewani taratibu. Hofu kuu ilikuwa imemtawala mwanamke huyu, lakini hakujua ni nini tu ambacho kilimsukuma aanze kuufata mwangaza huo, ingawa alijua uwezekano wa yeye kujipeleka kwenye mwisho wake ulikuwa huko.

Akaendelea kuufata mwangaza huo huku akiwa ndani ya hali yake ya utupu, na ingawa majani yalimchoma hapa na kule lakini hakukata tamaa kuendelea kuufata. Sauti ile ya mlio wa popo ikaacha kusikika, na mwangaza huo ukakatika ghafla kama umeme. Hali hiyo ya utulivu uliorudi baada ya Namouih kusimama ikamfanya aanze kusikia sauti fulani hivi kama za kitu kikitafunwa, au kunyonywa, hakuwa na uhakika. Zilitokea mbele yake kidogo, naye akaamua kupiga hatua chache kwa sababu ni sehemu hiyo hiyo ndiyo mwangaza ule uliishia. Alijitahidi kutembea kwa tahadhari sana mpaka alipofikia usawa wenye manyasi mengi marefu yaliyobanana sana, naye akayatenganisha ili aweze kuona kilichokuwa huko mbele.

Macho ya mwanamke huyu yalitanuka kwa kushtushwa na jambo aliloona mbele yake. Kulikuwa na giza ndiyo, lakini aliweza kuona kwa usahihi sehemu hiyo yenye mti, ikiwa imetundikiwa kitu kama kamba iliyoning'iniza mwili wa mtu ukiwa uchi kabisa, ukiwa bila ulimi mdomoni, na utumbo wake
ukininginia kutoka tumboni! Pembeni ya mwili huo kilisimama kitu fulani cheusi, kama mtu lakini mwenye mwili mkubwa sana, na alikuwa amekinga kama kopo la kisado sehemu hiyo ya tumbo iliyokatwa kwenye mwili ulioning'inizwa, akionekana kuziweka damu zilizomwagikia ndani humo. Namouih alikuwa anataka kugeuka na kukimbia, lakini ikawa kama vile analazimishwa kuendelea
kuangalia.

Akaanza kumwona kiumbe huyo akinyanyua kopo hilo juu, taratibu, kisha akalirudisha chini usawa wa mdomo wake na kuanza kunywa damu hizo! Alikuwa anazinywa taratibu, lakini sauti ya jinsi alivyozimeza ilikuwa inasikika vyema kwa Namouih. Aliona kero na kinyaa sana, na wazo la kwamba yeye pia alikuwa uchi sehemu hiyo isiyoeleweka ni wapi, mbele yake kukiwa na mwili uliokatwa namna hiyo, na jitu hilo likinywa damu kukazidisha hofu yake hata zaidi, naye akapata nguvu ya kugeuka na kuanza kukimbia. Alikimbia sana na kuanguka mara kwa mara, lakini
angenyanyuka na kuendelea kujitahidi kukimbia kwa nguvu zake zote. Alikuwa anajiuliza hii ni ndoto gani isiyoisha, yaani alitaka ikatike lakini ndiyo kwanza ikazidi kumpeleka mbali zaidi.

Akafika sehemu na kuanguka kwa nguvu sana, kitu kilichofanya abamize tumbo lake vibaya na kuhisi maumivu makali mno. Alipojishika tumboni, mkono wake ukaingia ndani kabisa, kuonyesha kwamba lilikuwa limechanika, na maumivu aliyohisi yalifanya jambo hili liache kuonekana kuwa ndoto bali kitu halisi kabisa. Akawa anapumua kwa shida sana, na ile aliponyanyua macho yake mbele akakutana na macho makubwa na mekundu sana yakiwa yanamtazama kwa ukaribu! Akapiga kelele lakini sauti yake haikutoka, na ndipo akahisi miguu yake ikianza kuburuzwa kwa nyuma, kitu kilichofanya maumivu yake tumboni yaongezeke! Alilia sana, akipiga kelele zisizotoa sauti yoyote ile, na ndipo.....


"Aaaaaaaaah!"


Namouih akaamka na mayowe hayo ya hali ya juu, akijikuta kitandani chumbani kwake. Alikuwa anapumua kwa kasi sana, naye akajishika tumboni kwake kuangalia kama alikuwa sawa. Akafumba macho na kuanza kulia kwa sauti ya juu, akiwa ameumizwa sana na ndoto hiyo mbaya mno, naye akaanza kumwita mume wake ili aje kumpa faraja angalau.

"Efraim... hhh... Efraiiim...."

Namouih akaendelea kuita tu, lakini hakupata jibu lolote lile. Akapunguza kasi ya upumuaji wake na kuanza kukitathmini chumba chake kwanza. Palikuwa kimya, na ingetakiwa kuwa jioni au usiku kwa kuwa alikumbuka kwamba waliporejea nyumbani kutoka msibani ilikuwa ni saa kumi na moja, hivyo hata giza lingekuwa limeshaanza kuingia. Lakini mwangaza uliokuwa chumbani hapo ulikaribiana na rangi ya weupe-weusi,
iliyofanya kila kitu kionekane kama hakina rangi. Akatazama mlangoni, palionekana kuwa mbali sana kutoka kitandani hapo kiasi kwamba alihisi asingeweza kuufikia haraka na kutoka, naye akaita tena jina la mume wake lakini akaambulia kunyamaziwa.

Nini kilikuwa kinaendelea? Bega lake likaguswa kutokea nyuma ya mgongo wake, na mishipa ya shingo ya Namouih ikakaza kutokana na kuhisi woga wa hali ya juu sana. Akageuka taratibu na kumtazama aliyemgusa, na macho yake yakatanuka kwa mshangao huku akitetemeka sana baada ya kumwona Felix akiwa amekaa karibu na uso wake huku akitabasamu!


★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next