CHANGE
A Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA SITA
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Namouih akashtuka na kujinyanyua kwa nguvu sana kutoka kitandani, yaani akiketi, huku akipumua kwa nguvu sana kutokana na hofu kubwa iliyokuwa ndani yake. Akatazama huku na huko na kutambua kwamba alikuwa chumbani kwake, taa zikiwa zimewashwa na ikiwa wazi kwamba usiku umeshaingia. Akapaangalia kitandani hapo na kukumbuka jinsi alivyonwona Felix ndotoni akiwa anatabasamu, naye akainamisha uso wake kwa kufadhaishwa sana na ndoto hiyo iliyojirudia mara mbili, ikiwa kama ni kitu halisi kabisa kilikuwa kinaendelea alipokuwa akiiota.
"Jamani... jamani... fuuuck!"
Namouih akaongea hivyo kwa hasira sana na kuanza kuirusha mito chini, akiwa amechoshwa sana na ndoto hizi, na ni hapo ndiyo Efraim Donald akaingia kutokea bafuni huku akimwangalia mke wake kwa mshangao. Akamfata kitandani hapo, na sasa Namouih alikuwa ameikunja miguu yake na kuikanyagisha kitandani huku uso wake akiuinamishia kwenye magoti yake, na mikono yake ikiibana kwa nguvu miguu yake kuonyesha mfadhaiko. Efraim Donald akakaa kitandani na kumshika Namouih kwenye nywele zake, na mwanamke huyu akashtuka na kujisogeza nyuma, akimwangalia Efraim kwa hofu sana.
"Namouih tulia... ni mimi. Vipi tena?"
Efraim Donald akamsemesha mke wake kwa kujali, naye Namouih akaangalia chini huku machozi yakionekana kumtoka.
"Mbona unapiga kelele? Umepatwa na nini?" Efraim akauliza kwa kujali.
"Hhh... Efraim me nachoka jamani... hizi ndoto... kwa nini lakini?" Namouih akaongea kwa huzuni.
"Umeota ndoto mbaya tena?" Efraim akauliza.
Namouih akatikisa kichwa kukubali.
"Umeota nini?"
"Ahh... yaani sitaki hata...."
"No, Namouih, naomba uniambie. Hili jambo linaweza likageuka kuwa tatizo kubwa. Jikaze uniambie..." Efraim akamsihi huku akimfuta machozi.
Kweli Namouih akajitahidi kutafuta utulivu kiasi na kuanza kumwelezea mume wake mambo aliyokuwa anaona kwenye ndoto hizo zenye kutisha. Alieleza namna ambavyo zilimfanya ahisi ni kama vile yuko sehemu halisi kila mara zilipompata, na hakujua kwa nini ila ilikuwa ni kama zimebeba ujumbe fulani wenye maana kwake ambao ulikuwa mgumu kuelezeka. Yeye hakutaka
hata kujua maana ya ujumbe huo lakini ilionekana kwamba ziliendelea kumpata kwa sababu ALITAKIWA kuelewa maana ya hizo jumbe. Efraim Donald alimsikiliza mke wake kwa umakini sana, akitambua kuwa kweli hiki kitu kingekuwa tatizo kubwa kama asingefanya jambo fulani kumsaidia mke wake; kama tu jinsi yule rafiki yake, Godwin Shigela alivyokuwa amemwambia.
Mume akamfariji tu mke wake na kumwambia labda angehitaji kujipumzisha zaidi, hasa akili yake. Namouih alikuwa ameweka wazi kwamba mambo yote haya yalimfanya hadi awe anaogopa giza kabisa wakati hicho ni kitu ambacho hakuwa nacho. Kwa kuwa sasa Efraim alikuwa amemwelewa zaidi akasema wangekuwa wanalala na taa zikiwa zimewaka ili kumpa ahueni zaidi, na baada ya hapo akamwambia mke wake waelekee chini kupata chakula kwa sababu ndiyo ilikuwa imefika saa mbili tu usiku.
★★★
Siku iliyofuata, hali ikaonekana kuwa shwari baada ya Namouih kuamka asubuhi bila kuwa amesumbuliwa na ndoto nyingine wala vioja vya usiku, naye akaanza kujiandaa kwa ajili ya kazi. Efraim Donald alikuwa anataka kuhakikisha kwamba mke wake yuko sawa kiakili na kihisia ili kumruhusu aende kazini, lakini Namouih akamwambia alikuwa vizuri, bila shaka kadiri ambavyo muda ungekwenda ndivyo ambavyo angezoea hali, nao wangetafuta wakati mzuri wa kutafuta utatuzi wa suala lake la ndoto mbaya. Baada ya kumaliza kujiandaa na kupata kiamsha kinywa pamoja, wanandoa hawa wakaondoka nyumbani hapo; Efraim akiendeshwa na Suleiman ndani ya Range Rover yake nyeusi na Namouih akiondoka kwa Premio yake ya silver.
Lakini mwanamke huyu hakuelekea moja kwa moja mpaka kazini, bali alikwenda kukutana na wakuu wa wapelelezi waliohusika na uchunguzi wa kifo cha mpelelezi mwenzao, Felix. Alipokutana nao akaanza kuwaambia kuhusiana na mambo aliyofikiria yalipelekea kifo cha rafiki yake,, naye akawaomba wafanye yote wawezayo kumchunguza Draxton; kwa kuwa aliamini kabisa kwamba mwanaume yule alihusika moja kwa moja na mauaji ya rafiki yake baada ya yeye Namouih kumwambia Felix amfatilie Draxton.
Wakuu hao wakawa wamwelewa na kumwambia kwamba wangemtafuta huyo jamaa na kumpiga uchunguzi wa ndani ili kuona kama kweli alihusika, naye Namouih akaridhia hilo na kuagana nao. Uzuri wa Namouih ni kwamba alikuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwenye maneno yake, kwa hiyo aliondoka akijua kabisa kwamba suala hilo lisingepuuziwa hata kidogo.
Alifika kwenye kampuni yao na kuanza kuelekea juu kwenye ofisi yake, na ile tu alipokuwa ameikaribia, akakutana uso kwa uso na Blandina, ambaye alikuwa amesimama na mwanamke mwingine aliyefanyia kazi hapo. Wawili hawa wakatazamana kwa ufupi machoni, kwa njia ya kawaida tu, kisha Namouih akatazama mbele na kuwapita bila kusema lolote mpaka alipoingia ofisini kwake.
Blandina alielewa wazi kwamba kofi alilomtandika rafiki yake jana bado lilikuwa linamwasha, na kwa kumjua Namouih vizuri alielewa pia kwamba kufanya amani naye isingekuwa rahisi sana hasa kwa sababu alijiona kuwa sahihi, lakini kwa wakati huu kulikuwa na jambo lingine alilohitaji
kumwambia, hivyo akamfata huko huko ofisini kwake na kuingia bila hata kupiga hodi. Blandina hakujali kwamba eti Namouih alikuwa kama "boss" kwake, yeye aliendelea kumwona kama rafiki yake tu haijalishi walikuwa wanapitia nini, hivyo akamsogelea mpaka mezani kwake na kusimama.
Namouih akafanya kama vile hajamwona kabisa, akiendelea kutazama kompyuta yake tu, na Blandina akatabasamu kwa kejeli huku akitazama pembeni, kisha akaona ni vyema aseme kilichompeleka na kuondoka. Akaanza kumwelezea kuhusiana na kazi fulani iliyohitajika kufanywa, ambayo ingempasa yeye Blandina kwenda nje ya jiji ili kuikamilisha leo leo kisha ndiyo angerudi kesho, halafu akamwekea kablasha mezani lenye orodha ya kesi ambazo angetakiwa kupitia ili achague zile alizotaka kufanyia kazi.
Namouih aliigiza kama vile hayupo hiyo sehemu, yaani hakumsemesha wala kumtazama, hivyo Blandina akashusha pumzi na kusema yeye angeondoka muda si mrefu, kwa hiyo Namouih akijisikia kukiweka kisirani pembeni basi angemtafuta wakati wowote aliomhitaji. Blandina akajiondokea tu hapo baada ya kumaliza kuongea hayo, na Namouih akatazama pale rafiki yake alipoishia mlangoni na kutoka.
Roho ilikuwa ikimuuma sana Namouih kumtendea mwenzake namna hiyo lakini bado na yeye pia aliumizwa na kitendo cha Blandina kumpiga kofi kisa mwanaume ambaye alimwona kuwa mbaya, kwa hiyo hakuona faida yoyote ya kuwaza sana juu ya hilo. Aliona kwamba ni Blandina ndiye aliyetakiwa kuomba samahani, na kwa sababu hakufanya hivyo basi ndiyo angemnunia mpaka kieleweke. Hii yote ilikuwa ni kwa sababu wawili hawa walipendana sana, basi tu. Kukomoana huku kusingechukua muda mrefu sana na kila mmoja alijua hilo, lakini bado hili suala lililosababisha utofauti wao lilikuwa zito mno na hivyo bila shaka muda ungepita. Namouih akalichukua kablasha lile na kuanza tu kupitia kazi ambazo Blandina alikuwa amemletea.
★★
Imefika mida ya saa nane mchana, Namouih akawa amemaliza kupata chakula na kutumia muda mwingi kwenye masuala ya kazi ambazo hazikumhitaji aende mahakamani wala wapi. Mwenye hiyo kampuni, yaani Mr. Edward, alikuwa amemwambia kwamba alitakiwa kwenda nyumbani kupumzika tu, lakini Namouih akasema alikuwa vizuri kuendelea na kazi.
Mkuu wake huyo akamsisitizia sana kwenda nyumbani kwa kusema alijua namna ambavyo siku hizi chache zimekuwa ngumu sana kwake, na moja kwa moja Namouih akawa ametambua kwamba Efraim alikuwa ameongea naye ili afanye jambo hili. Hakuona haja ya kubishana na mwajiri wake, kwa sababu hii ingempatia fursa ya kwenda tena kufuatilia ishu ya Draxton kwa wale wapelelezi, kwa hiyo akatii ombi la Mr. Edward na kuondoka.
Alikwenda moja kwa moja tena kuonana na mkuu wa wapelelezi wale, naye akapewa taarifa ambazo hazikuwa nzuri kwake. Walikuwa wamefanya uchunguzi kumhusu Draxton na kugundua kwamba usiku ule Felix alipouawa mwanaume huyo alikuwa pamoja na mpenzi wake kwa muda wote wa usiku ule mpaka kukucha, yaani walilala pamoja pale pale alipoishi Draxton.
Walikuwa wamemhoji Draxton asubuhi hii na hata kuongea na majirani zake ambao walisema ni kweli usiku huo wawili hao walikuwa pale, yaani Blandina na Draxton, na asubuhi wakaondoka pamoja. Draxton yeye alisema kwamba usiku huo alipokuwa na mpenzi wake walikutana na Felix na kutambulishana kwa mara ya kwanza, hivyo hakuwa akimjua mwanaume huyo hata kidogo isipokuwa tu kuwa rafiki ya Blandina.
Namouih akawa anasisitiza kwa kusema kwamba inawezekana mwanaume huyo alimwambia mtu fulani amuue Felix kwa niaba yake, kwa sababu huenda baada ya kumwona alitambua kwamba alikuwa anampeleleza, lakini Namouih akaambiwa kwamba kwa jambo hilo ingehitajika kuwa na uthibitisho zaidi; kitu ambacho hakikuwepo kabisa.
Draxton alikuwa msafi kuhusiana na jambo hilo. Ingawa hivyo, Namouih akaambiwa kwamba angetakiwa kusubiri ili wapelelezi waendelee na uchunguzi wao kwa sababu muuaji angeweza kuwa yeyote na wangehitaji kumkamata haraka sana, lakini Namouih aliziona hizo kuwa ahadi bandia tu. Akawashukuru kwa jitihada zao, kisha akawaacha na kwenda zake nyumbani.
★★
Muda ulitembea sana siku hii, mpaka inafika jioni baada ya Namouih kuondoka kazini alikuwa zake nyumbani tu akiendelea kufikiria njia za kumfichua Draxton. Mume wake alirejea kwenye saa nne usiku, nao wakapata mlo wa pamoja na kuzungumza kidogo mpaka walipokwenda kulala. Namouih alijitahidi kuonyesha kwamba sasa alikuwa sawa zaidi, lakini hiyo ilikuwa ni ili amridhishe tu mume wake. Aliendelea kuwaza sana kuhusu kifo cha Felix na nini afanye ili haki itekelezwe kwa mauaji yake, na jambo hili likamnyima hata usingizi.
Imefika saa saba usiku, mwanamke huyu akamwacha mume wake kitandani na kwenda kule chini kwenye ofisi yao ya hapo nyumbani ili ajaribu tena kuunganisha vipisi vya hapa na pale kubaini ukweli. Alitaka kuhakikisha ana vigezo muhimu vya kujua namna ya kumnasa mwanaume yule vizuri, naye akajikuta anaendelea kuumiza tu kichwa kwa muda mrefu zaidi ndani hapo. Akawa ameketi kwenye kiti chake ndani ya ofisi hiyo baada ya kuwa amejaribu kuunganisha mambo mbalimbali yenye kumhusisha Draxton na mauaji ya Felix bila kupata mafanikio yoyote chanya.
Efraim Donald, akiwa chumbani bado, akawa ameamka muda huu na kukuta mke wake hayupo kitandani, naye akajaribu kumwita akidhani yuko bafuni, lakini hakupata jibu. Akashuka kutoka kitandani na kuangalia saa. Ilikuwa ni saa nane usiku sasa, naye akaenda kuchungulia huko bafuni na kukuta kweli pakiwa tupu. Akatoka chumbani na kuzielekea ngazi, na alipofika kwenye kingo yake akaona chumba cha ofisi kule chini kikitoa mwanga, naye anajua bila shaka mke wake alikuwa humo. Akashuka na kuelekea mpaka huko, na baada ya kuingia ndani ya chumba hicho akamkuta Namouih akiwa ameinamisha kichwa chake mezani huku amekifunika kwa mikono yake, kama vile kuonyesha amechanganywa na jambo fulani.
Efraim akasogea mpaka hapo na kuona makaratasi kadhaa yaliyoandikiwa vitu vingi kwa njia ya mahesabu, michoro, na viunganishi, naye akatambua haraka kwamba hayo yote yalihusiana na suala la mke wake la kukazana kuthibitisha kwamba Draxton alihusika katika mambo mengi mabaya. Akamwangalia kwa umakini, kisha akamgusa taratibu kwenye mkono wake. Namouih bila shaka hakuwa ametambua uwepo wa mume wake ndani hapo kwa kuwa alinyanyua kichwa chake kwa njia ya kushtuka, ila baada ya kuona ni Efraim akatulia na kuendelea kumwangalia tu.
"Unafanya nini huku? Umeota ndoto mbaya tena?" Efraim Donald akauliza.
Namouih akatikisa kichwa kukanusha, na macho yake yalionyesha uchovu sana.
"Sasa mbona uko hapa? Tatizo nini?"
"Nilikuwa nimekuja tu... kusoma kidogo," Namouih akasema.
Efraim Donald akaichukua karatasi moja na kuanza kuisoma. "His car on sight when Agnes died... the tattoo... the same tattoo on his back... how he lowers his chin and tilts his head whenever.... ahh... kusoma? Namouih haya ndiyo unayoamka usiku wa manane kusoma?" akamuuliza.
Namouih akatazama tu mezani na kubaki kimya.
"Kwa nini unaacha kupumzika na kuja kukaa huku kufanya mambo yasiyo na faida yoyote? Draxton, Draxton, Draxton, mke wangu kwa nini hutaki kuachana naye? Amekukosea nini?"
"Vitu anavyofanya ndiyo vinanikosesha usingizi, na hakuna mtu anayetaka kuamini kwamba huyo mwanaume ni hatari mpaka atakuja kusababisha maafa zaidi," Namouih akaongea kwa hisia.
"Una uhakika gani ni yeye ndiyo anafanya hayo... Namouih mbona unakuwa hivi?"
"Sijapata tu ushahidi mzuri lakini najua ni yeye ndiye aliyemuua Agnes na Felix," Namouih akasema kwa uhakika.
"Okay. Kwa hiyo kama ni yeye ndiyo amewaua, wewe unataka nini?"
"Nataka nini?!"
Namouih akauliza kimshangao na kusimama.
"Unauliza nataka nini? Mtu amewaua watu naowafahamu, halafu unaniuliza nataka nini? Nikae nisubiri amuue Blandina next, au wewe si ndiyo?"
"Namouih acha utoto. Angekuwa muuaji kweli mpaka sasa hivi rafiki yako angekuwepo?"
"Ni utoto kwako ndiyo kwa sababu hujapoteza mtu yeyote muhimu. Angekuwa ameniua mimi je? Usingefatilia chochote kwa sababu ungeuona kuwa utoto, si ndiyo?"
Efraim akanyanyua kidole juu kumwelekea huku akimtazama kiukali, na Namouih akatulia.
"Nimechoshwa na hii tabia Namouih. Unapotea. Watu wanaofanya mauaji wako macho, na wewe ukikaa kujiingiza huko unaweza ukasababisha nikupoteze kweli. Sijali kingine chochote zaidi ya usalama wako, kwa hiyo nakukanya... achana na haya mambo," Efraim akamwambia.
"Kwa hiyo haujali jinsi navyohisi kwa sababu ya kumpoteza rafiki yangu?"
"Nimesema hivi... sijali chochote kile zaidi ya usalama wako. Ikiwa hizo hisia zako zitapelekea uumie, zitakuwa na faida gani kwangu? Acha kuwa mpuuzi Namouih, hata ukifanya nini huyo Agnes na Felix hawatarudi. Sitaki tena kusikia habari hizi. Iwe mwanzo na mwisho," Efraim Donald akaongea kwa ukali kiasi.
Namouih akawa anamwangalia mume wake huku akidondosha machozi kwa huzuni.
"Zima taa, twende tukalale," Efraim akasema kwa uthabiti na kuondoka hapo.
Namouih akaketi tena kwenye kiti taratibu, akiwa amehisi kuumizwa sana na maneno ya mume wake. Alilia bila kutoa sauti, na wakati huu alikuwa akilia kwa hasira. Aliuona ukweli kwenye maneno ya mume wake, kwamba hata kama angepata ushahidi dhidi ya mtu aliyehusika na mauaji, wale waliokufa wasingerudi kuwa hai tena. Kwa hiyo hasira aliyokuwa nayo sasa ilitokana na utambuzi wa kuwa njia ya haki katika kisa hiki ilikuwa ni kwa malipo ya damu, yaani uhai kwa uhai.
Alikuwa amejihakikishia moyoni mwake kabisa kwamba ni Draxton ndiye aliyewaua rafiki zake, hivyo kutokana na jinsi ambavyo wengine walipuuzia kile alichokiona kuwa uhalisia, sasa akawa ameamua kurudisha malipo hayo kwa mikono yake mwenyewe, na hangejali chochote kile ambacho kingejaribu kusimama mbele ya njia yake. Draxton angelipia kwa kifo cha Felix.
★★★
Asubuhi na mapema kulipokucha, Efraim Donald aliamka na kuanza kujiandaa kwa ajili ya kazi, huku akimwacha Namouih amejilaza kitandani. Mpaka inafika saa 3 bado tu Namouih alikuwa amelala, siyo kusinzia, bali hakutaka tu kunyanyuka kutoka kitandani. Kufikia muda huu sasa Efraim ndiyo alikuwa amemaliza kila kitu na kutaka kuondoka, hivyo akamfata mke wake ili amuage. Mwanamke alikuwa amelala kwa ubavu, mikono akiikunjia kwa pamoja kuelekea mpaka kwenye upande wa uso wake alioulaza kwenye viganja vyake; akiwa macho tu, na akiwa kimya tu.
Efraim Donald akachuchumaa karibu na uso wake na kumtazama kwa upole, kisha akamshika shavuni na kupitisha mkono wake mpaka nyweleni, lakini Namouih hata kumwangalia hakumwangalia. Efraim akamwambia 'mimi ninaenda sasa honey, tutaonana baadaye,' lakini ukimya ndiyo jibu pekee alilopewa. Kwa hiyo mwanaume akambusu tu mke wake kwenye paji la uso, kisha akamwambia angempigia baadaye, halafu akanyanyuka na kuanza kuondoka huku akimwangalia mara mbili-mbili kuonyesha namna alivyomjali sana. Namouih akaendelea tu kujilaza namna hiyo hiyo mpaka mume wake alipoondoka kabisa nyumbani, kisha akajinyanyua taratibu na kuketi.
Alikuwa ameweka uso makini sana, yaani hakuwa ameamka na hisi ya uchangamfu wala utani hata kidogo. Akaenda bafuni kujisafisha na kutoka kujiandaa, na haikuwa kujiandaa kwa ajili ya kazi. Akavalia T-shirt nyeusi yenye mikono mirefu iliyobana, suruali laini ya kijivu, na viatu vyeupe vya mazoezi. Akavaa na sweta jepesi lenye kofia ya kufunika kichwa, kisha akaingia kwenye vifaa vya mume wake na kuitoa bastola yake kwa mara nyingine tena wakati huu. Akahakikisha kuna risasi za kutosha, kisha akaiweka nyuma ya kiuno chake na kutoka chumbani hatimaye.
Ikiwa ni saa 4 sasa ndiyo Namouih anatoka ndani ya chumba chake, Esma alishangaa kiasi baada ya kuona jinsi alivyovaa na kujiuliza ikiwa alikuwa anaenda kazini au gym. Akamsalimia, lakini Namouih hata hakumwitikia. Akaelekea nje tu bila kusema lolote na kuchukua gari lake la Premo, kisha naye akaondoka hapo. Esma kwa kufikiri labda mwajiri wake huyo alikuwa amekorofishana na mume wake, akaamua tu kuendelea na shughuli zingine kama ilivyo kawaida.
★★
Inafika mida ya saa saba mchana, Efraim Donald akaanza kumtafuta Namouih kwa simu, lakini hakumpata mara zote alizojaribu. Akaamua kuacha mpaka ilipofika saa tisa, akampigia tena, lakini hakumpata. Ikabidi ajaribu kupiga ofisini kwake Namouih, naye ndiyo akataarifiwa kwamba leo mke wake hakukanyaga huko. Kwa kufikiri labda alikuwa amebaki nyumbani, akapiga namba ya Esma, na mwanadada huyo akapokea na kuweka wazi sasa kwamba dada mkubwa aliondoka nyumbani pia muda fulani baada ya yeye Efraim kuondoka, na hakusema lolote kabisa. Akamweleza namna mwonekano wa Namouih ulivyokuwa, naye Efraim akaingiwa na wasiwasi zaidi sasa.
Ikabidi mwanaume ampigie na Blandina pia, ambaye ndiyo alikuwa anarejea kutoka upande mwingine wa jiji alikokwenda jana kikazi, naye akasema kwamba hakuwa na utambuzi wowote wa ni wapi rafiki yake angekuwa maana hata yeye pia alijaribu kumtafuta leo bila mafanikio na kuchukulia labda bado alikuwa na kisirani naye. Kila mtu ambaye Efraim aliulizia kama amemwona
mke wake, jibu lilikuwa hapana. Hivyo akaamua kuacha mambo mengine ili kwenda maeneo mbalimbali kumtafuta.
Alielewa kwamba kilichotokea usiku wa kuamkia sasa ndiyo kilichokuwa chanzo cha maigizo haya kuanza, na kama mke wake huyo alipuuzia maonyo yake ya wazi, basi huko alikokuwa amekwenda ilikuwa ni kutafuta matatizo. Ikabidi ampigie na Draxton, akimuuliza ikiwa alikutana na mke wake leo, lakini mwanaume huyo akakanusha. Efraim hakutaka Draxton ahisi labda kuna shida fulani, kwa hiyo akasema tu kwamba hakuweza kumpata kwa simu yake na hivyo akadhani yeye Draxton akiwa mwanasheria mwenzake na mtu wa karibu wa rafiki ya mke wake angekuwa amemwona labda kimikutano na kadhalika.
Efraim Donald alihisi kuchanganyikiwa baada ya kufanya jitihada nyingi na kukosa matokeo
mazuri. Alizunguka hapa, huku, kule na huko akiwa na swali moja tu kichwani: Namouih angekuwa amekwenda wapi?
★★
Siku hii, Namouih alikuwa ameondoka nyumbani kwake, akibeba bastola ya mume wake, na ni sehemu moja tu aliyokuwa amekwenda; msituni/porini kule ambako alimfuatilia Draxton siku chache nyuma na kumshurutisha amwambie ukweli kuhusu matendo yake.
Tokea alipoondoka nyumbani na kufika huko, mwanamke huyu hakuwa na nia ya kufanya lolote lile zaidi ya kuusaka ukweli mwenyewe na kupata haki kwa ajili ya kifo cha Felix, na kwa kusema haki ilimaanisha ayaondoe maisha ya yule aliyeyaondoa ya rafiki yake. Hata ingawa jambo hilo lilionekana kuwa sahihi kwake, bado kilikuwa ni kitu ambacho hakuwahi kufanya kabla katika maisha yake, na hivyo hakujua uzito wa kile alichotaka kufanya tofauti na jinsi alivyotazamia.
Ingawa hivyo, tayari akili yake ilikuwa imeazimia kabisa kulitimiza jambo hili ambalo kwa maneno mengine lingeitwa kulipa kisasi. Alikwenda mpaka sehemu ile ambayo Draxton aliishia siku ile, kisha yeye akaliingiza gari sehemu za ndani zaidi za msitu huo ili kutafuta vitu vyovyote ambavyo vingethibitisha ubaya wa mwanaume yule, na alikuwa akiwaza kwamba kama angemkuta huko basi angehakikisha anamwacha akiwa maiti.
Alifanya uchunguzi wa hapa na pale bila kuchoka, kula, bila kunywa, na bila kukata tamaa. Hakujua ingemchukua muda mrefu kadiri gani kuuzunguka msitu huo wote, lakini hakutambua kwamba kadiri alivyoendelea kuzunguka huko ndivyo alivyozidi kupotea. Ili kutosumbuliwa na yeyote yule alikuwa ameiweka simu yake katika mfumo wa kutopokea mawasiliano kama mtu akiwa kwenye ndege (Airplane mode), na muda ukazidi kwenda na kwenda hadi inafika saa kumi jioni, ndipo akapata kuona jambo fulani.
Katika eneo la ndani zaidi la msitu huo, aliweza kuona kitu kama nyumba, iliyokuwa imekinzwa na miti mingi sana. Kwa eneo hili ilikuwa wazi kwamba hakukuwa na umeme, hivyo endapo kama giza lingepiga basi pasingeonekana kabisa. Ikambidi aliache gari na kwenda karibu zaidi ili aitazame vizuri, naye akaona namna ilivyokuwa ndogo kiasi, ikiwa imejengwa kwa mbao na magogo juu mpaka chini, lakini sehemu za madirisha zikiwa ni vioo. Hakukuonekana kuwa na mtu hapo, na ni sauti za ndege mitini na upepo uliopuliza matawi ya miti ndizo pekee zilisikika.
Eneo hilo, kwa jinsi tu lilivyokuwa, ingekuwa rahisi kwa yeyote kuogopa kwa sababu kulikuwa na hali fulani yenye kutisha, kama vile kujua hauko peke yako sehemu kama hiyo ingawa hakuna uwepo wa watu wengine. Lakini Namouih alijitahidi sana kuwa jasiri na shupavu, bastola ikiwa mikononi mwake alijiona kuwa na nguvu ya ziada iliyomsaidia kuzizima hofu zake kwa kadiri kubwa. Alikuwa akiwaza kwamba ni lazima Draxton alihusika moja kwa moja na sehemu hiyo, na alipotazama sehemu ambayo alijua ndiyo mwingilio wa nyumba hiyo ndogo, akaona pakiwa pamefungwa kwa kufuri kubwa na zito sana.
Kwa hiyo akaamua kurudi kwenye gari lake ili aende sehemu nyingine kwanza, ikiwezekana amsubirie mwanaume huyo afike huku ili yeye Namouih aitekeleze nia yake ya kuukomesha mchezo wake mchafu. Kila kitu kingetakiwa kufanyika kwa mikono yake kwa sababu hakuna mtu aliyetaka kumwamini, kwa hiyo angejivika roho ya kikatili pia ili kumwondoa mkatili.
Alianza kuendesha gari lake ili arudi kule alikotokea, na njaa aliihisi vyema ingawa alipuuzia hilo, lakini njia za kumrudisha alikotoka zikampiga chenga. Hakukuwa na barabara ya moja kwa moja iliyomfikisha huku alipofika isipokuwa tu kwa sababu ya jitihada zake za kutokata tamaa. Kurudi kule, angetegemea kifaa cha ramani cha kwenye gari, yaani GPS, lakini katika mzunguko wake NDANI ya msitu huo hakutumia njia hususa, hivyo akakosa kujua apite wapi.
Akajaribu hata kutumia maarifa; aangalie uelekeo mmoja kwenye kifaa chake ambao ungempeleka moja kwa moja mpaka kwenye barabara kuu, lakini shida ikawa kwamba miti, mabonde, na miinuko iliyoingiliana na uelekeo huo ingemzuia kwenda moja kwa moja, na kila mara ambayo angejaribu kugeuza mkondo, basi angetakiwa abadilishe uelekeo, yaani kwa maneno mengine aanze upya kila
mara ambayo angekutana na vizuizi vya namna hiyo.
Mwanzoni hii ilionekana kama shida ndogo tu lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda ndiyo ikawa wazi kwamba alikuwa amejipoteza sana, na msitu huo ulikuwa mkubwa kuliko alivyodhani. Inafika saa kumi na mbili jioni ndiyo wazo la kutafuta msaada kwa simu likamjia. Alipojaribu kutafuta mawasiliano, mtandao ukazingua. Piga, piga, piga, wapi.
Pole kwa pole giza likaanza kuingia, na wakati huu alikuwa akihisi njaa SANA, ila alichowaza zaidi ilikuwa ni njia ya kutoka huko haraka mno, kwa hali na mali yoyote. Akaendelea na jitihada zake za bila kuchoka kutafuta njia ya kutokea mpaka akawa anahisi kutaka kulia kwa sababu ya hali hii yenye kuvunja moyo sana. Hapa ni yeye ndiyo alikuwa anajaribu kutafuta haki kwa sababu aliona mambo yaliyotokea kutokuwa sawa kihaki, lakini bado tena ni yeye ndiyo akawa anaadhibika.
Akafika sehemu fulani ya wazi kiasi na kulisimamisha gari lake, na alipotazama saa akakuta ni saa mbili usiku tayari. Sasa alihisi kuchoka. Akatulia tu hapo na kuanza kulia kwa sauti ya chini, akikumbukia maneno ya mume wake alipomuonya kuhusu kufanya mambo ambayo yangemwingiza kwenye shida tu, na sasa alikuwa akiipitia.
Akainamisha kichwa chake kwenye usukani huku akipumua kwa nguvu, naye akaukaza usukani kwa viganja vyake akihisi kufadhaika sana. Lakini Namouih kama Namouih hakuwa mtu wa kupoteza matumaini kabisa, naye akanyanyua uso wake na kujifuta machozi, kisha akaanza kulitia gari mwendoni ili aendelee na jitihada zake. Halikuwa hata limemaliza mita mbili pale alipolisimamisha ghafla na kutazama mbele yake.
Hapo mbele, aliweza kuona gari lingine likija upande wake, taratibu, lakini kama vile linataka kuja kumgonga. Taa za mbele za gari hilo zilimulika sana hivyo Namouih hakuweza kutambua ni la nani hasa; katika maana ya ikiwa ni gari la mtu mwenye urafiki, au adui. Akaichukua bastola yake na kuishikilia kiganjani kwa utayari, na gari hilo likasimama mbele yake kwa umbali mfupi sana
kutokea kwenye la kwake, kisha taa zake zikazimwa. Namouih sasa akawa amejihakikishia kwamba hilo lilikuwa ni gari la Draxton. Kama waswahili wasemavyo, usiyempenda kaja.
Namouih akaendelea kutazama tu huko nje, akiona jinsi mlango wa gari hilo ulivyofunguliwa, Draxton akishuka na kusogea mbele kidogo, kisha akasimama kama anamsubiria. Namouih alikuwa anawaza atoke tu na kumpasua kichwa kwa kuwa jamaa alichagua muda mzuri sana wa kumfikia, usiku, hivyo angelimaliza tatizo hilo upesi na kuendelea na safari zake. Alikuwa ameshautia moyo wake ugumu namna hiyo, naye akaendelea kukaa tu ndani ya gari akisubiri kuona mtu huyo angefanya nini.
Draxton akaonekana kupindisha shingo kidogo kama vile anachungulia, kisha akanyanyua kiganja chake na kutoa ishara kama kuuliza 'vipi?' naye Namouih akawa anamwangalia kwa hisia kali. Taa za gari la Namouih bado zilimulika mbele hivyo Draxton alionekana vizuri sana. Alivalia shati la jeans lenye rangi ya samawati, ambalo hakulifungia vifungo kuonyesha T-shirt nyepesi nyeupe kwa ndani, suruali nyeusi pia na viatu vyeupe; mwonekano wake wa kawaida tu.
Namouih alikuwa akimtazama kwa chuki kuu moyoni, huku mapigo yake ya moyo yakidunda kwa nguvu sana kutokana na msisimko wa hisia nyingi kuvurugikana ndani yake. Akajivika ujasiri zaidi na kuufungua mlango, naye akatoka na kuanza kupiga hatua mbele huku mkono ulioshika bastola akiuweka kwa nyuma. Alikuwa anataka kusikia lolote lile kutoka kwa mtu huyo kabla hajamfumua risasi, ikiwa ni kitu alichodhamiria kufanya kwa asilimia zote. Akasimama mbele ya gari lake akiiziba taa moja kwa mwili wake, na akimwangalia Draxton kwa hisia kali. Draxton alikuwa anamtazama kwa umakini tu, na ikawa wazi kwamba wote walisubiri mmoja wao ndiyo aanze kusema kitu.
Draxton akavuta pumzi ndefu na kuishusha akiwa anaangalia pembeni, kisha akamtazama tena machoni. "Unafanya nini huku?" akauliza kistaarabu.
"Nikuulize na wewe," Namouih akasema.
"Namouih ingia kwenye gari... nifate."
"Unipeleke wapi? Kuzimu?"
"Kuna watu wanaokupenda, wanaowaza juu yako, wanaokutafuta sana kwa sababu hawajui ulipo..."
"Kwani me ni mtoto?"
"Huu unaofanya ni utoto Namouih! Kwa nini uko hapa? Bado una hii... crazy theory kwamba mimi ndiyo nimemuua rafiki yako, siyo? Watu uliowatuma jana wanipeleleze hawakukwambia vitu vilivyokuridhisha eh? Unafikiri kwamba utapata kitu fulani huku?"
"Sijaja kutafuta chochote ili kuthibitisha nachojua kuwa kweli. Nimekuja kuliondoa tatizo linalosababisha hayo yote."
"Namouih...."
Kabla Draxton hajaendelea, Namouih akamnyooshea bastola kwa uhakika kabisa na kuishika na mikono yote sasa. Draxton akaacha kuzungumza na kubaki amemwangalia kwa ufupi, kisha akatazama chini kwa njia ya kusikitika.
"Usifikiri leo nimekuja kimasihara. Huu ndiyo mwisho wako, Shetwani wewe!" Namouih akamwambia kwa mkazo.
"Namouih ni hatari sana kwako kuwa huku, hujui hilo."
"Acha kujifanya mwema, mpuuzi wewe. Unaniongelesha namna hiyo kwa sababu unajua nitakuua, siyo? Unafikiri unaweza kuitumia hiyo njia kunirubuni ili na mimi unimalize, si ndiyo?"
"Mambo hayako kama unavyofikiria. Sijaua mtu yeyote mimi..."
"Nadhani ulikuwa unaiambia hivyo hivyo maiti ya Felix baada ya kuikata ulimi na tumbo..."
"Kwa nini nimuue Felix, Namouih? Hata nilikuwa simjui!"
"Wapi imeandikwa kwamba ni lazima kumjua mtu ili kumuua? Logic mpya za ma-serial killer, au? Ulijua nilimweka akufatilie, na kwa kuwa angekuvuruga na yeye ukaona umuue."
"Ulimweka anifatilie?"
"Funga mdomo wako. Mwanzoni ulinifanya niogope, lakini sasa hivi hapana. Ni mimi ndiyo nilimweka Felix kwenye njia hiyo iliyomsababishia kifo... kifo kwa mikono yako. Ni bora hata nisingemwambia akufatilie... hhh... umemuua kwa sababu yangu. Na sasa nitahakikisha unalipia kifo chake," Namouih akaongea kwa hisia huku akilia.
"Ninajua Felix alikuwa muhimu kwako lakini unachofanya now si sahihi. Sijamuua. Kila jambo liko wazi kabisa kwamba sikumuua, umepofushwa tu na chuki yako kunielekea ndiyo maana hutaki kukubali ukweli. Namouih nakuomba ushushe bastola tuongee vizuri," Draxton akamwambia kwa upole.
Namouih hakutii hilo. Akaendelea kumnyooshea bastola huku akipumua kwa hasira.
"Ni vitu vingi vinakuumiza, hilo najua. Lakini unapaswa utambue kuwa hata kama ukiniua mimi, mambo unayodhani mimi ndiyo nasababisha hayatakwisha. Na itakuja kukuumiza zaidi ukigundua kwamba uliondoa maisha ya mtu asiye na hatia, na tayari itakuwa kuchelewa. Namouih wewe siyo muuaji, na wala usifikiri kuniua mimi itakupa amani... ni jambo baya sana litakalokuandama kwa maisha yako yote. Utanawa mikono yako lakini utakachobaki kuona itakuwa ni damu tu
uliyomwaga. Felix ameuawa kikatili, itakuwa jambo la busara tukishirikiana kujua ni nani amemuua ili apate malipo kwa ubaya huo..."
Draxton alipokuwa anasema maneno hayo alikuwa anapiga hatua chache kumwelekea Namouih mpaka alipofikia bastola yake, ambayo sasa ikagusa kifua chake kabisa. Namouih alikuwa anajitahidi kuonyesha kwamba amekaza bado, hataki kabisa masihara, hivyo akaendelea kumwelekezea namna hiyo hiyo huku akimtazama kwa ukali.
"Wewe ni mtu mzuri Namouih, usichukue hatua hii. Najua kuna mambo kuhusu mimi ambayo ni fumbo kwako, na haitakuwa rahisi kuelewa jinsi maisha yangu yalivyo lakini sijafanya ubaya huo unauosema juu yangu. Niruhusu nikusaidie, tusaidiane. Nina imani tutapata suluhisho kwa mambo haya lakini hili siyo suluhisho unalohitaji Namouih," Draxton akaongea kwa ushawishi.
Namouih hakutaka kabisa kumwamini, kwa sababu aliona maneno yote hayo ya jamaa kuwa njia ya kumrubuni ili aweze kumdhuru. Lakini tena kuna kitu ambacho kilikuwa kinamvuta nyuma kutofyatua risasi, kwa kuwa kwa ukaribu huu alianza kuona jinsi jambo hili lilivyokuwa zito kuliko namna alivyodhani. Draxton akashika viganja vya mwanamke huyu, na taratibu akaanza kuvishusha chini ili Namouih aache kumwelekezea bastola. Vilishuka ndiyo, lakini Namouih
akavipandisha tena na kumwelekezea silaha hiyo upya kifuani.
"Namouih tafadhali... tafadhali nipe hii silaha... hiki siyo kitu unachotaka kufanya..."
"Usiniongeleshe hivyo. Haunijui. Haujui ninachokitaka na nisichokitaka..."
"Najua hautaki kuwa mnyama, na ukifanya hivi utakuwa mnyama."
"Kama nani... kama wewe?"
"Ningekuwa nataka kukudhuru ningekuwa nimeshafanya hivyo, hata sasa. Lakini kwa nini hauoni kwamba ninakupatia nafasi ya kutambua mwenyewe aina ya mtu ambaye ni wewe?"
"Unanipa nafasi wewe kama Mungu au?"
"Namouih acha tafadhali... nipe hii silaha..."
Draxton akajaribu kuvishika viganja vya Namouih tena, lakini mwanamke huyu akagoma na kurudi nyuma kidogo. Ikabidi atumie nguvu kiasi ili aweze kumnyang'anya, naye Namouih akaweka upinzani zaidi na kuivuta kwa nguvu.
"Namouih acha... please... utajiumiza!"
"Niachie... nimesema niachie..."
Draxton akaivuta kwa nguvu, kitu kilichofanya Namouih avutwe kwake pia kutokana na kuingang'ania bado, na miili yao ikakutana karibu zaidi. Mikono yao ilikuwa kwa chini sasa katika vuta nikuvute hiyo, na ni hapo hapo mlio wa risasi ukasikika kwa nguvu sana!
Namouih akaachama huku ametoa macho kwa sababu ya mshtuko wa ghafla uliomwingia, huku akimwangalia Draxton ambaye bado alikuwa karibu yake sana. Draxton akaibana midomo yake na kufumba macho, kisha akainamisha uso wake kama mtu anayetaka kulia. Pumzi za Namouih zikaanza kutetemeka, naye akarudi nyuma kidogo na kutazama tumboni kwake. Damu zilionekana kulowanisha sweta alilokuwa amevaa, lakini hazikuwa zake. Alipomwangalia Draxton, akaona akiwa amejishika ubavuni huku damu nyekundu sana ikivia kwenye T-shirt yake nyeupe kama wino.
Namouih akaidondosha bastola kwa kuhisi ni kama nguvu imemtoka, naye akamwangalia Draxton, ambaye sasa alikuwa ameishika sehemu hiyo iliyopigwa kwa risasi kwa mikono yake yote huku akimwangalia Namouih kwa uso ulioonyesha alijitahidi kukaza maumivu. Akarudi nyuma kilegevu na kuliegamia gari lake kwa mbele, akiwa amekandamiza mkono mmoja hapo huku mwingine ukishikilia tumbo. Namouih alihisi kuchanganyikiwa. Midomo yake ilitetema sana, pumzi zikishuka na kupanda bila utaratibu. Aliogopa sana. Alivyokuwa ametazamia jambo hilo kwenda ikawa tofauti na uhalisia alioupata.
Akamwangalia Draxton na kuona jinsi alivyojitahidi kukaza maumivu, akipumua kwa nguvu sana na jasho likimtoka kwa wingi. Akashindwa kujua la kufanya, lakini ilikuwa ni kama akili yake ya kawaida ilimrudia baada ya jambo hili kutokea. Kweli alikuwa ni kama amepotea kabisa mpaka kufikiria kuua mtu, na uzito wa jambo hilo ukakolezwa zaidi baada ya kuona mwanadamu mwenzake akiteseka namna hiyo, tena kwa sababu yake. Kilichoingia akilini mwake sasa hivi ilikuwa ni kumsaidia Draxton kwa njia yoyote ile ambayo angeweza.
Akiwa bado anaogopa, akamsogelea karibu zaidi na kuanza kusema, "Draxton... D-drax... I'm so sorry... I'm... a... sikuwa... siku..."
Akawa anaongea kwa sauti tetemeshi iliyoonyesha woga wake mwingi. Badiliko hili la moyo kutoka kwa mwanamke huyu halikuvuta umakini wowote kutoka kwa Draxton kwa sababu alionekana kupambana zaidi na maumivu aliyokuwa akihisi.
"Tuna... tunahitaji uende... hospitali... twende hospitali... oh Allah... nimefanya nini? Draxton... twende kwenye gari... nikupeleke..."
Namouih alikuwa anaongea hayo huku akikumbuka vizuri kabisa kwamba njia ya kutoka huku hakuifahamu, lakini ilikuwa ni jitihada ya kuhakikisha angefanya lolote ili kumtoa mwanaume huyo kwenye maumivu. Akamshika upande wa juu wa mkono wake, akijaribu kuupitishia begani kwake, lakini Draxton akagoma kuutoa.
"Draxton tafadhali.... unahitaji tiba..." Namouih akasema.
Draxton alikuwa akipumua kwa nguvu sana. Alionekana kupata shida mno, na hilo likamwongezea simanzi mwanamke huyo. Akakishika kiganja cha Draxton ili aanze kumsisitizia kuhusu kwenda hospitalini kupata tiba, lakini akakiachia ghafla na kwa kasi sana. Kilikuwa cha moto kupita kiasi. Yaani aliungua mkononi kama vile amegusa maji au pasi ya moto. Akamtazama tena mwanaume huyo na kuona jinsi alivyopumua kwa uzito mwingi sana, naye akashindwa kuelewa ni nini kilichokuwa kikimpata zaidi.
"Draxton..." Namouih akaita.
Draxton akapiga ngumi juu ya buti la kufunikia sehemu ya mbele ya gari lake, nayo ikakunjika.
Namouih akabaki kumwangalia kimshangao.
"Nam... Nnamoouih..." Draxton akaita hivyo kwa sauti... mbili.
Namouih akabaki kumtazama kwa butwaa.
"Na... Namouih... nakuomba ukimbie... kimbia!"
Eh! Aliongea kwa sauti nzito iliyobadilika kutoka kwenye ile yake ya kawaida. Namouih hakuweza kuelewa ni kwa nini hiyo ilikuwa ikitokea, lakini akahisi kwamba bado angeweza kumsaidia.
Akamsogelea tena na kusema, "Draxton... nini shida? Risasi... una... unahitaji..."
"Nahitaji ukimbie Namouih... kimbia!" Draxton akasema hivyo huku ameinamisha uso wake kwenye gari.
"Lakini Draxton...."
Kabla Namouih hajamaliza maneno yake, Draxton akamgeukia ghafla na kumwangalia. Namouih alishtuka sana na kurudi nyuma kidogo, kwa sababu macho ya mwanaume huyo yalikuwa yanang'aa rangi ya blue kutokea kwenye lenzi zake. Yalikuwa yale macho makali sana kwa jinsi alivyomtazama Namouih, na jambo hilo lilimtia hofu sana.
Mwanaume huyo akatoa sauti ya muungurumo na kuinamisha tena uso wake kwenye gari, na Namouih akaanza kuona ngozi ya Draxton ikibadilika na kuwa nyeupe kama ya mzungu, huku kichwani kwake nywele nyeupe kabisa zikianza kuota; yaani zikiota na kuongezeka. Zilikuwa ndefu na laini, zikikua na kukua mpaka zilipofunika sehemu yote ya juu ya kichwa chake kufikia mgongoni, naye Draxton akapiga goti chini huku bado akiendelea kuhangaika. Mkono wake uliokuwa umeshikilia gari ukaanza kuota nywele hivyo hivyo sambamba na mkono wake mwingine, na makucha marefu yakaanza kuonekana yakikua vidoleni mwake!
Namouih alichoka. Yaani ikiwa na hii ilikuwa ni ndoto nyingine, basi alijua asingeamka kamwe, kwa sababu ilikuwa kwenye ulimwengu halisi.
"RUN!!!"
Sauti hiyo nzito kutoka kwa Draxton ikamwondolea mwanamke huyu bumbuazi la woga uliokuwa umepanda maradufu, naye akalifata gari lake upesi ili aondoke haraka sana. Akaingia na kuliwasha huku vidole vyake vikitetemeka haswa, na ile alipotaka kulirudisha nyuma kishindo kikubwa kutokea mbele kikamfanya apige kelele kwa hofu. Alitazama huko mbele na kuona kwamba, Draxton, au kiumbe huyo, alikuwa amepiga sehemu ya mbele ya gari na kusababisha
pajikandamize vibaya sana, hivyo kuna mifumo iliyoharibika na kufanya gari lisiweze kutembea tena. Akamwangalia tu na kumwona akiendelea kuhangaika na kugaagaa chini huko nje, naye Namouih akafungua mlango na kuamua kukimbia tu kwa miguu.
Moja ikageuka mbili ikageuka tatu ikageuka nne. Mambo yalizidi kubadilika na kubadilika. Yaani kila mara Namouih alipodhani amefikia ukomo wa jambo moja, lingine lingejitokeza tu, tena katika njia zisizofikirika kabisa. Aliendelea kukimbia msituni hapo huku akilia sana. Aliogopa. Palikuwa na giza, na mara kwa mara alianguka na kujigonga kwenye miti na vichaka, lakini akaendelea tu kusonga huko huko kusikojulikana. Alikuwa amechoka SANA. Kihisia, kimwili, kifikira, yaani alikuwa tupu kabisa isipokuwa ya hii nguvu ndogo asiyojua ilitokea wapi ambayo iliendelea kumsukuma ajitahidi kuikimbia shida ile.
Akafika sehemu moja na kusimama, akihisi kuishiwa pumzi, naye akawa anakohoa huku akilia kwa sauti ya chini. Akachuchumaa na kupiga magoti chini huku bado akilia, na kwa hapa akawa anayahisi vyema maumivu aliyopata mwilini kutokana na kujigonga na kuanguka mara kwa mara. Alielewa fika kwamba huenda jitu lile kwa jina la Draxton lingekuwa linamfatilia, hivyo kukaa hapo
kusingekuwa na matokeo mazuri kwake. Kwa kuwa alikuwa amechoka mno, akafikiria apande mtini na kutulia huko juu, hivyo akasimama na kuvua viatu vyake vyeupe, kisha akavirusha mbali, naye akaufata mti mmoja na kuanza kujaribu kuupanda.
Jitihada zake zikakoma na kumfanya atulie baada ya kusikia sauti fulani. Haikuwa sauti ya muungurumo kama aliotoa Draxton, bali ilikuwa sauti ya kicheko. Hakutaka hata kugeuka nyuma, naye akaendelea kujaribu kupanda mti bila mafanikio huku akitetemeka sana. Sauti hiyo ya kicheko ikasikika tena, lakini hakikuwa kicheko cha kawaida kabisa. Alipoweka umakini wake vizuri, sauti hiyo ya kicheko ikatambilulika kwake, naye akaelewa sasa kwamba ilikuwa ni kicheko cha fisi.
Upande kilipotokea, ilionekana kwamba fisi huyo alikuwa karibu sana, hivyo Namouih akaanza kuelekea upande mwingine tena, na wakati huu alikuwa mzito sana kutokana na miguu yake isiyokuwa na viatu kuumia kila alipokanyaga chini. Kila hatua aliyopiga sauti ile ya kicheko ilikuwa naye, nayo ikaongezeka idadi na kuwa ni kama fisi wengi ndiyo wanamfata huku wakicheka. Aliumia sana miguuni mpaka akashindwa kusonga mbele zaidi na kuanguka tu chini.
Akageukia nyuma yake huku akiwa amekaa, akizisikia sauti hizo bado, na zilikuwa zinamchanganya sana kwa kusikika huku na kule na hivyo yeye kushindwa kujua fisi hao walikuwa wapi kihalisi. Haya majanga aliyokuwa amejiingiza ndani yake yalizidi kuwa mabaya tu, na sasa hakukuwa na njia tena ya kutoka hapo akiwa salama.
Upande wake wa kushoto, akatokea fisi mmoja aliyekuwa akionekana zaidi macho lakini mwili ukifichwa zaidi na giza, naye Namouih akajitahidi kusimama na kubaki amemwangalia tu. Wazo la kwamba huenda huyo fisi alikuwa ndiyo Draxton aliyegeuka na kuwa fisi-mla-watu likamwingia, na hakuonekana kutaka kumsogelea Namouih kwa sababu aliendelea kusimama tu huko huko.
"Toka... toka!"
Namouih akajaribu kumtisha ili amwache, lakini mnyama huyo akaganda hapo hapo tu. Hajatulia vizuri, upande wa kulia wakatokea fisi wengine wawili kutoka vichakani, nao wakawa kama wamemzingira. Akajitia ujasiri tena masikini, akijaribu kuwafokea, lakini wakaanza kujongea taratibu kumwelekea. Aliogopa mno.
Alipomshtua wa upande huu, wa upande mwingine angemsogelea karibu zaidi, na walimfanyia kama mchezo wa kumfanya atambue kwamba hakuwa na sehemu ya kukimbilia. Namouih akawa analia sana, akihisi kuchoka, yaani kuchoka kuupambania uhai wake ambao alielewa haukuwa na thamani yoyote mbele ya viumbe hao isipokuwa yeye kuwa kama chakula tu. Hapa sasa ndiyo akawa amepoteza matumaini kabisa. Hivi hata alijikutaje kwenye hali hii?
Mwanamke huyu akiwa anaelewa wazi kwamba huu ulikuwa ni mwisho wake, na fisi hawa wakiwa karibu yake zaidi, sauti ya muungurumo wa chini ikasikika sehemu hiyo. Namouih alitambua kuwa sauti hiyo haikutokea kwa yeyote kati ya fisi wale, kwa kuwa hata baada ya wao kuisikia wakaacha kumfata na kusimama huku wakionekana kuangaza pande tofauti-tofauti; bila shaka kutafuta chanzo.
Namouih sasa alikuwa akipumua kwa hofu bila kulia, akitetemeka, na akiwaangalia fisi hao, pale muungurumo huo uliposikika kwa mara nyingine tena. Zamu hii, muungurumo huu uliendelea tu bila kukata, kwa sauti isiyo ya juu sana, na wale fisi wakaanza kutangatanga sasa. Muungurumo huo uliposikika karibu hata zaidi, Namouih akatambua kwamba ulikuwa unatokea nyuma yake, naye akageuka taratibu huku akihisi ni kama vile hana miguu kutokana na kuishiwa nguvu.
Kutokea kwenye kichaka kikubwa upande huo aliogeukia, akatoka mnyama MKUBWA akitembea taratibu sana, meno yake makali mdomoni yakiumana, na sauti hiyo ya kuunguruma ikiendelea. Namouih alimeza mate kwa shida kutokana na hofu iliyopanda zaidi ndani yake.
Mnyama huyo alikuwa mweupe, mwenye macho makali yaliyozungukwa na giza fulani hivi na lenzi zenye rangi ya blue, meno marefu, na mwili wake ulionekana kuwa na nguvu nyingi. Alikuwa wa jamii za mbwa mwitu (wolves), lakini wale hasa wanaopatikana kwenye milima ya mabarafu nchi za nje, kwa sababu kwa nchi hii hakukuwa na wanyama wa jamii hii. Lakini mwili wake ulizidi hata ule wa simba dume mkubwa, akionekana kuwa mara tatu zaidi ya hapo kwa sababu ingawa Namouih alikuwa mrefu kwa kusimama, bado aliangaliana naye machoni kwa usawa. Ni hapa ndiyo Namouih akadondoka kwa mara nyingine tena, akijua habari yake ni kwisha!
Mnyama huyo akaendelea kumfata na kumkaribia zaidi huku akiendelea kuunguruma, na hata wale fisi wakawa wanajirudisha nyuma lakini hawakuondoka hapo kabisa. Jinsi manyoya ya mnyama huyo yalivyokuwa meupe sana ilimfanya aonekane vizuri mno gizani hapo, naye Namouih akavilaza viwiko vya mikono yake chini na kukilaza kichwa chake chini pia baada ya huyu mnyama kumfikia karibu kabisa na uso wake. Ingawa alikuwa anaogopa, Namouih aliweza kuendelea kumwangalia, akitazamana macho kwa macho na kiumbe huyo hatari sana. Mnyama huyu alikuwa akimtazama Namouih huku ameng'ata meno yake kwa hasira, kisha akafungua kinywa chake na kuanza kuunguruma huku akirudisha kichwa chake nyuma kidogo.
Namouih akijua fika kwamba hapo alikuwa anajivuta ili aanze kumtafuna, akafumba macho yake na kugeuzia shingo pembeni, akiwa hataki kuona jinsi ambavyo kinywa hicho kingerudi usoni mwake. Mnyama huyo akaachama mdomo wake na kukielekea kichwa cha Namouih, naye akapiga kelele nzito ya muungurumo, kitu kilichofanya ionekane ni kama anataka kukimeza kichwa chote cha mwanamke huyo kutokana na upana wa mdomo wake. Ilimuumiza Namouih sana sikioni, naye akabaki tu kuyafumba macho yake kwa nguvu sana.
Lakini baada ya mnyama huyo kumaliza kupiga kelele hizo, akaelekeza umakini wake kwa wale fisi watatu, naye akawaungurumia pia kwa hasira. Fisi walionekana kuogopa lakini bado wakajitia ujasiri wa kuendelea kubaki hapo, hivyo mnyama huyo akamvuka Namouih na kuwafata. Namouih aliweza kuhisi uwepo wa mnyama huyo ukiondoka karibu yake, naye akafumbua macho na hapo hapo kusikia kilio cha maumivu kutoka kwa fisi mmoja.
Akajigeuza na kutazama kule ambako fisi walikuwa na kumwona mnyama huyo mkubwa akiwa amemkamata fisi mmoja mdomoni mwake na kumrusha huku na huko kwa nguvu sana, na wale fisi wawili wakakimbia kutoka hapo. Fisi aliyekuwa amekamatwa kwa mdomo akararuliwa vipande viwili na vyote kurushwa juu, kisha mnyama huyo mkubwa akaunguruma na kutoka kwa kasi sana hapo, akiwafukuzia fisi wale wengine.
Namouih alikuwa amebaki chini hapo akipumua kwa mtetemo, kisha akaanza kujitahidi kunyanyuka tena. Akili yake ilikuwa kama imekufa ganzi, hakuwaza wala kujiuliza chochote tena, ilikuwa ni yeye kunyanyuka na kuondoka. Akawa anainuka kilegevu na kuweweseka, jasho likimtoka sana, kifua kikiwa kimekaza, miguu ikitetemeka, na baada ya kujaribu kupiga hatua chache, akadondoka na kupoteza fahamu.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments