Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

FOR YOU

Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa 

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA SABA

★★★★★★★★★★★★★★★★


Masaa kama mawili yalipopita ya utafiti mwingi, Luteni Michael akawa amerejea na wengine alioondoka nao muda mfupi nyuma. Aliwakuta wanaume wa timu yake wakiwa wanajadili mambo kadha wa kadha, huku ACP Nora akiwa amejitenga kando akiwa amezama kwenye utafiti wa kina zaidi wa matukio yote haya kwa ujumla. Luteni Michael akamuuliza Bobby walikuwa wamefikia wapi kwenye utafiti ule ambao Nora alipendekeza.

"Tumefanikiwa kupata sehemu tofauti ambazo order hizo zilipelekwa, na karibia zote ni kampuni za serikali za security tu... chache ndiyo binafsi," Bobby akamwambia Luteni Michael.

"Hizo za kibinafsi ziko ngapi?" Luteni Michael akamuuliza.

"Mbili. Na zote zinajihusisha na kampuni za madini kutoka nje ya nchi," akajibu Bobby.

"Kwa hiyo umeweza kujua ikiwa walizibadili kwa njia fulani ziwe kama nguo nzima ya kuvaa mwilini?" akauliza Luteni Michael.

"Siyo rahisi kujua mpaka tuwafate kuwauliza, na sijui sana kama kuna mtu HUKU anayeweza kugeuza hizo kuwa overall clothing. Kama zilikuwa kwa ajili ya security wao basi tutaona, na kama ni vingine tutawabana mpaka waseme ni kwa nani na kwa nini wangezifanya ziwe namna hiyo," akajibu Bobby.

"Basi tuna safari nyingine," Luteni Michael akasema.

"Nimeona gari nyingine hapo nje, ni ya nani?" akauliza Alex.

"Ni ya ACP. Kuna mtu amemletea sijui aliiacha huko Dodoma..." akajibu Bobby.

"ACP anafanya nini?" Alex akauliza tena.

"Amesema anapiga observation ya kina zaidi juu ya haya yote. Inaonekana ana-focus vizuri zaidi akiwa kivyake," Vedastus akajibu.

Luteni Michael akamwangalia Nora.

"Mario nenda kafate msosi basi," Omari akasema.

"Kwa nini mimi?" Mario akauliza.

"Kwa sababu hakuna chochote unachofanya hapa zaidi ya kucheza game la kitoto kwenye hiyo simu yako!" Omari akamwambia.

"Hili siyo game la kitoto, fala wewe. Hii inaitwa Temple Run... hujawahi kuicheza ndo maana unaona ni ya kitoto... shika ujaribu," Mario akamwambia.

"Em' toka hapa!" Omari akasema na kufanya Mario acheke.

Luteni Michael akamfata Nora na kusimama karibu yake. Aliona jinsi alivyokuwa anaunganisha mambo mbalimbali kuhusiana na wizi huu kwenye karatasi aliloliandikia vitu vingi, naye akamwangalia kwa njia yenye hisia kwa kupenda jinsi alivyokuwa na bidii. Hussein na Mario wakaenda hapo pia.

"Vipi, umepata jambo lolote?" Mario akauliza.

"Bee... oh... Luteni umesharudi kumbe?" Nora akasema baada ya kugeuka.

"Ndiyo, sasa hivi tu. Research ya nini hiyo?" Luteni Michael akamuuliza.

"Aam... najaribu tu kuunganisha vipisi mbalimbali ili nipate ufumbuzi juu ya huu wizi. Kiukweli mambo mengi hayaeleweki," Nora akasema.

"Kama nini?" Hussein akauliza.

"Kama ni jinsi gani hizo pesa waliweza kuzitoa pale. Naona kama kuna... mchezo... sijui tu. Hawa watu ni ma-professional, kwa kilichotokea Mwanza wangetuua. Kwa nini hawakufanya hivyo? Baada ya mabomu kulipuka benki zilipita siku mbili ndiyo ikawekwa wazi kwamba trilioni 20 zimeibiwa, na kilichoendelea hapo kwa siku hizo zote mbili hakijulikani maana waliweka surveillance ya hali ya juu, hata waandishi wa habari walizuiwa. Surely enough wangeweza kudanganya hata ni kiasi gani kimeibiwa kama ingekuwa ni wizi mdogo, lakini kwa pesa yote hiyo iliyopotea wangehitaji hata kuomba msaada IMF, au mkopo World Bank, maana ni loss kubwa kupita maelezo kwa hii nchi. Lakini hawajafanya hivyo... kinachokaziwa akili tu ni kuwakamata walioiba hizo pesa. Je kama wamezichoma? Kuwakamata itarudishaje hizo pesa zote? Halafu...."

"ACP ngoja..." Luteni Michael akamkatisha.

Kufikia hapo, wanajeshi wote wa Luteni walikuwa wanamwangalia Nora kwa umakini sana, wakitafakari maneno yake.

"Kama ingekuwa ni kazi ya ndani ya wizi huu tungekuwa tumeshajua, lakini wewe mwenyewe umejionea kwa macho yako kwamba hawa Mess Makers ni watu halisi. Kwa hiyo sidhani ikiwa kufikiria mbali huko kote kuna faida dada yangu. Sisi tunatakiwa kufanya kazi yetu ya kuwashika na kuwatia mikononi mwa sheria, na hata ikihitajika basi ni kuwaua ikiwa wataleta shida. Inaeleweka?" Luteni Michael akasema.

"Ila Luteni... naona kama ACP yuko sahihi kabisa. Ukifikiria kwa undani, mambo mengi haya-make sense," Mishashi akaongea.

"Hiyo si sehemu ya kazi tuliyonayo sisi. Kazi yetu ni moja, na tayari kwa msaada wako ACP tunapiga hatua. Tu-focus tu kwenye kazi yetu; Mess... Makers," Luteni Michael akawaambia.

Wote wakabaki kimya kwa ufupi.

"Ila ngoja nikwambie ukweli ACP, una akili sana. Yaani kama nisingekutana na Janeth kabla yako ningekutokea mapemaa," Mario akavunja ukimya kwa kutania, na wote wakacheka.

"Asante Mario," Nora akasema.

"Ila hapa hagusi mtu, ACP Nora mtata sana," akasema Hussein.

Nora akatabasamu tu. 

Luteni Michael akawa anamwangalia Nora kwa tabasamu la hisia.

"Wewe, mimi kama vipi namtema tu Janeth. Ni ACP kunikubali tu, me natia kwato," Mario akatania.

"Ila nyie, yaani mnageuza mada za muhimu na kuwa karaoke," Omari akawaambia Mario na Hussein.

"ACP mwambie asijaribu, baba yako atamtoa hizo kwato," Mishashi akaongea.

Luteni Michael aliweza kuona uso wa Nora ukibadilika na kuwa wenye kukosa raha baada ya Mishashi kumsema baba yake. Akatambua kuwa mwanamke huyu hakupendezwa sana na maongezi yaliyomhusu baba yake, ijapokuwa hakujua sababu ni nini.

"Ayaa! Nilikuwa nimeshasahau! ACP usinisemee eti?" Mario akasema kiutani.

Nora akatoa tu tabasamu la kujilazimisha.

"Mara ya mwisho nimemwona mkubwa hadharani sijui ilikuwa lini... anajua kujichimbia huyo ahahahah..." akasema Mario.

"Acha! Me nina mwaka sasa hivi sijamwona. Ila Mario msumbue tu ACP Nora, ndo' utamwona vizuri mshua wake," Mishashi akatania.

Kwa kuona jinsi ambavyo kumzungumzia baba ya ACP Nora kulimfanya mwanamke huyu akose amani, Luteni Michael akaona abadili mada kwa sababu wenzake hawakuwa wametambua hilo.

"Oy Omari, Hussein, shughulikieni msosi wa kuleta hapa faster. Au ACP ungependa tutoke out ya pamoja?" Luteni Michael akasema.

"Hapana, asante. Kuna... sehemu nataka kufika kwanza," Nora akasema.

"Lakini hata hujala bado," Mario akamwambia.

"Ndiyo... nitakula huko huko," Nora akasema na kuanza kukusanya vitu vyake vichache.

"Basi niende na wewe maana, huwezi kujua... Mess Makers wanaweza wakakutokea muda wowote. Nikulinde," akasema Mario.

Wenzake wakaanza kumpondea wakisema ameshaanza mambo yake ya umendeaji.

"Haina shida, nitakuwa sawa. Tutaonana baadaye. Anything comes up, unijulishe kama nitahitajika," Nora akamwambia Luteni Michael.

Luteni akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa. Kisha Nora akaondoka hapo akiwaacha wanaume wanamwangalia kwa matamanio.

"Mtoto amekaa fresh," Mario akasema.

"Acha dharau, hiyo hadhi hauifikii,"  Alex akamwambia.

Luteni Michael akampiga Mario kichwani kidogo na kusema, "Kuanzia sasa, sitotaka kusikia mnamwongelesha ACP Nora kuhusiana na masuala ya baba yake, nimeeleweka?" 

"Kwa nini?" Mishashi na Mario wakauliza.

Luteni Michael akawakazia macho tu kiukali, naye Mishashi akanyanyua mikono juu kuonyesha kwamba 'yaishe' na kuelekea upande mwingine wa jengo hilo. 


★★


ACP Nora alichukua tu gari lake na kuondoka maeneo hayo haraka. Kihalisi alihitaji muda wa kuwa peke yake kidogo baada ya kuifikirisha akili yake sana, na pia kutokana na ukweli wa kwamba alijihisi kukosa amani kiasi baada ya wanajeshi wale kuanza kumzungumzia baba yake, kwa kuwa hakupendezwa mno na mada zilizomhusu mzazi wake huyo, a.k.a Jenerali Jacob. Hivyo akaondoka kuelekea upande mwingine wa jiji ambako kulikuwa na mgahawa aliopendelea kwenda mara nyingi nyakati zote alizokuwa Dar es Salaam. Kufikia wakati huu, ACP Nora tayari alikuwa amechukua chumba cha kuishi kwa muda kwenye hoteli fulani kubwa jijini hapo. Lakini huku alikokuwa akienda palikuwa sehemu tofauti ambayo aliijua vizuri zaidi. 

Alifika huko dakika chache baadaye, ikiwa ni sehemu iliyokaribiana na fukwe za bahari. Mgahawa huo ulikuwa mkubwa, ukiwa na jengo pana kiasi lenye ghorofa moja, na wingi wa kuta zake ulijengwa kwa mbao nene zilizolainishwa. Ulikuwa na mandhari ya kifukwe fulani hivi (beach), ukiwa na sehemu ya ndani iliyotengwa kwa ajili ya waliopata vyakula, na sehemu nyingine kama "bar" kwa ajili ya vinywaji, na upande wa nje uliokuwa mpana wenye sehemu za kujifurahisha na kuegeshea magari kabla ya kufika upande ambao ungeelekea baharini. Watu wengi walipenda kwenda hapo kufurahia milo na vinywaji kwa sababu ulijengwa kwa mtindo fulani wa sehemu za starehe kwa ajili ya watalii. Ulipewa jina "Sea House Bar & Grill." 

Nora alipendelea kwenda sehemu hiyo tokea zamani kwa sababu ilikuwa ni moja kati ya sehemu ambayo familia yake ilipenda kwenda kipindi cha nyuma. Alifahamiana vizuri sana na mwenye mgahawa huu mkubwa na baadhi ya watu waliofanyia kazi hapo, hivyo alipofika alikaribishwa vizuri na mwanamke aliyeitwa Emmanuela, ambaye alifanya kazi kama msimamizi msaidizi, na mara nyingine alijihusisha katika kutoa huduma kwa wateja. Akaenda kuketi kwenye kiti karibu na usawa wa mtoa vinywaji (bartender), kisha akaagiza glass moja ya wine aina ya Dompo, naye akawekewa na kuanza kunywa taratibu. Ilikuwa ni kwenye mida ya saa 9 alasiri sasa, naye hakuwa amekula chochote tena tokea alipopata kiamsha kinywa asubuhi kabisa kabla hajaondoka kule Mwanza. 

Kulikuwa na watu kadhaa hapo wakifurahia vyakula, vinywaji na maongezi. Akawa ametoa simu yake akipitia mambo fulani, naye akasikia habari kuhusu Kevin Dass ikitangazwa kutoka kwenye runinga iliyotundikwa kwa juu usawa wa sehemu aliyosimama bartender. Akatazama na kuona lilikuwa ni rudio la tangazo kuhusu msako wa mwanaume huyo, naye akapiga tu kinywaji chake na kuendelea kusoma mambo mengine kwenye simu yake. 

Lakini akawa akimsikia bartender kutokea pembeni anaongea na mwanamke mwingine kuhusiana na Mess Makers. Walikuwa wakichanganua kuhusiana na jinsi serikali inavyolishughulikia suala hili la wizi wa trilioni 20. Maongezi yao yakawa kama mabishano, na wanawake wengine wawili waliofanyia kazi hapo pamoja na Emmanuela wakajiunga nao kuwasikiliza pia. Nora akaendelea kusikiliza lakini hakuwatazama.

"Kwa hiyo unataka kusema kwamba hawa jamaa hawana kosa lolote?" Bartender akauliza, ambaye aliitwa Elias.

"Hakuna asiyejua kwamba kuiba ni vibaya, lakini mimi naona ni kama hawajaiba mali ya mtu kwa sababu kiukweli hizo pesa zilikuwa zimekaa tu," mwanamke huyo akasema.

"Kivipi?" Emmanuela akauliza.

"Wewe umevuta bangi, ama nini?" Elias akamuuliza mwanamke huyo.

"Ah aaaa... siyo bangi. We' fikiria kuna pesa nyingi namna hiyo kwenye majengo, halafu huku kwetu kuna watu wanalala na njaa," mwanamke huyu akasema.

"Sa' si ndiyo hizo pesa ambazo zimetunzwa ili kuiendesha nchi? Masuala ya miundombinu na madude mengine, ndiyo kama hizo zinatumika," Emmanuela akasema.

"Sikiliza Emma. Pesa zinatengenezwa, si ndiyo? Zinatoka benki zinaanza kutembea hapa na pale, kila kona, lakini mwisho wa siku zinarudi wapi tena?" mwanamke huyu akauliza.

Emmanuela akatafakari kidogo, kisha akajibu, "Benki."

"Sasa je!" mwanamke huyo akasema na kuanza kucheka.

Nora akageuka na kumwangalia mwanamke huyo. Alikuwa mwanamke fulani kijana mwenye sura nzuri mno, tena mdogo kiasi kiumri kwa Nora, naye akamtazama kwa umakini sana.

"Kwa hiyo unataka kusema hawa jamaa kuiba hizo pesa ni fair? Wameigharimu serikali yetu halafu wewe unajifanya mpambe wao?" Elias akamuuliza.

"Siyo hivyo, lakini me naona wamewapa kama kikumbusho kuwa wanapaswa kutumia pesa kwa maslahi ya watu na siyo kuzificha tu," mwanamke huyu akasema.

"Aliyesema walikuwa wamezificha ni nani?" Nora akauliza.

Wote wakamwangalia, kutia ndani mwanamke huyo.

"Enhee... tena afadhali. Madam Nora msikie huyu anasema eti hao jamaa wamefanya la maana kuiba hizo hela. Asitoke hapa bila pingu huyu," Elias akasema kiutani, nao wote wakacheka isipokuwa Nora.

"Kusema wamezificha nilikuwa namaanisha wameziweka tu...."

"Wewe unajuaje kama walikuwa wameziweka tu?" Nora akamkatisha mwanamke huyo.

Wengine hapo wakamtazama kwa umakini kwa sababu aliuliza kwa njia yenye udadisi wa kiaskari zaidi. Mwanamke huyu akamgeukia vizuri zaidi Nora na kumwangalia kwa umakini zaidi.

"Tunafanya tu maongezi ya kufurahisha hapa, mbona unaniuliza kiukali utafikiri wewe polisi?" mwanamke huyo akamuuliza.

Elias, Emmanuela na wadada wengine wakaangaliana kwa wasiwasi. Walijua kwamba Nora alikuwa askari, tena mwenye cheo kikubwa. Lakini mwanamke huyu alionekana kutojua hilo hivyo akawa amegusa pabaya.

"Wewe, usimsemeshe hivyo, huyu ni..."

"Haina tatizo Emma, napenda watu wakifunguka. Samahani dada kwa kukuongelesha kiukali, lakini... nilikuwa tu nataka kujua kwa nini unafikiri hivyo," Nora akauliza kiupole zaidi.

"Sawa. Yaani mimi navyoona... serikali yetu hii bwana ina madukuduku mengi yaliyofichika kama serikali zingine. Lakini kwa muda mrefu imekuwa ikionyesha kwamba kwa nchi yetu hali ya kiuchumi inapanda, ila ukiangalia siyo kweli hata kidogo. Kodi watu wanalipa kama zote dada, zitumike kimaendeleo... oh surely kwa sababu tuko kwenye nchi yao ni fair, lakini kwa mambo ambayo zingepaswa kutimiza, hayajatimia. Watoto wangekuwa wanasoma bure mpaka wanamaliza vyuo, hakungekuwa na uhitaji wa kulipa nauli kwa usafiri, maji, sijui umeme, kwa sababu kupitia hizo hizo hela za kodi hayo yangetimizwa, ili pesa nyingine inayochumwa na nchi ndiyo itumike kuliinua zaidi taifa. Lakini hebu angalia tulipo. Progress iliyoahidiwa iko wapi? Hizo kodi zinaenda wapi? Wamajuu ni kukenua tu kwenye TV kwamba nchi inaendelea kwa sababu tu kuna viazi wanapita na tugari pilipili barabarani..."

Maneno ya mwanamke huyu yaliwafanya waliokuwa wanamsikiliza wacheke, lakini wengine waliona alikuwa anasema mambo ya kweli na kuanza kukubaliana naye; kama ujuavyo sikuzote hakukosagi wapambe.

"Ila hamna kitu chochote kabisa hapo... hawa bodaboda wetu hawa wangekuwa wanalipwa kabisa mwisho wa mwezi na serikali, siyo watu wanaowahudumia... alaah!" mwanamke huyu akasema na kupiga fundo moja la wine.

Watu wachache wakacheka na wengine kuanza kusikika wakitoa maoni yao hapa na pale. Nora akawa anamtazama huku ameachia tabasamu hafifu.

"Kwa hiyo kuiba hela benki ndiyo italeta maendeleo unayotaka? Au walikwambia hizo kodi ndo' zimewekwa huko? Na mbona sasa hao Mess Makers hawajatupa hata senti?" akauliza dada mmoja mhudumu wa hapo.

"Hapo ndiyo msemo wa raha jipe mwenyewe utatumika. Wameshabeba wamesepa, kuna mtu anawadai?" mwanamke huyu akasema.

"Dah, yaani huyu mwanamke mswahili!" Emmanuela akamwambia Nora.

"Yaani huyu hamnazo kabisa. Au na we' mmoja wao nini?" Elias akamuuliza mwanamke huyo.

"Weee! Pesa zote zile ningekuwa na we hapa sa'hivi kulewa? Yaani vruum China... Marekani... Ufaransa... tabu kuzibeba zingebaki na nyie tu," mwanamke huyo akasema na kumsukuma kichwa Elias kwa kidole.

Wengine wakacheka pamoja naye.

Nora akawa anatabasamu tu, kisha akamuuliza, "Kwa hiyo kama wangekuita ujiunge nao, ungekubali?" 

"Nikatae tena? Najiunga nao, halafu nawageuka nazibeba pesa zote! Hakuna tena masuala ya mihogo kwenye chachandu," mwanamke huyo akasema.

"Ahahahah... utazifichia wapi wapi trilioni 20 zote?" akauliza Elias kichokozi.

"Chini-kati chini-huku, zitatosha tu," mwanamke huyo akajibu na kufanya wengine wacheke.

"Hey, hivi hujui kwamba unaongea na askari hapa," Emmanuela akamwambia mwanamke huyo.

"Wapi kuna askari?" akauliza.

Emmanuela akamwonyeshea Nora, na mwanamke huyo akabaki kumwangalia tu. 

Nora akatabasamu na kunywa wine yake.

"Sasa leo hautoki hapa mpaka uwataje wenzako wote!" Elias akamwambia kiutani.

"Ni askari wapi, acha zako," mwanamke huyo akamwambia Elias.

"Ish! Mkubwa, labda umthibitishie kidogo. Sijui umpige pingu ili ajue ni kweli?" Elias akasema.

Nora akatoa kitambulisho cha kiaskari na kumwonyeshea huku akiwa anatabasamu tu. Mwanamke huyo akaonekana kushtuka.

"Eh Mungu! Dada samahani sana... sikumaanisha... mimi nilikuwa na... yaani..." mwanamke huyo akaanza kubabaika.

Wengine wakaanza kumcheka.

"Wewe ni mgeni huku?" Nora akauliza.

Mwanamke huyo akabaki kumwangalia tu kwa wasiwasi.

"Mmmmm we' naye! Wanakutania tu hawa, unaogopa nini sasa?" Emmanuela akamwambia mwanamke huyo.

"Yaani... mnanitania kwamba... siele... siyo askari au?" mwanamke huyo akauliza kiwasiwasi.

"Ni askari, tena Kamishna kichwa wewe!" Elias akamwambia.

"Toba!" mwanamke huyo akasema kwa sauti ya chini na kuangalia pembeni.

Nora akacheka kidogo.

"Usiogope nawe... Elias anakutania tu. Huyu siyo mwenyeji sana hapa, ila amekuwa mteja wangu tokea alipokuja huku," Emmanuella akamwambia Nora.

"Aaaa..." Nora akaonyesha kuelewa.

Mwanamke huyo akawa ameshika shavu akiona aibu kumwangalia Nora, naye Elias akawa anamtania eti leo ndiyo ulikuwa mwisho wa mdomo wake mrefu.

"Okay, Elias inatosha bwana. Dada, usiogope wala, maaskari siyo wabaya kama mnavyofikiria. Umekuja Dar kwa ajili gani?" Nora akamsemesha mwanamke huyu.

"Nimekuja kwa likizo fupi... nafanya kazi Pemba," mwanamke huyo akajibu.

"Ni mtu mcheshi sana, unamzoea haraka," Emmanuela akamtaarifu Nora.

"Mwombe samahani sasa hivi la sivyo Segerea inakuhusu," Elias akaendelea kumtania mwanamke huyo.

"Samahani sana... mimi sikufikiri... yaani kwanza ndiyo nimekuja tu Dar me hata siwajui hao watu... kila kitu nilichosema sikijui, usinipeleke kunipeleleza bado ni mdogo sana mimi kwenda jela, ndiyo mwaka wa..." mwanamke huyo akaanza kujitetea.

"Ahahahahah... usihofu, sitafanya hivyo. Elias hebu mwache mwenzio bwana," Nora akasema.

Wengine wakawa wanacheka huku mwanamke yule akiwa anamtazama Nora kwa njia ya aibu kiasi.

"Unaitwa nani?" Nora akamuuliza.

"Naitwa Lexi," mwanamke huyo akajibu.

Nora akatabasamu tu na kutikisa kichwa kuonyesha ameelewa, akipendezwa pia na jina hilo, lakini bila kujua kwamba alikuwa uso kwa uso na adui yake mkuu. 

Lexi kwa kuigiza alikuwa hajambo! Alijifanya kama mtu fulani wa aina tofauti sana hapa, na lengo lake lilikuwa ni kuingia kwenye maisha ya Nora ili kuwa karibu naye zaidi, na hivyo awe na njia rahisi ya kujua mambo yanayoendelea upande wa timu ya Luteni Michael. Kutokana na taarifa kumhusu mwanamke huyu ambazo Torres alikuwa ameshampatia, aliona atumie njia hii sasa ambayo ingewasaidia kujua ni jinsi gani yeye na wenzake walikuwa wanawafatilia, na mipango yao ingekuwa ni nini, ili aweze kuiharibu kabla haijafanikiwa, na ili ya kwao ndiyo ifanikiwe.

Nora akamalizia kinywaji chake na kuwaaga wengine wa hapo, kisha akaondoka haraka. Elias na wenzake walibaki kumtania Lexi baada ya Nora kuondoka, huku akiwa anajifanya kwamba bado moyo unamdunda sana kwa kuwa aliogopa mno, lakini kihalisi mpango wake ulikuwa ndiyo umeanza mwendo. Akageuka na kutazama sehemu ya nje kumwona Nora anatokomea, naye akakaza macho yake upande huo kwa njia yenye hila.


★★★


IKULU


Ndani ya ofisi kuu ya Raisi. Kulikuwa na mkutano usio rasmi wa wanaume wachache ambao walikuwa na vyeo vya juu nchini, na ni kundi hili la wanaume hawa ndiyo ambalo kwa muda mrefu lilifanya mambo mengi mabaya gizani, huku likiwaficha wananchi kwa ujumla kwa kujifanya ni watu wazuri. Hapa aliyekuwa amewaita wenzake si mwingine ila Raisi Paul Mdeme mwenyewe, ambaye kupitia msaada mwovu wa wenzake hawa ndiyo alifanikiwa kufikia cheo hiki miaka 8 iliyopita na kuendelea. 

Kulikuwa na hali nzito ndani ya chumba cha ofisi hii, kwa sababu kuna siri kubwa iliyokuwa imejificha tokea wizi huo ulipofanyika, na ni hawa viongozi tu ndiyo waliojua kuhusu siri hii, lakini siyo wote walioafikiana na mawazo yao yaliyopingana kwa njia nyingi kuhusiana na jinsi ya kushughulika na suala hili. 

Kwa ujumla, walikuwa ni watu 7; kutia ndani Raisi Paul Mdeme pia. Wengine walikuwa ni pamoja na Makamu wa Raisi, aliyeitwa Eliya Kajuna, Waziri Mkuu aliyetwa Yustus Kagame, Gavana wa Benki Kuu aliyeitwa Laurent Gimbi, Jenerali Jacob Rweyemamu, bila kumsahau Luteni Jenerali Weisiko, na mwanaume tajiri aliyeitwa Salim Khan, ambaye alikuwa milionea mkubwa sana mwenye ufanisi mwingi ndani na nje ya nchi. 

Ni Salim Khan ndiye aliyekuwa "mheshimiwa" maalumu zaidi kwa sababu miadi aliyofanya na Raisi Paul Mdeme ya kumfaidisha kwa pesa, ilimsaidia (Salim) kufanya utajiri wake mwingi alioupata kwa njia haramu ufanikiwe hata zaidi, kwa kuwa Mdeme alisaidia kuficha kazi zake hizo haramu kwa uchochezi wake akiwa Raisi. Waheshimiwa hawa walihusika tokea mwanzo kabisa na suala zima la Demba Group miaka nane iliyopita, hivyo mpaka kufikia wakati huu walikuwa wakiendelea kufanya kazi kwa pamoja, na hivyo suala zima la Mess Makers lilikuwa linawafanya waumie sana vichwani.

"Salim sikiliza... ungekuwa uko chini ya hali yangu hata wewe ingekulazimu kufanya hivyo. Hakukuwa na njia nyingine," Raisi Paul Mdeme akasema.

"Ningekuwa sehemu yako ndugu yangu, ningepiga simu kwanza kwa wenzangu kuwauliza kama maamuzi yale yalikuwa sahihi... lakini wewe ukafanya tu ulivyoona kuwa sahihi. Hiyo haikuwa sahihi Mdeme. Sikuzote usi-panick kabla ya kufanya maamuzi, matokeo ndiyo haya sasa," Salim Khan akamwambia.

"Niliwajulisha! Lakini si niliwajulisha? Eh? General?" Raisi Paul akauliza.

"Ndiyo, ulifanya hivyo. Salim, hakuna haja ya kulaumiana, hiyo siyo sababu Mdeme ametuita hapa," Jenerali Jacob akasema.

"Najua sababu itakuwa ni blah blah blah blah blah tutawakamata hao pimbi, lakini mpaka sasa hawajapatikana na mzigo bado wanao. Watakapotaka kuchukua trilioni zingine watachukua tu tena, nini kitawazuia kwani?" Salim akaongea kwa jazba.

"Mambo mengi yanakwenda mrama mheshimiwa. Juzi kati hapo kama ujuavyo nilitoka kutoa pesa nyingi kama msaada kwa walemavu nchini, na tena ile ilikuwa show tu ili baadaye hizo pesa zirudi. Lakini kwa hii situation, ishakuwa impossible. Yaani sijui hata tunafanyaje," akasema Makamu wa Raisi Eliya Kajuna.

"Benki ya Dunia ilikuwa imeshaanza kuchunguza kuhusu pesa nyingi walizotoa kwetu kwa ajili ya miradi miaka mitatu iliyopita, na kiukweli... hawajaridhishwa na matokeo waliyopata. Muda si muda nahofia miiba itaanza kutuchoma kwenye kalio la hii nchi," akasema Gavana Laurent Gimbi. 

"Heroine zaidi ya tani 1000 nilizokuwa napitisha Ruvuma kutokea Malawi zilikamatwa... maana Sebastian anajifanya anajua sana kupekua mambo ili apate sifa. Sasa zimepotea na... yaani sijui ingekuwaje kama nisingefanikiwa kuwafunga midomo wale vijana... kila kitu kingepotea, lakini tayari kwa hapo mengi yamevurugika," akasema Waziri Mkuu Yustus Kagame.

"Umeona? Ni tetemeko kubwa sana hili kwetu Mdeme. Tumesaidiana sana, na ningeweza kukusaidia kwa mengi, lakini kwa suala hili ni ngumu sana kaka, mifuko yangu haitoshi kubeba tako la taifa zima. Deni la mkopo wa kwanza halikulipwa, halafu trilioni 20 zimeibiwa. Nani ataipa mkopo hii nchi? Wabunge wanakaa kupigana tu huko Dodoma maana mambo hayaeleweki sasa hivi, kama juzi nimemwona huyo Waziri wa Fedha na Mipango kwenye kuwasilisha mapendekezo kuhusu...."

Salim Khan aliendelea kulalamika sana. Raisi Paul Mdeme akamwangalia Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko kwa macho yaliyoonyesha alikerwa sana na jinsi mwanaume huyu alivyoongea, nao wakatulia tu kimya. 

".... unakuwa mnyonge Mdeme... unakuwa mnyonge! Sasa sa'hivi mambo hayaeleweki, pesa hakuna, unafikiri nini kitafuata? Dharau tu ndiyo ambazo...."

"Tulia kidogo mheshimiwa, usi-panick sana," Luteni Jenerali Weisiko akamkatisha Salim.

"Unasemaje wewe?" Salim Khan akauliza kwa jazba.

"Hakuna yeyote atakayemdharau Raisi, jifunze kuchunga maneno yako pia," akasema Weisiko.

Salim akamwangalia Mdeme na kuuliza, "Anaongea nini huyu? Umesahau unaongea na nani wewe mbwa?"

"Salim... tafadhali just... be patient. Kuna mzigo maalum unaingia kesho kutoka DRC, kwa hiyo usiwaze kuhusu mimi kudharauliwa na uwaze kuhusu kuendelea kunipa support. Tumefika mbali huku kote, niamini nikisema kila kitu kiko under control," Raisi Paul Mdeme akasema.

"Huo mzigo unaingiaje mheshimiwa?" akauliza Waziri Yustus.

"Nafikiri itakuwa bora ufike kwanza ndiyo mjue, lakini nyie mkae tu tayari. Hiyo ndiyo sababu niliwaita hapa kuwahakikishia kwamba kila kitu kitakuwa sawa. Ukishafika tu, angalau ndiyo tutapata nguvu ya kufunga midomo mirefu ya watu, na hao wapumbavu waliotuletea hasara tutahakikisha tunawashika na kuwaua wote," akasema Mdeme.

"Vipi kama hao Mess Makers watakuharibia tena? Maana ni kama wamekuweka kiganjani mwao tokea walipoiba hiyo... aagh! Una uhakika hawataweza kukuharibia?" Salim Khan akauliza.

"Watajuaje? Hii kitu ni top secret," akasema Jenerali Jacob.

"Ahah... eti top secret. Si tulidhani ya benkini ilikuwa top secret, sasa hivi imekuwaje? Mhm... ngoja tuone. Mdeme... nakuamini kaka. Fanya unavyosema iwe kweli, na kila kitu kitakuwa shwari, I promise. Nyoosha mambo vizuri ndugu yangu," Salim akasema.

Raisi Paul Mdeme akatikisa kichwa kukubali. 

Salim Khan akanyanyuka na kuisawazisha suti yake, kisha akamwangalia Weisiko kwa jicho kali na kumwambia, "Mpango huo ukifeli, nina kichwa chako."

Luteni Jenerali Weisiko akatabasamu tu kwa mbali na kupiga saluti, lakini kwa njia yenye kejeli. Kisha Salim Khan akawaaga wengine na kuondoka. 

Baada ya dakika chache, Waziri mkuu Yustus, Gavana Laurent na Makamu wa Raisi Eliya wakaondoka pia, wakiwaacha wanaume watatu tu humo; Weisiko, Jacob, na Mdeme.

"Nini kinaendelea? Bado tu hamjafanikiwa kuwakamata hawa wajinga? Sitaki kuendelea kupoteza muda kucheza mchezo huu Jacob," Mdeme akamwambia Jenerali Jacob.

"Tunafanya kila kitu mheshimiwa. Hawa watu... wanaonekana kuwa na kiwango kikubwa cha ujuzi katika kuficha waliko, ila tutawapata tu," Jenerali Jacob akasema.

"Nora amefanikisha lolote mpaka sasa?" Mdeme akauliza.

"Tulipata taarifa kwamba alifanikiwa kumpata mmoja wao lakini walipomkamata, wenzake wakawashambulia kabla hawajamleta huku," akajibu Luteni Jenerali Weisiko.

"Hiyo ilikuwa lini? Mbona hamkuniambia?" Mdeme akauliza.

"Una mambo mengi mheshimiwa, ingekuwa kukuongezea stress zisizo na maana kama tungekwambia kitu kilichopoteza faida tena," akasema Jenerali Jacob.

Mdeme akashusha pumzi, kisha akasema, "Wananchi wananipigia kelele, Salim naye ananipanda kichwani... yaani... anyway... ninajua Nora atasaidia sana, maana binti yako yuko vizuri, ndiyo maana nilimwambia aingie kwenye uchunguzi. Najua sikukwambia mapema kuhusu hill, lakini nakuhakikishia atakuwa salama."

"Nora nimemfunda vyema... anajua jinsi ya kujilinda. Lakini mimi pia huwa namwangalia, kwa hiyo usiwaze kuhusu hilo," akasema Jenerali Jacob.

"Kuhusu Salim... naona kama vile amekupanda kichwani mpaka kutaka kukinyofoa sasa. Mheshimiwa... kama ukihitaji... tunaweza..."

"No... hapana," Mdeme akamkatisha Weisiko.

Jenerali Jacob akamtazama Raisi Paul Mdeme kwa umakini.

"Weisiko... hatutasuluhisha mambo kwa njia hiyo sikuzote. Salim ana mdomo ndiyo lakini ni wa muhimu sana na ni rafiki yangu wa muda mrefu. Usifikirie kufanya chochote kitakacholeta shida zaidi maana ana nguvu sana," Mdeme akasema.

"Imeeleweka," Luteni Jenerali Weisiko akaongea.

"Walikutafuta tena?" Jenerali Jacob akamuuliza Raisi Mdeme.

"Bado, hawajanitafuta. Na kwa kuwa sasa hivi wanajua tumewakaribia sana, yaani tutarajie lolote," akasema Mdeme.

Jenerali Jacob akaanza kusema, "Mheshimiwa, najua unataka mambo mengi tuyashughulikie kwa uangalifu, lakini hawa wapumbavu siyo watu wa kuwakamata na kuweka ndani. Ikiwa watashikwa na watu wengine walio nje ya muungano wetu na kubanwa waseme ukweli, siri nyingi zitazagaa. Nafikiri ni muhimu pale tunapowapata tu, tunawashughulikia mara moja... kwa sababu sasa hivi pesa hizo ziko nje ya picha. Hauwezi ku...." 

Jenerali Jacob akakatishwa kwa alichokuwa anasema baada ya Raisi Mdeme kunyanyua kiganja chake kumzuia.

"Kama wangekuwa wana nia ya kuzagaza siri nyingi wangefanya hivyo, lakini la, hawajafanya hivyo. Hawa watu wanachojali ni hela tu, na wameweza kunichengua kwenye udhaifu mdogo tu ambao sisi tuliuona kuwa nguvu. Pesa hizo zinaweza kutokuwa za muhimu kwako, lakini bado ni za muhimu kwa watu. Ndiyo ninaleta vitu vingine, lakini hiyo haimaanishi nitapotezea trilioni 20 kijinga tu. Ni lazima wakamatwe na waseme ziko wapi. Kumbuka nilifanya yale yote ili kulinda muungano wetu, nikiwa na matumaini wangeshikwa, lakini kwa uchawi wao wakatuzidi akili. Kwa hiyo kuwashika na kuwaua papo hapo haitakuwa njia nzuri, zipo zingine za kuwanyamazisha. Fanyeni tu kuwakamata na kuwafungia sehemu ambayo hawataongea lolote mpaka MIMI ndiyo niamue ikiwa tuwaue au la. Inaeleweka?" Mdeme akaongea maneno yake kwa mkazo.

Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko wakamwambia kuwa wameelewa, kisha wote wakamuaga na kutoka ofisini kwake hatimaye. 

Raisi Paul Mdeme alikuwa na zigo zito sana mikononi mwake, na alielewa kuwa mambo mengi yaliyomwandama ni kutokana na uovu mwingi alioufanya kwenye maisha yake, lakini bado alikuwa tayari kuendelea kuyafanya ili kubaki pale pale kwenye cheo chake. 

★★

Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko waliondoka ikuluni kwa pamoja; ndani ya gari moja. Wakiwa bado mwendoni waliongelea kuhusiana na mambo yote ambayo yalikuwa yakiendelea.

"Mdeme ni mshenzi mkubwa sana! Anamwingiza binti yangu kwenye haya yote.... ****mae zake... yaani kama jambo baya lingempata mwanangu usiku ule haki ya mungu ningemuua!" akasema Jenerali Jacob kwa hasira.

"Inakera sana kwamba tunapaswa kuendelea kuigiza kama vile anaweza kutupelekesha jinsi anavyotaka. Ameshapoteza mihela yote hiyo halafu anatupa matumaini fake, eti analeta mzigo kutoka DRC, mzigo gani? Ah... yaani maraisi bana," akasema Luteni Jenerali Weisiko.

"We' tulia tu Weisiko. Acha tuendelee kujifanya tuko nyuma, lakini tusiache kuwa mbele ya kila jambo. Anaweza kuleta mzigo wake huo lakini bado hadhi yake itabaki kuwa pale pale machoni kwangu... chini. Sijui alikuwa mjinga kiasi gani kufanya uamuzi ule," akasema Jenerali Jacob.

"Salim yuko sahihi kabisa. Basi tu yaani hawa watu waliojaa siasa vichwani wanachotanguliza huwa ni pupa, hawaioni picha kamili," akasema Weisiko.

"Na ndiyo maana nakwambia yaani huo mzigo wenyewe hautamfaidisha kwa lolote, zaidi atautumia kuigiza kwamba baadhi ya hao Mess Makers wamekamatwa na kurudisha hela kadhaa ili wananchi wamwone yeye na mapolisi wao vilaza kuwa noma, wakati kazi yenyewe tunaifanya sisi," Jenerali Jacob akasema na kuvuta ulimi kwa hasira.

"Huo mzigo ni nini kwani?" Weisiko akauliza.

Jenerali Jacob akamwangalia na kusema, "Dhahabu."

"Aaaa... amewaomba wajeda wa jehanamu kisiri eeh? Zinaweza zikawa kilo ngapi?" 

"Tani moja labda... sina uhakika."

"Damn! Amewezaje kupata dili kubwa namna hiyo? Sijui itakuwaje asipoweza kulipa."

"Watamtafuna! Anajua IMF wangezingua kwo' kupita gizani ilikuwa lazima, lakini hata hizo atakazoleta hazitamfikisha mbali."

Weisiko akakaa kimya kiufupi, kisha akamuuliza, "Unajua ulichomwambia Mdeme kuhusu hawa washenzi ni sahihi General, hatuwezi kuruhusu wawakamate halafu wawa..."

"Ndiyo Weisiko najua," Jenerali Jacob akamkatisha.

"Lakini sasa Mdeme kama unavyojua na king'ang'anizi chake... tufanye nini General?" Weisiko akauliza.

Jenerali Jacob akamwangalia kiufupi, kisha akasema, "Nafikiri ni wakati wa kuanza kutumia silaha yako ya India, unaonaje?" 

Luteni Jenerali Weisiko akamtazama tu kama anatafakari maneno hayo, naye Jenerali Jacob akatazama mbele tu ya gari huku akitabasamu kwa hila.

"Tuitumie silaha yako ambayo uliiwekezea vya kutosha kuwa jinsi ilivyo leo... huu ndiyo wakati ambao inahitajika zaidi. Mdeme katu hatajua ni sisi," Jenerali Jacob akasema.

"Na siri je?" Weisiko akauliza.

"Ikiwa sisi hatutokuwa wa kwanza kuwakamata na kuwanyonya ukweli, silaha yako itatakiwa kuwaua kabla ya wengine kuujua. Vinginevyo, silaha yako ichukue ukweli wote kutoka kwa hao Mess Makers kisha ndo iwaue wote," Jenerali Jacob akasema.

"General... usimwite silaha, ana jina," Weisiko akasema.

"Okay fine, vyoyote vile. Ameundwa kwa ajili ya masuala ya namna hii kwa sababu huwa haangushi, na haachi trace zozote. Kwa hiyo hii ndiyo itakuwa dawa yao. Awe makini kufatilia nyendo za Luteni Michael na Nora ili wakiwakaribia tu hao wapuuzi, yeye awe wa kwanza kufika. Na jambo la muhimu... asimguse binti yangu. Unaelewa Weisiko?" 

Weisiko akatikisa kichwa chake kukubali. 

Mambo yalikuwa yameanza kupamba moto. Kila upande ulikuwa tayari kupambania kile walichoamini kingewapa faida kwa njia walizojua wenyewe. Vita ambayo ingeanzishwa katikati ya mchezo huu wenye siri nyingi sana ingechafua hali ya hewa ya nchi nzima kwa njia ambayo haikuwahi kutokea kabla.


★★★


Lexi anaingia ndani ya chumba chake kwenye hoteli fulani ya kifahari, ikiwa ni mida ya saa 2 usiku baada ya kutoka kwenye mizunguko yake jijini. Anaingia kwanza sehemu ya bafuni kunawa uso na mikono yake, kisha anaelekea upande ulio na kama makabati ya ukutani kwa ajili ya vyombo vya chakula. Anaanza kutoa kikombe pale anapohisi kuna mtu nyuma yake. Kwa kasi anachukua kisu na kukirusha kwa nguvu upande huo, nacho kinachoma sehemu ya mlango wa kuingilia na kunasa hapo hapo, kikiwa kimemkosa shingoni kidogo tu Mensah! 

Jamaa akaanza kucheka, huku Lexi akimtazama kwa umakini.

"Awesome throw!" Mensah akamwambia.

"Unafanya nini? Ningekuua!" Lexi akamwambia.

"Lakini haujaniua. Hiyo inaonyesha huwezi ua mtu kabla ya haujamwona," Mensah akasema.

"Naona bado Kiswahili kinakupa shida," Lexi akasema.

"Siyo sana. Ninajitahidi," Mensah akajibu.

"Umekuwa humu ndani muda huu wote?" Lexi akauliza.

"Yeah, sina muda mrefu toka nimefika. Nikaona nikusubirie chumbani," Mensah akasema kichokozi.

"Ningekuona kama ungekuwa chumbani. Ulikuwa wapi leo?" Lexi akasema na kuanza kujiwekea chai, kisha akatoa kikombe kingine pia.

"Mizunguko tu... kujifanya nauza supermarket, kusikiliza kelele za watu, yaani mambo yanaboa. Nahitaji action... excitement..." 

"Lakini si unapata ku-bang wateja wenye makalio makubwa?" 

"Tena wake za watu. Watamu hao!"

"Sasa je! Life siyo yenye kuboa sana nje ya kile tunachofanya. Ila ukikutwa na mke wa mtu siku moja tusitajane." 

Mensah akacheka kidogo. 

Lexi akampatia chai pia. Wote wakaendelea kusimama, lakini Mensah akiwa ameegamia ukuta na Lexi kwenye sehemu ile ile yenye vyombo na jiko. 

"Vipi setting?" Mensah akauliza.

"Tayari. Tunakutana na wengine kesho. Tuondoke saa kumi na mbili juu ya alama," Lexi akasema.

"Hiyo ndiyo excitement niliyokuwa nahitaji. Vipi ACP wetu, unamwonaje?" 

"Anaonekana kuwa mwenye akili. Torres amemsifia sana kwa bio zake, hiyo ikimaanisha huyo mwanamke anajua sana. Nitaendelea kumchokonoa nione amejengekaje zaidi."

"Ingekuwa bora kama mimi ndiyo ningemtokea."

"Ili iweje? Hana tako kama la maman'tilie, usifikiri utamweza."

"Ahahahah... basi kweli hanifai. Lakini hii ya ishu kesho tutahitaji kuwa care sana Lexi," akasema Mensah.

"Usijali. I got us," Lexi akasema.

"Yeah, nakukubali sana. Unajua... nilishawahu kumsikia Kevin anamwambia Oscar inawezekanaje mtoto mdogo kama wewe utuongoze sisi... na Oscar masihara yake akasema hiyo kwa sababu unafanana na Malkia Cleopatra," Mensah akasema.

Lexi akatabasamu na kusema, "Ningependa kama angesema nafanana na Cardi."

"Ahahahah... sura, swagger?"

"Vyote."

"Ahahah... lakini Kevin kiukweli..."

"Bado ni mtoto..."

"Usinitanie..."

"Najua kwa nini unasema haya yote Mensah..."

"Tokea mwanzo alijua kabisa kwamba tulipaswa kwenda kwa mipango uliyotupa, lakini akajifanya yeye kichwa gumu kuzurura. Yote yale Mwanza yasingetokea..."

"Mensah... haikuwa kwa sababu hiyo. Kuna njia fulani tu ambayo huyo mwanamke alitumia kujua kuhusu Kevin; huenda hiyo ingekuwa yeyote kati yetu. Wote tunaishi maisha ya kawaida huku siyo rahisi kwa yeyote kujua sisi ni nani, kwa hiyo acha kumlaumu sana Kevin," Lexi akasema.

"Lexi... wewe na boss mara nyingi huwa mna akili moja, lakini katika mambo kuwa waangalifu sikuzote we' ndiyo umekuwa ukituongoza vizuri. Sijawahi mimi kuangalia umri wako, ninaheshimu kila kitu unachosema na kukifuata kwa kuwa sikuzote umehakikisha tunafanikiwa. Mwanza tulikuwa tumefata moja jambo, kukutana tulipaswa pamoja, tugeuke pamoja. Yeye akaona aende kwenye mabati kutafuta demu, kumsubiri akatulazimu tuanze mwisho wa siku...."

"Mensaaah... please let it go. Imeshatokea hivyo, just... let's focus ahead. Najua wewe na Kevin hamtoki page moja ya kitabu lakini amekuwa msaada mkubwa sana kufanikisha mipango yetu, kama ilivyo kwako wewe na wengine pia. Wakati huu mwenzetu amejulikana, tunahitaji kuwa na umoja zaidi. Hivi vitu vidogo vidogo visitugawanyishe. Wewe ni mkubwa kwake. Jaribu tu kumwongoza na kuonyesha unamjali kama kaka... usigombane naye. Tafadhali Mensah..." Lexi akasema kwa upole.

"Katika yote uliyosema nimesikia kwamba mimi na Kevin hatutoki page moja ya kitabu. Hiyo ni kweli kabisa, sikupingi," Mensah akatania.

Lexi akatabasamu.

"Mimi kuwa kama kaka kwake siwezi Lexi. Akileta za kijinga next time namkunja tu, hiyo ndiyo version yangu ya kuonyesha umoja. Nimemaliza," akasema Mensah.

"Fair enough. Hata mimi nakukubali pia, kwo' tusiangushane," Lexi akasema.

"You got it. Okay, asante kwa chai. Naenda kupiga club kwanza then ndiyo naingia bed," akasema Mensah.

"Sawa tu, ila kesho usichelewe, la sivyo na me version yangu ya umoja utaiona," Lexi akatania.

"Ahahahah... usiku mwema mtoto wa boss," Mensah akamwambia.

"Nawe pia maman'tilie."

Kisha jamaa akatoka na kumwacha Lexi akimalizia chai. 

Baada ya hapo, Lexi alielekea tu sehemu ya chumbani na kuketi usawa wa kitanda. Alianza kutafakari mambo mengi sana kwenye maisha yake yaliyokuwa yamejaa visa vingi vya kutamausha. Kwa kuhisi fukuto mwilini, akaona aingie kujimwagia maji kisha alale; kwa kuwa hakuhisi njaa sana na hivyo kutohitaji kula. Alipomaliza kujimwagia, akaingia kitandani na kuwasha laptop yake ndogo, kisha akapitia mambo kadhaa na baada ya hapo kuifunga na kuiweka pembeni. 

Simu yake ilianza kuita, simu maalumu, naye akapokea.

"Umekutana naye?" sauti upande wa pili ikasikika. Huyu alikuwa ni "Boss."

"Ndiyo, nimekutana naye," Lexi akajibu.

"Vipi, unamwonaje?"

"Haonekani kuwa mchawi kwa sababu hakunitambua, kwa hiyo tuseme tu ni elimu yake ya Ufaransa ndiyo inampa kichwa."

"Mmmm... sawa. Utapaswa uendelee kumwekea jicho. Yeye na baba yake hawapaswi kuwa mwiba kwetu hata kidogo. Ujue aliweza vipi kumpata Kevin na uiharibu hiyo njia, la sivyo huenda wakatupata sisi wote..."

"Yeah, najua. Nitamweka karibu ili nimharibu."

"Vizuri. Kesho... mpango wako on par?"

"Yeah, leave it to us..."

"Bado sina uhakika ikiwa uko sahihi. Vipi kama... siyo unavyofikiria?"

"Hapana, nina uhakika. Torres alinisaidia kufanya uchunguzi huo na tukajua ni hakika. So don't worry... tutafanikiwa..."

"Okay. Umekula?"

"Yeah."

"Fanikisheni mission yenu kesho, then urudi huku. Nataka familia yangu yote iwepo ili tu-celebrate."

"Sawa. Omba tu tusife."

"Ahahahah... kifo kimekuogopa tokea zamani, kwa hiyo hapo siwazi. Remember... everything we do...."

"... is for them," Lexi akamalizia.

"Good. Kwa hiyo kifo hakitatuona mpaka tufanikishe malipo wanayostahili watu hao wote," boss akasema.

"Yeah."

"Okay. Kuwa care Lexi. Nakuchukia," boss akasema.

"Nakuchukia pia uncle Kendrick," Lexi akasema.

Kisha baada ya hapo akakata simu na kujilaza kitandani. 

Kuambiana "nakuchukia" ilikuwa ni njia ya wawili hawa ya kuambiana "nakupenda." Na ndiyo. Boss wa kundi la Mess Makers hakuwa mwingine ila Kendrick Jabari mwenyewe! Kapteni Kendrick Jabari wa miaka nane iliyopita, yule yule ambaye mpaka kufikia wakati huu alifikirika kuwa amepoteza maisha kwa kuungua kwa moto ndani ya nyumba yake.!

Kuna mambo mengi yaliyotokea usiku ule ambayo ndiyo yalipelekea mpaka visa hivi vyote kuanza kutokea, na yeye ndiye aliyekuwa sababu kuu....

★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA 

★★★★★★★★★★

Previoua Next