DOSARI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Uhalifu, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TATU
★★★★★★★★★★★★★
Maandalizi ya msiba kumuaga rasmi Lydia yalikamilika, zikiwa zimepita siku tano toka apatwe na ajali ile iliyosababisha atoweke duniani. Kwa kawaida ungetakiwa kuwa umekwishamalizika, lakini Reuben alitaka marehemu mkewe afanyiwe msiba wa pekee kwa kutumia siku sita za maombolezo kabla mwili haujafukiwa. Kwa hiyo mwili wa Lydia ulipewa matunzo ya hali ya juu, na wazazi wa Lydia na ndugu na marafiki zake wengi walifika jijini kwa ajili ya ibada ya kuuaga mwili wa marehemu kabla haujasafirishwa kwenda kuzikiwa kule kwao. Mama yake mzazi hakuwa katika hali nzuri kimwili, na sasa kifo cha binti yake ndiyo kilimwongezea mateso zaidi hadi kushindwa kutembea vyema, hivyo alihitaji kiti cha magurudumu kusukumwa kila alipohitajika kuwa.
Kwa upande wake Reuben, ni ndugu wachache wa ukoo, washiriki wakuu wa bodi kwenye kampuni yao, wafanyakazi wao, na marafiki waliofika kumpa pole. Hakuwa na baba, yaani baba yake mzazi alikuwa ameshakufa miaka mingi nyuma, na mama yake mzazi alikuwa amefika hapo kutokea nchi za nje, huko Uingereza, akiwa pamoja na wadogo zake Reuben wawili wanawake. Reuben alikuwa ndiyo mzaliwa wa kwanza. Kufikia hiyo siku ya tano kwa wengi wa ndugu za karibu, ule uchungu mwingi wa mwanzoni ulikuwa ukififia na wao kurudisha uimara zaidi kihisia, lakini kwa wazazi wa Lydia, Reuben, na binti yake, bado lilikuwa ni pigo zito sana. Hasa Larissa.
Misa ilifanywa kanisani kwa ibada ya pekee, watu wakivalia nguo nyeusi na kupeleka pole zao kwa wafiwa, huku mwili wa Lydia ukiwa ndani ya jeneza maridadi na kuonyesha uso wake usioweza kufumbua macho tena kamwe. Reuben alijitahidi kuwa imara, akisalimiana na watu waliompa pole, lakini binti Larissa hakuwepo kabisa hapo kwa nafsi. Alikuwepo kimwili tu, kwa kuwa watu wangejaribu kumsemesha na kumpa pole, hata wale ambao alikuwa amewazoea sana, lakini binti hakutamka neno hata moja kwa siku hizo zote toka alipofikishiwa taarifa ya kifo cha mama yake. Alikaa kwa utulivu tu, akiangalia chini, akimfuata baba yake ama mama wadogo zake walipomwongoza huku na kule, lakini kani yake ya utendaji iligeuka kuwa kama ya sanamu.
Reuben aliumia sana kumwona mwanaye hivyo. Stanslaus Mwita, rafiki yake ambaye alichomewa duka lake la bidhaa, alikuwepo pia na familia yake kumuunga mkono. Francis na dada yake, Josephina, walikuwepo pia. Francis na Stanslaus walijitahidi kuwajibika na mengi ya mambo ambayo kwa kawaida Reuben ndiye angeshughulikia, ili kumpa mkono kwa ukaribu kuhakikisha anakazia fikira zaidi hali njema ya binti yake ambaye killa mtu aliona ni namna gani alitikiswa vibaya na kifo cha mama yake.
Kwa hiyo baada ya misa kuisha, jeneza likaondolewa kanisani na kuingizwa kwenye gari tayari kwenda kuhifadhiwa kwanza kabla ya kumsafirisha marehemu hadi mahali alikozaliwa ili azikwe. Ndiyo angezikwa hiyo siku ya sita. Watu walikuwa wengi, na wakati wakiliangalia jeneza linaingizwa kwenye gari, Josephina akasogea hadi karibu na aliposimama Reuben na Larissa, akiwa pamoja na mtoto wake, yule Hans. Tokea msiba uanze, Josephina alikuwa amempa tu pole fupi Reuben akiwa na kaka yake, ila sasa alitaka kumwonyesha kwamba alikuwa karibu naye zaidi kwa kipindi hiki ingawa hawakujuana vyema. Alivalia gauni refu lenye kubana kiasi, mwonekano wake mzuri wenye kuvutia ukiwa wazi kwa wengi, hivyo kumkaribia Reuben kulifanya watazamwe zaidi.
Akiwa karibu naye hivyo, Josephina akamshika usoni Larissa kwa njia ya kuonyesha huruma na kuzilaza-laza nywele zake pia, halafu akamwangalia baba yake na kusema, "Reuben..."
Reuben akamwangalia na kusema, "Phina."
"Aa... nilitaka tu kukupa pole kwa mara nyingine tena. Mambo yamekuwa mengi, hatujaongea sana," Josephina akamwambia hivyo.
Baadhi ya watu wakawa wakiwatazama wawili hao walipoanza maongezi hayo na kuwaelekezea fikira zaidi.
Reuben akamwambia Josephina, "Asante dada. Wala usijali, nashukuru sana kwa support yenu."
Mwanaume akarudi kutazama tu jeneza, naye Josephina akasema, "Unajua... sisi kwetu huwa tunaamini kwamba kifo siyo mwisho."
Reuben akamwangalia.
"Mwenzetu anapoenda kwanza, haimaanishi katutoka kabisa. Anaendelea kuwa pamoja nasi, kutulinda... na najua mkeo ataendelea kuwa pamoja nawe na mwanao popote pale mtakapokuwa," Josephina akasema hivyo kwa kufariji.
Reuben akamwangalia na kutikisa kichwa kama kuonyesha shukrani, naye akasema, "Asante. Mna imani nzuri."
Josephina akamwonyesha tabasamu dogo.
Reuben akaangalia mbele na kusema, "Sijui sana kama hiyo ni kweli, ila... sijawahi kutarajia mke wangu aende mbali nasi ili ndiyo atuangalie. Ingekuwa ni ndani ya uwezo wangu, ningemrudisha hata sasa."
Josephina akamwangalia kwa njia ya huruma.
Reuben akashusha pumzi na kusema, "Lakini hamna namna. Najua hii huwapata wengi. Sikufikiri tu ingewahi kutupata sisi. Bado inauma sana, maana... kihalisi hapo naenda kuzika watu wawili."
Josephina akamwambia, "Pole sana Reuben."
Reuben akatikisa kichwa kukubali pole hiyo.
Josephina akakishika kiganja kingine cha mwanaume huyu na kukikaza, naye akamkumbatia hapo hapo na kisha kusema, "Tutakuwa pamoja katika kila hali kuanzia sasa. Ukihitaji chochote, niko hapa kwa ajili yako... na Larissa pia."
Alisema hivyo na kumtazama binti Larissa, ambaye alikuwa ametulia tu akitazama huko mbele.
Reuben akasema, "Asante. Nashukuru sana."
Reuben akaendelea kutazama mbele, na Josephina akiwa ameendelea kumkumbatia tu, akawa akitembeza kiganja chake mgongoni kwa mwanaume huyu kwa namna ya kumbembeleza, akimwangalia kwa hisia zaidi, ndipo Francis akawa amefika hapo na kusimama karibu yao pia.
"Kaka..." Francis akamwita Reuben.
Josephina akamwachia Reuben na kiganja chake, naye akasimama kwa utulivu na mwanaye pembeni.
Reuben akamtazama Francis, na mwanaume huyu akasema, "Kuna mambo hapo kasisi anataka tu-asses... kabla hatujaondoka. Tunaweza ku..."
Reuben akatikisa kichwa kukubali akiwa ameshaelewa, naye akamwangalia Larissa na kusema, "Baby, njoo huku kwa mamdogo, nikaongee na padri mara moja..."
Akiwa anataka kumvuta binti yake, Josephina akasema, "Oh, haina shida Reuben... nitakaa na Larissa mpaka mrudi. Njoo mama..."
Mwanamke huyo akamsemesha Larissa namna hiyo na kumshika mkono, naye akamvuta pembeni pamoja na Hans huku Reuben akimtazama binti yake kwa hisia makini.
Francis akamuuliza, "Ameshaongea?"
Reuben akatikisa kichwa kukataa, kisha akampita tu Francis kuelekea upande aliokuwepo huyo kasisi.
Francis akamtazama Josephina na watoto pale waliposogea kuchanganyikana na ndugu zake wengine Reuben, akiona mwanamke huyo alipojaribu kumsemesha Larissa kwa upendo, na mwanamke huyo akamwangalia pia. Kwa sekunde chache wawili hawa walipoangaliana, Francis alimpa utizami wenye maana fulani ambayo Josephina aliweza kuielewa, na mwanamke huyo akaacha kumwangalia akionekana kutoipenda maana hiyo na kuendelea kushughulika na watoto. Francis akaachana naye pia na kuelekea alikokuwa Reuben.
★★★
Tunakuja kwake Paulina. Zikiwa zimepita siku tano sasa baada ya mwanamke huyu kijana kuwa amekwenda kwa shangazi yake kuomba msaada wa pesa za matibabu ya mama yake, Roza alimpatia wazo la kazi ambayo angeweza kufanya na upesi imwingizie pesa nyingi kumsaidia afanikishe tarajio lake la kumwokoa mzazi wake mpendwa. Kulikuwa na watu kwenye jiji la mbali, ambao Roza alifahamiana nao, waliofanya biashara za kuuza wanawake kwa wanaume wenye pesa kwa ajili ya starehe zao, na walilipa pesa nyingi.
Shangazi akamweleza mpwa wake kuwa biashara hizo zilikuwa za hali ya juu, tofauti kabisa na zile za wanawake waliojiuza kwenye madangulo ya ovyo ovyo. Hapa alikuwa akiongelea kumuunganisha kwa wanaume matajiri ndani ya sehemu za gharama, na watu waliofanikisha mambo hayo walifanya kazi hizo kwa umakini na mpangilio mzuri. Hivyo, wanawake waliochukuliwa kwa ajili ya kupelekwa huko walitakiwa kuwa wazuri haswa. Sura, umbo, vivutio vyote mwilini mwa mwanamke kwa macho ya wanaume vikiwa safi kabisa, na wajue jinsi ya kuwapa wanaume hao burudani ya aina yoyote waliyohitaji. Malipo yalikuwa manono.
Kwake Roza ilikuwa ni kazi rahisi sana, ila kwa Paulina lilikuwa ni jambo zito mno. Hakujua kama angeweza kufanya mambo ambayo shangazi yake alitarajia angeyafanya, lakini kwa sababu ya kuwa chini ya shida aliamua kukubaliana na wazo hilo. Aliahidiwa kuweza kupata hadi milioni kwa mteja mmoja tu, sasa afikirie angepata kiasi gani kwa wateja watano na zaidi! Mwanamke huyu kijana alikuwa na sura na umbo zuri kwelikweli, Roza akitumia siku hizo chache kumtengeneza vyema zaidi kwa kumpamba na kumwandaa kwa jinsi alivyotakiwa kutenda akishafika huko jijini kuanza kazi hizo. Alimwambia kwamba gharama anayotumia kumpendezesha ingetakiwa kurudi, yaani akishafanya kazi na kupata pesa angetakiwa kumlipa Roza pia, hivyo bidii ya kupata wateja wa maana ilihitajika.
Kizungumkuti kingekuja juu ya nani angekuwa karibu na mama yake kumwangalia, maana kwa sasa hakuwa na mtu wa kumwacha huko hospitalni. Roza akamwambia hilo halingekuwa na shida kabisa, kwamba yeye ndiye angesimamia taratibu zote za utunzaji wa mama yake kama ambavyo kwa siku hizi chache alikuwa ameanza kufanya, kwa hiyo akili yote ya Paulina ilipaswa kuwa kwenye kazi iliyomhitaji huko mbali ili afanikishe kutuma pesa ya vyote vilivyohitajika upesi kumtibu mama yake. Roza alitia nguvu kubwa sana kumshawishi mwanamke huyu kijana, na Paulina akawa tayari kuondoka baada ya kumwona mama yake kwa ufupi hospitalni huko. Kwa uharaka uliomhitaji kuondoka mjini kwao, hakupata hata nafasi ya kuongea wala kumuaga rafiki yake wa karibu, yule Halima, na siku ya safari ikawadia.
Paulina akapandishwa basi alfajiri ya mapema sana kutokea mjini kwao, gharama zikiwa za Roza, na shangazi yake huyo alimwambia kwamba atakapofika huko jijini kutakuwa na mtu wa kumpokea. Ni kwamba katika maandalizi ya kumpeleka huko, Roza alikuwa amempiga Paulina picha mapema na kuzituma kwa "afisa mauzo" wa hiyo biashara, ambaye alihakiki kama kweli Paulina alikuwa na vigezo vilivyotosha kumwekezea, na hilo likiwa limetiki, sasa angefika tu huko na kutambuliwa bila tatizo lolote. Kwa hiyo ingekuwa ni kushuka kwenye kituo cha basi huko jijini, na Paulina angechukuliwa na mtu ambaye Roza alimwambia kwamba anaitwa Isaya. Alimwelekeza jinsi anavyofanana na kumwambia atii kila mwongozo ambao jamaa angempa, na ajitahidi kuacha kujionyesha kama mgeni sana wa kila kitu.
Hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa Paulina kusafiri kuelekea nje ya mkoa wao, na hakujua huko jijini pangempokeaje lakini alielewa kuzoea maisha mapya isingekuwa jambo rahisi. Hasa maisha aliyokuwa anaenda kuyaishi. Hata katikati ya safari hii, Paulina alijiona kuwa kama tamasha kwa macho ya wanaume fulani kwa jinsi alivyoangaliwa, hiyo ikitokana na namna ambavyo Roza alimpamba usoni na mwilini, kwa mavazi yenye kubana umbo lake na nywele ndefu za kusukwa zilizompendezesha kwelikweli.
Lakini alijitahidi kubaki mtulivu tu, akijali yake na kuwa makini kutozungumza mengi mno na yeyote aliyemsemesha ndani ya basi hilo. Ndiyo, alisemeshwa na abiria wenzake, wanawake waliomsifia kwa kupendeza na kutaka kujenga urafiki pia. Lakini alijitahidi kuepuka kabisa kujuana na mtu yeyote kwa undani na kuwa msikilizaji tu zaidi, mpaka wamelifikia jiji hatimaye ikiwa imekwishaingia usiku.
Paulina alivutiwa na vitu vingi vilivyoonekana kuwa maridadi sana ndani ya jiji hilo. Vitu na watu wengi walijongea kwa kasi, yaani harakati hapa au pale zilikwenda na muda, kila mtu akionekana kuwa makini na mambo yake. Yeye pia, akikumbuka vizuri lengo lake kuja huku ni ili kuchuma pesa haraka kwa matibabu ya mama yake, angehitaji kuwa makini kwelikweli, kwa hiyo akaweka ugeni pembeni na kujitia mwonekano wa mwanamke aliyeonekana kuwa. Stendi aliyoshukia ilikuwa na mambo mengi, alipokanyaga tu chini tayari akaanza kufatwa na watu, huyu akimwambia twende huku, huyu kule, lakini akajitahidi kuwaepuka na kusogea sehemu ambayo hakuandamwa sana. Alitakiwa kumwona huyo Isaya na kuondoka naye, lakini hakuweza kutambua upesi jamaa angekuwa wapi.
Ndipo, kutokea nyuma yake akawa ameshikwa begani, naye alipogeuka akakutana na mwanaume mrefu mwenye mwili mkubwa kimazoezi, akijaa ndevu nyingi mashavuni na mwenye sura iliyo makini sana. Alivalia kwa namna yenye kuvuta fikira kiasi, T-shirt nyeusi iliyomchora kifua, cheni nene shingoni, saa ya gharama mkononi, jeans nyeusi, buti za khaki, na alimshika Paulina begani kwa namna fulani ya kutaka kumtolea mkoba wake mdogo aliobeba, na mwanamke huyo akaukaza zaidi mkononi huku akimwangalia kwa kujihami.
Mwanaume huyo akamwambia, "Tulia mpenzi. Nakujua."
Paulina akabaki kumwangalia kwa umakini.
"Unanijua mimi?" mwanaume huyo akamuuliza.
Paulina akasema, "Isaya?"
"Mm," jamaa akakubali.
Paulina akalegeza mkoba wake.
"Twend'zetu," Isaya akamwambia hivyo.
Mwanaume huyo alionekana kwenda na wakati, na akiwa anataka kujenga picha fulani hivi, akamshika Paulina kwa kumwekea mkono begani kwake na kuanza kutembea naye kwa njia fulani kama namna ambavyo wapendanao hufanya. Paulina hakujihisi amani kabisa kushikwa namna hiyo, alihisi ni kama anavutwa kwa lazima yaani, lakini hakuwa na jinsi ila kukubali tu kwenda naye. Wakaelekea upande wa nje kutoka hapo kwenye stendi, na moja kwa moja wakalifuata gari lenye muundo kama hiace, jeusi, na walipolifikia, Isaya akauvuta mlango wa nyuma na kumwonyesha Paulina ishara kuwa aingie.
Mwanamke huyu akaingia taratibu ndani humo, na kukiwa kumewashwa taa, sasa akaweza kuona kwamba kulikuwa na wanawake wengine hapo. Wanawake kama sita hivi, wazuri, wakivaa kwa namna zenye kuonyesha kwamba walikuwa ndani ya ligi moja na yeye iliyomleta huku kwa ajili ya mechi zilizohitaji kuchezwa, naye akapita mpaka kwenye nafasi yenye uwazi kukaa, akaketi taratibu. Tayari Isaya alikuwa amekwishafunga mlango na kuelekea upande wa siti ya dereva, na baada ya kukaa akaonekana akiwa ameweka simu yake sikioni kuzungumza na mtu fulani.
Paulina aliwaangalia wanawake wenzake vijana kwa njia fulani ya kukagua, akiwa anajiuliza kwa upande wao ingekuwa ni nini kilichowafanya wajikute ndani ya kazi hii yenye utata, lakini mienendo yao ilionyesha ni kama hawakujali sana. Baadhi yao hata walizungumza kirafiki na kucheka kwa njia yenye kuonyesha wamestareheka kabisa, na yeye aliposemeshwa na mmojawao, hakuwa hata na ujasiri wa kutoa jibu na kubaki ametulia kama vile hayupo. Hapo sasa alikuwa katikati ya fungu moja la wanawake waliojiuza, na hakuwa na namna nyingine ya kukana kwamba yeye hakuwa mmoja wao. Alihisi huzuni sana. Isaya akamaliza kuongea na simu huku akiwa ameanza kugeuza gari, naye akawaondoa kutoka maeneo hayo.
★★★
Kwake Reuben. Mwanaume huyu sasa alikuwa mwendoni kwenye safari iliyowapeleka waombolezaji wa kifo cha mkewe huko nyumbani kwao kwa ajili ya mazishi, ukiwa kama msafara kutokana na magari kadhaa kufuatana na lile lililoubeba mwili wa Lydia. Wazazi wa marehemu walikuwepo, ndugu zao, na wasindikizaji kadhaa pia, kutia ndani familia yake Reuben. Alikuwa ndani ya gari jeusi la hiace aina ya Alphard, yeye, mama yake, dada zake wawili, pamoja na Larissa, wakiendeshwa na dereva wa kuajiri. Isingewachukua muda mrefu sana kufika maeneo ya kwao na Lydia kwa sababu tayari walikuwa wameshaingia mkoani humo.
Ndani ya gari lao kulitawaliwa na hali ya ukimya hasa kutokana na dada zake kutulia tu na kufanya mambo yao kwa simu zao, huku Larissa akiwa amesinzia na kujilaza kwenye miguu ya baba yake sitini walipokaa. Reuben alitulia pia, akitelezesha kiganja chake kwenye nywele za bintiye kama kumbembeleza taratibu, na mama yake aliketi pembeni kwenye siti ambayo ilikuwa ya pekee, akimtazama mwana wake kwa kujali sana.
"Reuben..." hatimaye mama yake akamwita.
Reuben akamtazama.
"Yule rafiki yako hakuja. Ni kwa nini?" akamuuliza.
Reuben akauliza, "Yupi?"
"Yule aliyekuwa aki-handle...."
"Ooh, Francis?" Reuben akaelewa.
"Yeah," mama yake akakubali.
"Angekuja, ila... kuna mambo alitakiwa kushughulika nayo... ya kikazi," Reuben akamwambia.
"Huyo ni rafiki yako kweli? Hakusindikizi kumzika mkeo, anabaki kufanya kazi?" mdogo wake wa kwanza, aliyeitwa Sorange, akamuuliza hivyo kutokea hapo nyuma.
"Haina shida. Ni vitu vilivyopangwa, hangeweza ku-change," Reuben akasema.
"Na yule dada yake, aliyekukumbatia... nani sijui... na yeye hajaja pia," akasema hivyo Sorange.
Reuben akabaki tu kimya.
"Nilifikiri hao ndiyo mko close zaidi," Sorange akasema.
"Siyo sana. Kawaida tu," Reuben akasema hivyo.
"Wana maisha yao na mipango mingi, huwezi kuwalazimisha wawe huku. Lakini kati ya wote, nimependa walivyojitoa kukupa support. Hasa Francis. Anaonekana rafiki mzuri sana," mama yake akaongea hivyo.
Reuben akatikisa kichwa kukubali tu na kuendelea kumwangalia binti yake.
"Hautamwamsha ale?" mama yake akaongea hivyo.
Reuben akamgeukia na kumtazama kwa namna iliyoonyesha subira.
"Inaenda kuingia saa nne sasa, Reuben. Mwamshe mtoto ale," mama yake akamwambia.
Reuben akamtazama Larissa kwa ufupi, naye akasema, "Ni vyema akiamka yeye mwenyewe. Mwache tu alale."
Mama yake akawaangalia mabinti zake wawili waliokaa siti za nyuma na kaka yao, Sorange akipandisha mabega kama kumwambia mama yake hajui la kufanya, na mama huyu akamwangalia Reuben tena na kusema, "Umeshafikiria kuhusu nilichokushauri, I suppose."
Reuben akabaki kimya tu.
"Reuben, talk to me. Hii ni serious," mama yake akamwambia.
"Haiwezi kungoja mpaka tukirudi nyumbani?" Reuben akauliza.
"It can't. Niambie sasa hivi," mama yake akasema.
Reuben akaishia tu kushusha pumzi.
"Okay, najua una huzuni... sisi wote tumehuzunika, lakini ni vema uanze kufikiri kuhusu hali ya huyu mtoto haraka. Reuben... naomba ukubali kile nilichokushauri," mama yake akamwambia kwa upole.
Reuben akamwangalia kwa ufupi, kisha akasema, "Lydia ameniacha, mama. Kwa nini unataka na mwanangu aniache?"
"Haiko hivyo. This isn't about you, Reuben. Hii ni kuhusu Larissa. Umeona jinsi haya yote yalivyom-affect, mpaka sasa hivi haongei, naona ni vema tufanye hivyo ili kwanza...."
Reuben akamkatisha kwa kusema, "Nitajua namna ya kumsaidia mwanangu, mama. Unachotaka nifanye... kipo out of question. Siwezi."
"Reuben..." mama yake akaishia tu kutaja jina lake.
Mdogo wake wa pili, aliyeitwa Cynthia, akamshika Reuben begani kutokea nyuma na kusema, "Haitakuwa rahisi kama unavyofikiri kaka. Larissa ni mtoto wa kike. Siyo kwamba mama anasema hauwezi, ila... kwa sasa hivi, angalau kwa sasa hivi, tunaona litakuwa jambo lenye faida kwa Larissa aki... akikaa mbali na haya yote kwa muda fulani..."
Reuben akawa anatikisa kichwa kukataa.
"Kaka... suala la Larissa linahusiana na impact ya mazingira haya magumu, ninaenda kuwa psychologist, trust me... najua. Mazingira haya yanaweza ku-force hali yake iwe mbaya zaidi kuliko unavyodhani, ni suala la mazingira tu kaka. Larissa atahitaji kubadili mazingira kwanza, na atahitaji upendo wa mwanamke ili arudie hali yake ya kawaida tena. Just think about it," Cynthia akajaribu kumshawishi.
Reuben alikuwa kwenye wakati mgumu sana kihisia, na ndugu zake hawa walimfanya ahisi ni kama wanauongezea makali tu. Ilikuja kwa namna asiyotarajia mama yake alipomshauri kwamba ingefaa Larissa akiondoka nao, yaani, wanawake hao watakaporudi Ulaya, Larissa aende pamoja nao. Haikuwa kwa nia ya kumwondoa mtoto kwa baba yake, ilikuwa ni ili kumsaidia hasa Larissa kurudia hali nzuri tena, kwa sababu kama Cynthia msomi alivyomwambia, mazingira ya huku yenye kuumiza ndiyo yalifanya binti ashindwe kuwa sawa kisaikolojia, hivyo waliona kumbadilishia upesi mazingira hayo ndiyo jambo ambalo lingemfaa.
Lakini bado Reuben hakuwa tayari kuafikiana na mawazo yao. Kumwacha Lydia aende lilikuwa jambo gumu sana kwake, walitegemea vipi kwamba angewaruhusu wamchukue na binti yake ndani ya hiki hiki kipindi? Hakutaka kabisa kukubali. Kama ni kumsaidia, angemsaidia bintiye kwa namna nyingine yoyote, lakini siyo kumwondoa kutoka karibu yake. Sasa kuliko wakati mwingine wowote ndiyo alimhitaji zaidi Larissa kando yake, hivyo kwa matarajio ambayo mama yake alikuwa nayo ya yeye kumsikiliza, angekuwa radhi kumvunja tu moyo.
Akabaki kimya tu baada ya vishawishi vyao kuishia hapo, mama yake pamoja na dada zake wakiona kweli hilo lilikuwa limegonga mwamba, hivyo wakamwacha tu na kutulia zaidi ili safari hiyo iwafikishe kule mwili wa marehemu ulipohitajika kuwa.
★★★
Akiwa ndani ya gari lililompeleka mahala ambako angeenda kuanza "kazi," Paulina alikaa kwa utulivu tu huku bado hali nzima iliyomzunguka ikiwa yenye kumtatiza sana. Wanawake wenzake wangeongeleshana kuhusu vitu ambavyo hata hakuvijua, na baadhi yao walimwangalia kwa namna yenye dharau sana kutokana na yeye kujiweka kivyake zaidi. Angalau ni wawili hivi waliokuwa watulivu kama yeye, wakijali biashara zao tu, lakini waliobaki ndiyo mapepe yaliwajaa hadi Paulina akaona hao walikuwa wamebobea sana kwenye mambo haya.
Lakini kwake hilo halikuwa lenye umuhimu sana. Alikuwa akiwaza zaidi kuhusu hali ya mama yake huko alipomwacha. Hakuwa na simu, na akiwaza labda huyo Isaya angekuwa ameshawasiliana na Roza kumjulisha kuwa amefika, akafikiria angeweza kumwomba aongee naye pia ili kujua hali ya huko. Isaya huyo aliendesha tu gari kwa umakini bila kujishughulisha na wanawake hawa mpaka walipofikia eneo lililokuwa na jengo pana lenye ghorofa tatu. Ilikuwa imeshaingia mida ya saa tano sasa, na Paulina alihisi njaa.
Walipofika hapo na kuanza kushuka, mwanamke huyu akamsogelea Isaya upesi na kujaribu kumsemesha kuhusu simu, lakini mwanaume huyo akampuuza kwa kumsogeza pembeni, akiufunga tu mlango wa gari, kisha akawaambia wanawake hao wamfuate. Paulina hakuwa na namna, na yeye ndiyo akiwa mwishoni kwenye mstari huo akafuata njia pia kulielekea jengo hilo. Isaya hakuwa ameegesha gari mbele ya jengo, bali alilituliza upande wa nyuma ambao haukuwa na mijongeo mingi ya watu kama kwa kule mbele. Aliwaingiza hapo kwa njia fulani ya kificho, wakipita makopo ya takataka na kuufikia mlango mwembamba kwa nyuma, kukiwa na hali ya ugiza.
Kwenye mlango huo, Isaya akagonga mara tatu, na kwa ndani ukagongwa mara mbili, kisha yeye akaugonga mara moja tena. Hiyo ikiwa ni njia ya kujitambulisha, mlango ukafunguliwa kwa ndani, na Isaya akawapisha wanawake ili wamtangulie kuingia. Wale ambao walijiamini walipita kwa madoido yao na kunesa, na Paulina akatembea pia huku bado akiwa mwenye wasiwasi. Aliyefungua mlango alikuwa mwanaume mwingine mwenye mwili mkubwa, kisha Isaya akapita pia na kugongeana naye ngumi kirafiki, halafu akaendeleza mwendo pamoja na wanawake hao mpaka walipozifikia ngazi upande huu wa nyuma na kuanza kuzipanda.
Hapakuwa na hali nzuri kabisa, yaani palitoa harufu yenye kukera pua na kutapakaa kwa vitu vingi vichafu sakafuni, hasa chupa za bia na kondomu, na kundi hili likafika ghorofa la tatu huko na kuingia kupitia mlango mwingine. Wakiwa upande huu sasa, ikawa wazi kwa Paulina kwamba palikuwa jikoni, papana, na hakukuwa na watu wala nini isipokuwa vyombo na harufu kali za nyama iliyovunda. Wakapavuka na kuupita mlango tena wa kutokea humo, na sasa wakawa kwenye korido moja lililoonekana kuwa maridadi zaidi.
Sauti za muziki uliodunda, watu wakipiga kelele za kufurahi, zilisikika zaidi kutokea maghorofa ya huko chini. Huku palikuwa na hali fulani tulivu zaidi, na Isaya akawaongoza wanawake kupita milango ya vyumba na kumbi chache kwa upande huo hadi walipofikia mlango mpana kuelekea mwanzoni mwa mwingilio wa ghorofa hilo. Walikuwa wakiwapita wanaume na wanawake waliojistarehesha, Paulina akiona mambo mapotovu yaliyofanywa humo ambayo hakuwahi kujionea kabla, lakini akaendelea kujikaza tu. Alipaswa kuzoea, apende asipende.
Isaya akagonga hodi, lakini hakujibiwa, hivyo akafungua mlango na kuchungulia, kisha akatoka tena. Akatoa simu yake na kumpigia mtu fulani, wanawake aliowaleta wakiwa wanamwangalia kwa subira, naye akaongea kifupi na huyo mtu kumwambia kwamba mzigo ndiyo alikuwa ameuingiza, na alikuwa "ofisini" kwake huyo mtu, akimngojea aje kuuona. Ikaonekana amepewa maelekezo fulani, kisha akakata simu na kuwaambia wanawake waingie ndani ya chumba hicho pamoja naye.
Mmoja baada ya mwingine, wakaanza kuingia huku Isaya akisimama mlangoni, na alikuwa akiyapiga makofi makalio makubwa ya wanawake wachache walioingia kwa kuyatikisa haswa, wakitabasamu baada ya kufanyiwa hivyo na kumwangalia jamaa kwa uvutio. Lakini alipoingia Paulina na Isaya kutaka kumpiga kalioni, mwanamke huyu akajigeuza na kukinga mikono yake kama kumkwepa, na Isaya akamtazama kimaswali.
"Ish, we' vipi?" Isaya akamuuliza.
Paulina akajisogeza tu pembeni na kumwepuka, halafu akawahi kuingia na kwenda kusimama pamoja na wenzake.
Isaya akacheka kidogo kwa pumzi na kusema, "Usiniambie Roza ametuletea mshamba."
Kauli yake ikawafanya wanawake wengine wajichekeleshe na kumwangalia Paulina kwa kuhukumu, na mwanamke huyu akaendelea kujituliza tu kwa kutazama chini.
Isaya akafunga mlango na kusema, "Hii ndo' ofisi ya bosi. Bosi wangu, bosi wenu. Mtulie, anakuja. Huwa hapendi mambo ya kijinga, kwa hiyo nikisema mtulie, mtulie kweli. Atawapanga vizuri."
Wanawake wachache walikuwa wakimwangalia Isaya kimatamanio tayari na kuonyesha hilo waziwazi kwa matendo yao ya kimwili, lakini jamaa akawa akimwangalia Paulina zaidi.
"Wewe..." Isaya akasema.
Paulina akamwangalia.
"Umesikia nilichokwambia?" Isaya akamuuliza kwa sauti makini.
Paulina akaingiwa na wasiwasi, na akiwa anataka kutoa jibu upesi, hapo hapo mlango ukafunguliwa na kufanya wote watazame huko. Akaingia mtu aliyevuta umakini wao wote, na Isaya akatabasamu kiasi baada ya kumwona na kumnyooshea kitu kama kadi ndogo ili kumpatia.
Akakipokea, akiwa anawaangalia wanawake wengine kwa njia ya kutojali yaani, naye akamtazama Isaya na kuuliza, "Ndiyo hawa?"
"Ndiyo, madam," Isaya akajibu.
"Walitakiwa kuwa kumi, mbona wako saba?"
"Wengine watafika kesho, kulikuwa...."
"Ah, umeanza visingizio Isaya! Unajua hatuna muda wa kupoteza!" mwanamke huyu akamfokea kiasi.
Isaya akaangalia chini na kusema, "Sorry, madam. Haitatokea tena, kesho tu wanaletwa, na tutaongeza wengine."
Madam huyu, akawaangalia wanawake hao na kusogea upande wao, akiwa kama anawakagua kwa macho.
Mmoja wa wanawake hao akatoa ishara ya goti na kusema, "Shikamoo?"
Madam akasonya na kusema, "Shikamoo mwenyewe! Unaniamkia, me bibi yako?"
Mwanamke huyo akabaki kumtazama "madam" kiwasiwasi, na wengine wakaendelea kutulia. Paulina pia alimwanglia kwa hisia makini, akiona namna alivyovalia kwa njia nzuri sana lakini iliyoonyesha kwa kadiri kubwa viungo vyake vya kuvutia macho ya wanaume, na alinukia ile harufu iliyoeleweka kuwa ya kibosi kwelikweli.
"Mnajua me ni nani?" mwanamke huyo akawauliza.
Wanawake wachache wakasema, "Boss."
"Ahahahah... aaa... eti boss!" madam akasema.
Isaya akatikisa kichwa huku akitabasamu.
Mwanamke huyu akawa makini zaidi, naye akasema, "Hapa hakuna cha bosi. Mshanielewa? Niiteni madam. Nani?"
"Madam..." wakajibu, isipokuwa Paulina.
"Yeah. Atakayewalisha na kuwavisha kuanzia sasa itakuwa ni mimi, kwa hiyo eleweni hii kwenu ni sauti ya Mungu, na inawataka mfanye kila kitu inachowataka mfanye. Mshanielewa?"
Wakatikisa vichwa.
Madam akasema, "Nikiongea kwa sauti...."
"Yes madam!" wanawake wakajibu upesi.
Mwanamke huyu akaangalia chini kwa ufupi, kisha akasema, "Hmm... naona kama vile kuniita 'madam' haitatosha. Niwaongezee na ring nyingine kidogo, eti?"
Isaya akamwambia, "Yeah. Wajue ni sauti ya Mungu gani inayowasemesha."
Mwanamke huyo akatabasamu kijeuri kiasi, Paulina akiona namna ambavyo alipenda sifa, naye ndiyo akasema, "Niiteni madam Phina."
Wanawake wachache wakasema, "Madam Phina..."
Mwanamke huyu akatabasamu kwa kupenda kusikia akiitwa hivyo. Ndiyo. Ikiwa ni Josephina mwenyewe dada yake na Francis rafiki ya Reuben, mwanamke huyu ndiye aliyekuwa kwenye kiti cha utawala huu wa biashara ya wanawake, nyumba hiyo ya starehe ikiwa ni yake, na akiongoza mambo yote ambayo Paulina angejikuta akiwa chini yake. Rangi zake za kweli zilifichika kwa watu wengi ambao hawakujua aina ya maisha aliyokuwa nayo kihalisi, na kutokea hapa ndiyo ingeeleweka yeye alikuwa nani, na alitaka nini kwa kujiingiza ndani ya maisha yake Reuben.
Huyo ndiyo alikuwa Josephina!
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Comments