FOR YOU 2
Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TANO
★★★★★★★★★★★★
MIAKA NANE ILIYOPITA....
Turudi miaka nane nyuma kufikia wakati wa usiku ule ambao familia za Kapteni Kendrick Jabari na Meja Casmir Sona zilishambuliwa na Luteni Weisiko pamoja na wanajeshi wenzake wawili. Kapteni Kendrick aliwasikia viongozi kadhaa wa siasa na jeshi wakati huo, baadhi wakiwa ni Kanali Jacob Rweyemamu na Makamu wa Raisi Paul Mdeme, wakizungumzia kuhusu mpango wao mbaya kuwaelekea wanaume hawa wawili na familia zao kwa kuwa walihofia wangewaharibia mipango yao mibaya ambayo bado haikuwa wazi ni nini.
Ikiwa utakumbuka vizuri, Kapteni Kendrick alitoka jengoni walipokuwa na upesi kuwahi nyumbani kwake ili aiokoe familia yake, na pia alimtaarifu Meja Casmir mapema kuhusiana na mpango huo mbaya wa viongozi hao. Alipofika nyumbani kwake, aliwaasa ndugu zake wawili wanawake pamoja na mama yake mzazi waondoke haraka kwa sababu maisha yao kwa ujumla yalikuwa hatarini. Alipokwenda chumbani ili achukue vifaa vichache muhimu kwake, Meja Casmir alimpigia na kumwambia wakutane kwenye nyumba ya zamani ya mjomba wake (Casmir) ili wajipange zaidi kuhusu ni jinsi gani wangezilinda familia zao na kisha wafanye nini kuhusiana na mambo yaliyokuwa yakiwapata.
Ndipo baada ya kuwa amekata simu, Kendrick alijisawazisha na kujiuliza ikiwa kuna jambo lolote la muhimu alisahau. Alipoangalia kabati lake la nguo tena, akatuliza macho yake hapo kwa sekunde chache, kwa sababu alikumbuka kuna kitu fulani cha muhimu kilikuwa humo, kisha akavua begi na shati lake na kwenda kuifungua. Akatazama kwa makini ndani hapo, halafu akachukua VAZI lingine na kuvaa, kisha akavaa na jaketi jeusi kwa juu.
Vazi hili lilikuwa ni vazi maalumu kwa ajili ya kuzuia risasi kifuani mpaka kufikia tumboni (bulletproof vest), hivyo alilivaa kama ulinzi tu wa ziada endapo kama mbeleni yeye na Casmir wangehitaji kupambana na maadui zao, basi lingempa faida kwa kadiri fulani. Baada ya hapo alibeba begi na kutoka chumbani ili ajiunge na wengine waweze kutoroka hatimaye, lakini ndiyo akakuta Luteni Weisiko ameshafika. Alishuhudia mama yake mzazi akiuliwa kikatili mbele ya macho yake na mwanaume huyo, kisha wanajeshi wa Luteni Weisiko wakamshikilia kwa nguvu Kapteni Kendrick baada ya yeye kukasirishwa sana na kitendo hicho.
Luteni Weisiko alimwambia kwamba mambo yote aliyofanya yalikuwa ni sehemu ya wajibu wake, naye Kapteni Kendrick akamlaani na kumwambia kwa ujasiri kuwa ipo siku mambo yote ambayo walikuwa wakifanya yangewarudia tu. Luteni Weisiko alimfyatua risasi tatu; mbili sehemu ya kifua na nyingine tumboni, na wanajeshi wale wawili wakamwachia Kendrick, naye akaanguka chini. Kwa haraka waliyokuwa nayo kutokana na kutaka kumfikia Casmir upesi, wanaume hao walifikiri Kendrick alipoteza maisha pale pale, lakini kihalisi risasi zile zilikuwa zimezuiwa kwa vazi la Kendrick la ndani. Mshtuo mkubwa wa risasi karibu kabisa na mwili wake ulisababisha Kendrick apoteze fahamu, lakini hakufa.
Alipoanza kurejesha fahamu zake taratibu, alijikuta ndani ya joto kali sana, na moshi mwingi uliyachoma macho yake na pia ukamfanya aanze kukohoa. Alijisawazisha vizuri na kutambua kwamba sehemu aliyokuwepo ilikuwa ikiwaka moto mkali sana kuzunguka nyumba yote, naye akajitahidi kunyanyuka haraka ili atafute sehemu ya kutokea. Aliweza kuiona miili ya wanawake wale watatu pale chini, naye akasikitika sana, lakini akajikaza na kuanza kutangatanga huku na huko kutafuta sehemu ya kutokea.
Moto ulikuwa mkali sana, na moshi ulimfanya aishiwe nguvu. Hivyo akaona hakukuwa na njia nyingine ya kutokea ila mlangoni pale pale. Akavua jaketi, kisha akaitoa bulletproof vest na kulivaa jaketi tena. Akaitumia bulletproof vest kujikingia usoni, na kwa kupigia mahesabu sehemu ya mlango ilipokuwa, akatoka kwa kasi akikimbia kuelekea upande huo. Moto ulimuumiza sana sehemu za pembeni lakini hakukata tamaa. Ilikuwa ni kama moto unamzuia asisonge mbele, na ilionekana kama haungekwisha, lakini HAKUKATA TAMAA.
Mwishowe, alitoka mpaka sehemu ya nje na kudondokea chini, akihisi maumivu mengi mwilini kwa sehemu zilizounguzwa kwa moto. Mpaka kufikia wakati huo hakukuwa na mtu hata mmoja aliyesogea hapo kwa kuwa nyumba hii ilikuwa imejitenga na zingine. Alipumua kwa presha akihisi maumivu mengi sana, lakini akajikaza na kunyanyuka, kisha akalielekea geti na kutoka mpaka sehemu alipoegesha gari lake. Akaingia na kuliwasha, na sehemu aliyokuwa akipanga kuelekea ilikuwa ni kule kule ambako Casmir alimwelekeza.
Lakini mwanaume huyu alipata shida sana kuliendesha gari akiwa ndani ya hali yake iliyozidi kuwa mbaya. Aliendesha kama mtu aliyekuwa amelewa, hivyo akaona asimame kwanza ili atafute msaada wa maji. Alitoka ndani ya gari na kuelekea kwenye nyumba moja ambayo aliita sana wenyeji wamsaidie. Kwa sababu ilikuwa ni usiku, watu wa pale waliogopa na kufikiri labda ni mtu mbaya, lakini baada ya kuona ameumia kweli, wakamsaidia. Walipendekeza kumpeleka hospitali, lakini Kapteni Kendrick akawaambia alichohitaji ilikuwa ni maji mengi tu kwa kuwa hakuhitaji kwenda hospitali. Walimpa maji, naye akanywa na mengine kuyatumia kujikandia.
Wenyeji walimshangaa kiasi kwa sababu alionyesha ustahimilivu wa hali ya juu sana, ila sababu ilikuwa ni uimara wa mwili wake wenye uzoefu na mafunzo ya kijeshi. Akawaomba wamsaidie vitambaa vyovyote ili afunike sehemu alizobabuka, na ingawa hawakuwa na vitambaa vingi, kwa fadhili mwenye nyumba akatoa shuka moja na kulichana-chana ili wapate nguo ndefu-ndefu za kumfungia. Walikuwa ni watu wazuri, naye Kendrick akawashukuru na kuwaahidi kwamba ipo siku angewalipa kwa ukarimu wao.
Bila kukawia, Kapteni Kendrick akaondoka hapo baada ya kuwa amejisikia uafadhali. Aliendesha gari lake kwa kasi sana kuelekea kule walikoahidiana kukutana na rafiki yake; akitumaini hakuwa amechelewa mno. Roho ilimuuma sana kwamba hakuweza kuwasaidia watu wa familia yake, hivyo kama angeweza kuisaidia familia ya rafiki yake, basi ingetosha sana, kwa sababu hao ndiyo waliokuwa kama ndugu aliobakiza.
Lakini matumaini yake yaliingiwa na vikwazo pale alipokaribia maeneo ya kule walikokuwa wakina Casmir na kuanza kusikia sauti za milio ya risasi. Akaona asimamishe gari umbali fulani kutoka huko ili aweze kwenda kwa njia ambayo hangeonwa kirahisi. Risasi hizo alizosikia zilikuwa kiashirio kwamba Weisiko aliwafikia marafiki zake, naye Kendrick akaendelea tu kuomba kwa Mungu na wao wasiwe wamewaua pia, ijapokuwa nafasi ilikuwa finyu sana.
Alijongea kwa umakini sana mpaka sehemu ambayo alianza kuwaona watoto wa Casmir wakitoka ndani ya gari huku wameshikiliana, na risasi zilikuwa zikifyatuliwa kuelekea upande wao. Akaangalia upande ambao risasi zile zilikuwa zikitokea, naye aliweza kuiona miili ya watu watatu ambao aliwafahamu vizuri sana; Salome, Casmir, na Alice pia. Aliingiwa na simanzi kubwa sana moyoni, naye akaanza kutokwa na machozi kwa kuwa sasa rafiki yake kipenzi pia hakuwa hai tena. Alijilaumu kiasi pia moyoni kwa kutoweza kufanya mengi ili kuwasaidia wapendwa wake.
Aliweza kumwona Luteni Weisiko pamoja na mwenzake wakijitengeneza, bila shaka ili kuwafatilia watoto wale, naye akaingiwa na hasira kali sana kwa kumwangalia mwanaume huyo aliyetumiwa kuwafanyia mambo mabaya sana watu wasio na kosa lolote. Akawaona walipoanza kuwafatilia watoto, naye akatoka alipokuwa ili aelekee huko huko, akiazimia kuwasaidia watoto kwa kukomesha unyama wa wanaume hao haraka iwezekanavyo.
Kwa kuwa aliwahi kuja huku na kutembelea baadhi ya maeneo yenye msitu ule, alitumia njia nyingine ambayo alijua ingemkutanisha kwa mbele na watoto wa Casmir. Ambacho hangeweza kujua ni kwamba watoto wale waliamua kujigawa kwa kutumia njia tofauti ili maisha ya wawili yaweze kuokolewa; ikiwa ni wazo la Xander kwa dada zake wawili Sandra na Azra. Kendrick pia alikuwa amechoka, alihisi maumivu mwilini na hata hisia za kupoteza matumaini, lakini bado aliendelea kufanya yote ili kupigania yaliyokuwa muhimu kwake, hata kama ingemaanisha kuuhatarisha uhai wake mwenyewe.
Alizungukia upande wa mbele wenye miti mingi akiwa na matumaini kwamba angekutana na watoto na kuwasaidia kutumia njia tofauti ya kutorokea ili kuwapiga chenga wale jamaa, kisha angehakikisha wanakuwa sehemu salama ili yeye ashughulike nao hatimaye. Alifika sehemu ambayo kwa kutumia maarifa yake aliweza kujua kwamba kuna mtu alikuwa ametulia hapo, kimya, lakini bado hakuweza kubaini ilikuwa ni nani, hivyo akaona naye atulie. Haikupita muda mwingi na hatua za kukimbia kwa mtu zikasikika, na hapo akamwona mwanajeshi yule, Goko, akisimama na kutulia huku anajaribu kuangalia huku na huko.
Kendrick alikuwa ameshaanza kupiga mahesabu ya kumfata, lakini akashtushwa kiasi baada ya kusikia mlio wa risasi kutokea upande tofauti usiokuwa mbali sana na hapo. Aliporudisha macho yake kwa Goko, aliweza kumwona sasa mtu yule aliyekuwa nyuma yake akinyanyuka na kutaka kumshambulia Goko kwa jiwe, lakini Goko akamkwepa na kupiga risasi hewani baada ya jiwe hilo kupiga bega lake badala ya kisogo. Mtu yule akaanguka chini, naye Kendrick akatambua sasa ilikuwa ni Sandra (ikiwa ni Xander kwa ndani), hivyo akaanza kunyata taratibu kumwelekea Goko nyuma yake.
Mwanajeshi huyo mwenye kiburi alikuwa akimwambia maneno ya dharau Sandra (Xander) wakati Kendrick alipokuwa amekwishamkaribia zaidi, na ile Goko alipogeuka tu, Kendrick akamrukia na kuangukia naye pembeni. Alianza kumtandika ngumi nzito za kichwa na usoni pia, na kwa jicho la mbali aliweza kumwona Sandra (Xander) akikimbia kwa hofu. Lakini akaona amalize kumshughulikia kwanza mwanaume huyo, kisha ndiyo angemfata mtoto.
Goko alikuwa akijaribu kujirudisha juu kibishi lakini Kendrick akamzidi nguvu na kumvunja vidole kwenye kiganja chake, halafu akachukua jiwe zito pembeni na kumponda nalo kwa nguvu kifuani. Goko akatulia tuli. Kendrick akajinyanyua upesi na kumvuta kwa nguvu, kisha akajitahidi kumbeba begani kwake. Alianza kutembea pamoja naye kuelekea upande ambao alijua ulikuwa na bonde refu sana kuelekea chini, na akiwa bado anatembea naye, mdomo wa Goko ulitoa damu zilizodondoka ardhini kufatisha njia aliyopitia Kendrick. Kendrick alipofika usawa wa sehemu ile, akamshusha mwanaume huyo na kumsukuma chini kule kwa nguvu sana.
Kisha akageuka na kuanza kurudi kule alikoelekea Sandra (Xander). Alimwona wakati alipokuwa anakimbia kwamba "binti" huyo hakuwa na nguvu za kutosha kwa sababu fulani, hivyo akajitahidi kuwahi kabla hajaingia mikononi mwa mtu mwingine mbaya. Ilikuwa kwa tukio baya tu kwamba alisahau kuichukua bunduki ya Goko kwa ajili ya kumshambulia adui, kwa sababu kile alichowaza hasa kilikuwa ni kuokoa watoto. Lakini pia hakujua wengine wawili walikuwa wapi, ingawa mlio ule wa risasi aliosikia ulimpa wazo la kwamba huenda walikuwa upande ulipotokea.
Akiwa anamtafuta Sandra (Xander) kwa bidii, aliweza kusikia tena sauti ya risasi sehemu ambayo alitambua haikuwa mbali. Akageukia upande huo, na upesi akaanza kuuelekea lakini kwa tahadhari kubwa. Alifika sehemu ambayo ilikuwa na vichaka kumzunguka, na hapo akaweza kumwona "Sandra" akiwa amejilaza chini. Alipoangalia mbele zaidi, aliweza kumwona Luteni Weisiko akiwa amesimama tu, hivyo kwa uangalifu akaingia sehemu ile ya kichaka alipojilaza Sandra (Xander) na kufika nyuma yake taratibu.
Sandra (Xander) alikuwa ameanza kujinyanyua kivivu sana, na kwa haraka Kendrick akatambua kwamba alikuwa anataka kumsemesha Luteni Weisiko. Akasogea karibu yake upesi na kumfunika mdomoni kwa kiganja chake kutokea kwa nyuma. Alipoangalia kuelekea pale aliposimama Weisiko, sasa aliweza kuwaona Azra na Xander (ikiwa ni Sandra kwa ndani) wakiwa wamelala chini kwa ukaribu, na wakionekana kuwa mbali na uhai. Kendrick akahuzunika sana.
Sandra (Xander) alikuwa akijaribu kujinasua kutoka kwa mtu aliyemfunika mdomo kwa nyuma, lakini nguvu zake zikamwishia na kupoteza fahamu. Kendrick akaanza kumvuta nyuma taratibu, kisha akamwangalia kwa umakini. Aliona jeraha lake la tumboni sasa, naye akatambua kuwa alikuwa amepoteza damu nyingi sana. Lakini "binti" huyu bado alikuwa hai, hivyo Kendrick akajikongoja tu na kumbeba mgongoni, kisha akaanza kuondoka naye kutoka sehemu hiyo. Mambo ambayo familia zao zilikuwa zimepitia usiku huo yalikuwa mazito sana.
Kendrick alijitahidi kwa uwezo wake wote kumwahisha "Sandra" sehemu ambayo angeweza kupata tiba ya haraka, na pia ili kuokoa uhai wake kutoka kwa Weisiko. Alijua hiki ni kitu ambacho rafiki yake aliyepoteza uhai angehitaji sana amfanyie, na kumbukumbu ya mambo mengi waliyopitia pamoja ilimwongezea nguvu ya kupambania uhai wa binti yake. Aliweza hatimaye kutoka ndani ya msitu ule akiwa bado kambeba "Sandra" mgongoni. Alikuwa amechoka sana, lakini akakazana. Yaani hakutaka kugeuka nyuma kwa kuwa alielewa sasa jukumu la kuokoa uhai wa mtoto huyu lilikuwa mikononi mwake. Akampeleka mpaka kwenye gari alilokuja nalo eneo hilo na kumweka ndani yake, kwa nyuma, kisha naye akaingia kwenye usukani na kuliondoa hapo upesi.
★
Mwendo mzima alikuwa akimuwaza sana mama yake, Casmir, Alice, Xander, Azra na Salome. Alitiririkwa na machozi mengi sana akihisi kama ni ndoto jinsi siku hiyo iliyotakiwa kuwa ya furaha (kwa sababu ya birthday ya Alice), ilivyobadilika na kuwa anga ya umwagaji wa damu. Ilikuwa ni saa 9 iliyoelekea saa 10 usiku sasa, naye akafanikiwa kumfikisha Sandra (Xander) kwenye Zahanati fulani ya kanisa la kikatoliki, eneo ambalo halikuwa mbali sana na mpaka wa kuingia mkoa mwingine.
Alishukuru sana Mungu baada ya kukuta wauguzi wawili hapo waliomwambia kwamba kuna daktari wa Zahanati hiyo ambaye hufika mida ya saa 11 kwa kuwa huwahi kuondoka baadae tena, hivyo wakamsaidia kumwingiza Sandra (Xander) ndani na kumwekea 'drip' muhimu upesi. Wauguzi wale walitambua kwamba Kendrick na Sandra (Xander) walikuwa wameumia vibaya sana, na walipouliza tatizo, Kendrick akasema walikumbwa na mambo mabaya kutoka kwa watu fulani waliotaka kuwaumiza. Akawaomba waangalie ikiwa itawezekana kuanza taratibu za kumwongezea damu "Sandra," lakini wauguzi wakamwambia kuwa hawakujua mambo mengi ya kufanya mpaka daktari afike.
Hii ingekuwa hatari kwa sababu mwili wa "Sandra" ulikuwa umepoteza damu sana, na kumsubiria daktari kwa saa zaidi ya moja huenda kungeleta matatizo. Hivyo Kendrick akawaomba sana watafute njia yoyote ile kwa sababu alikuwa amepoteza watu wengi sana usiku huo na hivyo hangetaka kumpoteza na "binti yake." Wauguzi wale walimwonea sana huruma, na kwa neema tu ya Mungu, mmoja wao akasema anajua mambo fulani kuhusu kuwaongezea damu wagonjwa, hivyo waangalie ikiwa kundi lake la damu liliendana na la "Sandra" ili waweze kutoa ya kwake Kendrick kiasi na kumwekea "binti yake."
Kendrick akakubali na upesi muuguzi huyo akampima na kulinganisha na ya "Sandra," kukuta zinaendana. Kendrick akafarijika sana. Aliendelea kuomba kwa Mungu kuwa angalau binti huyu apone, kwa sababu alitaka sana kuuokoa uhai wake kwa kuhisi alishindwa kufanya hivyo kwa wengine. Wauguzi wale walijitahidi kumsaidia kwa kadiri ya uwezo wao, na uzuri ni kwamba angalau kwa muda huo hakukuwa na wagonjwa wengine waliohitaji huduma za dharura, hivyo walikazia uangalifu kwa hawa wawili.
Sandra (Xander) aliwekewa drip iliyomwingizia damu sasa, na kilichokuwepo ilikuwa ni kusubiri daktari afike. Lakini tena, bado Kendrick alijua yeye kuwa hapo kwa muda mrefu ingekuwa hatari zaidi kwao, hasa kama taarifa kuhusu yeye na "Sandra" kufika kwenye Zahanati hii zingewafikia wabaya wao, na hivyo hata kuhatarisha usalama wa wale waliofanyia kazi hapo. Walikuwa wemeshakaa hapo kwa saa kama moja na daktari hakuwa amefika bado kama wauguzi wale walivyosema, na ijapokuwa alijua hali ya binti wa rafiki yake ilikuwa mbaya, akaamua tu kuondoka naye kabla ya daktari kufika.
Kendrick alimbeba ''Sandra" mikononi mwake kwa uangalifu, akiwa ameshikilia kimfuko na mrija uliomwingizia damu mshipani, naye akatoka naye kuelekea kwenye gari nje. Wauguzi wale walimshangaa na kumuuliza kwa nini alifikia uamuzi huo ambao ulikuwa hatari kwa mgonjwa, lakini Kendrick hakuwajibu lolote na kumpeleka "Sandra" mpaka ndani ya gari. Kwa akili akautundika mrija ule wa damu ndani ya gari kwa njia ambayo ungeendelea kumwingizia damu "Sandra" mshipani akiwa amelala kwenye siti za nyuma. Wauguzi wakadai kwamba alihitaji kulipia, lakini Kendrick akasema ni Mungu ndiyo angewalipa kwa msaada wao, kisha akaingia ndani ya gari na kuondoka eneo hilo.
★
Kila mara Kendrick alipofikiria kuhusu usalama wake na wa binti huyu aliyekuwa amepoteza fahamu, alishindwa kujua ikiwa angeweza kujificha huku akielewa kwamba mtoto huyu alihitaji tiba bora zaidi, kwa sababu kama sivyo, basi na huyu angekufa akiwa mikononi mwake. Akaendelea kuomba msaada kutoka kwa Mungu kwamba "Sandra" asikate tamaa na kuendelea kupambania uhai wake ndani kwa ndani, ili yeye Kendrick atafute mazingira mazuri zaidi ya kumsaidia binti huyu. Wazo moja la mtu ambaye angeweza kumsaidia likamwingia, naye akaiwekea akili yake sehemu ambayo angetakiwa kwenda ili kujilinda kabla ya msaada kutoka kwa mtu huyo kumfikia.
Aliendelea kuendesha gari lake mpaka akatoka nje ya mkoa huo, ikiwa inaingia saa 1 asubuhi. Alifika maeneo ambayo aliona vibanda kadhaa vya simu za mawasiliano, naye akasimamisha gari lake na upesi kwenda kule. Lakini alipofika akakumbuka tena kwamba alihitaji hela ya kulipia ili aweze kupiga simu, lakini hakuwa na hela mfukoni. Akarudi tena kwenye gari kuangalia kama kulikuwa na sarafu zozote ambazo aliweka humo kipindi cha nyuma na kuzisahau, kwa kuwa kihalisi alihitaji mia mbili tu kwa ajili ya kudumbukiza kwenye mashine ile. Akatafuta na kutafuta na hatimaye akapata mia sita za sarafu, naye akamwangalia "Sandra" kiufupi. Damu ile ilikuwa imeisha kufikia wakati huu, naye "binti" hakuwa amerejesha fahamu bado. Upumuaji wake ulionekana kuwa wa kawaida tu, hivyo Kendrick akatoka hapo kwa kasi tena kuelekea kwenye kibanda kile, kisha akaweka mia mbili na kupiga namba fulani.
"Hallo..." sauti upande wa pili ikasikika.
"Hello... General... ni mimi Kendrick Jabari...." Kendrick akasema.
"Kapteni... vipi mbona mapema? Halafu kweli, umenikumbusha kuna..."
"General, yametukuta matatizo makubwa sana! Meja Casmir hatuko naye tena, familia yake pamoja na yangu zimeuawa kikatili sana usiku wa kuamkia leo," akasema Kendrick kwa huzuni sana.
Jenerali Pingu akaweka umakini wake vizuri zaidi.
"Subiri Kapteni... unamaanisha nini?" akauliza.
"General mambo ni mengi sana ya kuzungumzia, lakini siwezi kusema kila kitu hapa. Nakuomba usiseme lolote kwa yeyote yule kuhusu simu hii... tafadhali sana," Kendrick akaomba.
"Unaongelea kuhusu... Demba Group au?"
"Hapana... ndiyo... yaani... ni..."
"Kendrick jaribu kutulia. Uko wapi?"
"Sijajua sana mkuu... ila nimetoka jijini huko masaa kadhaa nyuma ninaelekea kule ambako Meja na mimi tulijenga handaki chini, si unapakumbuka?"
"Ndiyo..."
"Ninaenda huko. Tafadhali General usimwambie yeyote, maisha yako pia yanaweza kuwekwa hatarini..."
"Si uniambie kinachoendelea kwa ufupi..."
"Siyo rahisi sana... ninahitaji kuwahi kwa saba... Gen... halloo... aagh!"
Muda wa kuongea ukawa umekwisha hivyo simu ikawa imekata. Kendrick akaweka mia mbili nyingine na kumpigia tena Jenerali Pingu.
"Kendrick..." akasema Jenerali Pingu baada ya kupokea tena.
"General... ni wewe tu zaidi ya Meja ndiyo unapafahamu huko, tafadhali usimwambie yeyote na uje peke yako. Ni suala la uhai au kifo. Watu tunaowaamini ndiyo wanaotuzunguka. Tafadhali futa au hata utupe simu mbali tukimaliza maongezi haya," Kendrick akasema.
"Kendrick umenichanganya sana kwa kweli yaani... sielewi nichukulie vipi haya yote..."
"Niamini General tafadhali. Nakusihi ufanye hivyo..."
"Sawa, nitafanya hivyo. Nitakuja moja kwa moja huko ijapokuwa nilikuwa na mipango mingine leo..."
"Asante sana. Nakuomba pia ukiweza General... uje na mifuko kadhaa ya damu type B, dawa za kuongeza nguvu, glucose, na vifaa mbalimbali muhimu vya kitiba... pitia kwa hospitali, sijui kama itahitajika gharama na nini lakini... ninahitaji kwa sababu nina mtoto hapa... ametokwa na damu nyingi... ameumia sana," Kendrick akasema.
"Aisee! Sawa Kendrick, usijali niko pamoja nawe. Nitaleta kila kitu. Natumaini pia mambo yote yatakuwa wazi nikifika. Nisubirie tu kijana wangu," Jenerali Pingu akamwambia.
"Nitashukuru sana... kwa heri," Kendrick akasema na kukata simu.
Akarudi kwenye gari haraka na kuliwasha ili waendelee na safari. Akamwangalia "Sandra" kupitia kioo cha juu mbele ya gari.
"Usijali binti yangu, Mungu ni mwema, utakuwa sawa. Keep fighting," Kendrick akasema hivyo.
Kisha akaliondoa gari hapo upesi.
★
Ilimchukua masaa kadhaa kufika kule alikodhamiria. Akashuka kutoka ndani ya gari na kumtoa "Sandra" akiwa amembeba, kisha akaanza kuelekea naye kule kwenye sehemu ya kujifichia.
Handaki hilo alilosemea Kendrick (tunnel), lilikuwa ni handaki walilosaidiana na Casmir kujenga kipindi cha nyuma, kwa ajili ya kujificha nyakati za hatari. Kuna wakati ambao kulitokeaga vita na taifa jirani, na wawili hao walipokuwa wakiwakimbia adui baada ya shambulizi la kushtukiza, walidumbukia kwenye shimo refu na kukaa humo kwa siku chache. Ndipo baadae walipofanikiwa kutoka, waliamua kuifanya iwe sehemu ya maficho kwa ajili yao na baadhi ya wanajeshi wengine, lakini hawakumwambia yeyote zaidi ya Jenerali Pingu kuhusu sehemu hiyo, ambaye aliwapendekezea waitengeneze vizuri na kulipanua chini kwa chini kwa ajili ya matumizi muhimu ya wakati ujao. Ilikuwa kwenye maeneo yaliyozungukwa na misitu na mashamba makubwa ya baadhi ya watu, lakini hakukuwa na makazi ya watu maeneo ya huku kipindi hiki. Njia ya kuingilia kwenye handaki hilo la chini ya ardhi ilifunikwa kwa mawe na mimea mingi yenye miiba, na kufikia wakati huu palikuwa panaonekana kama sehemu ya kichaka; hivyo haingekuwa rahisi kwa yeyote kutambua kulikuwa na handaki sehemu hiyo kwa sababu ilifichwa vizuri.
Kendrick akamweka "binti" chini na kuanza kuyaondoa majani na mawe sehemu hiyo, kisha akaanza kufukua udongo mwingi mpaka alipofikia chuma ngumu. Akauondoa udongo wa juu uliofunika chuma hiyo na kuivuta. Ilikuwa ni aina ya chuma nzito yenye umbo la duara ambayo ilikuwa kama mlango mdogo tu wa kuingilia chini huko, naye akauweka pembeni na kumfata "Sandra." Alikuwa makini kuangalia huku na kule kuona kama kungekuwa na mtu yeyote na kukosa, hivyo akambeba na kusogea naye pale.
Ilikuwa ngumu kuingia chini huko kwa sababu ya kuwa na mtu aliyepoteza fahamu, lakini Kendrick akajitahidi sana kuingia kwa uangalifu akiwa amemweka mgongoni kwake. Kushuka chini huko zilijengwa ngazi za shaba zilizokuwa imara, na ilionekana ni kama anaingia kwenye kisima. Akiwa amefikisha kichwa kwa ndani, akauvuta mlango ule mdogo wa chuma na kupafunika, kisha akaufungia kwa ndani. Alianza kushuka taratibu; mkono mmoja angekuwa ameutumia kuishikilia mikono ya "Sandra" iliyozungikia shingoni mwake, huku mkono mwingine akiutumia kushikia sehemu zile za ngazi. Hivyo kila akiposhusha mguu chini, angebadili mkono haraka wa kumshika binti na kutumia aliokuwa amemshikilia mwanzo kushikia sehemu za ngazi.
Akafanikiwa kufika chini, pakiwa na giza haswa, lakini kwa sababu alijua jinsi mpangilio ulivyokuwa, akatembea taratibu kuelekea upande ambao alijua kulikuwa na godoro chini. Akamlaza hapo taratibu na kuanza kupapasa sehemu ambayo alijua kulikuwa na viberiti, kisha akapata kimoja na kuwasha, naye akachukua chemli iliyokuwa humo na kuiwashia moto ili wapate mwanga.
Handaki hili halikuwa kama vile mahandaki ya wazungu ambayo yamejengwa kwa utaalamu, kwa sababu waliohangaika kulitengeneza walikuwa watu wawili tu, tena kwa miaka kadhaa. Jenerali Pingu alitaka iwe siri kwa kuwa ingekuwa ndiyo sehemu maalumu kwa wakati ujao kwa ajili ya masuala ya vificho, na kwa kipindi fulani ilionekana kama mipango hiyo iliahirishwa hasa baada ya majukumu yao jeshini kuongezeka, hivyo waliliacha tu kwa muda. Kendrick akawa ameketi karibu na "Sandra" akiangalia upumuaji wake na joto la mwili. Bado kijana alionyesha uvumilivu wa hali ya juu kwa kuwa hakupoteza uhai, naye Kendrick akaendelea kuomba kwa Mungu Jenerali Pingu awahi kufika, na akiwa salama.
★
Ulipita muda wa kama saa zima na nusu hivi pale Kendrick aliposikia kama kimlango kile cha chuma kinagongwa kwa kule juu. Akamwacha "Sandra" na kwenda kuangalia ilikuwa ni nani. Akapanda mpaka kufikia karibu zaidi, naye akatulia kusikilizia kama ungegongwa tena. Ukagongwa tena, naye Kendrick akagonga hapo kidogo pia, na sauti ya Jenerali Pingu ikasikika kwa juu.
"Kendrick, ni mimi. Nifungulie."
Kapteni Kendrick akafungua lock kwa ndani na kukinyanyua juu kidogo kimlango hicho, naye Jenerali Pingu akakitoa chote na kukiweka pembeni. Jenerali alishtushwa kiasi baada ya kuona jinsi Kendrick alivyokuwa amebabuka sehemu za mwili na upande mmoja wa uso wake, kuonyesha aliunguzwa vibaya sana kwa moto.
"Kendrick..."
"General, ingia haraka," Kendrick akamkatisha.
Jenerali Pingu akampatia begi moja ambalo lilikuwa na vitu vingi kwa ndani, naye akaingia pia akiwa amebeba begi lingine mgongoni. Akahakikisha ameufunga kwa ndani mwingilio ule kisha akashuka mpaka kule chini. Akamkuta Kendrick akiwa tayari amelifungua begi lile na kuanza kutoa vitu alivyohitaji kama mifuko ya damu, mirija, sindano, tochi, dawa kadhaa, akifanya upesi sana ili kumhudumia "binti" huyo.
Jenerali Pingu akasogea karibu zaidi na kuanza kumsaidia.
"Huyu si ni mtoto wa Casmir? Imekuwaje... nini kimetokea?" Jenerali Pingu akauliza.
"Nitakueleza kila kitu. Tumsaidie kwanza," Kendrick akasema.
Wakafanya yote waliyoweza ili kumsaidia. Wakamwekea damu, dawa, na kukisafisha kidonda chake cha kukatwa kwa kisu tumboni na kukiziba kwa dawa. Jenerali Pingu alikuwa ameleta maji na chakula kingi pia kisichoweza kuharibika, naye akampatia Kendrick ili aweze kula baada ya kuwa wamemaliza kumpa huduma "Sandra."
"Naona kama umewahi sana kufika General..." Kendrick akasema.
"Nilitumia helicopter kufikia kambi moja. Lakini kuja huku nilichukua gari na nilihakikisha sifuatwi," Jenerali Pingu akajibu.
"Natumaini haukuvamia hospitali kwa ajili ya vitu hivi vyote," Kendrick akasema huku akijaribu kumnywesha maji "Sandra."
"Hapana, nimenunua. Kendrick... mtoto anahitaji kuwa hospitali huyu. Na wewe unaonekana kama unahitaji tiba muhimu pia. Umeungua vibaya...."
"Niko sawa General... niko sawa," Kendrick akasema.
Jenerali Pingu akabaki kimya tu huku akimwangalia kwa huruma.
Kendrick akashusha pumzi huku ameinamisha kichwa chake kwa huzuni. Alionyesha kuchoka sana. Kisha akaanza kumsimulia Jenerali Pingu kila kitu kilichotokea. Kuanzia jinsi Kanali Jacob, Luteni Weisiko, Makamu wa Raisi, na wengine ambao hakuwatambua walivyoongea kuhusu mipango yao ya kumwondoa yeye na Casmir kwenye dunia ili mipango yao ifanikiwe. Alimweleza kuhusu jitihada zake na Casmir za kuwakamata Demba Group, na kwa kuunganisha matukio kwa haraka waliweza kubaini kwamba Demba Group ilikuwa ni kitu walichofanya watu hao. Jenerali Pingu akaweka wazi kwamba hakutoa amri yoyote kwa Kanali Jacob kuwaambia Meja Casmir na Kapteni Kendrick wahamie kule kwenye ofisi jijini kwao. Hii ilikuwa ni njia tu ya watu hao kuwasogeza wawili hawa karibu ili waweze kuwaangamiza kiurahisi. Kendrick akamweleza jinsi watu hao walivyo na ufundi katika mambo wanayofanya, ikionekana wanapewa nguvu kubwa sana, hivyo hata kwenda hospitali ingekuwa shida kwao.
Jenerali Pingu alikasirika sana. Alishindwa kuelewa ni kwa upumbavu kiasi gani wanaume wale waliweza kuruhusu tamaa ziwafanye watende unyama mkubwa namna hiyo. Hakukuwa na jambo lingine walilotaka tofauti na tamaa tu za kutaka kupata mambo makubwa; Jenerali Pingu aliona hilo wazi. Akamwambia Kendrick angeshughulika nao wote haraka sana, lakini Kendrick akamwambia alipaswa kuwa mwangalifu kwa kuwa watu hao walikuwa makini mno. Hakutaka kuhatarisha usalama wao hasa kwa sababu wangefikiri wamekufa, hivyo huenda Jenerali Pingu angemhatarisha tena "Sandra." Lakini mzee Pingu akamhakikishia kwamba haingekuwa hivyo, na kwa sababu Kendrick alikuwa amejifichia mbali, hangemhatarisha mpaka ahakikishe amewakomesha wanaume wale.
Baada ya kuwa ametumia muda huu na Kendrick, Jenerali Pingu akamuaga na kumwambia asitoke hapo mpaka atakaporudi. Kama ni vyakula vilikuwepo, dawa zilikuwepo, na hata ingawa ilikuwa chini ya ardhi, bado waliweza kupumua vizuri. Jenerali akamwahidi kwenda kuizimisha mipango ya wabaya wale haraka iwezekanavyo ili Kendrick na binti ya Casmir wasiendelee kujificha tena. Akamwambia akimaliza hayo, angemsaidia yeye na "Sandra" wapate matibabu nje ya nchi kabisa, naye akampatia Kendrick simu mpya ambayo aliiwekea laini maalumu anayoweza kuitumia hata akiwa nje ya nchi, na kumwambia wakati ambao angempigia tu, basi tayari angekuwa amekwishamaliza kuwashughulikia waasi wale.
Kendrick alijua wazi kwamba sikuzote matokeo huenda yasije kwa jinsi ambavyo wangetarajia, hivyo akamsihi sana Jenerali awe makini. Jenerali Pingu akaondoka hatimaye, na wakati alipotoka alihakikisha anaweka majani na mimea mingi ya vichaka kupaziba hapo juu ili hata kama nani angepita basi pasionekane kiurahisi, ingawa eneo hilo halikutembelewa na yeyote kwa ukawaida kutokana na kuwa kama msitu tu. Kendrick akabaki akimhudumia Xander, bila shaka yeye akifikiria ni Sandra, na wakati akiwa anaendelea kumwangalia usingizi ulimpitia kutokana na uchovu mwingi.
★
Kendrick alipokuja kuamka, bado alikuta "Sandra" amelala. Kipimo cha damu alichokuwa amemwekea kilikuwa kimekwisha, na "binti" alikuwa anatokwa na jasho sana, naye Kendrick akatambua kuwa homa kali ilikuwa imemtawala kwa sababu alichemka mno. Kendrick alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake wote kumpa huduma za kwanza ili kuituliza hali yake. Hakuchoka kumsaidia mtoto wa rafiki yake kwa sababu alihisi uhai wake ulikuwa mikononi mwake. Alimkanda, alimpa dawa kwa njia ya sindano, akambadilishia pamba kwenye kidonda, na kuendelea kuhakikisha anaituliza homa yake.
Ulipita muda mrefu wakiwa chini hapo, na wazo la kuiangalia simu ile likamjia. Akaiwasha na kuona ilikuwa ni Jumatatu sasa kwenye saa 4 asubuhi, ijapokuwa chini huku ungesema muda wote ni usiku tu, na kwa haraka alitambua ulikuwa umepita muda kiasi bila "Sandra" kula chochote. Hivyo akampatia maji kidogo na juisi nzito kama chakula, huku "binti" bado akiwa amelala. Alimnywesha taratibu na kwa uangalifu ili kiasi kingi kiingie tumboni mwake, na baada ya hapo akaanza kumkanda tena.
Kendrick aliwaza mengi kuhusu ni nini kilichokuwa kikiendelea kule nje. Alijua Jenerali alisema ni yeye ndiyo angemtafuta, lakini kwa sababu ya haraka yake kutaka kuondoka hawakutilia maanani kwamba mtandao chini huku ungeleta shida kubwa. Aliangalia uwezekano wa kupata hata "baa" moja ya mtandao, lakini haikuwezekana. Akaanza sasa kujiuliza afanye nini. Hakujua ikiwa "Sandra" angeendelea kuvumilia kwa kuwa uwezekano wa yeye kufa akiwa ndani ya usingizi ulikuwa mkubwa, na muda haukuwa rafiki kwao. Hivyo akaamua kutoka nje ili atafute mtandao, halafu ampigie Jenerali Pingu yeye mwenyewe. Akamwacha "binti" katika mazingira mazuri, kisha akaenda nje kule haraka. Bado eneo hilo halikuonekana na mtu yeyote, hivyo akaamua kwenda mpaka kule alikoliegesha gari lake kwa kificho. Akaingia ndani yake na kupiga simu kwa Jenerali Pingu. Mtandao ulikuwa ukileta shida, lakini hatimaye simu ya upande wa pili ikaita.
Ilipokea sauti ya mwanamke, naye Kendrick akasema ni rafiki ya Jenerali na alitaka kuzungumza naye. Lakini mwanamke huyo akamwambia kwamba Jenerali Pingu hakuwa hai tena, kwa sababu aliuawa kikatili na watu waliojiita Demba Group. Kendrick alichoka! Akauliza ilikuwaje, na mwanamke huyo akamweleza alivamiwa wakati wa usiku na watu hao alipokuwa amefika kwake, nao watu wote waliokuwepo nyumbani kwake wakauliwa pamoja naye.
Simu ikashuka taratibu kutoka sikioni mwa Kendrick kwa mshtuko mkubwa uliompata. Alijiuliza angefanya nini sasa, kwa sababu tumaini lake la mwisho wakati huu lilikuwa limetoweka pia.
★★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★★
Comments