Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

SEHEMU YA 23.

Yonesi aliishia kuinua kichwa na kumwangalia Hamza kwa  sekunde kadhaa na kisha akampotezea  na kuendelea na chakula chake , kitendo kile kiliwashangaza wengi na kuona au Hamza  ameshamuweza Yonesi.

Muda huo Hamza aliweza kuona  Yonesi alikuwa amejisevia Sausage kwenye sahani  yake  lakini hata yeye pia  ni moja ya chakula alichochukuwa , ki ufupi ni kwamba hakubakisha.

Mgahawa huo wa kampuni chakula kilikuwa bure  na kulikuwa na msururu wa  mapot makubwa ambayo yanachakula , ni kazi yako kupita na kujisevia tu.

“Kapteni , kumbe  na wewe unapenda kula Soseji , unaonaje nikikupatia na yangu?”

Maneno hayo yalisikika  kikarimu lakini  kadri alivyoyafikiria ndio aliona ni kama kuna zaidi ya maana  na  mwili wake ulianza kubadilika rangi na kujihisi kupatwa  na joto licha ya eneo hilo kuwa na AC, aliona kabisa Hamza alikuwa  akimfanyia hivyo makusudi kabisa.

“Usije ukanidhania vibaya , naamanisha soseji  ya kwenye sahani yangu…”Aliongea Hamza huku akijifanyisha ni mwenye aibu.

Kadri alivyokuwa akiongea ndio ambavyo maneno yake  yalivyoonekana  ya kihuni , wafanyakazi waliokuwa karibu   wakitega masikio yako kama  antena baada ya kusikia kauli  ya Hamza waliishia kucheka.

“Hakuna  ambae atasema wewe ni bubu ukikaa kimya.”Aliongea  Yonesi  huku akijitahidi kuzuia hasira zake.

Watu mpaka hapo waliona kitendo cha Yonesi kuweza kuvumilia utani wa Hamza  inamaanisha  alikuwa  hamuwezi  na  sifa zote walimpatia  Hamza.

Hamza aliishia kushindwa kuongea na kumwangalia  Yonesi namna ambavyo amevaa  , lakini ilionekana kutokana na tukio  la jana  alikuwa amefunga shati  lake mpaka  kifungo cha mwisho.

Hamza aliona ngoja anyamaze adili na chakula chake , lakini  Yonesi  mara baada ya kuona  ametulia yeye ndio aliongea.

“Wapi  umejifunzia mapigano?”

Hamza  alisikia hilo swali , lakini alijifanyisha hajasikia  na aliendelea  kuwa bize na chakula chake, lakini kitendo kile cha kupotezewa kilimuudhi Yonesi  na kumfanya apige meza kofi.

“Wewe , nakuuliza  swali , hujanisikia au?”

“Kapteni si umeniambia  nikae kimya , kwanini unataka niongee  tena , unajua unanitesa”

“Wewe..”Yonesi aliishia kusaga meno  kwa hasira,  alijua fika  mwanaume huyo  alikuwa akikwepa kujibu swali  lake  na kutokana na hasira zake aliishia kuinua sahani yake ya chakula na kisha akaondoka akimuacha Hamza mwenyewe.

Hamza aliishia kutoa tabasamu la kichokozi tu , huku akiangalia mandhari ya jiji  , aliona   inafurahisha sana kutania  wafanyakazi wenzake.

Wakati akirudi kwenda juu kuendelea na kazi Hamza hakusahau kubeba tena matunda kwa ajili ya Regina , siku hio hakuchukua  ma apple tu bali alibeba na zabibu.

Mara baada ya kufika katika mlango wa ofisi ya mkurugenzi , wakati akitaka kuingia aliweza kusikia majibishano kutoka ndani na kumfanya asimame.

“Mzee Sebastian, Mzee Willium ,  kama wakurugenzi wasaidizi  , hebu niambieni sababu ya kwanini  mpo kidedea kupinga  hili ,  naona mnafanya makusudi kabisa kunipinga bila sababu”Aliongea Regina na sauti yake ilionekana imejaa hasira.

“Mkurugenzi wewe ni  binti mdogo sana bado , maji unayotaka kujaribu kukanyaga  yana kina kirefu ,

ununuzi wako wa awamu hii ni wa kukurupuka”Aliongea Mzee Willium.

“Kukurupuka?, mimi ninachoona  hapa ni kwasababu  hamtaki kuona kampuni  inakuwa  kutoka levo iliopo kwenda nyingine  na wasiwasi wenu ni  kuogopa kupoteza nafasi zenu , mnaonaje mkiniambia ni hisa kiasi gani mnahitaji  ili muwe hiari  na msishindane na mimi?”Aliuliza Regina.

“Mkurugenzi sisi  ni wazee ambao tulikuwa nyuma ya  mwenyekiti wa kampuni  aliepita  mpaka kuifikisha kampuni ilipo sasa hivi  hatua kwa hatua , tunaipenda sana hii kampuni ndio maisha yetu , hivyo usiongee ujinga”

“Sitaki kusikia maneno yenu yasio na msingi , nitawapa siku tatu , kama hamtokubali kubadilisha mawazo yenu , kuweni makini maana  kuna uwezekano mkaondolewa kwenye nafasi zenu, nishamaliza , mnaweza kuondoka”Aliongea kibabe.

“Wewe mtoto , kwanini unatufanyia hivi ,  sisi ndio wazee,  msingi wa kampuni”

“In this company , only the subordinates  of the superior  have seniority”Aliongea  Regina kikauzu kwa kutumia kingereza  akimaanisha  wafanyakazi waliopo chini  ya uongozi  ndio wenye uzoefu zaidi.

“Hakuna shida Mkukufu Mkurugenzi , Willium tuondoke zetu , haina haja ya kuongea tena”Aliongea Mzee Sebastian  mara baada ya kupiga kofi kwenye sofa.

Dakika hio hio Mzee Sebastian na  Mzee Willium waliweza kutoka  na mara baada ya kumuona  Hamza ambae amesimama  mlangoni , wakurugenzi hao wasaidizi  nyuso zao zilizidi kuwa ngumu  na kumwangalia Hamza kwa ukali.

Hamza aliishia kupumua tu kwa  ahueni  huku akijiambia mambo hayo hayamhusu hata wamwangalie vibaya, hivyo aliingia zake kwa CEO.

“Unafanya nini hapa na wewe?”Aliuliza  Regina  mara baada ya  Hamza kuingia , alikuwa amesimama kwenye sofa akiwa na ukauzu.

“Kula matunda kidogo , punguza presha  na  acha  kujisababishia matatizo ya mwili kwa ajili ya kazi”Aliongea Hamza  baada ya kumkabidhi boksi lile lenye matunda akiwa na tabasamu.

“Sina hamu ya kula chochote muda huu ,  unaweza kuondoka nayo tu”

“Nishakula share yangu na yaliobaki ndio nimekuletea”

“Nimesema siyataki ,unaweza kuondoka nayo tu”

“Mbona matunda mazuri haya , unataka yaharibike”Aliongea Hamza.

“Sikia , nina kazi nyingi za kufanya sasa hivi , kula mwenyewe”Aliongea na kisha alirudi kwenye  kiti chake .

“Usiniambie unapanga kujipigia zako kile kinywaji tena , ukifanya hivyo  nampigia sasa hivi Shangazi simu”

Regina  mara baada ya kusikia  hivyo  aliishia kugeuza kichwa  chake huku akiwa amefura.

“Kinachokuuma ni nini?, inakuhusu nini  mimi kula  au kutokula , sisi sio wapenzi  bali tupo katika  maigizo tu  ya kimkataba , kwanini unanijali sana?”

“Halafu wewe  ni mwanaume , kuna haja gani ya kumhusisha shangazi kila kitu , Jiamini”

Hamza mara baada ya kusikia maneno hayo aliishia kutoa tabasamu hafifu na kisha aliweka matunda yale kwenye meza.

“Upo sahihi mimi ni mfanyakazi wa mkataba tu hapa ,  sio jukumu langu la kujali  unachokula wala afya yako , hata upatwe na vidonda vya tumbo  ukweli  ni kwamba halinihusu , lakini  ni  juu yangu  kumpa mtu yoyote  chakula  kama  hajala , unaweza kula nimeyaweka hapa au  ukiona vipi yatupe tu” “Wewe..”

“Kitu kingine , Shangazi yule kwako ni  kama mzazi  ambae amekulelea  mpaka leo  hii , kuhusu mimi sina hata wiki tokea tufahamiane , baada ya miezi mitatu kuisha iwe ni wewe au Shangazi sitokuwa na  uhusiano wowote na nyie, hivyo sio kwamba najaribu

kukutishia na yeye , sio swala langu  hili , ninachokukumbusha ni kwamba  ni sawa tu kujifanya mbishi  na mwenye hasira za karibu  lakini  siku zote jaribu kujali na watu wanaokujali”

“Sitaki unifundishe ..”Aliongea Regina mara baada ya kusikia maneno hayo , ni kama yalimgusa kidogo.

Hamza hakuongea lolote zaidi na alitoka katika ofisi  hio na kufunga mlango na kufanya  hali kutulia.

Mara baada ya kuona ameondoka , Regina  alisita kidogo    mara baada ya kukaa katika  meza yake na kuvuta droo , sasa ile  alivyokuwa akitaka kuchukua kile kinywaji cha virutubisho  aliishia kukirudisha chini.

Maneno ya Hamza ni kama yalikuwa yakijirudia rudia katika akili yake , alikuwa akimpenda mno Shangazi yake kwani ndio kama mzazi pekee ambae alikuwa akimwelewa , Regina alivuta pumzi  na kisha alifunga ile droo na kuchukua lile boksi la matunda na kuangalia ndani , lakini mara baada ya  kuona ni  zabibu  alielewa  kwanini  Hamza kafanya  hivyo na aliishia kuona aibu za kike.

“Muhuni sana huyu..”Aliongea na palepale alichukua  Zabibbu zile nyingi katika mkono na kuzisindilia zote mdomoni , zilikuwa na ukakasi , utamu wa aina yake na sukari.

Alitaka kumaliza haraka hivyo alikuwa akila kifujo fujo  ili arudi kwenye kuendelea na kazi ,kulikuwa na vipande vya matikiti pia  na alivichukua na kuvisindilia vyote  na kumfanya hadi mchuzi kumtoka  mdomoni.

Kitendo kile kilimfanya  mashavu kuvimba mnno kama vile ni  mtoto mdokozi anaejaribu kula haraka haraka asishutukiwe.

Muda uleule ndio  Hamza alifungua mlango na kuchungulia ndani  na aliishia kucheka namna ambavyo  mashavu ya Regina yalituna.

Regina alijikuta akitoa mguno mara baada ya  kugundulika alichokuwa akifanya huku akiziba mdomo na  mikono yake miwili.

Mdomo wake ulikuwa umejaa , alitamani kufoka lakini haikuwezekana  na vilevile  alishindwa kumeza kwa haraka  na aliishia kujionea aibu yeye mwenyewe , kwa mkurugenzi mwenye heshima zake na mwanamke ambae anajali taswira yake kuonekana akiwa ametuna mashavu namna hio wakati wa kula ilikuwa aibu.

“Haha.. nilijua tu , umependezaje , kula taratibu  usije ukapaliwa, hebu tukupige na kapicha”Aliongea Hamza.

Regina aliishia kukasirika ndani kwa ndani na kujiuliza kwahio alikuwa amesimama  muda wote mlangoni , inamaana aliotea  nitakula matunda kivurugu vurugu.

Aliona kama kweli picha  itachukuliwa taswira yake  ya mwanamke aliestaarabika itaharibika kabisa na  kwa haraka haraka aliinua  karatasi   na kuficha uso wake. Huku akijitahidi kutafuna na kumeza kwa haraka.

“Unataka kufanya nini , ondoka  ofisini kwangu la sivyo  mshahara wako utakuwa nusu”

“Ah , Boss usifanye hivyo  , hii simu kimeo  hata Kamera  haifanyi kazi, nilikuwa natania tu”

Mara baada ya kusikia jibu hilo kidogo alijituliza  lakini alivyowaza namna ambavyo ameonekana  alivyotuna  mashavu kwa ajili ya chakula  masikio yalishika moto.

Ukweli hakujua  nini kinaendelea lakini alijishangaa tu kupotezea msimamo wake mbele ya  Hamza.

Alijiweka sawa  na kisha akajifuta midomo na tishu  na  akaurudia ukauzu wake kama vile hakuna kilichotokea na kisha akaguna kidogo.

“Ukirudia tena  ninakuhakikisha mshahara wako utapata nusu”Aliongea   huku akionyesha hadhi yake ya ubosi.

“Sawa bosi , nitaenda kuendelea na kazi”Aliongea Hamza akiwa katika muonekano wa kizembe  huku akitingisha kichwa na kuondoka.

Regina mara baada ya Hamza kuondoka alijikuta akijibwaga kwenye kiti chake kama mtu ambae ametua mzigo mzito  kichwani.

Mara baada ya kuanza kufikiria kilichomtokea  sekunde kadhaa zilizopita alijikuta akicheka mwenyewe  na kujiambia hili  ni tukio lake la ajabu kumtokea akiwa kazini.

Kwa namna alivyocheka alipendeza mno , kana kwamba ni mmea uliochanua   wakati wa ukame  mwingi, lakini  kwa bahati mbaya  tukio hilo hakuna ambae aliweza kuona.

Hamza  hakuwa na chakufanya, kazi alikuwa amemaliza na alijikuta akiingiza gemu katika tarakishi na kuanza kucheza kupoteza muda  lakini  alikuja kusitishwa mara baada ya simu yake kuita , alipoangalia namba ilikuwa ngeni kwa maana hakuwa ameisevu.

Bila kujiuliza mara mbilimbili aliamua kuipokea  ili kusikiliza ni nani  anampigia ,  sauti  iliosikika ilikuwa ya mwanamke.

“Hello , Mr Delivery”

Ilikuwa ni sauti tamu kweli , pengine aliekuwa akiongea hivyo alikuwa ameilegeza.

“Naongea na nani?”Hamza alikuwa akihisi aliekuwa akiongea nae lakini alitaka kuthibitisha.

“Mteja wa vvungu , Hamza nahitaji   mzigo unifikie leo  hii , nadhani  Alex alikuambia”Hamza mara baada ya kuthibitisha mwili wake ulimsisimka.

Ukweli ni kwamba ni kama ana katabia ka  kusahau baadhi ya vitu , ijapokuwa alikuwa na shauku ya kutaka kujua vyungu vile vilikuwa na siri gani mpaka kununuliwa kwa kiasi kikubwa cha pesa , lakini  mara baada ya kujiunga na famiia ya  Regina ni kama alisahau kwa muda.

“Nakumbuka ndio , nitakuletea mzigo, ngoja niwasiliane na Alex kabisa, saa ngapi  nifike?”

“Muda ni uleule  Mr Hamza”Aliongea mwanadada Frida upande wa pili na sauti yake ilionekana  kuwa na ucheshi.

“Leo lazima nijue vungu hivi  vina siri gani?”Aliwaza Hamza na kisha paleale alitoa jibu kwamba muda  tajwa lazima awe hapo akiwa na chungu.

Hamza hakuwa akijua kwamba swala la  Frida kumchagua yeye kama mleta vyungu lilimfanya Alex kumchukia kwa kudhania mrembo huyo ana hisia za kimapenzi  na  Hamza.

Muda  husika mara baada ya kuwadia Hamza ilibidi kwanza akamuage Regina ili afahamu kwamba hawezi kwenda nae  nyumbani , alitaka kuunganisha moja kwa moja.

Mara baada ya kumwambia  kwamba kuna sehemu anapitia Regina hakuwa hata na haja ya kuuliza ni wapi , aliishia kuitikia tu.

Kwasababu hio Hamza hakuacha kujisikia vibaya  , kwa namna ambavyo  Regina alimchukulia , ni kama vile alikuwa na nafasi ndogo sana kwenye maisha yake , hakujua ni kwanini lakini  aliona yeye na Regina hawawezi kuwa  wapenzi  na ndani ya miezi mitatu kila mtu atashika lake.

Kwasababu hakuwa na usafiri ilibidi achukue mwendokasi kwa mara nyingine , muda ulikuwa umeenda na  kwa kuminyana sana aliweza  kufika  Mwenge ndani ya  dakika ishirini pekee , kutoka Mlimani city yalipo makao maku ya kampuni mpaka  Mwenge hapakuwa mbali.

Hamza  mara baada ya kufika katika kiwanda hicho  bado hakuacha kushangaa , kitu  kingine siku hiio kulikuwa na mabadiliko kidogo , wale wanawake ambao  walikuwa bize kutengeneza vyungu hawakuwepo  ni kama vile kiwanda kimesitisha utengenezaji kwa muda. 

Hamza hakujali sana , mara baada ya kujitambulisha  hakukuwa na maswali mengi , alipewa mzigo na utaratibu ulikuwa ni uleule  kama wa mwanzo.

Hamza alidhani angemuona  Alex ndani ya hilo eneo , lakini hakuwepo  hivyo pia hakujishughulisha kumpigia simu.

Muonekano wake ulikuwa mzuri zaidi kuliko wiki aliofika hapo kuchukua mzigo , alikuwwa amevaa suti ya bei ghali na viatu vya bei ghali , hivyo  ilifanya watu kumwangalia  kwa namna flani ya kumshangaa , wengi wao  ikiwemo wadada.

Kilichombeba Hamza licha ya kuonekana muda mwingine kama Mzembe ni muonekano wake wa kuchanganya rangi ,  kitendo cha kuingia   katika daladala na muonekano wake ni kama vile hakuwa na hadhi hio , watu walimpa hadhi ya kuwa na  usafiri binafsi.

Mambo yalienda haraka haraka kuliko  siku ile kwani alikuwa  ashajua anuani ya nyumba mzigo ulipokuwa unaelekea.

Baada ya kufika Madale kwenye geti  alibonyeza kitufe  na  aliitikiwa kwa ndani na mlango ukafunguliwa , lakini  siku hio mlinzi alikuwa tofauti , hakuwa yule wa siku ile ambae aliikuwa akimwangalia kwa macho  ya dharau dharau , aliekuwepo alikuwa ni kijana mdogo sana.

“Karibu Bro”Aliongea  yule kijana , alikuwa  humble kuliko ilivyokuwa kawaida, pengine ni kutokana na muonekano wa Hamza.

Hamza mara baada ya kupita getini  alielekezwa aende moja kwa moja ndani , ilikuwa ni tofauti na siku ile alipofika mrembo yule alikuwa kwenye  bwawa la kuongelea.

“Welcome!!”

Sauti tamu ya mrembo Frida ilimkaribisha, siku hio mwanadada huyo alikuwa na muonekano wa tofauti kabisa , alikuwa amevalia  suti  ya rangi nyeupe  na miwani ya macho , alionekana  kuwa katika mavazi ya kikazi zaidi tofauti na ya nyumbani.

Alimkaribisha Hamza kwa tabasamu , ilikuwa ni kama vile  anamjua na  jabo hilo  Hamza aliliona pia , lakini hakufikiria sana.

“Nimeleta mzigo boss  wangu , sijui utaratibu ni uleule  naufungua kwanza?”Aliuliza Hamza.

“Haina  haja , naamini  hakuna makosa”Aliongea  na  Frida hakumpokea Hamza  bali aligeuka  na kurudi ndani na Hamza alielewa  , alipaswa  kuingia ndani ya jumba hilo la kifahari.

Nyumba hio kwa nje ilionekana nzuri  , japo haikuwa kubwa sana kama ile ya   Regina lakini ilikuwa nzuri ya kupendeza ambayo ilitosha kuitwa Mansion.

Hamza mara baada  ya kuingia ndani  aliweza kuona uzuri  halisi  sasa , staili ya  upambaji ilikuwa ni ile ‘go 

all out’or maximalist  yaani juhudi kubwa zilitumika

kuhakikisha mapambo mengi kama hayo yanaendana na muonekano wa sebule na kufanya  ipendeze , ilikuwa tofatui na nyumba ya  Regina ambayo   samani za ndani zilikuwa  chache  huku upambaji ukiwa ni ule mwepesi, Hamza alijiambia iwe  upambaji  ni  vitu vichache au vingi  kilicholeta maana eneo hilo linapendeza na linaendana na tabia ya mtu.

Regina alikuwa kauzu  ndio maana hata mazingira yake yalikuwa mepesi , hakupenda kuzungukwa na mapambo mengi ya thamani ya juu  ,  Frida  alionekana kama mwanamke mcheshi  na anaependa kujiachia  na ndio maana alipenda kuzungukwa na mapambo ya kifahari.

Hamza alizungusha macho kwa haraka  na aliweza kuona tarakishi ikiwa juu ya meza  na  baadhi ya makaratasi yalionekana , ilionekana alikuwa akifanya kazi  na hivyo ilimpa  ishara  ya kwamba hakukuwa na  chumba cha ofisi  kama nyumbani kwa Regina.

“Siku ile nilidhani kwa urembo wako  utakuwa  celebrity , lakini napata hisia kazi yako itakuwa ni ya

kutaaluma zaidi”Aliongea  Hamza  na kumfanya Frida kucheka kidogo, alikuwa mrembo  na alipendeza alivyocheka.

“Nikajua mpole , ila unaonekana ni muongeaji”

“Mimi sio mpole , kuna muda  nakuwa mkimya  tu , ila nachangamka sana mbele ya wanawake warembo” “Haha..weka kwanza mzigo chini”Aliongea na kumfanya Hamza kukumbuka kumbe alikuwa amebeba boksi.

Frida  alimwangalia Hamza kwa umakini  , ni kama kuna kitu alichokuwa akikitafuta.

“Nilijua  pia  wewe ni mtu wa Delivery , ila   unaonekana sio wa kawaida?”Aliongea.

“Unamaanisha nini  mimi kutokuwa wa kawaida?”

“Mavazi yako , ineonekana umetokea  ofisini  na sio ofisi ya kawaida , mtu wa kawaida hawezi kumudu kuvaa  Armani , Jimmy  Choo , Audamars Piguet  na Monte Blanc, sio mavazi ya mtu  wa  hadhi ya delivery haya”Aliongea  Frida huku akiwa amemsogelea Hamza kwa ukaribu  na kuchunguza mavazi yake.

Hamza alikuwa ashasahau  kama amevaa mavazi ya bei ghali , ukweli ni kwamba  asubuhi alivyorushiwa na Regina nguo hizo hakujiuliza uliza ni Brand gani, pengine  labda ile staili ya  Regina alivyomrushia kama vile ni nguo za mtumba, lakini sasa ni kama anaambiwa  alikuwa amevaa suti ya Armani , Viatu Brand yya Jimmy Choo , Saa  Brand ya Audamars Piguet  na mkanda wa Monte Blanc, aliishia  kumlaani  Regina ndani kwa ndani kwa kumvalisha mavazi yasioendana na hadhi yake, alijiambia yaani anapokea mshahara wa milioni moja   lakini  amevalishwa mavazi ya milioni kumi , tena akapanda kabisa daladala.

Kwa mtu wa kawaida pengine  ingeonekana  mavazi  hayo kuwa kitu cha ajabu lakini kwa  mwanamke kama Regina ambae hela ni kitu cha kawaida, ukweli ni kwamba alifanya kuagiza tu  kwa kutoa vipimo na alieleta mavazi  ndio alichagua ya gharama ya juu, lakini hata kama angeenda mwenyewe kununua basi angechagua  mavazi ya bei hio hio , labda brand tofauti tu.

Hata hivyo  aliona  mrembo huyu  alikuwa na uwezo wa kuzifahamu Brand, maana ilikuwa ni kwa kuangalia tu ashajua.

“Usipagawe na haya mavazi  ya kawaida sana , mimi ni wale wa  nimevalishwa na .. ki ufupi ni kwamba  kutokana na muonekano wangu  nafanya matangazo ya nguo  , nikirudi navua nawarudishia  wenye  mali yao, nimebadilika muonekano ila sio hadhi”Aliongea Hamza akiwa na tabasamu lakini kauli ile ilimfurahisha  Frida maana imekaa ki uongo  sana.

“Anyway , niite Dr Frida  Franklin, nadhani  nimejibu swali  lako , mimi sio celebrity mpaka  kuvalishwa nguo kwa ajili ya  kutangaza biashara”Aliongea  kwa tabasamu na kisha  alibeba boksi lile na kuondoka sebuleni.

Hamza aliishia kutoa tabasamu tu  na sasa ndio anajua mrembo huyo ni Dokta , ndio maana alionekana   kitaaluma taaluma.

“Hehe. napenda wanawake wasiotabirika kama hawa..”Aliwaza Hamza  na palepale alikaa kwenye sofa.

Dakika chache tu Frida alirudi akiwa na kibunda  cha hela na kumpatia  Hamza jambo ambalo lilimfanya ashangae.

“Mbona  nyingi tofauti na malipo yaliopita?”Aliuliza kwa shauku.

“Leo nakulipa kulingana na  muonekano wako , hio  ni hela  ya delivery kuhusu malipo ya mzigo nishalipa kwa Alex  moja kwa moja”Aliongea  na kauli ile ilimpagawisha  Hamza , alikuwa akipenda hela , lakini kulipwa kitita  cha pesa  halikuwa jambo la kawaida.

“Hivi vyungu kwanini thamani yake ni kubwa , kuna haja ya kutoa  kiasi chote hiki  cha pesa?”

“Unataka majibu?”Aliongea  Frida akiwa na tabasamu  huku akikaa kwenye sofa.

“Ukinijibu utaiondoa shauku yangu?”

“Kilichokufanya kuwa na hiari ya kuleta delivery licha ya kuwa na muonekano huo  ni dhahiri shauku ndio inakusukuma , kama ilivyokwako , mimi pia kutoa  kiasi kikubwa hivyo  kwa ajili  ya kuleta delivery shauku yangu imenisukuma pia”Aliongea  

“Shauku gani?”

“I see you’re in the initial stage of sorcery,what led you  to the choice of delving into the study of magic?? 

“Naona  upo hatua za mwanzoni za kujifunza uchawi,nini kimekufanya  kuchukua maamuzi ya  kujifunza  ulozi”Aliuliza  kwa kingereza  lakini swali lile lilimfanya Hamza kubadilika ghafla  tu.

Previoua Next