MZIZIMA
Mvua zilizokuwa zimeambatana na upepo mkali zilikuwa zikiendelea kulisumbua jiji la bandari ya Salama, jiji la kale ambalo watu wa zamani walilijua kama mzizima. Mvua hizo ziliwafanya Tanesco wapate kisingizio kizuri kabisa cha kuweza kuukata umeme ambao ulikuwa unaimulika mitaa mbali mbali na kuonyesha umaridadi wake.
Kwenye chumba kimoja maeneo ya Kigogo Mwisho alionekana ndani mwanaume mmoja, kuonekana kwake kulidhihirisha wasiwasi na hofu ambayo ilikuwa imeugubika uso wake na simanzi ikauzidisha upole wa ile sura yake ambayo haikuwa ikionekana vyema huenda kwa sababu ya kukosekana kwa mwanga. Uso wake ulitoa taarifa ya kwamba maisha yake hayakuwa salama ndiyo maana alikuwa hana amani wala kuwa na utulivu wa kutosha, alikuwa ameketi kwenye mkeka ambao ulikuwa umetandikwa chini kwenye chumba kidogo cha hovyo ambacho kiligubikwa na joto kali kwa kukosa nyenzo mhimu za kupambana na joto. Sanjari na hilo udogo wa chumba nao ulichangia kwa kiasi kikubwa.
Mwanaume yule alijizoa kutoka kwenye ule mkeka na kusimama, alijisogeza kwenye dirisha dogo ambalo lilifunikwa kwa tambala kuu kuu lilolokuwa chafu, alifunua kidogo pazia hilo ili kujua kama nje kulikuwa na chochote lakini hakufanikiwa kuona jambo lolote lile zaidi ya radi ambazo zilikuwa inamulika kila wakati kwenye kiza totoro kilicho lifanya jiji hilo kuwa na utulivu ambao sio kawaida yake. Alirudi tena kwenye mkeka wake akiwa anatweta kwa jasho kutokana na joto kali huku akiwa anajifuta jasho hilo kwa kutumia shati lake ambalo lilikuwa mwilini.
Akiwa anaendelea kuhema kwa hesabu maalumu ambazo alizijua yeye na nafsi yake, alihisi kama kuna kitu kinamtekenya kwenye mfuko wake wa suruali, hapo ndipo akakumbuka kwamba kwenye mfuko huo alikuwa amehifadhi kisimu kidogo ambacho alikuwa amekifunga funga kutokana na uchakavu ambao kilikuwa nao. Aliipokea haraka simu hiyo ambayo namba yake haikuwa na jina na kuiweka kwenye sikio lake.
“Ondoka haraka kwenye hilo eneo, una dakika kumi na tano tu za kuyaokoa maisha yako, vinginevyo unakufa” sauti ya upande wa pili iliongea kwa msisitizo kisha simu ikakatwa. Alibaki kwenye mshangao mithili ya mtoto ambaye alikuwa ametelekezwa na mama yake mzazi huku akiamini kwamba alikuwa na usalama wa kutosha kwa sababu mama yake alikuwa karibu.
Alijizoa kivivu huku moyo wake ukiwa unamuenda mbio, alisogea kwenye ule mkeka na kuukunja upande wa juu ambapo eneo hilo kulikuwa na udongo ambao ulijazwa, aliufukua haraka haraka na kukitoa kimfuko cha plastiki. Alikifungua na ndani yake kulikuwa na pesa za kigeni maarufu kama dola huku pembeni yake kukiwa na bastola moja pamoja na kisu kimoja. Alizoa pesa haraka haraka na kuzitupia kwenye mfuko wake, bastola akaipachika kwenye kiuno chake huku kisu akikishika mkononi.
Alipafukia kama alivyokuwa amepakuta mwanzo na kuurudishia ule mkeka kwa mara nyingine tena kisha akanyanyuka na kuanza kutoka nje. Baada ya kufika mlangoni alikuwa amepoteza dakika tatu tayari, aliufungua mlango taratibu kisha akaangaza kila upande ili kuona kama angefanikiwa kuona kile ambacho alikuwa ameambiwa kinaenda kutokea lakini hali ilikuwa shwari kabisa hivyo akajitosa kwenye maji ya mvua na kuanza kutembea haraka haraka ili kuelekea kilipokuwepo kituo cha magari.
Alikunja kona ya kwanza akiwa anapishana na sauti ya kudondoka kwa maji, akakutana na uwazi ambao ulikuwa na mita kama kumi na tano, sehemu ambayo ilimshtua kidogo kwa sababu moyo wake ulimuenda mbio isivyokuwa kawaida. Alitembea haraka haraka ili aweze kulivuka eneo hilo salama huku kwenye mkono wake kisu akiwa amekishikilia vyema, ila hakupiga hatua hata kumi akahisi kabisa kulikuwa na harufu ya mtu ndani ya eneo hilo hali ambayo ilimfanya kupunguza mwendo na kumfanya aanze kutembea taratibu.
Aligeuka kuangalia nyuma yake, hakuona kitu zaidi ya anga ambalo lilikuwa linamcheka hivyo akahitaji kuendelea na safari yake tena lakini nafsi iligoma kabisa, moyo wake ulikuwa mzito na hakuwa mtu wa kuupuuzia huo mlango wake wa sita ambao ulikuwa wa hisia. Alishuka chini kama anajilaza kifudi fudi lakini hakufika chini kwa sababu ule mkono wenye kisu ndio ambao ulitangulizwa kisu ndicho kikafika chini na hata baada ya kufika pale chini kwa mkono wake hakuzubaa, alijigeuza kwa sarakasi kwa kuuviringisha mwili wake hali ambayo ilimfanya atue pembeni.
Mahesabu yake yalikuwa sahihi kwa sababu wakati anashuka pale chini, juu yake kilipitishwa kisu kutoka kwenye mikono ambayo ilionekana kuwa na nguvu kubwa na lengo la mtu huyo halikuonekana kuwa kumzimisha tu bali alikuwa anahitaji kuondoka na nafsi yake moja kwa moja. Hata baada ya kutua pale chini hakuzubaa kwa sababu alijua huenda akampa adui nafasi nzuri ya kuweza kufanikisha jambo lake kitu ambacho hakutaka kiweze kutokea kwake yeye ndiyo maana alijiviringisha kwa sarakasi na kutua pembeni. Kujiviringisha kwake kulimfanya kulikwepa buti zito la ngozi ambalo lilikuwa limeshushwa na mwanaume ambaye alionyesha kuwa na uhasama naye mkubwa mithili ya mtu ambaye alimuibia mkewe, buti hilo kama lingefanikiwa kutua kwenye mgongo wake basi asingefanikiwa kutembea tena kwenye maisha yake yote.
Kiza kinene kilimfanya mwanaume huyo ashindwe kumtambua mwanaume ambaye alikuwa amekuja mbele yake ila mwanga wa radi ulimumulika mtu huyo ambaye bila shaka alikuwa ni mweusi usoni akiwa kwenye ghadhabu isiyo pimika. Aliukunjua mkono wake ambao ulikuwa na kisu kwa sababu alijua kwamba anatakiwa kufa wakati huo asipo yatetea maisha yake, hakupata muda wa kutosha wa kupiga tathmini juu ya uwezekano kama alikuwa anamfahamu mwanaume huyo kwa sababu alikuwa anamjia kwa kasi pale alipokuwepo huku mabuti yake yakiwa yanapiga piga kwa nguvu kwenye maji ambayo yalikuwa yametuama chini.
Miguu yenye nguvu miwili ilikuwa inakuja kwenye uso wake, kama bahati tu, tope lililokuwa chini lilimsaidia kuteleza kidogo na kurudi nyuma hali ambayo iliifanya miguu hiyo kumkosa na badala yake akarushiwa maji machafu usoni ambayo yalimuingia kwenye macho. Mtetemo wa ardhi aliusikia vyema baada ya ile miguu ambayo ilimkosa kutua chini na kukita kwa nguvu. Aliyafumbua macho yake haraka ili kujilinda, alichelewa kwenye mahesabu, ngumi ilizama kifuani na kumfanya ahisi kama kuna mtu alimpasua na shoka.
Ngumi hiyo ilimburuza mpaka karibu na ukuta mmoja wa nyumba ambapo hakuruhusu kuufikia bali mguu wake ndio ulitumika kama ngao baada ya kuurusha na kukita kwenye ukuta wa nyumba hiyo ambao ulitingishika kwa nguvu na kutulia. Alitaka kujipanga vyema alihisi kuna kitu kinawaka kinakuja pale alipo, alifanikiwa kukikwepa kisu ambacho kilikuwa na makali ya kutosha, kilimbaraza kidogo kwenye bega lake na kumpatia maumivu lakini hakulizingatia hilo kwanza badala yake alikuwa anaangalia namna ya kumkabili mwanaume huyo ambaye bado alikuwa anakuja mithili ya mtu ambaye anachajiwa huku kisu chake kikizama kwenye ukuta wa nyumba hiyo ya tofali.
Alifanikiwa kuziona ngumi mbili zilizokuwa zimeulenga uso wake, alijisogeza pembeni na kumpa mtu huyo nafasi ya kumpatia goti la ubavu kisha akiwa anasikilizia maumivu mwanaume yule alikichomoa kile kisu na kukizamisha kwenye mbavu za mwanaume huyo hali iliyomfanya kutoa sauti kali ya mguno wa maumivu. Sasa alikuwa anajiona anakufa kizembe bila hata kumjua mtu ambaye alikuwa anamvamia hapo alikuwa nani.
Alisogea hatua mbili nyuma macho yake yakiwa makini kwenye kile kiza huku ubavu wake ukiendelea kuitoa damu taratibu ambayo ilikuwa inatoka kwa fujo mpaka wakati huo, yule mwamba ambaye alikuwa anaelekea kupata ushindi, baada ya kukichomoa kisu chake alikuwa anasogea kwa hatua chache ambazo zilimpa uhakika wa ushindi. Kusogea kwake mvamiaji naye alihisi kama kuna kitu hakipo sawa, mbele yake mtu aliyekuwa anamuwinda ni kama ghafla tu hakumuona na radi ilipo piga aliona mtu huyo akitokea pembeni yake ambapo alifanikiwa kuipangua ngumi yake moja lakini mkono ambao ulikuwa na kisu ulizama kwenye kifua chake.
Ndiyo kwanza tunaufungua ukurasa wa kwanza kabisa wa simulizi hii ya kusisimua. Ungana nami mpaka mwisho tuweze kuugusa wino huu bora mno.
Comments