Reader Settings

Alijaribu kuutoa mkono huo kwa nguvu lakini hakufanikiwa baada ya kushindiliwa na ngumi nyingine ya kwenye chembe iliyo mpa maumivu makali. Aliachiwa akiwa amejishika kifuani sehemu ambayo ilitobolewa huku akiwa amepinda maana ile ngumi ya chembe ilimuingia vizuri. Alijikaza na kukizungusha kisu chake kwa nguvu kumsogelea mtu wake pale alipokuwepo, alirusha mkono ambao ulikuwa na kisu ukapita karibu na shingo ya mwanaume ambaye alikuwa amevamiwa hivyo akapiga hewa. Wakati anajipanga kuurudisha tena alijikuta hata kisu kinamponyoka kwenye mkono wake baada ya kupigwa ngumi nzito za haraka haraka kifuani kwake ambazo zilikifanya kifua kilainike, uzito wa zile ngumi kifua kisingeweza kuuhimili.

Aliachiwa akiwa anayumba yumba, mguu mzito ulitua kwenye shingo yake na kumshusha chini kwa nguvu, alipotua chini alipigwa teke la uso ambalo lilimfanya agale gale akiwa anaburuzwa na nguvu ya ule msukumo wa lile teke. Mwanaume ambaye alikuwa kwenye mavazi makuukuu alimsogelea akiwa na kisu chake mkononi na kufika mpaka pale chini ambapo alikuwepo mwanaume yule aliye mvamia. Alijaribu kunyanyuka kwa nguvu ila alirudi chini baada ya kushindiliwa kisu cha kwenye bega karibu kabisa na ilipokuwa shingo.

“Mimi na wewe tunafahamiana kabla ya hapa?” ilikuwa sauti nzito ambayo ilitoka kwa yule mwanaume ambaye alikuwa amevamiwa akiwa anamuuliza mgeni wake.

“Lazima uf….” Yule mwanaume hata hakukamilisha sentensi yake kuna risasi ilimkosa na kutua kwenye ukuta, alishtuka baada ya kugundua kwamba kumbe mvamiaji hakuwa mmoja ndani ya hilo eneo hivyo alikizamisha kisu chake kwa nguvu kwenye shingo ya mwanaume yule kisha akakitoa na kujigeuza kwa sarakasi ambayo ilimfanya atue kando na baada ya pale aliichomoa bastola yake haraka na kuruhusu pia risasi ziende ule upande ambao alihisi unamshambulia lakini mtu huyo hakuonekana kuwa wa kawaida na yeye alikuwa amejeruhiwa hivyo akawa anatafuta namna ya kuweza kutoweka ndani ya lile eneo.

Alidunda kwenye ukuta ambao ulikuwa karibu na alipo simama, alijivuta na kudondokea upande wa pili na kuishia kwenye vichochoro ambavyo vilimezwa na kiza totoro. Mwanaume mmoja mwenye miraba minne ndiye alikuwa amefika pale akiwa ameghadhabika mno, alitafuta kila kona ya ule ukuta lakini hakuona mtu, licha ya kumsindikiza mwanaume huyo kwa risasi za kutosha lakini bado hakumpata. Alirudi pale alipokuwa mwenzake na kumsikitikia tu kwani alikuwa kwenye dakika za mwisho kuweza kushindana na kifo, alichanwa vibaya kwenye shingo yake kiasi kwamba alikuwa anahangaika huku na huko kwa maumivu hivyo mwenzake akaamua kumfanyia msaada kwa kumpiga risasi ya kichwa ili apumzike.

EDISON

Ndilo lilikuwa jina la mwanaume ambaye alikuwa amefanikiwa kuwakimbia wanaume waliokuwa wamemvamia eneo lile la kigogo mwisho. Licha ya kuwa na maumivu makali kwenye ubavu wake huku damu zikiendelea kumtoka kwa wingi kwenye mwili wake, haikuwa sababu ya kumfanya aweze kusimama ndani ya eneo hilo kwani hakujua wavamiaji walikuwa wangapi na kwa hisia zake ni kwamba hawakuwa tayari kuweza kumuacha hai.

Mwanaume huyo alikuwa anaendelea kulaani hali ile ambayo ilimkuta huku mvua ikiendelea kumzomea kwa kumnyeshea kiasi kwamba alilowa chapa chapa. Baada ya kufanikiwa kutoka ndani ya eneo lile, alikimbia kwa spidi kali akiwa anavikata vichochoro kadhaa mpaka pale alipokujuja kutokezea eneo la Mti Pesa. Mazingira yalikuwa kimya na tulivu huku akiwa anaona boda boda chache ambazo zilikuwa zinatokea ilipo bar ya King’ole.

Haikuwa dhamira yake kusimama ndani ya lile eneo hivyo akaendelea kushuka njia ambayo ilikuwa inaelekea Mabibo mwisho huku akiwa makini na mwendo wake. Macho yake yalikuwa makali kiasi kwamba hakuonekana kuwa mtu wa kawaida, aliingiza mkono kwenye mfuko wake mmoja wa nyuma na kutoa kimfuko kidogo ambacho alikuwa amekikunja, alikifungua na ndani yake kulikuwa na vidonge kadhaa na kichupa kidogo ambacho ndani yake kilikuwa na kimiminika.

Alikifungua kile kichupa na kukimwagia kile kimiminika sehemu iliyo tobolewa huku akitoa sauti ya miguno ya maumivu makali mpaka akaukunja uso wake lakini haikuwa sababu ya yeye kusimama. Alikitupa kichupa hicho kwenye mtaro wa kupitishia maji machafu huku akifungua pakiti ya vidonge na kumeza kimoja kisha vingine akavirudisha kwenye kimfuko chake kile, sekunde chache zilizo fuatia licha ya mvua kuendelea kumwagikia mwilini mwake lakini kile kidonda kilianza kukauka na damu ikaacha kutoka.

Hakuyasikia tena maumivu mwanaume na wakati huo alikuwa amefika ilipo shule ya Loyola, hakunyoosha na barabara ya msikitini badala yake alichepuka mkono wake wa kushoto kuiacha bara bara ya rami na kuifuata barabara ya vumbi iendayo TOT huku akiwa anaongeza mwendo taratibu. Baada ya kufika mbele alikutana na njiapanda hata hivyo hakujiuliza mara mbili akanyoosha na barabara ambayo ilikuwa imekunja kulia. Alianza kukimbia taratibu na kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda ndivyo alivyokuwa anaongeza spidi mpaka alipofika karibu na kanisa la KKKT ambalo lipo karibu kabisa na hosteli za Mabibo ambazo wanazitumia wanafunzi wa chuo cha NIT.

Edison alikuwa anatembea kuelekea ulipokuwa mlango wa kanisa hilo lakini alipunguza mwendo baada ya kuhisi hali ambayo haikuwa sawa ndani ya eneo hilo. Kilicho mshtua ni baada ya kuona mlango upo wazi halafu usiku wa maneno kama huo huku ndani yake ikionekana mishumaa imetaradadi na kufanya eneo hilo kuwa na mwanga japo maeneo mengine yalikuwa na kiza cha kutosha. Alichomoa bastola yake na kunyata kupitia nyumba ambazo zilikuwa jirani kabisa na eneo hilo mpaka alipo ukaribia mlango wa kanisa hilo kubwa.

Alichungulia ndani kwa umakini, hakuona mtu yeyote yule lakini alipo angalia chini kwa umakini aligundua kwamba kuanzia pale mlangoni alipokuwepo kulikuwa na maiti za wanaume ambao walikuwa kwenye suti zao. Watu hao walikuwa wamekufa kwa kupigwa risasi, aligundua kwamba hakukuwa na hatari kwa wakati huo kwa mazingira yalivyokuwa kwani watu ambao walionekana kufika hapo walikuwa wameikamilisha kazi yao hivyo hawakuwa na kingine cha kuweza kukisubiria.

Aliipakia bastola yake ndani ya kiuno chake na kuingia humo ndani kushuhudia walinzi walivyokuwa wamekufa. Alisikitika mno huku uso wake ukiwa na wasiwasi akiwa anaangaza huku na huko, bila shaka kuna mtu alikuwa anamtafuta ndani ya eneo hilo. Aliitoa ile simu yake ndogo kwenye mfuko wake na kuipigia ile namba ambayo kwa mara ya mwisho ndiyo ilimtahadharisha kwamba alikuwa na dakika kumi na tano tu za kuweza kuyaokoa maisha yake vinginevyo alikuwa anaingia kwenye hatari kubwa.

Simu ile ilianza kuita kwa fujo madhabahuni eneo ambalo lilikuwa limezuiwa na meza moja ya mninga ambayo ilikuwa ya gharama kubwa, alikimbilia eneo hilo na ndipo aliona kuna mtu ananyoosha mkono wake kana kwamba alikuwa anampa ishara alipo ila kwa taabu mno. Eneo hilo alikuwa ameketi mchungaji wa kanisa hilo, mwanaume ambaye alikuwa na umri wa kiutu uzima ndiye ambaye mwili wake ulikuwa umechakaa pale chini huku simu ya kisasa ikiwa pembeni yake inaita kwa fujo.

Edson alimkimbilia mwanaume yule mtu mzima na kumnyanyua akamuweka kwenye mapaja yake akiwa mwingi wa simanzi na usoni ameduwaa kama mtu ambaye alibananishwa na benki kwa kushindwa kulipa madeni kwa wakati.

“Nini kimetokea?” aliuliza kwa upole akiwa anahangaika kupekua namba kwenye simu yake, bila shaka alikuwa anatafuta ni msaada wa kuweza kumfikisha mwanaume yule sehemu ambayo ingekuwa salama kwa kujaribu kuokoa maisha yake lakini mwanaume yule alimzuia akiwa anatoa damu kwenye mdomo wake.

“Naomba unisamehe sana kwa sababu nimeshindwa kukulinda, nimeshindwa kutekeleza wajibu wangu” alitamka kwa shida mwanaume yule akiwa anaendelea kutoa damu nyingi kwenye mdomo wake.

“Nani amefanya haya?”

“Nenda nyumbani kwangu, kuna kitabu kidogo kipo chini ya banda la mbwa ukifungua chini kuna maelezo yote ya mhimu, hakikisha unakipata kabla mtu yeyote hajakitia kwenye mkono wake na uondoke haraka hili eneo kwa sababu polisi wanaweza kufika muda wowote ule na hutakiwi kuua polisi kwa sasa” aliongea kwa msisitizo huku mikono yake ikilegea na kushuka chini roho ikawa inaacha mwili. Edison aligubikwa na simanzi huku akiuachia mwili huo na kuibeba simu ya mchungaji huyo, alitoka na kupotea jumla ndani ya eneo hilo ambalo halikueleweka lilikuwa na nini hasa mpaka kanisa kulindwa namna hiyo.

UKURASA WA PILI UNAFIKA MWISHO

 

 

 

 

 

 

 

Previoua Next