Edisoni baada ya kutoka ndani ya lile eneo alipishana na polisi ambao walikuwa wanaingia lakini wasingeweza kumuona kwa sabaabu alikuwa ametoweka tayari. Alitembea haraka haraka kuelekea Mabibo Mwisho ambapo baada ya kufika hapo alichukua boda boda, licha ya boda boda huyo na wenzake ambao walikuwa hapo kumshangaa kwa namna alivyokuwa amechakaa lakini hakujali kwani alitanguliza pesa mbele hivyo boda akawa hana namna zaidi ya kumbeba na kumpeleka kule ambako alikuwa anahitaji kufikishwa haraka.
Safari haikuwa ndefu kwa sababu ilienda kuishia Lego, karibu na lilipo jengo kubwa la Ubungo Plaza. Edison alishuka hapo na kujiweka sawa kisha akarudi nyuma hatua kadhaa na kuingia kwenye njia nyembamba ambayo ilimfanya atokezee nyuma kabisa ya jengo hilo, alitembea kwa muda kidogo na kutokezea kwenye nyumba moja ambayo ilikuwa nzuri ila haikuwa kubwa. Rangi yake nyeupe iliifanya nyumba hiyo kuonyesha umaridadi wake kwa mumeta meta, taa safi ambazo zilifungwa ziliifanya kuendelea kuwa bora kwenye macho ya mtazamaji.
Alitembea taratibu kwa sababu hakuwa na imani na sehemu yoyote ile ambayo alikuwepo wakati huo hali ambayo ilimfanya kuwa makini zaidi. Alisogelea mpaka lilipokuwepo geti kubwa jeusi ambalo lilinakshiwa kwa chuma kizito, geti hilo lilikuwa linaelea kwa maana hiyo ni kwamba lilikuwa limefunguliwa na aliyekuwa amelifungua hakukumbuka kulifunga vizuri ili liweze kushika kwa usahihi, hapo akajua kwamba kulikuwa na ugeni ndani ya eneo hilo ukiacha yeye.
Aliichomoa bastola yake na kuanza kunyata kuelekea ndani baada ya kulifungua geti hilo taratibu, baada ya kuzama ndani kabisa ndipo aliona kuna watu watatu nje wakiwa kama wanabishana. Wote walikuwa wamevaa mavazi ya kiraia ya kawaida tu ila walikuwa na silaha zao mikononi. Alishagazwa na ukimya mkubwa ambao ulikuwepo hilo eneo kwa sababu lilikuwa na mbwa hivyo taa ya hatari ikawa imewaka kwenye ubongo wake kwamba huenda hata mbwa walikuwa wameuliwa.
Hakuwa na muda wa kuanza kujishauri kwa muda mrefu hivyo akakwea taratibu mpaka lilipokuwepo gari ndani ya uzio huo ili ajipange vyema. Upande wa kulia wa eneo hilo kulikuwa na tenki kubwa la lita 10000 kwa ajili ya kuhifadhia maji. Alifunga kiwambo cha kuzuia sauti kwenye bastola yake na kuachia risasi mbili ambazo zilienda kutoboa sehemu moja kwenye lile tenki na kufanya kuwa na tobo kubwa ambalo lilianza kutoa maji kwa fujo na kuwashtua wanaume wale watatu ambao walikuwa wanabishana ndani ya lile eneo kwani wote waligeuka kushangaa sauti ya maji iliyokuwa inamwagika kwa nguvu huku mvua ikiwa ni manyunyu tu.
Hali hiyo ilimfanya mmoja wao aelekee lile eneo huku wawili wakiingia ndani na silaha zao, yule mwanaume alifika lile eneo na kushangaa tobo la risasi ambalo aliamini kwamba kati yao hakuna hata mmoja ambaye alikuwa ameirusha hivyo akashtuka kwamba huenda lile eneo lilikuwa lina mtu mwingine. Aligeuka haraka nyuma yake lakini muda haukuwa sahihi kwake, modomo wake ulikutana na kisu cha mtu ambaye alionekana kuwa na hasira iliyo kithiri kwenye macho yake huku kwenye mkono mwingine akiwa ameishika bastola ambayo bila shaka hakutaka kujisumbua kabisa kupunguza risasi kwa kuitumia wakati alikuwa na uwezo wa kutumia njia nyingine.
Mwanaume huyo alikufa akiwa anahangaika kuweza kuongea neno lolote ila mwisho wa siku hakuna neno hata moja ambalo alifanikiwa kulitoa kwenye kinywa chake. Edisoni alitembea taratibu kuelekea ulipokuwa mlango wa kuelekea ndani, alichungulia sebuleni hakuona mtu hivyo akaachana na wazo la kuingia kwanza na kuelekea mwishoni mwa ukuta wa nyumba hiyo ambapo alifanikiwa kuchungulia lilipokuwa banda kubwa la mbwa, mbwa wote wawili ambao walikuwa ndani walikuwa wamekufa kwa kupigwa risasi maana miili yao ilikuwa inavuja damu kwa msaada mkubwa wa mwanga wa taa ambao ulikuwa eneo lile aliliona hilo.
Licha ya maelekezo kumtaka aweze kuingia ndani ya lile banda kuchukua kitabu lakini hakufanya hivyo kwa sababu alikuwa na kazi ya kufanya bado. Alirudi kwenye ule mlango wa kuingilia ndani akiwa na haraka kidogo tofauti na mwanzo, alichungulia ndani na kumuona mwanaume mmoja akifakamia matunda ambayo bila shaka aliyakuta kwenye friji, aligeuka na kupiga risasi zote ambazo zilikuwa kwenye bastola kwenye lile tenki la maji hali ambayo ilifanya kasi ya maji kuongezeka kumwagika na kufanya kelele kuwa nyingi.
Alimuona mwanaume yule akishtuka na kutoka nje, Ed alijibanza kwenye mlango mkono wae ukiwa na kisu, mwanaume yule alitokezea nje lakini akarudisha kichwa haraka ndani baada ya kuona mwenzake alikuwa amelala pale chini karibu na lile tenki la maji. Kurudisha kwake kichwa ndani ilikuwa pona pona yake kwa sababu alipishana na kisu ambacho kilikuwa kimelenga kutoboa shingo yake na huenda kingetokezea upande wa pili lakini hata hivyo hakwenda mbali kwa sababu ilikuwa ni ghafla na mhusika alikuwa amejitokeza mbele yake ambapo alimdaka kwa nguvu na kumvutia nje kisha akaupiga mlango teke ili wamalizane wenyewe wawili.
Mwanaume yule hakuwa mlaini, alijivuta nyuma huku akirusha teke ambalo lilikita kwenye ukuta baada ya kumkosa Ed ambaye aliinama chini, mwanaume yule wakati anarusha teke lingine Ed naye alikuwa ameurusha mkono ambao ulikuwa na kisu kwa nguvu hivyo teke hilo likakutana na kisu kikali ambacho kilitoboa kwa nguvu eneo la goti na kumfanya mwanaume huyo ahitaji kupiga kelele ila kelele zake alihitaji kuzipiga huku akiwa anainama. Kuinama kwake kwa maumivu ambayo aliyapata kulipelekea kuzamishiwa kisu kwenye koromeo kisha akakutanishwa na kisigizo cha uso ambacho kilimchomoa kwenye kisu hicho na wakati anatua chini, alikuwa maiti tayari.
Wakati Ed anammalizia mtu yule, alisikia hatua za mtu kutoka ndani ambazo zilikuwa zinaita jina ambalo bila shaka alijua ni la yule ambaye alikuwa amemuua wakati ule. Ukimya ndio ambao ulimfanya mwanaume wa ndani kutoka kwa tahadhari kubwa akiamini nje hakukuwa salama. Alitoka mzima mzima akiwa na bastola kwenye mkono wake ila aliganda baada ya kushuhudia mwili wa mwenzake ukiwa unavuja damu pale chini, damu ilikuwa bado mbichi na ya moto baada ya kuigusa. Alinyanyuka akiwa na ghadhabu moyoni, aligeuka kila upande lakini hakuona mtu ila akagundua kwamba chini kwenye mwanga wa taa kulikuwa na kivuli cha mtu hali ambayo ilimpa ishara kwamba juu ya paa la nyumba kulikuwa na mtu mwingine ambaye hakuwa mwenzake.
Aligeuka haraka na kurusha risasi ambazo zilipishana na mwanaume huyo ambaye alikuwa juu ya hilo paa la nyumba akiwa anashuka hivyo zikamkosa. Ed wakati anatua chini hakusimama kwa sababu mwenzake alikuwa na bastola kwenye mkono wake. Mwanaume yule wakati anakaa sawa alishuhudia kisu kikiwa kinakuja kwa kasi upande wake, alirudi nyuma kidogo kukikwepa huku akijiandaa kufyatua risasi lakini hakubahatika kuipata hiyo nafasi kwa sababu Ed alikuwa mbele yake na teke lake moja ambalo alilizungusha kwa nguvu lilitua kwenye ule mkono wenye bastola na hatimaye bastola akawa imemtoka mkononi yule mwanaume ambaye alitabasamu.
“Umewezaje kupona bwana mdogo?” swali lake ambalo lilimshangaza yeye mwenyewe baada ya kugundua mtu ambaye alikuwa hapo ndiye ambaye usiku huo walitumwa watu kumuua na huenda alitakiwa kuwa amekufa mpaka wakati huo lakini hakuweza kujibiwa badala yake alipewa mtihani wa ngumi nzito ambazo zilikuwa zinakuja kwake. Aliinama chini akiwa anazunguka na kunyanyuka kwa miguu yake ambayo ilitua kwenye kifua cha Ed kwa nguvu hata hivyo Eddy hakuwa mnyonge kabisa kwani naye aliachia ngumi moja ambayo ilitua kwenye mguu hivyo kila mtu akarudi nyuma akiwa anasikilizia maumivu ambayo mwenzake alimpatia.
Wote walinyanyuka kwa kasi kubwa kudhihirisha ubora wao huku yule mwanaume hesabu zake zikiwa ni kuiwahi ile bastola ila MUNGU alikuwa upande wake kwa sababu zile hesabu zake za kuweza kuiwahi ile bastola pale zingemponza vibaya baada ya kisu kutua pale na kumkosa vidole vyake. Aliyainua macho yake na kugundua kwamba alikuwa amefikiwa, alipigwa na mguu wa usoni ambao ulimpeleka ukutani, akiwa ukutani alishindiliwa na goti la tumbo ambalo lilimfanya apige kelele huku akiwa anarusha ngumi kivivu iliyokutana na ngumi ya Ed kiasi kwamba mifupa ilivunjika ikiitikia kwa nguvu.
UKURASA WA TATU unafika mwisho.
Comments