Reader Settings

“Nani amewatuma kufanya haya ambayo mnayafanya leo?” Ed aliuliza swali lakini mwanaume yule aliishia kumcheka tu huku akiwa anatoa damu mdomoni mwake.

“Lazima ufe, lazima ufe hahahahah hahaha” hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya mwanaume yule ambaye alimpandisha Ed hasira na kumfanya ampige na vidole viwili kwenye jicho lake ambalo lilitoboka hapo hapo na kuzalisha kelele kwa bwana yule. Ed alienda kukiokota kile kisu chake na bastola ya mwanaume yule ambaye alikuwa ana uhakika kwamba ilikuwa ni lazima amwambie ukweli wa kilichokuwa kinaendelea ila kwa bahati mbaya wakati anageuka na silaha hizo yule mwanaume alikuwa anatokwa na povu mdomoni, alikuwa ameng’ata ulimi wake ambao ulikuwa unatumika kuhifadhia vidonge vyenye sumu ili kuweza kujipunguza mwenyewe kuliko kusema kile ambacho alikuwa ameulizwa.

Ed alisikitika huku akijongea taratibu kuelekea ndani ambapo baada ya muda aligundua kwamba eneo hilo halikuwa na mtu mwingine bali walikuwa ni hao watatu tu. Alitoka nje mpaka lile eneo ambalo lilikuwa na banda la mbwa, alilifungua eneo lile na kuwatoa wale mbwa nje kisha akaanza kutafuta sehemu ambayo ingekuwa na uwazi, baada ya kuzungusha zungusha kisu chake kuna sehemu aligundua kwamba kisu kilizama hivyo akakilazimisha kwa nguvu na eneo hilo likaonyesha uwazi wa ndani. Alizungusha kwenye lile tobo mpaka alipo utenganisha mlango wa chuma ambao juu ulikuwa na zege lake akaufunua kwa nguvu. Ndani yake kulikuwa na kashimo kadogo ambako kalimfanya ainame na kuchukua box la chuma ambalo lilikuwa ndani yake funguo ikiwa juu yake.

Alilifungua na kukutana na kakitabu kadogo ambako kalikuwa kameandikwa kwa mkono wa mtu na sio mashine. Alikabeba na kutoka kwenye banda hilo kisha akarudi ndani ambako alikwenda kuoga na kuingia kwenye chumba kimoja ambacho alikitumia kubadilishia nguo na kuvaa nguo safi. Baada ya hapo alisogea kwenye shelf moja iliyokuwa ukutani, aliifungua kwa namba maalumu na kutoa mabunda mengi ya pesa kuyapakia kwenye begi kisha akachukua funguo na kutoka nje ambako alichukua lile gari la kifahari ambalo alilikuta pale nje na kuweza kutokomea kusiko julikana usiku huo wa manane.

JNIA

“Una muda gani tangu uanze kufanya hii kazi?”

“Ni miaka mitano sasa”

“Unajiskiaje kufanya kazi kama hii?”

“Mhhh kwangu hii kazi ni zaidi ya nafasi ya dhahabu, haya maisha ni marahisi kama mmekaa vijiweni na washkaji zako mnayachambua kwa kuangalia watu walio fanikiwa lakini haya maisha ni magumu kwenye uhalisia wake kuliko unavyo yafikiria, ndiyo maana wanao teseka ni wengi kuliko walio fanikiwa”

“Upo sahihi kwa hilo lakini unahisi ni sahihi kwa hii kazi ambayo tunaifanya? Kazi ambayo inayapunguza maisha ya watu, kazi ambayo inaacha vilio kwa familia zingine? Naona kama hatuko sawa”

“Nisikilize ndugu, haya maisha hayakupi nafasi mbili, una nafasi moja tu kwenye maisha yako na hiyo nafasi kama ukicheza nayo vibaya basi habari yako inaishia hapo hivyo ni wewe unavyoweza kuzichanga karata zako. Mimi nimeishi kila aina ya maisha, nimeishi maisha magumu, nimeishi maisha ya kukosa kila kitu kiasi kwamba kinacho tokea mbele yako haijalishi kimetoka kwa nani au kwa masharti gani huna namna zaidi ya kukipokea tu. Mimi nimeishi nikiwa mtu mwenye huruma kwenye maisha yangu kwa sababu nimekuzwa na kanisa lakini baadae nikaja kugundua kwamba hii dunia sio rafiki kabisa kwa watu wema. Walimwengu hawakumbuki juu ya mema yako ambayo uliwahi kuyafanya bali wanakumbuka kwamba ni nani mwenye pesa nyingi na jina kubwa na hapo ndipo nilipokuja kuchukia kuwa mtu mwema na huruma nyingi kwa sababu zilikuwa zimeyaponza maisha yangu;”

“Huruma yangu ilinifanya nikae jela miaka miwili kwa kosa la mtu mwingine na ajabu baadae akaja kunikataa, hakuna jambo ambalo nimelifanya kwa huruma na likaja kunilipa baadae mpaka nafikisha umri huu. Mimi sikuwahi kutaka kabisa kuendelea kwenye maisha yale ya umaskini, umaskini ni rahisi kuutaja lakini ni kitu kibaya kwenye haya maisha kwa sababu utakuwa mtu wa kujifariji na kauli za wahamasishaji wa mitandaoni tu ila kiuhalisia dunia inakuwa haitambui uwepo wako. Nilitaka niwe na kila kitu kwenye maisha yangu bila kujalisha natumia njia gani kuvipata hivyo vitu na leo ninapo ongea na wewe naweza kwenda popote pale na naweza kumnunua mwanamke yeyote ninaye mtaka mimi lakini naishi sehemu ambayo wanadaiwa kuishi watu wenye ukwasi zaidi ndani ya taifa hili, mpaka hapo unaniuliza kama naipenda hii kazi?” mwanaume mmoja ambaye alikuwa amezama kwenye maelezo na mwenzake ambaye alionekana kujutia kazi ambayo ilikuwa imewaweka hapo alimpa mwenzake maelezo kwa kina huku akiwa anavuta sigara ndani ya gari ambayo walikuwepo na kuutolea moshi dirishani kwa mbwembwe uso ukiwa siriasi.

“Na huyo mtu ambaye ulifungwa kwa ajili yake baada ya hapo kiliendelea nini juu yenu?”

“Nisikilize Paschal, huu ulimwengu hauna kumbukumbu, hakuna taarifa ambazo huwa zinahifadhiwa juu ya kile kizuri unacho kifanya labda uwe mtu mashuhuri. Nilikuwa tayari nimemsaidia, sasa unahisi angenikumbuka tena kwa lipi kapuku mimi? Alichukulia kwamba ni kama duniani hakuwahi kuzaliwa mtu kama mimi basi akaendelea kula maisha huku mimi nikikumbana na dhoruba la wanaume wa shoka huko jela ambako ukiwa legelege unaweza kuishia kuwa mke wa mtu ila mimi sikutaka kufikia hatua hiyo. Jela ilinibadilisha na kunifanya kuwa mwanaume, jela ilinikuza na kuyafanya maisha yangu yawe mapya kabisa kwa kujiunga na vikundi vya watu ambao walikuwa wakiogopeka kule. Wakati natoka jela nilikuwa mtu mwingine kabisa, sikuwa yule ambaye nilienda miaka ya nyuma na maisha ya jela yalinifanya niwe na maamuzi magumu mno. Yule bwana nilimuua yeye na familia yake yote kwa ule uhuni ambao alinifanyia kwa kushindwa kuheshimu kujitoa kwangu” maelezo yake hayakuwa na mwisho mzuri kwa sababu yalikuwa yanatisha.

“Dunia ina mambo ya kutisha sana”

“Jitahidi Paschal usiwe sehemu ya hizo stori za kutisha ukiwa kama mhanga kwa sababu utateseka ni bora uwe ndiye mwendeshaji wa hizo sehemu na sio mhanga” maelezo yao yalikuwa yamenoga lakini walikatishwa na simu ambayo ilianza kuita kwa fujo. Mwanaume huyo aliitazama simu hiyo na kuipokea

“Wameanza kushuka tayari”

“Kuna haja ya mimi kuja huko?”

“Hapana, tunakuja naye muda sio mrefu”

“Hazitakiwi kuzidi dakika kumi inatakiwa muwe mmetoweka humo ndani” mwanaume huyo aliongea akiwa anaikata simu na kumgeukia huyo ambaye alijulikana kama Paschal.

“Zima kamera zote ndani ya dakika ishirini ili zinavyorudi kwenye hali yake tuwe tumetoweka ndani ya hili eneo” aliongea kwa msisitizo mwanaume huyo akiwa anaitazama saa yake ya mkononi. Hayo wazungumzo yao walikuwa wanayafanyia nje ya uwanja wa ndege wa JNIA ulipo DAR ES SALAAM na watu ambao alikuwa anaongea nao walikuwa ndani ya uwanja huo wa ndege sehemu ya mapokezi wakiwa kama wenyeji ambao walikuwa hapo kuwapokea wageni wao.

Ukurasa wa nne unafika mwisho.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Previoua Next