Reader Settings

Kwenye eneo la kupokelea wageni, wenyeji walikuwa na vibango vyao vya majina mikononi kama ishara ya kutambuana kirahisi na ndugu zao lakini kwenye hilo eneo walikuwepo wanaume wanne ambao walikuwa wanaranda randa huku wakiwa na vifaa vya mawasiliano kwenye masikio yao na kuonekana kama walikuwa ni watu ambao walikuwa wanateta jambo fulani la siri. Ndani ya muda mfupi uliofuata lilitokea jambo la kushtukiza ambalo lilizua taharuki eneo hilo baada umeme kukatika ghafla kisha ukasikika mlio wa risasi. Eneo lilichafuka na kuwa uwanja wa vita hali ambayo ilifanya kuwe na mtafaruko mkubwa kwa dakika kadhaa huku watu wakiwa wanahaha huku na huko kuziponya nafsi zao.

Zilipita dakika ishirini ndipo umeme ukarudi, baada ya umeme kurudi kuna wanaume wanne walikuwa chini ndani ya mavazi ya suti zao wakiwa wamepigwa risasi za kwenye mapaji ya uso watu wakiwa wametawanyika hovyo kila sehemu. Lilikuwa jambo la kushtusha kwa sababu ilitokea ghafla bila kutarajiwa kabisa lakini haikuwa sababu ya kuamini kwamba halikutokea, tayari lilikuwa limetokea. Askari wa usalama ambao walikuwa eneo hilo iliwalazimu kuwakusanya wananchi ambao walikuwa wamesambaa hovyo kwa hofu huku wengine wakiendelea kukimbia kila sehemu na kusababisha idadi kubwa ya majeruhi.

Jambo la kushangaza ni kwamba wanaume walio uawa walikuwa ni wavaa suti tu wanne, hakuna mtu mwingine yeyote yule ambaye alikuwa ameguswa katika eneo hilo hivyo likahesabika kama tukio la kigaidi lakini wakati hayo yote yanaendelea ndani ya uwanja huo msafara wa gari tatu ulikuwa umenyoosha njia ya vingunguti kuelekea Kariakoo huku barabarani ukipishana na gari za polisi ambazo zilikuwa zinakwenda kwa kasi kubwa huko uwanja wa ndege kutokana na tukio ambalo lilikuwa limetokea. Kikosi hicho ambacho kilitokea uwanja wa ndege, kilikuwa maalumu kwa ajili ya kumteka binti mrembo ambaye alikuwa amefika ndani ya uwanja ule na walifanikisha hilo zoezi bila shida yoyote na sasa mwanamke huyo ambaye haikujulikana walikuwa na kazi ipi naye, alikuwa kwenye mkono wao tayari.

JNIA ilifungwa, vurugu na mauaji ambayo yalitokea yalifanya watu kutokuwa na uhakika na usalama wao hivyo kila mtu akawa ametawanyika upande wake huku wengine wakifanikiwa kutoka nje kabisa na kukimbilia walikokuwa wanakujua wenyewe kama sio kwa sababu ya presha lakini wengine walitulizwa na kuwekwa sehemu moja ili mtu yeyote asije akapata tatizo.

Baada ya muda mfupi kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es salaam, Raymond Kono alikuwa anawasili eneo hilo baada ya kupokea taarifa za kushtua kuhusu usalama ndani ya uwanja huo wa ndege mkubwa ambao unategemewa nchini. Baada ya kuwasili eneo hilo, aliikagua ile miili ya wale wanaume ambao walikuwa wameuawa kisha akamhitaji afisa mkuu wa usalama wa uwanja wa ndege kuweza kumpa taarifa zote juu ya kile ambacho kilitokea.

“Hawa watu wanaonekana kuuawa na mtu mmoja kutokana na jinsi walivyo uawa, unaweza ukanipa taarifa juu ya hili ndugu Jonas Moba!?”

“Ni jambo ambalo limetokea kwa haraka ila nahisi sio mtu mmoja ambaye amehusika kuua wote kwa sababu muda ambao umetumika ni mchache na kwa kiza kile mmoja asingefanikiwa hivyo walikuwa ni watu wengi ambao wanahusika na ni maelekezo ambayo walikuwa wamepewa ili kuweka ugumu kwenye kupatikana kwao baada ya hili tukio”

“Unasema unahisi?”

“Ndiyo”

“Hii sehemu ina ulinzi wa kamera kila kona, sasa unaniambia vipi kwamba unahisi?”

“Kwa sababu kamera zote zilizima na umeme ukakatwa na vyote vilipokuja kurudi tukio lilikuwa limetokea tayari kwahiyo sina uhakika na wahusika ambao wamehusika moja kwa moja”

“Kwamba kuna moja kati ya vijana wako wameisaliti nchi yao kwa kuzima kamera?”

“Bado siwezi kuthibitisha jambo hilo kwa sababu inaonekana ni mtu kutoka nje ndiye alifanya zoezi la kuzima kamera”

“Naomba unipeleke kwenye chumba cha kamera na uhakikishe hawa watu wote wanarejeshwa makwao saivi tena wakiwa salama kabisa”

“Sawa kiongozi”

Watu hao waliongozana mpaka ndani ya chumba ambacho kilikuwa kinatumika kuongozea kamera, ndani ya chumba hicho kulikuwa na vijana wa kike na wa kiume ambao walikuwa wakitwetwa kubonyeza tarakishi kwa haraka mno ili kuona kama wanaweza kuyaweka mambo sawa kwani kile ambacho kilitokea hakikuwa kitu kizuri kwa usalama wa taifa lakini walionekana kushindwa kuzipata zile taarifa ambazo walikuwa wakizitaka kwa wakati ule.

“Nionyesheni video ya dakika kumi nyuma kabla ya hili tukio kutokea” kamanda aliamuru ili kuweza kujipa uhakika kama anaweza kumuona mhusika hata mmoja ambaye angeweza kuanza naye kwenye hilo zoezi lake. Haikuchukua muda mrefu, dakika moja ilitosha kuwarejesha nyuma kidogo kuangaza kile ambacho kilikuwa kinaendelea humo ndani. Kwenye ile video ambayo ilirudiwa mara mbili ndipo kamanda wa polisi akashtuka, aliwaona wanaume tofauti wanne ambao walionekana kuwa watu wa kawaida wakiwa wamekuja kwa lengo la kuwapokea wageni wao ila aliwashtukia kwa sababu walikuwa wanaonekana kuwa makini kwenye maongezi na watu ambao hawakuwa wanaonekana.

Watu hao walikuwa wamejigawa kwenye maeneo manne tofauti wakiwa wanalitekeleza zoezi lao hilo. Kwenye mikono yao wanaume hao kila mmoja alikuwa na kibao chenye jina, hakutaka kukurupuka akataka kuhakiki uhalali wa majina ambayo watu hao walikuwa wameyabeba. Majina yote manne hayakuwepo kwenye listi ya wasafiri ambao walikuwa wamefika ndani ya eneo hilo, hilo likamuongezea mashaka na mwelekeo wa kazi yake ambayo ilikuwa imeanza.

Alizitaka picha za watu hao zikuzwe haraka, ndipo aligundua kwamba kwenye masikio yao wote walikuwa na mawasiliano wakionekana kufanya mazungumzo ambayo yalikuwa ya muda mfupi. Baada ya muda kidogo watu hao waliangalia saa zao kwa wakati mmoja na muda haukupita umeme ukawa unakatika lakini hilo jambo lilitokea muda mfupi baada ya binti mrembo kutokezea mapokezi akiwa na walinzi wake wanne. Hapo ndipo muda mfupi uliofuata, umeme ulikatika na kamera zote zilizima na kila kitu kilipokuja kurudi mauaji yalikuwa yametokea tayari huku watu wahitaharuki na kuanza kutoka nduki baada ya kushuhudia mauaji na yule binti mrembo hakuwepo.

“Kuhusu huu uzembe ambao umetokea hapa kwenye mikono yako Jonas tutaushughulikia baadae lakini hapa kuna mambo mawili ambayo tunatakiwa kuyashughulikia. Jambo la kwanza nataka kujua kwamba hawa watu ni akina nani, jambo la pili nataka kujua kwamba ni kwanini wamemteka huyu mwanamke? Kwa sababu ni dhahiri walikuja kwa lengo hilo tu na hili sio shambulio la kigaidi kama mlivyokuwa mnadai, kama ingekuwa hivyo basi kungekuwa na madhara makubwa na mauaji ya watu wengi na wasingetumia ustaarabu namna hii wangehakikisha watu wanapata madhara pamoja na vitu vyetu. Kwahiyo mpaka wanakuja hapa mlengwa wao alikuwa anafahamika, baada ya kujua haya nitahitaji kujua kwamba imewezekaje watu kuingia na silaha mpaka huku mapokezi kirahisi tu namna hii?” Kamanda alikuwa amefura kwa hasira wakati anampa maelekezo yake afisa mkuu wa kitengo cha usalama wa hapo uwanja wa ndege.

Watu wale wote wanne zilihitajika taarifa zao kwa sababu picha zilikuwepo, kati yao ni mmoja tu pekee ambaye taarifa zake zilikuja na wengine hawakuonekana kuwahi kutokea duniani kitu ambacho kiliacha maswali mengine mengi. Damasi Kazimoto, ndilo jina pekee ambalo lilitokea kwenye picha ya mwanaume mmoja kati ya wale wanne ambao walionekana uwanja wa ndege. Taarifa zake zote mwanaume huyo zilikuwa zinaonekana vyema kabisa, alikuwa mzaliwa wa kijiji cha Tambani, Mkuranga na kabila lake alikuwa ni Mndengereko.

Alikuwa ni mwanajeshi wa zamani wa jeshi la wananchi la kujenga taifa ambalo alijiunga nalo baada ya kumaliza tu shule ya upili. Damasi umri wake ulikuwa unasoma miaka thelathini na minne kwenye komputa hizo kubwa ambazo mbele yake ndipo alikuwepo kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es salaam. Jambo la kushangaza kwenye taarifa hiyo ni kwamba mwanaume huyo alikuwa amekufa miaka miwili ambayo ilikuwa imepita na wakati anakufa ndipo alikuwa na miaka thelathini na minne hivyo kama angekuwa hai maana yake angekuwa na umri wa miaka thelathini na misita.

UKURASA WA TANO umefika mwisho.

 

 

 

 

 

Previoua Next