ANGALIZO
Simulizi hii ni ya kweli.
Imesimuliwa kwa mwandishi na yeye akatumia ufundi wa kifasihi, kuiweka katika maandishi.
Kwa maana hio, majina yaliyomo yametumika katika kivuli cha sanaa, hayana uhalisia wowote ule.
Mwandishi anaomba radhi endapo yatagusa pasipolengwa!
Asante,
Godlove Kabati, Morogoro-Tanzania
KIKAO CHA HAKI
SEHEMU YA KWANZA
*******
MWAMUZI
Naam Mista Ansbert...
Umeniita hapa ili niwe mwamuzi wa mgogoro wenu: Wewe na huyu aliyekuwa mpenzi wako...dada Nadia.
Nadhani ni wasaa mzuri kabisa wa kuisikiliza hadithi yako..na baadae tutasikiliza upande wake.
Haya karibu utusimulie ni namna gani mlikwaruzana na ilikuwa vipi...
******
MWANAUME,
Asante sana, kwa kuwa umeshanitambulisha kwa jina, sidhani kama ni sahihi kwangu kupoteza sekunde kadhaa kuwaaminisha watu juu ya jina hili.
Eeer, Hapo mwanzo mimi na Nadia tulipendana sana.
Sikuwahi kufahamu ni shida gani kubwa
iliyotokea...lakini mimi na yeye tuliwahi kupendana sana.
Tulikuwa vizuri tu hapo mwanzo. Narudia tena kwa mara nyingine, tulipendana sana tena sanaa.
Mapenzi yetu yalifaa kabisa kuwa kama kivutio cha utalii, watu wengine waje washuhudie maana halisi ya
kupendana.
Tulienda vacation mbalimbali...tulivaa sare, tukazuru maeneo na vivutio mbalimbali hapa nchini na nchi kadhaa za ughaibuni.
Nikampatia ahadi nyingi.
“Baby mwakani tutaenda Philadelphia.
Au haupapendi...twende tukale raha mji wa Miami?”
Akajibu kuwa hapendi kwenda Amerika, anataka kwenda Dubai.
Tayari rafiki zake wameshamsimulia juu ya maajabu ya uzuri wa mji huo mkubwa wa kibiashara. Mi’ nikamkubalia...nilitaka daima mimi nisiwe chanzo cha huzuni yake.
Bali niwe chemchemi ya furaha yake. Unadhani nilifanya hayo tu?
Hata alipohitaji attention yangu nilimpatia. Muda wowote ule simu yangu ilipounguruma na nikaona lile jina nililomsevu la kimahaba,
‘Corazòn 💕🔐’ niliwahi fasta kuiokota...haijalishi ni ujumbe au alinipigia.
Kama simu yangu ingepata nafasi ya kuwa hai....nadhani ingeweza kuwa shuhuda wa wingi wa sekunde zote na dakika nilizowahi kuwasiliana naye.
Ingewaeleza juu ya zile meseji nzuri na tamu
zilizoundwa kwa herufi na silabi za mapenzi kisha zikapambwa kwa emoji na maua.
Simu yangu ingewashuhudia juu ya zile saa
tuliokaribishana mbele ya kila sahani yenye
chakula...ingewaelezea juu ya kuulizana kwetu kama kila mmoja ameshakula.
Hii simu hii....
Ingelalamika juu ya ule muda mrefu wa maongezi ambao niliutumia usiku kuongea naye, sauti yake ikiwa nyororo na ya kubembeleza na ya kwangu ikiwa nzito
na iliyotangaza usalama.
Mwisho wa maongezi kila mtu angesusa kukata simu.
Kila kitu kimebadilika, leo hii kila mtu amesusa kuliona jina la mwenzie kwenye orodha ya contacts.
Kuna imani kuu kwetu sisi wanaume, inayosema kuwa ni nguvu ya pesa pekee yenye uwezo wa kumuonesha mwanamke ni namna gani unampenda.
Hata mimi nilikuwa mmoja kati ya waamini wa imani hii. Kwangu pesa niliiona kama mbolea inayostawisha penzi katika shamba la mahusiano yangu mimi na yeye
Nadia. Basi niliiongezea fedha kwenye hili shamba langu. Ili kuboresha rutuba ya penzi letu.
Ni kweli kuwa mimi sio tajiri sana...
Lakini kwa kila nilichokipata nilijitahidi sana
kumtimizia mahitaji yake yote. Nilijitahidi sana kufanya kazi na kuongeza kipato changu ili kukidhi haja zake yeye.
Sijui atanilaumu kwa lipi.
Nakumbuka ahadi tulizowekeana kuwa hakuna atakayeuona utupu wa mwenzie kabla hatujafunga ndoa. Na kweli tukatunziana uaminifu wetu.
Nikiwa na ndoto iliyobeba maono ya kuwa baba wa watoto wake na yeye awe mama wa watoto wetu.
Tukaahidiana ndoa!.
Lakini alibadilika ghafla sana, akawa mwenye hasira kila muda. Kisha kama utani tu, Nadia akaanza kuteleza taratibu.
Kuna siku nilimpigia simu akawa anaongea
harakaharaka kuwa yuko bize.
Ubize gani huo wa ghafla aliokuwa nao siku hii? Haikuwa kawaida yake hakika!
Na mimi nikajipa imani kuwa labda alikuwa bize sana na kazi mchana, nitamtafuta usiku.
Nilipigwa na mshituko kuwa kumbe hata nilipompigia usiku akanambia kuwa amechoka sana.
Na wala hakuniambia ‘nitafute kesho’,
Aliniambia kuwa ‘tutawasiliana siku nyingine...’
Ajabu iliyoje hii!
Nadia ndio wa kuniambia mimi hivyo?! Lakini kumbe sikujua kuwa mimi ndiye nilikuwa nyuma ya muda.
Kuanzia hapo nikawa nimemkaribisha shetani kwenye penzi letu. Tena nikamkaribisha sebuleni nikampakulia na chakula kabisa.
Huyu shetani akawa amelichafua penzi letu mimi na Nadia. Nadia alibadilika sana, akawa mkavu na kunikaukia kabisa! Zile jumbe nyingi za mahaba zikageuka jumbe za kashfa na malalamiko. Ikawa sasa kila mtu anajali tumbo lake bila kuwaza mwingine
amekula nini.
Kila kitu kilipotea upesi sana kama barafu iliyoanikwa kwenye jangwa juani. Upendo wetu ukaanza sasa kuwa uadui. Ilikuwa ni kama tunatafutiana kosa ambalo lingetukatia tiketi ya kuachana.
Nikahisi labda nimekosea mahali...lakini sikuona kosa langu abadani. Labda ni kwa vile alijua kuwa nampemda sana nd’o sababu akanifanyia visa vyote hivi.
Kama maajabu tu, mimi na Nadia tuliachana bila hata kupeana taarifa. Alipotea kwenye maisha yangu na mimi ikanibidi nijifunze kumsahau. Mawasiliano nayo yalipoona tunayapotezea muda yakaamua kutuaga na kuondoka kati yetu daima.
Nafsi yangu ikamezwa na hisia kali za hasira, kila nilipozikumbuka juhudi zangu zote kwa Nadia, nikamuona kama aliyenidharau sana. Roho ovu ya kisasi ikanitembelea. Nikaamua kulipiza kisasi. Sio kisasi cha damu, hasha!
Lakini nilitaka azishuhudie hatua zote za maumivu atakazokuwa anapitia kwa macho yake na ubongo wake utambue.
Nikajikuta nimetoa kauli ya kishujaa kutoka kinywani mwangu,
“There is plenty of fish in the sea”
Kuwa samaki ni wengi sana kwenye hii bahari...na mimi kama mvuvi nisiwe na hofu maana bahari ni kubwa mno. Sikutaka ushauri, nikavua samaki wengine
kutoka baharini.
Nilianza kujihusisha kwenye mahusiano na mabinti wengine tena wengi. Na kwa kasi sana nikataka kumvimbia Nadia kwa makusudi mpaka ajue.
Atajuaje sasa?
WhatsApp status...kule ndiko kulikuwa bandari ambayo nilitia nanga ya hisia zangu zote na maumivu juu yake.
Nikacheza na settings...aone yeye peke yake.
Namna nilivyoteketeza pesa kununua vinywaji vya bei ghali....mimi na warembo wengine tukala bata kiasi cha kuku kuona wivu. Nikiandika caption za vijembe na mafumbo kumsuta yeye tu. Kiukweli nilimtumia
mishale mingi yenye sumu hukohuko mitandaoni.
Lakini yote haya nilifanya nikiwa na giza moyoni mwangu. Bado Nadia alikuwa na nafasi kubwa kwenye moyo wangu. Ni kama alikuwa amejenga makazi ya kudumu moyoni mwangu.
Nilikuwa naishi kwenye ndoto ya kuwa akiniona ,ataona wivu...labda atanirudia. Ataniomba msamaha na kuacha hizi tabia zake zote za maudhi. Nilikuwa najipa
matumaini bila hata ya kujua huko aliko anatembea na nani, yuko na nani kwenye mahusiano yake mapya.
Nilichokijua mimi ni kuwa upendo wake kwangu umepungua kwa kuwa amempata mtu mwingine. Bosi labda au kibopa mwenye pesa...au mwajiri wake huko katika kazi zake za uhasibu.
Mimi nikaendelea kujijengea tulizo la nafsi ambalo lisingeniponya jeraha la moyo wangu. Pombe inapunguza mawazo na maumivu kwa muda tu...lakini ikiisha kichwani matatizo yanabaki palepale.
Sikupata faraja yoyote ile, bado ilikuwa ngumu kumtoa akilini mwangu..
Alikuwa kama sumu iliyotapakaa kwenye mfumo wa damu yangu.
Itaendelea...
Comments