SEHEMU YA PILI
USHAHIDI WA MWANAUME
Mimi ni mfanyabiashara. Ninamiliki migahawa kadhaa hapa jijini.
Siku moja nikiwa kazini, nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu akaniambia kuwa niwahi haraka sana katika hoteli fulani kubwa tu hapa jijini Dar-es-Salaam.
Akaniambia kuwa kuna kioja cha kutazama na sio kusimuliwa...
Nikaziahirisha shughuli zangu zote nikawasha gari yangu na kuwahi eneo nililoambiwa.
Nilipofika nje, rafiki yangu akanielekeza ndani katika meza aliyokuwa amekaa na nilipotulia akaniambia nigeuke nyuma niangalie upande wa kushoto.
Nikageuka.
Macho yangu ya nyama yaliona vizuri sana.
Haukuhitajika msaada wa miwani ya lenzi au hadubini ya kisayansi...niliyemuona pale alikuwa ni Nadia, hakuwa peke yake-alikuwa na yule mwanaume aliyewahi kuniambia kuwa ni rafiki yake tu.
Na yeye sio kwamba hakuniona...aliniona pia. Lakini kwa macho ya dharau na kiburi tena cha kiwango cha lami...akanicheka!
Maajabu!
Macho yangu yalikuwa yanashuhudia kioja cha taswira. Nadia alikuwa na jamaa yake na huyu jamaa sura yake haikuwa ngeni. Picha yake iliwahi kutundikwa na Nadia kwenye status akidai kuwa alikuwa ni rafiki yake. Na
mimi kwa vile sikutaka kumghasi sana, nikakubali kishingo upande huku fukuto zito la sumu ya wivu likiuteketeza moyo wangu.
Mwamba huyu hapa!
Jamaa alikuwa amekamilika kwelikweli ;bila kutafuta ushahidi mwingi sana...hela ilionekaa ipo pale!
Mwili wake wa mazoezi ulitangaza ushupavu, ulivikwa mavazi nadhifu ya gharama na kwa kumkagua harakaharaka nilimkadiria kuwa kavaa laki tano hivi kama sio sita.
Saa yake ya mkononi tu ilipigilia msumari wa mwisho kwenye mlango wa utajiri wake,
NAVY FORCE brand ya kwanza kabisa.
“Oa Bro! Si Nadia yule au?” Rafiki yangu alinitupia swali ambalo hata yeye jibu alikuwa nalo. Tashtiti hii ilinishtua kutoka katika mawazo yangu nikiwa bado nimegeuka nyuma na macho yako yakigoma kutoka
kwenye ile meza alipokuwa Nadia.
Sikujua nimjibu nini. Ulimi wangu ulikuwa mzito, mate mdomoni yamechachuka na koo likaanza kuhisi kiu.
Nikawa kama nimepigwa ganzi ya ghafla. Hasira iliyochanganyikana na wivu, vilichemka sana mwilini mwangu.
Mikono yangu ikawa inanitetemeka sana kwa hasira kiasi kwamba hata jasho jembamba likaanza kuvuja kwenye viganja vya mikono yangu.
Hata muhudumu aliyekuja kunihudumia, sikumsikia kwa wakati huu.
Masikio yangu yalikuwa yametiwa uziwi.
“Kaka uletewe nini?!” alinishtua rafiki yangu.
“Si-si-sidhani kama nitatumia chochote kwa
sasa....asante” ilinitoka.
Muhudumu akaanza kuzihesabu hatua zake kuondoka pale mezani kabla koo langu halijanikumbusha kuwa nahitaji maji.
“Mu-muhudumu!! Dada! Tafadhali niletee maji ya kunywa!”, ikanibidi nimuite kwa sauti tena yule mhudumu. Sikueleweka kama nilihitaji huduma au sikuhitaji. Muhudumu yule akaniweka kwenye kundi la
wale wateja wasumbufu na wakorofi. Akakubali akiwa na sura iliyoonyesha kukereka!
Niliwatazama Nadia na mpenzi wake mpya, nikiwa nakunywa maji kupunguza hasira na kiu kwa pamoja.
Sikuwa na cha kufanya. Nilikuwa kama mbwa mkali aliyefungiwa kwenye banda imara, anawaona wezi na kuwabwekea bila kuwadhuru.
Nadia akazidisha mapozi...akawa anamtazama yule bwana kwa kulegeza macho.
Anajichekesha, mbaya zaidi akainamisha kichwa chake na kumpiga busu.
Dharau nyingine hii!
Tena mbele yangu.
‘Anafanya makusudi huyu ili akuumize’ fikra yangu ikanieleza.
“Oyah Bruno!” Nilimuita rafiki yangu ambaye muda wote huu alikuwa katulia tuli akiburudika na soda yake baridi.
“Nipange mwanangu”.
“Huu ni upuuzi!”. Tusi kali lilinitoka nikimtangazia rafiki yangu juu ya balaa ambalo ningeenda kulizua pale mezani kwa Nadia.
“Tulia babuh! Sasa demu si mliachana kitambo? We shida yako nini sasa. Ulitaka kujua anatoka na nani...nimekuita ujionee mwenyewe."
“Aah hii haivumiliki kaka.” Hisia za hasira ziliendelea kunitawala.
“Poa kama vipi tuondoke sasa. Tayari nimeona upuuzi niliotaka kuona. Nikiendelea kukaa hapa nitampasuapasua huyu manzi kudadek!!”
“Em tuliza hilo povu ...tusepe sasa”
Alimalizia soda yake kwa mafunda makubwa na tukaondoka pale.
Sikutaka kugeuka nyuma tena. Tayari dharau
alizonionyesha Nadia zilinitosha, sikutaka zaidi. ‘Ina maana muda ule wote walikuwa kwenye mahusiano?’
Bado akili yangu iligoma kuamini.
Niliingia kwenye gari mimi na rafiki yangu,
nikamuachia usukani aendeshe yeye maana
nisingeweza kuendesha kwa wakati ule.
Aliendesha akinishauri na kunisemesha maneno mengi ya faraja na hekima ambayo sikuyasikilizakwa makini, niliona tu mdomo wake ukicheza cheza. Maneno yake
yasingeubadilisha ukweli kuwa Nadia aliniacha na kuchukuliwa na yule aliyewahi kuniambia kuwa ‘ni rafiki tu’.
Jambo la maana sana lililofanywa na maneno yake ni kupasua lile anga la ukimya ndani ya gari. Maneno yake
pekee niliyoyasikia,
“...hawa wanawake ni nyoka kaka!...”
Siku ilikuwa imeanza vizuri kazini, ghafla ikawa siku mbaya kazini. Niliwahi kurudi mapema nyumbani kwangu.
Kila ujumbe wa binti ulioingia kwenye simu yangu niliuona ni kama unanicheka juu ya kiwango cha ubwege nilicho nacho. Sikujishughulisha kuujibu. Hata kama ungehusisha neno ‘pesa’.
Kila kinywaji kitamu nilichokizoea kilikuwa kichungu mdomoni mwangu. Hakukuwa na pombe yoyote ambayo iliwahi kuliondoa jina NADIA akilini mwangu,
hivyo niliacha kunywa pombe tangu zamani.
Nikamkumbuka yule jamaa aliyekuwa na Nadia kule hotelini, nikajilinganisha naye;
“Amenizidi nini yule kwani...labda anamjali sana au?”
Nikajiuliza mimi mwenyewe. Mishale ya saa pale juu ukutani ilielekeza kuwa wakati huo ulikuwa ni saa moja na nusu jioni.
Nikaokota simu yangu iliokuwa pale mezani nikaanza kuitafuta namba ya Nadia ambayo nilikuwa nimeiblock...mara chache sana nilikuwa naitumia hasa nikitaka kupost status za vijembe au kutegeshea kama nitapata ujumbe wowote ule kutoka kwake. Nilikuwa
nimeifuta mara kwa mara na kuisevu tena. Maana nilikuwa nimeikariri tayari.
Nikaipiga na ikaita! Alaa kumbe
hakuniblock?kuniblock kumbe! Nikapata lepe la furaha.
Lakini moyo ukasita...
“Huyu anaweza akahisi kuwa bado nampenda.”
Nikataka kukata simu, lakini nikakaza!
Ikaita mpaka ikakata. Nikavuta pumzi ndefu. Akili nyingine ikaniambia nisimpigie tena, ataona nina shobo nae. Atanifikiriaje huyu?
Nikavaa ujasiri, nikapiga tena namba ile...haikuita sana ikapokelewa.
“Haloo” ilikuwa sauti nyepesi ya kikee, sauti ambayo nilikuwa nimeizoea japo sikuwa nimeisikia kwa muda wa miezi mrefu sana. Sauti ya Nadia.
“Haloo Nadia! Habari yako?” Nilimjibu kwa sauti baridi, iliyotangaza simanzi.
“Poa mzima wewe?!...”
“Safi aisee za masiku?”nilimuuliza tena nikizidi kumjulia hali, bado sielewi nianze na mada gani.
“Poa tu...naongea na nani mwenzangu?” Japokuwa ilikuwa sauti nyororo lakini hili swali lilinichoma kama kisu kikali tumboni mwangu.
Hakuwa na namba yangu! Amenisahau.
Sekunde kadhaa zikapita nikiwa kimya.
“Haloo?” Aliniitaa.
“Mimi...mi..ni Ans..Ansbert hapa!” nilimjibu kwa kigugumizi.
“Eeh wewe...vipi?” Sikujua kama alikuwa ananiuliza swali ama ananishangaa.
“Eeer, uko poa?” Nikaendelea kumjulia hali huku nikijipanga kutoa sumu zangu.
“Nakusikiliza...” alinijibu kwa dharau.
“Nadia, yule uliyekuwa naye leo ni nani?”, lilikuwa swali langu la moja kwa moja kwake. Jibu nilikuwa nalo na sikuchagua kuliamini moja kwa moja mpaka yeye mwenyewe anishibitishie kwa maneno ya kinywa
chake.
“Aah makubwa, kwani we ulionaje na unaniuliza kama nani?”
Dharau!
Kauli yake ilinichoma kama mkuki wa moto. ‘Huyu demu kapata wapi hizi kauli za kibabe?’niliwaza. Na katika shangaa yangu hiyo akanitupia jibu la moja kwa moja,
“Kwa taarifa yako... uliyemuona ni mume wangu mtarajiwa! Mwezi ujao unakaribishwa harusini upo hapo?!”
Ajabu nyingine!
Natangaziwa harusi kwa kauli za mipasho na chuki zilizopambwa kwa hasira. Sikumbuki mara ya mwisho Nadia kuongea kwa hasira namna hiyo ilikuwa lini.
Lakini leo hii ananipatia mwaliko usiokuwa na kadi.
Nikidhani kuwa mwanaume yule alikuwa ni mpenzi tu kumbe ni mchumba kabisa. Nilikuwa ninapotea njia!
Hata jina la mchumba lilikuwa linamshusha cheo chake, ilibidi nimfahamu kama mume mtarajiwa wa Nadia.
Huu ulikuwa ni ukweli mchungu mno kuumeza.
Mwili wangu ulizizima.
Donge zito la hasira likajikita kifuani, siwezi kulimeza wala kulitapika. Pia sikutaka Nadia ajue kuwa amenikasirisha.
“Ooh! Hongera sana. Hivi nd’o umesema kuwa harusi yenu itakuwaa...mwezi ujao eeh? Safi sana. Nitafurahi kama nitapata kadi ya mwaliko.” Nilitamka nikiwa nimejikaza kisabuni tena kwa sauti tulivu mno ilioonyesha kuwa sikustaajabishwa na harusi ile.
Nikamsikilizia Nadia atanijibu nini...
“Aasanteeh...nitakutumia tu wala usijali. Vipi lakini mawifi zangu hawajambo?” ilimtoka.
‘Mtego huu!’ Nilishtuka tena.
Sasa Nadia alitaka kutumia bomu lilelile nililotumia mimi. Alitaka wote tuonekane tuna makosa. Lakini mimi sikutaka kunasa humo.
“Uum..Nakumbuka uliwahi kuniambia kuwa ni rafiki yako huyo jamaa...vipi lakini anaitwa nani?”
Kabla hajanijibu, nikasikia sauti purukushani kwenye simu. Ni kama Nadia alikuwa bize na mtu fulani huko alikokuwa.
Nikasikia kwa mbali ni kama sauti ya nzito ya kiume imeingia eneo lile, na kweli hali ile ya hewa ikajaaliwa kupata mchanganyiko wa sauti nyororo ya kike na nzito ya kiume. Mimi niliitambua hii ya kike kuwa ya Nadia
lakini ya kiume sikuitambua mara moja.
Nadia hakuwa anaongea na mimi tena, nikasikiliza sauti za vicheko na mabusu kadha wa kadha. Ndio! Hakukata simu yangu lakini hii dharau ya kuniacha hewani na kujishughulisha na mwanaume mwingine kilikuwa ni kiwango kikubwa mno cha dharau chenye daraja A.
‘Nani huyu kama sio yule jamaa mume mtarajiwa?’
Nilijihoji.
“Darling ongea na huyu hapa...msalimie” nikasikia sauti ya Nadia ikibembeleza ombi kwa huyo mtu aliyeitwa ‘Darling’.
“Hey haloo!” Sauti ya nzito ya kiume ilisikika
ikiutambua uwepo wangu katika simu ile iliyokuwa imesuswa na Nadia
Ilikuwa sauti ya mamlaka haswa haswa, sawa na mfalme aliyekuwa katika milki yake.
Niliganda kama sanamu. Mishale na mikuki ya dharau ambayo Nadia alinitupia haikumtosha. Sasa alikuwa anatumia silaha za nyuklia kuniangamiza kabisa!
“Haloo bro niaje?” nilijibu kwa sauti baridi.
“Kama kawa mzee...vipi hapo?” jamaa aliendelea kutaka kunijulia hali.
“Kwema sana...mishe nieje?”
“Sana tu... nani hapo?”
‘Nani hapo?’ Ningejitambulisha kama nani?
Rafiki wa Nadia? Hapana ningekuwa nimejishusha thamani yangu.
Kaka basi? Nilitaka kujizaba kofi, baada ya kufikiria hivi tena. Kaka? Yaani mimi niwe kaka yake Nadia.
Hapana. Nilipata kigugumizi cha ghafla.
Mimi ni nani kwa Nadia? Sio mpenzi, sio kaka, sio rafiki, nikisema mimi ni ex tena kwenye masikio ya mwanaume mwenzangu nitakuwa kichekesho.
Lakini yote haya ya nini...nimepiga simu kwa Nadia ili nijue nini ambacho sikijui? Kila ukweli mchungu niliotaka kuudhibitisha tayari nilikuwa nao mezani.
Nilijiona punguani hakika.
“Haloo ka…” kabla hajamalizia sentensi yake nilikata simu na kuitupa juu ya sofa.
“Mimi ni fala sana!” Nilijikuta najisemesha mwenyewe, nikayasindikiza maneno yangu kwa glasi ya kinywaji nilichokiona kuwa kichungu hapo awali.
Wakati huu kilirejea kuwa kitamu sana.
“Bonge la falaaa!!”
Nikatamka tena kwa sauti baada ya kumeza funda lile la kinywaji.
Nadia alikuwa amenifanya zuzu.
Upendo mwingi niliokuwa nao juu yake ulikuwa kama gereza la maisha kwangu.
Gereza lililonifanya nisikubaliane na uhalisia kuwa yeye sio wangu tena.
Ameenda!
Tayari alikuwa ameshinda huu mchezo, tena kwa magoli matatu bila. Na mimi sikutaka nimuonyeshe kuwa nashindana naye, sikutaka afahamu kuwa naumia kwa kushinda kwangu.
Kila kitu hupungua thamani pale kinapokuwa na machaguo yake ya ziada. Mimi kwa Nadia nilikuwa chaguo la mwisho kabisa.
Alikuwa amepata kilicho bora kwake.
Hii ndio ilikuwa siku yangu ya mwisho kuisikiliza sauti ya Nadia na ikawa siku ya kwanza kumuepuka na kujifunza kumsahau.
Hadi hivi leo niko naye hapa mbele yako imepita miezi sita tangu tumeonana au kuwasiliana. Huyu hapa leo, anahitaji nimsaidie.
Anahitaji msaada wa damu yangu, uhai wangu kumsaidia huyo mme wake. Ungekuwa wewe kaka ungemsaidia?
*******
MUAMUZI:
“Sawa bwana Ansbert tumeusikia upande wako.
Hadithi yako inaonyesha ni namna gani ulikasirishwa na tabia za Nadia jambo lililopelekea kutengana
kwenu.
Hukupendezwa hakika. Lakini kabla sijatoa uamuzi naomba tumsikilize dada Nadia pia...
Nadia karibu...”
****
Naam,
Ni wasaa wa kuusikiliza upande wa mwanamke, Nadia.
Unadhani ana hoja gani za msingi?!
Je zina mashiko?
Hayo yote tutayafahamu kwenye sehemu ijayo ya KIKAO CHA HAKI!
Kalamu ya mwandishi ina mengi ya kutujuza.
Comments