SEHEMU YA KWANZA;
Bukoba, Kagera
Jumamosi, saa kumi jioni.
KITENDO cha kukatika kwa umeme kiliuzika uchangamfu na kufufua hali ya kupooza kwenye genge la mtaa huu.
Hii sio hali ya kawaida kabisa,
Yaani kwenye genge la mtaa huu wa Buyekera mida hii ya jioni kuwa kimya namna hii?
Kwa kawaida, imezoeleka hali ya uchangamfu wa anga linalotetemeshwa kwa kelele za hapa na pale.
Duka lile utasikia midundo ya muziki murua wenye ladha ya Amapiano. Mara pale kwenye maduka ya kanda za video utasikia namna spika zinavyoshindana kupaza sauti za watafsiri wa filamu mbalimbali kutoka n'gambo.
Kule utasikia vipaza sauti vya wapiga minada kusifia upungufu wa bei za bidhaa zao. Na vibanda-umiza navyo havikutaka kuachwa nyuma, hupaza sauti za watangazaji mbalimbali wa mechi.
Ni kelele mtindo moja, ili mradi tu kila mfanyabiashara, biashara yake isikike vyema zaidi ya mwingine.
Genge hili kubwa hugeuka kuwa gulio dogo. Leo mambo ni tofauti kabisa.
Genge limepoa!
Kupooza huku kumefifisha hata idadi ya wanunuzi na wachuuzi mahali hapa. Kwa kawaida ardhi hii hukusanya watu wengi sana muda kama huu. Ardhi hupata suluba sana kuzibeba nyayo za viumbe hai wanaotembea juu yake. Lakini leo hali ni tofauti kidogo, genge limepoa sana. Ni kama watu wamelisaliti genge la mtaa huu.
Hakukuwa na tangazo lolote lile juu ya kukatwa kwa umeme kwa muda mrefu namna hii. Wakazi wa eneo lile walikubali kukosa umeme kwa siku moja, wakaukosa siku ya pili na sasa hii ilikuwa siku ya tatu.
Siku tatu bila umeme!
Maswali na lawama vikawa vingi kwa serikali yao, lakini majibu waliyopewa yalikuwa yaleyale waliyozoea kuyasikia siku zote,
"Kuna matatizo ya kiufundi. Ambayo yanafanyiwa kazi".
Walijibiwa hivyo.
Adha hii ikayumbisha biashara za wale waliotegemea sana umeme ili kuuza bidhaa au ujuzi wao.
Tatizo hili likawa kama ngumi ya pua kwa wale wafanyabishara wasioweza kumiliki majenereta ya umeme, na shughuli zao zilitegemea umeme ili wapate kipato.
******
Nje ya jengo dogo mfano wa kibanda, kilichonakshiwa kwa rangi na mchoro mkubwa wa aliyekuwa msanii maarufu wa marekani, Tupac Shakur.
Maneno makubwa yanasomeka pale juu ya mlango wa banda hili la mbao,
FEROOUZ HAIR CUTS.
Kijana mmoja wa kiume anaonekana kuketi umbali wa hatua nne hadi tano nje kidogo kutoka kwenye banda hili. Yeye pia akiwa mmoja miongoni mwa wahanga wa tatizo hili la kukatwa kwa umeme. Ikiwa ni siku ya tatu hii amefungua saluni yake bila kutoa huduma yoyote ile.
Amekaa juu ya benchi, ameegemea ukuta wa nyumba iliyokuwa mkabala na saluni yake.
Ameketi kuuelekea mlango wa ofisi yake hii uliokuwa wazi. Ni mtulivu ameifumbata mikono yake, macho mbele ameitazama taa ndani ya saluni yake.
Alikuwa amewasha swichi akitarajia kuwa taa ile itawaka mara tu umeme utakaporudi kutoka huko ulikokuwa umeenda kutalii. Lakini taa ikabaki kimya ikinin'ginia juu ya dari.
"Aah kudadek!", ilimtoka kinywani mwake.
"Wana nini hawa?". Haikujulikana kama anajiuliza swali au alikuwa analalamika.
"Hivi wanataka tule mchanga? Au wanataka tule mwanga wa jua kama Jadu. Yaani siku ya tatu hii wamekaa kimya tu. Sema ngoja! Wata-", hakuimaliza sentensi yake.
Aligundua kuwa hata akilalamika vipi, hatakuwa na namna yoyote ile ya kuiumiza serikali.
Kwani ni matatizo mangapi yamewahi kulalamikiwa na bado wakaishi humohumo?
Alibaki kufyonza tu.
Lilikuwa sawa na dua la kuku, lisiloweza kumpata mwewe.
Anasimama na kupiga hatua tano kuingia ndani ya banda hili. Amefika ndani na kunyanyua chupa yake kubwa ya maji ambayo ilikuwa na maji nusu ya ujazo wake kamili. Anazungusha mfuniko wake kulifungua lakini anakatishwa baada ya kusikia sauti ya muito wa simu mfukoni mwake.
Anaachana na chupa la maji, anachukua simu yake na kutazama jina la aliyempigia. Mara anaishusha chini simu yake akiwa amekunja ndita usoni kwa hasira. Akaiacha iendelee kuita, huenda huyu aliyempigia amemuudhi au hakutaka kuongea naye kwa muda huo...
"Huyu demu naye atakuwa anataka hela tu sa'hivi , sijui kwa nini nilimuahidi!"
Akajisemea peke yake,
"Sipokei simu yake!"
Akaamua kupiga mafunda kadhaa ya maji kutoka kwenye chupa lile.
Mara ikasikika sauti ya mtetemo wa pikipiki ambayo ilikuwa ikijongea kuelekea jengo lake la saluni lilipo. Mtetemo ule ukazimika ghafla, karibu zaidi na saluni yake. Hii ikamjulisha kuwa kuna mtu yupo nje ya saluni.
Akajaribu kuchungulia nje kupitia dirisha lake dogo, ili aone ni nani huyu aliyesimama nje ya saluni yake, huenda akawa mteja ambaye hakumtarajia kuwa pale muda kama huu.
Alichokiona kilimfanya atabasamu.
"Kijana Mtemi Moringo...naona mambo sio mabaya sana!" Feruzi akapaza sauti yake, ambayo ilimfikia yule mtu pale nje aliyejulikana kwa jina la Mtemi. Na yeye akatabasamu.
Mtemi akapaki pikipiki yake vizuri kisha akaanza kujongea kuingia ndani ya saluni.
"Oyaaae kijana Feruzi niaje hapa!" Akasalimiwa na huyu mgeni.
"Aah kaka, jau jau tu." Kijana huyu aliyejulikana kwa jina la Feruzi akamjibu kwa sauti iliyotangaza unyonge.
Mtemi akavua koti lake kubwa na kulitundika juu ya msumari mmojawapo uliochomoza kwenye ubao. Akaweka helmeti yake kwenye kiti kilichokuwepo pale ndani.
Kisha akajongea moja kwa moja mpaka mbele ya kioo kipana kilichokuwepo pale ndani, akachagua chanuo kubwa la nywele miongoni mwa vingi vilivyokuwepo pale kwenye shubaka. Akaanza kuchana nywele zake nyingi kichwani, zilizokuwa kwenye mtindo wa Afro, huku akijitazama kwenye kioo.
"Umeme bado hujarudi tu?!" Akatupa swali huku akiendelea kugeuzageuza kichwa chake mbele ya kioo.
"Yaani acha tu bro, siku ya tatu leo...wanataka tuwalambe miguu yao sijui?" Feruzi akatamka huku na yeye pia muda huu akiwa amekigeukia kioo akiitazama taswira yake...ambayo ilimkasirikia kama alivyokuwa amekasirika yeye.
"Lakini nasikia kuna nguzo imeanguka kule juu maeneo ya Kibeta! Huenda nd'o wanashughulika nayo muda huu" , akasema Mtemi.
"Nguzo? Ina maana muda wote huu tangu juzi wameshindwa kubadilisha? Hawajui kuwa watu huku tunakula upepo?" Feruzi, akaongea tena kwa makasiriko.
"Nd'o serikali yetu hio... siku zote mwenye shibe hamjui mwenye njaa."
"Aah hata kama bhana...unaona hapa mwanangu, leo tumbo langu halijasalimiwa na chakula chochote kile. Na sioni hata hela ya kununua hicho chakula napata wapi." Feruzi akaanza kuangusha malalamiko yake.
"Eboo! Kumbe nd'o maana una hasira. Hii yote ni kwa sababu ya njaa!" Mtemi akayasindikiza maneno yake kwa kicheko dhaifu, kilichoudhibitisha utani uliokuwepo tangu siku nyingi baina ya marafiki hawa wawili.
Maneno yake yakamfanya Feruzi ashindwe kujizuia na yeye akacheka. Japo kicheko chake kilionyesha wazi kuwa amechoka na ana njaa!
"Nimezoea muda kama huu tena wikendi! Wateja kibao sana, halafu nikifika huwa unanifukuza we fala!" Mtemi akatupa kauli nyingine ya utani.
"Duh! Hapa mwanangu unanionea! Lini nimekufukuza wewe. Wakati humu umepafanya kama sebule yako, tena huwa nakunyoa bure kabisa!" Feruzi akajitetea.
"Aah wapi we mshikaji huwa unatukataa wahuni. Sema hamna mbaya, ngoja nenge ikunyooshe kwanza! Hahaha"
Feruzi akasogea karibu na koti lililokuwa limetundikwa pale kwenye ubao.
Akalichukua na kuanza kulivaa kabla Mtemi hajamshitua,
"Oyah wee, namna gani tena? Wapi na koti langu tena"
Feruzi akalivaa koti kimya, kisha akasogelea helmeti iliokuwepo pale juu ya kiti. Akiokota na kuivaa kichwani mwake.
Muda huu wote Mtemi amemtumbulia macho akimshangaa, hajui ni nini rafiki yake amepanga kufanya.
Feruzi akamaliza kuvaa akiwa kimya. Halafu akamsogelea Mtemi na kunyoosha mkono wake,
"Em nipe funguo hapo chap, nikatafute chochote kitu."
Mtemi akaa kimya kwa sekunde tatu kisha akaangua kicheko.
"Kwa hio umeamua kuwa Sekido!" Akatamka Mtemi huku kicheko kikiendelea kumyumbisha.
(Sekido ni jina rejesta itumikayo katika jamii za wahaya, kumaanisha dereva pikipiki au bodaboda kama ilivyozoeleka na wengi)
"We leta hio kii, nikabebe wateja wawili watatu. Nipate chochote kitu." Feruzi akaendelea kusisitiza.
Ghafla simu yake ikaita tena, wote wakageuza shingo zao kutazama ni nani huyo aliyepiga.
Simu ikiwa juu ya shubaka, wakasoma jina 'Alinda'.
Wote wakatazamana na vicheko vikalipuka tena kutoka vinywani mwao.
"Unaona? Demu huyo hapo kanipigia tena, hii mara ya pili. Nilimuahidi afu tano tu ya kusuka ndo ananidai utadhani kanikopesha!" . Kwa utulivu Feruzi akajongea na kuikata simu ile, kisha akabonyeza kitufe chake kimojawapo ili aizime kabisa. Ikazimika!
"Khaa! Ndo unazima simu kabisa?" Mtemi akatoa kauli ya mshangao, bado yumo katika hali ya kicheko.
"Yaani mi sijui leo nitakula nini....halafu nimpatie demu hela ya kujiremba?! Au anadhani mi nitakula nywele zake." Akajibu Feruzi.
"Mademu zenu hao; mkiwa mnawaita gheto kuwakamia wakiwaomba hela msiwanyime! Hata hivyo ahadi ni deni."
"Eeh bwana ee...we nipe funguo nisepe bhana. Masuala ya mademu zetu tuachie sisi wenyewe!" Kwa kukasirika kidogo, Feruzi akadai funguo isiyokuwa yake ili mradi tu abadilishe mada.
Bila kusita Mtemi akachomoa funguo kutoka kwenye mkanda wa suruali lake na akampatia Feruzi huku tabasamu likiupamba uso wake.
"Kwani nina baya basi mzee? Chukua funguo hizi hapa. Sasa we kaendeshe kama unashindana na upepo, tutakuokota ukiwa mifupa!!"
"Aweee tulia bhana, fundi mimi. Haya mambo madogo madogo."
"Umezoea kushevu watu tu hapa...unapindisha mashine huku na huku, kazi simpo sana hizi. Nenda kafanye kazi za wanaume barabarani mdogo wangu!" Mtemi akatamba.
"Kazi simpo eh au sio? We nikikuacha hapa hata kwa masaa mawili tu. Utatoka umevimba mikono." Feruzi akamjibu huku akipokea ufunguo ule uliokuwa umeunganishwa barabara kwenye ringi ambayo ilikusanya jumla ya funguo nne, zilizoshindana kupiga kelele kila zilipogongana.
Feruzi akatoka nje akimuacha Mtemi ndani ya saluni.
"Kwa hiyo unarudi saa ngapi sasa?",.Mtemi akapaza sauti.
"Tulia bhana....sichelewi!" Akajibiwa.
"Angalia basi usinipaki humu ndani." Akapaza sauti yake tena akilalamika japo hakuwa na hasira.
Hakujibiwa!
Alichokisikia zaidi, ni muungurumo wa ghafla na mtetemo wa sauti ambavyo vilitosha kumjulisha kabisa kuwa pikipiki imewashwa. Halafu akasikia tena sauti ile ya mtetemo ikiishia, Feruzi aliondoka na pikipiki yake.
Akachungulia dirishani kumsindikiza kwa macho mpaka alipopotea kwenye upeo wa mwisho wa macho yake. Kisha akatabasamu!
Tabasamu lake daima liliupamba uso wake, lilikuwa tabasamu ambalo halikueleweka kama lilitafsiri furaha au huzuni moyoni mwake.
Akatoka dirishani, akaketi kwenye kiti kikubwa ambacho hukaliwa na wateja wanaponyolewa.
Akastarehe kwa kuegemeza mwili wake huku akijizungusha huku na huku. Macho yake yakilikagua dari la saluni ile.
Akawaza mambo mengi sana, kuhusu yeye na rafiki yake.
Alimuamini sana na rafiki yake,
Ni mambo mengi wamesaidiana na wameyafanya pamoja tangu walipokutana hapa mjini wote wakiwa katika utafutaji. Yeye akiwa kama dereva bodaboda na Feruzi akiwa kama kinyozi. Namna yao ya kukutana ilikuwa ya ajabu, ajabu sana!
Alipotaka kuikumbuka tu,
WAAH!
Mwanga mweupe wa taa kubwa ukammulika usoni mwake. Akafumba macho yake yaliyoumizwa na mwanga ule.
Umeme ulirudi!
Ghafla! Ndani ya sekunde chache tu, mziki mzito ukaanza kuunguruma ndani ya saluni ile.
"Aaargh, huyu naye alikuwa hajazima spika yake!" Akasimama kuelekea ilipo spika ili afanye alichotaka kufanya ambacho mimi na wewe hatukijui.
Labda alitaka kubadilisha mziki ule au kupunguza sauti au kuzima kabisa. Tumshangae tu!
Kabla hajamaliza hatua yake ya pili tu, saluni ikapata ugeni mpya. Watu wawili wakaingia wakihitaji kunyolewa. Mtemi hakupata nafasi ya kusema lolote la kuikana saluni hata kidogo, wakaongezeka watoto watatu walioonekana kuwa wa shule ya msingi .
Ikawa ni kama watu walikuwa karibu na saluni ile wakisubiri umeme useme wiiii na wao waitikie waaa, waingie ndani yake.
Tayari ulikuwa umesema wiiii na sasa wamo ndani.
Mtemi akakasirika lakini hakuwa na namna. Ilibidi amsaidie kazi rafiki yake ambaye kaenda kutafuta pia. Ilibidi wabadilishane kazi kwa muda kidogo.
Hakuwa mgeni katika kazi hii ya kunyoa watu, alikuwa na ujuzi kidogo wa kucheza na mashine ile ya kunyolea. Akavaa aproni akawasha mashine na kuanza kusuguasugua vichwa vya wateja kuondoa nywele zao.
Alikuwa na ujuzi japo hakuwa na uzoefu. Mkono ukaanza kumuuma akajizuia sana asitetemeke kuharibu vichwa vya wateja hasa wale walioonekana wanazijali sana nywele zao kuliko vichwa vyenyewe.
Kazi alioiita 'simpo' ikamfanya avuje jasho apate na mafua ambayo hakuwa nayo dakika kumi tu zilizopita.
--------------
Ni mwanzoni tu mwa riwaya yetu,
Ni nini kitajiri?!
Karibu katika sehemu ijayo.
Comments