MKUKUMKUKU,
aliivamia barabara akiendesha pikipiki yake kwa kasi sana.
Alivuta gia kwa fujo, akiiungurumisha pikipiki ile kwa mbwembwe, ili mradi tu kila mtu ajue kuwa anafahamu kuendesha pikipiki.
"Vijana wa siku hizi bhana! Hapo akisababisha ajali anayelaumiwa ni shetani. Utasikia mara ooh , shetani kanipitia!"
Mzee mmoja aliyekuwa anakunywa kahawa alitamka,
"Unadhani changamoto ni nini sasa pale kama sio bhange na mirungi?"
Mwingine akaongezea hoja yake. Wote wakimshuhudia Feruzi akiwa juu ya pikipiki, nusu ardhini nusu hewani...kwa kasi aliyochomoza nayo pale kando ya kijiwe cha kahawa.
Kwa upande wake yeye, ilikuwa ni kama faraja. Alikuwa na muda mrefu sana tangu ameendesha pikipiki, kwa maana hio alitaka afidie hamu yake.
Lakini utupu wa mifuko yake na njaa ya tumbo lake vikamkumbusha kuwa ana muda mchache sana wa kutafuta abiria.
Akasimamisha pikipiki yake kando kidogo ya barabara na akaangaza huku na huko.
Hakukuwa na dalili yoyote ile ya watembea kwa miguu.
"Aah huu mtaa jau sana, ngoja niingie hapo tauni kati. Hata hivyo hakuna nabii anayekubalika kwao."
Akaichochea tena pikipiki yake na kuendesha kuelekea mjini. Ambako alitarajia kupata abiria kwa urahisi kuliko mtaani kwake.
Akakata upepo kwa kasi kidogo kuelekea mjini. Na alipokuwa njiani kichwa chake kilikuwa bize kikikagua huku na huku.
Mara akamwona mwanamke mmoja kwa mbali aliyevaa mavazi mazuri na mkoba ukining'inia kwenye bega lake la kushoto. Mwendo wake ulionyesha wazi kuwa amechoka sana.
" Enhe kichwa hiki hapo ngoja nikakile!" Akaongeza kasi kuelekea kwa mwanamke yule mwenye umri wa makamo na alipomkaribia tu akapunguza kasi na kumpigia honi,
"Mamaah! Twendeeeee?!"
Mwanamke yule hakutoa jibu la moja kwa moja badala yake alisimama akaisogelea pikipiki na kuketi,
"Kashai matopeni!"
Feruzi akatabasamu na kuchochea tena pikipiki ile ya mkopo,
Akaanza tena kukata upepo kuutafuta mtaa huu wa Kashai matopeni. Tayari akili yake imeshapiga hesabu kali juu ya shilingi kadhaa ambazo angezipata kulingana na umbali ambao angemsafirisha abiria yule.
Dakika sita pekee zilitosha kumfikisha mtaani hapo.
Yule mama alishuka na kupekua mkoba wake taratibu kwa mkono wake wa kulia. Mkono wake ukaibuka na noti ya shilingi elfu moja. Akampatia Feruzi,
"Hii hapa nashukuru!"
Feruzi hakuamini alichokuwa amekipokea mkononi mwake. Mikono yake ilitetemeka kidogo.
"Eer mamaaa...samahani nadhaniii, umenipa pesa pungufu kidogo. Eeer ni buku jero mama, buku jero mpaka huku."
Akajaribu kutetea ujira wake.
Mama yule akapigwa na butwaa,
"Khee! Tangu lini tena...Yaani mpaka hapa elfu moja mia tano?"
"Eeh mama ni hiohio"
"Mmepandisha nauli kuanzia lini? Juzi tu hapa nimelipa elfu moja! Leo hii unaniambia ni elfu moja na mia tano?"
Feruzi akakumbwa na wasiwasi. Hakuwa akijua bei za nauli kwa maeneo mbalimbali, alikuwa akibahatisha tu. Na ili msala huu uishe kwa amani, akaamua kukubaliana na mama yule haraka sana maana hata wapita njia walikuwa wameanza kuvutiwa na maongezi yao.
Akawasha pikipiki yake na kuondoka!
Akaendelea kufanya msako wa abiria wengine...muda ukizidi kupotea, hakufanikiwa.
Abiria wengine aliokuwa akiwapigia honi kufahamu kama wanahitaji usafiri walimpungia mikono yao kuonesha kuwa hawahitaji usafiri. Na wengine hawakumjibu chochote, walimkalia kimya ,alishindwa kutafsiri kama ni dharau au hawako tayari kutumia usafiri wake.
Akazunguka mpaka akachoka, akatafuta kivuli akapaki pikipiki yake na kupumzika. Tumbo liliendelea kuunguruma kwa fujo likimdai chakula...akahisi ni kama utumbo wake ulikuwa ukitetemeka.
Akajipapasa mfukoni mwake na kuitazama noti yake ya shilingi elfu moja aliyokuwa ameipata baada ya kumsafirisha abiria mmoja tu.
Akakadiria bei za vyakula ambavyo angeweza kununua kwa fedha ile, akakunja sura yake baada ya kugundua kuwa fedha ile bado haitoshi.
"Mbona Mtemi aliwahi kusema kuwa yeye hawezi kukosa elfu kumi kwa siku? Hao abiria anawanunua au?", akajiuliza yeye mwenyewe.
"Yaani hadi sa hivi nina buku tu? Aah kudadek. Inabidi nikaze sana nipate angalau wawili wengine."
Akapanda tena pikipiki yake,
"Ngoja niende kule maeneo ya Tan-point, pale siwezi kukosa vichwa pale".
Akabadilisha uelekeo.
Akiwa njiani kwa mbalii akamuona mwanaume mfupi aliyekuwa katika mchakato wa kuvuka barabara.
Mwili wake ulifunikwa gubigubi kwa koti kubwa jeusi na kofia kichwani kwake ilipambana kuuficha uso wake. Haikuwa rahisi kuiona sura yake.
Mgongo wake ulibeba begi kubwa jeusi na mikono yake ilipakata mabegi makubwa ya wastani meusi pia, mabegi haya hayakuonekana kuwa na kitu chochote kile ndani yake.
Uso wake ulionyesha wasiwasi alipokuwa akikagua barabara huku na huko.
Haikujulikana kama ana haraka au ana hofu ya kupokonywa mabegi yake ambayo aliyashikilia barabara..
"Kichwa kile pale!"
Feruzi akakata kona kuelekea alipokuwa yule mwanaume mwenye mabegi.
Kwa mbaaali akamuona mwanaume mwingine amesimama kimya kaegemea mti. Lakini hakujishughulisha naye sana, akili yak
"Faza tuondokeee?! Hii hapa faza wapi hio?" Alianza kupaza sauti yake kabla hata hajamfikia.
Yule bwana akageuza shingo yake na kumtazama Feruzi kwa sekunde kadhaa, hakumjibu chochote.
Feruzi hakukata tamaa akaikokota pikipiki yake karibu zaidi,
Ikambidi atumie lugha ya kistaarabu labda angeushinda uamuzi wa huyu bwana.
"Baba yangu vipi nikupeleke?"
Bado bwana yule hakujibu kwa maneno, akatikisa kichwa chake kuashiria kwamba hakuitaji usafiri. Kimya! Na kwa utulivu mkubwa sana.
Akaendelea kutazama pande zote za barabara kwa hofu. Ilikuwa ni kama anasubiria usafiri wake binafsi ufike pale na kumchukua. Lakini jambo ambalo liliuvutia umakini wa Feruzi, ni ile wasiwasi yake usoni.
Na mbaya zaidi jasho lilianza kuulowanisha uso wake.
Feruzi, wakati huu akiwa amemkaribia kwa ukaribu zaidi. Akamtazama bwana yule vizuri.
Akawaza,
'Dah! Huyu faza, jamaa kavaa koti kubwa tena jeusi...halafu ana mabegi matatu meusi. Huyu anaenda wapi sa'hivi huyu?.
Lakini hawa nd'o huwa wana hela hawa. Em ngoja nimtongoze kwanza huyu dingi. Nalinusa buku tano hapa kabisa nje nje.'
"Baba yangu!",
Kwa upole na adabu zaidi Feruzi akajaribu kutumia maongezi yaliyotangaza heshima, huenda angeweza kumvutia huyu 'faza' awe abiria wake.
"Hapo ulipo nakuona kabisa umechoka baba yangu, au nakosea?"
Hakujibiwa. Lakini hata yeye hakusubiri jibu akaendelea,
"Una mizigo mingi mzee wangu, naomba basi kama hutojali. Nikusaidie tu kukufikisha huko unapoenda! Maana, sio jambo jema kwa mzee kama wewe kukosa usafiri na mimi nipo. Ni kweli natafuta, lakini kwako wewe ngoja nikufanyie kama msaada tu baba yangu!"
Bwana huyu mfupi alimsikiliza Feruzi kwa umakini sana. Kisha kwa taabu sana akajipekua kwenye mfuko wa suruali lake akipambana na ukinzani wa koti alilokuwa amevaa na mzigo wake mkononi.
Feruzi akanyoosha mkono wake kumpokea begi,
"Ngoja nikusaidie begi mzee wangu".
Kitendo cha mkono wa Feruzi kulifikia begi lile tu, kwa kasi ya ajabu mzee yule akapakata begi lake kwapani kwa nguvu zaidi. Hakutaka kupokelewa mzigo ule.
Jambo lililomshangaza Feruzi.
"Ni sawa tu baba yangu, kama hutotaka nikupokee." Akajitetea Feruzi huku moyoni mwake akiwaza
'Ina maana faza anadhani mi ni kibaka au?'.
Mkono wa mzee yule ukaibuka na simu ndogo kutoka mfukoni. Huku akitetemeka, akaibofyabofya kisha akaiweka sikioni mwake,
"Haloooo! Eeeh njalii njaa...njali a Bukoba." Akakaa kimya.
Mshtuko kwa Feruzi, hii lugha hakuielewa kabisa.
'Lugha gani tena hii?'
Mzee akaendelea, tena kwa wakati huu woga ulimuongezeka mara dufu zaidi. Jasho likimiminika kama maji usoni mwake, midomo ikimtetemeka. Na mkono ulioshikilia simu ukitetemeka pia.
"Jibooookaa! Jibooooka!.....Kyamuneeene...ano ano. Suruyuuuwe."
Akakata simu ile. Akaangalia kwa mara nyingine tena barabarani huku na kule. Kisha akamtazama Feruzi,
"Kyamunene!...Turatiaaa...Kyamunene!"
Akatamka huku amemtazama Feruzi.
Feruzi akiwa bado kwenye ganzi ya butwaa, alipatwa na kigugumizi kumjibu huyu bwana. Hakujua kama alitajiwa sehemu ya kumpeleka au alikuwa anafundishwa hii lugha asiyoifahamu.
Alichokifahamu pekee ni mahali hapo alipopataja huyu bwana, Kyamunene.
Lilikuwa ni eneo la kitalii lililokuwa ndani ya pori kubwa lililojulikana kama Rubare. Lilipambwa kwa maporomoko ya maji na mapango makubwa.
'Hili ni eneo la kitalii, huyu faza anaenda kufanya nini na mabegi yote haya?' Feruzi alijiuliza.
Lakini aliamua kutojisumbua baada ya kugundua kuwa yeye ni dereva pikipiki na hapa alikuwa na kazi moja tu, kubeba abiria.
Masuala ya kujua abiria huyu anafuata nini kule, hayakumuhusu.
Feruzi akubali kwa kutikisa kichwa pia na yeye akatamka,
"Kyamunene. Panda twende!" Akaongezea na ishara ya mkono kumuashiria yule bwana apande juu ya pikipiki yake, ameshatambua kuwa mtu anayezungumza naye haelewi Kiswahili.
Kwa haraka sana, huyu mwanaume akaruka juu ya pikipiki na kuketi. Bado ameyakumbata mabegi yake kwa nguvu.
Feruzi akawasha pikipiki yake na kuanza kuelekea huko inapopatikana misitu ya Kyamunene.
Njiani, hakukuwa na mazungumzo baina yao. Feruzi alikipa kichwa chake maswali kibao ambayo majibu yake yalichelewa sana.
Alishindwa kabisa kumuelewa huyu abiria ambaye amempandisha kwenye chombo chake.
Lugha yake, mavazi yake na hofu iliyokuwa imemvaa. Vyote vilimchanganya.
Hata huyu abiria huku nyuma alionekana kama anacheleweshwa kule anakoenda. Jasho jingi lilimvuja.
Safari yao iliyodumu kwa takribani dakika 7 kwenye barabarani ya lami, halafu ghafla huyu abiria akaanza kutoa maelekezo.
Kwa lugha yake ileile isoyoeleweka;
"Anuu anuu!"
Alitumia maneno na vitendo kwa mkono wake.
Uelekeo mpya ulikuwa tofauti! Haikuwa tena njia ya kuelekea Kyamunene.
Bila kuuliza swali, Feruzi akakunja kona na kuhamia kwenye barabara ya vumbi iliokuwa korofi kwa mwendo wao.
Wakaanza kuingia katika barabara yenye kona nyingi zilizofichwa kwa majani marefu na vichaka, halafu wakaingia ndani ya msitu na wakati huu wakaiacha barabara iliyoonekana kama ilikuwa ikikanyagwa na watu.
Feruzi akaanza kupatwa na wasiwasi.
'Huyu Bushman anataka kuniingiza wapi tena? Mbona ananipeleka ndichi? Au hawa ndo wale wanaoiba pikipiki nini? Huyu hanijui huyu...' akawaza.
Walikuwa wanaingia kwenye vichaka vikubwa na hakukuonekana kuwa na usalama katika sehemu walipokuwa wakielekea. Hakuweza kuuliza wanapoenda angeuliza nini sasa wakati mtu mwenyewe aliongea lugha asiyoifahamu,
Ni kikongo, kinaijeria, kiyoruba...hakujua! Kwa hio yeye alimchukulia kama mzigo ambao anaupeleka mahali maalumu kwa maelekezo maalumu.
Alichokiwaza pekee kwa wakati huu ni hela. Hela tu basi!
Wakaendelea kuingia kwenye vichaka,
"Jadhulaaa, anooo anoooo!"
Yule mtu akampigapiga begani kama kuashiria asimamishe pikipiki yake. Akasimama.
Yule bwana akashuka. Lakini kabla hajapekua mifuko ya suruali lake kutoa fedha ili amlipe, ghafla wakaibuka wanaume wawili kutoka vichakani ambao walikuwa wamevaa makoti makubwa meusi sawa na alivyokuwa amevaa yule mwanaume mfupi aliyeletwa na Feruzi.
Miili yao ilikuwa mikubwa. Mmoja akiwa amebeba koleo na panga kubwa lenye kutu. Na mwingine akiwa na shoka kubwa ambalo lilionyesha waziwazi kuwa linaweza kupasua kitu chochote kwa wakati wowote. Na wote miguuni mwao walivaa buti kubwa zilizochafuliwa kwa udongo mbichi wa mfinyazi, jambo lililowatambulisha kuwa walikuwa kazini!
Feruzi akawatazama usoni...nyuso zao hazikuonyesha dalili yoyote ile kuwa ziliwahi hata kufikiria kutabasamu tangu wazaliwe. Jambo lililowafanya waonekane kama majitu ya kutisha!
Mmoja wa majitu yale ya kutisha akasogea haraka mpaka alipokuwa yule mwanaume aliyeletwa pale na Feruzi ambaye naye alionekana kuwa haelewi ni kitu gani kinaendelea. Likatupa panga lake lenye kutu chini.
"Unuyuuu? Ambi likijaaa mbanuu? Enhe?!!!" Likamuuliza huku limemnyooshea kidole Feruzi.
Liliongea kwa sauti nzito na hasira huku ndevu zake nyingi mithili ya 'steelwire' zikipanda na kushuka kadri alivyotamka kwa sauti ile ya kutisha.
'Eboo?! Kumbe wanafahamiana hawa?' Feruzi akazidi kustaajabu.
Yule abiria akashusha mabegi yake chini, yungali anatetemeka...anaonekana anataka kujibu swali lile japo kigugumizi na woga vinamzuia.
Kofi kali likatua juu ya uso wake, likamfanya apepesuke kutafuta mhimili ili arejee kusimama wima tena.
"Ambiii likija mbanuu? Ambiiii?!!" Lile jitu likaendelea kumuuliza kwa hasira huku likilalamika. Bado mkono umenyoosha kidole chake kwa Feruzi. Feruzi amebaki akitazama tu huku mapigo ya moyo wake yakibadilisha kasi, yakaamua yaanze kwenda mbio. Ameshagundua kuwa yuko sehemu ambayo hakuitajika!
Ghafla! Jitu lilitumia sekunde mbili tu kumchota yule mwanaume kwa mtama mkali, ambao ulimuacha hewani kwa nusu sekunde na kabla hajatua ardhini akapigwa ngumi kali ya kifua.
Ngumi ambayo kama haikuuhamisha moyo kutoka sehemu yake basi ilinuia kumpasua kifua chake.
"Aaargh!" Akapiga kelele na kutua chini PUUH! Kama mzigo.
Akalala chali chini huku akiunguruma taratibu. Amekufa kwa kupasuka kifua? Amezirai? Hata hatujui.
Halafu jitu lile likamgeukia Feruzi ambaye alikuwa bado juu ya pikipiki akisubiria malipo yake.
Ndugu msomaji,
Hebu mshauri Feruzi afanye nini baada ya kuona madhara yaliyomkuta abiria wake. Aendelee kusubiri nauli yake? Au arudi tu town aendelee kusaka wateja? Tumshauri ndugu yetu Feruzi Kinyozi.
Unaweza kukisia hofu ambayo Feruzi alikuwa kwa wakati huo. Kipigo alichopokea abiria wake, kikamuacha na maswali mengi zaidi ya kumuogofya!
Feruzi akawaza mambo mengi sana, akilini.
'Hawa ni majambazi wanaofahamiana au ni kina nani hawa?'
Hata mwili wake ukashtuka, ikawa ni kama vipepeo vinarukaruka tumboni, koo likakauka na miguu ikamuishia nguvu.
Kama yule wanayefahamiana naye wamemfanya vile, itakuwaje kwake yeye wasiyemfahamu?
Lile Jitu likaokota panga na likamsogelea Feruzi huku pumzi zikipishana kwa nguvu kwenye pua zake kwa hasira. Na macho yake yakageuka kuwa kama ya mnyama wa kutisha kuashiria kuwa linaenda kumtenganisha vipandevipande.
Ni msituni! Apige kelele kwa nani kuuita msaada? Labda wewe msomaji unayemuona kwa fikra zako. Pengine atauawa na haya majitu na hatojulikana ni wapi alipo. Hakuna namna ambayo angalau vipande vyake vitaokotwa na kuzikwa.
Alikiona kifo na hakuwa na namna ya kujitetea!
-------------
Naam,
Mapema kabisa...Feruzi amekosea kona tayari. Ni nini watakachokifanya hawa majitu wa kutisha?
Haya yote tumuachie Godlove Kabati katika sehemu ijayo.
Comments