MWILI wake ulizizima!
Ardhi iliitikia kwa kutoa mtetemo kwa kila hatua ambayo jitu lile lilikanyaga juu yake. Ilikuwa ni kama inalalamika juu ya uzito wa mwili wake yule bwana.
Mkono wake wa kuume uliobeba lile panga kubwa lenye kutu ulikuwa imara, na tambo la mwili wake lilikuwa la kutisha sana.
Feruzi alikosa cha kufanya. Cha maana zaidi alichokifanya ni kuzima pikipiki yake na kusubiri kuona yule bwana amenuia kumfanya nini. Asingeweza kujitetea kwa lolote dhidi ya majitu haya mawili yanayotisha tena katikati kwenye pori hili kubwa.
Akiwa anatetemeka akajikuta anapambana sana kuuzuia mkojo wake lakini hata mfumo wa utoaji taka mwili nao haukumuacha salama! Akajikojolea..
"Shikaa..shikamooo!", akajikuta akitoa salamu ya kwanza tangu afike katika eneo hili ambalo kwa sasa lilimuonesha waziwazi kuwa ni ardhi ambayo atazikwa.
Lile jitu likamkaribia zaidi...
"Marahaba!". Likaijibu salamu kwa maneno kisha likafuatisha kwa vitendo huku likiutumia mkono wake wa kushoto kuushika ukosi wa koti la Feruzi na kuubana kiasi kwamba shingo yake nayo ikahusika kwenye mbano huu.
Kwa kutumia nguvu kiasi likamnyanyua juu na kumuondoa kwenye pikipiki yake kisha likamtupa ardhini huku pikipiki nayo ikianguka.
Yule mtu mkubwa aliyefanania na jitu akamtazama Feruzi pale chini huku akihema kwa hasira...macho yake yakimpa maswali magumu Feruzi ambayo asingeweza kuyajibu.
"Wewe ni nani? Na umefuata nini huku?!" Likamuuliza.
"Mi...mimi ni bodaboda tu mkuu, nime...nimeml..nimemleta abiria yule pale...!"
Feruzi akajibu kwa sauti iliyochanganyikana na kigugumizi, hofu na vikohozi vya nukta. Akitarajia kuwa huenda ataonekana kuwa hausiki na ataachiwa huru aende zake.
Lile jitu likageuza kichwa na kumtazama mwenzake ambaye alikuwa kimya akiwatazama tu, kisha likamrudia tena Feruzi ambaye alikuwa akitetemeka kwa woga pale chini.
Likabonyea chini na kupiga goti moja, kisha likaikita ncha ya panga lake ardhini na panga likanata kwa kutulia. Ukimya wa kutisha ukatawala!
Kwa kuliegemea kidogo panga lile likamkaribia Feruzi na kumuuliza,
"Una muda gani kwenye tasnia ya maigizo?"
Sauti yake haikuwa na dalili yoyote ya utani au kicheko...alikuwa makini na alimaanisha alichokizungumza. Lakini kauli hii iliwasha taa ya hatari kwa Feruzi, kuwa haaminiki.
"Hapana bro! Hapana mimi siigizi kweli kabisa...nime...nime nimemleta baba yule pale..kanambia nimelete huku misitu ya Kyamunene... sa'nd'o njiani akanielekeza mpaka hapa!" Feruzi akajitetea kwa sauti yenye machozi, kisha akaendelea.
"Tafadhali msiniue...naomba sana mkuu, mimi..mimi sina lengo baya sijui chochote..ni bodaboda tu.."
"Ni nani amekuambia anataka kukuua?" Jitu likamtupia swali.
Feruzi akatoa macho, hakuwa na jibu. Akashuhudia jitu lile likichomoa panga lile kutoka ardhini na kulinyoosha kwa Feruzi.
"Tungetaka kukuua tungekuwa tumeshafanya hivyo mapema sana...sekunde kumi zilizopita."
Likaweka kituo na kumtazama Feruzi.
Ukimya huu ukawa ni kama muendelezo wa hofu tu kwa Feruzi, kisha likaendelea,
"Lakini hilo halimaanishi kwamba hatutakuchinja hapana...tutakuua dakika chache tu zijazo, endapo tunachokifikiria juu yako kitakuwa kweli!". Likakaa kimya tena.
Ukimya huu ukawa ni kama umempasia kipaza yule mwenzie aliyekuwa amesimama kando. Yeye akakohoa kidogo kisha akasema,
"Tumekusikia ukimshawishi huyu mzee kwa nguvu sana, na ukambeba mpaka hapa!
Haya sasa tuambie haraka wewe ni nani? Na ni nani amekutuma!"
Sauti zao nzito na za kutisha zilifanana, na zote mbili hazikuwa na masihara kabisa. Feruzi akawa mdogo, akanywea na kuwa mpole. Akatambua kuwa yuko katikati ya wauaji. Madirisha ya macho yake yakafunguka na mifereji ya machozi ikaanza kumtiririka.
Taratibu akapiga magoti kwa unyonge, akaifumbata mikono yake kama mtu anayejiandaa kusali kisha akatamka,
"Jamani...mimi sihusiki kwa lolote. Mimi ni bodaboda wa kawaida kabisa! Sekido masikini kabisa. Niacheni tu niende. Nihurumieni jamani!"
Watu wale wawili bado wako kimya...sura zao komavu ziliendelea kumtazama tu na angalau basi zingempa matumaini kuwa ataonewa huruma, lakini zikamkatisha tamaa.
Hazikuonyesha kuwa zina tabia ya kuvaa vazi lolote lile lililoshonwa kwa nyuzi za huruma wala msamaha.
Kwanza sura zao zilikuwa na makovu, ambayo yalionyesha kuwa hata wao dunia haijawahi kuwahurumia. Sasa ni huruma gani aliitaka Feruzi?
"Yaani tumekusikia unamwambia mzee wetu kuwaa..unataka kumfanyia hisani ya bure tu...umelete hapa bure! Halafu unasema we ni bodaboda masikini? Umasikini gani huo ambao unakupa utu wa kuwapa lifti abiria usiowafahamu na kuwasafirisha maili nyingi, mpaka huku kwenye mapori ya kutisha! Mmh? Nijibu..."
Ndugu msomaji, kama umewahi kupatwa na msisimko wa ghafla ambao ulikudai maji ili kupoza koo lako, basi mfikirie ndugu yetu Feruzi kidogo.
Alibaa!
Koo likamkauka! Akashindwa kujibu chochote kile.
"Halafu ulivyo fala! Njiani ukawa unasema etii...huyu faza hanijui! Ngoja nitamuonyesha! Haya ulitaka kumwonyesha nini huyu mzee? Eeh tuambie...ulitaka kumwonyesha nini?
Au ni kwa vile haelewi Kiswahili...ukaona unaweza kutumia fursa? Eeh?"
Akazidi kupangiliwa orodha ya maswali ambayo yalimuwia magumu mno kujibu.
Swali moja tu lililokuwa kichwani mwake,
'Wamejuaje hawa?'
Kwa mara ya kwanza maishani mwake, Feruzi akakubaliana na ule msemo unaosema
"MDOMO ULIKIPONZA KICHWA!"
Angejibu nini?
Lile jitu lililokuwa karibu yake likashusha pumzi. Kisha likamtazama mwenzie,
"Nadhani tumpeleke kwa mkuu yeye atajua tumfanye nini."
Yule mwingine akatikisa kichwa kukubali.
"Haya simama!" Hii ilikuwa amri ambayo kabla hata haijamalizika tayari Feruzi alikuwa kasimama haraka.
Bwana yule akatoa kamba kubwa na kuifunga barabara mikono ya Feruzi. Kisha akachukua mfuko mkubwa mweusi akamvalisha Feruzi kichwani, asione anakokwenda.
Yule mwingine akajipa jukumu la kujitwika mwili wa yule mzee aliyekuwa amezimia. Wote wakashika ujia mdogo ulioingia katikati ya pori lile. Feruzi akiongozwa njia kwa kuburuzwa na kupigwa na ubapa wa panga ili asipoteze muda.
Mwendo wa mateka!
**********
Ulikuwa mwendo wa dakika ishirini za kujikwaa kwenye visiki, kuanguka na kuamka, kupigwa makofi mazito ya mgongo na kusukumwa ili mradi tu Feruzi aongeze mwendo.
Hatimaye wakafika sehemu ambayo aliambiwa asimame. Akasimama na ule mfuko mweusi ukatolewa kichwani mwake haraka...
Mwanga ukayaumiza macho yake yaliyokuwa yamelizoea giza kwa dakika zote hizo, akayafumba ili kupunguza maumivu yale.
"Kaa chini!"
Akapewa amri ambayo ilisindikizwa kwa kofi zito lililotua juu ya mgongo wake, likamkohoza kidogo. Akakaa chini bado mikono yake imefungwa kwa nyuma.
Macho yake yalipouzoea mwanga kidogo, akajaribu kuitazama sehemu ile kwa umakini. Macho hayakumfanyia ajizi, yakamtaarifu kuwa yuko katikati ya msitu mkubwa asioufahamu na yuko na watekaji ambao wanaweza kuiondoa roho yake mara moja kama tu watataka kufanya hivyo. Akaogopa!
Lakini macho yake yakavutiwa sana na mandhari ya eneo lile alipokuwepo. Ndio, ni kweli alikuwa katikati ya msitu! Lakini hapa palikuwa pa kitofauti kidogo.
Lilikuwa eneo kubwa lililo wazi limezungukwa na miti mikubwa, kiasi cha kutengeneza kiwanja kikubwa cha kadri chenye umbo la duara mahali pale.
Ardhi ya eneo hilo ilikuwa imetifuliwatifuliwa na ilionesha kuwa ni aidha imetoka kuchimbwa mda sio mrefu au imeshazoea kuchimbwa na kutifuliwatifuliwa mara kwa mara.
'Mungu wangu! Hawa majambazi wataniua halafu watanizika hapa!!' Mawazo ya hofu yakamkumbusha hatari iliyokuwa mbele yake. Alipotazama vizuri mbele yake akakutana na kiwiliwili cha mtu ambaye alikuwa amesimama na ameweka mikono yake nyuma, akajitahidi kumtazama.
"Unaitwa nani wewe? Na ni kwa nini unatufatilia?!". Sauti tulivu ya mamlaka ikasikika kutoka kwenye kiwiliwili kile. Hii ilikuwa sauti ngeni kabisa, masikio yake hayakuwa yamewahi kuisikia.
Mwanaume mtanashati, aliyevaa suti nzuri nyeusi ya gharama. Miwani nyeusi ikiyaficha macho usoni mwake, alikuwa amesimama mbele yake. Ni mtulivu na mikono yake akiwa ameifumbata nyuma, ni kama ambaye alikuwa ameficha kitu.
"Shika-shikamoo! Mimi ni bodaboda wa kawaida jamani, kiongozi naomba mniache tafadhali! Niache niende tu. Sihusiki kwa lolote." Feruzi akaendelea kutamka sentensi zilezile zenye kilio. Tena kwa wakati huu alipomuona huyu bwana mtanashati akategemea labda huyu atamuhurumia kuliko yale majitu ya kutisha yenye miili mikubwa.
Yule bwana akakohoa kidogo kisha akatamka,
"Unaitwa nani? Na ni kwa nini unatufatilia!" Sauti yake ni tulivu sana, anaongea kwa mamlaka na inaonesha kuwa yeye sio muumini wa maongezi marefu yasiyo na mantiki.
Kwa kigugumizi kilichochanganyikana na hofu Feruzi akajibu,
"Fe-Feruzi anko!...Naitwa Feruzi! Mimi ni kinyozi kuleeee Buyekera kulee" akataja jina lake, akataja na wadhifa wake kwenye jamii. Bado anatafuta kubonyeza kitufe cha huruma kwenye moyo wa huyu bwana ambaye hivi sasa angemuita mtekaji-mtanashati.
Sekunde mbili tu baada ya kumaliza sentensi yake, akashuhudia jitu mojawapo limemrukia, likashusha kofi zito usoni mwake ambalo lilimfanya apepesuke na kuona nyota zenye rangi tofauti tofauti.
"Kwani we ni mbwa?! Eeh? We una jina moja umekuwa mbwa?"
Jitu lile likabweka kwa hasira, mzuzu wa ndevu zake chafu ukicheza huku na huko.
Hakupata majibu ya moja kwa moja, bado Feruzi alikuwa anajiuliza kama amepigwa na kofi, radi au shoti ya umeme.
Hakujielewa!
"Dubu!! Muache....achana naye" yule bwana akaliamuru lile jitu liachane na Feruzi. Likatii likiwa bado linahema kwa hasira, macho yamelitoka. Linaonyesha waziwazi kuwa limezoea shari...na anayefanyiwa shari yupo hapa.
"Naitwa Adam Feruzi Adam." Feruzi akajibu kwa sauti chovu, bado akili yake haijakaa sawa, baada ya kupokea banzi zito kutoka kwenye kiganja cha lile jitu, lililojulikana kama Dubu.
Yule bwana akaondoa mikono yake nyuma, alikuwa ameshika fimbo ndefu ya kutembelea, akapiga hatua kwa taabu kuelekea kwa Feruzi huku akichechemea. Ni fimbo ile iliyompa mhimili. Feruzi akaendelea kumtazama tu, akili yake ikamkumbusha zile filamu za vikundi vya magaidi na wauaji. Na wale mafia aliowahi kuwasikia kwenye simulizi na filamu mbalimbali.
Yule bwana akachuchumaa kwa msaada wa fimbo yake akamtazama Feruzi akashusha pumzi kisha akatamka,
"Kazi yako wewe ni ipi? Dereva bodaboda au kinyozi?"...sauti yake ikaanza kubadilika kutoka kwenye utulivu ikaanza kunukia hasira na jaziba.
Lakini hayo hayakumfikirisha Feruzi hata kidogo, alichokifikira muda huu ni kosa lake jingine la kuchanganya majibu yake yeye mwenyewe,
Kawaambia ni dereva bodaboda halafu tena kajitambulisha kama kinyozi. Kafanya makosa mbele ya watu wabaya! Akajua kuwa kwa namna yoyote ile hawawezi kumuacha.
Machozi yaliyokuwa yamemkauka yakachukua nafasi yake tena, akarejea tena kwenye kitendo cha kulia.
"Miongoni mwa vitu ambavyo navichukia sana ni kuona machozi ya kinafiki! Tena kwa dume kama wewe uliyekomaa." Kauli hii ikakiyeyusha kilio cha Feruzi, kikapotea na sura yake ikavaa ukimya. Ukimya uliopambwa kwa wasiwasi.
"Mkuu, mimi ni kinyozi pale mtaani kwetu. Lakini nimeazima pikipiki ya rafiki yangu ili nipate walau hela kidogo mkuu! Hivyo tu."
Yule bwana akainamisha kichwa chake kwa huzuni kisha akasema,
"Hela! Unatafuta hela! Ooh Adam. Hela! Hela! Hela!" Akatoa miwani yake usoni kisha akamtazama tena Feruzi.
Uso wake haukuwa wa kawaida, ulitisha!
Alikuwa chongo, kovu kubwa lilipita katikati ya jicho lake la kulia na kuliharibu vibaya sana, lilikuwa ni kama linalotoa machozi muda wote. Uso wake pia ulionesha kuwa hata yeye amepitia mateso na adha mbalimbali katika maisha. Jambo lililozidi kumkatisha tamaa Feruzi kuwa asitegemee aina yoyote ile ya msamaha jioni hii ya leo.
Yule bwana akatazama ardhini na kuanza kutamka peke yake,
"Tulikukosea nini fedha?! Ni kwa nini unatutesa namna hii? Watu wanakutafuta kila kukicha na bado unaishia kuwaingiza shimoni. Kwa nini lakini? Hela! "
Akakaa kimya kisha akatoa leso kwenye mfuko wa koti lake na kulifuta chozi kwenye jicho lake lenye chongo.
Kisha akamtazama tena Feruzi kwa sura yenye udadisi.
Feruzi mwenyewe, bado haelewi ni kwa nini bwana huyu anailaumu fedha ambayo hata haioni na hata haiwezi kumsikia.
"Adam Feruzi Adam! Jina zuri sana... wewe ni kijana mwema sana, nadhani hata kama nikikuua, mbingu zitafurahi sana kukupokea. Eti Adam au nakosea?"
Maneno 'hata kama nikikuua, mbingu zitafurahi sana kukupokea' yakamtisha sana Feruzi. Akajua kuwa sasa hana muda mwingi sana pale porini atakufa!
"Si huwa mnasema kuwa Mungu amempenda zaidi marehemu? Sasa kama Mungu anakupenda unafanya nini hapa duniani. Dunia mbaya ambayo imechafuliwa kwa shetani anayeitwa fedha! Hela!" Yule bwana akazidi kutamka kwa sauti tulivu lakini iliyotangaza hasira.
Feruzi bado yupo kwenye mshangao, hakujua kama hawa viumbe watatu waliomzunguka wana akili timamu au la! Alianza kumvua vyeo vya heshima huyu bwana mwenye suti, maana aliyoyaongea na muonekano wake havikufanana hata kidogo.
Ni mtu gani ambaye anaweza kuilaumu hela? Tena kama vile anaongea nayo tu uso kwa uso. Feruzi akajihakikishia kuwa hakika huyu bwana ni punguani.
"Lakini wewe leo umekosea njia Adam Feruzi, umekosea njia mdogo wangu. Na wala sikulaumu kwa hilo! Lakini huyo jamaa mrugaruga nd'o amekupoteza njia." Akamnyooshea kidole yule bwana mfupi, abiria aliyeletwa pale porini. Alikuwa ameamka tayari japo anaonekana amedhoofu kutokana na pigo kali alilopokea nusu saa tu iliopita. Mtekaji-mtanashati akaendelea,
"Najua kuwa huoni kama utaokoka leo, na ni kweli hutaokoka. Hii siku itayabadilisha maisha yako Adam. Unatafuta hela?!
Hujui kuwa hela inasababisha kifo? Eeh...hujui Adam? Hela inaua.." Akamuuliza.
Sasa Feruzi akapigia mstari imani yake juu ya kifo chake, akaona ni kama wanampa nafasi ya kutoa neno lake la mwisho kabla ya mauti.
"Makusudio yangu juu yako yamekuwa tofauti. Lakini ngoja nikupe darasa kidogo Adam, em tazama hela inavyoweza kuua. Em tazama, tazama ninachokifanya!"
Akasimama kwa taabu akijitahidi kujiegemeza kwa ile fimbo yake...
Fimbo ambayo ilikuwa na sanamu la kichwa cha simba kwenye mshikio wake, ishara nyingine ya kuwa huyu bwana sio mtu wa kawaida!
Kisha taratibu huku akichechemea, akamsogelea mwanaume yule pale chini aliyekuwa anamtazama kwa macho yanayodai huruma.
Yule bwana mwenye suti akamtamkia maneno fulani ya lugha ileile ambayo ilikuwa ya kikabila. Lugha ambayo inaonekana wanaifahamu wao tu, isipokuwa Feruzi.
Yule bwana akamjibu kwa lugha ile ile, machozi yakiulowanisha uso wake. Yule mtekaji-mtanashati akanyanyua fimbo yake na kuivuta kama anaifuta, akachomoa upanga uliokuwa ndani ya fimbo ile halafu bila kusita kama utani tu,
akauvurumisha upanga ule hewani kama mtu anayejiandaa kufyeka kitu. Kisha akaushusha chini kwa nguvu juu ya kichwa cha yule bwana abiria. Kufumba na kufumbua, damu ziliruka hewani kama maji ya bomba lililopasuliwa.
Kiwiliwili cha kikadondoka upande wa kulia na kichwa kikadondoka upande mwingine. Lilikuwa tukio lililochukua sekunde tatu tu. Yule abiria aliyeletwa pale akawa tayari amekuwa historia!
Akauawa kwa upanga. Ilikuwa kama utani tu!
Feruzi anashuhudia kwa mauaji mubashara kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake.
Mauaji ambayo alizoea kuyaona kwenye filamu tu. Lakini leo hii akayaona kwa macho yake ya nyama.
-----------
Itaendelea...
Comments