Reader Settings

 

FERUZI alikuwa ametazama filamu nyingi sana tena za kutisha, alisoma simulizi nyingi sana za kuogofya. Tayari alizoea kushabikia mauaji kwenye filamu hizo na kuchagua upande kati ya muuaji au muuliwa.

Lakini leo hii alikuwa akiyashuhudia mauaji mubashara, kwa macho yake ya nyama.

Punde baada ya kutimiza unyama wake, yule bwana mtanashati mwenye suti akatoa leso nyeupe kutoka mfukoni mwake akaikung'uta na kuanza kupangusa upanga ule mrefu uliokuwa umechafuka kwa damu. Kisha akaurudisha vyema ndani ya fimbo ile.

Ulikuwa upanga mwembamba sana, lakini uwezo wake wa kupasua shingo ya mwanadamu kwa pigo moja tu tena kwa kipimo cha sekunde mbili tu ndio ulimuacha Feruzi kinywa wazi. Alishangaa!

Katika mazingira haya ya kutisha. Msitu ukatulia ukawa kimya! Kimya cha kutisha chenye mshindo mkuu! Ilikuwa ni kama hata viumbe hai vilikuwa macho kuusikitikia mwili ule ulionyofolewa kichwa chake bila hata kupewa walau nafasi ya kusema neno lolote lile.

"Atakuwa hajaacha wosia huyu mzee!" Ndege mmoja akamnong'oneza mwenzake juu ya tawi la mti.

"Dah! Sahau kuhusu wosia, huyu inaonekana alikuwa na miradi yake ya mashamba huko kijijini huyu. Sa sijui kamuachia nani amlimie!"

Akamjibu ndege mwenzie.

"Tatizo lako we unawaza kula tu." Akapaa na kuondoka zake.

Ukimya ukaendelea kutawala mahala pale.

"Adam Feruzi Adam!", yule bwana akapaza sauti yake na kulipasua anga lile la ukimya uliokuwa umetishia amani.

Haikujulikana kama anamuita Feruzi au analitaja tu jina lake.

Naye Feruzi akabaki kwenye duara lake lilelile la mshangao, hakuitikia.

"Umewahi kushuhudia kiumbe hai anachinjwa?" Mara hii hili swali likamhusu alijibu.

"Ha...hapana mkuu, sijawahi!" Akajibu kwa woga Feruzi.

"Ooh sawa...hamna shida Adam, hamna shida" akawageukia wale watu wawili wenye miili ya kutisha akawaambia,

"Duba, Dubu! Rafiki yetu hapa hajawahi kuona mtu anachinjwa...nadhani mkaishughulikie hii maiti mbali! Rafiki yetu asije akatuchukia bure!"

Kisha akamgeukia Feruzi pale chini.

"Eti si tutakukwaza kama tukimchinjia hapahapa, uwongo?" Kamtazama huku amebetua ndita zake usoni, kama anayeuliza kitu cha maana. Bado miwani nyeusi imeyaficha macho yake mabaya.

Feruzi ambaye bado ni mateka, amekaa kitako akashindwa kujibu swali hili. Badala yake mzigo mzito uliokuwa moyoni mwake ukamzidia nguvu akashindwa kuvumilia, akarudia tena kwenye ileile hali yake ya mwanzo, kilio!

"Mnaona! Tunamfanya mpaka analia! Haya haya jamani haraka, mtoeni hapa huyu maiti. Kamshughulikieni hukooo." Akatoa amri.

Yale majitu mawili yenye miili mikubwa ambayo sasa ilijulikana na Feruzi kwa majina kama Dubu na Duba, yakafanya himahima na kuondoa kiwiliwili kile pale na kwa maelekezo waliyopewa wakaacha kichwa chake mahali pale.

Feruzi akakitazama, macho yake yalikuwa ni kama yanamuuliza,

"Ni kwa nini umenileta huku?". Na yeye ikawa ni kama anakijibu kimoyomoyo,

"Ni kwa nini umeniagiza nikulete huku?"

Ghafla akashtushwa na umbo la mwanaume aliyekuwa kachuchumaa mbele yake. Ni yuleyule bwana mwenye suti. Akaondoa miwani yake na lile jicho lake bovu la kulia likaonekana tena. Lilikuwa linavuja chozi ambalo liliteleza taratibu kutoka jichoni mpaka kwenye kovu lile lililolijeruhi vibaya jicho hili. 

Huyu bwana akatumia leso ileile yenye damu kulifuta chozi lile. Halafu akakunja kitambaa chake na kukirudisha tena kwenye mfuko wa koti lake. Halafu akamtazama Feruzi usoni!

Huyu hapa, uso kwa uso na Feruzi na safari hii hakuivaa miwani yake nyeusi.

Ni heri basi angeivaa maana sura yake na mambo ya ajabu aliyokuwa akiyafanya vilikuwa ni kama muendelezo wa kumtisha Feruzi. 

"Adam Feruzi Adam, unaweza kuniambia ni kwa nini unatafuta hela?!", lilikuwa ni swali jingine baridi kutoka kinywani mwake kwenda kwa Feruzi.

"Eer..ndi..ndio mkuu. Maisha ni magumu, maisha tu bro! Ili niishi vizuri tu kaka, hivyo tu!"

Feruzi akajibu huku anajitahidi kuvuta kamasi zilizokuwa puani mwake, bado machozi yanamtiririka machoni.

Yule bwana akamtazama tu halafu akamjibu,

"Mara ya kwanza nilikueleza kuwa sipendi kuona machozi kutoka kwenye macho ya mwanaume!".

Feruzi akapambana kujizuia kulia akataka kuyafuta machozi kwa mkono wake lakini hakuweza, amefungwa mikono yake kwa nyuma.

Yule bwana akachomoa kisu kidogo kwenye koti la suti yake, akanyoosha mikono yake na kukata kamba zile, kisha akarudisha kisu kile taratibu kwenye koti lake.

Feruzi akapata walau uhuru wa kunyoosha viungo vyake na kusikilizia maumivu yake.

"Aliyekwambia hela inaweza kukufanya uishi vizuri ni nani? Eeh? niambie mdogo wangu? Ni nani huyo mchawi?" Sauti yake imebadilika na anaonekana mwenye jaziba.

Kutokana na jaziba yake, chozi jingine likachuruzika kutoka kwenye jicho lake na kama kawaida yake akalifuta kwa leso ileile yenye damu.

"Nisikilize mdogo wangu! Hela ni kama zawadi tuliyopewa halafu ikageuka kuwa laana. Inatutesa sana hii laana! Inatuteketeza ni kama sumu ambayo inatuua. Acha kujidanganya kuwa hela itakufanya uishi vizuri acha mara moja!" Akazidi kutamka kwa jaziba japo sauti yake ni ya chini. 

"Umesema kuwa hujawahi kushuhudia kiumbe anachinjwa? Ni kweli..kwa maana hio hujawahi kuchinja wewe?" Akamuuliza.

"Hapana mkuu...nimewahi labda kuchinja kuku, bata na mbuzi." Feruzi akajibu kwa utulivu. Halii tena japo sauti yake bado imejaa woga.

Kofi kali ambalo hakulitegemea likatua nyuma ya shingo yake, likamfanya ajikune.

"Simaanishi vitoweo dogo! Namaanisha watu!" Yule bwana akabweka kwa hasira. Lakini mara hii hali yake ikabadilika ghafla.

Ikawa ni kama anayesononeka akitaka kulia.

Mara hii jicho lake la kushoto likatoa chozi la kawaida lakini lile bovu la kulia likatoa chozi lililochanganyikana na damu!

Na yeye kama kawaida, akatoa leso yake ileile na kuyafuta machozi yake kutoka kwenye macho yote mawili.

"Nisamehe sana Adam Feruzi, nimekupapasa kwa kiganja changu. Japo mpapaso huo ni wa kawaida sana. Nataka nikuambie nini, em sikiliza. Sogea karibu!" Akaamrisha tena.

Feruzi akajiburuta pale mavumbini na kumsogelea kwa ukaribu zaidi,

"Kuna watu ambao wanachinja watu ili kupata hela! Halafu wanawachinja kama michezo ya kufurahisha. Yaani wanafanya michezo ya maonyesho ili tu wapate hela. Halafu nyie mnalipia hela nyingi kuwatazama huko kwenye mitandao yao!" Akaweka pumziko kisha akaendelea,

"Yaani unakuta mtu ameandaa jukwaa lake kubwa! Ameteka watu halafu anawaambia watazamaji wachague amuue yule mtu kwa mtindo gani, watu wanachagua. Halafu anamkatakata yule mtu kama hao kuku wako unavyowafanya Adam! Em fikiria. Hahahaha!", akacheka.

Feruzi naye akiwa bado haelewi nini afanye, naye akajikuta akimuunga mkono kwenye kicheko kile, na yeye akacheka kicheko cha kuigiza. Lakini ghafla yule mtu akabadilika tena,

"Kwa nini unacheka Adam Feruzi Adam!".

Kimya! Feruzi akashangaa sana, yaani ni mtu huyuhuyu alikuwa akiongea naye kwa urafiki tu sekunde kadhaa zilizopita. Halafu safari hii amebadilika tena.

"Yaani vitendo vya kutisha ninavyokuelezea wewe vinakuchekesha? Unajua mara ya mwisho mtu aliyecheka na mimi nilimfanya nini?"

Feruzi akatikisa kichwa kujibu kuwa hafahamu lolote lile.

"Nd'o yule abiria uliyemleta wewe sasa hivi. Nadhani amewahi kuzimu kukuwahia nafasi mtu kama wewe ambaye huna huruma na wanadamu wenzako!" Akamjibu. Akameza funda la mate kisha akaendelea,

"Hivi unadhani mtu kama yule ataenda mbinguni kweli? Hapana sidhani. Maana watu wote ninaofahamiana nao ni waovu mno! Ni wa kuchomwa moto tu yule!".

Feruzi akashindwa kukaa kimya, akavaa ujasiri na kumuuliza,

"Kwani amefanya nini yule mzee mpaka umuue kikatili namna ile?".

Yule bwana akapiga makofi matatu na kutabasamu kwa mara ya kwanza. Tabasamu lake lilipambwa kwa meno meupe angavu.

"Hapo nd'o nilitaka uniulize sasa...ili nikujibu majibu ambayo hutakiwi kuyasikia." Akaweka pumziko huku akimtazama kisha akaendelea,

"Leo ulimbeba mtu muovu sana mdogo wangu! Na wewe licha ya kutafuta hela kwenye njia zako za halali ukaacha kuzingatia hatari aliyokuwa nayo huyo abiria wako!" Akaweka kituo kisha akaendelea,

"Ina maana hukumuona namna alivyokuwa? Haya niambie alikuwaje?" Akamuuliza.

Feruzi akamjibu kinyonge,

"Alikuwa mwingi wa wasiwasi...halafuuu..alikuwa anatetemeka na alikuwa anavuja jasho jingi sana."

Yule bwana akamjibu,

"Yaani we ukaona hayo yote na bado ukabeba tu! Hivi unaona kosa lako ulilofanya?" Akamtazama kwa ukaribu zaidi. Kisha akashusha pumzi na kuendelea,

"Huyo naye alikuwa katika mahangaiko ya kutafuta hela kama wewe tu. Lakini yeye ametofautiana na wewe kidogo, yeye anaitafuta hela kwa njia haramu za kishetani. Na kwa bahati mbaya akakosea sheria. Na wewe ulikuwa unamleta kaburini kwake Adam!" Akaweka kituo na kumtazama.

Feruzi akazidi kuchanganyikiwa zaidi.

Maneno ya huyu bwana yakazidi kumtisha. 

"Sheria gani hizo?" Akauliza.

"Ukizijua hizo sheria utapotea mdogo wangu. Sitaki uzijue. Ninachokitaka ukijue wewe leo ni kuwa umekwepa kaburi lako. Na hautakaa urudi mahali hapa!" Akamjibu kwa sauti tulivu.

Wakati huo Duba na Dubu wakarejea wakiwa na furushi moja kubwa lililoonekana kuvimba, kwa kuwa na vitu ndani yake, wakalitua chini.

Yule bwana mwenye suti akaivaa miwani yake usoni na akasimama wima kwa kutegemea mhimili wa fimbo yake.

Akatazama saa yake na kusogea mahala pale kwenye furushi huku akijikongoja kwa fimbo yake ya mauaji.

Akalifungua furushi na kutikisa kichwa chake kukubaliana na alichokiona.

 

"Haya Duba! Chimba bunda moja kutoka shambani. Unipatie hapa!" Akaagiza.

Feruzi akamshuhudia Duba akiokota jembe na kusogea mahala kwenye ardhi ile akachimbachimba kwa hatua kadhaa na kuibuka na bunda moja la noti!

Ajabu!

Feruzi akazidi kupagawa,

Bunda lile likakabidhiwa mkononi mwa bwana mwenye suti, ambaye alilipukuta vumbi lake na akapiga hatua kumsogelea Feruzi pale ardhini.

"Haya chukua hii milioni moja! Najua nimekupotezea muda mwingi sana leo. Sasa hivi inaelekea saa moja jioni! Tusamehe sana Adam Feruzi Adam!"

Akanyoosha mkono wake na kumpatia bunda lile. Feruzi akiwa bado haamini akalipokea huku mikono yake ikimtetemeka.

Yule bwana akatoa tena miwani yake usoni na kufuta chozi kwenye jicho lake bovu. Akarudisha upya miwani yake usoni.

"Hizo noti zimeandikwa kuwa ni fedha halali za malipo, lakini hazijapatikana kwa njia halali. Ni fedha haramu mdogo wangu! Zinaweza kukupoteza kama tu utazitumia vibaya! Nielewe hapo!" Akaongezea.

"Sijajitambulisha jina langu kwako! Na wala usitamani kulijua jina langu. We niite shetani, ibilisi, lusifa, pepo mbaya , mwehu au hata mwendawazimu vyote ni sawa tu! Lakini siku ambayo utalifahamu jina langu. Basi na wewe utakuwa umejiingiza kwenye lile duara la watu wangu wa karibu ambao nimekuambia kuwa wakoje??!" Akamswalika,

"Ni watu waovu!" Feruzi akamjibu huku midomo yake ikimtetemeka.

Jibu lake likamfurahisha sana huyu bwana, haraka akaagiza aongezewe bunda jingine la noti. Na akapewa!

Ajabu nyingine hii... yaani fedha zinachimbwa ardhini tu na kugawiwa kama njugu. Feruzi alikuwa akilishuhudia ajabu la nane baada ya maajabu saba ya dunia.

"Umenifurahisha sana Adam Feruzi Adam! Kwanza we ni msikivu na mwema sana. Kijana mpambanaji anayetafuta hela kwa jasho lake! Hivi nilikuambia kuwa hutatoka salama humu sio? Basi leo utaondoka salama." Akatamka huku akitabasamu, mikono yake imo ndani ya koti lake. Kasimama wima kwa mamlaka. Akachukua leso yake ileile yenye damu na kuitia kwenye mfuko wa suruali la Feruzi kama anayempatia zawadi.

"Una mazoea ya kusoma Biblia, Adam Feruzi Adam?!" Akamuuliza.

Feruzi ambaye hakumbuki hata mara ya mwisho ameona Biblia wapi akamjibu,

"Mara moja moja..."

"Oooh basi kuna kitabu mle nakipenda sana...nimekuwa nikikisoma mara kwa mara hasa ninapookoka kutoka kwenye hatari ya kufa. Zaburi ya thelathini. Aliandika mfalme Daudi! Unaijua Zaburi, Adam Feruzi Adam?!"

"Ndi...ndio naifahamu!" Akajibu kinyonge.

"Basi kaisome leo kama ukifika salama huko uendako!" Akamaliza na akapiga hatua kuondoka mahala pale. Kama vile hakufanya chochote kile kibaya. Akaokota fimbo yake na kujikongoja kutoka eneo lile kuelekea mafichoni.

"Zaburi ya 30, kaisome leo!" Akakazia huku akiondoka.

"Muondoeni hapa!" Akapaza sauti yake!

Upesi Dubu na pacha wake kiumbo, Duba. Wakamfikia Feruzi na kumnyanyua kwa nguvu kutoka pale ardhini. Kabla hawajamvalisha mfuko ule mkubwa mweusi kichwani wakamsalimia kwa kofi kali la shavuni, lililomfanya aone nyota ndogondogo zikimetameta.

Halafu wakamburuza kumtoa eneo lile kwa kumharakisha.

Dakika kumi na sita ziliwatosha kumfikisha eneo lilelile ilipokuwepo pikipiki yake ikiwa imeanguka chini. Wakamvua mfuko ule kichwani, wakamshurutisha apande pikipiki yake haraka.

Akatii japo kwa kujivuta kidogo, maumivu yakimtesa.

"Dogo sikia! Jambo lolote lile uliloliona kule ndani libaki kuwa siri..yani kama likivuka ile miti iliokuwepo pale likasambaa huko kwa watu. You are dead!" Sauti yake ya kukoroma ikabweka!

"Nadhani tumeelewa au unataka maelekezo zaidi?!" Mwingine akahoji.

"Hapana hapana...nimeelewa!" Feruzi hakutaka shari, tayari amepokea mabanzi na makofi ya kumtosha sahau uovu aliouna kule porini kati. Sasa ni maelekezo gani hayo ya ziada aliyoyataka?

"Potea sasa! Unasubiri nini?" Dubu akafuta panga lake lilelile lenye kutu kumshitua Feruzi aendeshe pikipiki yake.

Nayo ilikuwa haieleweki kama inataka kuwaka au nayo imepagawa.

Anapiga kiki, inagoma. Mara gia hairudi namba moja, mara anazidisha moto. Amepagawa na pikipiki nayo imepagawa!

"Hio bodaboda inawaka au tuje tukusaidie kuwasha?" Baada ya kusikia sauti hii pikipiki ikawaka mara moja! Akachochea moto na kupotea eneo lile kwa kasi ya ajabu.

"Huyu dogo kwa huu mwendo akikutana na mlevi huko rodi, Mungu amsaidie aisee!" Duba akamnong'oneza Dubu. Nao wakapotea kurudi mafichoni kwao.

Walidhani kuwa hakuna aliyewaona, walidhani hivyo!

***********

 

"Zaburi ya 30, kaisome leo!" 

Sauti ya bwana mwenye suti bado ilikuwa ikiita kwenye akili ya huyu bodaboda ambaye alikuwa kasi sana barabarani.

Watu wakimshangaa kuwa huenda ni mkosaji na anakimbizwa ma askari polisi wa usalama barabarani.

Lakini yeye hakujali. Barabara aliona kuwa ni yake, aliona kuwa ni pana sana na inamtosha kufika aendako salama. Akaamua kuendesha kwa kasi.

Huyoo! Akaiacha barabara ya kwenda mkoani, akanyoosha kushoto kuukata mtaa wa Kasarani. Kwa kasi ya ajabu! Akawa ndani ya mtaa wa Buyekera, 

Huyooo! Akakata kona kali ya kushtukiza kama wale wanamichezo wa mashindano kwa kuilaza pikipiki na kurusha vumbi na mchanga hewani.

Vumbi likawabugudhi wazee waliokuwa bize wakiburudika na kahawa kwa soga mbalimbali,

"Eboooh! Huyu kijana mwehu nini? Ona sasa!" Akang'aka mzee mmoja ambaye kahawa yake ilichafuliwa kwa vumbi.

"Niliwaambia kuwa huyu kijana kama sio bange kichwani mule basi ni mirungi!" Mzee mwingine akawakumbusha hoja yake aliyoisema jioni hiyo.

Baadhi ya watu wakawa wanashangilia kwa alichokifanya lakini yeye hakujali...akafika mpaka nje ya saluni yake ambayo ilikuwa wazi. Bila kuzima pikipiki akaruka ndani ya saluni na kukutana na rafiki yake Mtemi Moringo akiwa anamnyoa mteja mmoja na wengine wawili wakimsubiri.

Kila mmoja akamgeukia kumtazama maana aliingia kwa pupa mle ndani, jasho likimtoka kama maji na anahema juujuu.

"Oyah! Bora umekuja aiseee, haya njoo umalizie hivi vichwa. Halafu umechelewa sana we fala, ulikuwa wapi wewe? Au nd'o ulikuwa unapakia wateja wa mji mzima?" Ni Mtemi Moringo kwenye moja na mbili za utani wake.

Bila kutoa neno, Feruzi akaanguka chini kama mzigo. PUUUUH!

-----------

Je Feruzi ameokoka kutoka kwenye mdomo wa simba?

Ama bado atazidi kufuatiliwa? 

Unaijua Zaburi ya 30? 😃

Previoua Next