AKISHTUKA kutoka kwenye usingizi mzito, akagundua kuwa kichwa chake kilikuwa kizito na mwili wake ulielemewa kwa uchovu. Akajitahidi kufumbua macho yake, akaweza japo ilikuwa kwa taabu sana.
Mwanga mkali wa taa ulimuumiza kwa mara ya kwanza lakini akajitahidi kupambana nao akaweza.
Alikuwa amedhoofu na hata alipojaribu kujikusanya ili ainuke alishindwa. Akayatazama mazingira aliyokuwepo, asingeweza kuyatambua vyema kama tu usingizi na uchovu vingeendelea kumlevya. Akajipa sekunde kumi na tano za utulivu.
Akavuta pumzi na kuitoa nje, ndani kisha nje tena mara sita.
Kisha akawa makini tena na mazingira yale aliyokuwepo. Mara moja akaziona kuta zilizosilibwa vyema kwa simenti na kupambwa kwa picha za mtu aliyemfahamu. Akakaza macho yake pale, akagundua kuwa yule bwana pale pichani amemiliki sura yake yeye mwenyewe.
"Eboh! Nimefikajefikaje hapa nyumbani?!"
Akatamka huku akijikusanya kwa taabu pale juu ya kitanda. Yupo chumbani kwake na hajui ni namna gani amefika pale.
Akajiinua na kuketi juu ya kitanda huku mkono wake mmoja ukiushikilia ubavu wake wa kulia uliokuwa ukimuuma na mwingine ukikipapasa kichwa chake. Akawa hakumbuki lolote lile lililomkuta muda mchache uliopita.
"Auuu...subiri kwanza, nilifika saluni pale, halafu ikawaje sasa? Halafu sasa hivi ni usiku! Ina maana- Ah!" Akapata utata.
Jibu lake likajibiwa kwa kufunguliwa kwa mlango kutokea nje. Na Mtemi Moringo akaingia akiwa na mfuko ulioonekana kuvimba baada ya kupakiwa vitu fulani fulani.
"Eeeh! Aiseee angalau umeamka aisee. Sasa kwanza ule!" Mtemi akatamka huku akipambana kurudishia mlango wa chumba kile, uliokuwa na tabia ya kuleta ubishi linapokuja suala zima la kufungwa endapo tu mfungaji alikuwa ndani ya chumba.
"Weka chomeko tu hapo. Bila hivyo huufungi!" Akatamka Feruzi huku akiketi vyema juu ya kitanda kile.
Mtemi akafunga mlango na kufika mpaka juu ya meza ndogo iliokuwa ndani ya chumba. Akautua mfuko ule pale mezani na kupakua baadhi ya vitu ambavyo alitaka kuvitoa mule. Na vingine akaviacha ndani ya mfuko.
"Oyah! Hivi wewe nd'o umenileta hapa ndani?!" Feruzi akauliza.
"Yaani umedondoka kama mzigo we jamaa, PUUH! Tukakuzoa mpaka nje, pepea wee pepea wee, wapi! Nikaamua nikubebe mpaka hapa kwako aisee." Mtemi akamjibu huku akiendelea kuandaa chakula alichokileta.
"Yaani ina maana nimezimia? Kule saluni au? Hapana bwana...yani mimi nizimie." Feruzi akauliza swali na kujijibu mwenyewe huku akitoa tabasamu hafifu.
"Au sio? Em jiangalie vizuri kwanza. Halafu nd'o uje uongee utopolo wako huo. Haya jiangalie kwanza!". Mtemi akaiacha sentensi yake ielee, ili Feruzi ajitazame kwanza.
Feruzi akasimama kwa taabu na kujikagua mwili wake. Alikuwa na michubuko mikononi na alichafuka suruali lake kwa vumbi kiasi.
"Umezimia pale saluni. Nikamshtua Sele, akatuleta kwa taxi yake ile mpaka hapa!". Mtemi akamalizia ile sentensi yake iliyokuwa hewani.
Akaivuta ile meza mpaka pale kitandani na kumkaribisha Feruzi chakula.
"Kwa hio hata hukunipeleka hospitali. Yani nimezimia halafu we upesi ukanifikisha hapa?!" Feruzi akirejea kwenye kitanda akaketi huku akimtupia swali Mtemi.
"Tulia bhana, hayo yote tutayazungumza mzee."
Mtemi akamjibu, kisha akaketi juu ya kitanda sambamba na Feruzi.
"Najua hujala tangu asubuhi, nd'o maana unazimiazimia ovyo. Haya kwanza njoo hapa tufinye halafu tutaongea vizuri make inaonekana umesababisha mabalaa leo!"
"Maba...mabalaa? Mabalaa gani hayo unayoyajua wewe?" Uso wa Feruzi ukabadilika ghafla. Nguvu zake zilizokuwa zimeenda likizo zikarejea kwa kasi mwilini mwake na uchovu ukapotea.
"Kula kwanza mzee...Hauna nguvu sasa hivi. Tuliza povu hilo ule halafu ukimaliza tutayaongea tu haya!" Akasisitiza Mtemi huku akiviringa tonge kubwa la ubwabwa kwenye kiganja cha mkono wake wa kulia.
"Aisee acha utani Mtemi. Yaani kama kuna kitu-". Akakatishwa.
"Kula hilo chee kwanza, halafu ujue huyo samaki nimemnunua buku tatu!" Ni mtemi ambaye anatamka, shavu lake likiwa limevimbishwa kwa tonge mdomoni, bado anajiandaa kuchovya tonge kubwa la ubwabwa kwenye supu ile nzito ya samaki aliyeungwa vyema.
Feruzi akaacha kulalamika na kuanza kula. Alimfahamu vyema rafiki yake namna ambavyo hakuwa na utani linapofika suala la kula naye kwenye sahani moja. Akaungana naye na kukifakamia chakula chote kilichokuwepo kwa pupa. Njaa iliokuwa inamtishia uhai wake ikamkimbia. Baada ya mlo wakanywa maji ya kutosha na kutulia.
"Kwenye koti lako kulikuwa na vitu vyangu viko wapi?" Feruzi akahoji.
Mtemi akamtazama kwa sekunde nne kisha akasimama na kuinama chini ya kitanda kile. Akaibuka na begi lake ambalo alilifungua na kutoka na mfuko mdogo mweusi.
Taratibu akatoa mabunda mawili ya noti za shilingi elfu kumi. Akayaweka juu ya meza ile ndogo.
"Nitataka maelezo juu ya huu mpunga wote halafu..."
Akatia mkono wake na kuibuka na leso iliokuwa imechafuliwa kwa damu. Hii aliishika kwa vidole viwili, cha kati na gumba kama mtu mwenye kinyaa. Akakiweka mezani pia.
"Nitataka na maelezo juu ya hiki kitambaa." Akatamka akiwa ameukunja uso wake kwa uchungu.
Ukimya wa haja, ukachukua umiliki ndani ya chumba kile kwa sekunde kadhaa. Kisha kwa utulivu wa hali ya juu, Feruzi akatamka kwa sauti ya kunong'ona,
"Nisikilize Mtemi." Akatoa leso ile mezani na kuirudisha ndani ya mfuko ule kisha akaweka chini ya godoro lile walilolikalia.
"Nakusikiliza hapa, yaani nataka uniambie ulienda kufanya nini leo na pikipiki yangu aisee. Kama uliteka watu au uliua uniambie!" Mtemi akatamka akiwa na hamaniko.
"Tulia Mtemi tulia." Feruzi akatamka kwa kunong'ona tena. Kisha akasogea mpaka karibu na dirisha la chumba kile akahakikisha kuwa hakuna mtu aliyekuwa akiwasikiliza kwa nje akalifunga vizuri. Akafanya hivyohivyo mlangoni.
Akarudi kitandani,
"Mambo niliyoyaona jioni hii ya leo ni ya ajabu na ya kutisha sana mwanangu!" Akameza funda la mate kisha akaendelea,
"Nitakueleza mwanzo mpaka mwisho lakini sharti ni moja tu. Hii siri nataka isitoke nje ya hizi kuta nne." Akaweka angalizo.
Feruzi akamsimulia Mtemi kisa chote, namna alivyokutana na masaibu huko porini. Mpaka namna alivyopata zile fedha na akapewa zawadi ile ya leso yenye damu na yule bwana mwenye suti.
Mpaka anamaliza kusimulia mkasa wake, Mtemi alikuwa ametoa macho yake kwa woga!
"Wewee!" Akamtamka akiwa mwingi wa hofu na mshangao.
"Eeh nd'o hivyo mzee, nadhani kama nimepona kifo leo pale msituni. Basi sitakuja tena kufa kwenye mazingira ya kutisha nakuapia aisee." Akafuta jasho lililokuwa likimtiririka usoni mwake.
"Aiseee!" Mtemi yuko kwenye mshangao, amemtumbulia macho Feruzi.
"Kwahiyo huyo abiria alikuwa anaenda kuuawa kule msituni? Na akakutumia wewe."
Akamuuliza.
"Yaani mpaka mimi sielewi. Wamenicharaza makofi ya kutosha aisee...mgongo wangu ulikuwa kama ngoma ya bendi leo!" Akajibu huku akiupapasa mgongo wake.
"Yale majamaa yanajiita Dubu sijui? Yale ni majayanti aisee sijawahi kuona! Yani sijui yanakula vyakula gani yale!" Akazidi kulalamika.
"Kwani wamehaidi kukufatilia tena?"
"Duh! Hapana aisee. Sema yule jamaa mwenye suti kanambia nisome Biblia. Sijui Zaburi ya ngapi ile, thelathini kitu kama hicho. Eeh Zaburi ya thelathini!" Feruzi akatamka kwa unyonge.
Mtemi akatabasamu kwa mara ya kwanza.
"Yaani majambazi yamekuagiza mpaka usome baibo? Aisee Hehehehe...hii kweli kubwa kuliko." Akasindikiza sentensi yake kwa kicheko. Kicheko cha huzuni.
"Unaweza dhani anatania mwanangu, yaani jamaa akishavua tu miwani yake. Anakuwa hana utani tena! Kama utani tu kanambia nisome Baibo mzee. Zaburi ya 30, eti nimeokoka kifo leo nikamshukuru Mungu!" Feruzi akanong'ona. Bado Mtemi anacheka kwa masihara.
"Yaani we unacheka! Oyah. Ukiwa mbele ya huyo jamaa, utalia sana. Sikumbuki mara ya mwisho nimelia lini. Lakini leo aisee nimetoa machozi kama mtoto. Usicheze na uhai kabisa!"
Mtemi akajikakamua kisha akasema,
"Naelewa naelewa, lakini em tuwe wakweli. Wewe mara ya mwisho kuona Biblia ni lini? Tuwe wakweli kabisa kwenye hili. Wewe Feruzi tangu lini umekuwa na urafiki na Biblia?!" Bado sauti yake ina kicheko, Mtemi akazidi kumtania rafiki yake.
"Kesho ni Jumapili. Bahati nzuri kanisani sio mbali, nenda kasali aisee. Toa sadaka! Halafu umuombe mtu baibo upitie hicho kifungu kitakatifu! Hehehehe." Akarejea kwenye kicheko.
Feruzi akatamka moyoni mwake,
'Huyu bado hajakutana nao wale kina Dubu.. Hawajui vizuri huyu.'
Mtemi akahamisha macho yake kutoka usoni kwa Feruzi na kutazama juu ya meza ile,
"Ulipozimia, sikukupeleka hospitali haraka kwa sababu nilipokukagua nilikutana na hivi vitu. Nikajua tu kuwa kuna mabalaa umeyafanya!" Mtemi akatia nukta.
"Una uhakika kuwa hakuna mtu yeyote yule ambaye amekuona ukivitunza hivi vitu aisee?" Feruzi akamuuliza kwa woga.
"Hakuna aliyeniona, nina uhakika wa asilimia mia moja!" Akatetea hoja yake.
"Kweli?!"
"Sasa ni lini nimewahi kukufelisha mzee baba? Hakuna aliyeniona yaani nilikuwa mimi na Mungu wangu." Akajigamba.
Feruzi akashusha pumzi kwa uchovu.
Akaokota bunda moja pale mezani na kulipima uzito wake,
"Kumbe milioni moja huwa inalingana hivi. Yaani hii nd'o kidogo initoe uhai leo." Akatamka huku akichezea bunda lile mkononi.
"Enhe utazifanyia nini sasa hizo hela?" Mtemi akamkandamiza kwa swali.
"Duh! Yani bado siamini kama wamenipa hizi hela burebure yaani. Make yule fala alinipatia kwa vitisho sana." Feruzi akanena.
"Enhe alisemaje kwani."
"Alinambia kuwa hizi hela ni haramu! Na zimetokana na shughuli zisizo za halali. Nikizitumia vibaya zitanipoteza. Sasa hapo nd'o sikumuelewa kabisa."
"Mmh mmh...Oyah kwani hizi ni hela za kishirikina? Zisije zikakutokea puani." Mtemi akajibu kwa hamaniko huku akiketi vyema pale juu ya kitanda.
"Huenda ni hivyo...ma'ke hata alipozitoa sikuelewaelewa, walizichimba kutoka ardhini mzee! Huwezi amini yaani. Zilichimbwa kutoka ardhini! Halafu ni kama kwao ni kitu cha kawaida kabisa!" Feruzi akajibu huku akitetemeka mikono yake.
"Unasemaje? Yaani hela wanazichimba ardhini? Kwa jembe au?" Maswali mfululizo yakamtoka Mtemi.
"Eeh mwanangu, kwa jembe. Sa sijui walizifukia pale. Yaani kama wanavuna karanga tu. Jembe moja chwaa, la pili chwaa chwaa, wanaibuka na burungutu." Akatamka Feruzi.
Mchoro wa eneo hilo ukajichora kichwani kwa Mtemi kwa haraka sana.
"Yaani ujue unaniacha njia panda! Yaani unamaanisha wanafukua hela. Au wanachimba hela kama mazao?" Akauliza kwa sauti yenye mshangao.
Feruzi hakumjibu. Badala yake akakusanya kitita kile cha fedha na kukitunza chini ya godoro lake pale kitandani kisha akajilaza kitandani na kujinyoosha.
"Hii inaonyesha hawa watu wana utajiri mkubwa sana. Yani wamekuteka kimakosa halafu wanakuzawadia milioni mbili? Tena wanachimba kutoka ardhini yaani kama karanga umesema." Bado Mtemi anaongea peke yake.
"Oyah leo utalala hapa mzungu wanne au niaje? Make ni kama usiku umeenda sana." Feruzi akabadilisha mada hewani.
"Hapa..nitalala hapa leo!"
"Poa mzee mi ngoja nilale. Siku ngumu sana hii, siku nyeusi. Sirudii tena kuwa sekido aisee, pikipiki yako ina gundu." Akajilaza juu ya kitanda.
"Duh lala tu jamaa yangu. We leo umeona mambo mengi mara Dubu! Mara Jamaa mwenye sura mbaya, mara hela za ardhini. Aisee!" Feruzi akanena huku akijilaza pembeni ya Feruzi ambaye usingizi ulimchukua punde tu baada ya kujitupa pale kitandani.
Mtemi naye akalala kando katika mtindo uleule maarufu kwa jina la 'mzungu wanne', uso wake ukitazamana na miguu ya Feruzi iliyokuwa inalalamika kutooshwa kwa muda mrefu ikitoa harufu mbaya.
"Mmh...oyah Feri eh! Halafu kesho ukiamka piganisha uoge aisee. Make kilichoko huku aisee, ni changamoto!" Akalalamika huku akiugeuza uso wake upande mwingine na kutazama na ukuta.
Akili yake inawaza juu ya ardhi hiyo ya ajabu ambayo inachimbwa na kutoa hela kwa mafungu ya milioni milioni. Alichelewa sana kulala, mpaka pale usingizi ulipoona kuwa inatosha. Ukamlevya na akalala!
**********
Giza jepesi limekifunika chumba kidogo kinachofanania na ofisi.
Kinafanania na ofisi japo mapambo yake hayana uhusiano wowote ule na ofisi. Ni meza, kiti pamoja na vitabu kadhaa vinavyokipa chumba hiki walau sifa kadhaa za kuitwa ofisi. Japo chumba kama chumba, kilikuwa ni kama ghala ndogo ya silaha za moto.
Kikimiliki makasha kadhaa ya risasi mbalimbali pamoja na mitutu ya bunduki ikiwa imetundikwa kwenye kuta zake.
Ukimya ukitawala ndani yake na kusababisha hali ya utulivu wa hali ya juu. Utulivu ambao unapafanya mahali hapa paonekane kama hakuna kiumbe hai chochote kile.
Jambo ambalo sio kweli!
Nyuma ya meza hii kubwa ya duara iliyo ndani ya chumba hiki, kuna kiti ambacho kimekaliwa na kiwiliwili cha mtu mkubwa kiumbo. Akiwa amevaa suti nyeusi na kofia kubwa iliyoufunika uso wake kiasi cha kusababisha kivuli kiufiche uso wake.
Mikono yake iko juu ya meza akiwa kimya kama mtu anayesubiria kitu au taarifa fulani.
Na ghafla simu yake ya mezani inaita,
Bila papara, anaiokota na kubonyeza kitufe kuruhusu sauti ya mpigaji irindime masikioni mwake.
Na sauti ile inaonekana kumjibu kwa maneno fulani fulani ambayo anayasikia na anayaelewa yeye mwenyewe na mpigaji.
Hamjibu na badala yake anaokota kalamu ya wino pale mezani na kuchana kipande cha karatasi kutoka kwenye daftari mojawapo.
Kisha ananakiri kile anachoambiwa,
"Hii namba una uhakika nayo?" Anauliza kwa sauti nzito na hana haraka kwenye kuongea maneno yake.
"Ndio mkuu, na sio tu namba! Mpaka picha nimechukua." Sauti ile ikamjibu.
"Safi sana, najua kuwa umechukua tahadhari na hakuna mtu yeyote aliyekuona!" Mtu huyu wa miraba minne akatamka tena.
"Sure mkuu! Sijafanya mistake yoyote ile!"
"Well done!" Akakata simu ile.
Kisha akakitazama alichokuwa amekinakiri juu ya karatasi kwa sekunde kadhaa. Kisha akatamka kwa kunong'ona,
"Hauna maisha marefu sana Franko! Nitakufikia na zawadi nzuri sana ya kifo chako huku nikitabasamu. Damu yako ni halali yangu! Bado sentimeta chache tu. Bado sentimeta chache kukufikia ulipo, Dario!"
Akatia nukta na kuitunza karatasi ile katikati ya vitabu vyake.
Kisha akasimama na kuondoka ndani ya chumba kile kidogo chenye giza. Akafunga mlango wake kwa funguo na kuacha ukimya uliopambwa kwa giza jepesi, kufuatia maneno yake ya vitisho aliyoyanuia kwa mtu aliyemfahamu!
--------
Mapema sana!
Msako umeanza, ni nani huyu Dario?
Je ni masaibu gani yatamkuta Feruzi?
Tukutane tena wakati ujao.
Comments