Wakati Regina anaamka alijikuta akiwa kwenye gari akiwa ameegamia kwenye siti.
Alijikuta akivuta kumbukumbu ya kile kilichotokea na alikaa kitako kwa haraka na ndipo aliweza kuona gari ipo kwenye mwendo na Hamza ndio dereva.
“Regina umeamka , vipi unahisi
kizunguzungu?”Aliuliza Hamza akiwa amegeuka na kumwangalia na tabasamu.
Regina alijikagua na kukagua mazingiara na kuthibitisha alikuwa salama.
“Wewe ndio umeniokoa?”Aliuliza
“Unaweza kusema hivyo , lakini haina haja ya kunishukuru , isitoshe hili limekutokea kwa sababu yangu “Aliongea Hamza
Regina aliishia kubakia kimya , alikuwa na hisia zisizoelezeka katika moyo wake na kujiambia inamaana huyu mwanaume ni kweli ameamua kuhatarisha maisha yake kweli na kuja kumsaidia.
“Umewezaje kuniokoa kwa wale watu?”Aliuliza maana alikuwa hana fahamu wakati Hamza akikinukisha.
“Nilifika pale na kisha nikawashushia kipigo , walivyoona hawaniwezi wakakimbia”Aliongea Hamza.
“Acha kunidanganya , mimi sio mtoto , wale watu walikuwa na visu na bunduki , halafu wewe ambae ulikuwa mikono mitupu ndio umewaweza mpaka wakakimbia?”Aliongea huku akionyesha kukasirika maana Hamza anamchezea akili yake kwa kumwambia uongo.
“Regina wewe hujui tu , lile lilikuwa kundi la watu wazembe , walikuwa wakikukuogopesha tu uwaone sio wa kawaida . halafu ile bunduki ulioona ni feki , ni kama zile wanazochezea watoto”
“Kama unachosema ni kweli , basi niambie kitabu cha Anka ndio nini , walisema sijui cha mti wa uzima?”Aliuliza huku akimwangalia Hamza kwa macho makali.
Hamza alijikuta akiingiwa na ubaridi mara baada ya kuulizwa swali lakini alirudi katika hali ya tabasamu kuficha wasiwasi wake.
“Anka ndio nini?”Aliuliza lakini kauli ile ilimfanya Regina asage meno yake kwa hasira.
“Wewe ni nani haswa , unajulikana kama mwanafunzi wa chuo na fundi,au wewe sio mwanafunzi kweli kama ulivyosema , kuna kitu unajaribu kuficha sio?”Aliuliza.
Hamza alijua hakuna uwezekano wa kumdanganya mwanamke huyo ambae vipimo vya IQ yake ni 180, hata kama anaweza asiwe vizuri kwenye maswala ya kimaisha lakini katika kitu muhimu kama hicho ambacho kilihusisha uhai wake ingekuwa ngumu kuepuka bila ya kujibu swali lake.
Lakini Hamza alijua kama Regina atajua vitu vingi kuhusu yeye basi moja kwa moja angekuwa katika hatari.
Alitaka kujali usalama wake sana kuliko kitu chochote ili isije ikatokea ajali huko mbele ya safari.
Hamza alienda kusimamisha gari ndani ya mgahawa wa Golden fork Mbezi beach.
“Hebu tutoke tukale kwanza , baada ya kumaliza kula nakuahidi nitakujibu maswali yako yote , sawa?”Aliongea Hamza.
Ni muda huo huo ndio Regina alijua kumbe walikuwa mbali sana na nyumbani , nje kulikuwa na giza hivyo hakuweza kuangalia hata walikuwa wapi.
“Kwanini tule hapa?”Aliuliza
“Saa tatu usiku sasa hivi , huoni kwamba mpaka tufike na kuanza kutafuta chakula itatuchosha sana, chukulia hii kama nafasi ya mimi kuomba msamaha kwa kilichokutokea, au unataka kula chakula kilichopikwa na shangazi?”
Regina mara baada ya kumsikia Hamza akimtaja Shangazi ndio wasiwasi ulimwingia.
“Vipi shangazi anajua kilichonitokea?”
“Usiwe na wasiwasi , nilimpigia simu na kumwambia tupo date”
“Mimi!? , Date na wewe?”Aliuliza huku akimwangalia kwa ukali usoni lakini hata hivyo aliridhika kuona Hamza alikuwa makini kutompa presha shangazi yake.
Alikuwa na njaa pia hivyo aliamua kutoka bila ya kuleta ubishi.
Mgahawa ulikuwa bize, jiji la Dar ilikuwa ni tofauti na maeneo mengine , saa tatu ndio watu walikuwa wakitafuta chakula cha usiku , mgahawa huo ulipendwa pia na wapenzi wanaowatoa out wenza wao, hivyo meza zilikuwa zimejaa watu wawili wawili.
Waliweza kupata meza ya wazi upande wa kulia karibu na mlango wa kuingilia , watu waliokuwa ndani ya eneo hilo walikwa wakiwapiga macho mno..
Ukweli ni kwamba walikuwa wakiendana sana , kwa urembo wa Regina na muonekano wa Hamza hakukuwa na tofauti kubwa kati yao na hakuna ambae anaweza kubisha kama wawili hao sio wapenzi.
Lakini macho ya wanaume yalikuwa yakimwangalia sana Regina ambae alikuw ana urembo usiokuwa wa kawaida , ijapokuwa nywele zake hazikuwa zimemkaa vizuri lakini alikuwa akivutia mno.
Pia kwa Regina alionekana kuzoea kuagalia hivyo haikumpa shida , lakini pia alipenda mgahawa huo.
Hamza aliagiza chakula kwa wote lakini aliomba maji ya kunywa yaletwe kwanza.
“Umesema utanielezea kilichotokea na wewe ni nani , niambie sasa”Aliongea Regina , hakuweza kuificha shauku yake.
“Usiwe na haraka , hebu tunywe kwanza maji tupoze koo maana siku imekuwa ndefu sana kwetu”Aliongea huku akimpatia glasi yenye maji.
Regina alikuwa na kiu pia hivyo alipokea na kunywa glasi ya kwanza akaongeza na ya pili na akawa ametosheka , aliishia kuangalia upande wa nje kana kwamba kuna kitu anafikiria.
“Shangazi alisema wewe ni Yatima, kabla ya kuzamia nje ya nchi ulikulia katika kituo gani cha kulelea watoto?”Aliuliza.
“Sikulelewa katika kituo chochote,niliishi mtaani”Aliongea Hamza, ndio njia jibu rahisi ambalo aliona linaweza kumridhisha Regina kwa muda huo.
“Ndio maana unaonekana mjanja janja, naamini haikuwa rahisi kuendesha maisha mtaani ukiwa katika umri mdogo”.
“Ni ngumu kwa mtoto yoyote asie na wazazi , iwe ni mtaani au katika kituo cha kulelea Yatima , ni swala la unafuu tu , kulikuwa na watoto wa mtaani ambao wametoroka vituo vya kulelea Yatima pia”Aliongea Hamza.
“Nimekulia kituo cha kulelea Yatima pia , mazingira yanaweza kuwa mazuri na kupata mahitaji yote lakini kisaikolojia kuna kitu unakosa hasa ukifikia ule umri wa kujitambua , nadhani ndio maana baadhi ya watoto wanatoroka , lakini ni kheri kituoni kuliko mtaani , ni asilimia ndogo sana ya watoto wanaokulia mtaani kuwa na maisha ya kawaida”
“Nakubaliana na wewe , Vituo vya kulelea Yatima ni njia nzuri kimalezi kwa Yatima kuliko mtaani ambako watoto hujenga tabia za ajabu , lakini vipi kama wale wamiliki wa vituo wakiwa na ajenda nyingine juu ya watoto hao?”
“Unamaanisha ajenda gani kwa mfano?”Aliuliza Regina lakini muda huo waliletewa chakula chao na kumfanya Regina kukikagua.
“Sipendi vitunguu vya hivi mimi?”Aliongea Regina mara baada ya kuangalia namna samaki alivyopikwa kwa kuungwa na Scallion(Vitunguu vya kijani).
“Hio ndio Recipe sasa inafanya samaki walioungwa na Scallion kuwa watamu, inakuwaje hupendi vitunguu vya kijani wakati ni vizuri zaidi kuliko vitunguu aina ya Bombay, kama vipi niongee na watu wa jikoni wakubadilishie”
“Acha tu , hata Shangazi anavipenda kweli .. halafu mbona unaongea kwa kukunja sura hivyo kama unanifokea”
“Nimekufokea saa ngapi wakati nilikuwa nikikuelezea faida yake , au ndio umechukia kukuchagulia chakula chenye viungo usivyopenda”
‘Sijamaanisha hivyo , ila tu sipendi harufu ya hivi vitunguu”
“Mh, inaonekana Shangazi anafanya juhudi kubwa kukuridhisha na chakula anachopika”Aliongea Hamza huku akichezesha vidole.
“Haikuhusu , nitakula hizi chipsi tu , hao samaki kula wote mwenyewe”Aliongea kibishi na kumfanya Hamza aishie kutabasamu kutokana na ujeuri wa Regina.
“Angalau leo kwa mara ya kwanza na ya mwisho tunakula nje pamoja japo hatujakuwa pamoja kwa muda mrefu”
“Unataka kusema nini?”Aliongea Regina huku akimwangalia Hamza maana ni kama amekuwa siriasi ghafla tu.
“Namaanisha baada ya kutoka hapa kila mtu ataelekea uelekeo wake”Aliongea Hamza na kumfanya Regina aliekuwa akichoma chipsi na uma kusita na kumwangalia Hamza usoni na ukimya ulimvaa ghafla.
“Umesema unakuja hapa ili kuniambia kilichotokea na wewe ni nani lakini mwishowe naona unataka tuachane”.
“Hatuachani kwasababu uhusiano wetu ni feki , tunachokwenda kufanya ni kusitisha tu mkataba wa kazi na kila mtu kuendelea na maisha yake kama ilivyokuwa”Aliongea.
******
Upande mwingine katika makao makuu ya kitengo
cha usalama wa taifa kinachodili na nguvu sizizoonekana kifahamikacho kwa jina la MALIBU kulikuwa na kikao kilichohusisha watu watatu , mmoja akiwa ni Kanali Msuya ambae ni mkuu msaidii wa kitengo hicho, Kapteni Kwavava na Afande Mdudu.
Wote macho yao yalikuwa kwenye skrini wakiangalia wanajeshi ambao walikuwa eneo la tukio.
“Afande wote wamepoteza maisha , hakuna hata mmoja ambae yupo hai, vifo vyao ni vya kikatili mno”sauti kupitia simu ya upepo ilisikika , simu ambayo ilikuwa imeshikwa na Afande Mdudu
Afande Msuya na Afande Kwavava waliangalia kwa mshangao na macho yao yalijaa maswali.
“Inawezekana vipi , au taarifa tulizopokea zilikuwa hazina ukweli wowote?”Aliuliza Afande Msuya. “Sidhani kama hazikuwa na ukweli , intellijensia ile ilikuwa ni sahihi kabisa Afande”
“Kwahio inamaanisha aliehusika na vifo vyao anaweza kuwa na uwezo wa juu kuliko wao?”Aliuliza na Afande Kwavava aliishia kutingisha kichwa.
“Afande Kiduma hakikisha mnapiga picha ya tukio zima na majeraha yao ili kufanyiwa uchunguzi wa kina”Aliongea Afande Mdudu.
“Sawa Afande”
“Hakikisha hili swala linabakia siri mpaka tupate ufumbuzi wa kila kitu kilichotokea”Aliongea Kanali Msuya na Afande Mdudu alipiga saluti na kisha akakaa chini.
“Mnadhani kuna kitu gani tunamisi?”Aliuliza Afande Msuya.
“Kwanini Afande?”
“Hawa wahalifu wameingia nchini kwa zaidi ya wiki mbili zote , lakini kitengo chetu kimejua taarrifa ya uwepo wao leo hii na ndio siku wamepoteza maisha wote, mnadhani hakuna kilichokosekana katika mfumo wetu wa intellijensia?”
“Mkurugenzi , unachoongea ni sahihi kuna kitu tunamisi , lakini nadhani hii haimaanishi kitengo chetu uwezo wake ni mdogo , ni swala la kuzidiwa kitaalamu tu na kama ilivyokuwa siku zote ndio namna tunavyochukulia kama changamoto ya kujioboresha zaidi”Aliongea Kwavava.
“Hiki ni kipindi ambacho vitengo vyetu vya usalama lazima viwe katika ubora wake hasa likija swala la kukusanya intellijensia , Uchaguzi mkuu unakaribia , kosa kidogo tu usalama wa taifa unaweza kuwa hatarini , Wahalifu hatari namna hii wanaingia nchini , lakini tumeshindwa kuwadaka katika lada zetu za usalama , mtu wa nje anatupenyezea taarifa na vikosi vyetu vinakuta wamepoteza maisha wote , Nani mhusika wa tukio hili la kutisha hata pa kuanzia hatuna”
“Kwa uchunguzi wa awali wa Afande Kiduma anasema Gonzo Fisheries ndio wamiliki wa Ghala, nimeongea na Mzee Sinzwe hana taarifa ya kukodishwa kwa ghala lake”
“Inamaanisha vijana wake ndio wamekodisha ghala hilo , kama ni hivyo basi lilikodishwa kwa muda mfupi tu”
“Ndio na kwasasa wote wapo baharini wanavua hivyo imekuwa ngumu kupata taarifa ya kilichotokea”Aliongea Afande Mdudu.
“Afande kwa taarifa niliozokuwa nazo juu ya hili kundi , wanajiita Waray Bounty hunters , jina lao la utani ni Tumbili wenye mbawa za mwewe , ukiachana na sifa zao za kimafia na umahili wa kutafuta watu lakini pia wanahusishwa kutokea Biringan”Aliongea Afande Mdudu.
“Unataka kumaanisha nini Mdudu?”
“Kama inavyosemwa ni kweli wanatokea Biringan basi sio watu wa kawaida , sijui kama mnajua hili ila Biringan ni eneo ambalo halipo kwenye ramani ya dunia zaidi ya hadithi za kiimani tu , pointi yangu kama watu wa aina hii wamefika Tanzania kwa ajili ya kutafuta kitu , basi moja kwa moja mpango wao umefeli na kuna uwezekano watarudi wengine”
“Mdudu unapendekeza nini?”Aliongea Afande Kwavava.
“Lazima tujue kwanza ni kipi ambacho wamekijia hapa Tanzania”
“Nadhanni tunarudi palepale tu , katika uchunguzi wetu tunachotaka kujua ni nani ambae amehusika kuwaua na ikitokea tumemfahamu basi ni dhahiri huyo ndio wanaemtaka hivyo tutaweza kupata majibu”
“Kwavava mkuu wako Dastani ana shida gani siku hizi , kwanini amekuwa bize sana , mpaka kwenye vikao muhimu kama hivi anakosekana?”
“Amekuwa akiwafatilia wale Wabrazili kwa muda mrefu , nadhani ndio kinachomfanya kuwa bize”Aliongea na Afande Msuya alionekana kutoridhika.
“Dastani ndio mtu ambae ana utashi mkubwa wa mambo kama haya , wasiliana nae na umshirikishe huu uchunguzi nahitaji majibu ya haraka”
“Sawa Afande”
“Kwavava kaa na timu yako ya intellijensia , nahitaji ripoti kamili kwanini idara yetu inazidi kuwa butu siku hadi siku na kushindwa kunusa hatari kwa haraka”
“Sawa Afande”
“Hakikisheni pia tunajua nani kapenyeza taarifa ya uwepo wa hawa wahalifu nchini kwetu , tunaweza kupata pa kuanzia”Aliongea na kisha alisimama.
“Afande kuna taarifa pia nahitaji kuripoti”
“Jnahusu nini?”
“Amosi ameshambuliwa na risasi , yupo mahututi hospitali ya jeshi?”Aliongea Mdudu na ilimfanya Afande Msuya kushangaa kidogo.
“Amosi si alikuwa chini ya Kanali Dastani , kwanini unaripoti wewe hii taarifa”
“Msemakweli katika kampeni zake ameendelea kuituhumu kushirikiana na Binamu , nadhani inafahamika ndani ya kitengo Amosi ameshawahi kufanya kazi kama undercover Agent kwa ajili ya kuwachunguza Binamu”Afande Msuya alijikuta akirudi kwenye Sofa na kuketi huku akionekana kuwaza kidogo.
“Kuna uwezekano Binamu ndio walimshambulia , lakini kwasasa hakuna uhakika kwani Amosi bado fahamu hazijamrudia, nina uhakika hili ndio sababu ya Kanali kutokuonekana katika vikao vyote leo, ila kama kweli ni Binamu basi watahakikisha wanaona kifo chake”
“Mtafute Kanali popote alipo , kesho afike katika ofisi yangu na ulinzi uimarishwe katika wodi ya Amosi , tutahitaji maelezo kutoka kwake”Aliongea na maagizo yale alipewa Mdudu na alitoa saluti na kisha akatoka nje.
“Anachosema Msemakweli sio uongo , lakini hili swala linachukua sura mpya , kumekuwa na mijadala mingi mtandaoni , inayozusha kile kinachoendelea mtandaoni , wengine wanadai Night Shadows wapo chini ya Binamu”Aliongea Afande Kwavava.
“Kwavava hivi unaamini hawa Night Shadows wapo kama watu wanavyozusha?”
“Kitengo chetu kimekuwa kikifanya uchunguzi kwa muda mrefu , lakini hatujafanikiwa kupata ushahidi wa moja kwa moja wa kuamini, maoni yangu ni aidha wapo kweli kama watu wanavyosema au kuna kundi la watu wanajaribu kujaza watu hofu”
“Sio sisi tu ambao tunawafuatilia hawa Nightshadows, serikali zote kubwa wanafatilia hili lakini hakuna ushahidi unaotolewa, inanifanya mwisho wa siku kuamini ni uzushi pia”.
“Lakini Afande una uhakika gani kama serikali kubwa duniani hawana ushahidi , vipi kama jambo hili wanalifanya kuwa siri kama ilivyotokea kwa tukio lililopita?”
“Kwasasa ni ngumu kwangu kuweka neno lolote kuhusu hili , isitoshe tunatarajia serikali mpya hivi karibuni , nadhani tulipe muda kwanza, Kwavava nadhani unajua ninachomaanisha” “Ndio Afande”.
Comments