SEHEMU YA 30.
Fellini alifikiria kwa muda na kisha alimwangalia Regina kwa uso kidogo uliokuwa hauna ridhiko.
“Miss Regina , naomba nikuambie tu kwamba hatuwezi kufanya kazi pamoja zaidi kwasababu hatuna maelewano ya kisera kati ya kampuni zetu”
“Inakuwaje Mr Fellini , tulijiandaa kukutana na wewe kwa muda mrefu na tumeshaandaa mipango ya kibiashara ya muda mrefu ya ushirikiano wetu, hujaona hata vipengele vya mkataba lakini kwasababu ya kutofautiana mtazamo unatukataa , hii sio haki”Aliongea Linda.
“Wewe ni msaidizi tu , hujapewa ruhusa ya kuongea”Aliongea Salma.
“Haina haja ya kubembeleza zaidi Linda , alichoongea Mr Fellini ni sahihi kabisa , mimi sina maarifa mengi likija swala la fasheni” “Mkurugenzi wewe sio mbunifu wa mavazi na hujasomea fasheni , haina haja ya kuwa mnyonge , ulichoongea wewe ni katika jicho la kibiashara”
Upande wa Fellini alionekana kwenye kutafakari kwa dakika kadhaa na kisha aliwaangaia wote wawili yaani Salma na Regina.
“Mnaonaje tukifanya hivi , wote wawili mmevaa na mmependeza sana , je kuna sababu yoyote ya kuchagua staili ya mavazi mliovaa leo?, watu wenye pesa hatuvai kupendeza tu , kuna mengi zaidi ya kuelezea kuhusu aina ya maisha yetu kupitia nguo , nataka kusikia kutoka kwenu”Aliongea , Fellini hakutaka kuonekana mkatili ndio maana alitaka kumpa Regina nafasi ya mwisho.
“Bila shaka nitaelezea”Aliongea Salma na kisha alisimama akiwa na tabasamu na kuonyesha vazi lake.
“Mr Fellini nadhani utakuwa umejua hili ni vazi kutoka Louis Vuitton lililovuma kwenye maonyesho ya wiki ya mitindo jijini Paris?”Aliuliza na Fellini alitingisha kichwa akikubali.
“Hili vazi linaweza kuonekana la kawaida lakini linadhihirisha ujasiri wa mbunifu, mpangilio wa eneo la kiuno unamfanya mwanamke yoyote ambae amevaa kumpa heshima yake kwa kuonyesha ni kiasi gani ni mrembo, dizaini iliotumika ni ya kibalkani na udarizi wa eneo la mkanda wa kiunoni pamoja na vazi lote juu hadi chini linaashiria tabia , sifa yangu kubwa ni ucheshi ndio maana nimechagua vazi hili leo hii”Aliongea na kisha akakaaa
“Vipi kuhusu Miss Regina , wewe unasemaje?”
“Vazi langu ni mtindo toleo la mwisho kutoka Zara”Aliongea na Fellini alitingisha kichwa.
“Najua kabisa ndio ni kutoka Zara , mimi ndio nilihusika na ubunifu wake, tulilipatia jina la Norse Goddes style , limekupendeza mno ulivyovaa ni kama tulikutengenezea wewe peke yako”
“Kweli… kwahio staili yake ndio inaitwa Norse , sikuwa hata nikijua , kwa macho yangu mimi ni gauni kama gauni tu, nimenunua kwa zaidi ya Euro elfu ishirini na tatu , lakini sokoni kuna staii hii hii bilaBrand ya Zara na wanauza kati ya milioni moja mpaka tano, kwangu mimi niliona ni vazi linalonipendeza na nikalipenda mno ndio maana nimelivaa lakini sababu nyingine niliamini kuvaa mavazi ya kampuni ya Zara itatuweka karibu zaidi kibiashara”
Mara baada ya kumaliza Fellin alishangaa hata kwa Linda alikuwa amekakamaa mwili wakati wa maelezo ya Regina.
Upande wa Hamza na sikio lake kama antenna za kisimbuzi cha Zuku aliweza kusikia kila kitu na alionekana kumkubali Regina , aliona ni kama kuna kitu ameelewa katika maelezo yake.
“Mr Fellini nadhani sasa umeona , Regina kila anachoongea ni katika msingi wa kibiashara , huyu ni mashine ya kutengenezea hela na hajali chochote zaidi ya faida , hawezi kujua thamani halisi ya vazi nje ya gharama yake”
Fellini upande wake alionesha kukatishwa tamaa kabisa na Regina na kulikuwa na ishara ya kukereka katika macho yake.
“Miss Regina nimependa ulivyomuwazi”
“Asante sana Mr Fellini , natumaini siku zijazo utajifunza pia kutoka kwangu na kuwa muwazi, maana umekuja nchini ukiwa tayari na mpango wa kufanya kazi na kampuni ya Salah na sio sisi , hivyo sidhani kulikuwa hata na haja ya kukutana”
“Hapana, umenielewa vibaya , sijafanya maamuzi kabla”Aliongea Fellini akijitetea.
“Kutoka mwanzo mpaka mwisho ulikuwa ukiongelea maswala ya utamaduni wa kampuni na sera ila hukuniuliza hata swala la soko lilivyo na mtaji kiasi gani tulipanga kuwekeza kwenye ushirikiano wetu , unajua kabisa nimesomea maswala ya uchumi , masoko na usimamizi , lakini mmeanza na kuongea nadharia zenu za fasheni na mambo mengine ambayo yapo nje ya taaluma yangu , unanilinganisha na Salma ambae amesoma chuo kikubwa dunniani cha mitindo na kazi yake ni ubunifu wa mavazi , ulichofanya ni kama kutengeneza mazingira ya kampuni ya Salah kushinda na si vinginevyo”
Mr Fellini mara baada ya kusikia kauli hio alijikuta kwa namna flani akiona aibu lakini alivuta moshi wa sigara kidogo kujituliza.
“Kama ndio unavyoamini basi sidhani kuna haja ya kuendelea na haya mzungumzo , kwa bahati mbaya hatuwezi kushirikiana na kampuni yako”
“Nashukuru hujachagua kampuni yetu kwani nisingependa kuishi katika ulimwengu wa kufikirika na mshirika mnafiki”
“Unasemaje , mimi ni mnafiki?”Aliongea mzungu yule huku uso wake ukijikunja .
Alikuwa maarufu kwa zaidi ya miaka ishirini sasa na kila mtu alikuwa akimheshimu lakini leo hii anatukanwa na msichana mdogo kutoka taifa masikini kama Tanzania.
Upande wa Regina hakujali tena kuhusu hasira za Fellini alimpa ishara Linda na kisha walisimama kuondoka.
“Regina simama hapo hapo”Alifoka Salma.
“Unaonyesha tabia gani mbele ya mtu mwenye heshima zake kama Fellin , unadhani ni mtu unaeweza kumtusi hivi hivi tu , omba msamaha kabla hujaondoka
“Miss Regina nakuhakikishia utalipa kwa dharau ulizonionyeshea, usisahau mikataba ulioingia na baadhi ya kampuni za mavazi tunamiliki hisa zetu pia”
Regina alisimama na kisha aligeuka , macho yake ya kirembo yalikuwa na ukauzu usiokuwa wa kawaida. “Kwahio mnajaribu kuniogopesha na kunitishia?”
“Kwahio vipi , ulimwengu wa mitindo sio mtu wa hadhi ya chini kama wewe unaweza kuingia unavyotaka”Aliongea Salma.
“Vyovyote vile , mwisho wa siku sio mimi nitakae anguka bali ni mtu mwingine”
Mara baada ya kumaliza kauli hio sauti ya mtu akipiga makofi ilisikika , alikuwa ni Hamza.
“Vizuri sana , hakika bosi wetu una ujasiri wa hali ya juu,Awesome”Aliongea Hamza huku akicheka akisogea karibu.
Regina na Linda waliishia kushangaa , ni kama sasa wanakumbuka Hamza alikuwa hapo , akiwa kimya tu akisikiliza.
“Wewe ni nani?”Aliuliza Salma huku akikunja mdomo.
“Kwa majina yangu naitwa Hamza Mzee , Msaidizi namba mbili wa bosi Regina , kuwa sahihi zaidi unaweza niita dereva wake”
“Haha.. Dereva, Hamza!!”Salma alicheka kwa nguvu kwa kejeli.
“Regina vigezo vyako ni vya chini mno , yaani umemuajiri mshamba kutoka porini huko kuwa dereva wako?, nadhani maamuzi ya Mr Felllini ni sahihi kabisa , kufanya kazi na mtu asiezingatia hadhi ya wafanyakazi wake ni kujidhalilisha tu na kushusha thamani ya Brand ya kampuni”Aliongea na kisha alimwangalia Fellini kama anamsapoti katika dhihaka zake.
Lakini upande wa Fellini alikuwa akimwangalia Hamza kwa macho kodo kana kwamba alikuwa ameona mzimu, alikuwa ameshikwa na bumbuwazi ashindwe kusema neno.
Hata kwa Regina waliona muonekano wa Fellini , alionekana kama ni mtu mwenye wasiwasi.
“Nini tatizo Mr Fellini , huyu mshamba kakuogopesha?”Aliongea Salma.
“No ,, impossible”Aliongea Fellini akisema haiwezekani huku akimsogelea Hamza karibu.
Mara baada ya kumfikia alishindwa kujizuia na kunyoosha mkono wake na kushika kolla ya nguo alizovaa Hamza.
Cha kushangaza ni kwamba mikono yake ilikuwa ikimtetemeka kana kwamba ameshika kitu cha thamani sana.
“Mr Fellini umepatwa na shida gani?”Aliuliza Salma asijue kwanini huyo mzungu alionekana kama vile amepandwa na wazimu.
Regina upande wake pia alikuwa kwenye hali ya kushangaa na alijiuliza au Fellini alikuwa amevutiwa na uchakavu wa tisheti ya Hamza
“Wewe Mzungu vipi , acha kunigusa bwana mimi sio bwabwa”Aliongea Hamza na kumzuia Fellini kwa kumshika mkono.
“Umesema unaitwa Mr Hamza si ndio , naomba nikuulize swali , umezipata wapi hizi nguo ulizovaa?” “Kuna mzee ambae ni rafiki yangu alinnipatia kama zawadi , ni miaka mingi kidogo imepita”Alijibu Hamza.
“Mzee rafiki yako , unaweza kunitajia jina lake?”Aliuliza na kumfanya Hamza kukunja kichwa.
“Mimi napenda kumuita Mzee Roboti , ila jina lake lote ni Alec sijui nini”
“Ni Alec Von Blumer sio”
“Ewaaa.. hilo ndio jina lake yule mzee , amenipa nguo nyingi sana kama zawadi, ni mkarimu sana haha..”
Mara baada ya kusikia hivyo Fellini alijikuta akijikokota kurudi nyuma kwa mshangao na alijitahidi kujiegamiza kwenye sofa asidondoke
“Mr Fellini what wrong?” Aliuliza msaidizi wake huku Salma na Regina wakiwa wameshangazwa pia na tukio hilo.
Fellini kwa haraka haraka alichukua glasi ya maji na kuigida yote na kuiweka chini akijitahidi kujituliza.
“Master George Alec Von Bliimer ndio mwalimu wangu , kwa maneno mengine ndio mbobezi …”Mara baada ya kuongea hivyo Regina , Linda na Salma walishikwa na mshangao wa kutokuamini.
“Mr Fellini si umehitimu kutoka chuo cha sanaa cha London , kwanini unasema una mwalimu wako?”Aliuliza lakini Felini alimdharau Salma kwa ujinga.
“The real art of clothing is not in any Academy , but in Seville street , Miss Salma haven’t you heard about it ?”Aliuliza Fellini.
“Najua ndio , Sevile ni mtaa uliopo ndani ya London Mayfair , sehemu wanapopatikana mafundi nguo maarufu , hususani mafundi wa nguo za kiume, ukisikia neno ‘Customized clothes’ asili yake ni katika mtaa huo, wafalme na viongozi wakubwa duniani walipendelea sana wazo la kushonewa nguo zinazoendana na wao katika mtaa wa Sevile , maduka mengi ndani ya Sevile yana historia ya karne kadhaa”Aliongea Salma.
Ilikuwa ni kweli kabisa, kama ilivyokwa mtu wa kawaida kupendelea kwenda kwa cherehani kushona suti inayoendana na vipimo vya mwili wake basi ipo hivyo hata kwa matajiri na viongozi wa daraja la juu ikiwemo wafalme wa mataifa makubwa.
Sasa mtaa wa Seville ndani ya London Mayfair ndio kunapatikana mafundi cherehani ambao hushona nguo hizo za watu wazito wazito.
Regina hata yeye ashawahi kusikia kuhusu Seville lakini hakujua hadhi ya mtaa huo ilivyo.
“Upo sahihi , tokea nilipokuwa mtoto ndoto yangu ilikuwa ni kuja kuwa mbunifu wa watu wazito wazito duniani , hivyo niliweka bidii na hatimae nikaja kufanikiwa kuingia mtaa wa Seville kama mwanafunzi wa ufundi cherehani na mbunifu , nilijifunza ufundi kwa mwalimu wangu George na hatimae nikawa fundi wa daraja la chini kigezo ambacho kilinifanya kushindwa kuendelea kuwa chini ya George , ni kwasababu sikuwa na kipaji kikubwa cha ushonaji , hivyo mara baada ya kutopata nafasi
zaidi niliamua kuachana na maswala ya ushonaji
nikaingia chuo “
“Nini, Mr Fellin mbona unakipaji kikubwa mno , unasemaje huna kipaji”Aliongea Salma.
“Salma unaweza ukwa umemaliza kwenye chuo kikubwa na ukawa mbunifu wa kimataifa lakini huwezi kufikia hadhi ya mwalimu wangu George , wateja wake ni wafalme , malkia , Watoto wa wafalme na Princess au watu matajiri duniani na wanasiasa wakubwa, hahitaji umaarufu wowote ndio maana wengi hawamfahamu , unadhani ana haja gani ya kutengenezea nguo watu wa kawaida , ki ufupi muda huo hana ndio maana hajawahi kujitangaza”
Maneno yale yalimsahgnaza Salma , Fellini alikuwa mtu mzito kwenye ubunifu lakini kulikuwa bado kuna watu wa hadhi ya juu kuliko yeye, liishangaza zaidi na zaidi.
Tatizo hapo sasa sio swala la huyo anaeitwa mwalimu kushonea nguo watu wazito , tatizo ni kwamba Hamza alikuwa amevaa nguo ambazo zimetengenezwa na mtu huyo.
Regina na Linda hawakutaka kukubali kirahisi , kwani dakika chache zilizopita walikuwa wakibeza mavazi ya Hamza.
Walijikuta wote wakiangalia mavazi ya Hamza lakini bado yalionekana ya kawaida mno , aina ya mavazi ambayo unaweza ukayakuta katika soko la mtumba .
Regina alienda mbali na kukumbuka aligombana na Hamza kwa kutotaka kutupa mavazi yake , alishindwa kuzuia hisia mbaya zilizoanza kumvaa na kujiambia kama kweli anachosema Fellini ni kweli basi mavazi hayo ya thamani si yatamfanya aonekane mjinga na mshamba.
“Mr Fellini macho yako yatakuwa yanakudanganya , haya mavazi aliovaa unaweza kuyakuta kila mkoa ndani ya Tanzania yanauzwa”Aliongea Regina kuepusha kuabika.
“Msiniambie hakuna ambae anaona uzuri wa mavazi aliovaa Mr Hamza pamoja na pensi yake?”Aliongea huku akiwaangalia mmoja mmoja kana kwamba anaomba kuungwa mkono.
Lakini wote walitingisha vichwa vyao kukataa , hakuna cha maana kwenye hayo mavazi zaidi ya uchakavu tu”
“Nyie watu hamjui kabisa , nadhani kwasababu sio mafundi, katika ulimwengu wa kifundi utaalamu wa juu zaidi ni kutengeneza vazi ambalo unao uwezo wa kulirudisha upya kwa mchakato mwepesi sana na ukauza sokoni kwa bei ileile”Aliongea mzungu huyo lakini hakuna hata mmoja ambae alielewa anachomaanisha, hata Salma aliesomea Person chuo namba moja cha mitindo kutoka Marekani hakuelewa.
MWISHO WA SEASON ONE.
Unadhani Hamza ni nani mpaka kuvaa nguo zilizotengenezwa na George Alec Von Blumer fundi nguo wa wafalme , matajiri na watu wa hadhi ya juu.
Unadhani Hamza ana siri gani tokea kuokolewa kutoka kwenye janga la Radi mpaka kuwa nchini Tanzania akiwa mtu mzima.
Vipi kuhusu kitabu kinachowindwa na watu , vipi kuhusu lugha iliokuwa katika kitabu hicho ambayo hakuna binadamu anaeijua , unadhani ni kweli Hamza anao uwezo wa kuijua lugha hio, Frida anamaanisha nini kusema Hamza kuna kumbukumbu hazikumbuki.
Unadhani Binamu ni Cousin mtoto wa Mjomba au
Shagazi au ni kitu kingine tofauti, vipi Sinagogi ni watu gani.
Wakuu ndio tunaanza yani , kuna siri nzito sana katika hii simulizi , Kodi nyingi zitatumika.
Comments