Kwa Ajili ya Upendo – Sehemu ya Kwanza
Vumbi lilikuwa limejifunika kila kona ya mji. Majani ya miti mikavu yakiyumbishwa na upepo wa jioni yalitoa mlio wa kusinzia, kana kwamba yalihisi uzito wa siri iliyokuwepo ardhini. Mji huu ulikuwa umejengwa juu ya ardhi ya chumvi, lakini watu wake walikuwa wamezoea kuitazama kama utajiri, si laana. Na katika jicho la vumbi hilo, kijana mmoja alikuwa anawasili – kwa mara ya kwanza – bila kujua kuwa hatima yake ingetikisa ngome nzima.
Aliitwa Sefu – kijana kutoka kijiji cha mbali cha Mwikala, aliyetembea zaidi ya siku tatu kwa miguu, akifuatilia alama za ndoto aliyokuwa akiota kila usiku kwa miaka mitano mfululizo. Ndoto za mji wenye ngome kubwa, lango la chuma, na sauti ya msichana anayelia kutoka kwenye mnara wa mawe meupe. Sefu hakuwahi kumwona msichana huyo machoni, lakini kila aliposikia kilio kile, moyo wake ulihisi kama umebanwa. Kitu kilikuwa kinamuita.
Aliposimama mbele ya lango la mji – lango la Ngome ya Chumvi, kama walivyoita wenyeji – aliinua macho na kuona maandishi ya kale yaliyochongwa juu ya mlango: "Mwenye kuingia, aache tamaa."
“Mzee wangu, hii ndiyo Dodoma au nimepotea njia?” aliuliza kwa sauti ya ukatiza upepo, akimwambia mlinzi aliyekuwa ameegemea mkuki wake kwa mkao wa uvivu.
Mlinzi alimtazama toka juu hadi chini, macho yake yakicheza na mavumbi yaliyomfunika Sefu. “Dodoma si jina la wote, mdogo wangu. Ulitaka kuja, sasa uko. Karibu. Kama moyo wako hauogopi.”
“Yaani kuna watu humu wanaingia huku mioyo ikiwa imetulia?” Sefu alijibu huku akipiga kicheko cha mtaa. “Mi hata sijui kilichonileta, lakini moyo wangu umekataa kukaa kijijini tena.”
Mlinzi hakujibu. Alimpisha kijana huyo aingie, lakini akamkazia macho kwa muda mrefu, kana kwamba alimjua kutoka zamani – au alihisi kuwa huyu si mgeni wa kawaida.
Ndani ya mji, mitaa ilijaa watu wa aina mbalimbali: wachuuzi wa asali ya nyuki wakijaribu kuuza kwa sauti za kutongoza, wanawake waliovaa vitambaa vyeusi wakipita kwa haraka kama wakienda mahali pasipo na majina, na watoto waliocheza kwa vumbi bila viatu huku wakigombania gari ya waya. Harufu ya viungo, jasho, na maisha ilijaa hewani. Sefu alijikuta akivutwa zaidi.
Alipotembea kuelekea sokoni, akakutana na kikundi cha watu waliokuwa wakisikiliza hadithi ya mzee mmoja aliyevaa kaniki nyeusi na kuwa na macho yaliyong’aa mithili ya mwewe. “Alifika usiku wa mwezi mweupe, akiwa na alama ya maji kwenye paji lake,” mzee huyo alikuwa akisema. “Na aliposema jina lake, milango ya ngome ilijifungua yenyewe.”
Wote walikaa kimya. Mzee akatazama moja kwa moja kwa Sefu, kana kwamba alikuwa anasoma moyo wake. “Huja wa kawaida anakuja. Atabadilisha mji huu kwa damu au kwa upendo.”
Sefu alihisi baridi kupitia mgongo wake. Alitaka kusogea lakini miguu yake ilikuwa mizito. Hii haikuwa ndoto tena – ilikuwa ni kweli.
Usiku huo, akiwa katika nyumba ya kulala wageni iliyo karibu na uwanja wa wazi, ndoto ile ile ilimjia tena. Sauti ya msichana. Kilio. Mnara mweupe. Lakini sasa, msichana aligeuka. Alikuwa na macho ya maumivu, lakini pia ya matumaini. Alimwambia kitu kwa mara ya kwanza.
“Njoo unisaidie... kwa ajili ya upendo.”
Sefu alishtuka. Alikuwa analowa jasho. Nje ya dirisha, mwezi ulikuwa mweupe – kama kwenye ndoto.
Comments