Kwa zaidi ya dakika ishirini au therathini hivi hakuna aliemuongelesha mwenzake , Regina alidhania Hamza angempa sababu japo kidogo tu ya kutuliza shauku yake , alitamani kusikia hata kisingizio tu pengine angeelewa lakini licha ya hivyo Hamza alikuwa akiendesha huku akipiga ukimya.
“Huna kitu chochote cha kuniambia?”Aliuliza Regina baada ya kukosa uvumilivu na kumfanya Hamza kuangalia kioo cha nyuma.
“Ni kweli asubuhi nilikuwa na dharula muhimu , ningechelewa kidogo kungekuwa na tatizo , alikuwa ni mteja wangu alienipigia , sikutaka kumpotezea”Aliongea Hamza lakini Regina hakuwa hata na haja ya kusikiliza hizo porojo.
“Sitaki kusikia kuhusu hilo , kwanini hukuniambia unafahamiana na huyo Master Alec?”
“Ah.. Unamzungumzia mzee Roboti , kwanini nimzungumzie sasa bila sababu?”
“Wakati ule nilikuambia ukatupe mavazi yako lakini ukang’anania kubaki nayo , kwahio ulikuwa ukinikejeli kisirisiri kwa kuwa mshamba sio , unaonekana kabisa umeisubiria kwa hamu hii siku kwa ajili ya kuniumbua mbele za watu, sasa hiivi nadhani unajichekea mwenyewe moyoni kwa raha zako”Aliongea huku akionyesha kinyongo.
“Regina unaongea nini , sikufikiria sana wakati ule ni kwamba tu nimezoea haya mavazi ndio maana, ni zawadi kutoka kwa mzee , isingekuwa vizuri kuyatupa ilihali aliweka moyo wake wote kwenye kuyatengeneza”
“Basi niambie wewe na huyo Master Alec mnafahamina vipi?”
“Nilikutana nae Shardland Bar huko Uingereza kipindi flani hivi cha mwaka mpya na ndio tulianza kuongea kwa kubishana na urafiki wetu ukaanzia hapo”
“Unaniona mjinga , unadhani naweza kuamini huo uongo , mbona unapenda kuniona kama kichekesho?”
“Ananiona mjinga huyu sijui yukoje , yaani mtu amemtisha Fellini vile lakini sasa hivi anasema amekutana nae bar “Aliwaza Regina huku akiwa na hasira kali.
Muda uleule wakati washafika Kigamboni Hamza alisimamisha gari pembeni na kumshitua Regina aliekuwa kwenye mawazo.
“Wewe .. unafanya nini?”Aliuliza lakini Hamza hakujibu zaidi ya kufungua mlango na kutoka nje na kutembea upande wa madukani, Regina na yeye hakutaka kukaa ndani ya gari , alishuka na kumfuata huko huko na kufanya watu kumkodolea macho kutokana na urembo wake.
Baada ya kumfikia Hamza alimuona akiwa amesimama mbele ya Freezer akichagua Ice Cream za Bakhresa na alichukua yenye Strawberry na kumpa Regina ambae aliipokea bila kupenda.
“Unafanya nini sasa?”
“Mrembo maswali mengi ya nini , huoni hio ni Ice Cream”Aliongea na muda huo Hamza alichukua na ya kwake ya ukwaju na kisha akaenda kulipa na sasa hapo ndio Regina alijua kumbe huyu mwehu kaja kununua Ice Cream.
“Acha kusimama hapo twende , tumeegesha gari sehemu mbaya , hata kama una hela huwezi vunja sheria za barabarani”Aliongea Hamza na kumshitua Regina ambae alikuwa kwenye mshangao.
“Nani kakuambia nina shida ya Ice Cream , jali mambo yako”
“Kama hutaki ilete basi ninao uwezo wa kula zote mbili kwa pamoja”Aliongea Hamza akijaribu kumpokonya lakini Regina alipindisha mkono mbali.
“Unasema huitaki , nataka kuichukua unaktaa , nyie wanawake ni viumbe wa ajabu sana”
“Unasemaje wewe…”Aliuliza Regina lakini Hamza
alijifanyisha mjinga na kumuacha Regina akiwa amesimama
Wateja baadhi na watu wauza maduka waliishia kutabasamu , kwani walionekana kama wapenzi.
Hamza mara baada ya kuingia garini aliliwasha na kupiga honi na kumfanya Regina kwa hasira kukimbilia na kuingia.
Baada ya wote kuingia kwenye gari na Hamza kulirudisha kwenye barabara aliendesha kwa mkono mmoja huku mwingine ukishikilia Ice Cream , Regina hakuuliza tena swali , aliona hata akiuliza kusingekuwa na majibu hivyo alijikaliza zake kimya , huku akila Ice Cream kwa kutumia kijiko
Kama alivyosema Hamza wanawake hawaeleweki , Kwa Regina ilikuwa hivyo hivyo kulikuwa na wanaume kibao ambao washawahi kumtongoza kwa kumpatia zawadi kama vile magari , vito vya thamani na ahadi kibao , lakini kitendo cha Kununuliwa Ice Cream ndio zawadi ya thamani ya juu iligusa moyo wake.
Wakati wanafika nyumbani Shangazi alikuwa sebuleni akiangalia TV, na hata walivyoingia hakuweza kuwaona.
“Shangazi unaangalia nini , mpaka kuwa siriasi hivyo?”Aliuliza Regina.
“Taarifa ya habari , wanasema kumekuwa na mauaji mfululizo ya wanawake ndani ya jiji la Dar es saalam na muuaji hafahamiki hivyo wanaasa raia kuwa makini, Regina uwe makini , ukitoka kazini hakikisha uwe na Hamza pembeni yako , wakati wa mchana usitoke peke yako pia”
Hamza aliangalia taarifa hio ya habari na alishangaa na kuona namna muuaji alichokuwa akifanya , tofauti na kuua tu alikuwa pia akikata maeneo nyeti ya wanawake kama vile manyonyo na ngozi, yalikuwa mauaji ya kikatili mno.
“Muuaji wa namna hii muda si mrefu atakamatwa , shangazi huna haja ya kuwa na wasiwasi sana”
“Natamani wakimuona wampige risasi wamuue kabisa , jamani mtu anaua watu wasio na hatia kikatili namna hio , tena wasichana wadogo”Aliongea Shangazi na muda huo huo kengele iligonga ikionyesha kuna mgeni.
Shangazi alienda kufungua mlango wa geti na alishangaa baada ya kuona ni Polisi.
“Ndugu polisi kwanini…”
Walikuwa ni Polisi wanne wote wakiwa katika sare zao za kipolisi , aliekuwa mbele alikuwa na uso ulichongoka na mweusi Tii.
“Mama hapa ni nyumbani kwa Regina Wilson?”
“Ndio , upo sahihi , mnamtafuta?”
“Naitwa Afande Mlonga kutoka kituo cha polisi mjini kati idara ya uchunguzi , kuna kesi inayomhusu Regina Wilsoni na tupo hapa kwa uchunguzi”
Muda uleule Regina alikuwa ashatoka nje baada ya kuona Shangazi harudi na mara baada ya kuona ni polisi alimwambia shangazi awaruhusu.
Polisi wale walikaribishwa mpaka ndani sebuleni huku wakiangaza angaza kulia na kushoto kwa namna ya kuchunguza uzuri wa jumba hilo kabla ya kukaa kwenye sofa.
Shangazi kwa haraka hraka alikimbilia friji na kuwaletea maji kama walivyoomba , lakini alikuwa na wasiwasi mno kiasi cha mikono yake kutetemeka.
Afande Mlonga macho yake yalikuwa kwa Hamza tu , ni kama alikuwa akimchhunguza , upande wa Hamza alikuwa zake bize akitafuna ma’apple’.
“Miss Regina naomba kuuliza huyu Mr hapo ni nani kwako?”Aliongea Mlonga na swali lile lilimfanya Regina kusita lakini kutokana na uwepo wa Shangazi aliamua kuongea.
“Ni mpenzi wangu”
Baada ya kujibu hivyo Afande Mlonga na wenzake ni kama hawajatarajia jambo hilo.
“Tulisikia habari nyingi unaenda kuolewa na mtoto wa Mzee Benjamini , hatukutarajia kuona tayari una Boyfriend”
“Naona taarifa zangu zinazagaa sana lakini hili linanihusu mimi na yeye , sikuona haja ya kuliweka wazi, sidhani kama ni kosa?”
“Hakuna mgongano wowote baada ya hili na familia ya Mzee Benjamini?”Aliuliza Mlonga huku wakionyesha kunakiri majibu.
“Nyie wote ni polisi , sidhani ni vizuri kuuliza maisha yangu binafsi”
“Usituelewe vibaya Madam , ni kwasababu kilichotuleta hapa kina uhusiano na maisha yako binafsi”Aliongea na muda uleule Afande Mlonga aliweka picha chini , zilikuwa ni za gari ya Regina.
“Hili gari limesajiliwa kwa majina ya Regina
Wilsoni ambapo tunaamini wewe ndio mmiliki halali , juzi limeonekana katika kijini cha Wavuvi Zinga bagamoyo na Dereva aliekuwa akiendesha gari hio ni moja ya mhangwa wa mauaji.. wakati wa kurudi gari ilikuwa ikiendeshwa na huyu mwanaume ambae umesema ni Boyfriend wako”Aliongea huku akiweka picha ya Hamza akiendesha gari hio hio na gari ikiendeshwa na mwanamke, alikuwa ni Corresa.
Regina mikono yake ilicheza na bila hata kujijua alihikilia sketi yake , akiwa na wasiwasi, mwanamke aliekuwa kwenye picha alimfahamu ni moja ya watekaji.
“Kwahio amekufa?”
“Kwanini unauliza , inamaana hujui kama amekufa, tunaamini watu wote waliokufa walikuwa ndani ya gari lako”
Regina aliishia kugeuza kichwa chake na kumwangalia Hamza lakini upande wa Hamza hakuonyesha wasiwasi kabisa , lakini kwake aliona hio kesi sio nyepesi, baada ya kufikiria kwa muda Regina aliona aeleze moja kwa moja kilichotokea.
“Nilitekwa siku hio , lakini sikujua watu wale walikuwa ni wakina nani maana walikuwa ni raia wa kigeni , nilikuwa sina fahamu na pale niliposhituka nilikuwa nishaokolewa tayari na Hamza , kuhusu watu hao kufa sikuwa nikijua chochote”
“Kwahio unamaanisha huyu Mr Hamza ndio aliekuokoa na baada ya hapo akawaua hawa wahalifu?”
“Ma afande mnakosea , sijaua mtu , mimi nilienda nikawapa kichapo tu , sidhani kama mnaweza kunilaumu kwa hilo”Aliongea Hamza lakini Regina aliona hali inazidi kuwa mbaya na alitaka kutumia nguvu yake hivyo alisimama.
“Afisa mna ushahidi wowote wa kuonyesha Hamza ndio aliewaua?”
“Usipaniki Madam , hata kama Mr Hamza ndio aliehusika sio kosa , kwasababu hawa wahalifu ni kama Mr Hamza tu , lakini tunahitaji kuchunguza hili swala, tunataka kujua imekuwaje Mr Hamza akawa na uwezo wa kuua hawa wahalifu wa daraja la juu , wanaosakwa dunia nzima”
“Mimi ni mwanafunzi wa chuo na fundi , nina nguvu nyingi hivyo mapigano yalikuwa makali sana , lakini sijua mtu”Aliongea Hamza.
“Mr Hamza tunakuahidi hatutokutia hatiani kwa kuuwa hawa watu , tunachotaka kujua ni kilichotokea katika mazingira ya kirafiki tu”AliongeaMlonga huku akiwa na tabasamu bandia.
“Kama mnao ushahidi wa kutthibitisha niliwaua basi nitawaelezea kilichotokea , lakini ushahidi hamna na mpo hapa mnanijaribu siwezi kuwaambia chochote”
Polisi hao walijikuta wakiwa kimya , alichoongea Hamza kilikuwa na ukweli ,hata hivyo kesi haikuwa chini yao , baada ya kesi hio kutolewa ktuoka kitengo cha MALIBU na kuhamishiwa idara ya polisi Afande Mlonga ndio alipewa kazi ya kuongoza uchunguzi , lakini licha ya kupata picha hakukuwa na alama za vidole zinazomlenga moja kwa moja Hamza ndio alifanya mauaji.
“Afande Mlonga kama hakuna ushahidi siwezi kukubali mpenzi wangu kusingiziwa , kama kuna ambacho nitaweza kufanya kwasasa ni kumshirikisha mwanasheria wangu ili muongee nae yeye , hivyo naomba muondoke nyumbani kwangu na mkatafute Warantt kwanza”
“Madam , mpaka sasa nadhani umeona taarifa ya habari inayohusisha muuaji anaeua wasichana wadogo kwa kuwakata viungo vya siri , unadhani
ni salama kwako kukaa na mtu ambae humjui vizuri”
“Chunga maneno yako afande , chochote utakachoongea bila ushahidi nitakushtaki nacho”Polisi wengine walitaka kuongea lakini Afande Mlonga aliwazuia.
“Kama ni hivyo basi hatuna haja ya kukaa zaidi na tutaondoka , ila kama kuna ushahidi tutarudi”Aliongea na kisha wote kwa pamoja walitoka nje.
“Regina nini hiki kinaendelea , ulitekwa?”Shangazi ndio aliekuwa akiuliza huku akionekana kuwa na maumivu ya moyo.
“Shangazi sikufanya makusuti kutokukuambia , sikutaka kukufanya kuwa na wasiwasi , lakini lishaisha”Aliongea na Shangazi aliishia kuvuta pumzi huku akijikalia kwenye sofa.
“Asante Mungu angalau amekukutanisha na Hamza angalau anaweza kukulinda, ningefanya nini mimi kama ningekuwa peke yangu”Aliongea Shangazi akijituliza lakini wakati huo Regina alimwangalia Hamza kwa macho ya kuchukia.
“Sijui kama umeua au hujaua , lakini hili swala linapaswa kuisha ukiwa hujaua”Aliongea. “Haha.. Regina asante sana kwa kunijali”
“Eti kukujali , sitaki kuhusika katika hili ndio maana , nina kazi nyingi za kufanya”Mara baada ya kuongea hivyo kwa hasira alipandisha juu huku akifunga mlango kwa nguvu.
Upande wa Shangazi alimwangalia Hamza kwa macho yenye umakini mkali , ni kama kuna kitu anakitafuta.
“Hamza hukupata tatizo?”Aliuliza.
“Shangazi usiwe na wasiwasi ni swala dogo na lishaisha”Aliongea na Shangazi alitingisha kichwa kuelewa.
“Naona unatafuna sana matunda , kama hamjala mchana niwaandalie chochote”
“Hakuna shida shangazi”
*****
Upande mwignine mara baada ya mafande wale kutoka walisogelea gari ya Land Cruiser na kuingia ndani , kulikuwa na watu wawili ndani ya gari hio tayari , mmoja akiwa dereva na mwingine akiwa ni mwanaume mnene hivi mwenye kitambi aliekaaa nyuma.
“Kanali , tumemaliza mahojiano nae , lakini mambo yamekuwa magumu kuliko tulivyotarajia”Aliongea Mlonga akimwambia yule mzee aliekuwa kwenye gari.
“Nini kimetokea?”
“Amekataa yeye kutohusika kabisa , cha kushangaza sio dereva wala mlinzi tu ni Mpenzi wa bosi Regina”
“Nini , mpenzi!!, Sio James tena”
“Hata sisi tumeshangaa , inaonekana kuna kinachoendelea , lakini sidhani kama kinahusiana na hii kesi”Aliongea Mlonga na kumfanya mwanaume alieitwa Kanali kufikiria kidogo.
“Mlonga nakuamini uwezo wako wa kumjua mtu kwa kumwangalia tu , wewe unamuonaje , unadhani ndio aliehusika kuua watu hatari kama wale?”
“Dastani sijui hata namna ya kumuelezea , ukiachana na ushombeshombe wake nimemuona kama mtu wa kawaida sana… lakini kuna kitu sio cha kawaida nimekiona”Aliongea.
“Kitu gani mmekiona?”
“Hakupaniki kabisa , ni kama vile alitarajia ujio wetu na wala hakuonyesha kukasirika hata tulivyomwambia ameuwa watu wale , ki ufupi hakuonyesha kuwa na wasiwasi wakati tunamuuliza maswali, lakini ukiachana na hilo sioni kama ni mtaalamu , anaonekana kama vile ni mfanyakazi wa kawaida tu wa kwenda kazini na kurudi nyumbanni kuangalia TV”Aliongea na Kanali Dastani alionekana kuwaza.
“Kanali hii kazi haiwezi kuwa rahisi kama ikiendelea kuwa chini ya Idara ya polisi , Kitengo cha MALIBU kina kila rasilimali ya kufanikisha hili”Aliongea Mlonga.
“Unadhani hatujui kuhusu hilo , unadhani kwanini sikutaka kuambatana na nyie moja kwa moja kwenda kufanya mahojiano nae , hizi ni taratibu za kitengo pia katika hatua za ki uchunguzi”
“Mkuu unamaanisha na nyie mnaendelea na uchunguzi kimya kimya?”
“Mlonga licha ya kwamba upo vizuri kwenye mahojiano lakini kuna baadhi ya sehemu haupo vizuri , Ni lini ushawahi kuona MALIBU wakimhoji raia moja kwa moja , tunatumia idara ya polisi kufanya kazi hii , hivyo mlichofanya ni kutimiza wajibu wenu na sisi tutatimiza wajibu wetu”Aliongea na Mlonga alitingisha kichwa kukubali
“Ila Kanali kama kweli ndio amehusika na mauaji ya maninja kutoka Ufilipino basi ni mtaaamu wa hali ya juu na atakuwa ameficha ushahidi wa sisi kumfikia , hivyo uchunguzi chini ya idara yetu utakuwa mgumu kweli”
“Kama unahisi hivyo , basi atakuwa haogopi hata tukiwa na ushahidi kuna kinachoniambia sio wa kawaida”Aliongea moja ya polisi akitoa mchango wake.
“Kama ulivyosema ni sahihi , unadhani kwanini hakukuwa na alama yoyote hata ya vidole tu kuonyesha yeye ndio muuaji , alionekana kuwa makini , hata kama ameonekana kwenye gari ashajiandaa namna ya kujitetea”
“Kanali kwanini tusimkamate moja kwa moja , kuna uwezekano akawa na uhusiano na mauaji ya wanawake yanayoendelea”
“Hatuwezi kwenda moja kwa moja kwenye hitimisho , iwe yeye ndio muuaji au sie kama polisi mnapaswa kuendeleza uchunguzi wetu na kuwe na ushahidi , muuaji lazima akamatwe na haya ni maagizo kutoka juu , mkitimiza wajibu wenu na sisi wa kwetu kazi itakuwa rahisi , Mlonga hili lipo juu yako na timu yako, Ondoa gari napaswa kwenda kuripoti makao makuu”Aliongea Kanali na gari iliendeshwa muda uleule.
Nusu saa tu Kanali Dastani alikuwa akiingia katika kitengo cha MALIBU makao makuu , na alipiga hatua zake kana kwamba hataki kufanya watu wajue amefika.
Hakuelekea moja kwa moja katika ofisi ya mkuu wake bali alienda moja kwa moja katika ofisi yake , alitaka kukusanya ripoti kamili kabla ya kuiwasilisha.
Siku kadhaa nyuma alipewa kazi ya kuhakikisha anajua ni nani aliehusika katika kuuwa wale raia wa kigeni na kazi hio alikuwa ameifanya kwa uadilifu mkubwa mpaka kumpatia majibu aliokuwa akitaka.
Mara baada ya kufika katika ofisi yake aliingiza nywira katika tarakishi yake na palepale ilionekana Vidio ambayo ilionekana ilikuwa ikicheza lakini ikasitishwa kwa muda.
Kanali mara baada ya kukaa kwenye kiti aligusa batani na palepale Vidio ile ilianza kuonyesha Kapteni Yonesi akipigana na Master Konki na kudhibitiwa na ghafla tu Hamza anaingilia na kumuadhibu Master Konk.
Aliichezesha kwa kuirudisha mbele na nyuma kwa zaidi ya mara tano na alionekana kufikiria kitu.
Baada ya kukaa kwa muda katika ofisi yake , ujumbe wa meseji uliingia kupitia watsapp na alipoona jina lililomtumia ujumbe huo alifungua haraharaka na alikuta kuna kiambatanisho cha nyaraka iliokuwa katika mfumo wa PDF.
Kwa haraka haraka aliihamishia kwenye tarakishi yake na kisha akaigeuza nyaraka ile kwa kuiprint, kadri alivyokuwa akiisoma ndio jinsi uso wake ulivyojikunja.
“Hamza ndio muhusika , nina uhakika asilimia mia moja , kabla ya ripoti ngoja nikutane na Yonesi kwa siri kwanza”Aliongea na kisha palepale alizima tarakishi yake na kuchukua karatasi alioprinti na kujiandaa kutoka lakini muda uleule simu yake iliiita na alipoangalia jina lilisomeka Dokta Bensoni.
“Bensoni’Aliongea mara baada ya kupokea.
“Amosi amerudiwa na fahamu nusu saa iliopita” sauti ilisikika na kufanya moyo wa Kanali Dastani kudunda.
“Nakuja sasa hivi Dokta , mdunge kwanza sindano ya usingizi?” “Kuna tatizo Dastani”
“Tatizo gani?”
“Nimefanya kupigiwa simu baada ya kurudiwa na fahamu , lakini nafika hospitalini Amosi hayupo”Aliongea na Kanali Dastani palepale uso wake ulikunjamana. “Unamaanisha nini Bensoni”
“Ametolewa hospitalini na haieleweki amepelekwa wapi , ki ufupi Amosi ametoweka”
“Fu**ck , unanitania Bensoni , Amosi anatoweka vipi ndani ya hospitali ya jeshi”
Kanali Dastani hakuwa hata na muda wa kumfikiria tena Yonesi , aliona analo swala muhimu zaidi la kushughulika , hofu ilimvaa , kama Amosi ametoweka bila ya kupata maelekezo yake kuna hatihati familia yake inaweza ikawa mashakani , lazima Amosi atakuwa anafikiria kulipa kisasi kwa kumsaliti.
****
Hamza hakuwa hata na wasiwasi juu ya polisi waliofika hapo , mawazo yake yalikuwa siku ya kesho wapi anamtoa out mpenzi wake Eliza, ki ufupi hata swala la Frida hakulitilia maanani kabisa.
Sio kama hakuwa na uzoefu , ukweli ni kwamba pengine Eliza anaenda kuwa mwanamke wake wa kwanza kuwa nae katika mahusiano yenye usiriasi.
Hamza aliona kabisa amekuwa mzembe , kitendo cha mrembo Anitha wa chuo kumkataa ilithibitisha kabisa alikuwa mzembe na mvuto wake umeshuka , hivyo alitaka kujua namna ya kumpagawisha Eliza.
Baada ya kuwaza kwa muda alienda mpaka chumba cha kujisomea cha Regina na aligonga mlango na kuambiwa aingie na mara baada ya kuingia Hamza alianza kuangalia vitabu vilivyokuwa kwenye Shelf bila ya kuongea.
“Wewe unafanya nini?”Aliuliza Regina , wakati huo aliwaza Hamza alifika kwa ajili ya kuelezea kwanini wale watekaji walikuwa wamekufa lakini anaanza kuchunguza vitabu vyake.
“Naangalia kama nitaona kitabu cha kunifaa hapa” “Naona umekumbuka kuwa ni mwanachuo , kitabu gani unataka?”
“Hehe.. kinachohusiana na mapenzi”Aliongea na kauli ile ilimshangaza Regina.
“Yaani hakuna kitabu cha maana unachotafuta zaidi ya vitabu vya kipuuzi namna hio?”Aliongea kwa hasira.
“Nataka kujifunza namna mapenzi
yanavyoendeshwa , jinsi vitu vya kumfanyia mpenzi wako akolee bila ya kumhonga , kuna haja gani ya kukasirika hivyo bosi?”
Mapenzi!, Regina hakujizuia na kuwaza au Hamza anataka wawe wapenzi kweli , baada ya wazo hilo aliona aibu za kike na kugeuka.
“Sina hivyo vitabu , unaweza kuondoka”Aliongea akiwa siriasi.
“Kama huna ngoja nikatafute mtandaoni, nilijua pengine na wewe una shauku ya mapenzi yalivyo”Aliongea Hamza na kisha alitoka nje.
Regina mara baada ya Hamza kutoka alijikuta akivuta pumzi nyingi , mapigo yake ya moyo yalikuwa yakienda kasi mno kana kwamba amekutana na Simba mkali , alijikuta akishika uso wake na kuona umepatwa na joto.
“Mjinga huyu , kuna haja hata ya kusoma kwenye kitabu..”Aliwaza.
Baada ya kukaa akifikiria kwa muda alishika tarakishi yake na alisita kwa muda lakini alijikuta akiingia mtandao wa Google na kuandika , How to fall in love.
*****
Asubuhi kama kawaida Hamza aliamka mapema na kucheza mdundiko nje katika mpangilio maalumu , na baada ya kunywa chai alibadili katika mavazi mapya kabisa alionunuliwa na Regina.
Wakati akishuka kutoka chini Regina alikuwa sebuleni akiangalia taarifa ya habari kupitia CNN. “Regina nadhani leo hakuna kazi yoyote , si ndio?” “Ndio huna kazi ya kufanya leo , vipi unatoka?”Aliuliza na kumwangalia Hamza namna alivyopendeza.
“Ndio , nitatoka leo siku nzima , msinihesabu chakula cha mchana wala usiku”
“Unaenda wapi , kwenye kazi zako za ufundi kama kawaida , kama ni kazi ninazo nyingi tu unaweza kunisaidia”Aliongea Regina huku maneno yake akiwa hana uhakika nayo , alijua Hamza alikuwa na koneksheni kubwa hivyo hata hela lazima alikuwa nazo sasa alijiuliza kwanini anasoma chuo , kwanini aliishi maisha ya kimasikini kama vile hana hela.
“Wewe usinipe kazi ,nimepndeza vyote hivi niende kufanya kazi tena za nini, nina mtoko na mtoto mzuri leo , hivyo bosi leo ni siku yangu usinipigie simu”
Regina mara baada ya kusikia kauli hio , alijikuta akinywea lakini alibadilika dakika hio hio.
“Haina haja ya kuripoti una mtoko na mtoto mzuri”
“Haja ipo , tunaishi ndani ya nyumba moja na mimi ni mfanyakazi wako , sitaki itokee dharula nikiwa nakula bata uniambie nirudi nitamkera mpenzi wangu , lakini hata hivyo usiwaze sana , mpango wangu ndani ya miezi mitatu ikiisha sitotaka kuchelewa kuondoka hapa hata kwa sekunde, ila kwasasa nitahakikisha jambo letu linaendelea kuwa siri “
“Sina haja ya kujua kama una mpenzi hayo ni maisha yako ungeondoka zako tu bila kuniaga , kuna haja gani ya kuniambia”Aliongea Regina kihasira na kutupa Rimoti kwenye sofa na kupandisha zake juu.
Hamza aliishia kukuna kichwa chake na kujiambia kwani kosa lake ni lipi hapo , yeye kaomba ruhusa kwa bosi ni kufuata itifaki, hakutaka itokee anakula maisha na mrembo Eliza mara Regina anapiga wakutane.
Comments