SEHEMU YA 33.
Hamza aliona hakuwa na uhusiano wowote na Regina zaidi ya mkataba tu hivyo hana kosa , mara baada ya kuwaza hilo moyo wake ulijaa amani tele , na alizipiga hatua kutoka ndani ya nyumba hio kwenda nje.
Japo Regina ana magari mengi lakini hakutaka kutumia gari , isitoshe anapoishi Eliza ni wilaya hio hio na Eliza ana gari.
Baada ya kutoka mji huo wa kisasa wa Egret alichukua boda ambayo ilienda kumuacha nje ya jengo la Apartment za Lotus na aliruhusiwa kuingia moja kwa moja.
Alipishana na warembo kadhaa lakini hakuwa na habari nao na moja kwa moja alienda kusimama nje ya mlango wa Apartment ya Eliza na kisha alibonyeza Kengere.
Ilichukua dakika kama moja na nusu hivi mpaka kufunguliwa na Hamza alishangaa kumkuta mrembo huyo akiwa katika nguo za kulalia tena na Mask usoni, alishangaa maana sio kitu alichotarajia , alijua muda huo pengine Eliza atakuwa ashajipodoa na kupendeza tayari.
Eliza baada ya kuona aliekuwa mlangoni ni Hamza na alikuwa ametoka kulala alitimua nduki kurudi ndani na kuingia moja kwa moja bafuni.
“Eliza mbona unakimbia?”
“Mbona umekuja mapema hata kuniambia kwa simu ,, bado sijajiandaa”Sauti ya Eliza ilisikika kutoka bafuni.
Hamza alisogelea mlango wa bafuni na kisha alianza kuinama kutafuta upenyo wa kupiga chabo. “Haina shida , ni mzuri hata wakati wa kuamka”
“Naonekana kama zombie , hebu kakae sebuleni usinichungulie”Aliongea huku akifunga mlango wa bafuni vizuri na Hamza alirudi zake sebuleni kukaa.
Baada ya kufika hapo ndio aliweza kuona nyaraka kibao zimesambaa kwenye meza na wazo la Eliza kufanya kazi usiku kucha licha ya kuwa wikiendi lilimvaa, pengine ndio maana amechelewa kuamka, Hamza hakuona ni jambo baya , pengine Eliza alifanya hivyo kwa ajili ya kumaliza viporo vyote ili kupata amani wakati wa kutoka out pamoja, alijikuta akitoa tabasamu.
Baada ya nusu saa Eliza alitoka bafuni , ule mpauko wa uso ulimfanya avutie mno.
“Endelea kunisubiri nivae nguo haraka haraka”Aliongea huku akikimbilia chumbani na kufanya Hamza kuishia kumeza mate na uvumilivu ulimshinda na kumfuata huko huko , alitaka kuona urembo wa Eliza wakati akibadili mavazi.
Lakini sasa ile anafika mlangoni ni kama Eliza alishitukia Hamza angemchungulia na alirudi mlangoni kwa ajili ya kuuloki na hapo ndio alipoiona sura ya Hamza ikiwa imekodoa macho. “Wewe muhuni , ukiendelea hivi tutaachana ujue”Aliongea huku akimkodolea macho na Hamza alisimama vizuri na kuweka nguo sawa.
“Umenielewa vibaya nilikuwa nataka kwenda chooni ,nimekosea mlango ..”Hamza alijibaraguza lakini Eliza hakuwa hata na muda wa kumsikiliza kilichosikika ni mlango kubamizwa kwa nguvu huku ufunguo ukizungushwa kwa ndani na kumfanya Hamza kwa masikitiko kurudi kwenye sofa.
Baada ya kukaa kwenye sofa kwa zaidi ya dakika ishirini uvumilivu ulimshinda tena na kujiambia au hizo nguo zinamshinda kuvaa maana muda unaenda mno , lakini dakika ambayo anataka kugonga mlango hatimae ulifunguliwa.
Eliza nywele zake zilikuwa zimechanwa vizuri huku eneo la mbele zikipindishwa kidogo na ule weusi wake wa chocolate ulimfanya kuvutia mno , Hamza alikosa hiari na kuwaza ndio maana mtu kama Zefa alitaka kumbaka, Eliza alikuwa mrembo na urembo wake unahitaji ukaribu zaidi.
Alikuwa amevalia kitopu cha rangi ya kijani isiokolea cha maua maua, huku kikiwa na mistari flani hivi upande wa mabega , chini sketi ya rangi ya Dark Bluu iliovuka magoti lakini yenye kuacha wazi miguu ya bia.
Utofauti wa Eliza na wanawake wa kileo ni muonekano wake wa kiutu uzima licha ya sura yake kumpunguzia hio sifa , licha ya kwamba alikuwa akivaa kama wale waimba kwaya lakini alivutia mno.
Eliza alijikuta akiwa na furaha kwa namna ambavyo Hamza alikuwa akimwangalia kwa mshangao , hakuwahi kuweka juhudi kwenye kujivalisha kama hivyo kwa muda mrefu , alivyokuwa single hakujali sana.
“Hamza tuondoke sasa nishamaliza”Aliongea mara baada ya kukohoa kidogo kusafisha koo.
Hamza alijikuta akicheka kidogo na kisha kumsogelea Eliza na kumshika mkono. “Tutaanza na chakula cha mchana kwanza , nimepata eneo tulivu kwa ajili yetu”Aliongea Hamza.
“Mh , chakula cha mchana mapema yote hii?”Aliuliza na kumfanya Hamza kukuna kichwa.
“Sasa Babe ni wapi unataka twende kwanza ?”
“Nataka kwenda kumsalimia mama kwanza , Daktari anaesimamia wodi ya Sanatorium alinipigia jana , amesema kuna kitu anataka tuzungumze , pili nataka mtu wa kwanza kuniona nikitoka out na mpenzi wangu ni Mama , nataka aone nimeshatoka kivulini na sasa nipo tayari kuyakaribisha maisha mapya”Aliongea na Hamza upande wake aliona sio wazo baya , ijapokuwa mama yake alikuwa katika hali ya kutoweza hata kuongea lakini alikuwa ni mama yake na lazima angefurahi kuona binti yake hapotezi maisha yake kumhudumia yeye tu na ana mpenzi sasa.
“Hakuna shida , tukishamaliza kumsalimia mama yetu tutaenda kula chakula cha mchana”
“Mama yetu?!”Aliongea Eliza huku akiona aibu za kike.
“Ndio ni mama mkwe , kuna tatizo?”
“Unajiaminisha sana , unadhani nimekukubalia moja kwa moja wakati ndio tunaanza kuwa wapenzi”
“Sawa bibie , vyovyote vile nitahakikisha anakuwa mama yetu”Aliongea Hamza kwa kujivunia na wakati huo walishatoka tayari na E.liza kufunga mlango na kuingia kwenye lift.
Baada ya kufika maegeshoni ya magari, Eliza alikuwa na gari nzuri sana , ilikuwa ni mali ya kampuni lakini kwa wakati huo ni ya kwake kwani sio kwamba angeacha kufanya kazi ndani ya Dosam leo au kesho, isitoshe cheo chake kinapanda siku hadi siku na ni mchapakazi mzuri , ilikuwa ni Sedan, Toyota Crown Camry Silver Mettallic.
Hamza ndio aliekuwa dereva , isitoshe Eliza alikuwa amevalia High heels hivyo ingekuwa ngumu kuendesha, uzuri ilikuwa ni upande huo huo wa Kigamboni na kadri walivyokuwa wakienda mbele ndio walivyoingia kwenye eneo lenye miti mingi ikiwemo Miarobaini(Neem tree).
Jua lilikuwa la saa tano lakini ni kama la saa saba na kufanya eneo kuwa na harufu ya kuungua kwa majani ya miti.
Baada ya Eliza kumuonyesha sehemu ya kuegesha gari , hatimae wote walitoka.
“Mazingira ya hapa naona sio mabaya na hili eneo naona ni jipya kabisa,si utakuwa unalipa kiasi kikubwa cha pesa kumuweka mama yako hapa?”
“Hii ndio sehemu nzuri zaidi Dar nzima kwa huduma ya watu wasiojiweza, nalipia jumla ya milioni sitini kwa mwaka”
“Milioni sitini , hizo zote ni hela zako tu?”Aliuliza Hamza kwa mshangao.
“Baba ni mstaafu na yupo kijijini kwa sasa akiendeleza maisha na kiinua mgongo chake cha ualimu , sikuona haja ya kumpa mzigo kumuuguza mama , usiwe na wasiwasi nimemhamishia mama hapa mara baada ya kupanda cheo na kuwa meneja wa idara ya mauzo, mshahara wangu sio mdogo , ukijumlisha na posho ninazopata”
Aliongea na Hamza aliona huyo mrembo alikuwa na majukumu makubwa mno ya kifedha, kwa haraka haraka aliamini lazima mshahara wake wote anatumia kumuuguza mama yake , jambo ambalo sio baya lakini yeye kama mwanaume alimuonea huruma.
Wote waliingia kwenye jengo hilo la ghorofa , kulikuwa na lift pana mno ya kutosha kitanda cha
mgonjwa , baada ya kufika floor ya nne walitoka na kwenda moja kwa moja kwenye chumba alichokuwepo mama yake Eliza.
Baada ya kuingia ndani ya chumba hicho kulikuwa na vitanda viwili , vyote vilikuwa na wagonjwa ambao walikuwa katika hali ya Vegetative, walimkuta nesi pia ambae mara baada ya kumuona Eliza alitoa tabasamu na aliandika vitu flani kwenye Cardboard yake na kisha akaondoka kuwaacha.
Hamza aliweza kumuona mama ambae sio mtu mzima sana , aliekonda upande wa kushoto na alijua bila ya kuambiwa ni mama yake Eliza maana walionekana kufanana rangi.
“Mama, mwanao nimekuja kukuona”Aliongea Eliza akiwa amekaa kwenye kitanda akishika kwa namna ya kupangusa paji la uso wa mama yake.
“Naomba unisamehe mama yangu , nimekuwa bize wiki hii kazini ndio maana sikupata muda wa kuja kukuona , usikasirike mama…”Aliongea huku macho yake yakianza kugeuka mekundu , mama huyo hakuwa amefumba macho alikuwa akiona lakini hakuwa na uwezo wa kuongea.
Hamza aliamua kukaa kwenye sofa la mtu mmoja huku akimwangalia Eliza na mama yake , hakutaka kwenda moja kwa moja alitaka Eliza yeye ndio amtambulishe.
Eliza alitumia muda mwingi kumwambia mama yake kila stori iliomjia akilini na mambo yanayoendelea nyumbani na baadae alimgeukia Roma.
“Mama nimekuja leo na mpenzi wangu , nimepata mpenzi mama anaitwa Hamza , ni mhuni kidogo lakini anajua kunilinda , kwanzia sasa mama usiwe na wasiwasi , nina mwanajeshi pembeni yangu…”
Baada ya kumtambulisha Hamza hatimae alirudi katika hali yake ya kawaida akizima majonzi yake.
“Naenda kuonana na daktari , vipi
nisindikize?”Aliuliza na Hamza alitingisha kichwa bila hiyana , hata yeye alikuwa na shauku ya kutaka kujua kwanini dokta anamtafuta Eliza , alitaka kujua kama kuna tatizo ili aweze kusaidia.
Walitoka kabisa nje ya jengo hilo na kwasababu ilikuwa jumapili , wafanyakazi wengi hawakuwepo na kufanya eneo kuwa kimya mno.
Jengo la madaktari lilikuwa upande wa pili na walitembea katikati ya barabara hio yenye maua
mpaka katika jengo hilo na kusimama katika mlango uliokuwa na bango CHIEF PHYSICIAN OFFICE na Eliza aligonga.
“Dokta Maonga..”Aliongea Eliza kiheshima akimsalimia mwanaume aliekuwa na umri wa makadirio ya miaka theratini na tano kwenda arobaini hivi , alikuwa amevaa miwani ya macho na alikuwa na uwalalaza , ila alipendeza kwa namna alivyozichana nywele zake , alionyesha kujipenda.
“Eliza umefika, karibu”Aliongea na muda huo mara baada ya kuiona sura ya Hamza uso wake ulijikunja.
“Huyu ni…”
“Ni rafiki yangu , nimekuja nae”Aliongea Eliza , alitaka kusema ni mpenzi wake lakini aliamua kuwa makini.
Upande wa Dokta Maonga aliweza kuona kuna kitu hakipo sawa , lakini alijitahidi kuweka muonekano wake wa kitaaluma.
“Kumbe ni rafiki yako , lakini maongezi ya leo ni ya siri , hivyo itakuwa vizuri huyu bwana akitembea tembea kuona mazingira ya hospitali yetu”Aliongea na mara baada ya kusikia hivyo Eliza alijisiikia vibaya kidogo.
“Hamza nisame..”
“Usijali Eliza , ngoja ninyooshe nyooshe miguu , nipigie simu ukishamaliza”Aliongea na Eliza aliishia kutingisha kichwa tu.
Mara baada ya Hamza kuondoka Maonga alimkaribisha Eliza na baada ya hapo alifunga mlango kwa ndani.
“Dokta nini kimekufanya kuwa makini sana kuhusu afya ya mama?”Aliuliza Eliza lakini Dokta Maonga alisogelea kwanza Dispenser na kumimina maji kwenye glasi.
“Usiwe na wasiwasi Eliza , nitakuelezea taratibu taratibu , kunywa kwanza maji”
“Asante Dokta”Eliza alikuwa na kiu , kutokana na haraka alishindwa hata kukumbuka kunywa maji.
“Kiua tatizo juu ya afya ya mama yangu?”Aliuliza mara bada ya kumaliza kunywa maji yote.
“Mgonjwa Ratifa Mlowe amekuwa katika hali ya kutojitambua kwa zaidi ya miaka miwili sasa , uwezekano wa yeye kupona ni chini ya asilimia tano , nafikiri..”
“Dokta hata kama ni asilimia moja , siwezi kumkatia tamaaa mama , kama unataka hela zaidi nipo tayari kulipa lakini naomba usiache kumtibu”Aliongea Eliza kwa kubembeleza.
“Bila shaka tupo tayari kutumia fursa hii lakini kama ujuavyo kuna hospitali chache sana ndani ya taifa hili ambazo zimejikita katika kuhudumia wagonjwa wasiojiweza , kikawaida kutokana na asilimia chache za Ratifa kuamka ilitakiwa ndani ya mwaka mmoja awe amesharudishwa na kuugulia nyumbani na kusubiria wakati wa Mungu kumchukua”
“Lakini Dokta wakati namleta mama hapa ulinihakikisha kutakuwa na matibabu ya hali ya juu ambayo yatamuwezesha mama kuamka , inamaana hukumaanisha”
“Usinielewe vibaya , uwezekano huo upo lakini mpaka sasa tunapokea wagonjwa wengi sana na wengi wameomba nafasi katika wodi zetu , tukisema tukuruhusu mama yako aendelee
kutibiwa hapa , itahitajika malipo makubwa zaidi ya mwanzo”
“Hayo malipo yatakuwa ni kiasi gani?”Aliuliza Eliza, hakuwa tayari kuona mama yake anarudishwa nyumbani kwenda kusubiria kifo chake , hata kama kulikuwa na asilimia moja ya matumaini alitaka kuishikiria hio hio.
Dokta Maonga aliishia kunyanya kidole hewani na kuchora namba na Eliza macho yalimtoka.
“Milioni saba kwa mwezi!!?”
Eliza alijikuta akipagawa , kiasi hicho kilikuwa sawa na mshahara wake wote ukiondoa posho , ijapokuwa alikuwa katika nafasi ya juu ya kampuni lakini hakuwa kama Regina ambae ni Mkurugenzi maana yeye hakuwa na hisa kama wafanyakazi wenzake , wakati wenzake wakinunua hisa za kampuni kama njia ya uwekezaji yeye alikuwa akimuuguza mama.
“Hapo tu haitoshi kwani lazima nikaombe kwa wakubwa kumuacha mama yako aendelee na matibabu , wanataka wagojywa wanaobaki wawe angalau na asilimia ishirini na tano za kuamka” Eliza hakujua kwanini lakini mara baada ya kusikia hio namba saba , kichwa chake kilikuwa kikimzunguka, lakini baada ya kufikiria kidogo alipata wazo.
“Hata kama ni hio hela nitalipa tu ili kumuacha Mama aendelee na matibabu”Aliongea lakini kwa Dokta Maonga alionyesha ishara ya ajabu.
“Ukweli ni kwamba kuna namna ya kuokoa kiasi hicho cha pesa na utaendelea kulipia milioni nne kwa mwezi kama kawaida”Aliongea na Eliza aliona sio wazo baya.
“Ni njia gani hio?”Aliuliza na Maonga palepale alinyanyua mdomo wake na kutoa tabasamu la ajabu , alisimama kutoka kwenye kiti chake na kumsogelea Eliza
“Eliza unajua tokea mara ya kwanza na kutia machoni nilikuona mwanamke mrembo sana , tena unaendana na mimi vizuri”Aliongea huku akinyoosha mkono wake kutaka kumshika Eliza lakini mwanamke huyo aliwahi kushituka na kusimama.
“Dokta naomba usifanye hivi … nipo tayari kulipia kiasi ulichonitajia lakini sio hili”
“Eliza kama unataka mama yako kuendelea kutibiwa hapa ni kheri utulie na kukubali ombi langu”
“Wewe… kwahio unamtumia mama kuni…”Eliza alijihisi kichwa chake kikianza kuwa kizito mno huku kizunguzungu kikimvaa na macho yalianza kujfiumba yenyewe bila ridhaa yake.
“Haha.. vipi tena , naona unataka kusinzia?”Muda uleule ndio sasa Eliza aliangalia kikombe alichotumia kunywa maji na kuhisi tatizo.
“Umeniwekea dawa kwenye maji?”
“Hehe.. ndio ili usishituke niliweka dawa nyingi maji yote , lakini dozi yake inatosha kukufanya usinzie , usiwe na wasiwasi kabisa , mpaka muda utakaoshituka kila kitu kitakuwa kimemalizika”
Eliza moyo wake ulianza kujawa na majonzi huku akijihisi kuwa dhaifu kutokana na ukali wa dawa aliowekewa ,hakuamini dokta kama huyo anaweza kufanya kitendo cha namna hio, lakini hata hivyo aliona sio wa kumlaumu Dokta Bensoni pia alionekana kama mtu wa heshima kwake lakini mwisho wa siku alimuomba rushwa ya ngono.
Eliza alijiona kama mwanamke mwenye mikosi na hapo hapo machozi yalianza kumbubujika , katika maisha yake alipona chupuchupu kubakwa mara nying , pengine jaribio la siku hio linakwenda kuwa mara ya tano katika maisha yake.
Alijikuta akilegea na kwenda kukalia sofa bila ya kupenda , muda huo Dokta Maonga alikuwa na tabasamu la ushindi na aliingiza mkono kwenye koti lake la kidaktari kutoa simu.
“Ni muda wa mzee Gabusha kutimiza ahadi ya upande wake”Aliongea huku akiwa haamini anakwenda kupokea hela nyingi.
Lakini sasa kabla hajafanya chochote mlango wa chumba hiko ulipigwa teke na kufunguka kwa nguvu, japo ulikuwa umefungwa kwa ndani lakini loki zake zilipinda na ukafunguka.
Kitendo kile kilimshitua Dokta Maonga kiasi cha kudondosha simu chini na mara baada ya kuona ni Hamza alijikuta akipandwa na hasira.
“Wewe.. unathubutu..”
“Dakika ambayo umeniona nikifika hapa ulionekana kutoridhika na ujio wangu kana kwamba nimeingilia mpango wako , kila ulichokuwa unakiwaza kilikuwa kimejiandika kwenye uso wako , unadhani ingekuwa ngumu kwangu kutokukushitukia”Aliongea Hamza.
“Hamza… naomba unisaidie…”Eliza alikuwa ndio anasinzia , alimuona Hamza lakini alidhani ni kama anaota.
“Lala tu usiwe na wasiwasi , nitakulinda”Aliongea Hamza huku akiwa na uchungu moyoni, ukweli hakuwa hata na haja ya kumruhusu alale maana ilikuwa ndio sauti yake ya mwisho kabla ya kupotelea usingizini.
Dokta Maonga baada ya kuona kitumbua kimeingia mchanga aliangalia mlango na kitendo cha Hamza kuangalia pembeni aliusogelea kwa spidi , lakini Hamza anamwachaje akimbie kwa mfano.
Ile anapiga tu hatua alikuwa ashainua mguu na kumpiga eneo la kigoti cha mguu na kilichosikika ni’ kacha’.
“Arghhh…!!”
Maonga alijikuta akipiga ukulele huku akikaa chini na kidogo tu apoteze fahamu maana maumivu hayakuwa ya kawaida.
“Nisamehe , Bwana mdogo naomba usiniue nina familia”Maonga alijikuta akibembeleza ili kujiokoa katika hali hio , lakini Hamza hakutaka kumuacha alimpiga teke lingine na kumvunja mguu mwingine na alipotaka kuzimia Hamza alimshika shingo kwa nguvu.
“Umeweka nini katika maji uliompatia mpenzi wangu?”
“Hapana … ni vidonge vya usingizi .. uwiii miguu yangu , naomba usinipige tena”Aliongea huku mwanaume akitokwa na machozi mfufulizo.
Hamza alijikuta akivuta pumzi ya ahueni , aliona angalau huyu mhuni hajatumia dawa ambayo haieleweki la sivyo mambo yangekuwa magumu.
Hamza alichukua simu ya Maonga iliodondoka chini na kisha aliitoa nywira na kwenda moja kwa moja upande wa Vidio rekodi.
“Nataka ujirekodi kila kitu ulichofanya kupitia hii
simu , vipi unajiona upo tayari au niongeze kidogo maumivu?”
Hamza hakutaka kumuua , wala pia hakutaka itokee Maonga kuja kumshitaki hivyo aliona atengeneze ushahidi kabla ya kuondoka hapo.
“Una chaguzi mbili tu , ya kwanza ni kuongea kila kitu ulichofanya na pili nipigie simu polisi na
nikufungulie kesi ya ubakaji, hivyo fikiria kipi ni nafuu kwako”
Maonga alijua chochote atakachochagua hakuna namna anaweza kulipiza kisasi , lakini vilevile alitamani kumtaja Mzee Gabusha kama ndio alimpa kazi hio lakini hakuwa tayari kwa hilo , alijua nguvu ya Gabusha anaweza akawa hai ndio lakini ni rahisi kupotezwa na Gabusha muda wowote, hivyo aliona bora achague chaguo la kwanza pengine akipona anaweza kuendelea kuwa daktari huku akipata fidia kutoka kwa Gabusha.
Alikuwa na akili mno , alikuwa na familia hivyo akili yake ilikuwa ikicheza, hakuwa na jinsi na alielezea mwanzo mwisho mpango wake wa kutaka kumbaka Eliza kupitia matatizo ya mama yake.
Hamza mara baada ya kuridhika alituma ushahidi huo katika Email yake na akamchukua Eliza kimyakimya na kumuingiza katika gari.
Bila ya watu kushitukia kinachoendelea aliweza kutoka ndani ya gari na kuingia ndani ya jengo la hospitali , akiwa na mpango wa kutafuta dawa ya kumumsha Eliza haraka iwezekanavyo ili waendelee na mtoko wao.
Bahati ilikuwa kwake baada ya kufika katika chumba cha dawa mlango ulikuwa umerudishiwa tu na aliingia haraka haraka na kutafuta baadhi ya dawa na pamoja na sindano na kutoka nazo.
Alirudi kwenye gari na kisha alifyonza maji katika kijichupa na kuchanganya na unga unga kisha alivuta na kumwingizia Eliza kwenye mshipa wa damu kutumia sindano.
Kwa jinsi alivyokuwa akifanya Hamza utadhani ni daktari mzoefu wa miaka mingi , alionekana kujua kile alichokuwa akifanya.
Eliza alikuwa amelala mpaka anatoa sauti lakini alionyesha dalili ya jasho hivyo Hamza alimwegamiza vizuri kwenye siti na kumtoa kibanio cha nywele na baada ya hapo alirekebisha ubaridi wa gari, nusu saa kupita hatimae Eliza alifumbua macho kivivu.
Bado dawa ya usingizi ilikuwa kali hivyo alikuwa akiona ukungu tu , kwa dakika tano hatimae akili yake ilirudi katika hali ya kawaida na kukumbuka kilichomtokea na alikaa kitako kwa mshituko na kuangalia pembeni.
“Hamza imekuwaje nikafika kwenye gari , kidogo tu ni…”
“Usiwe na wasiwasi tena , yule mpuuzi nimempa kibano lakini sijamuua”Aliongea Hamza na mara baada ya Eliza kusikia hivyo alijikuta akihema kwa nguvu akionyesha ahueni.
Lakini mara baada ya kuwaza kilichotaka kumtokea hali ya woga iliamza kumvaa na kadri alivyokuwa akifikiria ndio macho yake yalivyoanza kuwa mekundu na ghafla tu alianza kulia kwa kwikwi.
“Eliza usilie sasa , hili limeisha”Aliongea Hamza akijaribu kumfariji.
“Asante , asante sana kwa kuniokoa mara nyingine , lakini vipi kuhusu mama yangu mimi , nini kitampata mama kwa staili hii”
Wazo la kuona mama yake akikosa matibabu sahihi moyo ulizidi kumuuma.
Hamza hata yeye hakufikiria hilo lakini alijikuta akiwaza kwa mdua namna ya kufanya.
“Eliza usiwe na wasiwasi , kuna daktari namfahamu na uwezo wake sio mbaya sana , unaonaje tukimchukua mama na kumrudisha nyumbani kwanza na kumtafutia mtu wa kumhudimia na nitawasiliana na huyo dokta , akifika atamwangalia au ikishindikana tutamsafirisha moja kwa moja nje ya nchi”
“Una rafiki ktuoka nje ya nchi ambae ni dokta, na yeye anahusika na ugonjwa kama wa mama?”
“Sijui ila anaonekana kama Dokta wa magonjwa yote , ni MD hata kama hajui jinsi ya kutibu lazima atakuwa anafahamu madokta wenye uwezo”Eliza alitaka kuongea neno lakini alisita mara baada ya kuona sindano na mabomba ndani ya gari.
“Hizi sindano ndio ulinichoma nazo , sio kama umenitingisha nikaamka?”
“Ndio nimekuchoma , wewe unadhani ungemka mapema hivi?”
“Kwahio unajua kumchoma mtu sindano?”
“Mimi ni dokta ndio tena wa moyo , mambo ya kushika kisu na kumchana mgonjwa kwangu rahisi sana , nikishamaliza kumpima kama hivi kazi inaanza taratibu , shwa , shwaa!!”Hamza alikuwa akifanya utani huku akijifanyisha anampima Eliza mapigo ya moyo kumbe anashika nyonyo, ila kitendo kile kilimfanya Eliza kuficha kifua chake.
“Unamdanganya nani hapa , eti daktari, mateja tu wanajua kujichoma sindano , unadhani nadanganyika kirahisi” “Sawa bwana kama huniamini”
“Kwahio umenichoma dawa gani na umezitoa wapi?”Aliongea huku akinyanyua vijichupa vya dawa vilivyokuwa kwenye siti.
“Nizitoe wapi tena wakati mimi sio Dokta , niliziiba wakati wakiwa bize na simu zao , hii hapa sijui wanaiita Benzo nini huko ila kazi yake ni kupoza nguvu ya vidonge vya usingizi “ “Vipi kuhusu hii nyingine?”Aliuliza
“Hio ni Mannitol “
“Kazi yake?”Aliuliza na kumfanya Hamza kusugua pua yake.
“Eliza unaonaje tukienda kula kwanza , unaonekana una njaa”
“Acha kubadilisha topiki , niambie kwanza hii dawa kazi yake?”
“Ni nzuri kwa afya yako , kwanini unauliza sana?”
“Kama ni nzuri kwangu niambie kazi yake nini?”
“Kuhusu hio.. basi ngoja nikuambie , vipi kwanza hujisikii mkojo kukubana”
“Labda wewe ndio mkojo umekubana , niambie kazi ya hii dawa acha kuzunguka zunguka”
“Hio ni dawa ya kukufanya ukojoe ili kupunguza sumu mwilini”
“Kwanini umenipa dawa ya kunitoa mkojo wakati tupo date”Aliongea Eliza huku akimpiga piga Hamza na kumfanya acheke.
“Usinipige bwana , nilikuwa na wasiwasi , kama usingemka mapema kuna uwezekano ungejikojolea , bahati nzuri umewahi kuamka”Eliza alitaka kumpiga lakini alihisi mafuriko yakijikusanya na aliishia kusugua meno kwa hasira.
“Nitakushikisha adabu nikirudi, ngoja uone”Aliongea na kisha alifungua mlango na kutimua nduki kwenda chooni kama mwanariadha.
Wakati wa kurudi alishindwa kuzuia aibu aliokuwa nayo.
“Babe naona sasa umekaa sawa , haha ..tuendelee zetu na mtoko sasa , tunaanza kula kwanza”
“Nitakusamehe leo kwasababu umeniokoa , ila siku nyigine ukinichoma sindano zisizoeleweka , sikuongeleshi tena”Aliongea na Hamza hakutaka kurefusha hilo jambo hivyo alikubali kwa kutingisha kichwa.
Kabla hajawasha gari wazo lilimjia palepale na aliinama kuelekea upande wa Eliza na kisha alichomoa mkanda wa siti.
Eliza alijua kuna kitu Hamza anataka kumfanyia , lakini mara baada ya kuona ni mkanda wa gari alijikuta akipumua kwa ahueni.
“Nitafunga mwenyewe”
“Tulia hivi hivi , jana nimekula shule ya mapenzi mtandaoni na wamesema ukimsaidia mpenzi wako kufunga mkanda unajinyakulia pointi za mapema sana , ni namna ya kuonyesha unajali”
Kauli ile ilimfanya Eliza kujikuta akicheka mpaka basi.
“Vipi kama mpenzi wako hataki kufungwa mkanda?”
“Hapo ndio pagumu sasa maana walinihakikishia
kabisa nitajinyakulia pointi , vipi wewe hupendi kufungwa mkanda?”
“Haha..hebu endesha huko , siku nyingine nitafunga mwenyewe .. unalishwa matangopori unayabeba kama yalivyo”
Hamza alijikuta akijifanyisha kuona aibu na mara baada ya kumwangalia Eliza walijikuta wakicheka wote.
****
Muda wa saa sita Mchana Mzee Gabusha aliingia nyumbani kwake na wala hakumjali hata Chriss aliekuwa bize na simu bali alivua koti la suti pamoja na tai na kisha alikimbilia friji na kuibuka na Vodka pamoja na glasi.
Kwa haraka haraka alimimina kinywaji kile katika ile glasi na kupiga pafu kwa nguvu kana kwamba anakunywa maji.
Kitendo kile cha baba yake kurudi akiwa katika hali hio alijua lazima kuna swala ambalo limetokea na hio ilimpa shauku Chriss.
“Mzee nini tatizo?”Aliuliza Chriss.
“Hakuna tatizo”Aliongea huku kifua kikipanda na kushuka.
“Dad tunaishi wote na nakujua ukiwa katika mudi tofauti tofauti , ukiwa na kitu kinachokusumbua lazima utumie Vodka”
Kabla hata hajajibu swali la Chriss simu yake ilinguruma na aliitoa haraka haraka na kuangalia jina la anaepiga na alipokea palepale.
“Boss ashaanza matibabu, amevunjika miguu yote miwili”
“Vipi kuhusu Eliza hajaongea chochote , hakunitaja wala kutoa ushahidi wowote?”
“Imekuwa ngumu kumhoji kwasasa maana ndio amerejewa na fahamu , bosi nitachukua maelezo kutoka kwake”
“Sawa nitaarifu ukifanikiwa”Aliongea na kisha akakata simu na Chriss shauku ilizidi kumjaa.
“Mzee nini kinaendelea”
“Yule boya kamvunja Maonga miguu yote”Aliongea na kauli ile ilimfanya Chriss kuwa na hali ya kuchanganyikiwa. “Baba unamaanisha boya yupi?”
“Alievuruga mpango wangu na Eliza na kumfanya Amosi kujitoa kabisa baada ya Chatu kumtishia maisha yake”Aliongea huku akichukua kinywaji kingine na ukigida na kufanya jicho kuwa jekundu.
“Imekuwaje Maonga akaingia katika hili sakata Mzee ..usiniambie?”Aliongea Chriss na wazo lilimjia palepale na kujikuta akikaa kwenye sofa huku akimwangalia mzee wake kwa mshangao.
Mzee Gabusha hakujali muonekano wa chirss na alichukua koti lake pamoja na tai na kisha aligeuza akitoka nje , haikueleweka alikuwa akienda wapi maana ndio amefika nyumbani.
Chriss aliishia kutingisha kichwa tu, huku akijiambia mzee ni mkatili sana na hakutarajia kama angekamilisha mpango wake muovu.
Dakika chache kupita mlango wa kuingilia ulifunguliwa na Alex ambae alikuwa na yeye mbiombio na kumfanya Chriss ajiulize leo hawa ndugu zake wana matatizo gani.
“Hey! Chriss , mjomba amekuwaje mbona mbiombio hata namsalimia haitikii?”
“Mpango wake na Eliza unaonekana kubuma , ndio maana yupo hivyo?”Aliongea Chriss kivivu na Alex mara baada ya kusikia kauli ile alienda kukaa haraka haraka kwenye sofa na kumkazia Chriss macho.
“Kulikuwa na mpango ambao siujui?”
“Unajuaje wakati siku sita zote huonekani na hata taarifa hujatoa , unazingua?”Aliongea na kumfanya Alex kunywea kidogo.
“Niliitwa na Madame , yule mwanamke akisema njoo hata upo chooni unaacha unaenda , sikupata
muda wa kukutaarifu. Niambie ni mpango ngani uliofeli?”
“Unajua Mzee na mambo yake , juzi ananiambia ana mpango wa kumtia Eliza mimba , hivyo ameanza kufatilia mzunguko wake wa hedhi?”
“Nini , Mjomba anajua mzunguko wa hedhi wa
Eliza , kivipi?”
“Mzee juhudi anazowekwa kwa huyu mwanamke ingekuwa ni kwenye biashara zetu tungeipita hata Dosam muda mrefu , lakini ndio hivyo juhudi anazoweka hazimpi majibu, Inaonekana huyu Eliza anapata maumivu wakati wa hedhi na kutumia vidonge flani hivi vya kuyapunguza, duka analopenda kununulia Vidonge hivyo ni lile la Mzee Benjamini kule Kigamboni , nadhani ndio alijua hapo kwa kupiga mahesabu ya siku ambayo anaingia kwenye mzunguko”Aliongea Chriss na kumfanya Alex kutoa macho.
“Aisee Mjomba kafanya yote haya kwa ajili ya huyo mwanamke , mbona shauku inanijaa , nataka kumuona huyo mrembo”
“Hata mimi nimejikuta nikipatwa na shauku ya kutaka kumuona , nilitaka kutumia kisingizio cha kwenda kumuona Prisila kazini kwake ili anikutanishe na huyo Eliza ila kwasasa yupo likizo”
“Sasa imekuwaje mpango ukafeli?”
“Wewe mpaka hapo ulitakiwa uwe ushaelewa nini mzee angefanya , mpango wake ulikuwa ni kumbaka Eliza akiwa katika siku za hatari ili amtie mimba , juzi wakati ananiuliza maswala ya mzunguko wa hedhi yanavyokuwa nilimdadisi
lakini hakufunguka sana , ila leo baada ya kurudi akiwa amefura nishausoma mchezo mzima, Dokta Maonga ni Mkuu wa Vizda Sanatorium na huyo Eliza mzazi wake ni mgonjwa ambae hajitambui hivyo ni lazima atakuwa yupo huko Vizda na Mzee Kamtumia Maonga kufanikisha mpango matokeo yake Maonga kavunjwa miguu”Aliongea huku akicheka.
“Maonga kavunjwa miguu?”
“Ndio na Mzee kwa ninavyoona wasiwasi wake ni kama Maonga amemtaja katika tukio hilo, nadhani ndio kinachomsumbua zaidi akili kwa sasa”
“Huyo jamaa aliefanikisha kitendo cha kumvunja miguu Dokta Maonga ni nani huyo, au ndio yule yule aliemfanya Jasusi kukimbbia”
“Ndio huyo , kasema tu yule boya kaharibu mpango wangu”Alex alijikuta akifikiria.
“Siwezi kumcheka Mjomba wakati na mambo yangu hayajakaa sawa kabisa , Frida katoweka na sijui kaelekea wapi?”
“Katoweka au kasafiri?”Aliuliza
“Kusafiri unajua mtu kaenda wapi , ila huyo katoweka , sijui hata kama amesafiri” “Amesafiri huyo na atarudi ,unadhani mfanyakazi wa taasisi kubwa kama Haliz anaweza kupotea tu hivi hivi , tumia akili bro”
“Nimefikira hivyo pia , lakini hata akirudi sidhani kama pale nitang’oa , itafikia hatua naweza kutumia hata njia ya mjomba”
“Wewe na Mjomba mnafanana sana tabia , nimehangaika na Prisila mwaka wa ngapi huu lakini sijaambulia chochote zaiti ya mate tu , lakini sijawahi kufiikiria kumfanyia hila , nitaenda nae
taratibu mpaka ajae kwenye himaya yangu”Aliongea.
“Wewe Chriss unachofanya ni uboya , endelea na ubaba paroko ,utakuja kushitukia demu sio wako tena , unaweza ambulia mate kuna mwenzako anapewa zaidi ya hivyo”
“Acha uboya Alex , namjua Prisila vizuri, unadhani mpaka muhuni kama mimi ku fall in
love ni rahisi hivyo”Aliongea .
“Simu yako inaita”Aliongea Alex akinyooshea simu iliokuwa juu ya meza ya kioo,
Chriss aliichukua haraka haraka na mara baada ya kuangalia jina la mpigaji mapigo yake yalienda mbio.
“Huyu Jasusi baada ya wiki kupita ndio ananipigia sasa hivi simu, nimemtafuta sana”Aliongea kwa hasira mara baada ya kuona jina la Mzee Amosi kwenye kioo cha simu yake.
******
Hali ya Eliza iliimarika mara moja na hio ilimpa
amani ya kuendelea na siku yao kama walivyopanga.
Walitoka hospitalini na moja kwa moja walienda kwenye mgahawa ambao Hamza aliuchagua , wakiwa njiani Hamza alimwelezea Eliza namna alivyodili na Dokta Maonga.
Eliza hata yeye baada ya kusikia kibano alichokutana nacho aliona haina haja ya kwenda kushitaki , kwani ingempotezea muda tu , isitoshe vitendo vya namna hio vilikuwa vikikemewa kila siku lakini havikuwahi kukoma.
Kwa mara ya kwanza mrembo huyo alijisikia vizuri sana ana mwanaume ambae anaweza kumlinda wakati wote , siku zote alikuwa peke yake akihangaika huku na huko na hata kuombwa rushwa ya ngono , lakini malaika Hamza kujitokeza ni kitu kilichomfanya ampende zaidi.
Siku nzima hakuacha kumwangalia Hamza huku akiwa na tabasamu
Upande wa Hamza na yeye alifurahi kuwa karibu na mrembo huyo na ni mwanamke wake wa kwanza kuingia nae katika mahusiano kwa kipindi kirefu.
Aliweza kumjua kiundani zaidi Eliza na alijua ashawahi kuwa katika mahusiano huko nyuma , hakushangaa , kwa uzuri wa Eliza lazima wanaume wengi walijaribu bahati zao na ni ngumu kuwakatalia wanaume wote, ki ufupi hakuona tatizo Eliza kuwa na Ex.
Saa tatu kamili za usiku ndio Hamza alimaliza mtoko wake na mtoto mzuri Eliza , ijapokuwa ilikuwa mapema lakini kwasababu siku iliofuatia ni Jumatatu hivyo Eliza alitaka kuwahi kupumzika.
Hamza wakati anafika nyumbani aliweza kumkuta Shangazi akiwa bado macho , akiwa bize na kuandaa vifungua kinywa kwa ajili ya siku inayofuara asubuhi.
“Hamza bora umewahi kurudi , hebu chukua hizi doghnut na hio chai ya maziwa umpelekee Regina , hajakula chochote tokea mchana”
“Regina hajala chochote tokea mchana?”Aliuliza Hamza kwa mshangao.
“Ndio , nadhani ni maswala ya kampuni ndio yanamuumiza kichwa , nashindwa hata kumuelewa ila anaonekana kutokuwa na raha kabisa , nimeenda hapo supemarket na kununua hizi Doghnut”
Hamza alishangaa kuona Shangazi na giza lote ameenda kutafuta Doghnut kwa ajili ya Regina , kwenye mfuko zilikuwa nane na zilikuwa zikinukia harufu flani hivi nzuri ya Strawberry, Hamza aliishia kujiuliza Regina atamaliza zote hizo.
Ukweli ni kwamba mwenyewe alikuwa aksihangaa yaani mtu aache kula chakula cha usiku na ale doghnut saa nne kasoto ya usiku.
“Usiwe na wasiwasi kabisa , Regina huwa anazipenda sana hizo , huwa akiwa hana hamu ya kula ndio naendaga kuzinunua na kumpa , hizo nane ni chache sana mbona”Aliongea Shangazi lakini Hamza hakuamini, aliishia kuchukua maziwa yaliochanganywa na majani na kisha kupandisha juu.
“Regina upo ndani?”Aligonga lakini hakuna suati iliosikika kutoka ndani.
Comments