SEHEMU YA 34.
Hamza aligonga mlango kwa muda mrefu kidogo , lakini hakusikia majibu hivyo aliamua kushika kitasa na kuufungua kisha akaingia ndani.
Mara baada ya kuingia katika chumba hicho cha kujisomea aliweza kugundua Regina alikuwa amelalia meza akiwa usingizini , huku mbele yake kukiwa na furushi la nyaraka ambazo ilionekana
alikuwa akizifanyia kazi, Hamza aliishia kujiuliza inamaana huyu mwanamke tokea mchana alikuwa akifanya kazi licha ya kwamba ni jumapili.
Hamza licha ya kwamba alikuwa mpenzi feki , lakini kumuona namna alivyokuwa akijitesa kwa kufanya sana kazi alijisikia vibaya.
Alijikuta akisogea upande mwingine na kumwangalia Regina , na kwa jinsi alivyokuwa amelala alikuwa ni kama mdoli kwa jinsi alivyokuwa mzuri , ule ukauzu wote ulikuwa umepotea akiwa usingizini na kumfanya kuzidi kuvutia.
“Sura yako ingekuwa muda wote kama hivi , ingekuwa vizuri lakini tabia yako ya ukauzu inaficha mengi ya kuvutia”Alijiongelesha Hamza.
Chumba kilikuwa na ubaridi wa AC mkali mno lakini bado alikuwa amelala na kutoa sauti kabisa , Hamza hakutaka kumuamsha hivyo aliweka alivyoshika mkononi na aliona shuka kwenye sofa na kumfunika lakini kitendo cha kumaliza tu Regina alishituka.
Aliishia kuegamia kiti chake huku akitoa miayo na mara baada ya kufikicha macho yake ndio sasa anagundua kuna mtu pembeni yake
Hamza upande wake alikuwa amekodoa macho tu , alikuwa akiushangaa uzuri wa mrembo Regina hata wakati wa kuamka.
“Unafanya nini hapa , nani kakuruhusu kuingia?”Aliongea kibabe.
“Sijafanya makusudi kuingia bila ya ruhusa , ulikuwa umelala , Shangazi kanipatia hizi doghnut na chai nikupe , anasema hujala chakula cha usiku” “Mh Doghnut! “Regina alijikuta akigeuza macho yake na aliweza kuona Doghnut nane kwenye sahani na alishindwa kujizuia zaidi ya kumeza mate.
Kitendo hicho kilimfanya Hamza kuona itakuwa kweli Regina anapenda sana hizo Doghnut.
Regina muda ule alijihisi kuna kitu kilikuwa kimemfunika mabega yake hivyo alipeleka mkono nyuma kukitoa na aligundua ni shuka.
“Wewe ndio ulinifunika?”
‘Ndio , chumba umekifanya kimekuwa na ubaridi mkali ndio maana nimekufunuka , haina haja ya kunishukuru kwa upendo wangu”
“Nani kasema nitakushukuru , ulitakiwa kuniamsha baada ya kunniona nimelala sio unanifunika”
“Nilikuwa nikijali kuhusu afya yako , ningejuaje kama ulitaka kuendelea na kazi”
“Huna haja ya kunijali, hatuna uhusiano wowote , nadhani itakuwa vizuri ukiweka akili yako kwenye kumjali mpenzi wako , unaweza kuondoka sasa”Aliongea kikauzu.
Hamza aliishia kupumua kwa masikitiko , alikuwa akionyesha vitendo vya kumjali kama bosi wake , lakini anakasirika , alijiuliza kwanini kuna utofauti mkubwa kati ya Eliza na huyu mrembo.
Ijapokuwa Regina alikuwa amemzidi kila kitu Eliza kwanzia muonekano , akili , mali mengineyo lakini Eliza alikuwa rahisi sana kuishi nae.
“Kheri nikale zangu tembele kila siku na Eliza kuliko kula vinono na Regina, mtu gani ana tabia kama za Mzimu uliolazimishwa ndoa bila mahari”Aliwaza Hamza. “Una mwemweseka nini?”
“Hamna , naenda na mimi kula hivyo vitairi”
“Utajua mwenyewe , toka nje”
“Nani kakuambia nataka kuendelea kukaa hapa?”Hamza alitamani kuongea kwa sauti lakini aliishia kumezea ndani kwa ndani na kutoka kwa hasira.
Hamza wakati anataka kuelekea kwenye chumba chake Shangazi alimwita tena. “Hamza njoo tena”
“Shangazi kuna nini tena?”
“Nimesahau kuweka sukari kwenye ile chai , hebu nisaidie ukamuwekee”Aliongea Shangazi na kumpatia Hamza mkononi.
Hamza alitamani kutoa chozi , alijiuliza kwanini huyu shangazi alikuwa akimuonea hivyo , lakini baada ya kukumbuka ni mpenzi akiwa hapo nyumbani aliishia kukubali kinyonge.
Awamu hio alikuwa na hasira hivyo baada ya kufikia mlango hakujisumbua hata kugonga na alisukuma mlango na kuingia.
Lakini picha alioiona pengine asingeisahau kwenye maisha yake kuonyeshwa na mwanamke kama Regina.
Regina alikuwa ameshikilia Doghnut mbili mikono yote huku zikiwa zimeng’atwa zote , mdomo ulikuwa umetuna kiasi kwamba alikuwa akitafuna kwa shida, kilichomshangaza zaidi alikuwa akitingisha kichwa kwa furaha zote kiasi kwamba kiti kilikuwa kikinesa nesa.
Hamza alijiambia huyu Regina aliemfurusha ndani kwake ni wa tofauti sana , kama mbingu na ardhi , hakuwa na ule kauzu tena bali muda huo ni kama mtoto anaeshindana na chakula.
Hama alijiuliza au Regina ana tatizo la akili la kuwa na nafsi mbili kwa wakati mmoja .
Ughh!!
Regina alijikuta akitoa macho mara baada ya kugundua kuna mtu ameingia na aligeuza uso wake na kugundua ni Hamza , aliishia kupepesa macho kama ana kifafa huku akianza kuwa mwekundu.
Tukio lile lilimfanya Hamza kujiambia atakuwa ameona kitu ambacho hakustahili kuona
Alijifanyisha Mzembe na kisha alipeleka sukari mpaka kwenye meza.
“Samahani bosi kwa kukusumbua wakati unakula , shangazi kaniambia nikuletee hii sukari kwa ajili ya kuweka kwenye maziwa”
Baada ya kumaliza aliondoka haraka hraka ndani ya chumba hicho akiwa katika hali ya utulivu na kufunga chumba.
Baada ya Hamza kutoka Regina kivivu alijikuta akiweka kila alichoshikilia kwenye mikono yake na kulalia mikono yake kuzika kichwa , uso ulipata moto na alitamani kuingia chini ya meza kwa aibu alizokuwa akisikia.
Upande wa Hamza picha ya Regina kutuna mashavu huku akisindilia vile vitairi ilikuwa ikijiurudia rudia na alijikuta akikaa kwenye ngazi na kutoa kicheko cha ajabu kama kichaa.
Kutokana na tukio hilo hasira yake zidi ya Regina iliisha mara moja , aliona tukio hilo linachekesha zaidi kuliko la kule kazini.
Hamza mara baada ya kurudi chumbani kwake na kumaliza kuoga , aliweza kuona lile boksi alilopewa na Frida jana yake na shauku ilimvaa hapo hapo na kutaka kujua ni mshumaa gani ambao alikuwa akizungumzia.
Hamza alichukua kile kiboksi na kurudi nacho kwenye kitanda haraka sana na kufungua ndani na mara baada ya kuona kilichokuwa ndani yake aliishia kuguna tu , haukuwa mshumaa kama mshumaa , bali kifaa cha kieletroniksi kilichokuwa na muonekano kama wa mshumaa , pengine ndio maana kiliitwa mshumaa, kwa chini kulikuwa na kitako kama cha Bunsen Burner za gesi , kilikuwa cha rangi ya zambarau huku eneo la katikati kukiwa na kifaa kama kioo , juu kabisa kulikuwa na kioo pia kama vile ni hadubini.
Hamza aliangalia kwenye boksi na aliweza kuona pia waya wenye adapter, ilionekana ni kama chaji ya kifaa hiko, hakukuwa na kingine cha ajabu zaidi kutoka katika huo mshumaa wa nuru zaidi ya Manual, kikaratasi flani hivi cha maelekezo.
Hamza aliweka pembeni na kuanza kusoma kile kikaratasi taratibu na aliweza kuelewa maana kiliandikwa kwa lugha ya kingereza.
Hakuwa na cha ajabu sana zaidi ya maelekeo ya kufunga mlango na madirisha wakati wa kulala na kuchomeka kifaa hicho kati ya saa tano na saa sita za usiku kwenye umeme.
Hamza hakuwa akimwamini Frida bado hivyo hakutaka kukurupuka na kufauta maelekezo aliompatia.
Hivyo alirudisha kama vilivyo na kujitupa kitandani na hakuchuua muda alishapotelea usingizini.
*****
Ilikuwa ni siku ya jumatatu na mara baada ya Hamza kushituka aliona kwanza siku hio aende kazini na siku inayoafuata aelekee chuo kwa ajili ya kwenda kuchukua barua na kujua utaratibu wa kimasomo utaendelea vipi.
Baada ya kujiweka sawa kimwili walivaa mavazi yake kama kawaida na kisha alishuka chini.
Regina alikuwa tayari ashajiandaa na alikuwa mezani akipata kifungua kinywa na muonekano wake ulikuwa uleule wa siku zote, ilikuwa ni kama jana hakuna kilichotokea.
Upande wa Hamza aliona Regina alikuwa akiigiza kuwa kauzu tu mbele yake hivyo aliona inafurahisha sana.
Baada ya wote kumaliza kifungua kinywa Hamza alishika usukani na safari ya kuelekea kazini ilianza, wakati huo Hamza alikumbuka swala la kampuni ya Zena ilio chini ya James kununua kampuni ya Omega na shauku ilimvaa.
“Regina hivi..”
“Kaa kimya, sitaki kuongea chochote na wewe”Aliongea na kumfanya Hamza kushangaa na aliwaza au alidhani anauliza swala la jana.
“Sio kama nataka..”
“Nimekwambia kaa kimya , kama huwezi funga mdomo wako shuka kwenye gari”Aliongea akiwa siriasi na Hamza aliishia kuufyata.
Hamza palepale alipata wazo na alitumia mkono mmoja kuendesha gari na mkono mwingine alitoa simu yake na kuandika maneno kadhaa kwenye simu na kumuonyesha Regina kuona.
“Nilitaka kuuliza kama kuna tatizo kubwa na kampuni ya Zena juu ununuzi wa Omega?”
Regina mara baada ya kuona aliona alikuwa amemdhania vibaya juu ya kile alichotaka kuongea , ukweli hakutaka utani wowote kutoka kwa Hamza juu ya tukio la jana ndio maana alizidisha ukauzu.
“Huna haja ya kuwa na wasiwasi , nina mpango wangu”Alijibu
“Nauliza , hata hivyo haina maana mimi kuwaza , ninachotaka kusema usijipe presha sana , jaribu kutafuta kitu kitakachokufanya angalau utulie, kama vile jana ulivyokuwa ukisindilia…”
“Nyamaza”Alifoka Regina , kwa jinsi alivyobadirika ni dhahiri angekuwa na nyundo ingetua katika kisogo cha Hamza. “Hey , usipaniki hivyo nimeacha”
*****
Baada ya kufika kwenye kampuni Hamza kama kawaida aliingia katika ofisi yake na kuanza kuvuna Bitcoin mpaka inatimia mchana muda wa chakula ndio alitoka.
Baada ya kwenda mgahawani na kuonekana mbele ya wafanyakazi watu walionekana kumwangalia.
Warembo wengi walionekana kumwangalia kwa macho ya kumkubali kitu kilichomfanya kujiuliza kwanini wanamwangalia sana.
“Hamza kumbe haikuwa utani unajua mapigano hata kumzidi Yonesi , hatimae tumejua siri kwanini umefanywa kuwa msaidizi wa bosi kumbe upande mwingine ni bodigadi”Aliongea Asha wa idara ya mauzo na sasa Hamza alijua kwanini walikuwa wakimwangalia.
Wiki iliopita kitendo cha kumdhibiti Master Konki mara baada ya Yonesi kupigika , swala hilo lilionekana kusambaa katika kampuni kwa wafanyakazi wote.
“Hamza hebu tuambie , tulisikia sijui ulitumia mbinu ya kucha za tai , hivyo vidole unaweka vipi tuonyeshe”Aliongea Mirium rafiki yake Asha.
Hamza aliwaza na kujiambia mbinu hio ya Kucha za tai ina historia kubwa sana tokea enzi za kale , sasa anawezaje kuwaelezea kirahisi, lakini mara baada ya kuona wamejawa sana na shauku , aliamua kuwaelezea ki uwongo uwongo kama mtoto anaejifanysiha kujua mapigano, kitendo kile kiliwafanya Mirium na Asha kuvuta midomo na kumuacha.
Lakini hata hivyo Hamza kutokana na kuangaliwa na wafanyakazi wengi kwa macho yaliojaa sifa , kichwa kilimvimba na mara baada ya kuchukua chakula chake alibadili mwendo kabisa na kuanza kudunda huku akisogelea meza aliokaa Yonesi akiwa peke yake.
“Habari Kapteni , naona leo sioni Suasage kwenye sahani yako?”
“Hebu jali mambo yako , muone kichwa kilivyokuvimba , kumfukuza yule mzee ndio unaona umefanikisha kitu kikuubwa?, mpaka mwendo unabadilika”Aliongea Yonesi
“Hehe .. najua hata wewe mwenyewe unanikubali lakini unaona aibu kusema waziwazi , hata usiongee mimi naelewa unachojjisikia moyoni”
“Nani anakukubali , unadhani mimi ni chizi?, Wewe nisubiri nishaanza kufanya mazoezi makali , nakuhakikishia lazima nikupige mpaka uombe
msamaha , ni kazi tu ziliniweka bize na nikaacha kuchukua mazoezi ndio maana”Hamza hakuongezea neno na aliishia kukaa kimya.
“Unadhani natania , nilibweteka kwa muda tu ndio maana”
“Najua kapteni wewe ni mtaalamu wa hali ya juu”Aliongea Hamza lakini Yonesi hakuridhika.
“Najua unanidanganya tu kunifariji , kwenye moyo wako unaniona mnyonge”
“Kapteni , unadhani ni kipi napaswa kukuambia ili nipate amani ya kula chakula changu”
“Kama unataka kula chakula chako , nenda meza nyingine, kwani lazima ukae kwenye meza yangu” “Hapana lazima nikae meza moja na wewe”Aliongea Hamza na Yonesi hata yeye aliona kabisa Hamza alikuwa kila siku na mpango wa kukaa meza moja na yeye , ukweli ni kwamba kulikuwa na wanawake wengi ambao walikuwa wazuri kuliko yeye , hivyo aliuliza kwanini analazimisha wakae meza moja.
“Kwanini?”
“Huchoki kula peke yako kila siku , mimi nipo hapa kukupa kampani , anagalu sasa hivi sio mpweke sana maana una rafiki”
Yonesi mara baada ya kusikia hivyo alishangaa na kuguswa na jambo hilo na mwili wake ulikakamaa.
Yonesi hakuwa mzaliwa wa jijini Dar , ki ufupi ni wa mkoani na kutokana na baadhi ya mambo alijikuta akitofautiana na wazazi wake na ndio maana alikuja kuhamia Dar akiwa nje ya kazi , katika kipindi hicho cha upweke ndipo alipokuja kukutana na Regina na akafanywa mkuu wa kitendo cha ulinzi wa kampuni ya Dosam baada ya Regina kutumia ushawishi wake serikalini na Yonesi kupewa ruhusa.
Lakini sasa kutokana na mazingira aliokulia na namna alivyosoma elimu yake kuanzia akiwa mdogo mpaka ukubwani , ilimfanya kuwa ngumu sana kutengeneza marafiki , hata kwa walinzi wenzake wakike hakuweza kuendana nao zaidi ya maswala ya kikazi tu.
Alikuwa akiishi peke yake , kazi alikuwa akifanya peke yake , kula peke yake, kila kitu peke yake , kila siku ilikuwa hivyo kwa miaka mitatu yote.
Kula kwake ndani ya mgahawa wa kampuni ukiachana na wanaume ambao walikuwa na ajenda zao mpaka kutaka kula nae hakuna mtu alishawahi kuja katika meza yake kwa ajili ya kuwa rafiki tu , wala kujali kama alikuwa mpweke.
Katika macho ya wafanyakazi wenzake , Yonesi alionekana kama sio mtu wa kawaida wa kufanya nae urafiki.
Yonesi alikuwa imara kwasababu alikuwa ni mwanajeshi hivyo anao uwezo hawa wa kuishi jangwani , lakini haikumaanisha kwamba yeye sio mwanamke ambae upweke haumuathiri.
Hivyo mara baada ya Hamza kusema ni mpweke alijihisi huzuni moyoni mwake , aliishia kugeuza macho yake pembeni ili asionekane machozi yalikuwa yakitaka kumtoka.
“Napenda kula peke yangu , sijawahi kusema mimi ni mpweke , na pili sihitaji muhuni kama wewe kuwa rafiki yangu , kaa mbali na mimi”
Upande wa Hamza hakumjali kabisa na aliishia kucheka tu huku akiendelea kuwa bize na chakula chake.
Yonesi aliishia kutulia na kuendelea kula chakula chake taratibu huku mara kwa mara akimwangalia Hamza kwa jicho la pembeni.
Hamza mara baada ya kula kama kawaida alichukua matunda na kupandisha nayo juu.
Baada ya kufika katika ofisi ya Regina aliweza kukuta baadhi ya sura anazozifahamu na nyingine asizozifahamu , walikuwa ni wafanyakazi wa juu wa kampuni na ilionekana kuna kikao kilichokuwa kikiendelea na kitendo cha kuingia bila ya hodi ni kama iliwafanya wote wamkodolee macho.
Comments